Ilikuwa siku ya kesi, ni kesi ya kuamua kama pingamizi
la kusitisha mnada likubaliwe au la,….na
hakimu alikuiwa mkali kweli, kutokana na kesi ya kwanza ilivyokuwa, watu
wanafika mahakamani hawana ushahidi.
Watu wa benk walikuwa wanashinikiza kuwa mnada
ufanyike kwa vile walipaji hawana uwezo wa kulipa tena, au wamepuuzia,…
‘Sisi tunachotaka ni hayo madeni yalipwe, na wadaiwa
wanapoteza muda bure tu, maana kila kitu kipo wazi, ushahidi wote tulishauonyesha
hapa mahakamani kwenye hukumu ya awali, tatizo ni kuwa, bado wanafikiri kuwa deni hilo, au madeni hayo hayakuwa ya marehemu, hayo madeni yana ushahidi,...kila moja lina kumbukumbu zake kisheria,.. na tatizo ni kuwa, hayo madeni yamekaa muda mrefu, hatuwezi kuvumilia tena…’akasisitiza
wakili wa benk.
‘Sasa kwa vile inavyoonekana wadaiwa hawana jinsi ya kulipa hayo madeni, tunaomba kwako Muheshimiwa hakimu, tuendelee na taratibu za mnada, pingamizi lao halina nguvu, kwa vile wao hawana ushahid, ushahidi wa kimaandishi,...wanachofanya
wao ni kupoteza muda ..’akasema wakili wao.
Wakili anayetetea watu wanaodaiwa akasimama na
kusema;
‘Muheshimiwa
hakimu,…hatujafika hapa kupoteza muda, ..na tuna uhakika mwisho wa siku haki
itatendeka, maana sisi tunatetea haki zao za watu waliodhulumiwa, na madeni
wanayodaiwa sio haki ya
wadaiwa,..’akasema wakili upande wa wanaolalamika kuwa madeni sio haki yao.
Miongoni mwa wanaolalamika, ni mama mjane, ..ambaye
inasadikiwa , kutokana na ushahidi wa benki, mumewe alifariki akiacha deni
nyuma yake. Na hilo deni limekaa muda mrefu bila kulipwa!
‘Ndugu muheshimiwa hakimu… benki wanataka madeni yao
yalipwe, lakini hawataki kuangalia uhalali wa hayo madeni , tumejaribu kuwaomba
tushirikiane nao, ili tuone huo uhalali, lakini imekuwa ni vigumu sana, wanadai
wao wana uhakika kuwa hayo madeni ni halali kwa wadaiwa, na sisi tumegundua
kuwa, hayo madeni sio halali kwa wadaiwa…’akasema
‘Uhalali kwa vipi, mbona vidhibiti, nyaraka, mikataba
ipo, na kila kitu kipo sawa, ulitaka sisi tuhakiki kivipi, je awali kesi
ilipofanyika, watu wenu hawakuviona hivyo vidhibiti, waliona ushahidi wote
ikiwemo mikataba, je sahihi, na hiyo mikataba sio halali..?’ akauliza wakili wa
benki.
‘Hivyo vidhibiti, au nyaraka, vina walakini..’akasema
wakili mtetezi.
‘Walakini gani, je mahakama iliyopitisha hukumu
haikuona hilo tatizo,..?’ akauliza wakili wa benki.
‘Tutakuja kuliona hilo tatizo, hapa mbele ya
mahakama, na kitu cha kujiuliza, ni kwanini haya madeni yote wanaodaiwa ni marehemu, nyie kama benki kwanini hamjiulizi
hilo swali…’akasema wakili anayetetea wanaodaiwa. Na hapo wakili wa benki
akasema;
‘Kwenye madeni haijalishi huyo mdaiwa ni marehemu au
yupo hai,…ndio maana wadaiwa waliweka dhamana, dhamana maana yake ni nini, kama
itatokea mdaiwa hawezi kulipa, basi dhamana hiyo ndiyo italipa hilo deni,
ikitokea mdaiwa kafariki, dhamani hiyo ndio inalipa hilo deni, ni utaratibu wa
kawaida tu..’akajitetea wakili wa benki.
‘Sawa…lakini kwa kukumbusha tu, hebu turejee miaka ya
nyuma wakati benki yenu ilipokumbwa na tatizo la wafanyakazi wasio waaminifu,
…benki yenu iliwafukuza wafanyakazi karibu wote, ambao mliwashuku kuwa ndio
chanzo cha tabia hiyo chafu… ‘akasema wakili na wakili wa benk, akaingilia kati
na kusema;
‘Hilo ni jambo la kawaida, kwenye taasisi, au
kampuni, watu kama hao hutokea,..benki au kampuni yoyote inaweza kuwafukuza
wafanyakazi wake hata wote..kama hao wafanyakazi sio waadilifu, lakini taratibu
za kikazi zipo pale pale, maana kumbukumbu zipo…’akajitetea.
‘Ndugu wakili …ni zamu yangu kutoa maelezo, usiwe
unaniingilia,…nataka kuelezea, mkasa huo ulivyokuwa, hadi watu wasio na hatia
kupewa madeni yasiyo haki yao…’akasema wakili na hakimu akasema aendelee, na
wakili mwingine atulie.
‘Na ukiangalia lini madeni hayo yalitolewa ,
utagundua ni kipindi kile benki hiyo ilikuwa na matatizo, hiyo benki ilikumbwa na kashfa nyingi, … na muda
huo mtandao wao wa kimahesabu, uliharibika…, kwanini uliharibika , na kwanini hawataki
kuliweka hilo wazi , kwasababu wanafahamu kuwa walioharibu huo mtandao wao ni
hao watu waliowafukuza...’akasema
Wakili wa benki akataka kuoingea, na alipoona hakimu
hamruhusu, akaanza kuongea tu.
‘Sio kweli, mtandao kuharibika sio sababu ya kuharibika
kwa kumbukumbu za kikazi,.. kumbukumbu zote za kuambatatisha madeni hayo zipo,
…na mtandao kuharibika sio kupotea kwa ‘data’..na ukiangalia, pamoja na
kuharibika kwa baadhi ya nyaraka, lakini kumbukumbu za madeni ambayo
yalihakikiwa, bado zipo, na yana nyaraka zake zote, yale ambayo hayana nyaraka
stahiki, tuliwaita tukakubaliana…’akasema.
Wakili wa utetezi wa madeni, akasema;
‘Tuna ushahidi wa kutosha kuwa madeni hayo yote,
yalikuwa ni mbinu za wafanyakazi wenu mliowafukuza kazi…na uzuri wake, wengi
wao bado wapo hai….’wakili aliposema hivyo, wakili wa benki alitoa pingamizi akitaka
kuingilia kati, na hakimu akasema;
‘Mnaweza kuutoa huo ushahidi…?’ akauliza hakimu
‘Ndio muheshimiwa hakimu, tunao ushahid wa kutosha…’akasema
wakili
‘Leteni huo ushahidi…tusipoteze muda mwingi, maana
kesi hii ilishatolewa hukumu, na kilichosababisha hukumu kutolewa kwa masilahi
ya benki, ni nyie wadaiwa kutokuwa na ushahidi wa malalamiko yenu…sasa je mnao huo
ushahid wa madai yenu, kuwa hayo madeni sio halali kwenu..?’ akauliza hakimu.
‘Tunao ushahidi
huo muheshimiwa hakimu…’akasema wakili
‘Leteni huo ushahidi wenu…’akasema hakimu.
‘Ushahidi wetu upo kwa kupitia mashahidi….’akasema na
wakili. Hapo wakili wa kutetea benki akaingilia katu na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu, tatizo ni lile lile kama
ilivyokuwa awali, watu hawa wanapenda kuongea tu, bila kutoa stakabadhi, au
kumbukumbu za maandishi, sisi kama benki hatuwezi kukubali maneno matupu, na
nina shaka kuwa hao mashahidi watakuwa wametengenezwa tu…’akasema wakili huyo.
‘Kama nilivyokwisha kutangulia kuelezea, kumbukumbu
za kibenki walizo nazo zina walakini, na uwalakini huo unatokana na hao watu
waliokuwa wakifanya kazi kipindi hicho, na ndio maana tunataka wao wenyewe
walithibitishe hilo, kuwa kweli ni wao walitengeneza hayo madeni…’akasema na
hakimu akasema kwa mshangao.
‘Wao wakubali kuwa ni wao walitengeneza hayo madeni,
kwa vipi, yawezekana kweli, msije mkawa mumewatesa ili wake kutoa ushahidi kama
huo..?’ akauliza hakimu.
‘Wao wenyewe kwa ridhaa yao, …wengien wamesema ni
kutokana na imani yo kuwasuta, kwa vile walitenda, na dhuluma imewafanya
wajisikie vibaya,…dhuluma imewatesa wao wanyewe, kwahiyo sasa wanataka kukiri
mbele ya mahakama yako tukufu, na kama mtu kateswa, yupo huru kusema …’akasema
wakili.
‘Muheshimiwa hakimu, umesikia alivyosema, …ina maana
hao watu kama watakiri, basi ni kutokana na mateso waliyoyapata, hayo mateso ni
mateso gani, na tunakataa kauli ya wakili huyo, ..sio kweli kuwa kumbukumbu
hizo zilitengenezwa, maana zina vitu muhimu vya kuthibitisha, zipo sahihi, na
lipo dole gumba…’akasema wakili.
Alipoongea huyo wakili wa benki, wakili wa utetezi…akatabasamu
kidogo, halafu akasema;
‘Ukweli wote utajieleza, usiwe na shaka na hilo,
tatizo la benk walijua hao marehemu wameshafariki, kwahiyo hakuna mtu wa kuja
kuwatetea,..na pia walijua hawataweza kupatikana..’akasema wakili wa kutetea
madeni.
‘Haya waite hao mashahidi, lakini pia tunahitajia
kumbukumbu za kimaandishi…’akasema hakimu.
Waliitwa mashahidi baadhi ya wafanyakazi wa
benki…ambao, walitakiwa kutoa kauli yao kuhusiana na hali ya benki ilivyokuwa
kipindi hicho, na wengi wao waliwanyoshea kidole, viongozi wa vitengo
waliokuwepo kipindi hicho…, baadae ikaja zamu ya mzee mtupe..
Mzee huyo alifika akiwa kafungwa mkono,..kuonyesha
kuwa ana jeraha … na swali la kwanza likawa;
‘Mzee, umefanya nini huo mkono wako…?’ akaulizwa.
‘Niliumizwa kwa risasi…’akasema.
‘Na nani…?’ akaulizwa.
‘Na polisi…’akasema , na aliposema hivyo wakili wa
benki akacheka na kuonyesha ishara kuwa, ‘mnaona’
‘Kwasababu gani, polisi walikupiga risasi huo mkono
wako…?’ akaulizwa.
‘Nilikuwa natimiza wajibu wangu wa kumlinda mtu
aliyeniajiri…’akasema
‘Wewe ni askari…?’ akaulizwa
‘Sio lazima mtu awe askari ndio afanye hiyo kazi,
hata hivyo, niliwahi kuwa askari enzi zangu, kama unataka kuhakiki ubora wangu wa
kikazi,…niliwahi hata kupigana vita vya Idd Amini, niliporejea nikaacha kazi,
kwasababu za kiafya…’akasema
‘Kwahiyo hiyo kazi ya ulinzi, uliipewa kwa vile
unajua jinsi gani ya usalama wa mtu, au sio..je sheria za kazi hiyo
inazifahamu..?’ akaulizwa.
‘Ndio, nazifahamu sana, lakini ningeishije…ndio
niliacha kazi kwasababu ya afya, lakini maisha yangu yalikuwa magumu sana, sina ujuzi, zaidi ya ujuzi wa kijeshi..na
nataka niishi, …naeleza haya, ili mnielewe kuwa hayo niliyoyafanya sio kwa
kupenda, ni hali halisi ya maisha…’akasema.
‘Unacho kibali cha kuifanya hiyo kazi, ya kumlinda
huyo mtu uliyekuwa ukimlinda, unayo leseni …?’ akaulizwa.
‘Ndio ninacho kibali…na mwajiri wangu ana barua ya
mkataba wa kumlinda, kwahiyo niliifanya hiyo kazi kwa mujibu wa mkataba…’akasema
akitoa vielelezo vyake.
‘Kabla ya kufikia kumtaja huyo bosi wake ni nani,
ngoja tuhakiki, baadhi ya ubadhirifu wa watendaji, ambao walipewa dhamana,
lakini hawakuweza kutimiza wajibu wao,…’akasema wakili
‘Lakini je huo ubadhirifu kama ulivyouita, unahusiana
na hilo deni, inahusiana na kesi yenu..?’ aliyeuliza sasa ni hakimu
‘Ndio muheshimiwa hakimu, tunakwenda hatua kwa hatu,
kuhakiki ukweli wa madai yetu…’akasema wakili..
Vielelezo vile vilipitiwa, na vilivyofikishwa kwa
wataalamu wa kazi hiyo ambayo wanatoa vibali, muhusika wa kutoa hivyo vibali, akasema;
‘Vielelezo hivi ni halali, lakini vilitolewa kimakosa…’akasema
‘Kwa vipi hebu tuelezee…’akaambiwa
‘Aliyevitoa vielelezo hivi ni mmoja wa watu
waliofukuzwa kazi kwa tabia hiyo chafu ya kutoa vibali, kimakosa, kwasababu
mbali mbali, na moja ya vibali vilivyogunduliwa kuwa vilikuwa na makosa ni hiki
hapa..hata kwenye kumbukumbu zetu za ofisini utaliona hilo…’akasema muhakiki wa
hivyo vibali.
‘Sasa tutamleta huyo aliyetoa vibali hivyo, ili
uhakika ukamlike..’akasema na wakili wa benki akapinga kuwa hilo haliendani na
kesi husika, hakimu akamuangalia mtu wa
benki, kwa makini, halafu akasema
‘Hebu mleteni tuone huo ukweli wake, tunataka
kuhakiki hiyo shutuma…’akasema hakimu.
Hakimu alipsema hivyo, wakili wa benki, akawa
analalamika, akidai kuwa hilo sio kosa
la mshitakiwa, kwani yeye alipewa vibali hivyo kihalali, sasa kama mtoaji katoa
kimakosa sio kosa la mtuhumiwa. Na ushahidi huo hauendani na kosa
linalozungumziwa…
Hakimu alishapitisha kuwa shahidi huyo aitwe…
‘Ngugu muheshimiwa hakimu, nataka kuionyesha mahakama
yako tukufu, kuwa kesi hizi zimekuwa zikikwama kutokana na watu waliopewa
majukumu yao, kutokuwa wadilifu…taratibu zinafuatwa, lakini kwa hila…mtoa
kibali anatoa kibali kwa masilahi, binafsi,au nyaraka zinatolewa lakini
zimegushiwa…tutakuja kuliona hilo..’akasema wakili
‘Na kutokana na hilo, wenye haki zao, wameshindwa
kesi, na kesi mojawapo ndio ya mama mjane, na wengine ambao wana madeni ya
ndugu zao, na ndugu zao hao ni marehemu,…mama mjane mume wake, aliambiwa
alindoka akiwa kaacha deni lililosadikiwa ni la mume wake, lakini sio kweli,
hizo ni njama zilizotengenezwa kiujanja kama tutakavyokuja kuoonyesha hatua kwa
hatua…’akasema wakili.
‘Mnao ushahidi wa kimaandishi…’akauliza wakili wa
benki
‘Tutakuja kuuona bila shaka…’akasema wakili
anayetetea wanaodaiwa.
‘Kutokana na watendaji wabovu, …taasisi iliyopewa kukusanya
madeni, imekuwa akitumia vibali hivyo,, vielelezo hivyo, nayaraka hizo,…ambazo
zilitengenezwa kwa hila, udanganyifu,.na kugushiwa kitaalamu...’hapo wakili wa
benki akaweka pingamizi, kuwa wakili huyo anatoa kauli za kashifa athibitishe
maneno yake hayo.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, tutamuita mmoja wa kutoa vibali hivyo,
athibitishe haya, aliyekuwa mtoa vibali vya walinzi binafsi…’akasema na wakili
wa benk akapinga, akisema huyo mtu atasema kwa vile alifukuzwa kazi,na huenda
atasema hivyo kwa shinikizo, kwa kulipiza kisasi tu, na..hata hivyo mambo ya
ulinzi yanahusiani vipi na hilo deni.
‘Ngoja tumsikilize kama kweli anafanya hivyo kwa
kulipiza kisasi au la..nia ni kuhakiki hayo madeni, lakini hayo madeni
yalitengenezwa na kundi la watu…wakili, usiwe na shaka na hilo, hapa naanza
kukuonyesha madeni hayo yalivyokuwa yakitayarishwa, na nani sasa…’akasema
wakili.
Hakimu akataka kumsikia huyo mtendaji atasemaje,
ikabidi huyo mtendaji aitwe kutoa ushahidi…huyo jamaa alipoitwa, kila mtu
alishikwa na butwaa..
‘Jina lako ni nani…?’ akaulizwa
‘Mimi naitwa Mkwatue..bin…’akataja jina la baba yake.
‘Baba yako anafanya kazi gani..?’ akaulizwa
‘Alikuwa mganga wa kienyeji…’aliposema hivyo watu wakacheka,
hakimu akagonga rungu lake kunyamazisha watu.
‘Kwa jina maarufu alikuwa anaitwa nani…?’ akaulizwa
‘Mtaalamu…’akasema, na watu wakacheka,..
‘Haya hebu tuambie..wewe ulipokuwa umeajiriwa kazi
yako ilikuwa ni nini…?’ akaulizwa
‘Kazi yangu ilikuwa kutoa vibali vya walinzi, walinzi
jamii, walinzi ambao wanawalinda watu, kwa sababu mbali mbali…’akasema
‘Je wewe kipindi hicho, uliwahi kutoa kibali kwa huyo
mzee Mtupe…?’ akaulizwa
‘Ndio muheshimiwa…’akasema
‘Ulitoaje, …?’ akaulizwa
‘Alifika na maombi yake ya kutaka kibali, kibali chake hakikupitia kwa wengine kama ilivyokuwa kawaida,..hata hivyo, ni nani angelipinga hilo,..mimi mwenyewe nilipitisha sehemu zote hadi mezani kwangu...'akatulia
'Kwanini ulifanya hivyo..?' akaulizwa
'Nia ni mzee afanye kazi yake kihalali...'akasema
'Kihalali...?' akaulizwa
'Ndio kama, ana hicho kibali, basi kazi yake ni ya halali, au sio...'akasema
'Kwahiyo wewe ndiye mtu wa mwishi wa kuidhinisha hicho kibali, ?' akaulizwa
'Ndio, hata ukiangalia hivyo vibali kuna sahihi yangu...'akasema.
'Hayo maombi yalipofika kwako wewe ulifanya nini..?' akaulizwa.
'Nifanye nini, maana sio kitu kigeni kwangu,, niliweka sahihi yangu sikuwa na haja ya kuhakiki,kwa vile mimi nilishafahamu ni kibali cha nani na kwanini…’akasema
‘Ulishafahamu kwa vipi…?’ akaulizwa
‘Tulipanga na wenzangu…’akasema na watu wakagunda
‘Je nyaraka hizo zilikidhi masharti yote…?’ akaulizwa
‘Mhh…kiukweli sikujali hayo,…nilipitisha tu, kwa vile
yeye ni babu yangu, ..’akasema
‘Babu yako…babu yako kwa vipi?’ akaulizwa.
‘Ndio ni babu yangu, ….mzee mtupe, alizaliwa tumbo
moja na baba yake baba yangu…’akasema
‘Baba yake baba yako, ..ukiwa na maana baba yake
mtaalamu au sio, na kwahiyo mzee mtupeo kwako, ni babu yako, au sio..?’ akaulizwa
‘Ndio muheshimiwa…’akasema, wakili akacheka,
akimuangalia wakili wa benki ambaye alionekana kushikwa na butwaa.
‘Unaona hii ni familia iliyojipanga,…hapo sasa mtoto,
baba , babu… na walihakikisha udugu wao hautambulikani, kwanini walifanya hivyo...kuna jambo limejificha hapo...na je ni nani alikuwa anajua hilo, kuwa mzee
mtupe ana udugu na mtaalamu, hawa watu walikuwa hawaivani, au sio, ilivyoonekana kwenye jamii…?’ akauliza na watu wakaguna, na wengine wakasema
‘Hakuna…aliyejua,...’akasema na hakimu akainua rungu akitaka
kuligonga, lakini hakufanya hivyo, akawa anamuangalia huyo shahidi na mzee
mtupe.
‘Swali kwanini walifanya hivyo…hayo tutakuja kuyaona
huko mbele, hatua kwa hatua…’akasema
wakili na wakili wa benk akasogea kuongea na wasaidizi wake..
Wakili upande wa benki, akawa anateta na wasaidizi wake,..., huku wakili wa kutetea
haki za wanaodaiwa akiendelea.
Hayo yakiendelea huko, …mimi nilikuwa bado nimelazwa,
nipo hospitalini, nikiwa naendelea na matibabu.
************
Siku hiyo ya
kesi, nikiwa hospitalini, aliletwa tena yule mtu mbele yangu,…
‘Oh, umeletwa tena, wewe si ulisema unataka kwenda
kutoa ushahidi mahakamani…?’ nikamuuliza
‘Wamenikatalia wanasema ushahid wangu hautakubaliwa
kwa vile eti nina matatizo ya akili…’akasema
‘Je itakuwaje, maana wewe umsema bila yaw ewe ukweli
hautagundulikana…wewe ndiye unafahamu kila kitu, je unayo nyaraka yoyote,
ushahidi wa kimaandishi utakaotusaidia mahakamani..?’ nikamuuliza
‘Mimi nipo sawa kwa hivi sasa, ila nilitaka kuonana
na wewe kwanza…’akasema na docta akaingilia kati na kusema;
‘Mimi nimeamua
kufanya anavyotaka yeye, yeye ana imani
akionana na watu wawili, mtu wa jamii, na mama mjane basi atapona kabisa, , …na
kupona kwake, ndio kutasaidia wengi, sasa nimelata kwako, muongee naye, ili
tuone kweli kapona..’akasema docta.
‘Lakini mimi sio docta…’nikajitetea..
‘Usijali, ..mimi ni docta, nitasikiliza, na
anavyoendelea kuongea, nitajua ukweli wa utaalamu wangu kama kweli kapona na
ushahidi wake unaweza kukubalika au la…’akasema docta.
Yule jamaa leo alionekana tofauti, hajafungwa, lakini
kuna askari wapo tayari, kama lolote likitokea..
‘Nimekuja,…nataka tuongee, najua wewe umeshaufahamu
ukweli, najua …ulitakiwa ufe ili ukweli usijulikane, na mimi nimeshaahidi kuwa
nitasema ukweli wote…’akasema sasa akiongea vizuri tu.
‘Je unataka kuniambia nini, maana benki wao
wanahitajia ushahidi wa maandishi, sio maneno, na wewe kwa hali yako, kisheria
haitakubalika kutoa ushahidi, na leo nasikia kesi inaendelea huko…’nikamuuliza
na yeye akasema;
‘Wewe si unataka ushahidi eeh, ushahidi wa kukusaidia
mahakamani, au sio…ili huo ushahidi uweze kuhakiki ukweli wa hilo deni, au sio,
mimi ninaweza kusadikisha hilo, na benki wanalijua hilo ..?’ akaniuliza na
kusema.
‘Swali langu umelielewa, wewe utasadikishaje, je
unazo nyaraka, kumbukumbu za kibenki, za kulisaidikisha hilo, muhimu benki
wanataka kumbukumbu za maandishi….?’nikamuuliza.
‘Kazi hiyo
nitaifanya huko mahakamani, ila kwasasa nimekuja kwako kwa kukuomba msamaha,
nataka nianzie kwako, kabla muda haujafika, je umenisamehe…?’ akasema na
kuniuliza hivyo.
‘Mimi hujanikosea, uliowakosea wapo, ila kama kweli utasaidia ukweli kupatikana, na
ukweli ukapatikana, msamaha wangu upo wazi..na msamaha wa hao uliowakosea
utakuwepo tu…muhimu ni haki itendeke..’nikasema hivyo.
‘Haya, mimi waniepeleke huko mahakamani,…nitasema
kila kitu, sidanganyi safari hii, nitamtaja muhusika mkuu wa hujuma hiyo bila
kuficha, na jinsi hujuma hiyo ilivyofanyika…’akasema sasa akionyesha uso wa
wasiwasi.
‘Docta, unasemaje..?’ nikamuuliza docta
‘Kitaalamu, mimi siwezi kusema uwongo, kwa hatua
aliyofikia, hajambo, na anaweza kuongea ikakubalika,..lakini yategemea pia, …je
akifika huko hali ikabadilika,…’akasema
‘Kwanini ibadilike…?’ akauliza huyo jamaa
‘Siku zote inakuwaje, si unaonekana mzima baadae hali
inabadilika…’akaambiwa
‘Sio sasa…hali yangu kwa hivi sasa yategemea ukweli
nitakaousema, nikichelewa na hali ikarejea tena, ndio basi,..naombeni tafadhali
mniwahishe huko mahakamani…’akasema huyo jamaa.
Baadae huyo mtu akapelekwa mahakamani, …, nilitamani
sana niwepo huko mahakamani, lakini docta alisema mimi bado sihitajiki
kutembea,
Kesi siku hiyo ikafanyika na nilikuja kuambiwa
kilichotokea siku ya pili yake, na aliyekuja kuniambia ni mama mjane.
‘Vipi mbona huna raha, mahakamani imekuwaje…?’
nikamuuliza na badala ya kunijibu akaanza kulia..
Nb: Huyu mama mjane alilia nini....naona nisiwachanganye niishie hapa kwanza.
WAZO
LA LEO: Haki ina nguvu, ..haki itashinda tu, na hata haki
ikizuiwa, ni swala la muda tu, ipo siku haki itafanya kazi yake na ukweli
utabainika tu.
No comments:
Post a Comment
Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com