Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, June 12, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-10


Mlango ulifunguliwa,…!

‘Aheri  umefika shemeji …’ akasema mama mjane.

Akili yangu ilikuwa kwa mtoto, lakini niliposikia kauli hiyo,…’shemeji..’ kwa haraka akili yangu ikahamia kutaka kumuona huyo mtu….

Tuendelee na kisa chetu

                                                                    *********

  Akaingia jamaa mmoja akiwa kavalia, kinamna yake, suti kali na briefcase mkononi, na mawani ya jua usoni,…anatembea kama muheshimiwa fulani hivi….au  kama ofisa fulani katokea safari ni  Ulaya, ….;

Hakujali jinsi tulivyo kuwa, akatembea taratibu hadi kwenye meza akawa briefcase yake, na taratibu akavua mawani yake, na kutoa leso, akayafuta, halafu akapanidhs mikono kuelegeza tai, ..halafu taratibu akageuka kutuangalia…hakusema neno, aliyeongea ni mama mjane…

‘Oh  karibu, nimeshindwa hata kukupokea,…maana kili zimetingwa na hali ya mtoto, na nilipokuona nikashukuru mungu….’huyo mama akasema akionyesha matumaini.
Sasa shemeji mtu ndio akageuka upande ule nilipokuwa, bado nimesimama na mtoto,…japokuwa akili ilishahamia kwa huyu jamaa, lakini akili nyingine kwa kiasi kikubwa ipo kwa mtoto…naona tunachelewa…

Kwanza nilishangaa, muda mchache nyuma, mama mjane alishaanza kunilaumu, kuwa ni mimi nimesababisha yote haya, nilitegemea kabisa asingelipoteza muda, tuwahi hospitalin, lakini sasa kamuona huyo jamaa ambaye kwa kauli yake ni shemeji yake,..amekuwa kama hajali tena safari hiyo ya hopitalini.

Yule jamaa kwanza aliniangalia..ile ya dharau …, halafu akaweka mawani yake vizuri kuining’iniza kwenye mfuko wa suti yake,…taratibu akasogea hadi pale nilipokuwa nimesimama,

Akawa anaendelea kuniangalia mimi,..ni kama vile anakuja kwangu, sio kwa mtoto…na aliponifikia, akanyosha mkono wake, ni kama anataka kunisalimia, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nimembeba mtoto nisingeliweza kuinua mkono..

Bado huku akiniangalia, akanyosha mkono wake, na kushika shavu la mtoto kupima joto….alivyokuwa akifanya utafikiri docta, akatikisa kichwa kama kukubali kitu,..sasa akawa anamuangalia mtoto, akafunua sehemu ya migii yake, akawa anaipima joto, na kwa haraka kamuachia kwa haraka, …akaguna tu kusema

`Oooh,…’ haraka akageuka kumuangalia shemeji yake, na kuuliza

‘Imepita muda gani…?’ akauliza

‘Hata robo saa haijapita…’akasema shemeji yake.

Akashikanisha viganja vya mikono baada ya kuvipuliza, halafu akaviwekea viganja vyake kichwani kwa huyo mtoto,  akawa awewesa maneno, sikuweza kuyasikia vyema, mdomo ulikuwa ukicheza cheza tu, alifanya hivyo kwa muda, mtoto kimia, akamwangalia mama yake, akatikisa kichwa, akasema;

‘Shsmeji mumefanya nini tena, umesahau maagizo uliyopewa, mbona hamna huruma na huyu mtoto,..ni nini lengo lenu, kumuua huyu mtoto…’akasema na mama mjane akanitupia jicho, hakusema neno, na shemeji mtu akaendelea kuongea

‘Unakumbuka  kipindi kile,…alizidiwa sana zaidi ya hivi, eeh,…aah, mimi sijui nyie watu mpoke, haya basi tusipoze muda zaidi…nipe ile dawa ya unga…..’akamwambia shemeji yake.
 Shemeji mtu akawa kama anasita kidogo, lakini baadae kwa haraka, akageuka na kuelekea kwenye vyumba, ..na kuingia kwenye chumba kimojawapo,  na wakati anaondoka, huku nyuma  simu yangu ikawa inaiita lakini sikutaka hata kuipokea, ….

‘Pokea simu yako….’akaniambia huyu mjamaa. Huyu jamaa anavyoigiza, sijui umweke fungu gani, maan alisema hivyo akageuka kuangalia dirishani. Mimi nikamweka mtoto vizuri, na kuipokea simu, ujue muda wote huo nimembeba mtoto.

Nikatoa simu kutoka mfukoni,  na kuiminya kitufe cha kupokelea,..
Walikuwa ni watu wangu niliwaomba taarifa mbali mbali, zinazomuhusu huyo  mama, nikawa nasikiliza kwa muda, …nilichosikia kilinifanya nianze kuwa na mashaka …nikawa najiiba kumtupia jamaa jicho, hakuwa na wasiwasi na mimi alikuwa kanipa mgongo.

Mara akageuka …akawa sasa anamuangalia mtoto, akawa anachezesha chezesha viganja vyake vya mkono, akivisugua sugua  na badaye kuvipuliza, akawa anafanya hivyo kwa muda, ni kama mikono yake inasikia baridi sasa anaipasha moto…nilimuangalia mtoto, yupo kimia…

Kwa muda nilikuwa bado naendelea kusikiliza maelezo ya vijana wangu mmoja baada ya mwingine, halafu nikasema;

‘Nyie endeleeni…tutaongea baadaye,…nipo site…’nikasema na kukata  simu,

‘Site….’ Jamaa akasema hivyo, akitikisa kichwa huku akitabasamu ile ya dharau, mimi nikamweka mtoto vizuri, sasa nikisogea kwenye sofa na kukaa,…niliona hakuna cha kufanya, ngoja nisubirie wanachotaka kukifanya.

Nilitaka kuurudidhs ile simu mfukoni , lakini nikakumbuka kitu, … sasa akili ilishaanza kufanya kazi, nikajua sasa nipo kwenye mapambano, sitakiwi kupoteza kitu,  nikaiminya simu sehemu ya kurekodia matukio, bila jamaa kufahamu, nikaiweka ile simu kwenye meza.

‘Site..hizi simu jamani, unaambia upo site, kumbe…hahaha..’akasema na kucheka, na mimi hapo hapo nikasema;

‘Hizi simu kwa sasa naziona hazina maana,..sitaki kuzipokea tena, unajua mimi hapa nimechanganyikiwa kuhusu huyu mtoto, mimi nawashangaa, hamtaki tumpeleke hospitalini….’nikasema huku nikiiweka ile simu pale mezani.

Akawa anaangalia ninachokifanya, akasema;

‘Hiyo simu ya bei mbaya, unaweka hapo mezani, …unaweza ukasaishau, na watu leo wanaingia humu ndani na kutoka…’akasema huyo jamaa akiitizama pale nilipoiweka ile simu

‘Ni za kawaida tu…sitaweza kuisahau…nikisahau wewe si utanikumbusha au..’nikasema kama nauliza

Mara shemeji akaja na karatasi imekunjwa, kuonyesha kuwa dawa imekwisha,…

‘Shemu mbona umechelewa hivyo,…muda, unajua kwa jinsi unavyochelewesha, damu inaganda..unaelewa hivyo, tokea miguuni, mtoto anaweza kupooza,….dawa ..mbona karatasi tupo, dawa ipo wapi…?’ akauliza.

‘Imekwisha, …nilijua imebakia kidogo, kumbe hakuna kabisa…’akasema mama mjane.

‘Shemeji, shemeji, ….nilikuambiaje,…hii iwe kama kinga yako, ikitokea tu, unaitumia, kama nilivyokuelekeza,…sasa imeishaje, kwani alishawahi kuumwa tena na tena..au imemwagika,  shemeji hiyo dawa ni aghali sana…?’ akawa anaongea kwa kituo, haionyeshi kukasiri, japokuwa maneno yake ni kama kulalamika

‘Imetokea mara kadha ..nikawa naitumia…wala haijamwagika..’akasema mama mjane.

‘Mhh..hata sijui kama nina akiba, ngoja nione…’akasema akifungua ile briefcase yake, akatoa kichupa, na akakitikisa,…

‘Bahati nzuri, iiipoh, ngoja tuone,…, asante mungu…ipo…ok, sasa eeh….’akasema , huku akimimina unga kwenye karasi, kiasi tu, ..halafu akamkabidhi shemeji yake..halafu akajiwekea kidogo, kwenye kiganja cha mkono,…akawa kama anaisomea maneno kwa kuwewesa, halafu, kwa kutumia  vidole viwili, akachota , na kuweka puani mwa huyo mtoto, na mara huyo mtoto akapiga chafya, mara tatu…..

‘Tayari,…mmh, naona  keshaondoka huyo….’akasema  sasa akitikisa kichwa kukubaliana na hilo tendo.

‘Nani…?’ nikajikuta nimeuliza hivyo,na huyo jamaa akageuka kwa haraka akanitupi jicho mara moja, halafu akageuza kichwa na kuendelea kumuangalia mtoto kwa sekunde kadhaa,  baadae akasema;

‘Huwezi kuelewa haya…anajua shemeji, ….’akasema

Baadaye akawa anasema maneno fulani huwezi kuyasikia vyema,…., akampaka Yule mtoto usoni ile dawa, halafu taratibu bila wasi wasi akasogea hadi kwenye sofa,  akakaa, na kukunja nne, yaani utafikiri docta anayejua anachokifanya,  inaonekana huyu jamaa ana majigambo fulani hivi.

Mimi nilikuwa bado nimempakata huyo mtoto, na Yule mtoto sasa akaanza kujitikisa na baadaye akawa anajiinua kutaka kusimama, lakini akawa bado hana nguvu, nikamsaidia kuinuka, akasimama…hapo nikapumua, eehuuuuh, …..

Mtoto akasimama akitaka kuinua mguu,  akawa anayumbayumba, mimi kwa haraka  nikajiinua kidogo ili kuweza kumshikilia, asidondoke…

‘Haina haja,..yupo safi, wala usiwe na wasiwasi…’jamaa akasema pale nilipojitahidi kumshikilia huyo mtoto…Kiukweli mimi  bado nilikuwa sina imani, moyoni nataka tumpeleke huyo mtoto hospitalini. Nikasema;

‘Jamani huyu mtoto tumpeleke hospitalini…hii hali sio ya kukaa nyumbani..muoneni alivyo mdhaifu…’nikasema

‘Haina haja,…yupo safi, nimeshakuambia, hayo eeh,..ni …mambo ya kimila basi…hata ukimpeleka hospitalini, haitasaidia kitu, muulize mama yake…’akasema huyo jamaa, sasa nikainua uso na kumuangalia vyema huyo jamaa usoni, nahisi niliwahi kumuona mahali,…sikumbuki wapi, hata hivyo,kwa muda ule akili yangu ilikuwa bado kwa mtoto..

Nikageuka kumuangalia mtoto, sasa aliweza kutembea hatua kadhaa, akipiga miayo! Nikaona bado niendelee kusisitiza mambo ya hospitalini..

‘Huyu mtoto kwa hali hiyo inabidi tumpeleke kwa docta bingwa wa watoto, msiseme tu haina haja, mlishawahi kumpeleka huyu mtoto  kwa docta bingwa wa watoto, …kama tatizo kama hili huwa linajirudiarudia ujue kuna kitu anatakiwa kuchunguzwa, kwenye kichwa, msikimbilie mambo ya kimila, mlifanya hivyo….?.’nikauliza.

‘Hayo sio maradhi ya kupelekwa hospitalini, hata hivyo,…ni kweli mtu akiumwa, hasa mtoto inatakiwa kufanya hivyo, na sisi mwanzoni tulifanya hivyo, au sio shemeji….’akasema akimgeukia shemeji yake, na sheemji yake hakujibu kitu, yeye akaendelea kuongea

‘Na kwa vile tulikuwa hatujui kuwa tatizo ni nini,…tukahangaika hivyo unavyosema..lakini haikusaidia kitu..na huko kwa  docta bingwa, tena bingwa hasa wa watoto…yule anaitwa nani vile shemu….hebu mwambia huyu mtu…’akasema akimuangalia shemeji yake

‘Yeye huyo docta akasemaje…?’ mimi nikamkatiza na kumuuliza hilo swali

‘Hana tatizo, vipimo vyote hakuna tatizo, …unajua inashangaza sana, unamuona alivyo kuwa na hiyo hali, ukimchukua mkafika hospitalini, atazindukana, pengine hata kabla hujafika kwa docta, na…hapo hapo atachangamka, kwa furaha, akacheza na wenzake,…, wakati tulimchukua hajiwezi…kama hivyo ulivyomuona…hata docta ukimuambia anaumwa, inakuwa kama haamini…’akasema  mama mjane

Yule jamaa akawa anatikisa kichwa kukubaliana na hayo aliyoongea shemeji yake, halafu akanionyeshea mikono, kama kusema, umesikia, baadae kukawa na ukimia, mimi bado nikimuangalia yule mtoto, na mara jamaa akasema;

‘Ehe niambieni…kulitokea nini…maana nilishikwa na majukumu…’akasema na tukawa kimia, alipona hivyo akamgeukia shemeji yake na kuuliza;

‘Kuna nin kinachoendelea, maana hii sio bure, umefanya nini tena shemeji….?’ Akamuuliza shemeji yake

‘Kwahiyo …unasema ni mambo ya kimila, au…?’ mimi nikadakia kabla shemeji hajaongea neno, huku nikiendelea kumuangalia yule mtoto , kwa muda ule alikuwa akicheza na mwenzake utafikiri sio yule aliyekuwa kazidiwa.

‘Shemeji hebu muambie huyu. Eeeh, sijui ni nani….’akasema sasa akinikagua vyema kwa kuniangalia usoni, na mimi sikumpa mdua huo nikawa nimegeuka kumuangalia mtoto.

 Yule mtoto sasa akawa kachangamka, akamwendea mama yake, na mama yake akamwinua na kumpakata miguuni mwake…., mama alimuangalia mtoto wake kwa macho yenye huzuni, …na mara machozi yakaanza kumtoka huyo mama, pale nilipo nilihisi hasira, sijui ni hasira za nini…nikageuka kumuangalia  huyo jamaa. Alikuwa sasa kashika simu, anachat, au …huku akisema haya maneno;

‘Hawa watu bwana, unaona wananilaumu mimi, kwani imekuwaje, mimi sijui kinachoendelea….walitaka kuja kesho, eti kuna mtu kawazuia,…hata sijui ni nini kinachoendelea…’akawa anaongea peke yake

‘Unajua shemeji, kuna matajiri watatu, wanauhakika wa kulipa pesa nzuri, sasa…yupi ni yupi, tutaangalia dau lao, watashindana, hadi kile kiwango kinachofaa, mwenye kisu kikali ndiye atakula nyama, au sio shemeji….ngoja tuone.’akainua uso na kumwangalia shemeji yake, akamuona shemeji yake machozi yakimtoka,  alipoona hivyo akasimama na kumsogelea shemeji yake, huku akisema;

‘Shemeji lakini si nilikuambia, … usivunje miiko, unaona sasa, unamtesa huyo mtoto bure,…kuna kitu ulitaka kukifanya, kweli si kweli…., ulitaka kufanya nini, au umefanya nini,?’ akamuuliza shemeji yake lakini shemeji akawa anatoa machozi tu.

‘Shemeji, wewe unajua kabisa,…. baba yake huyu mtoto hataki mambo hayo, …si unakumbuka maagizo tuliyopewa…sasa haya ni matokeo yake, kwahiyo ukilia, haisaidii kitu kama hutatimiza hayo uliyoambiwa,….kutokutii hayo maagizo…itaendelea kuwa hivi, na sasa hali hiyo ilipofikia ni kubaya zaidi.’akasema jamaa

‘Samahan kidogo, umesema baba yake hataki, baba yake yupi hataki mambo hayo, baba yake si….., marehemu au ?’ nikauliza na kabla sijajibiwa nikauliza swali jingine…

‘Na hataki mambo gani?’ sasa nikawa nimemkazia macho huyo jamaa na huyo jamaa akaniangalia na kusema;

‘Shemeji anajua,…mhh…haya, samahani kidogo, nikisema hayakuhusu…’akasema akionyesha dalili za kunishangaa, alinitizama kwa muda halafu akageuka kumuangalia shemeji yake.

‘Na mimi nataka kujua pia, maana hii sio hali ya kawaida…mtoto anakuwa hivyo, halafu ….hapana, niambieni tatizo ni nini…’nikasema kama mtu mwenye mamlaka

‘Kwanza wewe ni nani unayetaka kujua mambo ya nyumba hii?’ akaniuliza akigeuka kuniangalia, ilikuwa sauti ya msisitizo kama mwenye nyumba.

‘Mimi pia ni kaka wa  mtoto, …’sasa nikajifanya ni kaka wa mama mjane, ili niweze kuingiza miguu yangu

Akaniangalia kwa uso wa kujiuliza, hakusema neno, na mimi nikaendelea kuongea

‘Kama mjomba wa mtoto, ….nataka kujua kwanini imekuwa hivi, mtoto alikuwa mzima ghafla akaanza kuumwa, na wewe umekuja, umemshika kichwani akapona,….na hutaki tumpele hospitalini,  kuna nini kinachoendelea kwenye hii nyumba,… , hebu dada niambie, maana hili sio jambo la kawaida..’sasa nikajifanya ni kaka, mjomba wa mtoto mwenye mamlaka, wajomba wana mamlaka yao.

‘Ndio hivyo, kama ulivyoona, inaniuma kwa kweli,lakini nitafanya nini, ni hivyo kama ulivyoona akianza kuumwa hapo ni …aah, inakatisha tamaa, sasa mimi sijui, wao wanadai eti kuna mizimu…’akasema

‘Wao akina nani…?’ nikauliza

‘Si hawa baba zake,…sasa mimi sijui kwanini mambo kama hayo yanawafuta watoto wadogo wasio kuwa na hatia…’akasema

‘Ni ajabu…basi ni wachawi…’nikasema hivyo, na jamaa akatabasamu kwa dharau huku akitikisa kichwa, huku mama mjane akiendelea kuongea;

‘Hawa watoto masikini ya mungu wana makosa gani, …wangenifuata mimi basi, si mimi mkosaji, basi iniandame mimi, sasa..sasa…kwanini wananitesea watoto wangu….’akasema huyo mama kwa uchungu.

‘Anayewatesa watoto ni wewe usiyetaka kuelewa shemeji, mimi nilishakuambia hilo, hiyo ni mizimu, huyo ni baba yake, hataki maswala hayo unayoyataka kuyafanya wewe….., nilikuambia kabisa achana nayo, naona kama ulitaka kufanya kitu, unataka kufanya nini wakati kesho hawa watu wanakuja kumalizia tatizo, yeye huko alipo hana raha, yaonekana hivyo, ogopa sana deni, hata ukifa, utasumbuliwa tu…’akasema

‘Deni…?’ nikauliza kama vile sijui kitu

‘Hebu shemeji……hivi nikuulize wewe unaona nyumba hii ina maana sana kwako, kuliko afya ya mtoto, kuliko,..ina maana unataka mwenzako huko alipo aendelee kuteseka, eeh…’akasema akionyeshea kidole kuzungusha hewani, kuonyesha nyumba

‘Bado mimi sijaelewa…’nikasema na jamaa hakujali yeye akaendelea kuongea;

‘Shemeji, hawa watoto wakipata shida watakuja kukulaumu wewe kwa kujali mali zaidi,..muhimu ni afya yao, muhimu ni uhai wao,…hivi huyo mtoto akifa, hatuombei mabaya, lakini kwa jinsi tulivyoambiwa, ukichelewa tu,….ukiendelea kufanya hivyo mara tatu, ikamtokea mara zaidi ya tatu, mtoto utamkosa, sasa utakuwa na furaha gani, hata ukiipata hii nyumba na mtoto keshakufa….hutakuwa na raha yoyote…’akasema huyo jamaa.

‘Samahani  kidogo hapo…, ni nani atamuua huyo mtoto ndio hiyo mizimu, au….mimi nijuavyo mtu akifa anakufa kwa mapenzi ya mungu au sio,…’nikasema na huyo jamaa akanitupia jicho la dharau, halafu akasema;

‘Lakini ….eeh,  wewe mwenyewe  si-umeshuhudia hapa, huyo mtoto alikuwa na hali gani, , ….jinsi mtoto alivyobadilika, si uliona, sasa nikuambie kitu, sisi hayo, tulihangaika nayo, mpaka basi, hebu jiulize, ….je sasa nisingelitoka kwa muda muafaka ingekuwaje, hebu niambie  unafikiri kingetokea nini hapo, walisema ikitokea hivyo, mtoto akaachwa saa moja,…basi…tunakwenda kuzika’akatikisa kicha kusikitika

‘Kweli…..ni nani huyo ana mamlaka ya mungu..!!’ nikasema kwa mshangao

‘Ndio..hivyo..sio mamlaka ya mungu.., akiwa katika hiyo hali, damu imesimama,…akaachwa zaidi ya saa moja akiwa kapoteza fahamu, wewe unafikiri itakuwaje, hata kitaalamu tu,wewe si umesoma kidogo..damu ikiwa haitembei mtu anakuwaje…?’ akaniuliza

‘Sijakuelewa…’nikasema

‘Tatizo labda shule haikupanda..ila hali hiyo ya kupoteza fahamu ni dalili mbaya, mwanzoni alikuwa hapotezi fahamu , ni joto tu kuwa kali, sasa hii,…ya kupoteza fahamu kutokana huyo mtaalamu alivyosema hiyo ni dalili mbaya shemeji …achana na hiyo tamaa, nyumba, nyumba ….nyumba kitu gani mbele ya uhai wa mtoto ,….’akasema akimuonyeshea kidole shemeji yake.

‘Lakini sijafanya kitu shemeji….huyu ….huyu , she-, eeh,… kaka yangu, alikuwa akiniulizie jinsi gani tulivyofuatilia, nikataka kumuonyesha jinsi tulivyohangaika, sasa…..’shemeji akamkatiza kwa kusema.

‘Shemeji hao jamaa hawadanganyiki,..unajidanganya mwenyewe…huyu sijui nani, au yoyote yule hataweza kukusaidia kwa hili, vinginevyo, walipe deni, au sio…’akasema , halafu akanigeukia na kusema.

‘Kwani wewe unasemaje, una…taka nini …?’ akaniuliza na mimi badala ya kumjibu nikauliza swali

‘Jamaa gani hawadanganyiki..?’ nikauliza

‘Mizimu….’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akasema;

‘Unajua ndugu, Sisi  tumemuhangaikia sana  huyu mtoto na ndio tukaambiwa ni baba yake hataki maswala ya kesi, …na baya ni kuwa kaondoka duniani akiwa kaacha deni, hilo deni linamtesa, kwahiyo anataka hilo deni lilipwe kwa gharama yoyote ile,….ili yeye aweze kupumzika huko alipo, kauli ya marehemu ni muhimu sana, maana hatujui huko anapata shida gani….., sasa huyu shemeji yangu sijui haelewi…’akasema

‘Kauli ya marehemu, alitamka lini…sijakuelewa hapo, yeye, keshafariki, au sio, sasa hiyo kauli aliitoa lini, kabla hajafariki au baada ya kufariki..?’ nikauliza na jamaa akanitupia jicho la haraka, ilionyesha kama mshtuko, au …

‘Haijalishi….muhimu ni deni….’akasema

‘Ohooo kwahiyo kumbe, nilikuwa sijaelewa, ….kwahiyo kumbe mtoto alipoanza kuumwa ndio mkaenda kwa mganga,au sio? Si ndio hivyo au? Na huko  mkaambiwa kuwa tatizo lake sio la hospitalini, ni maswala ya kimila, au sio…?’ nikauliza na kujifanya nipo pamoja na yeye

‘Haswa,…..lakini hatukuanzia kwa mganga, hapana…..wewe, usininakili vibaya,…sisi sio watu wa namna hiyo…kwanza tulihangaika na mambo ya hospitalini, kila akipimwa hana tatizo, mtoto anazidi kuteseka, homa haishuki….mtoto anaweweseka, wengine wakasema ni degedege, wengine UTI, naimonia na nini sijui ..lakini kwenye vipimo hakuna kitu kama hicho, akifika hospitalini mzima hajambo,, sasa ana tatizo gani, ni shidaa..’akasema

‘Mlikwenda hospitali gani…?’ nikauliza na hakunijibu akasema

‘Ni kama ulivyoona leo, ….je nikuulize wewe , ulipokuja hapa ulikuta huyu mtoto anaumwa….?’ Akaniuliza

‘Hapana alikuwa mzima kabisa…sikumuona na dalili yoyote ya kuumwa,japokuwa anaonekana mdhaifu tu, hiyo ni dalili kuwa anaumwa umwa, au  sio…..’nikasema

‘Sasa umeona, kuna mambo yakifanyika mambo amabyo yanakwenda kinyume na matakwa, maagizo tuliyopewa, miiko….mtoto huyo huanza kuumwa,…’akawa anachezesha mkono kama anaongea jambo, lakini sasa akawa  hatamki neno kwa sekunde kadhaa, baadaye akasema;

‘Ujue  na sisi awali tulikuwa hatujui hilo….tunahangaika huku na kule, hospitalini ,dawa hizi na zile…wakati  tunafuatilia, maswala ya mkopo, maswala ya deni, kumbe hayo ndio tatizo,hatujui masikini,, twauliza huyu mtoto ana nini, mbona hivi, mtoto anaumwa haponi….homa inageuka sasa kama anapandisha mashetani, mtoto mdogo apandishe mashetani, wapi na wapi, ….tuliona ajabu sana….hospitalini akipimwa, hana ugonjwa,…’akatulia

‘Mara kwa bahati akatokea mzee mmoja, akasema nyie huyu mtoto mpelekeni kwa mtaalamu,…kwa mtaalamu!, ….’akasema akitamka neno hilo la mwisho kwa mshangao.

‘Ndio….tukabakia kuulizana ni nani huyo mtaalamu…. Unajua tena sisi wa siku hizi  mambo ya waganga wapi na wapi….lakini sasa tufanyeje, na mimi ndiye baba yao, nikamwambia shemeji hilo…shemeji naye ndio mambo hayo hayajui kabisa, …nikaona na yeye anasita sita, Mimi nikaona hakuna jinsi, mimi ni baba yake…nikaanza kazi ya kuulizia,maana hao watu wapo wengi, na wengine hawaaminiki…nikampata anayestahiki….’akaonyesha mkono wa kishujaa akiwa kakunja ngumi.

‘Na kwa bahati nzuri kipindi hicho hapa nyumbani kulikuwa na ndugu yake shemeji, yeye alikuwepo hapa kumsaidia dada yake…yeye ni mkubwa kwa shemeji, ana akili za utu uzima akajitolea kwenda na mimi, ….tukaondoka naye…kama angelikuwepo mungemuuliza vyema yeye, ….maana mimi nikisema mtaona labda aah...lakini ujue mimi ni baba yake  mdogo, mimi ni mzazi wa mtoto pia, nina uchungu zaidi….’akatulia

‘Ni sawa nakuelewa, hebu nieleze mlipokwenda huko kwa huyo, umesema nani..….?’nikasema na kuuliza

‘Mtaalamu…’akasema

‘Ndio nani, mtaalamu wa nini, sijakuelewa hapo…?’ nikauliza

‘Wewe wa wapi eeh...au ndio nyie mnajifanya hamuamini hayo mambo,…shemeji mwenyewe alikuwa haamini, sasa kipo wapi, amekuja kuamini, huwezi kuamini haya mambo mpaka yakukute…na hasa kwa mtoto, mzazi lazima utaaumua, labda uwe huna watoto….wewe una watoto…?’akasema na kuuliza mimi sikujibu swali lake, nikamuuliza hivi;

‘Sawa, ulipokwenda huko, ukaambiwaje…?’ nikamuuliza, hapo akasimama, akajinyosha kidogo, na baadae akamuangalia mama mjane, …baadae akaanza kusimulia…

NB: Alisema nini huyu jamaa…ngoja niishie kwanza hapa, kabla hatujaenda huko kwa mtaalamu.


WAZO LA LEO: Utu wema ni pamoja na kujali,…kujali wenzako, kuwajali watoto wa wenzako, sio kuwajali watoto wako tu, kumbuka ukijali watoto wa wenzako na wa kwako pia watajaliwa,..wema  huzaa mema, na kamwe wema hauozi.
Ni mimi: emu-three

No comments :