Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 18, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-22


‘Sawa..si unataka tupambane mimi na wewe, sawa mimi nitakaa, uniulize hayo maswali yako, na uthibitishe hiyo kauli yako…kwa ushahidi, la sivyo, mimi na wewe tutapalekana kubaya, sasa hivi sitanii tena, naona unataka sasa kumjua Dalali ni nani akikasirika…’akakaa, huku akiwa kakunja uso.

 ‘Dada natumai upo huru sasa,…usiwe na shaka na lugha yake ya kutishia amani watu, unasikia…., kuanzia sasa tunaitafuta haki, …na haki hiyo tutaipata kwa kutafuta ukweli wa hilo deni, je ni kweli ni deni la mume wako, au ni udanganyifu umetendeka…’nikasema

‘Uliza hayo maswali bwana…’akasema Dalali

‘Na huo ukweli utaanzia hapa hapa nyumbani…’nikasema bila kumjalia Dalali

‘Shemeji huyu mtu hajui lolote …anachotaka yeye ni kutuchuuza,…mimi naogopa sana kuhusu mtoto, je ikitokea tena itakuwaje, sio kweli kuwa mimi naweza kuzuia hayo,…nitawezaje mimi, eeh.. toka lini mimi nikawa mganga wa kienyeji..eeh, eti shemeji wewe si unanifahamu mimi nilivyo..?’ akauliza.

‘Lakini umeweza kumtibia, hebu nikuulize hiyo hali hadi sasa imetokea mara ya ngapi, kwa kauli yako ..ulisemaje, kuwa ikitokea zaidi ya mara tatu haitawezekana tena, je ..imeshatokea mara ngapi nab ado umeweza…’nikasema.

‘Jamani, mimi sifanyi haya kwa utashi wangu mimi, nafuata maagizo ya huyo mtaalamu, na nimetimiza wajibu wangu, sasa ikitokea tena akisema haitawezekaan tena, mimi sitakuja kulaumiwa, ..nitaondoka zangu…’akasema
‘Baba wa familia unakimbia au sio…huwezi kuondoka, hii ni familia yako…’nikasema

‘Kwahiyo sasa umeshaifahamu sehemu yangu kuwa mimi ni nani…’akasema

‘Nafahamu sana ndio maana tunakuandama wewe, ili uwajibike…’nikasema

‘Nimesema nini, na watu hawatii…mtoto anateseka, mama upo, unataka nini shemeji …sijui mnataka niseme nini, eeh,…watu hawajali…tamaa, tamaa tu…mimi nimechoka..ikitokea tena mimi sipo…’akasema

‘Kwani mimi nimefanya kosa gani…?’ akauliza shemeji mtu
‘Kosa hulioni, haya kwanini yametokea,…shemeji, wakati mwingine hizi lawama zitakuangukia wewe…kuteseka kwa mtoto, sasa hivi sababu ni wewe…’akasema Dalali

‘Haitatokea tena dada, asikutishe huyu mtu…, hilo nakuthibitishia, ilimradi shemeji yako yupo hapa, na akikimbia, atakumbana na nguvu za dola ..’nikasema

‘Kwanini unajiaminisha hivyo, mimi nitafanya nini ikitokea, tatizo sio mimi, ndugu hebu nielewe…, kwanini unanitwika mzigo nisioweza kuubeba…’ akasema Dalali

‘Nayasema hayo, kwa kujiamini kwa vile…yote mliyokuwa mkiyafanya wewe na huyo mganga wako wa kienyeji yameshagundulikana…nikuambie hivyo, ili unielewe,  na..muda si mrefu, hayo madude yenu yatakuja kuwageukia nyie wenyewe..’nikasema

‘Nini…’ akauliza sasa akionyesha mashaka fulani, halafu akatabasamu, huku akitikisa kichwa kama kusikitika.

‘Ndio hivyo..ndio maana nimekuambia…usipoangalia hili tatizo kuanzia sasa litakugeukia wewe mwenyewe, na wenzako watakuwa hawapo nawe..’nikasema

‘Hahahaha…..bro bwana, …ndio maswali yenyewe hayo…’akasema sasa akimuangalia mpelelezi.

‘Ni nani aliyekwenda kwa huyo mtaalamu, si wewe ulikwenda kwake, sasa swali ..ulikwenda kwake kufanya nini,…?’ nikamuuliza na hapo, akaondoa ile sura ya kutabasamu sasa akaonyesha uso wa kujali, akasema;

‘Ndio maswali yenyewe hayo bro,… sio kwamba naogopa kukujibu, ila nataka niwe na uhakika..?’ akauliza

‘Nauliza hivi Je huyo mtaalamu alikuja kwako, au ni wewe ulikwenda kwake…?’ nikauliza, bila kujali swali lake

‘Sijakuelewa bado hapo, naomba tuwe wawazi, maana maswali mengine yanaingilia utawala binafsi, kisheria naweza kusema siwezi kujibu hilo swali, kwa maana halina mantiki na huu mjadala…’akasema

‘Hiyo ni hoja ambayo mtaalamu atakugeuka nayo, kuwa yeye hana hatia, wewe ulikwenda kwake kama mteja, ukiwa na shida zako, ukataka kuangaliziwa..si hivyo au kupigiwa ramli, au sio…, na yeye akatimiza wajibu wake, …’nikatulia

 ‘Hahaha bro, wauliza majibu sio, maana umeuliza maswali na majibu unayo wewe mwenyewe,nikuulize tu, kwa hayo maswali eeh.. unataka kuhakiki nini, kuwa mimi nimefanya dhambi ya kwenda kupigiwa ramli au sio..lakini wewe ni mzazi kama mimi, na haya yanaweza kukukuta hata wewe pia, sisi na shemeji ilibidi tuhangaike hivyo,..’akasema

‘Je wewe ulimwambia shemeji yako kuwa unakweda kupiga ramli, kuhusu hali ya mtoto, na yeye  akakubali, ya kuwa wewe na yeye mlikubaliana kuhusu hilo…?’ nikauliza

‘Vyovyote utakavyosema mimi nishaelewa lengo la hayo maswali yako, nia ni kunipata mimi matope, ili nionekane mimi ni mbaya, lakini hutafanikia..’akasema

‘Nimekuuliza swali…’nikasema

‘Nilishakuambia huko  sikuenda mimi peke yangu, nilikwenda na ndugu yake shemeji..na hata hilo wazo la kwenda huko, sikulitoa mimi mwenyewe, hilo wazo alilitoa huyo huyo ndugu yake shemeji..’akasema

‘Je na  kwenda huko kwa huyo jamaa yako siku hiyo ilikuwa ndio mara yako ya kwanza…au ulishawahi kwenda kuonana na huyo jamaa kabla…?’ nikamuuliza

‘Yah…ilikuwa ni mara yangu ya kwanza…au..una maana gani kwa hilo swali lako…?’ akauliza, akishtuka mtego niliomuwekea.

‘Ulikuwa hujawahi kuonana naye kabla ya siku hiyo..?’ nikamuuliza

‘Kuonana kwa maana ya ….ya kufuatilia hilo jambo, au…unajua nikuambie kitu, huyo jamaa yupo na wateja wengi sana, huwezi kwenda kwake kama huna jambo muhimu na yeye, na usichanganye mada, kwenda kwake kwa ajili gani, weka wazi hapo….’akasema
‘Au nikuulize hivi, huyo jamaa yako, nikiwa na maana mtaalamu mnafahamiana naye kwa muda gani…?’ nikauliza

‘Mhh… sikuwa na namfahamu sana kivile,…siwezi kusema kwa muda gani…’akasema

‘Una uhakika na hilo jibu lako…?’nikauliza

‘Nina uhakika kwa vipi, si nimeshakujibu, kama jibu la hilo swali sio sahihi, wewe niambie jibu lake ni lipi....’akasema

‘Wewe na mtaalamu hampo na ukaribu fulani…?’ nikauliza

‘Mimi nina watu wengi nipo nao karibu, siwezi ….sijui…labda ufafanue ukaribu kwa vipi…’akasema

‘Una ukaribu naye kuhusiana na maswala gani…?’ nikamuuliza.

‘Kazi yangu ni nini, ..ni udalali, na kazi ya udalali wateja wako ni kila mtu mwenye shida hiyo, eeh, mimi nafahamiana na watu wengi sana…’akasema

‘Akiwemo huyo mtaalamu,…kweli si kweli…?’ nikauliza

‘Kufahamiana kwangu mimi na yeye, zaidi imekuja baada ya kupatwa na hilo tatizo, vinginevyo…mimi sikuwa na ukaribu naye …., pengine tulijuana naye kama alikuwa na jambo linalohusiana na kazi yangu…labda…’akasema

‘Dalali, nakumbuka afande hapo alikuambia uwe mkweli,…’nikasema na hapo akageuka kumuangalia mpelelezi.
‘Sasa ulitaka nijibu vipi, hivyo nilivyokujibu ndio hivyo, sikuwa na mazoea sana na huyo jamaa,…’akasema.

‘Kwahiyo kujuana kwenu zaidi, ni siku ile ulipokwenda na ndugu yake shemeji, hukuwahi kwenda kwake kabla…?’ nikauliza

‘Nisikilize maana nimeshajua lengo lako…mimi kwenda kwake, kama ilitokea kabla, ni kutokana na kazi zangu za Udalali…’akasema

‘Ulikuwa ukimtafutia wateja,..maana hiyo ni moja ya kazi za udalali, au sio…?’ nikamuuliza

‘Hahaha…. hapana, bwana, jamaa huyo hakuhitajia udalali katika kuuza kazi zake, yeye mwenyewe anajulikana sana…’akasema

‘Kuna kipindi mke wako alikuwa akisumbuliwa na maradhi, ambayo,…ilibidi mumutafute mtu wa namna hiyo, je kipindi hicho ulikwenda kwa nani..?’ aliposikia swali hilo akashtuka, na haraka akasema;

‘Hizo ni siku nyingi sana, na baada ya hapo ilishapita muda, sikuwa na kumbukumbu naye sana, hata nilipoelekezwa tena, ndio nikaja kumkumbuka…’akasema

‘Aliyekuja kukuelekeza baadae ndio huyo mzee Mtupe..?’ nikauliza

‘Ndio…’akasema

‘Wewe na mzee Mtupe mnaelewana sana…?’ nikauliza
‘Sio kivile..unajua huyo mzee ana tabia ya kuchunguza chunguza watu, mimi siipendi hiyo tabia yake, tulikuja kukosana kwa hilo…’akasema

‘Alikuchunguza kuhusu jambo gani..?’ nikamuuliza na hapo akageuka kumuangalia shemeji yake.

‘Mengine hayana umuhimu sana kuyaelezea,..mzee huyo ana tabia chafu, mpaka watu wanamuhisi kuwa yeye ni mchawi..sio mchawi huyo mzee, watu hawamfahamu tu…’akasema

‘Wewe una uhakika gani na hilo…?’ nikamuuliza

‘Huyo mzee ni uchimvi wake tu…ana na tabia za kuchunguza chunguza watu na kujenga fitina, na fitina zake zinazoweza hata kuvunja ndoa za watu…’akasema

‘Huwa anajenga fitina gani kwa mfano…?’ nikauliza

‘Yeye anafikiria kila watu wakikaa karibu, mke na mume wana mambo ya kimapenzi, sio hivyo, mimi kutokana na kazi zangu nakutana na watu wengi tu, wawe wanawake au wanaume…’akasema.

‘Hata wake za watu…?’ nikauliza

‘Hajilishi..ilimradi nachunga maadili….’akasema

‘Kama hamkuwa mnaelewana kivile ilikuwaje yeye akakuelekeza huko kwa mtaalamu..?’ akauliza

‘Siku hiyo wakati tunaongea ni namna gani ya kumtibia mtoto, bahati nzuri na yeye alikuwepo, ndio akasema yeye anamfahamu mtu mmoja anaweza kutusaidia, anajulikana sana…’akasema

‘Na hapo ndio ikawa mara yako ya kwanza kumkumbuka huyo mtu, si ndio hivyo…baada ya kusikia kutoka kwa huyo mzee, ina maana kabla ya hapo, hukuwahi kuliongelea la mtaalamu kabla,…?’ nikauliza

‘Sikuwahi…maana sikuwa na wazo hilo, na akili yangu haikuwa na mawazo ya mtu kama huyo, nilishamsahau kiukweli…’akasema

‘Una uhakika…?’ nikamuuliza

‘Muulize hata shemeji…’akasema akimgeukia shemeji yake

Shemeji yake akashtuka, maana alionekana kuwa mbali kimawazo, na haraka akasema;

‘Mhh…hapo samahani…shemeji unakumbuka uliwahi kunielezea hilo jambo hata kabla ya siku ile, ukasema kuna mtu unamfahamu, ..na nakumbuka ulimtaja kabisa hata jina, ukasema ni mtaalamu mnzuri…, naona umeshasahau…’akasema shemeji yake.

‘Mambo mengi shemeji na huyu jamaa..anayesema ni ndugu yako ananichanganya tu…’akasema

‘Umeona umuhimu wa shemeji yako kuwepo hapa, kukumbusha yale uliyoyasahau, sasa..mimi nashangaa, Dalalai unakuwa msahaulifu sasa, awali uliwahi kusema wewe Dalali, kutokana na kazi yako, unakumbuka sana mambo…je mbona hili umelisahau.

‘Mimi ni binadamu bwana, kusahau sio kosa, au sio…’akasema, akimtupia shemeji jicho kama la kutokupendezewa na jinsi alivyosema.

‘Haya shemeji yako kakumbusha,…kwahiyo ni kweli kuwa wewe ulikuwa ukimfahamu huyo mtu hata kabla hujaenda kwake, na …hata huyoo mzee Mtupe alipowashauri hivyo, wewe ulikuwa umeshakuwa na huo mpango wako…ni kweli si kweli…?’nikasema na kuumuliza.

‘Huyo mtaalamu anafahamika na watu wengi, kumfahamu mimi sio ajabu…na kama niliwahi kwenda kwake kabla,..naweza..ila sio jambo..la ajabu au sio…na sikumbuki vyema…kama niliongea na shemeji kabla ya siku hiyo…’akatulia

‘Shemeji…hukumbuki…tulikuwa tunabishana sana kuhusu hilo, sikulipenda, wewe ukawa unanisihi sana….hukumbuki kweli shemeji….’akaambiwa

‘Mhh…yawezekana…ila, …sio vizuri…’akasema akimuangalia shemeji yake

‘Sio vizuri kwa vipi, kukumbusha au…?’ nikauliza

‘Haya ni mambo ya kifamilia, …heshima ya mke ni kuwa na mume wake,..sio kwa vile mimi ni shemeji basi aniumbue tu mbele za watu…’akasema

‘Samahani shemeji, mimi nilitaka kukumbusha tu…’akasema shemeji yake.

‘Umefanya vizuri sana..ukweli ni jambo jema sana…’aliyesema hivyo ni mpelelezi, na Dalali akageuka kumuangalia mpelelezi, na kusema;

‘Ni kweli, nashukuru kanikumbusha,..hamna shida,…sio kwamba nilisema uwongo kuficha jambo hapana…’akajitetea Dalali.


‘Dalali…haya ninayokuuliza yameshafanyiwa kazi, sio kuwa nakuuliza tu kupoteza muda, uwe mkweli ili ujiweke salama..’nikasema

‘Mimi nimekuwa mkweli kuwa asilimia kubwa, na nikiteleza kidogo, …tusameheane, nimeulizwa mambo mengi sana akili nayo inachoka..na.., tatizo la huyu jamaa unauliza maswali ya kunitega, ili niingie kwenye anga zake, nisema jambo, ili nionekane muongo, na zaidi ni kama anataka kunishuku mimi kwa jambo lisilo kuwa la kweli…mimi sihusiki kwa shutuma zake…’akasema

‘Sasa …nakuuliza tena je wewe na mtaalamu hamfahamiana sana, sio mtu wako wa karibu ambaye mnakutana mara kwa mara..sio jamaa yako mliyeshibana ambaye mnafanya shuhuli nyingine pamoja…’kabla sijamaliza simu yake ikaingia ujumbe

Aliusoma ule ujumbe halafu akatikisa kichwa kama kukubaliana na hilo jambo akasema;

‘Mtaalamu anasema, tusiwe na wasiwasi ila tuwe makini na mipango yetu, mipango yetu iwe inalenga jinsi gani ya kulipa hilo deni, yeye huko atajitahidi kuhakikisha kuwa angalau tunakuwa salama kwa leo…’akasema

‘Ni hayo tu…’nikasema

‘Ndio…’akasema

‘Hajakuambiwa jambo jingine…’nikamuuliza na hapo akabakia kimia

Nikageuka kumuangalia mpelelezi, na mpelelezi akawa anaandika jambo, na mara simu yake ikalia,…akawa anaongea na simu kwa dakika mbli hivi, alipomaliza mimi sikutaka kujua nini huyo mpelelezi alikuwa anaongea, nikasema

 ‘Dalali tusipotezeane muda hapa, sema ukweli wako, kuhusu wewe na mtaalamu..je wewe na yeye hampo karibu sana, na mara kwa mara unakwenda kwake..je huko unakwenda kufanya nini…?’ nikamuuliza
‘Bro,… thibitisha hiyo shutuma yako, hilo la kwenda kwa mtaalamu mara kwa mara, umelitoa wapi, sio kweli..niende kwake mara kwa mara kufanya nini…?’ akauliza

‘Dalali, maswali yangu yalikuwa bado, …hapa nilitaka kukuonyesha ulivyo, kuwa hata haya yanayoendelea hapa, unayafahamu…sasa ni kwa kiasi gani na kwanini inatokea hivyo, tunataka wewe uwe muwazi kwetu..je kuna ajenda gani ya siri kati yako na mtaalamu..’nikasema

‘Hakuna muheshimiwa, mimi zaidi ya kazi zangu, na zaidi ya hili tatizo la mtoto hakuna jingine,..mengine ni hisia zako mbaya tu…’akasema

‘Huyo mtaalamu wakati anakupigia simu kasema yupo wapi..?’ nikamuuliza

‘Atakuwa nyumbani kwake…’akasema

‘Una uhakika …?’ nikamuuliza

‘Mimi sasa nitajuaje…kama kweli hayupo nyumbani kwake au la…mfano mimi nipo hapa, ukanipigia simu, si ninaweza kusema nipo nyumbani, ni nani atajua, …kwa mtizamo wangu huenda yupo nyumbani kwake, kama hayupo huko mimi sijui…hilo sio swali, na mimi sina mamlaka ya kujua wapi alipo…’akasema

‘Una uhakika, wewe hujui huyo mtu yupo wapi…?’ nikamuuliza

‘Mimi ninachoweza kusema, huyo mtu yupo nyumbani kwake, kama hayupo huko mimi siwezi kujua …’nikasema

Nikamgeukia afande, na kusema;

‘Afande samahani…mtaalamu ni mmoja wa shahidi muhimu kwenye hii kesi, kama ulivyoona hapa, kuna kitu kinachoendelea kati ya hawa watu wawili…nataka kuthibitisha kuwa huyu mtu hapa, anadanganya yeye anajua wapi alipo huyo mtaalamu…’nikasema

‘Kwani hayupo nyumbani kwake..?’ akauliza mpelelezi

‘Hayupo afande,na hajulikani wapi alipo..’nikasema

‘Kwahiyo unataka mimi nikusaidie nini hapo..?’ akauliza afande..mimi nikasogea pale alipo afande nikamnong’oneza jambo, afande akatikisa kichwa kukataa, akionyesha kuwa hakubaliani na mimi, akasema;

‘Una gani, una uhakika na hili jambo, sikiliza usitunge hadithi zako hapa, siwezi kufanya mambo kitamithilya,… una uhakika gani sasa….?’ Akauliza na simu yake ikaita,…na sasa akasema;

‘Nataka kwenda kuongea nje kidogo…’akasema na kutoka nje, tukabakia watatu, na Dalali akaniangalia akiwa na tabasamu la kejeli.

‘Hivi wewe unataka kufanya nini, unanishuku mimi kwa kosa gani..?’ akaniuliza

‘Nataka kupima uaminifu wako…’nikamwambia Dalali

‘Ili iweje…?’ akauliza

‘Ili kweli tuwe na uhakika wa hilo deni, uaminifu wako ndio utafichua siri ya hilo deni..’nikasema

‘Mimi sikuelewi…hilo deni na uaminifu wangu vinahusianaje, sio mimi nilyekopa, na wala sikuwa na nalifahamu hilo deni, mbona unanichanganya akili yangu..unanitaka nini wewe mtu..?’ akauliza sasa akionyesha uso wa kukerwa.

‘Subiria afande aje,…na kumbuka jambo moja, yeye alishakuonya uwe mkweli, alikuwa na maana yake kubwa sana ya kuja kukusaidia, lakini kwa jinsi tunavyokwenda umeonyesha kuwa wewe ni muongo..’nikasema

‘Mimi sijasema uwongo wowote.., na kwanini niseme uwongo, ili iweje…’akajitetea

‘Kwanini umeficha ukweli kuwa wewe na mtaalamu mnafahamiana..?’ nikamuuliza

‘Mimi ni kama docta, wakati mwingine unatakiwa kuficha siri za wateja wako, nisingelisema nafahamiana naye,..na maswala ya waganga wa kienyeji, unayafahamu, ..kama ulivyosema awali kuwa ramli ni dhambi, lakini inabidi kufanya ..hata kwa siri, sio lazima nikuambie kila kitu bwana…’akasema

‘Ungelisema huo ukweli, tungelikuelewa,… lakini inavyoonyesha,  kuna jambo zaidi ya hilo,..na umeficha ukweli kuhusu huyo mtu kwa vile kuna jambo mumelifanya wawili, na hutaki lijulikane..’nikasema

‘Unataka kusema nini sasa, kuwa kuna kitu unanishuku mimi, ina maana hata kuuliza maswali yako yote hayo, wewe unanishuku mimi kufanya ubaya, haya ni ubaya gani huo nimeufanya mimi..’akasema

‘Dalali…sema ukweli wako..mimi ninaweza kuficha baadhi ya mambo, wewe na mtaalamu mna ajenda gani ya siri…je haihusiani na hilo deni, labda kama ulitaka kumtumia ili kulificha hilo deni labda…hebu niambie, ili niweze kukusaidia..?’ nikamuuliza

‘Hahaha…bro…hizo hisia zako unazitunga kichwani…deni halina ujanja hilo, hata kama utakwenda kwa mganga wa kienyeji, hilo haliwezi kufichika,..benki wana ushahidi wote, na nimesikia huko, benki wametuma barua ya kulalamika mahakamani…’akasema

‘Kakumbia nani hayo..?’ akauliza

‘Sina pokea ujumbe hapa, ..’akasema

‘Nani kakuambia..?’ nikamuuliza

‘Watu wangu,..hata mimi nafuatilia kujua ni nini kinachoendelea, kama unavyofanya wewe, mimi ni dhamana ya hii familia, lazima nijue kinachoendelea…’akasema

‘Ni mtaalamu au ni mtu wa banki kakuambia..?’ nikamuuliza

‘Sio lazima nikuambie hilo…’akasema na mara mpelelezi akaingia, na alionekana kakunja uso, …hakuenda ile sehemu yake, alikuja na kunishika mkono, akanisogeza pembeni, akaniuliza;

‘Unajua unaleta matatizo…umefanya mambo kinyume na utaratibu, umezuia maamuzi ya kimahakama bila utaratibu, na …mumetoa pesa kama hongo, kufanya zoezi hilo lisifanyike, hilo ni kosa kisheria…amri imetolewa wewe ukamatwe,…’akaniambia
‘Mimi nikamatwe…!! Kwa kosa gani..?’ nikamuliza

‘Kuzuia amri halali ya mahakama, na kutoa rushwa…’akasema

‘Mimi nina uwezo gani wa kuzuia amri halali ya mahakama…na ni nani katoa shutuma hizo..?’ nikauliza

‘Nimearifiwa kutoka ofisini, …na mpelelezi mwenzangu kaitwa na wakubwa,…ilivyo, wewe inabidi nikukamate hadi kituo cha polisi kwa shutuma hizo…’akasema

‘Afande, wewe umekuwepo hapa, umesikia jinsi nilivyomuhoji huyo jamaa, wewe huoni kuwa kuna kitu kwa huyu mtu…kuna dhuluma inayotakiwa itendeke, na je…kwanini wewe ulitaka kumuhoji kuhusu hiyo ajali, ….?’ Nikamuuliza

‘Hayo ni mambo yangu…hayana uhusiano na hilo jambo lako…’akasema

‘Mimi naweza kuthibitisha kuwa kuwa yote hayo yana mahusiano…ajali, deni na hawa watu wawili…’nikasema

‘Kwa vipi…?’ akauliza

‘Nipe nafasi hiyo…lakini kabla ya hilo jambo, nataka huyu mtaalamu atafutwe mahali alipo, huyu mtu ni mtu muhimu sana kwenye hii kesi…’nikasema

‘Amri ya wakubwa wangu ni wewe ukamatwe, mim siwezi kulikiuka hilo mengine yatafuata baadae, ..’akasema na nilimtupia jicho Dalali, nikaona akisoma ujumbe kwenye simu yake, na akawa anatabasamu, na hata kusema;

‘Nilijua tu…tapeli mkubwa huyu…’akasema na Mpelelezi akageuka kumuangalia, na Dalali alipoona anaangaliwa akashisha simu yake na kuweka mfukoni.

Mpelelezi akaniachia mkono na kumsogelea Dalali

‘Nipe hiyo simu yako…’akasema mpelelezi


‘Ya nini afande, …?’ akauliza Dalali, akishangaa

‘Nipe hiyo simu yako..’akasema afande sasa kwa sauti ya ukali

NB:Tuishie hapa kwa leo.


WAZO LA LEO: Ukweli na uaminifu unaweza kukusaidia kuepukana na majanga , ukajenga heshima, na hata kusaidiwa sehemu ambayo ungeliingia matatani, Tujenge hulka ya ukweli na uaminifu..ili tuwe salama wakati wowote, uwe wa shida au raha. 

Ni mimi: emu-three

No comments :