Monday, September 10, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-46



‘ Ndugu muheshimiwa hakimu, naomba msichoke maelezo yangu, maana bila kuyaelezea haya, ukweli halisi hautaweza kueleweka, na tatizo linaweza lisimalizike, na haki isitendeke, mimi nataka tatizo hili limalizike kabisa, ili nami niweze kupumzika kwa amani…’akasema.

‘Kama ni jela,..au kuwa huru, au…kaburini…yote yawezekana au sio kama kweli mtahuku kwa haki …’akaongezea hivyo.

‘Najua yaliyotokea yamewaumiza wengi, ..lakini tunasahau, kuwa kuna waliokwisha kumia zaidi yao…, mara nyingi tunajali waliopo, ina maana ambao hawapo hawana haki au sio, asiyekuwepo na lake halipo…najiuliza tu,..je kama haki haikutendeka, kwa hao ambao hawapo duniani,…ndio basi tena…ila ni lazima hili liishe maana wengine tunasumbuliwa na ndoto, tunasumbuliwa na kumbukumbu za nyuma…’akatulia.

‘Kabla sijaingia kwenye kujibu swali lenu la msingi, japokuwa nimeshaanza kulijibu kwa wenye kufikiri,..kuwa hilo deni ni la nani hasa.. ….’akageuka kumuangalia wakili wa benki, halafu akageuka kuangalia kule alipokuwa ameelekea,…

‘Najua nyote mna haraka…mnataka nisema tu, hilo deni ni la marahemu au sio au ni langu, au ni la mtu fulani, au sio….lakini kwanini nisema jibu tu, bila kuelezea ukweli wa hilo jibu..sasa naanza hivi…’akainama kidogo.

‘Lazima niwarejeshe huko …deni lilipoanzia, au sio…kwangu mimi deni hili lilianzia siku ile  nilipopokea ile zawadi, ..maana ndipo mambo yalianzia…siku nilipojitambua, na kuoenekana  sina thamani mbele ya jamii..lakini thamani yangu ilikuwepo, na kihalali kabisa..lakini ungelisemaje…eeh, mtoto wa jalalani kama mimi…’akageuka kumuangalia halimi.

‘Ni lazima nieleze kila kitu, tafadhali mnipe muda wa kutosha…’akaendelea kusema
Tuendelee na kisa chetu…

*******

Siku.moja aliniita mama mlezi, kipindi hicho ndio alizidiwa sana, kwani naye alikuwa anaumwa, magonjwa yale yale yaliyomuondoa mama yangu duniani, japokuwa yeye, hayakutokana na kupigwa, yeye yalianza tu, japokuwa kihistoria yawezekana ni kutokana na dhahama za dunia, hilo sitalielezea maana sina ushahidi nalo.

‘Ila nina imani hiyo, waliosababisha yote hayo…na wao wataishia huko huko…mimi sijui, lakini nahisi hivyo, …


‘Mimi naweza kusema tu, yeye alipatwa na maradhi hayo kutokana  na majawaliwa ya mungu…kiukweli alikuwa anaumwa haswa,…alivyoniita , nikajua labda, anataka kuniagiza kitu….’akatulia


‘Naomba tuwe na subira…’akasema pale alipoona wakili wa benki akitaka kumkatiza. Na hakim naye akamuashiria huyo wakili atulie kwanza…


'Mama unasemaje, vipi wajisikiaje …’nikamuuliza.


'Mwanangu mimi ninakupenda sana,..’ akaanza kusema hivyo, sikuona ajabu maana kauli hiyo sio mara ya kwanza kuisikia kutoka kwake,..ila moyoni nikahisi kuna jambo…akili yangu huhisi vitu kiajabu sana.


‘Mwanagu, bahati mbaya mimi  sikujaliwa kupata mtoto, na ikatokea bahati nzuri kukupata wewe…, namshukuru  sana marehemu mama yako kwa kuniachia wewe , uwe mwanangu....'akasema…na mimi wakati huo nimekaa karibu yake kwenye kitanda

 Pale nilipokaa kitandani, nikahisi machozi kama machozi yanataka kunitoka, maana nilimpenda sana  huyo mama, alinilea kama mtoto wake, na kwa vile sikuwahi kupata malezi yangu  mama mzazi, naweza kusema,…huyo mama alinilea huenda zaidi ya angelifanya hivyo mama yangu,..sijui kama nakosea, mnisamehe tu…’akatulia


'Ndio mama, utapona tu, na nimeshapata kazi, japokuwa sio nzuri sana, lakini nitajitahidi utibiwe …’nikasema.


‘Mimi niliambia usiache shule usome maana kusoma ndio maisha yako ya baadae, unafikiri utapata pesa gani ya kunitibia mimi…hutaweza, na hakuna dawa tena ya ugonjwa wangu…’akasema.


Aliposema hivyo, machozi yakaanza kukubujika, siku alinikatisha tamaa, kiukweli pamoja na mengine mengi, mama huyo ametaabika sana kutokana na hayo maradhi, ilifikia mahali hawezi hata kutoka nje, jamaa zake wamemuacha tu, hawaonekani…walijitahidi awali baadae wakachoka. Nikawa nahangaika naye, ndio maana yangu nitafanya nini…


'Mwanangu wala usisumbuke, najua sitapona, na bora nijifie tu, kuliko kuendelea na mateso haya, na nimemuomba mungu anijalia nife, ili nisiendelee kukutesa wewe zaidi…’akasema.


Hapo mimi nilihisi mwili ukiniisha nguvu,  lakini nilijipa ujasiri wa kiume. Nikijua ni maneno ya kukata tamaa, ila nikipata pesa ni lazima nimfikishe hata nchi za nje akatibiwe…angalau niweze kulipa fadhila, japo kidogo.


'Sikiliza mwanangu, nilishawahi kukuambia kuwa  mimi sio mama yako wa kukuzaa, na hata kuendelea kukulea wewe, wengi hawakupenda, waliona kuwa nahangaika na mtoto baki, wakati watoto wa ndugu wapo wengi tu, wakati mimi mwenyewe nidhofuli hali, sina mbele wala nyuma ila nina utajiri, nyumba, maeneo niliyowahi kukuonyesha yote ni mali, na yatakuwa mali yako, unakumbuka mipaka vyema , si ndio hivyo…’akasema.

‘Ndio nakumbuka sana….’nikasema nikikumbuka maeneo ambayo mama huyo alipenda kunionyesha na mipaka yake, lakini kipindi hicho sikutilia maanani kivile, niliona tu,…kama mama anamuonyesha mwanae tu..najua muda wote tutakuwa naye.


‘Na hii ndio sababu ndugu zangu wengine hawataki hata kuja kunisaidia, eti nabeba mizigo isyo yangu, eti nataka kumpa urithi mtu asiye damu yangu, ila nasema mali yangu yote hata nikifa leo, ni ya kwako… na kumbuka jambo moja, nilikuwa hivi mimi…siwezi kukuacha mwanangu, niliapa mbele ya mama yako kuwa nitakulea hadi pumzi yangu ya mwisho, na wewe ndiye mwanagu, nimpe nani mali yangu eeh, niliwaelezea hata ndugu zangu, ndio maana wakaamua kunitelekeza…’akasema


'Mama najua sana hilo, unanipenda sana, mimi sitak mali, na kama mali ipo kwanini mama tusiiuze ili utibiwe tu… maana juhudu zangu zote ni ili na mimi niweze kulipa fadhila zako, japokuwa sitaweza, lakini nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kila mshahara nitakao pata itakuwa kwa ajili yako…’nikasema.


‘Ahsante sana mwanangu, mola akuzidishie moyo huo..ila wakati umefika,..siwezi kukudanganya tena…muhimu ni wewe kupambana na maisha, najua nikiondoka hapa duniani, utakuwa peke yako, ila hutakuwa masikini…’akasema, na mimi muda huo sikuwa na mawazo ya mali yake kabisa, ..ningelikuwa na wazo hilo ningelifanya jambo la kuja kunisaidia baadae, niwe na kumbukumbu za kisheria..


‘Mama, huwezi kuondoka ukaniacha…’nikasema


'Sawa,..basi tutakufa wote…’akasema kiutani, huku  akijaribu kucheka.


‘Hapana Mama hutakufa..nitakupigania, utaenda kutibiwa India…’nikasema kwa kujiamini.


‘Hahaha india, wanaweza kutibu kifo au….Sikiliza mwanangu, maradhi haya yalianza zamani…kipindi napambana na ndugu zangu, kuhusu maeneo aliyoniachia mama, mimi nilizaliwa peke yangu kutoka tumbo la mama yangu, lakini tupo wengi kwenye familia ya baba, maana baba aliona wake wengi tu..lakini hayo hayakuhusu.


Ila la muhimu ni ujumbe kutoka kwa marehemu mama yako,… koho, kohooo…’akasema akikohoa kwa shida.


‘Nakumbuka siku moja,  niliwahi kukuambia kuna zawadi aliniachia mama yako, na nikakuambia ukifanya vizuri kwenye masomo yako, ukapata kazi, ndio nitakupatia hiyo zawadi,..unakumbuka hilo…’akasema


‘Zawadi, ndio..lakini hukuwahi kunipatia..japokuwa nilifaulu vizuri masomo yangu, sema tu, nimekatiza kusoma ili niweze kutafuta kazi, ili nipate pesa ukatibiwe, kwani ilikuwa ni zawadi gani…?’ nikauliza


‘Ni zawadi maalumu kwako…ila yenye masharti….’akasema na mimi hapo akilini niliwaza zawadi hiyo ni ya maelekezo tu, ndivyo akili ilinituma, lakini kwa kauli hiyo ya mama, nikahisi kuna zaidi ya hivyo ninavyowaza…


‘Mama yako alisema nije kukupatia hiyo zawadi, wakati muafaka ukifika…lakini naogopa kwa jinsi alivyoniambia, sizani kama muda huo utafika,…na pia…kohokohoookh….ooh, mungu nisaidie tu, nitimize haya…’alasema hivyo akionekana kuchoka.…’akatulia.


‘Mama, naona hali yako sio nzuri, wewe lala utulia, mimi sitamani zawadi yoyote, wewe ndiye zawadi muhimu kutoka kwa mama yangu, bila yaw ewe maisha yangu yangelikuwaje,…, achana nayo, muhimu ni wewe mama yangu..’nikasema


‘Sikiliza, ahadi ni deni, ogopa ahadi uliyoitamka mbele ya marehemu akiwa hai, kuwa kifa ufanye kadha wa kadhaa..…, zawadi hiyo mama yako alisema nije kukupatia, ukiwa tayari na maisha yako.., ili isije ikawa sababu ya kushindwa kuendelea na maisha mengine …maana ya hiyo kauli mimi  siijui..ila alisema hivyo tu…’akasema


'Oh..ni zawadi ya namna gani mama...?’ nikauliza ili mama asiendelee kuteseka.


'Siku ile mama yako kazidiwa, akiwa ndio keshajua kuwa hataishi tena, kama ilivyo kwangu mimi,….aliniomba nikamnunulie karatsi zile za zawadi, akaniambia nimsaidie kuifunga mbele yake, zawadi hiyo iliweka kwenye bahasha kubwa kwahiyo siku ilikuwa ni kitu gani…


Akasema sasa nifunge na ile karatasi ya zawadi,  akihakikisha hiyo zawadi imefungwa vyema kama alivyotaka yeye,…nikafanya hivyo, kwahiyo kilichomo humo…hata sijui ni kitu gani…’akasema


‘Oh, mama, utapokeaje zawadi hata hujui kuna nini..ndani yake, wewe ungefungua na kuangalia, najua mama yangu hawezi kunipatia kitu kibaya, lakini wewe ndiye mama yangu mlezi ulitakiwa ujue kilichomo au sio…’nikasema.


‘Sawa nakuelewa, lakini hujui kwanini mama yako alifanya hivyo,..huenda aliogopa fitina, huenda aliogopa, nikifungua, na kuona kilichopo, tamaa itanishika nishindwe kukupatia, kila mtu ana mawazo yake, na ibilisi ana nguvu sana, sasa mimi sikutaka kukupatia hiyo zawadi mapema, bado nilikuwa na mashaka kuwa hujatulia, kimaisha…’akasema.


'Mhh, haya mama niambe ni zawadi gani hiyo, nisikuchoshe, watakiwa kupumzika…’nikasema

 Basi, Mama akainua godoro, akatoa mfuko wa rambo, ndani yake akatoa bobksi lililofungwa kizawadi, akaniambia, …


'Hii ndio  zawadi yenyewe…na aliniambia huo ndio urithi wake ambao alijaliwa kuuweka kwa ajili yako…’akasema.


Nikaipokea ile zawadi, kwa kusita sita…akili yangu husoma hisia za watu, lakini hizia za nani hapo, maana hata huyo mtoaji zawadi hajui kilichomo,…nikaipokea na kutaak kuifungua..yeye  akasema…


‘Aaah, kama alifanya hivyo nisijue kilichomo ndani yake basi chukua muda, ukiwa umepumzika ndani, peke yako, ndio ufungue hiyo zawadi, hakikisha umejiandaa vyema, usichukulie mzaha…’akasema.


‘Lakini mama mbona yaonekana kama ni …aah, hata sijui ni nini...’nikasema nikimtafsiri huyo mama anavyowaza, kama ni maagizo ya jambo fulani muhimu, ambalo mama alipenda nilijua, kama ni mali ipo wapi, au…hapo sikuweza kutafsiri zaidi,  moyoni kwa muda huo nilitaka nikitoka hapo nikafanya hata harambee huyu mama yangu akatibiwe, nishapanga mikakati yangu kichwani.


'Hiyo ndio zawadi na urithi aliyoniachia mama yako, kwa masharti, usije kufanya kufukuru nayo…alirudia sana kauli hiyo, kuwa ‘usije kufanya kufuru nayo, usije kukengeuka ukafanya mabaya, usije ukachukulia vibaya, uwe muadilifu na usimamie kwenye haki …sasa sijui kwanini alisema maneno hayo…’akatulia.


'Mhh, kufuru...ni …na ni mabaya gani nitafanya mimi, mama wewe umenifindisha niwe mwema kwa watu..ndivyo nitakavyo hivyo…mimi nahisi kwa hali ya mama aliyokuwa nayo, aligundua jambo, ..akashindwa kulifanya, au sio…sasa anataka mimi mwanae nilifanye,..au ..kitu gani kinaweza kukaa kwenye hilo boksi mapaka nije kufanya kufuru…’nikasema.


'Wewe utakuja kujionea mwenyewe, sasa ni zawadi yako na mimi nimetimiza wajibu wangu japokuwa nilivyoona mimi, wakati wake ulikuwa bado, lakini nitafanyaje..na siwezi kumpatia mtu mwingine ili aje kukupatia ukishafikia mahali kama alivyotaka mama yako..zaidi ya hapo mimi sijui……….’akasema akihema kama kweli katua mzigo.


'Ok. Sawa mama mimi nitafanya kama ulivyoniagiza,…sasa mama nikakununulie nini…?’ nikamuuliza.


‘Kaninunuli chochote laini kinachoweza kupita kooni…’akasema mama, maana hata kula kipindi hicho, ilikuwa ni shida, na ninashangaa siku hiyo aliweza kuongea vizuri.


'Sawa mama ngoja nikaiweke hii zawadi, halafu niende sokoni, nitanunua viazi mbatata, nikupigie kama uji,..na nyama, si utapenda …?’ nikasema na yeye akatabasamu na kuonekana kama analala..


Basi nikachukua ile zawaidi, nikaihifadhi kwenye vitu vyangu muhimu,..bila kuifungua, na cha ajabu sasa…, nikawa nimesahau kabisa kuhus hiyo zawadi maana wakati huo mawazo yangu yapo kwa jinsi gani nitamsaidia huyu mama apone…na kiukweli mtu akinipatia maagizo , hasa watu wakubwa, huwa sina kawaida ya kusahau , lakini hilo nilipitiwa…’akasema.


Haikupita wiki  mama yangu mlezi akafariki,…’hapo akatulia kwa muda ikawa kama vile hataongea tena…


‘Vipi …’akasema hivyo hakim.


‘Naombeleza muheshimiwa hakimu, samahani sana…ni tukio ambalo sitaweza kulisahau..

‘Sawa… siku ya mazishi sasa…ndio mambo yakanza, kwanza siku ile ile ya kuzika, tumeshamaliza, nipo kwenye kaburi la mama mlezi, nalia, mtu akaja nyuma yangu akanishika bega.

Nikageuka,..alikuwa mzee mmoja hivi kashika barua, akasema;

‘Haya ..hii ndio barua yako…’akasema hivyo tu, na kunikabidhi mkononi, nikaishika sikupenda kuisoma, huyo mzee alipoona hivyo akasema;

‘Isome kwanza…kabla sijaondoka…’akasema

Wakati nataka kuisoma, kumbukumbu za nyuma zikanijia, kumuhusu huyu mzee,..huyu mzee, kipindi fulani alikuwa akifika kwa mama, na hawaishi kugombana, na nikimuuliza mama kwani huyo mzee akifika wanasihia kugombana, mama akasema, hayo nisiyaingilie, kwani hayanihusu…kwahiyo mimi kama mimi sikutaka kufuatilia zaidi.


Leo huyu mzee ndiye ananipatia hiyo barua..


Hiyo barua nilitakiwa niisome pale pale…


'Mwanangu, kwaheri, najua nitakufa...nilitamani nikulee, nilitamani wewe uje kuwa ni jembe langu..nilitamani unizalie wajukuu, waje kunisumbua, ili nijue usumbufu wa watoto ..

Lakini, sikuumbwa kuyaona hayo, sikuumbwa kuja kuipata raha ya dunia, maisha yangu kwa ujumla yamekuwa ni mateso, tokea siku ulipoingia tumboni kwangu …’Nilipofika hapo ndio nikajua hiyo barua ilitoka wapi..sio ya kutoka kwa mama mlezi.


‘Ni kwanini, maisha yangu yalikuwa hivyo.....jibu lipo kwenye zawadi atakayokupatia mama niliyempa jukumu la kukulea, najua atakuja kukupatia, hiyo zawadi muhimu katika maisha yako,…na baada ya hapo, utaona kila kitu,, utasikia kila kitu, utajua kila kitu…

Na kwa hali hiyo wewe…utajua ni nini cha kufanya..maana hapo ..sijaficha kitu chochote, …mungu ni shahidi yangu,..huenda hiyo ikawa ni sababu nyingine ya maisha yako ya baadae..zaidi na hayo niliomba mungu akupatie.kitu ambacho kitakusaidia, katika maisha yako iwe karama kwako,..sasa hilo mimi sijui mungu atakupatia karama gani.


Kwaheri mwangu siwezi tena kuandika zaidi..

Hebu firikia hali kama hiyo, wewe kama mimi ungelijisikiaje…nilihis ni misiba miwili ipo mbele yangu..

Naona hata herufi za jina lake hakuweza kuandikwa vyema….mwisho wa hiyo barua, nikamaliza kuisoma na huyo mzee akasema

‘Sasa huo ndio ushahidi kuwa wewe ni nani..unasikia, …kabla hatujaanza kuingie kwenye mambo ya mirathi, ..unanielewa lakini…’akasema huyo mzee , mimi pale sikumuelewa, nikasema.


‘Sawa mzee ahsante..’nikasema hivyo, na yeye akageuka kuondoka zake nikabakia mwenye makaburini, nikilia na kuombeleza…


**********

Kiukweli hapo mimi nilijiona kama nina msiba juu ya msiba nilijiuliza sana, kwanini mama aliniandikia hayo, na kwanini …mama mlezi naye kafariki, na kuna nini mbeel ya haya yote.., hapo ndio nikaingiwa na hamasa ya kwenda kuifungua ile zawadi…aliyoniachia mama mlezi, lakini sikupata muda huo…


Baada ya mazishi, ikawa ni kikao cha familia, …


‘Wewe kijana…hatutaki kukufukuza, wewe utendelea kuishi kwenye hii nyumba lakini utaishi hapo kama mpangaji, ..’kauli ya huyo mzee aliyenipa hiyo barua, ikasema na kuniacha kwenye mshangao, maana mimi nilijua yeye ndiye atakuwa msemaji wangu mkuu, kwani yeye ndiye aliyeambiwa yote na mama mlezi.


‘Lakini babu…nilizoea kumuita hivyo..’babu’ , japokuwa kumbe ni ndugu mkubwa kwa mama yangu.. na hakupenda kabisa mimi nimuite hivyo.


‘Unapenda sana kuniita babu, kwa dharau sio, mimi sio babu yako,..na ukome kuniita babu,… wala hatuna udugu na wewe, babu , babu, nenda kamuite babu yako hivyo, kama unaye…’akasema kwa hasira.


‘Samahani mjomba…nilitaka kusema tu, mama aliniambia hapa ndio kwangu hata akiondoka duniani..nyumba na mali..yaani maeneo yote ni mali yangu..’nikasema


‘Hahaha, nilijua tu, unajua wewe umetokea wapi…sisi tulikosana na ndugu yetu huyu kwasababu yako, na nilijua ipo siku itafika, na ..haya yatafanyika, wewe huna damu na hii familia kabisa na wala hatujui wewe baba yako ni nani..kwahiyo wewe huwezi kurithi chochote, kwenye hii familia,.. unasikia, nenda kaulize, au hata kushitaki, hili eneo, na h ii nyumba ni mali ya familia husika, unasikia..’akasema.


Kiukweli mimi sikutaka kugombea chochote maana kweli mimi sio mwanafamilia hiyo, nilelewa tu hapo, moyoni nikasema, msiba ukiisha naenda kutafuta nyumba ya kupanga,..ila watu sasa, . watu waliojua hayo, hawakuniacha nifanye hivyo…


Watu wakanishawishi nifungue kesi…ilikwenda nikafanya hivyo, …hahaha, kesi ilinibwaga kama sijulikani,..sina ushahidi wa maandishi, sina hata ndugu mmoja au jamaa aliyesimama upande wangu,… na mmoja wa mashahidi aliyekuwa upande wa mzee…pamoja na ndugu wengine,  ni huyo  mwenye hiyo nyumba nzuri, inayotaka kupigwa mnada...
..

‘Huyo jamaa alikuwepo kipindi hicho cha kesi, sijui wanajuanaje na huyo mzee, na akaongea mengi ambayo, …ooh, yalinifanya nisiwe na hamu ya kudai tena…’akasema


Sasa baada ya hapo eneo hilo likauzwa, na aliyeuziwa sasa…ndio huyo aliyenga hilo jumba la kifahari, nakumbuka siku kabla nilifika na kutaka kuongea naye,  huyo aliyeuziwa, ,,kipindi hicho nyumba niliyokuwa naishi na mama bado ipo, ila mimi mwenyewe sikupenda kuishi hapo tena, ila vitu vyangu bado vilikuwepo humo ndani,…


Huyo jamaa alinicheka sana,..kwa dharau..


‘Wewe mtoto kupata bahati yakulelewa na wanajami wenye huruma ndio umeona mali ni yakko,..kijana nakushauri jambo moja muhimu kwenye maisha yako…, soma, jitahidi,usome ili upate kazi, na bidii yako ndio itakusaidia, utafute mali yako ya halali.., usiwe na tamaa na mali za watu wengine unasikia,…’akaniambia


‘Lakini mimi nilitaka tu nikueleze ukweli alivyosema mama mlezi, wewe umenunua eneo la dhuluma, sio vizuri hivyo…’nikasema.


‘Dhuluma unaijua wewe, na mimi sina makosa, maana eneo hili nimenunua kihalali, kama kuna tatizo kamuulize mzee mtupe, au nenda mahakamani, kwani mahakama wamekosea, wewe kiukweli huna haki na mali hiyo kabisa…’akasema hivyo


‘Oh, haya bwana, ..lakini sijamalizana na nyie, ipo siku tu…’nikasema


‘Hahaha, sawa kama unahisi nimefanyiwa vibaya, kwanini usiende tena mahakamani, haki yako utaipata lakini sasa utaipata wapi, labda ukaongee na huyo mzee aliyeniuzia eneo hili, akupatie eneo jingine lakini sio hapa, hapa nilipapenda sana, pamekaa kiulaya ulaya..ndio maana nimepanunua kwa bei mbaya sana…, na hapa nitakuja kujenga hekalu langu, hata kama pangelikuwa ni pa kwako ningepanunua kwa bei unayoitaka wewe, …lakini sasa sio kwako na sio halali yako kabisa, kama nilivyowahi kukushauri nenda shule, huo mwili usikudanganye, wewe bado mdogo sana…’akasema


‘Ina maana ndio maana umerubuniwa ili uje kutoa ushahidi wa uwongo..ili uje ujenge hekalu lako hapa…kiukweli umefanya vibaya sana…’akasema


‘Nimekuambia hivyo, kama unahisi umedhulumiwa,…nenda mahakamani, mimi sijui, niliongea ninavyojua mimi…nilivyoambiwa, na kusikia,…sasa mengine siyajui,na kwanini ung’ang’ania, wewe umezaliwa na huyo mama, .?’ akaniuliza


‘Niende mahakamani ili iweje, mimi nilijua wewe ni msomo, na unaongea kisomi, lakini usomi wako umeuelekeza kwenye kufanya mimi nidhulumiwe, ina maana mtu kama mimi sina haki, je kauli ya marehemu haithaminiwi…na kwa hivi sasa…nitadai nini tena,..mimi mtoto wa mitaani, majalalani, kama jina langu, yote namuachia mungu..’nikasema


‘Kama marehemu alisema hayo, ushahidi upo wapi…hakuna , hiyo ni kauli yako tu, ni nani ataamini kauli yako eeh…hata mimi siwezi kukuamini….’akasema



Kiukweli huyo jama nilianza kumchukia…moyoni nikaapa kama nitapata nafsi basin a mimi nitakuja kumuonyesha…


Kipindi hicho alikuwa karudi mara moja kufuatilia ujenzi wa nyumba yake,…mimi ndio nahangaika nimepata kazi ya kujishikiza tu, na kazi hiyo nikafukuzwa, maana niliacha kufika bila taarifa, nikifuatilia hizo mali, na mali nimezikosa..ila ushauri wa huyu jamaa ukanifanya niingiwe na ari ya kusoma tena, ili nipate elimu nije kupambana naye,..kiukweli kumri bado nilikuwa mdogo sana.


Nikaanza sasa kusoma kwa bidiii…ukumbuke mimi nilikuwa na akili ya ziada, kila nilichosoma ikawa nafanya vizuri, mpaka nikashindwa kujua fani yangu ni nini…


Ukumbuke hadi hapo, sijaweza kuja kuchukua viti vyangu kwenye ile nyumba na sijakumbuka kuifungua ile zawadi , ikitokea nikikumbuka, kunatokea tukio fulani la kunisahaulisha..siku zinakwenda, mwezi, mwaka,…miaka sasa…


Siku moja ndio nikaota ndoto…moto unawaka, unaunguza kumbukumbu zangu,…unaunguza vitu muhimu sana kwangu, nikawa nakimbilia kuuzima huo moto, na wakati nakimbia, nikamsikia sauti ya  mama ikisema;


‘Mwanangu, ule moto umeusababisha wewe mwenyewe…, umeunguza kumbukumbu zote za maisha yako, moto ukiunguza kitu hakuna kitakachobakia,..moto…ndio unaoweza kuharibu kumbukumbu zote, unalielewa hilo,..je  unakumbuka nilikuambia nini…’akasema


‘Mama sikumbuki, lakini nitafanya nini…maana kumbukumbu zangu zote zimepotea..’nikasema


‘Kamuulize mama yao mlezi atakupatia nyingine, ..na usisahau ujumbe wangu, hapo yaweza kuwa ni mwanzo tu…moto utawaka sana, usipokuwa makini, …na ukichelewa hutaweza kuuzima, .utaharibu kumbukumbu zote za maisha yako, na hakuna wa kuja kukusaidia…unasikia, haya fanya nilivyokuambia...’akasema.


‘Nifanye nini sasa..?’ nikauliza.


‘Wewe ni mjinga sana, nimekuambia nini,..tumia akili yako vyema,…na kabla ya kuitumia akili yako vyema ni bora wewe mwenyewe ukajijua , wewe ni nani, hivi kweli unajijua wewe ni nani, kumbuka jambo moja,…akili yako ndio hazina yako, acha ujinga wewe..’akasema.


 Nakumbuka sana kauli ya mama mlezi, alipenda kuniambia hivyo, wewe ni mjinga sana tumia akili yako vyema…na kuna siku mama mlezi akasema, kauli hiyo alizoea kuitumia sana mama yangu mzazi, ukikosea, au akitaka kukuelekeza jambo fulani,..’wewe acha ujinga, usiwe mjinga, tumia akili yako…’ lakini hakuweza kuyatamka mane ohayo vyema, kwani hakuweza kuongea vyema…


 Asubuhi yake, nikaondoka, kwenda kule kwenye ile nyumba, nafika nyumba haipo tena, imeshavunjwa, kila kitu kimetupwa tupwa, moto unawake, kuunguza hayo mabaki ya nyumba, iliyovunjwa na vitu karibu vyote vimeungua,,kuna nyumba nyingine inaanza kujengwa, kuna mawe yameletwa hapo…haaah…hakuna kilichobakia, kisa, ili jumba la kifahari liweze kujengwa,


‘Kwanini msingesubiria nichukue vitu vyangu…’nikauliza

‘Mwenye eneo kasema, tuvunje, maana humo ndani hakuna cha maana, na tuchome moto kabisa.., maana kuna kunguni…’nikaambiwa,


Moyoni hasira, chuki, vikatawala…zawadi ya mama haipo,na wala sijui itakuwa wapi, nikitaka kwenda kuitafuta siruhusiwi, walinzi wakanizuia na hata kunipiga, hata pale nilipowaomba wanisaidie kutafuta kama wanaweza kuiona kitu kama hicho, hawakunisikiliza zaidi ya kunicheka kwa dhihaka.
.

Usiku mmoja nikavizia, walinzi hawapo ndio nikaenda kuchakura chakura…bahati nikakuta baadhi ya vitu havijaungua sana, na kuhangaika,..nikaona mfuko wa Rambo, na…nikaufungua, ni ule ambao uliweka hiyo zawadi, ..lakini sikuweza kuiona kitu kama hicho, yaonyesha kabisa kuna mtu aliuona, akaitoa hiyo zawadi, ….au ndio imeteketea kwa moto.


Ni nani huyo…ilinipa shida sana, na wakati nahangaika mara  akatokea mtu kwa nyuma yangu, nikajua ni hao walinzi, hapo nisubirie kipigo…


‘Unatafuta hiki eeh,…unatafuta hiki…haya chukua, ….ndio hapo utajijua wewe ni nani na huna haki yoyote na hii mali, chokoraa mkubwa wewe, mwanaharamu,…mtoto wa jalalani…’akasema huyo mtu na kunitupia usoni…huku akitamka maneno ya dharau,kwa kadri alivyoweza..


NB: Zawadi ndio hiyo, je itanisaidia nini, je ilimfanya nini huyo jamaa.., JE inahusiana vipi na hilo DENI....tutaona kwenye sehemu ijayo…



WAZO LA LEO: Tusipende kutoa ushahidi bila kuufanyia kazi, tukahakiki , ukweli wa hicho tunachoombwa kutolea ushahdi, watu wengine huwatumia wenzako wawe mashahidi ili wanufaike na masilahi yao.

Ni mimi: emu-three

No comments:

Post a Comment

Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com