Askari, wakawa
wanafuatilia, kuzima hizo fujo, na kuwatoa watu nje..walitaka pia kuona kuna tatizo gani.
Na baadae huyo mtu aliyekuwa akiendeshwa kwenye kigari cha wagonjwa, akawa keshafikishwa mbele akiwa ndani ya kigari hicho..., nyuma yake
yupo docta, anakisukuma hicho kigari, na muda huo hakimu alikuwa kasimama, akitaka kuondoka,…
'Kuna vurugu gani, kesi ijayo, sitaki kuona hili likitokea, kama watu hawana busara, wasifike hapa mahakamani..'akasema hakimu kwa hasira.
Akamuona huyo mtu, akisogezwa mbele, hakutaka hata kufahamu huyo mtu kaletwa wa nini, ...kwa haraka akaanza kutembea kuondoka, huku akisema;
‘Hatuwezi kufanya
lolote kwa muda huu, lolote ulilo nalo wewe kwa sasa, itabidi lisubirie muda mwingine,
…’alisema hakimu huku anatembea kuelekea mlango wake wa kutokea,
.
Huyo mtu aliyekaa
kwenye hicho kigari, akasema kwa sauti kubwa;
‘Samahani muheshimiwa
hakimu, lakini hili haliwezi kusubiria kesho,…ilimradi kauli imeshatoka, ya
kunishutumu mimi, na hatujui kesho itakuwaje, ninaogopa isije kutokea kama ilivyowahi kutokea huko nyuma, watu wameondoka na kuacha maswali nyuma,…naomba tafadhali, unisikilize japo
kidogo tu…’huyo mtu kwenye kigari akasema
Hakimu akawa anatembea
kuondoka, na huyo jamaa akazidi kusema kwa sauti kubwa
‘Mimi ndiye....alimaarufu,.. Dalali…’Aliposema
hivyo, hakimu akasimama, na kwa haraka akageuka kumuangalia huyo mtu, alitulia
kidogo akimuangalia ...
‘Dalali…ndio wewe
ndiye uliye- ….’akasema hakimu na huyo jamaa hakusubiria hakimu amalizie,
akasema;
‘Ndiye mimi muheshimiwa
hakimu, ndiye mimi niliyeshutumiwa na mengi, kutoka kwenye kinywa cha kijana
anayedai kuwa yeye ni mtoto wangu…’akasema huyo mtu, na hakimu akawa sasa kasimama.
‘Mimi imenibidi
nijitokeze tu, ili haki iweze kutendeka, siwezi kuvumilia tena, nahisi kuna njama za kuupotosha ukweli, na tukiendelea kunyamaza, mabaya yanaweza kutokea, nahisi wakati sasa umefika kuusema ukweli wote,...kwahiyo muheshimiwa hakimu tafadhali, nipe angalau muda kidogo,...naogopa kwa hali ilivyo, kesho inaweza
isinikute nikiwa hai…’akasema huyo jamaa.
‘Kwanini unasema hivyo, kuna nini kimetokea na kwanini upo katika hiyo hali,,…?’ akauliza
hakimu, sasa akiangalia saa yake.
‘Nimetishiwa uhai muheshimiwa hakimu, yanayotokea kwangu, ni majinamizi tu, nafanya bila kujijua nafanya nini...'akasema
Hakimu sasa akageuka kumuangalia huyo mtu
'Na cha muhimu ni iliyotolewa na huyo kijana, sasa kwa vile una haraka, mimi nasema hivi, sio kweli kuwa mimi nimechukua hilo deni, sio kweli kuwa
mimi ndiye nilikopa hizo pesa, sio kweli kuwa mimi nilijua kilichokuwa
kinaendelea kwenye hilo deni, nayatamka haya yasikike,…ili hata wakinua leo,
kauli yangu iwe ndio hiyo…’akasema huyo jamaa.
Hakimu akaangalia saa, na kuanza kuondoka, huku akisema;
‘Sawa kauli yako
imenakiliwa, kesi itaendelea kesho, au siku itakayopangwa kwa leo hatuwezi
kufanya lolote..unasikia, sheria za mahakama zinafuatwa, kesi hii imesitishwa
kwa leo…’akasema hakimu , akaanza kuondoka, lakini ghafla akasimama , na kwa sauti
kubwa akasema;
‘Ila wewe itabidi uwe
mikononi mwa watu usalama, watu wa usalama, hakikisheni huyo mtu analindwa kwa nguvu zote, hadi kesi itakapoendelea tena…’akasema huyo hakimu, na huyo
akafunguliwa mlango, na kutoka eneo hilo la mahakama.
Watu wa usalama kwa
haraka wakamfuata huyo mtu aliyeingia ambaye lijitambulisha kuwa yeye ni …alimaarufu,
Dalali na kuondoka naye.
Kisa kinaendelea..
*********
Kesi hiyo ilibidii ipangiwe
siku iliyofuata,hiyo ni kutokana na kilio cha watu wengi ambao walianza
kulalamika kuwa kesi hiyo inachukua muda, huku wao wakidhulumiwa haki zao, wana mashaka na haki zao, kwani wamepewa madeni yasiyo halali yao…
Na wakati huo huo, waendesha mnada walikuwa wakilalamika,kuwa na
wao wanazuiliwa kutekeleza majukumu yao, wakati wana kibali rasmi, cha kuendesha
minada hiyo kwa niaba ya benki..
Na watu wa haki za
binadamu, wanajamii,…haki za akina mama na watoto na wao walishaanza kupaza
sauti, kuwa matajiri, wanatumia mapesa yao, kuhakikisha, haki za wanyonge
hazipatikani…
Jambo hili likaingia
kwenye siasa, …wanasiasa nao, wakaona hiyo ndio sehemu ya kujijengea majina,
wakaanza kupaza sauti, kwa wananchi…
‘Haki..haki..haki…haitendeki
ipasavyo….’
Kwa mashinikizo hayo,
yakaifanya idara ya mahakama kuingilia kati, na kesi hiyo ikapewa kipaumbeme…
hakimu akaona kesi hiyo iendee siku iliyofuatia.
‘Kutokana na ratiba
zetu, siku ya kesho haina kesi nyingi, kwahiyo kesi hiyo itaendelea, na natumai , siku hiyo ndio itakuwa siku ya mwisho ya kusikiliza ushahidi wenu, na muhakikishe kila
kitu kinakuwa tayari,…ili tuone kama tunaweza kuihitimisha hiyo kesi, au la, hatutaki idara hii kuingiliwa na watu wengine…’akasema msemaji wa
hakimu akiongea na mawakili wa pande zote mbili.
Na wakati hayo yakiendelea,
Majaliwa alikuwa bado kapoteza fahamu, na alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi,
….na ndiye alionekana kuwa shahidi muhimu wa kuhitimisha hiyo kesi, watu wengi walikuwa wakimzungumzia yeye, na wengi walitaka wawepo kwenye hiyo kesi.
‘Kama shahidi huyo
muhimu anaumwa hajitambui, tutaendeleaje na hii kesi hapo kesho, tunaona tusubiria labda..?’ akauliza
wakili wa benki.
‘Tutaendelea na
mashahidi wengine, kuna huyo mmoja aliyejitokeza,…hatuwezi kumpuuza, na
ikizingatiwa kuwa yeye katajwa kama ndiye muhusika wa hilo deni la mama mjane…’akasema,
msemaji wa hakimu.
‘Sio kweli…’akataka
kusema wakili wa benki lakini akanyamazishwa,
‘Hayo tutayasikia huko
mahakamani, lengo la kikao hiki ni kuwaarifu tu, kuwa kesho muwe mumejiandaa,
hatutaki kupoteza muda kwa kesi moja tu…’akasema huyo msemaji .
**
Basi kesi ikaendelea
siku iliyofuatia,…na siku hiyo watu walijaa..isivyotegemewa, na ikaonekana
mahakama haiwezi kukusanya watu wengi kiasi hicho,…, ikabidi kikosi cha kuzuia
fujo kifike kuwatawanya hao watu waliojazana na wengi bado walikuwa wakiendelea
kufika.
‘Kama hamtaki kutulia,
inabidi muondoke eneo hili…’wakaambiwa watu, na wachache wakatawanyika, wengine
wakatafuta sehemu pembeni ya mahakama wakakaa, wakisubiria ni nini kitatokea.
Sauti mahakamani
ikasikika, …
‘Dalali…unakumbuka
uliwahi kuambiwa ueleze ukweli wa deni ambalo benk wanadai kuwa ni deni la
marehemu, aliyekuwa mume wa mama mjane ambaye ni mmmoja wa watu wanaodai kuwa
deni hilo sio la kweli…’akaulizwa.
‘Ndio nakumbuka sana muheshimiwa
…’akasema
‘Lakini kwa mara zote
ulizofika mahakamani, au kuhojiwa na polisi wewe…, hukutaka kusema ukweli,…’akaambiwa.
‘Mimi nilisema yale
yaliyostahiki kusemwa kwa wakati huo…’akasema Dalali.
‘Sasa kwa vile ukweli
umeshajulikana, kuwa wewe ndiye uliyefanikisha deni hilo,sasa swali je hiyo
sahihi ya kaka yako ilitoka wapi, kama ni wewe uliyefanikisha deni hilo…?’
akaulizwa…?’ akaulizwa Dalali.
‘Kabla sijajibu hilo
swali, nataka tuwe wakweli , je hilo linawezekana kweli..tuweni wakweli tu…, kwa taratibu za
benki, zilivyo kwa mtu kama mimi, au kwa mtu yoyote kuweza kuchukua deni,
achilia mbali, kwa niaba….lakini hapa kuna swala la sahihi ya mtu, kuna dole gumba, la muhusika, je mimi
nilikubaliwaje kuchukua , au kuweka sahihi kwa niaba..je ni kweli sahihi hiyo
ni yangu, kwa niaba ya kaka yangu, ambaye ni marehemu…?’ akauliza.
‘Utuambie wewe sasa,
maana sisi hatukuwepo, na wewe umetajwa kuwa ndio wewe ulifika kuchukua hilo
deni, ukaleta kumbukumbu zinazohitajika, na wewe ulifanikisha hilo…’akaambiwa.
‘Jibu ni kuwa
haiwezekani,…si ndio hivyo,..huo ndio ukweli, haiwezekani, na kama alivyosema,
msemaji mmoja, maswala la mikopo yaliwekewa kitengo maalumu na waliohusika
walifika kwenye kitengo hicho maalumu, sasa mimi sikumbuki…kwakweli, naomba
nifahamishwe vyema, ilikuwaje….?’ Akauliza.
‘Sisi tutakufahamisha
nini, …wewe kwa vile umetajwa kuwa ndiwe uliyehusika kwa hilo, tunataka
utuambie wewe ulifanyaje, au ilikuwaje..’akaambiwa.
‘Kabisa… kabisa
mnakubaliana na kauli hiyo,..ya maneno tu, kuwa mimi ndiye nilihusika na hilo, kwanini
mumuamini kiasi hicho,..! Jamani,
fanyeni kazi yenu vyema, mimi sielewi hapo….’akasema na kukaa kimia.
‘Tunakusikiliza wewe,
hatuna muda wa kupoteza leo….leo, hatuwezi kuchukua siku nzima kwa hii kesi
moja tu…’akasema hakimu.
‘Ina maana kuna mbinu
zilitumika, muheshimiwa hakimu, sio bure tu, ..na hizo mbinu haziwezi kufanywa
na mtu nje ya benki,…kwani benki wana taratibu zao, na mtu wan je huwezi
kuzivunja, au sio, sasa iweje mimi mtu wa nje nishutumiwe kwa kauli ya mtu
mmoja tu…’akasema, na hakuna aliyemjibu.
‘Ni sawa,…mimi nakiri kuwa
kweli nilikuwa natumika kwa niaba ya bro ambaye ni marehemu, nilikuwa nachukua
pesa kwa niaba yake…lakini nasema kwa kuapa, sikuwahi kujaza au kupeleka fomu
ya kuomba mkopo kwake, akajaza akaweka sahihi, nikarejesha benki,…hilo halipo
jamani…’akasema
‘Kwahiyo…unataka
kusema nini…ni nini kilichokuleta hapa?’ akaulizwa
‘Kwahiyo, mimi nasema
hivi, kama hilo deni lilitolewa,… mimi sijui lilitolewa vipi, na ndio maana
nikawa nimesimamia kwenye ushahidi wa benki nikiamini huenda ni kweli hilo deni
lilitolewa kwa bro, labda bro alichukua na hakutaka mimi au mkewe alijua hilo…’akasema
‘Usitake kutuchanganya
hapa…’akasema wakili wa kutetea madeni.
‘Sio kuwa
nawachanganya, huo ndio ukweli jamani,…hapa ni mahakamani, mimi naongea kama
Dalali, najua dhima ya hili kama nitadanganya, mimi sijui lolote zaidi ya
nakala za benki kuwa deni hilo lilichukuliwa na marehemu, sasa kama kulikuwa na
mbinu nyingine kiukweli mimi sijui…’akasema Dalali.
‘Kwahiyo huyo shahidi
aliyepita, alidanganya , kwa kusema wewe ndiye unahusika na hilo deni…?’
akaulizwa
‘Alisema hivyo kuwa
mimi ndio muhusika wa hilo deni…?’ akauliza
‘Unauliza kama hujui,
kwanini sasa umefika hapa kuikana hiyo kauli, …huyo shahid alisema wewe ndiye
uliweka sahihi, ya hilo deni kwa niaba ya kaka yako, na wewe ndiye ulifanya
utaratibu wa kupata dole gumba..’akaambiwa.
‘Mimi ndiye niliweka
sahihi, hapo kwenye hiyo stakabadhi ya benki, kuna onekana sahihi yangu, kuwa
nimechukua kwa niaba…sio kweli…huyo shahidi aje ayaseme hayo maneno mbele
yangu, anithibitishie kwa ushahid kuwa mimi ndiye nilifanya hivyo…mimi
sikubaliani na shutuma hizo…’akasema Dalali.
‘Unasema hivyo kwa
vile wewe unajua kuwa msemaji hyupo hapa, hajiwezi,…si unajua huyo shahid ni mahututi, hataweza kuja kupingana na wewe
hapa, na wewe unachukua nfasi hiyo kupoteza muda hapa…’akaambiwa.
‘Lakini hii ni
mahakama, kauli yangu inukuliwe,..kuwa mimi sijui lolote kuhusu hilo deni zaidi
ya ushahid wa benki kuwa deni hilo ni la marehemu kaka yangu, sasa kama kuna
vinginevyo, kuwa kuna njama zilifanyika, mimi nanawa mikono, sizijui kabisa…’akasema.
Dalali akaigiza kama ananawa mikono…alipomaliza
kufanya hivyo akaendelea kuongea;
‘Na kusema ukweli
mbele yenu , mimi sikuwa na ufahamu wowote wa hilo deni, wakati kaka yupo hai…hilo
deni nimelisikia siku walipoleta benki barua ya kujulisha kuwa kaka yangu
anadaiwa…’akasema
‘Kaka yako hakuwahi
kukuambia benki kuna deni, …awali hakuwahi kukuambia kuwa benki pesa yake
inachukuliwa bila ya yeye kufahamu…?’ akaulizwa
‘Ni kweli ipo siku,
kaka aliliongelea hilo, kuwa anashangaa kuna pesa imetolewa bila ya ridhaa
yake, akaandika barua, na benki wakasema watafuatilia…na…siku moja wakati…ni.ni
siku ile ilipotokea ajali,..hapana siku kabla, ..ooh, sijui kichwa changu
kipoje…’akawa anajikuna kuna kichwa.
‘Ilikuwaje siku hiyo…?’
akaulizwa.
‘Ndio alinipigia simu
akilalamika…kuwa kuna tatizo benki, nirudi haraka na gari,..kwa muda huo
nilikuwa nalichunguza gari,…na kiukweli, sikuweza kupata muda wa kulichunguza,
ila nilihisi gari lina matatizo…’akasema.
‘Je hayo matatizo ndio
yalisababisha gari, kupata ajali…?’ akaulizwa.
‘Kiukweli…labda
nijilaumu mimi…wakati najaribu hilo gari, nilihisi kuna tatizo..nikaona
nilipeleke gari gereji…sasa wakati nimelifungua, ndio nikasikia simu..ya
bro..kuwa nirejee nyumbani haraka, kuna tatizo benki…’akasema.
‘Ni nani alikupigia
simu…?’ akaulizwa.
‘Unajua hilo
nimeliwaza sana, nimejaribu kufanya uchunguzi wangu binafsi...tatizo,kiukweli
kwa siku ile,…sikuwa makini kukagua ile namba, niliyopigiwa simu, ..na
sikumbuki ilikuwa namba gani, ila …nilijua ni bro…’akasema.
‘Ina maana namba ya kaka
yako haipo kwenye simu yako, hukuangalia kuwa ni namba ya kaka yako au la..?’
akaulizwa.
‘Namba hiyo ninayo
kwenye simu yangu, ila mimi .nasema hivi, siku ile nilipokea bila kutizama
mpigaji, na nikasikiliza, na mimi nikajua ni kaka…kwa haraka , nikijua labda
kuna tatizo kubwa, ikabidi nifunge gari, na kuendesha gari kurudi nyumbani,
muito wa kaka ulionyesha kuwa kuna tatizo kubwa sana…’akasema.
‘Wakati unaendesha
gari kurudi nyumbani ilikuwaje…?’ akaulizwa.
‘Kuna hali,…nilihisi
sio ya kawaida,…lakini akili yangu ilikuwa mbali, kuwazia, hicho alichoniitia
kaka yangu…na nikafika nyumbani, kaka akiwa kakasirika kweli, na muda huo
ameshajiandaa kuondoka…’akasema.
‘Hukumuambia kuhusu
tatizo hilo la gari…?’ akaulizwa.
‘Hakutaka hata kuongea
na mimi…kwa haraka akasema nimpe ufunguo, akaweka mizigo yake kwenye gari..na
kuanza kuondoka….’akasema.
‘Hukumzuia kuondoka na
gari hilo, ukiwa unafahamu kuwa gari
hilo lina matatizo…?’ akaulizwa.
‘Sikuweza,..kaka
akikasirika huwezi kuongea neno mbele yake, usubirie mpaka atulie,..sikuweza
kabisa na ilipotokea ajali, nilijilaumu sana, kuwa mimi nimehusika, kwanini
sikuweza kufanya hivyo, kumzuia…’akasema
‘Kiukweli,... kaka alipoondoka,
nilimuuliza shemeji kuna tatizo gani, shemeji akasema hata yeye haelewei
kitu..basi mimi nikaomba mungu tu..kaka aweze kuende salama na aweze kurudi salama…lakini siku hiyo
haikupita ndio tukapokea taarifa ya hiyo ajali…kwakweli kwa hilo hadi leo mimi najilaumu sana..., ni mimi nimesababisha kifo cha kaka…’akasema sasa akijizuia kulia
‘Kusababisha kwa vipi sasa…?’
akaulizwa
‘Nilishindwa kumzuia,
nilijua gari hilo lina matatizo, lakini yeye hakutaka kunisikiliza ningelifanya nini sasa…’akasema
‘Wanasema wewe ndiye
ulikuwa wa kwanza kufika kwenye hilo gari,...baada y aajali kutokea, kweli si kweli…?’ akaulizwa.
‘Kwa vipi…!?' akauliza kwa kushangaa. Halafu akaendelea kuongea...
'Unajua...mimi
nilifika kwa haraka baada ya kupokea taarifa, ...nilifika na kukuta gari linawaka moto mkali sana…na niliuliza kaka yangu yupo wapi, je
kaweza kutoka kwenye hilo gari, watu wakasema
hawajaona mtu akitoka,..'akatulia kidogo.
'Mimi nikawa sasa nataka kwenda kwenye hilo, gari, moto ni mkali kweli.. watu wakanishikilia,…kwa watu walioweza kuiona
hiyo ajali, watakuwa ni mashahidi wangu, waulizeni watu waliokuwepo siku hiyo,
mimi ninashangaa kusikia eti …nilikuwa wa kwanza kufika kwenye hilo gari,
ku-ku, kiukweli inaniuma sana…’akasema.
‘Baada ya hapo
ilikuwaje…baada ya moto kuzimwa, ..wewe ulifika kwenye gari…?’ akaulizwa.
‘Ndio, lakini kwa kuitikia wito wa askari,…..ili niweze kuutambua mwili wa kaka,..maana ...walisema, aligonga nguzo, akapoteza fahamu, na huo moto unawaka, hakuwa na fahamu, na ilitokea kwa kasi sana, walivyosema watu..mimi nuilifika kwenye hilo gari kwa muito wa askari, kuhakikisha kuwa mwili huo ni wa kaka yangu, nitakuwaje wa kwanza kufika hapo…’akasema.
‘Mbona unarudia uwongo
ule ule..’akaambiwa
‘Sio uwongo
jamani…mimi sasa hivi nasema ukweli ulivyo, nifiche ili iweje,…na huyo anayejiita ni mtoto wangu, aje hapa
athibitishe hilo...'akasema
'Athibitishe nini sasa, kwani alikuwepo kwenye hiyo ajali..?' akaulizwa
'Athibitishe kuhusu hilo deni, maana …mimi sijui lolote kuhusu hilo deni…’akasema hivyo na watu wakaishia kuguna, na ...mara watu wakawa wanaongea kila mtu na lake mpaka hakimu akaingilia kati.
‘Kwahiyo unataka kusema huyo kijana
wako anadanganya, na kwanini unasema ‘huyo anayejiita, mtoto wako..’,?' akaulizwa
'Ndio anayejiita,...nina sababu zangu kusema hivyo....'akasema hivyo.
'Ni kweli kuwa hata yeye hata yeye kasema hujawahi kumkubali kuwa yeye ni mtoto wako, ni kwanini wewe, unamkana
kuwa huyu sio mtoto wako, wakati mama yake kaandika hivyo, kuwa wewe ndiye chanzo cha huyo mtoto…?’ akaulizwa.
‘Sijasema nimemkana…na
ndio ni eeh, eeh,…kwa kauli ya marehemu nikiwa na maana, mama wa huyo
kijana,..'akasita watu wakiguna.
'Nimesema hivi , mimi sikatai, spingi kauli ya huyo mama, …ni kweli, eeh...aliwahi kuniambia ana mimba yangu…lakini
hatukuwahi kulithibitisha hilo, na …kutokana na mageuzi, kuwa mimi nimeoa,…nina
familia yangu, siwezi kukubaliana na hilo, ..kwani kukubali hilo ni kuleta
uhasama ndani ya ndoa yangu…’akasema.
‘Lakini hayo
yalitendeka kabla hujaoa, si ndio hivyo, kuwa wewe uliwahi kumbaka huyo mdada, na mbele ya mahakama
ulikana hilo, alipokushitakia, kwenye kesi, aliyokushitakia wewe…’akaambiwa
‘Mbele ya mahakama
iliamuliwa tukalimalize hilo nyumbani, maana kulikuwa bado na utata mwingi, na sikuweza kukubali au kukataa…’akasema hivyo,
‘Ni ikawaje…?’
akaulizwa
‘Alipoitwa kwenye
kikao cha kifamilia hakuwahi kufika, alikuwa anaumwa,…’akasema
‘Sasa kwanini mke wako
aje kukwazika na jambo kama hilo, hukuwahi kumwambia uliyowahi kuyafanya
ujanani mwako, sizani kama hayo ya ujanani, yatamfanya mke wako akwazike,…na
kuleta uhasama kwenye ndoa yenu…’akaambiwa.
‘Ni
kweli…lakini…mnielewe hapo, mimi sikuwahi kukaa na kukubaliana na huyo marehemu
kuwa huyo mtoto ni wa kwangu, kutokana na historia ilivyokuwa, na niliongea hayo
hata mbele ya mahakamani,..na angelifika siku hiyo ya kikao cha kifamilia pale nyumbani sizani kama
ingelileta shida,…kama ni mtoto wangu, ningekubali tu…’akasema.
‘Je hukuwahi kumfanyia
hayo aliyosema yeye kuwa wewe ulimfanyia…?’ akaulizwa.
‘Ujana una mambo mengi…..na
na…kwa vile kijana mwenyewe hajataka kulikubali hilo, kwanini mimi
ning’ang’anie…'akawa anaongea tofauti na swali lenyewe,
'Yeye, kama anaona kweli mimi ni baba yake alitakiwa tukae meza
moja tulijadili hilo, yeye kama alivyokuwa mama yake ni kiburi tu…sasa mimi
nifanye nini…’akasema.
‘Kwahiyo wewe na yeye
bado mna uhasama…?’ akaulizwa.
‘Yeye ndio ana uhasama
na mimi, mimi sina uhasama na yeye…na visa vyote hivyo anavyovi-fanya vya
kunitia mimi matatani, kunitega,kwa mambo mbali mbali ili mimi nionekane muhalifu,…havitasaidia
kitu , maana kama ni kosa lilishafanyika, na hayo yalikuwa mimi na huyo mama
yake, na niliwahi kumuomba msamaha, …’akasema.
‘Kwa kusema hivyo,
unamaanisha, huyu kijana ndiye kakutega na hilo deni, kuwa wewe uliweza
kulipokea hilo deni kwa niaba ya kaka yako..wakati kaka yako hana ufahamu na
hilo…si ndio hivyo?’ akaulizwa.
‘Narudia tena,
tafadhali mnielewe…mimi sijui lolote kuhusu hilo deni, zaidi ya ushahid wa
benki, kama yeye kanitega kwa hilo deni, mimi sijui..sina ushahidi wa hilo, na
nisiwezi kumsemea hivyo,....ila kumbekeni maswali yangu ya awali,...'akasema
'Maswali gani...?' akaulizwa
'Inawezekanaje
deni hilo lifanyike hivyo,..kwa mujibu wa sheria za benki, na lipite hivyo
kirahisi,..yawezekanaje kwa mtu wa nje kama mimi, nije kuyafanya hayo,...hebu jkaribuni kulifikiria hilo, ..ni hekima ndogo tu,..kiukweli mimi sina ushahidi wa kumnyoshea mtu kidole,..ila jiulizeni hilo...’akasema.
‘Kwanini sasa akutaje
wewe kuwa ndiye uliyeweka sahihi kwa niaba ya kaka yako, ?’ akaulizwa
na kabla swali halijamalizika, yeye akasema;
‘Mimi hapo kwakweli sijui…kwanini anisingizie mimi hivyo..., ndio maana nilitaka niliongee hili mbele yake, anielezee ilikuwaje,...lakini kwa bahati mbaya nilipofika tu yeye, sijui kwa kuniogopa akapoteza
fahamu..’akasema.
‘Kwanini akuogope?’
akaulizwa.
‘Labda ni kutokana na..mimi
sijui, kwanini ilitokea hivyo, labda alimuona mama yake, au mzimu wa mama yake..ukamuonya kuwa anachokifanya sio sahihi,…nimesikia akisema kuwa mama yake alimkanya kuwa
asije kunilipizia kisasi mimi..kwa haraka hapo utafikiria nini,..wanawake wa siri kubwa
mioyoni mwao..’akasema.
'Una maana gani kusema hivyo...?' akaulizwa
'Nawaza tu..kutokana na historia ya huyo mama, ilivyokuwa...mengi yalisemwa juu yake, na ..sio kuwa yote yalikuwa ni kweli..lakini kuna ambayo mimi nayafahamu, ..siwezi kuyasema hapa...'akasema
‘Je ni kweli kuwa wewe
uliwahi kumfanyia mama yake huo ubaya, na unyama wa kumkata ulimi, kwa kifaa
chenye kutu..?’ akaulizwa.
‘Hayo, mengine kiukweli mimi siyajui, na…na kiukweli, …jamani siku ile ilikuwa na mikanganyko mingi,
nililewa…sikujua nilitendalo…sasa mimi siwezi kukubaliana na hilo moja kwa
moja,....ni kweli kuwa niligombana naye, na siku ile, alitamka maneno ya
kunikera, yaliyonifanya nikasirike sana…'akasema
'Je ni kweli uliwatuma watu wafanye hivyo...?' akauliza
'Lakini mimi sikuwaambia wamkate ulimi...sikuwaambia wa..wa...muue, hapana hayo sijui yalitoka wapi,,,niliwaambia wamfundishe adabu tu ..’akasema.
‘Ina maana hayo
aliyoyaandika huyo mama kuwa wewe ndiye ulimfanyia hivyo, na wakati yanafanyika hivyo wewe ulikuwepo, kaandika uwongo,..je ni kweli kuwa wakati kitendo hicho kinafanyika wewe ulikuwepo maana yeye aliandika hivyo…?’ akaulizwa.
‘Nasema hivi mimi…siwezi
kuyakataa hayo madai,,… kipindi kile , ujana, ulevi, na…na kuogopa, ilibidi
nifanye mambo ambayo sikutaka yafanyike, ..lakini sikumbuki kitendo hicho cha
kumkata ulimi, mbona ni unyama mkubwa sana huo,…aah, hapana, labda wale wahuni
tu, sio mimi…’akasema.
‘Kwa kauli yako hiyo , kwa hivi sasa inatufanya tukutilie mashaka, kuwa wewe sio mkweli…hayo maneno aliyaandika
marehemu, ..na inavyoonyesha kwenye maandishi yake yeye alikuwa akikupenda
sana,..sasa kwanini akusingizie kitu kama hicho…?’ akaulizwa.
‘Jamani, hayo ya mimi
na yeye, ningeliomba tuyaache,..kiukweli mimi nakiri kumkosea, lakini
aliyoyafanya, yeye ndiyo yalinitia hasira…hamjui alinifanyia nini, na sio
vizuri mimikumuongelea vibaya marehemu, wakati hayupo hapa duniani,..…mengine kayaficha
hakuyaandika,…nahisi kwa kwa masilahi ya mtoto wake, je nyie mnataka yasemwe, sio
vizuri jamani…’akasema.
‘Ni hasira gani za
kufikia kumfanyia binadamu unyama huo wote, hapo ndio sisi hatukuelewi, hasira
zilitokana na nini…?’ akaulizwa.
‘Jamani, sijui
nisemeje…labda mnataka nionekane kuwa mimi ni mnyama, au sio ili nifungwe,
ninyongwe..si ndio hivyo, sawa..., kama hilo litasaidia eeh, ili nisamehewe dhambi zangu, sawa...mimi nipo
tayari…nifungeni tu, au ninyongeni tu…lakini siwezi kuyaongea hayo mengine sio vizuri…’akasema.
Alikaa kimia baadae
akaongeza haya maneno….
‘Na…mengine
niliyafanya,..naweza kusema ni akili za ujana ..na kutokujitambua, na, na..nilifanya
vile…ili kujiokoa kwenye mikono ya kaka yangu, …’akasema.
‘Kwa vipi…ujiokoe kwenye mikono ya
kaka yako…?’ akaulizwa.
‘Kiukweli kama kaka
yangu angeliligundua hilo..misaada yote kwa ajili yangu, maana mimi nilikuwa nasaidiwa na yeye, ...na..nilikuwa na ujana mwingi,..ila nijua kuigiza, ili kaka anione ni mwema sana,..kiukweli kaka aliniamini sana,...sasa ninani angelikubali hiyo misaada isitishwe, na nina
imani, ..angehakikisha kuwa mimi nilifanya hivyo kwa huyo binti....ningelifikishwa…kwahiyo kwa akili za kitoto,
niliona bora,..huyo mwanamke atokomee, asioekane hapo karibu...’akasema.
‘Kwahiyo kumbe kweli
ulidhamiria kumuua, au huko kumtokomeza kulikuwa na maana gani..?’ akaulizwa
‘Mnataka mimi nisemeje
sasa…ule ulikuwa ni ujana. Jamani, nimeshawaambia hilo, hasira zilinizidi
kupita kiasi...kiukweli nyie hamjui tu, mtu nilimuamini, nikajitolea…nikamuhifadhi
sehemu, kwa gharama zangu, tena za kudanganya hapa na pale,halafu, hapana …inaniuma sana,…’akatulia
‘Unajua sisi bado
hatujakuelewa, yeye kakiri kuwa yeye alikupenda sana,ndio maana hakutaka kabisa uje
kufanyiwa lolote baya, lakini wewe unavyoongea ni kama haupo hivyo, ni kwanini…?’ akaulizwa.
‘Hivi mumesikia, ni kwanini nilitamfutia sehemu...tatizo ni kuwa yeye alikuwa mfanyakazi wa ndani...sasa, mnajua wenyewe nina maana gani,...na...unajua mengine sikutaka kuyasema...'akatulia, halafu akaendelea kusema;
'Ni kweli nimeyasikia
hayo, kuwa kweli alinipenda hivyo, ..na hata akawa radhi kesi yetu imalizikie
nyumbani, akanisamehe, na mimi kuonekana
sina hatia, maana kama kweli angeliamua, ningefia jela,…najua kiukweli mimi nina hatia, na nipo tayari …kuwajibika kwa hilo…lakini..’akasema na kutulia.
‘Hilo umelikubali,
..kuwa kweli ulimfanyia huyo mama unyama huo aliandika, sasa huoni madhara yake yamekimbilia
kwa mtoto kalifahamu hilo, ..unafikiri kama ungelikuwa wewe mama yako kafanyiwa
hivyo, ungelikaa kimia..?’ akaulizwa na hapo akabakia kimia.
Muulizaji akaendelea...
‘Kijana wako kwa kauli
yake alisema hivi…’Aliyechukua huo mkopo, aliyeweka sahihi, si mwingine,… bali
ni Dalali, baba aliyemuangamiza mama yangu…’..na kweli wewe umekiri kuwa wewe ulimfanyia mama yake hayo mabaya,.. sasa tunajiuliza wewe uliwekaje sahihi, na sahihi inayoonekana ni ya kaka yako..
Pili,.dole gumba liliwekwaje...maana dole gumba ni la kaka yako...na wewe ndiye inasadikiwa, kwa kauli ya kijana wako, ndio wewe ulifanikisha hilo kwa vipi, tuambie, ili tujue kuwa wewe ni mkweli na unataka kesi hii iishe...'akaambiwa
Na tatu, nilini haya yalifanyika ni baada ya kaka yako kufariki, au yalifanyika kipindi bado yupo hai, ..sasa kwa mara ya mwisho, sisi tunataka kauli yako,
ili tusije kulaumiana tena kwa hilo, je yeye, kijana wako kadanganya, kwa hiyo
kauli, sio kweli kuwa wewe unahusika na hilo deni, au wewe ndiye unadanganya, sisi tuna ushahidi wote hapa, …?’ akaulizwa hilo swali.
Dalali, akabakia kimia...kama anawaza jambo...halafu akainua kichwa na kumuangalia hakimu...ndio akaanza kuongea...
NB: Nimeshindwa
kumalizia
WAZO LA LEO: Ndani ya hasira yupo ibilisi.. hasira mara nyingi humvuta mtu
akafanya yale anayoweza kuja kuyajutia baadae, wengine wanasema wakiwa na hasira
ni bora waseme sana, au wafanya jambo, hata la kuumiza,…wengine hufikia kulia
tu... Je baada ya matendo hayo, unakuwa umefaidika na nini hasa..hujaumiza watu
wengine huenda walikuwa hawana hata kosa…tujue fika,..hasira ni hasara,
Ni nini iliyobora
ukifikwa na mtihani huo, kwanza,…tulia, fikria kwa makini, huku ukimuomba
msaada mola wako, ili akupe utatuzi wenye busara, kumbuka jambo moja, kila
jambo lina sababu yake, je hilo jambo lililokufanya ufikwe na hasira
ulishalifahamu ni kwanini lilitokea, je ni kwa dhamira mbaya ya mtendaji au ni
bahati mbaya….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment