Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, October 10, 2018

CHOZI KUTOKA MOYONI




CHOZI KUTOKA MOYONI…

                        UTANGULIZI

Nilifika ofisini asubuh kama kawaida yangu, nikafanya shughuli zangu kwa haraka, nikijua leo bosi akija cha kwanza tu nafika ofisini kwake nimpa ripoti yangu ya wiki, ya kazi zangu nilizofanya , ndivyo tunavyofanya, … halafu namkabidhi barua ya mkopo...lengo la mkopo, kulipa ada za watoto, mengine ni siri yangu..

Moyoni nikawa namuona mke wangu akifurahi, ..kama vile nimeshaupata huo mkopo na sasa namkabidhi sehemu ya fungu anampeleka mtoto hospitali na nyingine atafanyia biashara..na mawazo hayo yalikatishwa na mawingu ya sauti zenye kunitia mashaka …sauti za kumbukumbu…

'Kama usipolipa ada yako mwezi huu… watoto wako wasije tena hapa shuleni..'barua ya shule ilisema hivyo, na ujumbe wa simu, kwenye simu yangu..


Hawa walimu bwana...hivi hawajui hali halisi,...ngoja nipate pesa, mimi  nitawalipa pesa yao yote, niwe huru, watoto wangu na wao wasome kwa amani, najua elimu ni bure lakini nimeona niwalete huku angalau wasome kama watoto wa bosi, japokuwa shule yenyewe sio sawa na ile ya bosi,..angalau lakini..nikawaza moyoni,

‘Lakini wapi pa kuzipata hizo  pesa…’nikasema moyoni

‘Mhh, hizi sasa. ni ndoto za Alinacha…’nikazidi kujisemea.

Mara nikasikia sauti nyingine akilini hii ni ya kutisha kabisa…hadi mwili ukazizima kwa uwoga.


'Unasikia, kama usiponilipa hilo deni,...nitakachokifanya usije kunilaumu...'hiyo ilikuwa sauti ya muuza duka. Huyu muuza duka wanasema awali alikuwa ni jambazi mkubwa, na pesa alizoanzishia hilo duka ni za uporaji, na wanasema yeye kwake kuua ni kazi ndogo tu, askari wameshindwa kumpata kwa vile hajawahi kukamatwa, na ushahidi.


'Nitakulipa ndugu yangu...kesho nikifika kazini nitaomba mkopo, najua bosi atanipatia tu...huwa najituma sana kazini..'nikasema nikiwazia wazo la mke wangu.


'Mkopo ulipe mkopo, hahaha, unanishangaza sana wewe mtu, sawa, ila niamini, sitaki mzaha kwenye pesa yangu...'akasema muuza duka


'Wewe hujui maisha...ndivyo tunavyoishi, wewe subiria pesa yako, na kama nisipokulipa,...njoo, kachukue chochote nyumbani...'nikasema kwa kujiamini


'Hahaha haya bwana,...wewe hutaamini nitakachokifanya...'akasema , ni kweli muuza duka huyu ni rahisi kukukopesha, lakini muda ukipita, wewe sikilizia vumbi lake, wengi wanamfahamu wakikipa haraka hurudi kumlipe deni lake, kwahiyo wengi wanakopa wakiwa na uhakika wa kuja kumlipa, hana wasiwasi kukupa kitu.


Mimi nilikuwa na imani nitapata pesa, maana nimekuwa nikijtuma sana kazini, wakati mwingine nafanya kazi hadi usiku, bila hata malipo ya ziada,..,..na sijawahi kuomba mkopa kwenye hiyo ofisi kwa vile naifahamu ilivyo, huyo bosi kutoa mkopo ni nadra sana


Na tokea awali sikuwa na wazo kabisa la kukopa ofisini hapo, kwa jinsi nimjuavyo huyp bosi na hali halisi ya ilivyo, lakini hadi kufikia uamuzi huo, ni kutokana na ushawishi wa mke wangu ndiye alinishauri,


'Mume wangu waonaje kutokana na hii hali, ukakope kiasi fulani ili nikifanyie biashara,..na kiasi kingine tulipie ada, watoto wasifukuzwe wapo mwaka wa mwisho...na kufukuzwa fukuzwa kuna wavunja nguvu..na nyingine tumtibie huyu mtoto wetu anayeumwa, unajua tunazarau hali yake, inaweza kutuletea matatiz baadae…tukaja kulaumiwa na madocta..'akasema mke wangu.


'Mhh, mke wangu, ..ungelijua...ofisini kwetu, mpaka bosi akupe mkopo labda, itokee miujiza...bosi wetu hajali kabisa masilahi ya mfanyakazi zaidi ya mshahara wako,.na imefikia hata mshahara analipa tarehe 35 au 40….na hata hivyo hali ya kiofisi ni mbaya,biashara hakuna, na  pesa hakuna kampuni ina hali mbaya sana..'nikasema


'Wewe nenda kajaribu tu, huwezi jua, muelezee hali halisi yeye kama mzazi ataelewa, si yeye ana watoto pia, anasomesha kama sisi, anauguliwa kama sisi, wewe mjaribu tu.....usijitwike mzigo kabla haujatua kichwani mwako...'akasema mke wangu .


'Mhh...haya...'nikasema hivyo.


Hapo ndio na mimi niliingiwa na wazo hilo la kukopa kazini…, nikajipanga, nikiona kweli kwasasa ina haja ya kufanya hivyo,.utaenda wapi sasa, muajiri wako ndiye wa kukufaa wa wakati wa dhiki…nimefanya mengi ya kuiaidia kampuni, kwanini mimi wasinisaidie na mimi..

‘Nikipata huo mkopo, sehemu yake nitamlipa yule muuza duka deni lake, maana mhh…asija kunkata kichwa, …sura hata macho yake yanatisha..na hilo deni hata mke wangu halifahamu..’nikajisemea hivyo.


**************
Japokuwa nilikuwa nawajibika sana kazini, lakini siku hiyo moyoni mwangu nilihisi wasiwasi,…ni kama vile unahisi kitu kibaya chaweza kukutokea, labda ni mawazo ya maisha, na nikakumbuka labda….


Nikahisi labda ni ile taarifa niliyoisikia wiki iliyopita, kutoka kwa wafanyakazi wawili wakiongea,...ni mazungumzo ya kawaida tu ambayo yanaongelewa kila siku.


'Nasikia bosi kapanga kupunguza baadhi ya wafanyakazi...'nilisikia mfanyakazi mmoja akisema.

'Acha afanye hivyo bwana..’akasema huyo mwingine

‘Yaani wewe unaona ni sawa tu..’akasema mwingine

‘Ndio hata mimi ..namuunga mkono bosi…, maana wanaajiriwa wafanyakazi wapya , eti wasomi, halafu wanalipwa mishahara mikubwa zaidi yetu sisi. Hebu wewe angalia, sisi tupo hapa kwa muda gani, tokea kampuni hii inaanzishwa, hatuongezwi kitu, tunakuwa wasindikizaji tu, mimi nitafurahi wakiondolewa tu....'akasema mwingine.

'Wewe una uhakika gani kuwa hutaondolewa hapa kazini?'akaulizwa.


'Mimi najua tu, siwezi kuondolewa, mshahara wangu ni mdogo sana, hauwezi kuitia kampuni hasara, …nakuambia kitu,…wote wamekuja na wote wataondolewa, wewe niamini hilo…’akasema

‘Mhh…unajiamini …’akasema mwenzake.

‘Mimi nakuambia..hao, wataondolewa wote..wametukuta, na watatuacha na kampuni yetu,.."akasema kwa kujiamini na kucheka, sikujua kwanini huyo mfanyakazi anajiamini hivyo.


'Ni kweli, uzuri wake sisi bosi tumeshamjulia, hawa wageni wakija , wanajifanya wanajua kuliko hata bosi,..hawamjui huyu bosi wetu alivyo, anakupenda akiwa na shida na wewe, shinda yake ikiisha, hajali, atakuondoa tu...'akasema mwingine.




Wafanyakazi hao kazi yao ndio hiyo, wakifika ofisini asubuhi, asilimia kubwa ni kuteta, magumzo vibarazani, hawafanyi kazi mpaka wamuone bosi..


Bosi akiingia hutaamini,...wanajituma utafikiria sio wale waliokuwa wamekaa , wakiongea, kusoma magazeti…au kupiga gumzo la mipira au siasa..lakini ngoja bosi afike, huwezi amini, watakavyowajibika,..na bosi akiwepo, kweli wanawajibika,...na wanahakikisha bosi anaona kile wanachokifanya....kiukweli wanajua kuigiza. na wanampatia sana huyo bosi


'Ukitaka bosi huyu akupende iwe hivi, na jingine eeh…usije kumuomba pesa, anaipenda pesa zaidi ya benki…na jingine usije kumlalamikia shida zako, hapendi kusikiliza shida za mtu, kwake yeye umuonyeshe kazi, uongee naye kuhusu kazi zake, atakuwa rafiki yako,…ole wako uende kulalamika mambo ya mshahara hautoshi, umechelewa,…hahaha, utaniambia..'aliniambia mmoja wa wafanyakazi siku nilipomuuliza kwanini wanafanya hivyo.


'Kiukweli mimi hivyo siwezi, nitafanya kazi kwa mujibu wa taaluma yangu, akiwepo au asipokuwepo, na akija kama sina zaidi, nimemaliza kazi nahitaji kupumzika kidogo nitafanya hivyo, ilimradi nimetimiza wajibu wangu…mimi sio mtumwa wa kuigiza...'nikasema


'Hahahaha haya, na kwa jinsi anavyowalipa, moyoni hafurahii kabisa, ipo siku wewe utaniambia wewe jitume tu...'akasema jamaa huyo.


Pamoja na kujituma kwangu, kuwajibika kwa mujibu wa kazi yangu, niliona kama wafanyakazi hao walikuwa hawaniangalii kwa jicho jema, mimi sikuwajali nikijua udhaifu wa binadamu ulivyo, husuda na chuki ni hulka zetu.


**************

Basi mara nikasikia bosi mwenye kampuni kafika, kwa haraka nikaweka barua yangu vyema na kuhakikisha kila kazi niliyotakiwa kuifanya nimeikamilisha, nikatengeneza taarifa ya kazi yangu ya wiki ili iwe chambo cha kuanzia, sikutaka matatizo


Wakati ndio nataka niende ofisi kwa bosi, mara nikasikia nikiitwa.


Nilihisi moyo ukinilipuka, phaa...sijui kwanini,.. hata hivyo sikujali sana, nikajua labda bosi leo kanianza mimi, anahitajia kujua nilichofanya wiki nzima iliyopita.


'Hamna shida sasa nimepata wapi pa kuanzia...'nikasema nafsini mwangu.


Kwa haraka nikakusanya makabrasha yangu, na laptop, ili niwe kamili kamili,...sikutaka uzembe kwenye kazi zangu, kwa haraka nikaelekea huko.


Sasa wakati natembea kuelekea kwenye hiyo ofisi, nikakutana na wafanyakazi wale wawili, , wakaonyesha tabasamu, kama la kujali na kunipa moyo na nilipogeuka kuangalia ninapokwenda, wao wakaangaliana na mimi nikawa nimegauka kwa haraka kuwaangalia


Niliwaona wakionyesheana ishara ya dole gumba...mimi sikuwajali, haraka nikaingia ofisi ya mkubwa wa kampuni.


'Habari za asubuh bosi...'nikasalimia kwa heshima na bosi kwanza akahema kwa nguvu, halafu akasema.

'Nzuri tu,...hebu kaa hapo, nina mazungumzo na wewe..' akasema hivyo. Hapo, nikaanza kukata tamaa, maana nilitaka aanze kuniulizia hali za familia, ili niweze kuchomeka matatizo yangu halafu, phaa...namkabidhi barua ya mkopo.


'Bosi mimi ripoti yangu ipo tayari kama ndio uliyoniitia...'nikasema


'Sio kuhusu ripoti, nimekuitia,jambo jingine tu, wewe kaa hapo, na weka pembeni kazi zako. ...'akasema na kutulia kidogo, hapo nikaanza kuwaza mengine, kaniitia jambo jingine kuhusu nini...binadamu unaweza kuwaza mambo mengi kwa sekunde chache tu.


' Kiukweli, mimi nimefurahishwa na utendaji wako wa kazi, hata kwenye vikao vyetu, huwa tunakupongeza sana...'akaanza kusema hivyo.


Hapo moyoni kidogo nikaanza kuingiwa na tumaini jema,..nikajua labda natakiwa kuongezwa mshahara, japokuwa katika hiyo kampuni kuongezwa mshahara haijawahi kutokea.


Jingine lilinitia mashaka kidogo, niliona bosi kama anakwepa kuniangalia machoni...sio kawaida yake , yeye huwa akikuita ofisini kwake akianza kuongea na wewe anahakikisha anakuangalia moja kwa moja machoni.


'Nashukuru bosi...'niliposema hivyo, akainua uso sasa kunitizama machoni.


'Lakini kwa hali ya kampuni, nashindwa hata kuelezea, hata wewe mwenyewe umeiona au sio, kama tumefikia hatua hatuwezi kulipana mshahara kwa wakati...eeh,...na hata tukilipana twalipana nusu.mishahara, ni jambo mimi sipendi kabisa..'Hapoi nikahisi moyo ukinienda mbio.


'Wewe ni mmoja wa wafanyakazi tunaowalipa vizuri, na nilipenda niendelee kufanya hivyo...ndio kwanini nisikulipe hivyo wakati, elimu yako inaruhusu, achilia mbali utendaji wako...'akasema


'Ahsante bosi najitahidi tu..bado, sijafanya kile ninachokitaka...'nikasema


'Inatosha,..umefanya vyema tu...'akasema hivyo, halafu kama vile hataki niongee zaidi akasema


'Kiukweli, umekuwa ukinipa moyo,..uliyoyafanya ni makubwa sana...ndio maana nilipowaza,..eeh kutokana na hali ya kampuni ilivyo ngumu, niliona labda niwapunguze mshahara, ili tuweze kumudu hali halisi...kwako wewe niliona sio sahihi...'akatulia


'Kutokana na hali halisi ilivyo, ...hili nimeamua mwenyewe, usije kusema ni ushawishi wa mtu,...mimi nimeona tukupatie nafasi, ili utafute kazi sehem nyingine...'hapo akaangalia pembeni.


'Bosi mbona sijakuelewa...'nikasema


'Kiukweli sina uwezo wa kuendelea kukulipa, ...nimejitahidi kila mwezi, hata kukopa huku na kule, lakini uwezo wangu umefika mwisho...na naanzia kwako, pengine hata nikiona naweza kufunga kampuni....'akasema


'Oh...bos lakini...nilikuwa na matatizo...ndio nilitaka nikuelezee...'nikasema


'Matatizo ...hasa yanayohusu pesa, sitayaweza tena, mimi nakuomba ufanya jambo moja..muda wa mwezi huu, jitahidi kutafuta sehemu nyingine ukipata, basi...lakini baada ya mwezi huu,...sitaweza kukulipa tena mshahara...'akasema


Hapo, nikanywea,...akili ikaganda...nguvu zote zikaisha...kila nikitaka kumuangalia huyo bosi nashindwa, macho yameshakuwa mazito...


'Ndio zaidi ya hayo, ningeliomba uanze kumzowesha yule mwenzako kazi zake...najua utapata kazi sehemu nyingine wewe ni mchapa kazi mnzuri sana..na ukipata mimi mwenyewe nitakudhamini, maana nakufahamu sana...'akasema sasa akiweka mambo yake vyema mezani kuwa niondoke.


Taratibu nikasimama, na kuanza kutoka, sasa mwili hauna nguvu, akili ikaenda mbali,...watoto shule tena basi, nilijaribu kuwatoa kwenye shule za awali walizokuwa wakisoma ili wasome kwenye shule za kulipia, angalau wawe japo sio sana na watoto wa mabosi,…sasa haitawezekana tena.. na itakuwaje, kwa yule muuza duka, asiponiona leo, familia yanagu inaweza kuwa hatarini, na nikimuendea, kwa hasira alizo nao anaweza kunikata kichwa,…lakini la zaidi ...mtoto anaumwa anataka matibabu nifanyaje.


Niliwaza hivyo hata sijui nilifikaje mezani kwangu, ...nilipofika nikainamisha kichwa, nikawaza, na kuwazua, sijui ilikuwaje, chozi likanitoka, ...sijui chozi la nini, na sijui namlilia nani sasa mie mtoto wa kiume,..kiukweli lilikuwa chozi lenye hisia kali....'CHOZI KUTOKA MOYONI..


'NB: hiki ni kisa kifupi cha rafiki yangu, kanitumia,..kwa yaliyomkuta....nashindwa kukiendeleza kwa hivi sasa maana na mimi nipo kwenye mitihani hiyo ya maisha…ila kwa faraja nimeona nikitume siku isipite bure.


WAZO LA LEO: Baada ya dhiki huja faraja, baada ya magumu fulani mwisho wake huja mafanikio, je inapotokea umefanya jitihada zote, umepitia ,magumu mengi sana, na inafika muda wa kutegemea faraja, bahati mbaya, ikaja kutokea machungu utafanyaje...

‘litakutoka chozi …’ 
Ni mimi: emu-three

No comments :