Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, June 18, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-12‘Huna haja ya kurudia swali lako, ….ila nikueleze jambo moja unielewe, sisi sote hakuna mtu aliyejua kuwa hilo deni lipo…tumekuja kulifahamu hilo deni, eeh… baada ya kupata barua kutoka benki, ya kutuarifu kuwa kuna deni kama hilo,…unasikia sana…’akatulia na mimi nikawa kimia tu kumsikiliza.

‘Ilikuwa ni mshtuko kwetu, kwa jinsi tunavyomfahamu marehemu…’akageuka kumuangalia shemeji yake.

‘Basi… kwa haraka mimi nilikwenda huko huko benki, kuwauliza, kwasababu muda huo shemeji alikuwa hajitambui, ilibidi mimi niwajibike kwanza,..na nilijiuliza ni kwanini taarifa hiyo haikuja mapema, wakati mimi niliwahi kupeleka barua ya mirathi, kuwa mimi ndiye ninayestahiki kusimamia mambo ya benki,…hawakuniambia kuhusu hilo deni,…wao wanakuja kusema kipindi ambacho tunajua hakuna deni...ilitakiwa katika madeni ya marehemu hilo liwepo, hii ni kuonyesha , au huo ni ushahidi wetu kuwa hakuna aliyekuwa akilitambua hilo deni..hata mahakama wanalitambua hilo,…’akatulia.

‘Wao wakalisemaje..ulipokwenda kuwatembelea…?’ nikauliza

‘Kuwatembelea…!! Hiyo sio lugha sahihi…anyway…wao walisema,… wao eeh, walikuwa katika utaratibu wao wa kuhakiki madeni,..madeni yapo mengi, na kipindi hicho walikuwa na matatizo ya kiofiosi,..wanajua wenyewe ni matatizo gani, hawakutaka kuniambia, ..na wanasema walipofikia kwenye deni hilo,..ndio wakaligundua, na..ilishawangaza ni kwanini deni kubwa hivyo bado liliendelea kuwepo, unasikia ..’akatulia

‘Hata hivyo, wao walikuwa hawana wasiwasi na hilo deni, kwa vile lina dhamana yenye mshiko…unaona, ni kama walitutega..ili tushindwe wafanye hicho wanachotaka kukifanya..hizo sasa ni hisia zangu..,nikahangaika nao, nilionyeshwa kila kitu…mimi ni mbishi hasa kwenye deni, na liwe la mashaka mashaka, lakini kwao nilisalimu amri,…na nilichoka pale waliposema  kuwa wao wan utaratibu wa kutuma makumbusho(remeinder), kila mwezi…’akatulia

‘Uone,…ilivyo, mimi sikukubali kirahisi kihivyo…wao walikuwa wakiandika barua kwa mdaiwa, kumkumbushia, na bro…eeh I mean marehem…eeh, alikuwa akiandikiwa, sasa…kwanini akawa msiri kiasi hicho, sielewi kabisa, mungu amsamehe tu kaka yangu, hakuwa hivyo…siwezi kuamini, …’akasema

‘Hizo barua zilikuwa zinapitia wapi..?’ nikauliza

‘Posta,…zilikuwa zinapitia posta ,tatizo bro,… alishaachana na …kutumia hilo boksi…siku nyingi tu, kumbe kule kwenye mkopo aliweka hilo boksi la posta,..na wao wakawa wanatuma hizo barua zao za kukumbushia huko… huko, hakuna aliyewahi kwenda huko, ni la nini tena wakati tunafahamu kuwa limesha-fungwa..huwezi hata kufungua tena…’akasema.

‘Kimahakama, hawakuhitaji huo ushahidi…maana ni muhimu kulithibitisha hilo…?’ nikamuuliza

‘Mhh….baada ya ushahid wa kumbukumbu za benk,…kuonyesha hizo nakala za barua,… maana wao walikuwa na nakal zao, na tarehe…zipo walionyesha, haikuwa na haja ya kufuatilia huko posta, maana boksi lenyewe tulishafungiwa, nani angelifungua, ni kujishitaki tena, na huko nako kuna deni,..lakini sio kubwa,..akili zimemezwa na hili..,…’akasema

‘Kwahiyo yote hayo uliyafuatilia wewe mwenyewe kuhakiki,..kuwa ni kweli, kuwa kulitumwa hizo barua, na…nilikuuliza awali, wewe kutoka moyoni, ulijirizisha kuwa kweli hilo deni lilikuwa la kaka yako, maana ulifuatilia wewe mwenyewe awali, au sio, lakini je nafsini mwako uliijirizisha, na ukaamini kuwa kweli  hilo deni ni la kweli, na ni la kaka yako..?’ nikamuuliza

Kwanza akaguna mgono wa kama kucheka, akatikisa kichwa, halafu akamgeukia shemeji yake…

‘Hivi shemeji, hujamuambia ukweli wote huyu mtu…pamoja na huu ninaomuambia wa ushahidi, mimi hapo ningelifanya nini, eeh, maana haya maswali sasa yananikera…shemeji hebu nisaidie.. hivi bado hata wewe hujaamini kuwa deni hilo ni la kaka…hivi, si tulishaongea haya na kuyamaliza, kwanini tena….mimi nitasema nini hapo, kuwa ..sio kweli, eeh, kwa vipi jamani, mbona mnaniweka kwenye wakati mgumu, haya ..na haya ya mizimu …hamuamini, wamejuaje…eeeh,..?’  alipomgeukia shemeji yake mimi sikujali, nikaendelea na maswali;

‘Kaka yako alikuwa akikushirikisha kwenye mambo yake karibu yote au sio…ikiwemo kwenda benki kumchukulia pesa,…siku nyingine, nyingine, au sio… au hata kutuma kuweka pesa kwenye hiyo akaunti yake…, ni kweli si kweli…?’ nikamuliza,hapo kwanza akasita baadae akasema.

‘Ndio,..kiukweli kaka aliniamini sana, nilikuwa mtu wake wa karibu sana,  lakini mimi nashangaa, ni kwanini kwa hilo, hakuweza kuniamini, akanificha…’akasema.

‘Na hujawahi kutumwa kuchukua statement ya kumbukumbu za account yake..?’ akaulizwa

‘Hapana, hilo hakuwahi kuniagiza,……bro yeye ..eeh, alikuwa akinituma kuchukua au kuweka tu….na kuchukua, anajaza mwenyewe kila kitu, ila kuweka,…wakati mwingine najaza mimi mwenyewe…’akasema.

‘Kwenye mali zake, akinuanua vitu kama mashamba, nk..wewe ulikuwa mtu wake wa karibu, na kama sikosei, aliwaweka mbele nyie ndugu zake kwenye hivyo vitu vikubwa zaidi ya mkewe, ni kweli si kweli…?’ nikamuuliza. Hapo akasita halafu akamgeukia shemeji yake, na kumuuliza.

‘Eti shemeji hilo ni kweli, umelalamika nini…mmh…, kwa….ka-ka..yako kuwa kaka, hakukujali …au ?’ akauliza na mimi nikamuwahi.

‘Nijibu hilo swali wewe…, nataka nisikie kauli yako, kutoka kinywani mwako wewe…?’ nikauliza.

‘Sikiliza, usitake kutogombanisha, ..kama shemeji alilalamika hivyo, kafanya makosa, kaka hakuwa hivyo, kaka alikuwa muwazi kwa kila mtu…hakupenda mambo ya siri, kila jambo aliliweka kwa mizani yake…’akasema na kutulia kidogo.

‘Ndio kuna maswala ya kiume, alijua hili halina umuhimu kwa wanawake, aliweza kulipeleka hivyo hivyo, ila kwa busara zake, shemeji anafahamu hilo…labda kwa hivyo, wanawake wanaweza kulalamika kuwa wanaonewa,…ni hivyo shemeji eeh…?, ..lakini kwa kaka alikuwa makini sana, mtu akimlaumu kwa hilo anakosea, hakuwa mchoyo, labda kwa ….’hapo akashtuka,…na akatulia halafu akasema.

‘Labda kwa hilo la deni…..’akamalizia hilo baada ya kutulia kidogo

‘Ndio maana mimi nina mashaka na hilo deni, kama hata wewe uliyekuwa karibu yake, si wewe ulikuwa karibu yake kwa kila jambo, ikiwemo hilo la benki, na wewe hujui kitu…kama kaka yako alikuwa hivyo, unavyosema, ..kuwa hakuwa mchoyo, alikuwa muwazi ,…sizani angeliweza kuchukua deni kubwa hivyo, bila ya kuwashirikisha nyie ndugu zake, bila ya kumshiriksiha mkewe, bila hata kuacha kumbukumbu kwa mkewe…mimi kutoka nafsini mwangu, nahisi hilo deni lina utata…’nikasema

‘Siwezi kukushangaa kwa hilo,..unasikia, ni sahihi yako kufikiria hivyo, hata sisi yakhe...’akasema.

‘Basi kama ni hivyo, tusaidiane kuutafuta ukweli…’nikasema

‘Unajua wewe ni kama unaturudisha nyuma, yote hayo sisi tulifikiria,… yote hayo, yalituumiza kichwa,…unaonaeeh..tukahangaika weeh…na hadi …ilipofika benki, tukahangaishana nao, kiasi cha kutoleana maneno makali, kawaulize benki….na tulipofika mahakamani, tukasalimu amri, wao wana vithibitisho…wana ushahidi uliokubalika kisheria…utafanyaje hapo,..?’ akaniuliza

‘Tutafanyaje hapo,tu-ta…’nikasema hivyo kwa msisitizo.

‘Tutafanyaje!!...hahaha, sio mimi tena, labda shemeji..hapana mimi nimechoka…, lakini utafanyaje hapo..ni wewe sasa, sis tulishahangaika vya kutosha…., hebu wewe utuambie labda,  ni wapi tulikosea, tuonyeshe njia,…kama tutaigudua tutakuambia huko hatukupitia,….sawa kwa hivyo tunaweza kushirikiana, sawa..au sio shemeji?’ akamgeukia shemeji yake halafu akasema;

‘Shemeji huyu..unasema ni ndugu yako,…kifupi huyu mtu anachotaka ni kutupozea muda, …kwani huyu mtu ni wakili eeh, kama ni wakili eeh, ni hao wanatafuta pesa tu…huku mtoto aendelee kuteseka, sisi tumeshachoka…au sio shemeji…!?’ halafu akanigeukia mimi alipoona shemeji yake kakaa kimia tu, akasema;

‘Umesikia,….wewe huna uchungu na mtoto maana sio damu yako,..hata kama ni kaka, huna uchungu huo zaidi yetu sis…..sio kama mimi baba yake, au huyu mama yake, eeh,…..tumechoka,…’akasema sasa akihema kwa nguvu

‘Hivi ni nini mali..ni nini nyumba eeh..halafu hilo ni deni, lipo wazi..haya hebu tuambie, una mikakati gani mipya, labda unajua labda mimi nakosea, au sio shemeji, tumuache tuone hija zake au sio…’akaniangalia mimi huku akanikazia macho, mimi nikatulia kwanza sikusema kitu, na ndio akaendelea kuongea

‘Ok…ok….labda mimi nisichukulie hivyo, huenda, ukasaidia,..haya hebu niambie wewe, kwanini una mashaka, na hilo deni, na mimi si naruhusiwa kukuuliza maswali au sio..…maana hata sisi tulikuwa na mashaka hayo hayo…huenda kweli akatusaidia…’akamgeukia shemeji yake

‘Au sio shemeji, ..tumsikilize kwanza, hata mimi nitafurahia…ila muda sasa..sijui haya kama hamjali hilo la muda sawa,….’akasema na kutulia
Alipoona mimi bado nipo kimia, ….akanigeukia, halafu akamgeukia shemeji yake, akionyesha mikono ya kushangaa, na kukata tamaa, halafu akasema;

‘Unaona shemeji ni yale yale..kama ilivyokuwa sisi, kwa mtu anayemfahamu kaka, ni lazima atakuwa na mashaka hayo…, siwezi kushangaa kwa hilo, lakini ili kuyaondoa hayo mashaka, huyu mtu, yeye mwenyewe aende huko benki, akafuatilie, sisi…mimi mwenyewe nilihangaika kufuatilia hilo, nikachemsha, maana hatujui ,  na hata shemeji naye akajaribu akachemsha, ukweli ni kuwa hilo deni lipo, na ushahidi upo, hatuna ujanja nalo…’akatulia kidogo

‘Ushahidi…’nikataka kuongea, yeye akaendelea kuongea

‘Tatizo kaka alichukua mkopo huo bila kumwambia mtu, na matokea yake ndio haya,…unaona, hakuna anayefahamu uhai wake, ilitakiwa angalau amwambia hata mkewe, unaona eeh…sasa hata mkewe alikuwa hafahamu,….. matokea yake ndio hayo…’sasa akawageukia watoto.

‘Unajua isingelikuwa watoto…isingelikuwa mtoto anaumia..mimi nilipanga nipambane nao, hata kwa mwaka mzima,…lakini huruma,…mimi ni baba…yupo mama yake hapa,..kwanini mtoto ateseke..kwanini hiyo hali iende kumgusa mtoto, unaona jinsi ilivyokaa vibaya…mtoto wa watu anateseka kwasababu ya hilo deni, ….sisi tufanyaje kama wazazi…’akawa kama ananiuliza

‘Je tujali mali, au afya ya mtoto, na sio afya tu,…uhai wa mtoto….sisi baada ya kuhangaika kote huko, tuliambiwa baada ya hapo, mmoja baada ya mwingine ataelekea kaburini, …..kaanza mtoto, hatujui…hatuombei mabaya,….na najiuliza yu, ni nini mali, mali ipo, na tutaiacha, kama alivyoiacha marehemu…si alikuwa na mali, sasa hivi yupo wapi, inaniuma sana…’hapoa akaongea kama anataka kulia

‘Kwa-kwa….’akachukua leso na kufuta usoni, halafu akasema….

‘Muhimu ndugu yangu, ni jinsi gani ya kulilipa hilo deni, kama unafahamu namna nyingine sawa, tusaidie kwa hilo tutashukuru sana…sisi kama familia,…hakuna mwenye uwezo huo…’akatulia

‘Mlivyouza mashamba si mngepunguza punguza ili kuonyeshe dalili ya kulipa lipa huku mnafuatilia eeh, mimi nahisi kwa mashamba yote hayo ingelisaidia, au pesa za shamba mligombea wana ndugu…?’ nikauliza

‘Mashamba…hahaha, kumba unajua mengi, shemeji keshakuambia kila kitu, hahaha….unasikia nikuambie kitu…’ kwanza alionyesha mshangao, halafu akaongea huku akijikwangua kichwani. Na mimi nikazidi kutia mafuta;

‘Nyie si mliuza mashamba yake au sio…mkisema ni mali yenu…mali ya familia kuu, sio mali ya marehemu …lakini marehemu alikuwa sehemuu ya familia kuu, je sehemu yake ilikwenda wapi, , au hilo halihusiani na deni…?’ nikauliza hapo, akagwaya, halafu akamgeukia shemeji yake, na kusema;

‘Shemeji, swala la mashamba si tulishalimaliza au sio…hilo halihusiani na familia hii, mashamba yalikuwa mali ya familia yetu, familia kuu, kaka alikabidhiwa kama msimamizi tu…, sasa hayupo,hatuwezi kusema ni mali yake…’akasema

‘Una uhakika na hilo kuwa kaka alikuwa msimamizi tu..sio kwamba yeye alinunua , na kila akinunua anawashirikisha na nyie, si ndio hivyo…?’ nikamuuliza

‘Hilo sitaki kuliongea maana hayo ni maneno ya mitaani, undani wa hayo mashamba naufahamu mimi na familia yetu..haikuhusu, na…kwa hilo, haina haja ya wewe kuniamini au la, maana hayo hayakuhusu kabisa,…’akasema

‘Mimi nimeongea hilo, kuwa kama nyie mngekuwa mkimjali kaka yenu,kama alivyokuwa hai, basi kwenye mauzo ya mashamba hayo, kwasababu yeye alikuwa ni miongoni mwenu au sio.., na alikuwa na sehemu yake..au sio..basi hiyo sehemu yake baada ya familia kugawana, hiiyo sehemu yake ingesaidia kupunguza deni, na nyie kama familia mngechanga kiasi ili kupunguza deni, au……’hapo akanikatisha na kusema

‘Yeye pia alipewa fungu lake,…tena alipendelewa, akapewa sehemu kubwa zaidi, lakini iliyouza hilo shamba, hiyo sehemu yake, ilitumika kwenye matibabu ya shemeji..shemeji ni kweli sii kweli…?’ akamuuliza shemeji yake, na shemeji yake akainua uso kama kutaka kusema mimi nikaingilia kati.

‘Sijakata ushahidi, nataka wewe unijibu…’nikasema

‘Ni lazima hilo tulithibitishe kwa kauli yake ili tusipotezeane muda, ....ndio maana tokea awali nilikuuliza je shemeji hajakuambia ukweli wote, kama alikuelezea maswala ya mashamba, basi angelimalizia na ukweli huo, kuwa mashamba yalikuwa mali ya familia kuu, na yeye , marehemu alipewa fungu lake, na fungu lake lilitumika kumtibia yeye, je kwa kufanya hivyo tulikosea…’akasema kama anauliza

‘Kwahiyo nyinyi kama ndugu zake, …mumesaidiaje kuhusu hilo deni…?’ nikauliza

‘Sisi kama familia, tulisaidia sana, kutegemeana na hali zetu, deni la marehemu ni deni letu sote,..lakini tufanyaje , hali zetu sio nzuri kihivyo,…awali tulichangishana, si unajua tena, ndugu ni ndugu,…tunafahamu sana dhima ya deni, basi, tukashikama mashati, ..kulipatikana nini basi..pesa ndogo tu, ambayo haikusaidia kitu…’akasema na alipoona nataka kuuliza swali jingine kwa haraka akasema

‘Unajua ndugu muda ni mali,…tusipotezeane muda, cha muhimu ..ni jinsi gani ya kulilipa hilo deni, ungetakiwa uje na mikakati hiyo..jinsi-gani-ya-kulilipa-hilo-deni ..vinginevyo, kama walivyoamua wenyewe banki, hatuna ujanja, hatuna jinsi, ..kama unayo wewe , haya endelea, uwanja ni wako, ila…’akasema akimgeukia mtoto, na mimi sikutaka arudie rudie yale maneno ya vitisho, nikauliza kwa haraka.

‘Benki waliamua nini..?’ nikamuuliza kama sielewi kitu

‘Si wewe unafahamu taratibu za beni ukikopa kwao, dhamana ni lazima, au sio…inabidi banki wafuate hivyo, kuwa kwa vile kaka aliweka dhamana ya nyumba, basi, wao wataipiga hiyo nyumba mnada,….walitupatia muda wa kulipa ikaonekana hatuwezi, basi wakatuita, na kutuelezea msimamo wao, kuwa ikipita muda huo wao, hawana jinsi…watapiga nyumba mnada, na pesa itakayopatikana italipa deni, na itakayobakia…wanakabidhiwa warithi..sio haba, kuliko kukosa vyote, mimi nikawaambia sikubali ndio tukaenda mahakamani, kipo wapi…hatukuwa na cha kujitetea, hatuna ushahidi wowote, ilikuwa ni aibu…’akasema

‘Kwahiyo kwa msimamo wako, kwa hekima zako, wewe umeona ni vyema  tuache, nyumba ipigwe mnada, ili lilipwe hilo deni….huoni kuwa tutakuwa hatujawatendea haki hawa wanafamilia, mama na watoto wake?’ nikauliza

‘Hii ilikuwa nyumba ya marehemu na yeye ana mamlaka ya kufanya apendavyo,..hata kama hayupo hapa duniani,.. au sio…labda nitumie lugha hiyo ili unielewe…kama ilikuwa nyumba yake ndio maana aliweka kama dhamana, kuwa hata akiwa hayupo deni lake litalipwa, au sio…kuna kosa gani hapo…’akasema kwa lugha nzito kidogo

‘Au nimekosema ndugu yangu eeh, niambie …si ilikuwa nyumba yake hii, au shemeji, niambie hii nyumba alijenga nani, eeh, au nadanganya,…eeh,…?’ akawa sasa anaongea kwa lugha ya kama kukasirika, halafu baadae akashusha sauti na kusema

‘Na  maswala ya watoto jamani eeh, na wao wana riziki yao, labda mungu hakupanga hii nyumba iwe riziki yao, na mungu hana lawama, eeh, yeye mwenyewe anafahamu jinsi gani ya kugawa amali,..riziki zake kwa waja wake, na wao, …hizo pesa zitakazobakia watajenga nyumba kutegemeana na uweo…tutasaidiana, nitafanya nini na mimi ni baba yako eeh…’akatulia

‘Wewe unaamini hivyo, kuwa nyumba hii haikuwa riziki ya hawa watoto…?’ nikauliza

‘Sasa nitasemaje hapo… mungu atawajalia hawa watoto watakuja kupata ya kwao, hata mimi sio kuwa napenda iwe hivyo, hiyo ni amri ya benki, kama kuna namna nyingine tusaidiane tu ndugu yangu,…au wewe niambie sisi tufanyaje au tutawezaje kuzipata hizo pesa, maana sio pesa ndogo ya kusema tutakuja kulipa, hatuwezi…?’ akasema

‘Mimi sijakataa ..maana kama imefikia hapo ina maana ulijitahidi kutafuta njia nyingine ukashindwa, hata huko kwa mtaalamu wako unayemuamini,..hata yeye alishindwa ndio akaja na mipango hiyo ya kutishia amani, au sio….’nikasema hivyo kumpandisha jazba, watu kama hawa unatakiwa ujaribu njia zote

Jamaa kwanza  akacheka, na kutikisa kichwa..haalfu akasema, jamaa …anajua ….sivyo kama nilivyotegemea, akasema hivi;

‘Hahaha..hizo ni imani tu, kwenye…deni, hasala benki, huwezi kufanya lolote…hayo unayosema unayasema wewe…mungu akusamahe tu…’akasema hivyo

‘Lakini kwani nadanganya, wapo wanadai kuwa wanaweza kulipoteza deni, kumvuta mpenzi, nk…sasa wewe hukujaribu hilo,..nahisi ulijaribu ukashindwa, …na kama nilivyofahamu hapa, ina maana mkopaji alikopa akiwa na malengo, alikuwa kapanga namna ya kurejesha huo mkopo au sio…na kwa vile hamkuwa na taarifa ya huo mkopo, mtakuwa vile vile hamjui jinsi gani ya kuurejesha  au sio…l?’

‘Ndio…hapo tupo sawa, kabisa, kabisa, hatuna jinsi, hatujui kabisa yeye alipanga nini,…hayo ya kusema ..eti..mtaalamu kafanya hivyo kutishia, sikulipenda hilo…ulitakiwa uniombe radhi..lakini sawa, mdomo ni wako, unaweza kusema upendavyo, ila mimi kama baba, kama mzazi wa hii familia, nitaangalia kile chenye usalama kwao..unanisikia….’akasema akitikisa kichwa kukubali

‘Ndio maana,  mimi ninakuwa na mashaka na huo mkopo, yawezekana huyo kaka yako hakuchukua huo mkopo…kama aliuchukua mkewe angelijua, wewe ungejua, na kungekuwa na mradi…kitu cha kuzalisha, au shughuli kubwa ya huo mkopo, na mkewe angeliweza kulijua hilo, au wewe unafahamu kaka yako alikuwa na mradi gani mkubwa, zaidi ya hiyo shughuli yake, au alikuwa akijenga mahali, au ndio hiyo alinunulia mashamba, hebu tuambie…?’’nikauliza.

‘Hakuna mradi kama mradi aliouacha kaka,…nijuavyo mimi, miradi yake ilikuwa ya kuchukua mizigo anauza, mzigo ukiisha anakwenda kuchukua mwingine ni hivyo tu, na ni biashara ambayo hakuianza karibu, baada ya kuachana na shughuli za ajira,…na akiba akawa anaweka benki…na ni pesa ndogo tu tuliyoikuta benki,… ina maana basi alipoondoka alitoa pesa karibu yote, kwenda kuchukua mzigo, akijua akirudi, atapata fadia kubwa, sasa sijui…maana hatukukuta kitu…kwenye gari lake,…, hakuna pesa wala mizigo….’akasema

‘Hapo sasa ndio naona kweli yeye hajachukua huo mkopo, wewe hulioni hilo…kuna namna, kuna mtu kachukua huo mkopo kwa ujanja-ujanja,..akili yangu haikubali…, yaani mpaka hapo, mimi naanza kupata picha, …..’nikasema

‘Unaanza kupata picha gani, hebu tuambie, maana wewe sasa, …usipoteze muda, kwani wewe ni wakili au una ..unawezaje kuzuia haya ya mahakama….’akasema halafu akacheka kwa dharau,

‘Wewe unasema alichukua pesa iliyokuwa benki karibu yote ili kuchukulia mzigo, huo mkopo mkubwa hivyo ulikuwa ni wa nini,..kwanini kama alichukua mkopo eeh, kwanini akombe tena balance yake ya benki… je alikuwa na account ngapi benk…kama alikuwa na biashara, anauza pesa anaweka benki, na siku hiyo kwa kauli yako, alichukua pesa karibu yote…je ni mzigo gani mkubwa hivyo, wa kununulia pesa hiyo yote, mkopo na ..…hebu fikiria hapo…?’ nikamuuliza hapo akasita kidogo.

‘Huenda alichukua kwa shughuli nyingine, sisi hatuwezi kulifahamu hilo….’akasema kwa kunywea kidogo, nikaona sasa naanza kumweka sawa.

‘Kama ipi…ambayo hata wewe huijui, au mkewe haijui, kuna mtu kachukua na deni hilo ,….’nikasema na yeye akanikatiza kwa kusema

‘Mimi siwezi kujua zaidi, kama ilivyo mkopo wenyewe. Na unaposema labda kuna mtu mwingine alichukua, hebu niambie, huyo mtu mwingine angelichukuaje,…unakuwa kama hujasoma bwana, mkopo uchukuliwe benki na mtu mwingine uwekwe kwa mtu mwingine, kwa vipi…wewe kweli sikuelewi,…nakutilia mashaka na elimu yako….au huwaamini  watu wa benki au….’akasema

‘Nitakuja kukuonyesha elimu yangu ipoje, usijali hilo, ila kwanza nataka uelewe kuwa hata huko benk kunaendeshwa na watu, na watu wote sio sawa, na kuna ushahidi huo, nitakuja kukuonyesha hilo,.na mahakamani pia,… ila kwasasa nakuambia hivi,…nina mashaka kabisa na hilo deni halikuchukuliwa na kaka yako…unasikia, ndio kauli yangu hiyo, jiandaeni kwenda mahakamani….’nikasema kwa kujiamini utafiki kweli nimeshakuwa na ushahdii wa kutosha

‘Hilo sasa ni jipya, …hahaha, twende wapi, yaani sijakuelewa hapo ndugu yangu, hahaha, haya buana, maana unajiamini sana, hata mimi ilikuwa hivyo hivyo…’ akacheka kwa dharau, halafu akasema;

‘Ndio hivyo…’nikasema sasa nikiangalia saa yangu

‘Wewe ni mtu wa ajabu, nyie ndio mnaopenda kuzusha mambo…, hata wapelelezi wa polisi hawakuwahi kusema hivyo,…wewe unasema hakuwahi kuchukua…sawa, hata wao walikuwa na shaka shaka hiyo, je walipata nini…wanaishia kusema eeh, kweli deni lipo, ..lakini tuna shaka nalo, labda sio yeye alichukua, sasa…tuonyesheni huyo mtu mwingine kwa ushahidi,…watasema nini hapo, sasa wewe umevuka mpaka kuwashuku benki, hahaha….’akasema

‘Kwani hao polisi walisema nini, kuhusu hiyo kuwa waonyeshe mtu mwingine kwa ushahidi …?’ nikamuuliza

‘Wao walihisi kuwa mimi nilikuwa najua hilo deni , maana deni lilishathibitishwa kuwa kweli  lipo…ya kuwa kaka  kweli kachukua, wao wakahisi kuwa huenda  mimi nafanya mbinu labda, ili hilo deni lifutwe, wakanibana kwa maswali, vitisho, hata wengine kuanza kunitesa,lakini mkuu wao, akasema no…, huwezi kumtesa mtu hapa..….sasa wewe unakuja na hoja ya kuwahuku benk, wao wana kila kitu eeh,…je wewe hujiulizi tu, hizo hati alizosaini bro, zilikuwaje, kweli hazina sahihi yake, hilo hujalifikiria,..nakufungua macho na akili hapo tu….’akasema

‘Mliziona hati alizosaini, sawa, na sahihi ni yake sawa…si ndio hivyo, ndio kigezo chako kikubwa hapo,..lakini pia watu wanaweza kuwa wajanja kwa hilo, sasa hizo sahihi, na mikataba ndio itakuwa ushahidi wetu ….’nikasema

‘Hahahaha, hivi wewe vipi,… samahani lakini mimi nina mashaka na elimu yako, kama wewe ni wakili, haah, aisee, watu wanaliwa pesa yao bure tu…sijui lakini,…ila shemeji huyu mtu, kama ni wakili eeh, umeliwa….’akasema akimuangalia shemeji yake baadaye akanigeukia na kusema;

‘Hivi  nikuulize swali, eeh, inawezekana vipi isiwe kweli wakati kuna sahihi, ..haya achilia mbali sahihi, na dole gumba je…mimi sikuelewi, ndio maana mimi natilia shaka, utaalamu wako, nisamehe tu ndugu yangu,… ‘akatulia

‘Mimi nina shaka na hata hilo dole gumba, …’nikasema

‘Eti, nini, …jamani, ….huyu mtu vipi,….?’ Akauliza sasa akionyesha uso kwa kutahayari.

‘Mimi nina shaka na sahihi, na hilo dole gumba, mimi nina shaka na hilo deni kwa ujumla, …na lazima tutafute ukweli wa hilo deni,….hilo deni sio sahihi, …sio deni la kaka yako…’nikasema

‘Haya wewe niambie, labda nishuke ni sawa na wewe, haya niambie wewe, toka lini mtu akaweza kutumia sahihi ya mtu mwingine, sahihi umesema mtu anaweza kugushi, haya hilo dole gumba….unawezaje kugushi, nakuuliza wewe…?’ akauliza

‘Ndio hapo, mimi nataka tuifanyia kazi hiyo iliwezekanaje hivyo, watu wakagushi, sahihi na dole gumba, …’nikasema

‘Oooh…kumbe, nilijua tu, wewe wataka kupotezea wengine muda wao,…nakuambia hivi benk wameleta vithibitisho vyao ndio hivyo…, hebu na wewe leta vya kwako, ili tuone kama kweli sio deni halali…’akasema

‘Vitaletwa…’nikasema

‘Kama kweli utalifanikisha hilo, mbona utatusaidia sana…’akasema akimminyia shemeji yake jicho alifikiri mimi sijaona,…

‘Kwa ushirikiano wako, hilo litafanikiwa…’nikasema

‘Kwa vipi, mimi tena….ujue hapa tunapambana na muda, kesho, huenda huo mnada ukafanyika japokuwa nasikia fununu tena, kuwa huenda, umesitishwa, hapo sielewi ni kwanini, mimi mwenyewe…nimeongea na benki wakasema hawana jinsi nyingine, zaidi ya kufanyika kwa huo mnada, na sio hapa tu, kuna wadeni wengi tu watafanyiwa mnada…’akasema

‘Huo mnada hautafanyika…’nikasema kwa kujiamini.

‘Eti nini, hautafanyika, nani kakuambia, wakati kila kitu kipo tayari, unajua mimi sijakuelewa wewe ni mtu gani, kwani wewe ni nani na unataka nini, una ushahidi gani kuwa hilo deni sio la kaka,  na …na sasa unaongea kwa kujiamini kuwa huo mnada hautafanyika, unakaidi amri ya mahakama,…bwana wewe usitupotezee muda, au kama una ushahidi utoe, eeh, unao huo ushahidi….?’ Akauliza

‘Kwanza tunachotaka kujua ni ukweli wa hilo deni, hilo deni ni halali,…ok, kwa kumbukumbu za kibenki hilo deni lipo, lawezekana likawa nihalali,..lakini hebu kwanza kabla hatujafikia huko kwenye vidhibiti vyenyewe, tuchangamshe vichwa vyetu kwanza,.. tuanze kulipekenyua hilo deni, je hilo deni lilianzia wapi, lini…?’ nikauliza

‘Kawaulize watu wa  benki….’akasema hivyo

‘Ni nani wa kuwauliza watu wa benki, …ni mimi au ni wewe…?’ nikauliza

‘Ni wewe mwenye shaka na hilo deni….’akasema
‘Ni wewe uliyepewa hiyo dhamana, au unaikana hiyo dhamana, ukweli halisi unatakiwa uanzie kwako, kabla hatujafika huko benki, kwasababu wewe ndiye uliyepewa hiyo dhamana…unakumbuka mimi nilikuuliza awali je ulijirizisha kuwa kweli hilo deni ni la kaka yako ulisemaje..?’ nikamuuliza

‘Lakini sikukuambia kuwa alichukua lini, tarehe gani, hayo mimi sikuwa na shaka nayo, kwasababu tarehe hazina maana, kama mkataba upo, na …” akatulia

‘Unaona eeh, ina maana kiukweli hukujiridhisha vya kutosha,…. kwahiyo ili kusaidia hilo, ili tujue huo ukweli, na undani wa hilo deni,..lini, lilianzaje, mtu wa kuweza kutusaidia ni wewe….’nikasema

‘Kwa vipi…?’ akauliza

‘Ehee…utasaidiaje, ni kwa wewe kunijibia maswali yangu muhimu sana, ambayo, yatakuwa ushahidi mahakamani….’nikasema

‘Mahakamani, unarudia tena….mahakamani…?’ akauliza sasa akikunja uso, na kutupa jicho kwa shemeji halafu kwa mtoto.


‘Shemeji huyu ni ndugu yako kweli, ni nani huyu, huyu anataka kuleta matatizo mengine kabisa, unamuona lakini ni kama ananitupia lawama mimi,…mimi sitakuwa kuja kulaumiwa tena, kwa hayo yatakayotokea kwa mtoto wa-ko…’akasema akimuangalia shemeji yake akiwa katoa macho, kama kutishia vile.

‘Sikiliza mimi nina uhakika wewe ukinijibu maswali yangu ya msingi, tutakwenda sawa, na maswali hayo na majibu yake yawe katika maandishi ili yaje kuwa ushahidi, na kwa hayo hatutapotezi muda kabisa, maana ni kwa ajili ya masilahi yenu, au sio, ni kwa ajili ya haki ya hawa waliochwa ukiwa, mama mjane na watoto..ni kwa ajili ya kupambana na dhuluma kwa hiyo aliyetaka kutenda dhuluma, na kamwe dhuluma haidumu…au sio muheshimiwa..?’ nikamuuliza

‘Kwahiyo unataka kusema nini…?’ akauliza, na mimi nikatoa karatasi , kujifanya nataka kuandika, lakini kwa jicho jingine nikawa naangalia ile simu kama bado inachukua hayo mazungumzo, niliona kama imezimika hivi,

‘Nataka nianze kukuuliza maswali, na iwekwe kwenye rejea, maana majibu yake yatatusaidia huko mahakamani…’nikasema

‘Kwanini Mahakamani, mahakamani,..mahakamani, huko tumeshafika sana,…sikiliza unataka kuniuliza maswali gani, wewe uliza..’akasema kwa hasira

‘Ila nakuasa kitu kimoja, …haya unayotaka kuyafanya wewe sasa ndiwe utakuwa na dhamana ya huyo mtoto,…mimi sitaki tena hiyo hali  imrudie huyo mtoto, na ikirudie unajua hatari yake, eeh, mama yake huyu hapa analifahamu hilo,mimi sina uwezo wa kufanya lolote, ndivyo mtaalamu alivyosema, hata angelikuwa nani, hawezi kumsaidia tena huyo mtoto, kwahiyo sisi..tutampoteza mtoto kwa uzembe wenu, mimi sipo ….’ Akageuka kumuangalia shemeji yake

Shemeji yake akawa kimia, kainamisha kichwa chini..

NB: Ni nini kitaendelea hapo, ni maswali gani hayo, na je hayo maswali yatasaidia nini wakati benki wameshathibitisha kuwa sahihi na dole gumba ni za marehemu…je na hivyo vitisho vya shemeji ni kweli..mtoto anaumia kweli!


WAZO LA LEO: Tusiangalia sana masilahi kuliko haki na ukweli, wengi wetu wanapopewa madaraka wanaegemea sana kumrizisha bosi …au kufanya kwa ajili masilahi, bila kujali taaluma aliyoajiriwa nayo hata kama ukweli upo wazi, na matokea yake anawaumiza hata wale wasiostahiki, tukumbuke, madaraka ni dhamani, utakuja kuulizwa jinsi gani ulivyoyatumia hayo madaraka yako.
Ni mimi: emu-three

No comments :