Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, July 16, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-21


Dalali aliposoma ujumbe kwenye simu yake, niliona uso wake ukibadilika, japokuwa alijitahidi sana kulificha hilo,…na kwa haraka akageuka kama anaangalia nyuma, halafu akageuka kutuangalia, sasa uso ukiwa umejaa tabasamu akasema;

‘Unajua nimepoteza muda mwingi hapa, napoteza pesa, napoteza, yaani nyie hamjui tu, sisi wa kazi za kubangaiza, ambao hatuji mwisho wa mwezi, mnatutesa kwakweli, siku moja kupotea bure ni hasara kwakweli, lakini sawa tu…..’akatulia akiaangalia simu yake, kuna ujumbe mwingine uliingia, akawa anausoma, alipomaliza akasema;

‘Haya kinachoendelea ni nini, maana nahitajiwa huko…?’ akauliza

‘Kinachoendelea ni kwanza utuambie huo ujumbe uliotumiwa umesema nini….?’ Nikauliza, hapo akaniangalia kwa uso kwa kutahayari, na kusema;

‘Bro, hii ni simu yangu bro…, na mambo ndani ya simu yangu ni mimi na watu wangu hayakuhusu, samahani kwa hilo…labda nikuulize hivi, kweli kuna sheria zakuingiliana kwenye mambo binafsi..?’ akaniuliza halafu akamgeukia mpelelezi na kuuliza.

‘Eti afande hebu tusaidie kwa hilo…labda mimi sina uhuru huo, labda…japokuwa sheria hata mimi nazifahamu kidogo, hii sio haki, au sio afande…’akawa anamuangalia mpelelezi.

‘Inategemea, kama ni mambo ya uhalifu, sheria ipo wazi….’akasema mpelelezi

‘Na nani ni muhalifu hapa…?’ akauliza Dalali.

‘Dalali, watu wanataka kula…familia ina njaa, je utafanya ulivyoagizwa au utakwenda kinyume chake, hayo ni maagizo ya mizimu au sio, kuwa uhakikishe familia imekula…au nadanganya…ujumbe umesemaje, sio hivyo, au…’nikasema na Dalali akaniangalia sasa akinywea, na baadae akasema;

‘Wewe..nimekushakugundua , kuna kitu mnanichezea, mimi sio mtoto mdogo kihivyo,… mimi ni mtoto wa mjini..yawezekana watu wako wameiba namba ya mtaalamu…halafu wanatuma ujumbe,..wakijua ni nini kinandelea hapa, halafu wana..ni..chezea akili, haiwezekani wajue mhhh…’akasema, sasa akiangalia simu yake.

‘Unaona, nilikuambia nini,…kuwa wenzako wote hawapo na wewe tena, sasa maamuzi ni yako, kusuka au kunyoa, ila muhimu tunahitajia hii familia iwe na mazingira ..tunataka shemeji yako aweze kuingia huko jikoni kwa amani..na wewe ndiwe wakala wa mambo hayo, sijasema unahusika,ila wewe si unaelekezwa tu…na mizimu au sio…?’ nikamuuliza na huku nikigeuka kumuangalia mpelelezi.

Mpelelezi akawa ananiangalia kwa hali ya kutaka kuniuliza maswali, lakini hakuweza kufanya hivyo,…najua alishaona akifanya hivyo ataharibu, kwahiyo akakaa kimia,na Dalali akasema;

‘Ok..ok..ngoja tufanye hivi….’ Sasa akatoa unga kwenye kichupa chake, …akasogea pembeni, akachukua chetezo cha mkaa.., akaweka ule unga unga kwenye hicho chetezo, halafu…, akachukua kibiriti, akawasha.

Moto ukawa utafikri ule unga unga ni mafuta ya taa, na haikupita muda, kukajaa moshi, uliokuwa unaenea taratibu, taratibu, na harufu kali ya manukato ikasambaa eneo lote..

Tukawa kimia, tunasubiria…ule moshi ulipotulia, Dalali ambaye alikuwa kainamisha kichwa karibu na kile chetezo, akasimama…na kutuangalia, hakusema neno hapo kwa hapo, ….baadae akasema;

‘Ok,..nimefuata nilivyoelekezwa, sasa shemeji unaweza kwenda kuandaa chakula…na, hata kuingia chumbani,..hakuna tatizo,..hii ni kwa mjibu wa mtaalamu, kanitumia ujume wake nifanye hivyo…’akasema

‘Umeonaeeh, na mimi kumbe naweza kuongea na mizimu…’nikasema huku nikitabasamu, na jamaa akacheka kicheko cha dhihaka, huku akisema;

‘Hahaha…bro, bro….unasema umeongea na mizimu, hahaha…unanichekesha kweli, hao ni mizimu wa familia, hakuna mwingine zaidi ya familia hii anayeweza kuongea nao,labda na wewe uwe mtaalamu wa mambo hayo…’akasema

‘Labda na mimi ni mtaalamu je…’nikasema

‘Lakini bro…wewe si mchezo, …umenipatia changamoto, isingelikuwa haya matatizo, nilitaka tuwe marafiki kidogo…’akasema

‘Kwanini…kwani sisi ni maadui..?’ nikauliza, sasa nikijaribu kutengeneza hali ya kuaminiana.

‘Sikiliza…ninashangaa jinsi gani ulivyofahamu niliyoandikiwa na mtaalamu…lakini sio tija, kwa vile sio maswala yangu, mimi ni mtumishi tu, sina wasiwasi na hilo….sina shaka kabisa…’akasema

Wakati huo shemeji alishaelekea jikoni, na baadae akarudi na kuulizia, ..

‘Kwahiyo hivyo vitu vyote ni vya humu,…maana naona ni vingi sana…?’ akauliza

‘Ndio…ni vya humu, kwa taarifa niliyopewa ofisini …ni bahati sana kupata msaada kama huo, maana mara nyingi hutolewa kama kuna janga la kijamii….lakini haina shida, muhimu haya mambo yaishe..’akasema mpelelezi

‘Tunashukuru sana afande…’akasema Dalali, kukapita ukimia kidogo

Halafu Dalali akanigeukia, na kusema

‘Sasa twaweza kuongea,…maana akili hapa ilikuwa inaniwanga, najiuliza hawa watu watakula nini..huko kwangu kwenyewe ..mmh, hata sitaki kulalamika hapa, lakini huko hakuna shida…najua wife atachakarika,..maana kiukweli leo nimepigika, sina kitu kabisa hapa mfukoni…’akasema Dalali.

‘Wewe ukikosa si unaongea na mizimu yenu tu, wanakuleta chakula…’nikasema kiutani

‘Hahahaha, bro bwana, acha hayo, mimi sio mtaalamu, hata wataalmu wenyewe hawafanyi hivyo, kula ni jasho lako bwana, kama huna pesa huna..utalala njaa, hat yule mtaalamu anategemea wateja waje ili apate riziki yake ya siku, hayo mambo yana masharti yake..’akasema Dalali.

‘Mimi nimeongea na mizimu yako, imesema haya mambo yana mkono wa mtu, na huyo mtu yupo ndani ya hii familia…’nikasema, hapo Dalali, akaniangalia akiwa kanikazia macho, halafu akacheka

‘Hahaha, bro bwana…usilete masihara hapa, hii familia ni mimi na hawa wanafamilia niliokabidhiwa…sasa ukisema hivyo,..ni nani unamshuku…?’ akawa kama anauliza.

‘Mimi sijui ila mizimu ndio imesema hivyo…’ nikasema


‘Afande huyu mtu ni mjanja sana, unajua kama una hasira unaweza ukakosana naye kwa haraka sana, ..ana mbinu mbinu za kuchokonoa mtu, akasirike ili aongee ovyo..lakini sio mimi, mimi ni mjanja, …na hataamini, nitakuja kumshiak seehmu ambayo hataamini, ndio atajua mimi ni Dalali,…’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo..?’nikamuuliza..na Dalali akacheka  ile ya dharau, halafu akasema;

‘Unajua kiukweli niwaambie, …haya mambo yapo..mizimu, ni tofauti na mambo mengine ya uchawi, tusiyachanganye jamani, awali mimi nilikuwa siamini, lakini nilipokutana na huyo mtaalamu , sasa naanza kuamini kuwa hayo mambo yapo..na sio mambo ya kuchezea chezea…’akasema

‘Lakini mimi nasikia hata hayo mambo ya mizimu kama ulivyo uchawi wengine huenda kufanyiwa kwa wataalamu, ….wananunua huo utaalamu, kwa ajili ya kuwahadaa watu wengine…’nikasema

‘Kununua…hahaha, hiyo ndio naanza kusikia kwako,..sikiliza mambo ya mizimu ni ni ya mababu wa familai husika, sasa utayanunuaje, mimi hapo sikuelewi…’ akasema

‘Kama unataka kufanikiwa katika mambo yako, si unayanunua ili uweze kufanikiwa au sio..kwasababu nionavyo mimi hayo mambo hayana tofauti na uchawi..’nikasema

‘Hapana sio kweli, hapo naona upo kinyume na mambo hayo, na hapo ndio naona hujui kabisa mambo hayo…halafu ,..ili iweje, hapana hata kama watasema nitakuwa tajiri, kwa kupitia mambo hayo mimi..siwezi, ..unajua kuna mambo unatakiwa uwe makini nayo, mojawapo ni hilo…kujiingiza kwenye mambo ya mizimu unajifungia kwenye maisha yako ya kawaida..., utaambiwa ukae hivi, usile hivi, usifanye hivi, ni shiida….’akasema

'Kwahiyo wewe umeshaingia kwenye kifungo hicho au sio...?' akaulizwa

'Hapana..sio mimi...mimi ni mumbe tu, ...'akatulia

‘Ni kweli wewe ni mjumbe tu,.., kama ulivyosema, maana hivi sasa hii familia inateseka, sababu si ndio hiyo hiyo ya mizimu, je hiyo mizimu haina huruma, ina maana wewe na ujumbe wako, huna huruma na familia yako…ndio maana mimi nasema huo sasa ni uchawi tu,…’nikasema.

‘Familia hii haiteseki kwasababu ya uchawi hapa..., kuteseka kwa hapa, kama nilivyosema awali..ni sababu ya hilo deni, tukimaliza na hilo deni haya hayatatokea tena..ila kama tutajifanya wajanja, ..si unaona mtaalamu kawaomba, kawazimisha kwa muda, baadae watarudi tena, maana agizo lao halijafanyika, lakini kama tutakuja na njia sahihi ya kulipa hilo deni, aah, hutawaona tena hapa…’akasema.

‘Nikuulize tu, huo mtaalamu kawazimishaje, kawafanyaje hadi wakatoka humu ndani..hao mizimu wenu..?’ nikauliza.

‘Hapo wewe wataka mimi niwe kwenye kichwa cha mtaalamu au sio..’akasema

‘Mhh..lakini wewe si unajua-jua hayo mambo, labda, yeye mtaalamu, kutokana na mizimu au sio, kawalilia hali,  kawaomba kuwa tufanye hivi na vile, watuvumilie , si ndio hivyo, au...sasa najiuliza hivi, ina maana wao mizimu hawajui dhamira yetu..?’ nikauliza

‘Mimi sijui lolote kuhusu hilo,…labda swali hilo tungelimuuliza mtaalamu yeye mwenyewe, au sio…’akasema.

Tuliongea hayo maongezi tukisubiria shemeji awepo maana tulitaka maswali yakiulizwa na huyo shemeji yake awepo kama shahidi, …

Na kweli , mara shemeji akaja kutuarifu kuwa chakula kipo tayari mezeni, tukajumuika na kupata chakula, baadae maongezi yakaanza…

Na aliyeanzisha mjadala huo ni Dalali yeye mwenyewe...

‘Shemeji, ..sasa hivi mimi nimeshawaelewa hawa ndugu zetu, kiukweli nimegundua kuwa, wapo na nia safi ya kulimaliza hili tatizo, hata mtaalamu kaliona hilo, na mtaalamu kafanya mambo yake, kawaomba hao mizimu watupatie muda, ili tutafute namna ya kulipa hilo deni, ..sasa sijui maana hawa jamaa zangu hawajaniweka bayana...'katulia.


'Ila kiukweli mizimu wamesikia kilio chetu...hatujui mpaka lini, kinachotakiwa ni juhudi zetu...zionyeshe dhamira ya kweli ya kulilipa hilo deni, kwahiyo ...eeh, shemeji mimi nakuomba, usiwe na wasiwasi kabisa…’akasema Dalali.

‘Kwahiyo mimi nitakuwa huru kuongea ninavyosikia, ..ukweli wa ninavyojua mimi,..?’ akauliza.

‘Sawa ilimradi iwe hoja ya kusaidia hilo deni lilipwe..’akasema Dalali

‘Nauliza hivi…maana awali sikutakiwa kulipinga hilo deni, …na kila nikifanya hivyo, kuna majitu yanaotokea mbele yangu, je sasa hivi nikifanya hivyo hayatatokea tena, je nikifanya hivyo mtoto wangu hatateseka tena, …?’ akauliza akiwaangalia watoto wake.

‘Dada, sasa hivi lolote likitokea mbaya wako atakuwa ni huyu shemeji yako..unasikia, kutokana na hao mizimu, huyu ndiye anatakiwa kuwazuia, ana uwezo huo wa kuwazuia…’nikasema.

Dalali, akasimama…

‘Unataka kwenda wapi..?’ akauliza mpelelezi.

‘Kama mambo ndio haya mimi sitaki kuendelea na haya maongezi, tulikuwa tunaongea wanaume mambo yetu, utani nakadhalika, sasa kumbe huyu jamaa kachukulia kuwa ni ukweli, mambo gani haya sasa…’akasema Dalali.

‘Sikiliza,…kama likitokea baya jingine wewe ndiye utawajibika, hili sasa naliweka mikononi mwa afande hapa, kama unataka nithibitishe kuwa wewe unahusika na haya subiria maswali yangu, kama..unakimbia ina maana wewe kweli ndiye unahusika..’nikasema.

Dalali, akawa bado kasimama, na mara simu yake ikaingia ujumbe akausoma, ..akatabasamu, ..akasema.

‘Sawa..si unataka tupambane mimi na wewe, sawa mimi nitakaa, niuliza hayo maswali yako, na uthibitishe hiyo kauli yako…kwa ushahidi, la sivyo, mimi na wewe tutapalekana kubaya, sasa hivi sitanii tena…’akakaa sasa kakunja uso.

NB:Kwa leo inatosha, siku mbili sijatuma muendelezo tulikuwa na msiba, mama yetu mdogo katungulia mbele ya haki. Twamuomba mola amsamehe madhambi yake na ampe mkazi  mema peponi Aamin.

WAZO LA LEO: Mara nyingi watu huona kusema uwongo ni jambo rahisi tu, halina madhara…,lakini tunasahau madhara hayo yanayompata huyo tuliyemsema uwongo, je tutawezaje kumlipa huyo mtu…ni rahis tu, kutamka, lakini twajua ni ni mzigo gani tunaoubeba wa dhambi hiyo, tutakuja kujiteteaje mbele ya mola wetu.
    Tukumbuke jambo moja…za mwizi huwa ni arubaini, unapodanganya huna tofauti na kuiba, umeiba uaminifu aliokupa huyo mwenzako, na uwongo mara nyingini mbio fupi, na  mbio zake huishia ukingoni.


Ni mimi: emu-three

No comments :