Wednesday, September 12, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-47


 ‘Ni zawadi gani ilitoka kwa mama…..?’ shahidi akawa kama anauliza

Akageuka kumuangalia  hakimu, kama kuhakikisha kuwa hakimu huyo bado anafuatilia maelezo yake,…na hakimu naye akawa amemkazia macho. Hapo shahidi huyu akarizika, na kuendelea kuongea…

‘Najua nilianza kutoa kitabu, eeh dafutari, hicho ni kitabu sema tu hakijapigwa chapa..na mungu akijalia nitakitoa kiwe kitabu, maisha halisi ya mama, au nikiite nani kama mama,


‘Huo ni ushahidi hasa, uliobainisha, …unyama aliofanyiwa mama, na maisha yake baada ya hapo…na kwangu ndio ushahid ulionisaidia mimi kujijua, nimetokea wapi, watu walisema nimeokotwa majalalani…sawa..lakini hicho kitabu kimefichua hilo..kumbe mimi ni..zao la …’hapo akasita kumalizia.


‘Kwahiyo zawadi hiyo ilikuwa hicho kitabu…’akawa anaangalia lile dufutari pale lilipowekwa.

‘Nilipobaini kuwa ni kitabu tu, tena cha kuandikwa kwa mkono, mwandiko mnzuri wa kike,….swali la haraka lilinijia,..kiukweli nilijiuliza mimi mwenyewe, …eeh,… kama mama alithaminisha hicho kitabu na zawadi kubwa sana kwangu, …thamani yake ni nini kwangu,…’akahema kidodo.


‘Sawa nilipokisoma niliona yaliyokuwepo, huenda kwa wengine hayana thamani,,…labda thamani yake ni hiyo, mimi kuumia moyo,…mama alivyoteswa, na…sawa, nilie, sawa…  kupotewa na fahamu, kuwa kichaa..eeh, halafu nikae kimia, si ndio jamii inataka hivyo, uwe muungwana.’akatulia


‘Jamani baada ya hayo, baada ya kutambua hayo, hivi, ni binadamu gani ataweza kuvumilia, au kwa vile sisi ni masikini..au mlitaka mimi nifanye nini, kama mama alifika mahakamani, akiwa anaumwa, akiwa na ushahidi kamili wa mwili wake…hakushinda kesi, je mimi…jamani mlitaka mimi nifanye nini, labda niwaulize hilo nyie mnisaidie…’akasema kwa unyonge, huku akionyesha dalili ya kutaka kulia.


‘Kiukweli…thamani ya zawadi hiyo ni kubwa,japokuwa mama hakumaanisha hivyo, kipesa, au kimali, .ila bila hata kauli, thamani yake ilikuwa kama kuuliza  ..HAKI  YANGU IPO WAPI, …swali kwenu,  JE HAKI HIYO Ilitendeka, ..hahaha, haki kwa mnyonge, lini ikathamaniwa, eeh, niambieni, msiogope kusema ukweli, mnyonge hana haki hapa…’akasema sasa akiwaangalia watu, na baadhi wakapiga makofi.


‘Sihutubii mimi, ila naelezea uhalisia…ili uwe na haki, ni lazima uwe na ushahidi…na ili uupate ushahid wa kisheria ni lazima uwe na wakili..ili umpate wakili ni lazima uwe na pesa, masikin ataipatia wapi hiyo pesa…manielewa nina maana gani, hapa namuongelea mama, masikini ….’akatulia.


‘Haya maswali..nilijiuliza sana mimi, nilijiuliza..na kujiweka sehemu ya mama.., kichwa kiliniuma,..na akili zangu zote hapo niligwaya,.sikupata jibu, nikawaza kupitiliza..nikikumbuka pia kuwa nimenyang’anywa mali halali…kisa, matajiri wape…siwezi kusema kwa vile ni mali ya familia nyingine…’akageuka kumuangalia wakili.

‘Kama ilikuwa mali ya mama mlezi, na mimi ndiye mwanae wa kufikia, na mimi ndiye nilihangaika naye,..hadi..siku ya mwisho…kwanini kauli yake isithaminiwe…niliwaza sana…hadi nati za kichwa zikakatika, ti-ti-ti, uchizi huooo


‘Uchizi ulinianzia hapo ndugu wapendwa,…niwaulize tena, nyie, ningelifanya nini hapo…mmh, mimi kwa udhaifu wangu,…nikaona jibu rahisi,…nitatumia akili yangu, si ndio nimebakia nayo,…akili,….nitafanya vile akili itanituma, labda hivyo ni ujinga kwa matajiri, lakini kwangu,…niliamua hivyo …’akahema kidogo.


‘Nakumbuka sana, kauli ya mama…’…niache ujinga…nitumia akili yangu…’ nami nikaamua kutumia akili yangu,nilitumia vipi basi…’akageuka kumuangalia hakim


‘Hahaha watu wanafikiria kuwa mimi labda ndio nikalitengeneza hilo deni, hahaha, kwanini nifanye hivyo, deni limejileta lenyewe, kulipa deni,..sasa niwaambie wazi, deni kwa deni, japokuwa deni lao, haliwezi kabisa kulipa hilo deni, la mama, na…walichonidhulumu, lakini mimi sijatengeneza deni….’akahema na kumwangalia wakili wa benk, aliyekuwa akikubaliana naye.


Kuwaza sana, kusononeka, sana, na kuumia kila nikisoma kile kitabu, nikawa sasa mtu mwingine….kichaa.


Mhh,nikaanza kuchanganyikiwa …kila nikijaribu kusoma kitabu cha mama, ndio nazidi kuumia,…kulia, kuwaza…unajua kama mama angelijaliwa kuishi,  angelikuwa mwandishi mnzuri sana tu, waandishi wazuri, huandika uhalisia,..na mama aliandika hali halisi iliyomtokea, na inagusa ndani ya moyo…kiukwel,  wema hawana maisha.


Japokuwa alinza kuandika kipindi cha baadae, lakini alijitahidi kuwa na mpangilio mzuri tu, unaoeleweka,.. kwahiyo mengine aliandika kwa jinsi alivyokumbuka. Isipokuwa yale yaliyoendana na tarehe wakati anaanza kuandika,  ndio aliweza kuaandika tukio na tarehe yake…kama mtakavyoona kwenye hilo dafutari..kumbukumbu halisia, au shajara kwa Kiswahili fasaha na kwa kiingereza ..diary..


‘HIYO NDIO ZAWADI YANGU KUTOKA KWA MAMA…


Siku nilipoanza kusoma, ilikuwa ni usiku,…nakumbuka ilifika muda kichwa kikawa kama sio changu, nilipiga ukelele, unajua ukelele, huku naita mama, jamani,…ni mateso gani hayo, ..unyama, hadi mtu anachukua bati lenye kutu, anakata ulimi wa mama, mja mnzito,..hivi jamani,..mnahisi kama ninavyohisi mimi…kama hamna hiyo hisia nyie sio binadamu wa kawaida..


‘Hapana…msiseme kwa midomo yenu huku hamumaanishi hivyo, eti nani kama mama, na kawaelezea vyema, tu, nasikia wakati anaelezea alivyofanyiwa ili bidi awe anaandika,…hahaha, ni nani angelisoma,…dharau…kwahiyo sasa mnataka na mimi nikae kimia,..dunia itanishangaa..naomba mnielewe…maana nimeamua kusema ukweli, na ukweli uwekwe kwenye maandishi..’akatulia

‘Siku nilipomgundua huyo baba…we acha tu, usione watu wanaua, usione watu wanageuka kuwa wanyama..inaumiza, kuna watu wamepitia mateso, na unafanyiwa mateso, huku unakebehiwa, unadharauliwa,…sasa ufanye nini, ujitoe mhanga,…mimi sijui, niambie nyie…’akasema akiwaangalia watu.


Nikawa sasa nateseka na maumivu ya kichwa,…kichwa kinauma kama kinataka  kupasuka,…usiku huo, nilipoanza kusoma..ikafika hatua siwezi tena..…sijui kilichotokea nini..kichwa, eeeh, mara nziiii, giza, hapo tena sikuweza kujitambua, nilipoteza fahamu, sijui.


Baadae,…,..kumbe majirani walisikia huo ukelele, wakafika, wakagonga, kimiaa…mtu nimeshapotea…sipo duniani tena…hata walipoamua kuvunja mlango, mimi sikuwasikia,.waulizeni hao majirani ili mpate ushahidi…kweli walivunja mlango, wakanikuta nipo sakafuni nimpoteza fahamu…waiteni muwaulize si mnataka ushahidi…’akasema

Taabu ikaanzia hapo…

‘Ndugu zanguni, hali hiyo ilinitesa sana, tena sana, kila nikijaribu kusoma hiyo zawadi kutoka kwa mama,  naingiwa na hiyo hali…yaliyoandikwa humo ndani, inataka moyo kuyasoma..ikizingatia kuwa huyo ninayemsoma,.. sio mwingine ni mama yangu mzazi, aliyekatwa ulimi, na ile hali ikasababisha kuleta tetenasi na kuzalisha ugonjwa usiopona…hayo maelezo yapo humo na cheti cha docta kipo humo, na ndio ilikuwa  sababu yake ya kutangulia mbele ya haki, mola aiweke roho ya mama na mama mlezi mahali pema peponi…’akatulia kwa muda,


Baadae…


 ‘Niliwahi kupata nafasi ya kwenda kusoma nchi ya jirani kwa ufadhili fulani, hapo ni kabla sijarudi ..na niliporudi ndio nikakumbuka kuhusu hiyo zawadi, na ndio nikakuta nyumba imeshavunjwa,..nianda mbele na kurudi nyuma, lakini najua mnanielewa, au sio…ukichaa ukawa sasa unaongezeka. Na muda huo natakiwa kuanza kazi…



Usione hivyo, kila ninapozidiwa natamani nifike ufukwenu kupata ule upepo wa kule..ndio maana nikaweza kutengeneza ofisi yangu kule, kule..hadi leo sijaweza kulimaliza hilo dafutari, lote, someni nyie mnaoweza , na labda mtaona ni kisa cha kutunga…’akatulia


 Kazi nilishapata kutokana na akili niliyokuwa nayo, ilikuwa rahis tu, lakini sasa akili, imeshavurugika,..lakini cha ajabu nikiwa ofisini nikatulia, nafanya kazi za watu vizuri tu, ila ikitokea namna ya kukumbuka..na kingine kilichonisaidia…, ni karama aliyonipatia mungu, akili ya kusoma akili za watu wengine,..sijui …lakini ndivyo nilivyokuwa, nasema ndivyo nilivyokuwa, kwasababu hiyo hali ya kusoma akili za watu wengine ishapotea, haipo tena.


 Ilipotea kwasababu gani,…akili yangu ilikuja kutekwa na kitu kimoja,…kisasi..kisasi, kitu ambacho mama hakukitaka..lakini hata hivyo, mimi ningefanya nini, ni lazima nifanye jambo au sio, ..wengine wanasema ilitakiwa nifungue kesi upya…hahaha, nitaulizwa ushahidi upo wapi…ni lazima nitaulizwa hivyo…upambane na yule baba mjanja kama nini…hadi leo kakataa kabisa kukubali kuwa alimfanyia mama hivyo….’hapo akainamisha kichwa chini.

‘Sasa kisasi…’ ikawa ndio dhamirana mikakati yangu, .. hatua ya  kwanza ni kumfahamu vyema huyo baba, huyo aliyemfanyia hivyo mama, huyo mtu ni nani, kwangu mimi, sio baba tena, kwasababu kwanza aliikana mimba, na hata nilipozaliwa alinikana kuwa mimi sio mtoto wake, mimi ni mtoto haramu

‘Sio baba yangu, kwa kinywa chake na matendo yake..’akasema

Upelelezi ukaanza, maana mama mlezi hakuwhai kuniambia hata siku moja baba yangu ni nani, yeye, anasema anayemtambua ni mama, baba yangu hajulikani..kumbe yupo, na kama mama mlezi angelikiuka maagizo ya mama mzazi, akaifungu ahiyo zawadi, huenda angelimfahamu baba yangu ni nani.


‘Nasema hivi, mimi sina baba, kwa mujibu wa matendo yaliyotendeka, na kwa mujibu wa kauli yake…hadi leo,…kwa mara ya mwishi nilimuuliza, akakataa kata kata…sasa mtu kama huyo utamfanya nini,..mimi ndio nijipendekeze kwake,..isingelikuwa shida, ningekubali yaishe,..sio shida,…ila niliposoma hilo dafutari,..thubutu….’akatikisa kichwa.


Nikafanya upelelezi, nikamgundua huyo baba..na siku moja nikakutana naye, wakati huo, huwezi kunijua ni mimi yule niliyekuwa chokoraa..maana sasa ni msomi, na nina kazi,…nilijaribu sana kuipoteza sura yangu ya asili, yawezekana tu, wala sio kwa kutumia madawa…’akatulia.


Sasa katika uchunguzi wangu, nikaja kugundua kuwa, kumbee…huyo baba, ana udugu na huyo mtu aliyenidhulumu ardhi yangu..anayetumia pesa zake kuwasaidia ndugu zake, ambao, wanadhulumu wengine, pesa zake…ndio sababu, ok…pesa ndio sababu au sio…nikaanza mikakati ya kupambana na pesa zake…


Nikisema hivyo wengi wanasema nimekosea, aliyenidhulumu mali yangu, sio huyo, …aliyemfanyia mama mabaya sio huyo ni mtu mwingine, LAKINI wote lao moja,..kama huyo tajiri angelinielewa, asingelinunua hilo eneo…asingetoa ushahidi ambao hana uhakika nao, na hata nilipojaribu kujieleza kwake, hakutaka hata kunisikiliza,..aliishia kunikejeli, dawa ya kuwamaliza wote hao, ni kudhibiti mali yao..PESA ndio ilikuwa inawapa kiburi, si ndio hivyo..


Nikaja kugundua kuwa mzee, yaani, mjomba naye ana udugu na yule msamaria mwema..mtu wa madawa asilia..…mnamkumbuka eeh, mtaalamu,..lakini yeye sio mtaalamu, utaalamu ule aliupata zaidi kutoka kwangu, na hata jina hilo, mimi ndiye niliyekuwa nikimuita wtu wakifika nyumbani kwake, nawachagamkia, mumekuja kwa mtaalamu eeh……hahaha..’akacheka .


‘Mtu yule pamoja ya kuwa anafahamu madawa ya kienyeji, lakini wakati mwingine alikuwa anawadaganya watu kwa ramli za uwongo, baadae akaenda wapi sijui, aliporudi anadai kapata shetani gani anaeweza kumsaidia kuagua, na kupiga ramli, ushetani mtupu…mimi nipo mbali na hayo..nikawa najaribu kumfundisha hiyo karama yangu..akanipenda sana…hakujua lengo langu ni nini…nilifanya hayo, huku jamaa hajui kuwa namchunguza, na kuwachunguza maadui zangu…ilikuwa kazi yangu ya kwanza.



Yaliyoendelea kati yangu na huyo mtu,..ni mengi saa,… nitawachelewesha, nikianza kuyaelezea, muhimu ni kuwa, watu watatu sasa nimeshawafahamu vyema, na iliyobakia ilikuwa kuangalia, nitawafanya nini..kila hatua nikijaribu nahisi nitafanya makosa,..sitaki kumdhulumu mtu…sikutaka kuua mtu, .’akatulia.


 Siku zikawa zinaenda…sijapata ufumbuzi na sijui nifanye nini tena…..’akatulia


Siku zikaenda,…ajira mpya, ikawa inaniliwaza nikiwa kazini, mawazo ya mama , na maisha mengine yanapungua, hapo…akili ninayo, kazi sasa ninayo, lakini moyo hauna raha,…wazo likanijia tu, nifanya jambo, lakini wazo hilo linahitajia pesa, na mimi japokuwa napata pesa, ni ile ya ..kawaida tu,..hapo kwa mara ya kwanza nikaanza kuingiwa na tamaa ya pesa. Ili nifanikiwe hilo jambo langu.


Alipofika hapo hakimu akasema;


‘Muda umekwisha sana, na ..nimekuachia tu, utoe maelezo yako upendavyo,..kinyume na utaratibu, hadi hapo, tunaweza kusema wewe, ..uliyokuja kuyafanya yalikuwa  kulipiza kisasi, sasa nikuulize swali, je katika kulipiza huko kisasi chako, ndio hapo ukatengeneza hilo deni…?’ akaulizwa


‘Samahani muheshimiwa hakimu, mimi sijasema nilitengeneza deni…’akasema


‘Deni la marehemu lilifikaje kwenye akaunti yake,…na kama ni wewe ulifanya hivyo hilo deni lifike kwenye akaunti yake, mbona unamuadhibu mtu ambaye hakustahiki,…wewe kwa maelezo yako, baba yake ndiye alimkosea mama yako au sio, ulimfanya nini baba yako,…?’ akaulizwa


‘Muheshimiwa hakimu, mimi sijatengeneza deni lolote, mnielewe hapo tafadhali, hilo deni wanalijua wenyewe watu wa benki, huo ni wajibu wao, na msinitupie mzigo ambao sio wa kwangu…’akasema na watu hapo wakashikwa na butwaa…hakuwajali, akaendelea kuongea.

‘Kwa maelezo yako umesema wewe na mama yako mnadai pesa nyingi sana , kwa thamani haimithiliki au sio, ndio ukabuni namna ya kulipiza kiasasi , na kisasi hicho ulifanyaje…?’ akaulizwa.


‘Mimi ndio nadai,…nadai mali nyingi zenye thamani nyingi, nadai haki ya mama yangu na mama mlezi…lakini…mmh, habu niliweke hili hivi… akatulia kwanza


‘Hebu fikirieni hilo eneo, lipo sehemu gani…, na sehemu hizo, maeneo yanauzwa kwa bei mbaya sana, mnaweza wenyewe kukisia, na eneno lenyewe sio eneo dogo, ni karibu ekari moja, limeuzwa, na sikupata hata senti moja, je kiukweli , kihalali, hayo malipo, au hiyo mali,  haikuwa ni haki yangu, je thamani yake ni shilingi ngapi eeh, hapo ni eneo, na je haki ya mama…?’ akawa kama anauliza.


‘Utasemaje ni eneo lako, wakati huna ushahidi wa kulimiliki, kwa mujibu wa wanafamilia, wewe sio mwanafamilia, na eneo lilikuwa na familia, au…au kama mama mlezi alitaka wewe urithi eneo hilo…, ushahidi upi wa kukuwezesha itambulikane kuwa hilo eneo ni kwako..?’ akaulizwa.


‘Safi kabisa, mumefika huko ninapokutaka, sasa eeh…nauliza na nyie mnaodai kuwa hilo deni sio la marehemu, ushahid gani mliokuwa nao, si maneno matupu kama yangu, hata kama ni kweli, ushahidi wenu upo wapi..eeh,…hapo sasa jibu mnalo, semeni ..ushahid wenu upo wapi…?’ akauliza akimgeukia wakili wa utetezi wa wanaodaiwa.


‘Ushahidi wetu ni maelezo yako…maelezo yako yanaonyesha dhahiri hilo deni ulilitengeneza wewe kwa nia ya kulipiza kisasi…umekiri mwenyewe mbele ya mahakama…’akaambiwa


‘Mimi nimekiri hivyo, …!! Sijakiri hivyo,…na kiukweli, nyie hamna  ushahidi huo kuwa mimi ndiye nimelitengeneza hilo deni, kwanza kwa vipi hapo mnaongelea benki, ambao wana utaratibu unajulikana kisheria,…deni halitoki hivii hivi…mimi nitawezaje kufanya hivyo,…hadi hapo  hizo ni hisia zenu tu, au sio..?’ akauliza.


‘Ushahidi wetu ni wewe na wenzako, mlioshirikiana nao, wewe umeshasema hayo yaliyofanyika hadi kutokea deni ni kutokana na chuki zako kwa hao watu waliokufanyia mabaya wewe na mama yako, au sio..?’ akaulizwa.


‘Kama ushahid ni mimi na wenzangu, basi hata haki yangu ipo..maelezo yangu, na ushahidi wangu utambulikane, na mashahidi kwa haya niliyoyaeleza wapo,yupo huyo mzee, japokuwa wengine ni marehemu..lakini hapa yupo, yule mzee, muiteni kama hatathibitisha haya niliyowaambia,kuwa ni kweli tupu…’akasema


‘Japokuwa huyo  aliyempa mimba mama yangu akamfanyia unyama, hataki kukiri hilo kosa hadi sasa hivi…’akasema


‘Kama ni hivyo tutaaminije maelezo yako…?’ akaulizwa


‘Maelezo yangu yana  ushahidi mwingi tu..sawa nimejaribu kumfanya akiri, lakini kagoma…lakini dhambi zake zinamtafuna kidogo kidogo,..maana .malipo ya dhambi nyingine ni hapa hapa duniani, ile hali aliyoipata mama, itamtafuna nay eye, na wote  walioshiriki, mmoja baada ya mwingine,watawajibika kwa hilo…’akasema.


‘Kwa kusema hivyo ina maana kuna jambo umewafanyia,..je ni nguv za giza, na je ndio hilo deni, tuambie tusipoteze muda …?’akaulizwa.


‘Mimi sio mchawi, msije kusema, mimi nimewafanyia hao watu kitu chochote, ningelitaka ningelifanya hivyo kwa kupitia marehemu, mtaalamu, aliwahi kunishauri hivyo, lakini sikutaka……’akasema


‘Je ni kweli kuwa wewe na mtaalamu mlitumia nguvu za giza, kuwatesa familia ya marehemu, na hao maadui zako, je ni kwanini ulifanya hivyo, ni ili wakubaliane na hilo deni, si ndio hivyo,…na umekuwa ukitumia nguvu za giza kuwatisha,  si ndio hivyo, ..?’ akaulizwa.


‘Mimi sikuwa na haja ya kufanya yote hayo, na wala mimi sina uwezo huo wa nguvu za giza, mimi nina karama ya kusoma watu, nilikuwa nayo..lakini sikuwa na ..uchawi, hiyo kazi nilimuachia mtaalamu, yeye alijua ni nini cha kufanya, kazi yangu ilikuwa kwenye pesa, maana hawa watu ili kulifanikisha hilo walihitajia pesa, ili baadae lengo lije kutimia na haki ije kupatikana …’akatulia.


‘Haki gani na haki hiyo ungeipata vipi..?’ akaulizwa


‘Haki ipi, ina maana hadi hapo, hamjafahamu haki yangu ni ipi, basi kama ni hivyo, ndivyo…ukweli unakuwa bayana, kuwa watu kama sisi hatuna haki, hata kama tukifanyiwa mabaya, na kama ni hivyo, kwanini tusitafuta namna ya kulipwa madeni yetu,eeh… leo hii nimesimama hapa mahakama, nikitambua kuwa haki yangu itapatikana, mbona haki bado inapingwa,…’akasema.



‘Kwahiyo wewe ulikuwa hujui kinachoendelea kati ya mtaalamu na familia ya marehemu..kuwa huyo mtaalamu ndiye alikuwa akiwatesa watoto wasio na hatia na mama yao, kwanini alikuwa akifanya hivyo, na kwasababu ya deni au tuambie..?’ akaulizwa


‘Nimesema hivi, hiyo sio kazi yangu, kazi yangu ilikuwa kutoa pesa, wao wafanye wafanyalo ili wapate pesa kutoka kwangu..aliyekuwa akijua siri yangu angalau kidogo, ni huyo mtaalamu, …na mambo kama hayo mjuzi wake alikuwa ni yeye, sasa kama aliwatesa watoto wa watu, muulizeni yeye, kwanini mimi nishiriki kuwatesa hao viumbe wasio na hatia, eeh.., haikuwa na haja kufanya hivyo..’akasema.


‘Kwanini sasa huyo mtaalamu akafanya hivyo, au hukubali kuwa alifanya hivyo,..?’ akaulizwa.


‘Kwasababu ..labda, kwa vile walitaka kuhakikisha wao hawagundulikani, au…hata sijui, maana hata maswala ya deni, hawakuwa na ujuzi nalo, walikuwa hawalifahamu hilo, si ndio hivyo…labda kama walifahamu ni baadae sana, lakini hadi hapo, nilipoamua kuwaelezea walikuwa hawalijui hilo, na hadi ilivyobainika, sizani kama wapo waliofahamu kuwa kuna hilo deni ni la nan hasa, ila kama benk  wanavyodai hilo deni ni la marehemu, aliyejenga hiyo nyumba sehemu isiyo halali kwake,…’akasema


‘Una maana gani., kwanini hutaki kuliweka hilo wazi , kumbuka wewe umesema utakuja hapa kuwa mkweli, je huo ndio ukweli wote, kwanini hilo deni huliweki bayana.?’ Akaulizwa.


‘Nina maana gani kwa vipi…hivi kwanini hamuangalii upande wangu..eeh, mnaangalia upande wa ..benki sijui, au wa…je mimi haki yangu ipo wapi, je mnakubaliana na ..hukumu, kuwa hilo deni ni la marehemu au mnapinga, na kama mnapinga kwa vipi, na kama mnakubaliana na hilo deni, je deni langu na waliotangulia, mama na mama mlezo, atalilipa nani, mnanielewa hapo sasa…?’ akauliza.

‘Fafanua…’akaambiwa


‘Kama mnakubaliana na dhuluma hiyo kuwa mama yangu alichofanyiwa ni sawa tu kwa vile yeye ni masikini, eeh..basi, haina haja ya mahakama hii, ..na kuwasaidia tu,..hebu wekeni hayo madai yangu na marehemu wazazi wangu  kwenye thamani ya pesa, …mnaweza kukadria hilo, mtaona kuwa hilo ni deni kubwa sana, kuliko hilo deni la benki, haya ni nani anamdai nani hapo, je hadi hapo hamjanielewa mimi…?’ akauliza


Alipoona watu wapo kimia,akaendelea kuongea…

‘Nawashangaa sana…, nyie hii leo mnahangaika na shilingi ngapi hizo za deni la benki....ni sawa ni pesa nyingi kwa hali ya kipesa, lakini je thamani yake inazidi hayo aliyofanyiwa mama yangu,..?’ akauliza.


‘Haya…achilia mbali, mama mlezi, je thamani yake inalingana na dhuluma waliofanyiwa, haya je inalingana na mali niliyotapeliwa,, huenda mali hiyo mkasema ndogo, mimi sijui..kuna thamani ya eneo na nyumba inathaminika, au sio, hivyo ni bei gani, ..haya pigeni mahesabu ni shilingi ngapi, kama ingelikuwa kuuzwa, jumlisha na hiyo nyumba iliyovunjwa,..…’akawa kama anauliza.


‘Acheni jamani, huyo anayedai, kuwa deni si lake,..ni muongo, hilo deni ni lake,..na benki wanaodai kuwa ‘niaba’…wanadai deni,…, wanamudai huyo mdaiwa..ni sawa, wafanye hivyo, kwa vile wao ni wakala tu,…na wao wametumika hivyo, mnielewe hapo, yaani nawashangaa kwanini vichwa vyenu ni vigumu hivyo…’akasema na kucheka kidogo


‘Una maana gani hapo…?’ akaulizwa


‘Hahaha…mimi hadi hapo nimeelezea vya kutosha, huo ndio ukweli wote…hilo deni ni la marehemu,  kwa maelezo niliyokwaisha kuyaelezea, kama alikubali, eeh, kubeba jukumu la wanandugu zake, akatumia pesa yake, sasa ni wajibu wake kubeba hilo deni kwa niaba yao,, waacheni benki wafanya kazi yao…’akasema


‘Bado tu hamjanielewa hadi hapo eeh…?’ akauliza akiwaangalia mawakili na baadae hakimu.


‘Ndugu usitake kutupotezea muda hapa…tuambie hilo deni limepatikanaje, na ni nani mwenye hilo deni, ni marehemu au..na je benki wana haki ya kulidai hilo deni, wamdai nani ambaye ni halali ya hilo deni, kama wewe ulilitengeneza kwa utapeli wako, kwanini hilo deni walilipe watu baki, wewe si ulitakiwa umdai baba yako au sio, sasa kwanini ukalipeleka kwa marehemu..?’ akaulizwa

‘Hahaha, mimi sasa ninaweza kusema hiyo kazi ni ya polisi, au kama mumeshindwa mtafuteni mtaalamu na mjuvi,..ataweza kuwasaidia kwa hilo, ila mimi nimeleezea ule upande wangu,..zaidi ya hapo mnanipa kazi mimi ya polisi, thibitisheni kwa nyaraka, hilo deni sasa ni la nani..mimi siwezi kufanya kazi hiyo maana  mimi sio polisi…’akasema


‘Wewe mtu vipi,..usitupotezee muda wetu hapa, …ulisema upo tayari kukiri kosa, na upo tayari kubainisha kuwa hilo deni ni la nani,..hapa unaongea kama mtu aliyechanganyikiwa, unawachanganya watu,, awali sisi tulikuelewa,lakini sasa yaonyesha umechanganyikiwa…’akaambiwa


‘Mimi nimechanganyikiwa kwa maelezo hayo…hahaha,…waulizeni madocta kuhusu akili yangu mimi,….…tafadhali, nimejaribu kuwalezea kwa namna ya kipekee kabisa, wenyewe mumeona yaliyotokea, na hayo niliyowaelezea ni ukweli mtupu, sijadanganya, hata kidogo, mashahidi wapo, je deni la benki na deni la wadhulimuwa ni lipi kubwa, ni nani anatakiwa kumlipa nani,…na je si hilo deni sio halali kwa marehemu, chukueni kalama na …mtagundua kuwa, hilo deni bado ni dogo sana.. ..’akatulia

Hakim sasa akawaangalia mawakili wawili,….

‘Kwa kuwasaidia tu,…wajiulizei, je hilo jengo lililojengwa lilijengwa kwenye eneo halali, kama sio halali, hilo eneo ni la nani, walitafute hilo kwanza..na je ni kweli mama yangu aliwhi kutendewa hayo, huo unyama, na huo unyama una thamani gani, ni nani walifanya hivyo,..kwanini hukumu haikutolewa, kihalali,..hiyo sio kazi yangu, au sio, nitakuwa naingilia kazi za polisi, muheshimiwa hakimu, naomba haki itendeke…’akasema huku akiinamisha  kichwa chini kama kuomba hivi…


‘Wewe ulipoanza kuongea awali, ulisema umekuja kukiri kosa, na kukiri kosa maana ni kukubali ukweli….je huo ndio ukweli wa kukiri kosa,..ni nani atakuelewa hapo, au lengo lako lilikuwa kuongelea kuhusu mama yako, ili hakimu akuonee huruma…?’ akaulizwa na wakili.


‘Nyi mlitaka kufahamu  ukweli wa hilo deni, si ndio hivyo, ukweli wa hilo deni ndio huo nimeshawaambia…je waliotenda hivyo, hawana deni…semeni ukweli wenu kutoka moyoni, je ni haki kilichotendeka, hilo deni la benki ni kigezo cha kuivuta mahakama, ije kuwajibika, na nyie watendaji mjue wajibu wenu, ..sasa nimewafafanulia…’akasema



‘Tunachotaka kufahamu kwanza n jinsi hilo deni wanalodai benki, lilivyofanyika, mengine yatafikiriwa na hakimu, ukweli umeuelezea, amesikia, kuna harakati za kuutathimini, kama ni kweli au la..ila kwasasa tunataka kujua ukweli kuhusu hilo deni lililopo benki…’akaambiwa


‘Mimi naona ushahid wangu umetosha, …na kama mtachukua maelezo yangu kama ushahidi basi msisahau kuchukua maelezo ya mama na ya kwangu, kama ushaihidi kwa ajili ya haki ya wazazi wangu, kwa ajili ya mali iliyochukuliwa isivyo halali..kwa vile tu, eti mimi ni mwanaharamu…’akasema na kutulia kimia


Hakimu akageuka na akawa anaongea na wazee wa baraza, baadae akawageukia, watu na kusema;


‘Mawakili wa pande zote mbili waje hapa mbele..’akasema hakimu na mawakili wale wawili wakafika, pale mbele ya hakimu, wakawa wanaongea, kukawa na ubishani fulani,..hasa kwa mawakili hao wawili, baadae hakimu akawa anawaelezea jambo, na baadae wakaambiwa warudi sehemu zao.


‘Hii kesi ni ya ina yake…tumepoteza muda mrefu sana ili kuweza kuipata maelezo y akutosha, ili haki itendeke… na mengi aliyoongea huyo shahidi, yana mantiki, yanakera na kama itathibitika kuwa ni kweli, sheria itachukua mkondo wake,..kwa hivi sasa bado hayana ushahidi wa kutosheleza …,’akatulia


‘Yeye kasema wapo mashahidi wa kuthibitisha hayo, hebu tumsimamisha mzee mtupe tena, athibitishe hayo maelezo yake…, lakini baada ya hapo, tunahitaji, wewe ..uliyetoa maelezo yako hapa utuambie hilo deni limetokaje benki..achilia mbali, ulipizaji wako wa kisasi, tunataka jinsi gani deni hilo lilivyotoka benki na kwenda kwa marehemu, je ni kweli marehemu alikopa yeye, au ni hujuma zako wewe mwenyewe au kuna kitu kilifanyika huko benki…’akaambiwa


‘Sawa muheshimiwa hakimu…lakini bado tunadai ushahidi upande wa wanaodi kuwa deni hilo sio la marehemu, ni haki yao kutupatia huo ushahidi, bila hivyo, mimi yangu yatakuwa ni maelezo tu, na mwisho wa siku benki wana ushahidi wa kisheria, itasaidia nini hapo…sasa kama maelezo yangu bado hayajaeleweka, mimi nitawatupia mpira wanaodai vinginevyo, nitaendelea kuongea tu,…’akasema


‘Mzee mtupe aje sehemu ya mashahidi…’akasema hakimu..


Hakimu aliposema hivyo sauti yake ikamezwa, na ghasia,  kule mlangoni kukatokea ghasia, kuna mtu alikuwa anataka kuingia, na watu wamejazana..kwahiyo ikawa kama ghasia fulani ya kusukumana.


‘Ni nani huyo anayeleta vurugu huko mlangoni…na nyie askari mnafanya nini sasa…?’ hakimu akauliza


‘Ni mimi muheshimiwa hakimu, ..nimekuja kutoa ushahidi unaohitajika..’sauti ikasema


‘Ushahidi gani huo unaohitajika, na ni…, nani kakuambia anahitajia ushahid wako kwa hivi sasa…?’ akaulizwa


‘Ushahidi wa deni, linalozungumziwa hapa, naomba kwa hisani yako niweze kuuonyesha..’sauti ikasema


‘Wewe ni…’kabla hakimi hajamaliza hiyo sauti ikasema


‘Muheshimiwa hakimu…, ili tuimalize hii kesi, huyo shahidi aliyepita ni mjanja, anataka kupoteza muda, ili hilo deni liendelee kueleweka hivyo kuwa benki walilitoa kihalali, kiu ambacho sio kweli,……’sauti ikasema na hakimu akamuangalia wakili anayetetea madeni, halafu wakili wa benki.


Huyo mtu sasa akawa kapewa nafasi ya kupita kwenye kundi la watu…watu wakawa wanampisha kwa heshima sasa…


‘Ni nani huyo, ..?’ akauliza hakimu akiwaangalia mawakili.., na kabla hajajibiwa, huyo mtu aliyeongea kwenye kundi la watu akajitokeza,..


‘Ni mim muheshimiwa hakimu…’akasema


‘Mtu wa jamii…umetokaje hospitali…?’ aliyesema hivyo, ni wakili wa madeni, akimuangalia huyo mtu aliyeingia,, halafu akaangalia kile alichokuwa ameshikilia huyo mtu.


‘Ni nini hicho, …?’ akauliza wakili wa utetezi

‘Ushahidi, ule ushahidi tuliokuwa tukiutafuta ambao ndio utabainisha ukweli wa hilo deni, na shahidi aliyekuwa akiongea analifahamu hilo,…’akasema na hapo wakili  wa kutetea madeni,akamgeukia hakimu na kusema;


‘Muheshimiwa hakimu naomba muda kidogo nitete na huyu shahidi yangu mpya, alikuwa mgonjwa, katika harakati za kutafuta ukweli wa hilo deni,…na sasa keshapata nafuu, natumai baada ya kuongea naye, nitajua kama asimame yeye kutoa ushahid au tumsimamishe mzee mtupe…’akasema wakili


‘Mzee mtupe nimemsimamisha mimi, nataka ahakiki maelezo ya huyo shahidi aliyekuwa akijieleza hapo…maana yeye kaongea mambo mengi, ni lazima hayo maelezo yake yahakikiwe kwanza, kama kweli watu waliumizwa, kama kweli maeneo yaliyochukuliwa isivyo halali,..nataka ushahidi wa hilo, na hayo yanahusiana vipi na hilo deni,…’akasema muheshimiwa hakimu.


 Hapo mzee mtupe akawa keshafika kwenye kizimba cha kutolea ushahidi, na kufuata utaratibu wa kimahakama, baadae akaanza kuhojiwa,..


‘Mzee mtupe unamfahamu huyo mtu, shahidi aliyetoa maelezo marefu ya maisha yake…?’ akaulizwa akionyeshewa huyo shahidi aliyepita


‘Ndio ninamfahamu…’akasema


‘Kwa vipi…?’ akaulizwa


‘Kwanza, nilikuwa simfahamu vyema awali…, kuwa ni nani..kabla hajaniambia ukweli kuhusu yeye,..na huo ukweli kanielezea siku chache kabla hatujakamatwa, na kuletwa hapa…tuje kutoa ushahidi ..nilimfahamu kama bosi wangu aliyeniajiri kama mlinzi na mpelelezi wa mambo yake…’akasema

‘Wewe ulikuwa ukitafutwa na polis kwa makosa gani…?’ akaulizwa na wakili wa madeni

‘Nilifanya kama muajiri wangu alivyonielekeza nifanye,…’akasema

‘Muajiri wako ukiwa na maana gani…?’ akaulizwa

‘Huyo aliyekuwa akitoa maelezo …’akasema

‘Uliambiwa ufanye nini…?’ akaulizwa

‘Nikanyamazishe nguvu alizowekeza marehemu, kuhusu ….’akasita kumalizia

‘Kuhusu nini, elezea…’akaambiwa

‘Kuhusu kuwatesa wanafamilia hao,…’akasema


‘Kwanini wateswe…?’ akaulizwa

‘Hayo anayafahamu huyo mtaalamu,na huyo mwajiri wangu hakulipedna hilo, alipogundua kuwa kuna watu wanateseka, akaniamrisha mimi nifanye juhudi za kidawa, ili hayo mateso yakome…’akasema

‘Ulifanyajae sasa…?’ akaulizwa

‘Niliwahi kuongea na marehemu, mtaalamu, aliwahi kunielezea hizo nguvu zinapatikana wapi, kwahiyo, ilibidi nifanya safari,…nilifanya, lakini pia kuna mambo nilitakiwa niyafanye haraka, kala sijaondoka, ,…ili kuwaokoa watu wengine waliotakiwa kuuwawa ..ilikuwa sio kazi rahisi, ..maana mfani kuna mtu mmoja nitakiwa nimuwahi, asije kunywa simu, nikafika nikakuta tayari keshakunywa, ..nikawahi kumpa maziwa na dawa ya kuondoa ile sumu, polis walinielewa vibaya…’akasema

Hakimu akaingilia kati na kusema;

‘Ngoja kwanza, naona kuna mambo mengi kumuhusu huyo mtu, nia yangu kumsimamisha sio hiyo, ni kuhusu deni kwanza…’akasema hakimu, na wakili aliyekuwa akimuhoji akatulia.


‘Je hayo aliyoelezea, kuwa wewe ulimdhulumu eneo, nyumba, kutoka kwa ndugu yako marehemu, ni kweli, …?’ akaulizwa


‘Siwezi kulikataa hilo,…au kulikubali,… ni kweli dada, au mdogo wangu ..aligawa eneo kwa huyo shahidii, lakini kiukweli, haikuwa ni sahihi, eneo lile lilkuwa mali ya urithi wa familia…’akatulia.


‘Familia kama familia inatambulikana.. , na sisi ndio wanafamilia wa hilo eneo.., ni kweli eneo lile alipewa marehemu kulihudumia, baadae akalimikisha kivyake bila kukubaliana na wanafamilia,…sisi hatukuwa na ugomvi kwa yeye marehemu dada..kulimiliki maana yeye alikuwa mwanafamilia,..na kila mwanafamilia alikuw na eneo lake,  sasa…’akatulia kidogo, akionekana kusikia maumivu.


‘Una tatizo gani…mbona kama unahisi maumivu…?’ akaulizwa


‘Nina maumivu yananitesa sana, upande huu wa kushoto, na..huku kwenye koo, kuna uvimbe..vyote hivyo vinanitesa sana,..na siku za karibuni wameniambia eti nina ugonjwa, ambao…ooh, wanahisi kuwa ni kansa…’akasema na watu wakaguna kidogo


‘Kansa, una uhakika na hilo…?’ akaulizwa

‘Ni kweli, nimepimwa, wakagundua hilo…’akasema

‘Ilikuwaje, ina maana ni kweli alivyosema shahidi..?’ akaulizwa

‘Wameniloga tu hao watu,…nilikuwa nakula samaki mfuka ukanasa kooni, ukawa hautoki, hadi leo, unanitesa sana na huku upande wa kushoto, ni mshutuko,..niliupata mshutuko, basi nikahis kitu kama sindani ikichoma,..na imekuwa ikiendelea hivyo hivyo hadi leo, nateseka sana…’akasema


‘Sasa kwa kauli yako ni nani wanakuloga..?’ akaulizwa


‘Hata sijui…nahisi ni hao watu wanaodai mali isiyo halali yao…’akasema akionyesha kuogopa


‘Sasa tuambie ukweli..elezea ilikuwaje kama mlikuwa na maeneo yenu kwanini sasa mkataka kuchukua na eneo la dada yenu wakati mnafahamu ni mali yake halali, je uhalali wa mali yake ni upi kama haruhusiwi kufanya apendavyo..?’ akaulizwa


‘Ni mali ya familia, na isingelikuwa ni tatizo , kama angeliendelea kulimiliki yeye, lakini tatizo ni kwasababu alimrithisha mtu baki, …sasa kila mmoja akifanya hivyo, kizazi cha familia husika kitapatia wapi eneo, hamuoni kuwa maeneo yataishia kwa watu baki…’akasema.


‘Swali hapo, je ni kweli huyo marehemu dada yako, aliamua kwa hiari yake, kulimilikisha hilo eneo husika na nyumba…, kwa huyo shahdii na wewe ulikuwa unalifahamu hilo…?’ akulizwa.


‘Ndio lakini…muheshimiwa hakimu…’akataka kujitetea, lakini wakili wa benki akasema;


‘Inatosha, jibu lako limetosha usieleze usiyoulizwa…’akasema huyo wakili, hakimu akasema,

‘Huyo ni mtu ninamuuliza mimi maswali, nataka uelezee…’akaambiwa

‘Sisi kama familia tulikaa kikao, tukajadiliana, tukaona sio sahihi, na hayo yalifanyika hata wakati marehemu yupo hai, lakini yeye aliamua kufanya hivyo, kutokomoa kwa vile yeye aliona hana matoto na hapendi watoto wa ndugu zake wafaidike na urithi w a mabau zetu…’akasema

‘Lakini umekubali kuwa eneo hilo lilikuwa halali kwa dada yenu, kama ilivyo kwenu, kila mmoja ana eneo lake, haijalishi kuwa ni mwanaume au ni mwanamke.. si ndio hivyo…?’ akaulizwa

‘Ni halali kwake kwa vile lipo mikononi mwake, lakini bado lilikuwa linatambulikana ni la familia, yeye ni mmoja wa wanafamilia, …sasa ikitokea yeye kafariki, eneo hilo hurudi kwenye mikono ya familia, kwa manufaa ya familia,…maana maeneo yote ni haki ya damu ya familia, sio haki ya damu nyingine za kurithi,..ndio mila zetu zilivyo…’akasema huyo mzee.

‘Lakini eneo hilo mlikuja mkaliuza kwa damu nyingine isiyo ya familia, kuna tofauti gani hapo…?’ akaulizwa

‘Limeuzwa kwa makubaliano ya wanafamilia wote, na kilichopatikana kimegawanywa kwa wanafamilia wote, ..na tumefanya hivyo, ili isije kuleta fitina baadae..hayo ni mambo ya kifamilia, na kisheria yanakubalika, …sijui kama nimekosea, kama nimekosea, naomba nirekebeshwe…muheshimiwa hakimu,…’akasema

‘Unaweza kurudi sehemu yenu ya mashahidi utaitwa, ukihitajika tena…’akasema hakimu.

Baadae hakimu akaangalia saa yake…, halafu akamuangalia wakili wa utetezi wa madeni, huku akisema

‘Muda umebakia kidogo, je wakili umeshamaliza kuongea na shahidi wako mpya..?’ akaulizwa

‘Nimeshaongea naye, muheshimiwa hakimu…na ningelipenda mahakama yako tukufu, imruhusu shahidi wetu aliyefika, asimame , ili aweze kutoa ushahidi ambao mahakama inautaka, ushahdi utakaothibitisha hilo deni ni la nani..’akasema hakimu na wakili wa benk akataka kutoa pingamizi, lakini baadae akasita.


‘Kuna pingamizi lolote kutoka kwako wakili wa benki ..?’ akauliza hakimu…wakili wa benki akasogea mbele, akasimama, na baadae akamuangalia hakimu, akasema;


‘Ndio nina pingamizi…..’akawa anafungua makabrasha yake



WAZO LA LEO: Kwenye kuitafuta haki, tusiangalie ile haki inayobeba ubinafsi wetu tu, ya kuwa hilo lifanyike kwa vile tu litasaidia masilahi yanayoigusa nafasi etu, au masilahi yetu. Haki ya kweli huangalia pande zote, kuwa lifanyike hilo kwa masilahi ya wote hata kama kwa muda huo halitagusa nafasi zenye masilahi yetu. Haki iwe kwa wote sio kwa masilahi binafsi, huo ndio uadilifu.

Ni mimi: emu-three

1 comment:

  1. Way cool! Some very valid points! I appreciate you penning this post plus the rest of the website is very good.

    ReplyDelete

Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com