Thursday, September 6, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-44



Mimi kiumri bado ni mdogo sana, lakini ilibidi nipambane na watu wazima walionizidi sana umri, wengine sawa na baba zangu au babu zangu..na ilibidi nifanye hivyo, na huenda ni kutokana na maombi yangu kwa mungu, kuwa anijalie niwe mkubwa, niweze kulipiza kisasi cha mama yangu..

Kisasi..ndio kisasi…japokuwa kwa maandishi mama alisema nisije kufanya hivyo, kwani mungu pekee ndiye anaweza kulifanya hilo.

Nashukuru mungu kuwa  mwili wangu umekuwa kwa haraka sana, na akili yangu ya darasani ilikuwa kubwa, kwahiyo nikasogezwa madarasa mbele, na bado nilionekana ni zaidi ya wenzangu, ..nimeanza kazi nikiwa mdogo sana, hata nikitaja umri wangu watu hawaamini, kutokana na umbo langu kuonekana kubwa.

 Ili mnielewe vyema, nitaanzia pale mama yangu alipokuwa mfanyakazi wa ndani, ..kwenye familia ya mtu aliyempachika uja uzito, ulionizaa mimi,..’akasema na kutulia kidogo.

‘Kipindi hicho mama alikuwa bado mdogo tu, na uja uzito huo aliupata kwa kuwekewa madawa ya kulevya, na kijana wa  humo humo ndani, ambapo mama alikuwa akifanya kazi za ndani.

Siku hiyo alipowekewa madawa hayo, watu w humo ndani hawauwepo, zaidi ilikuwa yeye na kijana mmoja wa humo ndani…..mama alipozidiwa ndio akafanyiwa ukatili huo, na huyo kijana.

Kiukweli kitendo hicho  ilikuwa ni mara ya kwanz kwa mama, na tendo hilo lilikuwa la kwanza kwa mama, na haikuwahi kutokea tena, kukutana na mwanaume mwingine, ndivyo alivyoandika mama..na kutokana na tendo hiloa mimba ikatengenezwa.

Kwahiyo mama alibeba mimba kwa njia ya kubakwa…na haikuwa hiari yake,…na hajui kabisa mwanaume aliyetembea naye kwa hiari yake, ..zaidi ni matendo ya kuzalilishwa tu, kwa nguvu…na hilo tendo la mwanzo lililopa mimba, hakuwa na ufahamu nalo…maana lilifanyika akiwa hana fahamu

‘Naliongelea hili ili kuondoa tuhuma dhidi yake kuwa eti mama alikuwa changudoa…sio kweli, muogopeni mungu wenu, na nani anaweza kuja kuthibitisha kuwa kweli mama alikuwa changudoa, kwa watu wanaomfahamu, aje mtu hapa mbele,athibitishe hilo kwa kiapo mbele ya mungu,….’akageuka kuangalia huku na kule.

Hakuna aliyejitokeza…

‘Aje ili na mimi niwe na ushahidi huo, kama kweli mama alikuwa hivyo…’akasema na watu walikuwa kimia.

‘Baadae ikagundulikana kuwa mama ana ujauzito, na mwenye nyumba alishampa masharti hayo kuwa yeye kwake mfanyakazi akibeba mimba, ndio kwaheri hakuna cha mjadala, …hutakiwi hata kubembeleza..na kweli familia hiyo haikuwa na msamaha kwa makosa kama hayo.

‘Nakuona siku hizi umebadilika kwa vile unapendeza…’alisema mama mwenye nyumba, alipomuona mdada nikiwa na maana mama yangu, akiwa na mabadiliko badiliko…umri kama huo wasichan hupendeza…

‘Lakini mama mimi sina tabia hiyo chafu, siwezi kuwa hivyo kwasababu najua mimi sina baba wala mama…’akasema mama.

‘Sawa mimi nakuangalia tu, ipo siku ukweli  utasema na kumbuka masharti yangu, mimi sitaki hata kukaa kikao…ukibainika una mimba.., unaondoka, unaondoka,…unasikia…’akaambiwa.

‘Sawa mama, mimi nitafanya hivyo, …sitakubali kuhadaiwa, maana najua nilipotoka,…’akasema huyo mdada..

Kijana wa hapo nyumbani anayasikia hayo..roho inamuuma, ..kijana huyo alikuwa muhuni sana, lakini akijitahidi wazazi wake wasifahamu,…ila huyo mdada alishamfahamu, kwani muda mwingi anamuona huyo kijana akitembea na wasichana, kwa siri, lakini asingeliweza kusema.

Huyo kijana alipoona mdada anapendeza, akaanza kumtongoza, mdada akamkatalia kata kata…

 Haya likatokea,…mdada huyo maana namuita mdada, kwa enzi hizo hajanizaa, akafanyiwa huo unyama, na aliyemfanyia ni kijana wa humo humo ndani, alihangaika mpaka akapata hayo madawa, na alifanya hivyo baada ya kujaribu kila njia, akakatakiwa.

Baada ya kukataliwa ndio …, akaona atumie mbinu hiyo…na kwa kipindi hicho, huyo kijana alikuwa akiishi humo na wazazi wake baada ya kufeli kidato cha nne, akawa mpiga debe, mara anafanya shughuli hii na ile,…hana shughuli muhimu, ila amekuwa akiwadanganya watu kuwa kasoma sana, …na mengi kama anavyosikika, akisema mitaani,..wenzake, ndugu zake wa kiume walikuwa hawaishi humo, wengine walikuwa masomoni nje, au wanaishi kwingine. Na wanawake walikuwa wameolewa.

 Na siku mdada ilipogundulikana akafukuzwa..tena ilikuwa ni usiku…uone jinsi watu hao walivyo,.,hawakutaka hata kumuuliza hiyo mimba ni ya nani…usiku huo angelienda wapi, akawa analia kuomba asikilizwe..lakini hakupata nafasi hiyo, hakusikilizwa,…akafukuzwa kama mwizi.

Ilibidi alale upenuni mwa nyumba,…akilia, hakuna kulala hapo, analia tu, na bahati nzuri, hawakutoka nje kuangalia kama kaondoka au la, kwani kama wangelimuona hapo nje, wangelimfukuza pia,..na muda huo akawa anajiuliza aende wapi, wakati yeye huko kijijini hana mama wala baba au ndugu wa kumtumainia.

Yeye, kwa kifupi, alizaliwa kwenye mazingira magumu, na mzazi ambaye aliletwa hospitalini, na jamaa wakamtekeleza,…akazaa na mama yake hakuweza hata kumuona, alifariki baada ya kujifungua alikuwa na tatizo la damu, na..hata sijui…,

Mama ndio akazaliwa,…akawa analelewa hapo hospitalini baadae akapata msamaria mwema,..na baadae ndio akapata huyo muajiri wake wa kazi za ndani…nangea kwa kifupi,

Yule msamaria mwema aliyemlea kule kijijini akawa kahama, na haijulikani alihamia wapi,..je usiku huo angelienda wapi, na hata kukipambazuka ataenda wapi..kwahiyo mama alikuwa yatima asiye na wazazi, wala ndugu.

Kwahiyo naweza kusema mimi asili yangu ni kizazi cha mitaani,..na kwa dharau wakati cheti kinaandikwa, muandikaji jina ndio akaandika ‘majalalani’ naweza kusem..aliandika hivyo kwa dharau, na ndio asili ya jina langu,..na hilo la moto nikaja kuliongezea mimi baade nikiwa shule.
Ni kwanini moto…akili za shuleni zilinituma kuwa mimi kama asili yangu ni majalalani, basi hayo, majalala nitayachoma moto…awali ndio nikaficha hayo majina, na..mtu akiniuliza nasema hivyo, jina lako nani,…emu al emu…maana huwezi kujiita ‘maozo al majalalani…na hii AL…mhh, …ni katika kutamka tu, labda ilikuwa ni ‘L’.. Lakini badae nikalipenda hilo jina.

 Asubuhi mama akamsubiria huyo kijana aliyempa mimba, akamwambia...awali huyo kijana labda kwa kuogopa, akasema atamsaidia, maana alijua kitakachotokea kwake, zaidi alimuogopa sana kaka yake ambaye ndiye aliyekuwa msaada wake kubwa, kamsomesha, na bado akafeli, nab ado huyo kaka yake alikuwa tayari kumsomesha zaidi, ili alipewa masharti awe kijana mwema,..akawa anadanganya kuwa kweli yeye ni kijana mwema,

Tatizo la mama, alijigundua mapema kuwa kabeba mimba baada ya kubakwa, lakini aliogopa, kusema akijua aliyefnya hivyo ni mtoto wa bosi..hadi alipokuja kugundulikana, na akawa hana ujanja tena, akafukuzwa.

Sasa huyo kijana  akamwambia…

‘Mimi nitakusaidia, ila usije kunitaja…’akasema

Mama hana jinsi akakubali…

Hebu fikiria huyo kijana angelimsaidia nini, mtu mwenyewe hana mbele wala nyuma, kula kulala…

‘Ok, usijali mimi nitakusaidia,  nitakutafutia sehemu ya kujihifadhi, ila usije kunitaja kuwa ni mimi nimekupa hiyo mimba…’akaambiwa

‘Sawa mimi nitafanya nini..wazazi wako wamenifukuza…’akasema mama

‘Usijali, ni kawaida tu…’akasema kijana

Ilibidi, mama kwa kuogopa akakubaliana naye, ..hakujua kuwa mwenzake ana lengo gani. Kijana huyo alikuwa keshaanza maisha ya utapeli,..kwasababu ya kuongea sana…alikuwa anaweza kudanganya watu, wakamkubalia.

Mama akapelekwa kwenye chumba kimoja, akalipiwa miezi mitatu,..akawa anaishi humo, si chumba cha maana,…akatafutiwa godoro la kuokota tu, na vifaa kidogo vya kujikimu, basi akawa anaishi hapo, siku nyingine anapewa  pesa za matumizi ,  kutoka kwa huyo jamaa, akidanganya huku na kule, au kuiba huko nyumbani kwao..basi siku zinakwenda, mama yeye alikuwa hajui njia yoyote ya kujiingizia kipato.

Siku zikaenda, ikafikia muda hata jamaa haonekani kabisa, ikabidi mama amtafute hadi  nyumbani kwao, maana kodi inahitajika,…ipo siku moja alimkuta kaka yake huyo kijana, huyo kaka yake akamfurusha kwa mateke na magumi…hakuamini..sio tabia ya huyo kaka, maana huyo kaka alikuwa ni mtu mwema sana kipindi anaishi hapo, imekuwaje sasa amchukie hivyo..

Alikuja kugundua kuwa ni fitina …za kuwa yeye alikuwa muhuni,…changudoa, anajiuza usiku,… anatoka usiku kwenda kwa wanaume, ndio akabeba mimba,..na mengine ambayo..hayana  umihimu kuyataja hapa, kwahiyo kaka mtu huyo akawa anamchukia kweli, huyu mdada, hakutaka hata kumuona.

 Siku alipokwenda hapo, akafukuzwa, taarifa ikafika kwa huyo jamaa aliyempa mimba, maana siku hiyo hakuwepo, alikuwa chuo, kuna chuo alikua akisomea, ufundi ufundi wa magari..

Basi aliporejea ndio akasikia hivyo kuwa mdada alifika hapo,..jamaa akahamaki, ila hadi hapo ilikuwa haijajulikana kuwa ni yeye kampa mimba huyo mdada.

Usiku ule ule, huyo jamaa  akawatuma vibaka, wahuni wa mitaani, wakafika hapo kwa huyo mdada, kwenye hicho chumba walichomfanyia mama,  ajuae ni mungu pekee..karibu mimba itoke…aliponea miujiza ya mungu tu. Kutokana na hiyo hali, akawa ameteguka ubavu mmoja, kwahiyo akawa anaishi na mateso hayo, mimba inakua..
Ikabidi sasa awe omba omba…na siku moja akakutana na tajiri mmoja… akamuomba msaada na huyo tajiri akaamua kumsaidia, …akawa anapata pesa ya kujikimu, ikaja kugundulikana kwa huyo jamaa kuwa mama ana mfadhili fulan tajiri..

Yule jamaa aliyempachika mimba kuona hivyo, akawaita jamaa tena wakamfuatilia hadi huko alipohifadhiwa, sasa alikuwa akiishi sehemu nyingine ambayo alikuwa akihifadhiwa na huyo mfadhili,  siku hiyo ndio ilipangwa kifo chake,…walimzalilisha wakampiga kipigo cha mbwa,…

‘Kwanini unataka kunuia mimi, mbona nilishakoma kuja kukusumbua, huyo mbaba, kaamua kunifadhili tu, ana familia yake hana tabia mbaya kabisa..?’ akauliza mama.

‘Huwezi ukatembea na tajiri yule unamfahamu wewe, hujui yule ana udugu kwenye familia yetu, je ukija kumwambia ukweli, kuwa hiyo mimba ni ya kwangu…wewe unataka mimi nije kunizalilishwa, lazima ufe..’akaambiwa.

‘Basi nisamehe, ..ili nijifungue salama…’akasema

‘Hutajifungua salama, ukijifungua salama ni nani atamlea huyo mtoto,  nataka upotee kwenye hii dunia na huyo mwanaharamu wako…’akaambiwa

 Ni kweli alipigwa, hadi kutaka kupoteza fahamu,  kabla hajapoteza fahamu aliwahi kukimbia,…wakati anakimbia akawa anarushiwa mawe, huku wakiita changudoa, Malaya, kafumaniwa..maneno kama hayo ili watu wahisi ndio tabia yake,…

Mama alikimbi hadi nguvu zikamuishia, ikafika sehemu akashindwa, na jamaa mwenyewe akamuwahi, kwa teke la nyuma lile la kurukia, mama akadondoka paji la uso, na uso, uliwahi kwenye jiwe,…hata kabla hajatulia jamaa wengine wakaja..hata siwezi kusimulia kilichotokea hapo, …’hapo akatulia, akijizuia kulia.

Walijua ameshakufa…wakamburuza  hadi kwenye bonde.

‘Huyu anaweza akapona, tukate huu ulimi wake..’akasema huyo jamaa yake..wakawa wanahangaika kuvuta ulimi, wakiwa na bato lenye kutu wakaanza kuukata huo ulimi..angalia ni unyama gani, sema muda huo alikuwa kapoteza fahamu.

Sasa wakati wanahangaika kuutoa ulimi wake..huku wanajaribu kuukata, wakasikia sauti, ikabidi wamtupe hivyo hivyo huko bondeni,…wakijua atakuwa keshakufa.

Huko alidondoka vibaya sana….na bahati nzuri ndio akakutana na mtu mmoja alikuwa akitafuta madawa, bonde hilo lina miti miti..huyo mtu alipomuona na hiyo hali akajua ni maiti,…kwanza aliogopa hata kumsogelea, mdomo umejaa damu umevimba..kichwa halikadhalika, hapa mbele kumetuna..mama hadi anafariki hapa mbele kumatuna.

Huyu mtu alipochunguza vyema akaona huyu mtu ana uhai, akatumia dawa zake kumpatia mama huduma ya kwanza,..dawa zake zilikuwa nzuri kwakweli, zikamsaidia mama.

Baadae huyo mtu akatafuta njia za usafiri akamfikisha hospitalini,..ilikua kituo kidogo tu, akawaomba wamsaidie huyo mama,..maana yeye kamuokota tu, na hajui kapatwa na nini, pale kituoni awali walikataa, wakijua hiyo ni kesi, lakini baadae wakaamua kumtibia…ila wakafika sehemu wakaona ni kazi ngumu kwao.
,
‘Huyu inabidi apelekwe hospitali kubwa…’wakashauriwa

‘Ni nani atafanya hivyo, mimi simjui kama mnataka nyie fanyeni hivyo…’akasema huyo msamaria mwema, pale hospitalini walikuwa hawana huduma za kumsafirisha huyo mama, basi wakawa wanapanga kesho kesho..siku zinaenda,…mama akawa na unafuu fulani, lakini kumbe ule unafuu ni wa nje tu, mbavu bado zinamtesa,…mdomoni kwenye ulimi kumeaathirika,na muda huo hawezi kuongea.

Miezi  tisa inakaribia,…na muda wote huo, aliyekuwa akimsaidia ni huyo mbaba,…muuza madawa ya kienyeji…kwani baadae alimchukua huyo mdada mwenye mimba,  akawa anaishi kwake…

Wakati anakaribia kujifungua, hali yake ikawa mbaya ikabidi sasa apelekwe hospitali kubwa,..huku hawakuamini, mtu yupo na hali mbaya vile, …ikawa ni kesi, lakini ikanyamazishwa kiaina,..mama akatibiwa, lakini akawa hawezi kuongea, …na ikagundulikana kuwa kwenye ubongo kuna athari, ndio maana kapooza upande mmoja.

Akaendelea kutibiwa hadi ikafikia kujifungua,…akajifungua kwa upasuaji. Wakati anajifungua, madocta, walisema, ni yeye au mtoto kupona..mama akasema bora afe yeye tu, wamuokoe mtoto wake.. , bahati nzuri wakapona wote,…ilipangwa mama apitie mateso hayo, aje kumuona mtoto wake..

Kwa hali aliyo nayo, …japokuwa kwa muda wanasema ni nifuu, lakini sio nafuu ya mtu wa kawaida, mate yanamtoka ovyo mdomoni…upande mmoja hauna nuvu anakuwa kama anajiburuza hivi..ikaja kugundulikana kuwa ana mtindio wa ubongo..na zaid kutokana na ulimi kuharibika, akawa hawezi kuongea.

Kuna tatizo lilikuwa halijagundulikana, lilikuja kugundulikana baadae.. ulimi wake ukawa unavimba…hiyo ikawa inamtesa sana…na ilipoendelea kwenye matibabu wakagundua kuwa kidonda kile kimetengeneza tetenasi, lliyopelekea kutokea kansa…na imeshafikia kwenye hali mbaya.

‘Huyu kupona ni miujiza ya mungu…’wakaambiwa watu waliokuwa wakijaribu kumsaidia.

Kipindi hicho bado nanyonya,ikabidi ashauriwe, aniachishe ziwa…kuongea na yeye ni kwa maandishi,…uzuri pamoja na hayo mama bado alikuwa anaweza kuandika, …wakataka mimi nichukuliwe nikalelewe kwenye vituo vya kuelelea watoto mayatima
Mama akalipinga hilo, akaandika kuwa atanilea yeye mwenyewe, wakataka kutumia guvu, wakanipeleka huko, mama akapagundua, akaja,…hutaamini mama aliamua kukaa na mimi kituoni hapo akininyonyesha hadi …’hapo akatulia,..

Jamaa alishindwa, akalia..

‘Sitakiwi nilie …’akasema, watu wote kimia.

Katika harakati hizo, kulitokea watu wakafuatilia hadi wakaja kugundua kuwa aliyenisababishia hayo yote ni nani,…akaja kukamatwa, na kufunguliwa mashitaka, wakati kesi inaendelea mama, akaitwa kuthibitisha kuwa huyo ndiye aliyemfanyia hivyo, akathibitisha kwa maandishi,…jamaa sasa ikawa kwenye wakati mgumu, maana kesi ilishamgeukia huyo jamaa, ..japokuwa ushahid wa moja kwa moja haukupatikana, kama walivyodai wao.

 Bahati nzuri kwao, ndugu yake aliyekuwa ulaya akawa yupo hapo kipindi hicho, yeye akamuamini ndugu yake,  akamtafuta wakili ambaye alisimamia hiyo kesi. Ikaja kuonekana yeye eti hana kosa,… hakuna ushahidi wa moja kwa moja,…eti kweli mama alikuwa changudoa, na akapigwa …katika wizi..watu wakathibitisha hilo.

Waliothibitisha hayo, wa kwanza ni huyu huyu baba mlezi, muuza madawa, na wa pili ni mzee mmoja hivi…wakadai wanamfahamu mama, na tabia yake hiyo chafu, walitoa ushahidi mwingi tu, wa uwongo,…kuwa mama aliwahi kufamaniwa mara nyingi akakimbizwa na mawe… na kwa ushahidi huo ikaonekana ni kweli, kuwa mama alikuwa changudoa, alikuwa mwizi, anawaibia wanaume aliotembea nao.

Kesi ikaisha jamaa, akaachiwa, na alipachiwa akaapa kuwa mama atakufa tu, …hajachoka naye ni kwanini kamzalilisha…, alisema mama akiendelea kuwa hai, anaweza akamtuungia kesi nyingine ya uwongo, na mimi sio mtoto wake, mimi ni matokeo ya uchangudoa wa mama….

Na kipindi hicho, hali ya mama ikaendelea kuwa mbaya, na..ndio hivyo tena mapenzi ya mungu yakatimia, . ikafika muda wa mama kupumzika kwa amani, baada ya mateso marefu, akaiga dunia..aliaga dunia, nikiwa pembeni yake, na haikujulikana hadi siku inapita, mimi najua mama kalala, sitaki kumuamusha,..nilishakuwa kuwa, lakini bado mtoto..sio ule wa kutambua jambo..ila naikumbuka hiyo siku.

Sasa wakati mama anafariki kumbe aliandika yote yaliyompata, kutokea anavyojua kuhusu kuzaliwa kwake, hadi siku anakaribia kukata roho…aliweka na ushahid kadhaa wa kuthibitisha hayo, picha..nk, ili nije kuziona, na siku anakaribia kufa, akamkabidhi hilo dafutari aliloandika mambo yake yote ni kubwa,…akamkabidhi huyo mama mlezi wangu ambaye aliapa kuwa atanisaidia…aliambiwa aje kunipatia wakati nimeshajitambua.

Hapo shahidi huyo akatoa hilo dafutari….

‘Humo ndio niligundua maisha yangu, wapi nilitokea hadi hapo mama alipofariki,…kuna watu walinisaidia kunielezea mengine, nilifanya uchunguzi wangu wa siri…ndio maana kuna mambo mengine nilikuja kuyaongezea kwa karatsi za ziada, utaona nimezibandika kwa gundi.

Nilikuja kugundua kuwa huyo baba mfadhili wa kwanza wa mama, alikuwa na usuhuba na huyo jamaa aliyemtekeleza mama, ndio maana baadae aliamua kumfukuza mama nyumbani kwake. Na kukubali kutoa ushahidi wa uwongo, na …kama mlivyoona awali, kumbe huyo jamaa pia ana udug u na huyo mzee mwingine. Huyo mzee mwingine alikuwa akimtambua huyo binti tokea alipoletwa kutoka kijijini. Alitakiwa asema ukweli, lakini kwa sababu ya pesa hawakutaka kuusema huo ukweli.

‘Hadi leo hakuna amediriki kuusema huo ukweli, ndio maana nilitaka huu ukweli wote uje kujulikana hapa mbele ya mahakama, ili ibakie kuwa kumbukumbu ya kudumu, na isije kupotoshwa…na haki itendeke...’akatulia.


Na aliyefanikisha hivyo kwa pesa zake, ni huyo ndugu aliyekuwa akisoma ulaya, na kufanya kazi huko ..ambaye baadae alikuja kujenga nyumba ya aina yake.
Kila nikiiona hiyo nyumba, nahisi unyama aliofanyiwa mama, nahisi jinsi gani matajiri walivyo, wanatumia hata pesa zao kuwadhulumu watu wasio na hatia,..niliapa, kuwa ipo siku nyumba hiyo itawaka moto..

'Siku nilipokabidhiwa hili dafutari, nikasoma maisha ya mama yangu, nililia sana, hadi kupoteza fahamu,..na kila nikitaka kusoma, najiwa na hali hiyo, na sijaweza kusoma hili dafutari lote, na ndio nikaanza kupatwa na matatizo ya kichwa...kuwaza sana...ndio maana nimekuwa nikijitenga na watu, huko nitalia...sasa sijui jamani, hivi kwa hali hiyo mlitaka mimi nifanye nini...?' akawa kama anauliza

'Nishitaki, ...nishitaki kwa nani, wakati..mama alisaidiwa hadi mashitaka yakafika sehemu kama hii, kulitokea nini....hivi masikini kama mama,..masikini kama sisi..japokuwa mimi sasa sio masikini, hata hivyo, hiyo haki nitaipataje..hapana, niliona ni lazima na mimi nifanye jambo, jambo ambalo hata mimi nitaifurahisha nafsi yangu...'akatulia

 'Na mtaniuliza ni kwanini sijapenda kutaja majina ya hao wahusika,..hapa…kwa vile kwanza hamjaniuliza niwataje…, lakini pia hakujathibitishwa kuwa kweli hao watu ndivyo walivyo..., sipendi kulilazimisha hilo, ila ukweli ndio huo, hao watu ndivyo walivyo, hata wakijipaka mafuta...…'akatulia

'Sasa ..hiyo ni sehemu ya kwanza ya maisha , ya wapi nilipotokea….'akainamisha kichwa, na alipoona kimia, akainua kichwa na kuuliza;

‘Je niendelee sehemu ya pili…au kuna maswali..’ akauliza.

Hakimu akatoa leso mfukoni mwake na kufuta machoni, yaonekana alikuwa akizuia machozi...au ni kuchoka,..haijulikani.

‘Ni kweli hayo uliyoyaongea…?’ akaulizwa na hakimu.

‘Ushahidi wangu kwa hayo niliyoyaongea ni hilo dafutari,na tangazo la kuzaliwa kwangu ambali lina jina langu,...na badhi ya picha za mama, aliwahi kupiga picha, ..zipo humo ndani, nimezibandika.....na kwa upande wa mashahid wa kwanza alikuwa ni marehemu,najua yeye alivyo...sijui kama angeendelea na msimamo wake huo, japokuwa yeye alikuja kuniambia anisaidia kulipiza kisasi..

'Hata hivyo, kwa hapo, yupo shahidi mwingine  …’akasema

'Ni nani huyo...?' akaulizwa..na hapo akasita kumtaja.

'Mahakama inataka kumfahamu..kabla hatujaendelea...'akaambiwa

'Ni huyo mzee,...'akasema.

‘Huyo mzee gani…?’ akaulizwa

‘Mzee mtupe…mlinzi wangu…’akasema.

‘Kabla mzee Mtupe hajalithibitisha hilo, nawapatia mawakili nafasi ya kumuhoji huyo mtu, ….japokuwa muda umekwisha..na kama nilivyosema kesi hii imekuwa na mambo tofauti ya utaratibu..nimeona niache hiyo hali iendelee , kwa vile kesi yenyewe ina utata mwingi, na hadi hapa, sijaona ushahidi wa kutosha,...'akasema hakimu.

Wakili wa kutetea wanaodaiwa akamgeukia huyo shahidi na kuuliza..

‘Wewe kwa kauli yako umesema kuwa, ni kweli hilo deni ni la marehemu, lakini hadi hapo hakuna sehemu inayosadikisha hilo, je hayo maelezo yako yatasadikisha vipi hilo, kinachoonekana hapo ni chuki ya kulipiza kisasi tu…?’ akaulizwa na aliyejibu swali hilo ni wakili wa benki, akasema;

‘Shahidi ameshasema hilo deni ni KWELI NI LA MAREHEMU, unataka asema nini zaidi, kama umeyaamini hayo mengine, yaliyofanya awe na chuki, ya kulipiza kisasi,  kwanini usiamini hiyo kauli yake pia…’akasema wakili, na sauti ikasikika kutoka kwa watu waliofika hapo;

‘Hilo sio deni la mume wangu, mimi sikubaliani na hiyo kauli mume wangu aliingizwa kwenye matatizo hayo bila ya yeye mwenyewe kufahamu undani wake…’aliyesema hivyo ni mama mjane bila kuruhusiwa, na shahidi akamwangalia yule mama kwa makini,…

‘Muda umekwisha, kesi itaendea…’

NB: Kesi inaendelea, je ndio haki itatendeka, au …


WAZO LA LEO: Kila mzazi huvutia kwake , kila mwenye tatizo, huangalia upande wake zaidi, na kusema labda tatizo lake ndio zaidi ya mwingine. Haki ndio mwamuzi wa haya yote, kama kweli haki itatendewa haki yake. 
Ni mimi: emu-three

1 comment:

  1. My spouse and I stumbled over here coming from a different website and
    thought I may as well check things out. I like what
    I see so i am just following you. Look forward
    to looking over your web page repeatedly.

    ReplyDelete

Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com