Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 20, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-23


Dalali akawa anasita kuitoa hiyo simu, na mpelelezi sasa akawa kamkabili kasimama mbele yake,  wanaangaliana.

‘Afande hiyo sio haki…’akawa analalamika Dalali, huku taratibu akitoa simu yake mfukoni…, na niliona vidole vikihangaika kubonyeza batani za ile simu, na mpelelezi kwa haraka akanyakua mkononi mwake..

‘Lakini afande hiyo sio halali, kuna kibali gani cha kuichukua simu yangu, mimi sio muhalafu, au nimefanya kosa gani, na …’akalalamika, na mpelelezi, akawa kaishikilia tu ile simu, bila hata kuiangalia, na wakati huo huo hiyo simu ikaanza kuita. Kwa mngurumo,ina maana hakuweka sauti ya kengele au mlio wa simu.

Mpelelezi, akatizama namba,…na alibonyeza kitu, akainua ile simu na kumkabidhi Dalali, ..

‘Pokea simu yako…’akasema, na Dalali akaichukua huku akimtizama huyo mpelelezi machoni, kwanza niliona uso wa kujiuliza kitu kama hicho,  alijua sasa simu inachunguzwa, lakini hakuona mpelelezi akifanya hivyo, na sasa anarejeshewa…

‘Pokea simu yako…’akasema mpelelezi, na Dalali akageuka nyuma, na akawa anaipokea ile simu…hakussema halloh, ila sauti kubwa ikasikika humu ndani..ikisema;

‘Mbona nakupigia simu hupokei, bado upo nahao watu,..sasa sikiliza, uwe makini sana..na kuanzia sasa usinipigie simu, kama nitakuhitajia nitakupigia mimi, unasikia, kuna hali inayoendelea siipendi kabisa, yale mambo yameanza kuleta matatizo, nilikuonya lakini….’ Kumbe mpelelezi alikuwa kaweka spika, sauti ikawa inasikika.

Dalali alipoona hivyo, akawa anahangaika kuzima hiyo simu, lakini hakuweza kufanya hivyo na sauti ikaendelea kusikika;

‘Mbona kimia…’ sauti ikasema na dalali akakohoa tu.

‘Kama bado upo na hao watu sawa,…..ila mimi nitapotea kwa muda…mpaka hali itulie, na sitaki uongee lolote kunihusu mimi tena,..haya uliyataka wewe, na nilikuonya kuhusu hilo, unaona matokea yake…sasa unaniharibia maisha yangu,…siwezi kukaa ofisini tena, natafutwa, kwanini natafutwa..lolote likitokea nitakuonyesha kuwa mimi ni nani…kwaheri…’simu ikakatwa.

Mpelelezi, akawa anamuangalia Dalali, Dalali akawa kanywea, lakini kwa haraka akasema;

‘Huyu jamaa bwana…unajua …nilitakiwa nikutane naye, ni mteja wangu, …’akasema Dalali akasema;

‘Ni mteja ndio lakini ni nani…?’ mpelelezi akauliza

‘Nimesema ni mmoja wa wateja wangu, wa kazi zangu, je nahitajika kuwataja wateja wangu kwako, kwa kosa gani, kwanza , kwanini, nina haki yangu afande..’akasema Dalali

‘Anaitwa nani, ..?’ akauliza mpelelezi

‘Ninalinda haki za wateja wangu, kama kuna kosa nimefanya, basi, lielekewe, ili hata nikimtaja nilindwe kisheria,..’akasema Dalali

‘Dalali…Dalali…nilikuoanya tokea awali, ..nilikuambia nini..?’ akauliza mpelelezi

‘Niwe mkweli…’akasema Dalali

‘Lakini  umekuwa muongo,..nauliza tena huyo uliyekuwa ukiongea naye ni nani..?’ akauliza mpelelezi

‘Ni mteja wangu afande..’akasema

‘Ndiye huyo uliyekuwa ukiwasiliana naye awali mbona hiyo namba haina jina la mpigaji, ..?’ akaulizwa

‘Hap-hapana afande, sio yeye, huyu ni mwingine afande, lakini…’akataka kuongea lakini afande akamkatiza

‘Naomba hiyo simu yako..naona sasa hatuaminiani…’akasema mpelelezi, na Dalali, akamuangalia mpelelezi kwa uso wa kushangaa.

Sasa hivi Dalali, akamkabidhi Mpelelezi ile simu, huku akionyesha kutokujali, na mpelelezi akaichukua ile simu akawa anakagua kagua, kwa kubonyeza bonyeza namba, …hatukujua anachokifanya, baadae akasema

‘Namba iliyopigwa sasa hivi, sio hiyo iliyokuwa unatuma ujumbe,..niambia ukweli, ni nani huyu mtu..maana mimi nitafuatilia..na kwanini akuambia anatafutwa na polisi mumefanya kosa gani…?’ akauliza mpelelezi

‘Huyu ni mmoja wa wateja wangu,…ni mambo yetu, wakati mwingine watu hujiingiza kwenye kesi za kutapeliana,…siwezi kukueleza zaidi,….’akasema Dalali

‘Basi mimi nitakukamata kwa kosa la kujiingiza kwenye biashara za kutapeliana..’akasema mpelelezi.

‘Afande, huo ndio utaratibu kama kweli unahisi nimefanya kosa, mimi sijakueleza kuwa nimeingie kwenye bashara hiyo, ila mwenzangu kashukiwa hivyo, na sio kweli kuwa kafanya hivyo, na…utaona hata wakienda mahakamani hana hatia..’akasema

Mpelelezi akawa anainakili ile namba kwenye simu, yake, halafu akageuka nyumba akatembea hatua mbili akiwa anapigia ile namba, …halafu akageuka

‘Haipatikani..’akasema na baadae akawa anapiga namba nyingine

‘Haipatikani nayo pia…’akasema mpelelezi..

‘Mimi sijui kwanini kazima simu yake..’akasema Dalali
Mpelelezi baadae akanigeukia, na kusema;

‘Jamaa yako huyo…anajifanya mjanja,…’akasema mpelelezi.

‘Niendelee naye…?’ nikauliza

‘Hapana kwa amri ya wakubwa zangu, wewe sasa upochini yaulinzi kama nilivyokuambia, kwa makosa niliyokutajia, mengine utakwenda kuyaongelea huko mbele,…kazi yangu ni hiyo kwasasa,…’akasema mpelelezi.

‘Afande hapa tunacheza na muda!….’ nikasema

‘Sikiliza mimi natimiwa wajibu wangu, siwezi kujadili amri ya wakubwa wangu..na kwa taarifa tu, huenda kesho mnada ukafanyika..’akasema

‘Ndio maana nilitaka nimalizane na huyu Dalali, ili uone kosa lipo wapi, ili na wewe ukaweza kulitetea hili..nakuthibitishia kuwa hapa kuna tatizo, na hilo deni, lina utata..na huo utata, tunaweza kuujua kwa kupitia kwa Dalali..’nikasema

‘Sawa ….kwani napinga hilo, lakini kwanza natimiza amri ya wakubwa zangu..’akasema

‘Ni sawa siwezi kukukatalia hilo, ila…jambo moja, ..nikuulize tu, mimi nimefanya kosa gani kwa hivi sasa, kwa jinsi unavyoona wewe, sema ukweli wako kutoka moyoni , mimi nakufahamu sana wewe…, wewe ni mtu unayesimamia sheria, na wakubwa wako wanaweza kukosea, kuna mtu kawaingilia huko juu,..’nikasema.

‘Hilo halitasaidia kitu…’akasema akiangalia saa yake

‘Wanadai mimi nimeingilia amri ya mahakama?, mimi naweza kufanya hivyo kweli hebu lifikirie hilo kwanza, ..?’ nikamuuliza

‘Si ndio hivyo umeshafanya, kwanini amri ya mahakama haijafuatwa, kwa maelezo ni wewe umemtumia wakili kuweka pingamizi,..lakini je una kibali gani cha hii kesi, huna, kwa ushahidi wangu huna kibali, au niambie umepatia wapi kibali..?’ akaniuliza

‘Afande mimi nilikuwa naumwa, na nikamtuma wakili afuate taratibu zote,..na wakati anafanya hivyo, tuone jinsi gani ya kukusanya ushahidi, na haya yanatakiwa yafanyike kwa haraka kutokana na muda..’nikasema

‘Kwahiyo kweli uliagiza amri ya mahakama isifanye kazi yake…?’ akauliza

‘Tuwe wa kweli afande …mimi nina uwezo gani wa kufanya hivyo, ..haya unadai nimetoa rushwa,…kwa pesa gani nilizo nao mimi..unanifahamu nilivyo, ..je hao watu wamepewa shilingu ngapi, na nani..?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui hayo ni madai yaliyofikishwa huko ofisini…’akasema

‘Afande, je unataka haki itendeke au hutaki, je kama ingelikuwa wewe ni marehemu sasa hivi, familia yako inafanyiwa hivi, na umepewa namna ya kuangalia, ungelijisikiaje..tusisahau kuwa na sisi ni marehemu watarajiwa…’nikamwambia

‘Sikiliza hayo unayoyaongea sio jukumu langu, na sasa hivi tunaondoka,..sema nataka kumalizana na huyu mtu kwanza…’akasema akimgeukia Dalali.

‘Basi mimi naomba muda kidogo, tumalizane naye kwanza, ili niweke mambo yangu bayana..na huko tutakwenda tu, najua hakuna jambo …’nikasema

‘Muda gani unahitajia…’akasema sasa akiangalia saa yake.

‘Mhh…’kabla sijasema kitu Dalali akadakia

‘Afande huyu mtu ni mwongo, hana jipya, tokea awali, anadai ana maswali ya kuniuliza, haya tumempa nafasi hiyo, kauliza nini cha kukusaidia wewe…hakuna, ni kubuni buni uwongo tu,…sijui ni mtunzi wa hadithi za kufikirika nini…’akasema Dalali.

‘Hujakosea ndio kazi yake…’akasema mpelelezi.

‘Ndio maana…nilikuwa najiuliza hayo maswali yote yanatokea wapi,..afande huyo mtu ni tapeli,…uwe makini naye…’akasema Dalali, na hapo nikaona kanipatia mwanya wa mimi kuingilia kati.

‘Utapeli wangu ni nini…?’ nikamuuliza Dalali

‘Kwanza umekiuka amri halali  ya mahakama, kwasababu ilishahukumu kuwa nyumba hii ipo kwenye taratibu za mnada baada ya mahakama kurizika na ushahidi,  kuwa kweli hilo deni lipo,…’akasema Dalali.

‘Na… na mwenye deni aliweka nyumba hii kama dhamana,…na benki wana haki yao kisheria, sihitaji kukufanulia tena wakati nilishakuelezea kila kitu..na mengine yanayoendelea ndani ya nyumba hii ni kutokana na hilo deni, hakuna jingine, deni lipo linamtesa kaka…’akasema Dalali

‘Hebu nimuuliza hutu mtu, afande…, huyo mkopaji ni nani na ni nani alikubaliana na hilo kuwa nyumba ipigwe mnada?’ nikauliza

‘Kutokana na mahakama ni mwenye nyumba hii…’akasema Dalali

‘Huyo mwenye nyumba hii yupo wapi ….?’ nikauliza

‘Mwenye nyumba ni marahemu…’akasema

‘Ni marehemu sio…sasa yeye alikubalije kuwa mnada upigwe wakati ni marehemu?’nikasema kwa kuuliza

‘Si aliandikisha kuwa nyumba yake iwe dhamana,..ina maana kwa kufanya hivyo, hata akifariki nyumba hiyo inaweza kulilipa hilo deni, si ndio maana ya dhamana au, hata kidini mtu akifa cha kwanza ni kuuliza madeni ya marehemu, au sio ?..........’akasema Dalali

‘Ni nani kwenye nyumba hii alilithibitisha hilo..au ushahidi gani uliowahi kutoka kwenye nyumba hii au kwenu nyie, maana tangia awali ulisema marehemu alikuwa hapendi deni,…’Dalali akanikatiza

‘Ushahidi upo benki…humu ndani hata kama hakuna ushahid , lakini ushahidi wa kisheria umepatikana, wanao wanaodai…kitu muhimu ni kuangalia mkataba unasemaje..marehemu aliweka dhamana, na ujuavyo dhamana inawekwa kwa mali zisizohamishika..’akatulia

‘Sitaki nikufundishe sheria, lakini wewe unanilizimisha,…na taratibu zote za kisheria zimefuatwa , sio kwamba ni maamuzi tu yangu mimi, hapana, na sio mimi nalifurahia hilo, hapana, nafanya kwa ajili yakuhakikisha haki inatendeka…na kaka huko alipo roho yake ipate kuwa  huru…’akasema

‘Kwa taarifa za kibenki hilo deni lilikuwepo tokea awali marehemu akiwa hai..ni kwanini hilo lisijulikane kwenu..kwanini likaja kujitokeza baada  ya kifo cha huyo marehemu..?’ nikamuuliza.

‘Inavyoonekana labda bro, hakutaka hilo deni lijulikane kwa vile hakupenda kukopa, na nia yake huenda ni kulilipa haraka iwezekanavyo..’akasema

‘Hilo deni lina muda gani..?’ nikamuuliza

‘Mhh..kumbukumbu za benki zitajionyesha, hilo siwezi kulijibu maana sijaweka mahesabu yake,…ila banki wanaweza kukujibu hilo swali lako.

 ‘Afande tulichogundua sisi kwa muda mfupi tu, hilo deni limewekwa kwa marehemu kinamna, …hilo deni sio  la marehemu,…’nikasema na Dalali akadakia na kuuliza

‘Una ushahidi gani, hapo unaonyesha jinsi gani ulivyo mbumbu,..benk wanajua kazi yao, haiwezekani eni lihamie kwa mtu mwingine kirahisi hivyo…’akasema

‘Mimi nina ushahidi….unataka nikuonyeshe….’nikasema na jamaa alishtuka kidogo halafu akacheka tena kicheko cha dharau, na kusema;

‘Ni deni la nani, hizo hati aliweka nani sahihi , unasema eti una ushahidi, huna lolote bwana, asidanganye watu hapa…mimi nimefuatilia kila kitu…mimi ndiye mwenye uchungu wa hilo, nilihakikisha nimefuatilia hadi kwa wakubwa huko benki, unataka kusema nini wewe..’akasema

‘Si nimekuambia mim nina ushahidi, hutaki nikuonyeshe…?’ nikauliza

‘Nionyeshe…kama utanionyesha mimi nipo tayari kufungwa…’akasema kwa kujiamini

‘Nikuonyeshe ushaidi sio…?’nikasema na mpelelezi akawa makini kulisikia hilo, nikajua sasa nimerejesha mjadala mahali pake;

‘Onyesha, na mimi naapa ukinionyesha huo ushahidi …nipelekeni jela, …siwezi kuitekeleza familia yangu, hii ni mali yetu, nitakuwa na furaha gani ikichukuliwa, ..ni kitu hakiingii akilini..’akasema Dalali

Mpelelezi akakohoa, na kusema

‘Umesema una ushahidi kuwa deni hilo sio la marehemu, unaweza kunionyesha…?’ akauliza mpelelezi

 ‘Ndio lakini kwanza nina ombi kwako…’nikasema na hapo Dalali akacheka kweli na kusema

‘Unaona…huyu mtu hana kitu, onyesha huo ushahidi bwana

‘Una ombi gani….na ushahidi gani ulio nao wewe..?’ Akauliza mpelelezi

‘Ombi langu nataka kuendelea kumuhoji huyu mtu, kuna maswali nilitaka kumuuliza kuhusu uhalali wa hilo deni, na yeye anaweza kunisaidia kwa hilo,…kuna siri kubwa imejificha hapo, nataka kuigundua…’nikasema

‘Ni ushahidi gani ulio nao wewe…?’ akauliza tena mpelelezi

 ‘Ushahidi wangu wa kwanza ni yeye mwenyewe….’nikasema na mpelelezi kwanza akatulia akiwaza jambo halafu akauliza

‘Kwa vipi….?’ Akauliza huku jamaa anacheka kweli kweli, huku akionyesha kwa mikono kuwa kipo wapi .

‘Afande wewe hulioni hilo…?’ nikauliza

‘Niambie wewe…’akasema afande hapo moyoni nikachekelea na kuanza kuelezea;

‘Haiwezekani mtu awe na uchungu na familia, awe na uchungu na kaka yake, atokee mtu mwingine kutaka kusaidia kuupata huo ukweli, halafu yeye awe mstari wa mbele kumpinga huyo mtu, huo ni ushahidi namba moja, tumia hekima utaligundua hilo, YEYE NDIYE USHAHIDI WANGU WA KWANZA…..’nikasema na huyo mpelelezi akaangalia saa yake, halafu akageuka kumuangalia jamaa na jamaa alikuwa bado anacheka kwa dharau, na alipoona mpelelezi anamtizama akatulia

‘Kwahiyo…’akasema afande

‘Nipe muda mchache tu. Utaligundua hilo zaidi..’nikasema

‘Sawa….muulize hayo maswali…’akasema mpelelezi

Mpelelezi aliposema hivyo, nikaona uso wa Dalali ukinywea, akabakia kimia akimuangalia mpelelezi halafu mimi…baadae akasema

‘Afande mimi naufuta huo anaouita ushahidi wake, tusipoteze muda hapa, ni hivi…’akatulia kwanza , halafu akaendelea kuongea;

‘Afande…huyu anasema mimi japokuwa ni ndugu lakini sionyeshi uchungu, je mimi sikufuatilia benki, ushahid huo upo, nilifuatilia ngazi zoye hatua kwa hatua, na ikafikia muda hata kugombana na watu wa benki, kaulizeni hilo

‘Lakini kuna jambo moja, tuwe wa kweli, sheria inasemaje kuhusu deni…ngoja niende kama anavyotaka yeye, eeh…hata kama angekuwa ni mtoto wangu wa kuzaa kakiuka sheria siwezi kuipuuza sheria ya nchi..lakini zaidi ya hayo ni muito wa marehemu, marehemu anataka deni lilipwe,ndio maana haya yanatokea je mimi sijaeleze hayo…’akatulia

‘Umemaliza kujitetea kuhusu hilo…?’ nikauliza

‘Sijamaliza,..nataka nikueleweshe kama mwalimu wa shule kwa mtoto wake,…naona kichwa chako ni kigumu kuelewa…’akasema Dalali

‘Afande…kuna amri ya mahakama..sisi tulikuwepo kwenye kesi, tukashindwa…imeniuma, lakini nitafanyaje,…eeh, sasa kama imefikia hatua hatuna ushahidi hatuna cha kujitetea, ndio nifanye fujo, au…’akatulia

‘Je mimi raia mwema mwenye heshima zangu, nitawezaje kuipinga amri ya mahakama, pili la ziada..ni hilo... la imani, wengi hawaamini, lakini yakizidi huna ujanja,....ni huo  muito wa kaka yangu, hamjui tu..nateseka usiku, silali, familia hii hapa inateseka,,….yote hayo yana uzito, ndio maana nikawa mstari wa mbele kuhakikisha hilo deni hilolinalipwa sasa kwa njia gani, hilo ndilo lilikuwa la msingi la kusaidiwa..’akatulia

‘Afande,…mimi sina pesa, shemeji hana pesa, ulitaka tukaibe…eeh niambe bwana mtunga hadithi za uwongo, afande kasema ndio kazi yako, mimi sijui…niambie sasa,….huo ushahidi wako  una mshiko hapo….hahahaha.’jamaa akasema .

‘Umemaliza kujitetea..?’ nikauliza

‘Umerizika na hoja yangu, …?’ akauliza

‘Sijarizika …maana mimi nilishaanza kuelezea hayo kwa undani,…nilikuwa nakuuliza maswali yenye kubainisha kuwa wewe..uliamua kumtafuta mtaalamu ili kushinikiza hilo deni lionekane ni la kaka yako, ..bado nilikuwa sijafikia maswala ya benki..’nikasema

‘Kwa vipi…?’ akauliza mpelelezi.

‘Umeona yaliyotokea…mwenye uchungu hilo deni anasaidiwa kushinikiza hilo deni lilipwe kwa kupitia mizimu,..ni kwanini…na wakala wa mzimu ni Dalali…akifanya udalali wa mizimu, chini ya kivuli cha Mtaalamu.

‘Ni kwanini kuwe na shinikizo la mizimu, kama ni mkopo wa benki, benki wanafuta sheria..wana ushahidi wao wa kibenki, inatosha, au sio…, sasa kwanini iibuke hiyo mizimu, kuisaidia benki..?’ nikauliza

‘Sawa Dalali anasema ni shinikizo la marehemu maana huko marehemu alipo anateseka, kaacha deni halijulikani, si ndio utetezi wake huo….
Nikageuka kumuangalia Dalali…akatabasamu na kusema

‘Ndio nashukuru umelielewa hilo…’akasema

‘Tuwageukie hao hao mizimu tuwaulize..nyie mizimu ni nani..jibu la haraka ni vivuli vya marehemu kwa njia ya roho au imani…kwa mujibu wa wazee wetu, …lakini je kitaalamu, kiimani za dini , mizimu ni nini….ni vibwengo, au mashetani..’nikasema

‘Sio kweli..’akasema Dalali

‘Kama sio kweli kwanini wanatesa watu wasio na hatia…’nikauliza na hapo Dalali, akakunja uso kwa kufikiri, na kusema

‘Unataka jibu…nilishakujibu, ila wewe ni mgumu kuelewa..’akasema

‘Je wewe si unachungu na hii familia, ..na wewe ndiye mwenye dhamana hiyo,…wewe ndiye jemedari, kwenye vita ni nani anatafutwa,…si kiongozi wa jeshi, kiongozi wa jeshi hapa ni nani…ili deni lishinikizwe kulipwa..?’ nikauliza

‘Hahaha…’akacheka, kabla hajaendelea nikasema

‘Kiongozi ni wewe..ndio maana umehangaika, sasa kwanini hiyo mizimu isikutese wewe au familia yako, inakwenda kuwatesa mayatima, na mjane, ambao hata mwenyezimungu anawatetea sana…’nikasema

‘Sijui….hayo ni mambo ya mizimu..’akasema

‘Hao sio mizimu ni mashetani,…mashetani yaliyotengenezwa..’nikasema

‘Hahaha, …umeishiwa….’akasema

‘Mbona huulizi yametengezwa na nani…’nikasema

‘Kwanini niulize hivyo…?’ akauliza

‘Kwasababu hayo mashetani yametengezwa na mtaalamu…unabisha…?’ nikasema

Hapo mtaalamu akajifanya kucheka sana, lakini niliona kicheko cha kujilazimisha tu.

‘Rejea mazungumo kwenye simu iliyopigwa na huyo mtu asiyejulikana , alisema nini…?’ nikauliza;

‘Huyo ni mteja wangu…’akasema Dalali

‘Alisemaje…nanukuu  ‘’ila mimi nitapotea kwa muda…mpaka hali itulie,….. na sitaki uongee lolote kunihusu mimi tena,..haya uliyataka wewe, na nilikuonya kuhusu hilo, unaona matokea yake…sasa unaniharibia maisha yangu,…siwezi kukaa ofisini tena, natafutwa, kwanini natafutwa..lolote likitokea nitakuonyesha kuwa mimi ni nani…kwaheri’’ mwisho wa kunukuu...'

Dalali akabakia kimia

‘Huyo mtu aliyepiga hiyo simu ni nani...?' nikauliza

'Nilishasema ni mteja wangu...'akasema

'Mtaalamu ni mteja wako sio…’nikasema

‘Wewe ni Muongo, huyo sio huyo mtaalamu…’akasema Dalali

‘Ndio yeye, kaamua kutumia namba nyingine…na kapigia simu hiyo akiwa ufichoni…’nikasema

‘Thibitisha huo uwongo wako…’akasema

‘Kabla sijalithibitisha hilo…nataka ufahamu jambo moja…’nikasema

‘Jambo gani…?’ akauliza

‘Tumeshamfahamu huyo mtaalamu ni nani…’nikasema

‘Ili…iweje, haijalishi hata ukimfahamu, kwangu mimi yeye ni mganga wa kienyeji...’akasema.

‘Ni kwanini huyo mtaalamu amekimbia, hayupo huko nyumbani kwake..na ofisini kwake hakosekanagi kwa muda mrefu, bila taarifa maalumu kwa mkewe, mkewe hajui wapi mumewe kaenda,…’nikasema

‘Mimi nitajuaje,...na, mimi siwezi kumfuatilia,...hata hivyo, mimi naweza kuthibitisha huo uwongo wako, ngoja nimpigie  ….’akasema

‘Mpigie sasa hivi kama utampata…’nikasema

Dalali, akachukua simu akaanza kupiga, ….akatulia akasema

‘Hii inaita…’akasema sasa akiwa anacheka, na mpelelezi  akamsogelea na kuichukua hiyo simu akabonyeza kiwambo cha spika ya nje..kwa haraka, na Dalali, akawa kakunja uso..sasa mlio wa kuita ukawa unasikika.

'Sio sahihi afande...'akasema Dalali...na mara sauti ikasikika.

NB: NAISHIA HAPA


WAZO LA LEO: Mtihani mkubwa wa duniani kwa hivi sasa…, ni kupenda mali, kupenda utajiri, kila mwenye nafasi kwa wakati wake…bila kujali mali hiyo au utajiri huo unapatikanaje,…watu wapo tayari kudanganya,…matajiri kuwanyonya masikini, waajiri kuwanyonya wafanyakazi wao…wafanyabiashara kuwanyonya wanunuzi..nk.. inafikia hata kuwadhulumu mayatima, au hata kuua, watu wanaua hata watoto wao ..ili wapate mali. Hatujiuliza je hiyo mali itatufanya tuishi mielele…wangapi matajiri wameshatangulia mbele ya haki…Tumuombe mola atusaidie katika kuushinda mtihani huo, tupate riziki ya halali, na hata tukipata utajiri uwe ni wa halali.
Ni mimi: emu-three

No comments :