Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, April 4, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-105


‘Kama ni kweli, mtu umekosea ulitakiwa kukiri kosa na kuomba msamaha jamani au sio…?’ nikawauliza wajumbe wengi wao wakatikisa kichwa kukubaliana na mimi..

Mume wa familia akawa bado kainamisha kichwa chini...

‘Lakini hilo halikuwahi kutokea hadi tunafika hapa, ina maana kazi yetu yot hapa hakiweza kufanikiwa…umeona hata hayo maswali niliyokuwa nikimuuliza yalikuwa ni namna ya kumzindua, lakini yeye, aliona kama ninamkera,…’nikageuka kumuangalia.

Bado alikuwa kainamisha kichwa chini...

‘Sasa..labda ni mimi ndiye niliyekosea, ni mimi ndiye natakiwa kuhangaika, kumuomba msamaha…au wajumbe nimekosea, je ni nani anastahili kumbembeleza mwanzake, kwa hali kama hii,…ni mkosaji au ni yule aliyekosewa...?’nikawa nimeuliza hivyo, lakini sikutaka jibu la mtu nikasema

‘Mimi kwa uoni wangu naona bado kuna tatizo, na huenda hilo ni tatizo sugu...nakiri kusema hivyo,…mungu anisamehe tu…’nikainama kidogo.

'Unamuuliza mtu swali kwanini ulifanya hivyo, makosa kama hayo... anakujibu nilifanya hivyo kama mume wa familia katika kuhakikisha familia yangu inakuwa salama,…na nilifanya hivyo kama kuwajibika,....hivi hayo makosa yalikuwa na muenendo huo….sawa labda...yapo, ...mengine utasingizia kuwa alifanya hivyo  kwa kulazimishwa, labda kwa vile…lakini yaangalie hayo makosa, na muda yaliyofanywa…

‘Sasa kiukweli kwa majibu hayo, ilinifanya nifikirie mara mbili je ni nini mstakabali wa maisha bora ya mume na mke mwema...hivi nifanye nini mimi...unajua ni kazi kubwa sana kuchukua maamuzi hayo magumu!

‘Je…, ni, nini mstakabali wa watoto wangu...watakuwa wakiuliza baba yupo wapi...lakini je wataishije..watajifunza nini,, ili wawe na maisha bora, tabia njema,..ili waje kuiga tabia ya wazazi wao..’hapo nikageuka kumuangalia mume wa familia ambaye kwa muda huo alikuwa bado kainamisha kichwa chini, lakini sasa alikuwa akiniangalia kwa kujiiba.

‘Je maisha mema,…ndio hayo ya kutumia ubabe, uwongo, hadaa, ulevi... na ukikosa hutaki uambiwe umekosa, badili yake unatafuta visingizio...na zaidi hutaki kukiri kosa, …..hapana hatuendi hivyo, mimi sikulelewa hivyo...’nikamwangalia mwenyekiti, na mwenyekiti alikuwa katulia akijifanya anaandika andika.

‘Wazazi wangu nawashukuru sana kwa hekima zenu, kwakweli najisifia kwa kuwa  na wazazi kama nyie, kwani mnafahamu jinsi gani ya kuishi na watu, kwani baada ya haya yote nilitarajia mungelikuwa na hasira na kuniambia kuwa mimi nimejitakia,…’nikatulia tena nikiwaangalia wajumbe.

‘Ni kweli kwa haya nimejitakia, mwenyewe, wema wangu ndio umeniponza…kwani mlishanikanya lakini sikuwasikia..nikajiona nimekuwa, nikajiona naweza kujibea mimi mwenyewe..sasa muda umefikia .., nibebe mzigo wangu mwenyewe, lakini baada ya yote haya mumekuwa mstari wa mbele, mkiniomba haya tuyamalize kwa amani, tusameane....ikibidi turejeane...kama mke na mume...haya nilikubaliana na hayo mawazo yenu, je ..mume yupo tayari kwa hilo…

‘Nimewaelewa sana, na mimi kama binadamu nahitajika kujirudi, kusamehe na kuangalia kuwa kweli kuna kuteleza, kuna kukosea,..na mkijitambua kama wazazi, kama mke na mume kama binadamu mwenye utashi, mnaweza mkayasahihisha makosa yenu mkaendelea mbele..nimelikubali hilo, ...’nikatulia.

Wajumbe wakajikuta wakipiga makofi, sikuelewa wanapiga makosa kwa lipi hasa, lakini sikuwajali kwa muda huo, …mwenyekiti alikuwa akiniangalia tu, mama alikuwa kainamisha kichwa chini…

‘Kabla ya kutoa maamuzi yangu, mimi nimefikiri sana, nikaona kuna haja ya kufanya yafuatayo..’nikasema hivyo na hapo mume wa familia akainua kichwa kuniangalia…Nilitulia kwa muda,…mpaka watu wakafikiria nimeshindwa cha kuongea..

 ‘Kwa vile mume wa familia lengo lake kubwa ni mali, lengo lake kubwa ni kupata utajiri, lengo lake ni kubwa ni kuwa na hali nzuri, basi, mimi kwa ridhaa yangu mimi mwenyewe nimekubali kumuachia kampuni yake, kwa asilimia mia moja…’nikasema hivyo

‘Yeye ...achukue hisa zote, na amilikishiwe moja kwa moja kama kampuni yake binafsi, …. Mimi sitakuwa na hisa tena kwenye kampuni hiyo, ina maana ni mali yake moja kwa moja...hilo mimi nimeliamua kwa moyo wangu wote, kuonyesha mapenzi yangu kwake..na hili wazazi wangu naomba mnisaidie hata kama kuna madeni, myasamehe…’nikasema na kumuangalia mwenyekiti.

Mwenyekiti akatabasamu kidogo, akawaangalia mawakili, lakini hakusema neno.

‘Kwa kufanya hivyo, sasa yeye ni tajiri, kwani ana kampuni ambayo ni yake, ambayo itakuwa haina madeni, na madeni yake anayodaiwa mimi nitajitolea kuyalipa, ina maana madeni ya kampuni hiyo yatahamia kwangu, unataka nini tena wewe mwanaume...’nilimuona mwenyekiti akiniangalia kwa macho makali hapo.

Nakumbuka wazo kama hilo niliwahi kuongea na wazazi wangu wakanipinga sana, kuwa kwa kufanya hivyo namdekeza mume, lakini mimi nikaona ndio njia pekee ya kumsaidia mume w familia, ili afikie malengo yake na huenda akajirudi na kufanya zaidi ya hapo.

‘Mimi nitabakia na kampuni yangu na hisa za mume wangu zitaondolewa kwa vile nimeshamkabidhi kampuni yake awe yeye ndiye mumiliki, na mimi sitajihusisha na kampuni yake tena

‘Ila kama akitaka msaada kwangu,kwa ridhaa yake yake mwenyewe nipo tayari kumsaidia…lakini sasa..

Katika hilo, wapo watu wa karibu yake, watu waliopigana naye bega kwa bega, hao hawezi kuwaacha, lakini hayo ni kwa utashi wake..anaweza kuwauzia wenzake hako hao hisa kama washirika wenza…

‘ni vizuri kufanya hivyo, ili kuonyesha wito wema, nakushauri ufanye hivyo ili kuonyesha ukomavu, na ubinadamu, au sio…watu hao ni aliyekuwa rafiki yangu,... na pia amuuzie, mpenzi wake wa asili baadhi ya hisa, hili ni pendekezo langu ndio maana nikaamua kuyachukua mdeni yote ili muweze kuanza kwa pamoja.

‘Nwaombe mfanya kazi hiyo kwa pamoja na kwa bidii kubwa,..nina imani kuwa mtafanikiwa,…nawafahamu wote kuwa ni wachapakazi…hodari…, hii itawasaidia wote, na ile ndoto yao ya kupata utajiri itakuwa imekamilika,..natumai wakiwa pamoja wataweza kufanikisha hili jambo, na ndio njia mojawapo ya kusaidiana..

‘Mimi nimeona tusaidiane kwa hilo, ili kila mwenye nacho amsaidie na mwenzake, kwani huenda haya yote yasingelitokea kama watu tungelipendana, wale walio nacho japo kuwa kidogo, wawasaidie wale wasio nacho, na kupandishana, katika namna ya kupeana majukumu, sio kupeana tu kama zawadi...ingelikuwa hivyo, nina imani  dunia hii ingelikuwa ya upendo na amani..

 ‘Lakini pamoja na yote hayo, nafahamu kuna watu hawatosheki, nafahamu mtaka nyingi nasaba, anaweza akakosa yote, kama bado mume wa familia hajatosheka na hilo…’ nikatulia kidogo

Mimi nilimuuliza swali kubwa, je yeye anataka nini…hakunielewa nilikuwa na maana gani, nilitaka awe muwazi tu….hakuweza kunijibu, ila mimi nimeona ni kitu gani anakitaka, sasa je hilo hajatisheka nalo…

‘Kama hajatosheka na hili sijui mimi nitamsaidiaje, mimi kwa mtizamoo wangu, kama yeye hatariziki na hilo,  itabidi twende mahakamani,…itapibidi turudi mahakamani ili sasa sheria ichukue mkondo wake,.. ili haki yake ipatikane, anayoitaka yeye,..

Na ikiwa hivyo basi mkataba wetu upo wazi utasimama hayo yote,..mkataba wetu ni ushahidi tosha, mengi tuliyaficha ficha ili kesi ibakia huko kwa wauaji watu, lakini haya yetu tuliona tuje tuyamalize hapa nyumbani..

Sasa kama mume wa familia hajarizika na hilo, basi mimi sitarudi nyuma tena, ...mkataba utafanya kazi yake na yeye hatakuwa na haki ya kupata kitu chochote, sasa ni uamuzi wake...’nikasema na kumwangalia mwenyekiti.

Mwenyekiti akatulia kwa muda halafu akaniuliza, ...’mbona hatujakuelewa, hatujasikia maamuzi yako, au hayo ndio maamuzi yako ya mwisho..., ?’

**********

‘Nilisema kabla sijatoa maamuzi yangu,nilitaka niyaweke hayo wazi, nilitoa hayo kama utangulizi, kabla sijatoa uamuzi wangu, ...nimefikiria sana…

Kwanza…nielewe wazi, moyoni nimeshasamehe yote yaliyotokea, na walionikosea nimeshawasamehe, akiwemo mume wangu, rafiki yangu na wengineo ....kama binadamu yeye anastahili kusamehewa, natumai hatarejea makosa kama hayo tena.

Niliposema hivyo mwenyekiti akatabasamu, mama ndiye aliinua kichwa akaniangalia kwa macho ya mshangao…

‘Kama alivyosema mwenyekiti, kusamehe ni wajibu wangu, ni hilo nimelitimiza, na nilishamwambia mwenzangu kuwa sina kinyongo nayeye tena.., lakini nataka kuyasema haya kama binadamu wa kawaida..

‘Baada ya yote hayo na kuyapima yote kwa makini zaidi, mimi nimegundua mengi, ambayo yatanifanya nitoe maamuzi yangu kama binadamu, natumai mtanielewa, kwa hayo nitakayo yasema....’nikatulia na watu wakaguna, kukawa kimiya.

‘Unajua kuna kitu kimoja nimekiwaza sana…ndoa ni ya mke na mume, ni mafungamano yenye usawa, kila mmoja anawajibika kutegemeana na hali yake..na nafsi ikubaliane na hilo..kama nafasi haitaki huwezi kulamisha, au sio..lakini kama unaweza ukasema nitajitahidi basi, pambana na nafsi yako..mungu atakusaidia,...

 ‘Nilishaongea na mwenzangu na kumtaka asome katiba yetu vyema, ili sije akasema mimi nilikuja kubuni Katiba nyingine, lakini alikataa..hilo.

‘Yeye alikuwa kaninunia tu, na kubakia kuniangalia kwa macho ya hasira na chuki,na alipoanza kuongea alikimbilia kunilaumu mimi na wazazi wangu kuwa ndio tumesababisha haya yote, hadi akawekwa ndani, kwa kosa ambalo hakulifanya, na aliyofanya yeye, alikuwa akiyafanya kwa minajili ya kuilinda familia yake, alijitolea muhanga kwa ajili ya familia…ni sawa, kama mlivyoona  au sio kwa hilo namshukuru sana.

‘Lakini hawezi kututupia sisi lawama mimi na wazazi wangu....jamani hivi ni sisi tuliofanya hivyo, au ni matendo yao mabaya... je kwa hayo aliyoyatenda ni nani angelistahili kumkasirikia mwenzake...hapo mimi sikumuelewa...’nikatikisa kichwa.

‘Ina maana kweli mtu hajajifunza kwa hayo yaliyotokea, kuwa yeye ndiye mkosaji, yeye  ndiye aliyestahili kuomba msamaha, na kunyenyekea kwangu, na kwa hawo walioathirika kutokana na matendo yake machafu.

Hivi kama mzazi, angelifurahia mtoto wake afanyiwe hivyo, au hata hilo la kumbaka mtoto wa kazi ni mbinu za marehemu…, kamuharibia mtoto wa watu mipangilio yake ya maisha...hilo halioni, na lo hilo ni kosa langu.

Haya labda..kama anavyodai labda, mimi sikuweza kumtosheleza…...yote kwake anaona ni kuwa hay a aliyoyatenda kama mume wa familia,..yeye anaona alivyotenda ni sawa tu kama anavyodai kuwa alifanya hayo akijua anawajibika kama mwanaume,labda kwa vile alikuwa akitafuta mtoto wa kiume, lakini kawapata wangapi, mbona alikuwa bado hajatosheka

‘Kwa mtizamo huo ninakuwa na mashaka, ,...msahamaha upo pale pale, nimeshamsamehe…lakini…’nikatulia kidogo

‘Huenda mwenzangu bado haajtosheka, huenda mwenzangu bado anahitaji muda wa kujirusha na kila mwanamke anayempenda, huenda nafsi yake ilikuwa haijatulia, ndio hivyo tena, yeye alinioa tu kwasababu kuna kitu alikitaka,…mali,

Lkini mali haiji hivi hivi, inabidi tufanyie kazi, ndivyo nilivyokuwa nafanya mimi, nilijitahidi kumjenga afahamu hivyo, natumai atayakumbuka maadili yangu kwenye kazi zake.., akiwa kama kiongozi mkuu, atajua kwanini nilikuwa namfanyia hivyo, akiwa sasa hamtegemei mtu atakuja ni kwanini nilikuwa nafanya hivyo....’nikamwangalia na yeye akawa ananiangalia kwa macho ya dharau hivi.

‘Sasa mimi nimeona nimpe kile alichokuwa akikitaka, natumai moyo wake utarizika, na huenda akatulia, ..huenda, akawa mume mwema, na kuweza kujenga familia yake kwa amani na upendo, maana watu wa namna hii hawatosheki bwana, lakini sasa atafanya hivyo akiwa anataka nini tena,...’nikatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Mimi nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kutimiza wajibu wangu,sikuwahi kuvunja masharti makubwa ya ndoa hata siku moja, ina maana mimi nilikuwa mjinga, au sikuwa na vishwawishi vya hapa na pale…ina maana mimi sikuwa na tamaa ya kimwili,..

 Wapo watu walikuwa wananikera, lakini mimi nilifahamu kabisa kuwa ni mwanandoa, na ndoa ina masharti yake, ...nikayatimiza, ina maana mimi nilikuwa sina hisia za kibinadamu kweli, ina maana mimi nimeumbwa kwa jiwe, hapana sio kweli hata mimi kama binadamu hali kaam hiyo ilikuwa ikinishika, lakini niliweza kuitawala nafasi yangu.

‘Kwakweli kila nikiliwazia hilo ninaumia sana, kwa ujumla nimekwazika kupita kiasi, nimezalilika, hasa pale ninapoambiwa sikuweza kutimiza wajibu wangu ndio maana mwenzangu akafanya hayo...

‘Jamani..hamfahamu jinsi gani mwanamke anavyojisikia pale mume wake anapotembea na wanawake wengine wakati yeye ni mke wa ndoa, inaumiza mtu kisaikolojia, unajiuliza mawali mengi, hivi mimi nina kasoro gani, hivi..hivi...unaumia sana, lakini ni nani atalifahamu hilo...’nikasema kwa machungu.

‘Lakini mungu ni mkubwa ukweli mara nyingi una nguvu, ukweli ukadhihiri, ukweli ukajileta, na mambo sasa yapo hadharani, kumbe  hayo waliyapanga hata kabla hawajaingia kwenye ndoa, walichokuwa wanakitafuta ni sababu tu,...na sababu ikapatikana,…tunabakia kumsingizia marehemu…

‘Sawa mimi nakubali nifanyeje sasa…au sio.. ndiooo, kama binadamu hata mimi nilikuwa na madhaifu yangu, kama alivyodai, kuwa mimi mara nyingi sikuwa karibu naye, kutimiza wajibu wangu wa kindoa

Lakini hilo lilikuwa swala la kuongea, mimi ningelimuelewa au sio....hakuniambia, hakulalamika mbele yangu…mume na mke ni kuambizana, kubembelezana, ..ina leta raha zake…, akafanya aliyoyafanya kwa wale wa chapu chapu, wasiohitajia hayo, pesa ikaongea au sio.....lakini hicho ni kisingizio tu, walishayapanga hayo kabla, wakishirikiana na mwalimu wao...wameshajieleza hayo, ushahidi upo…

‘Udhaifu wangu, haukuwa wa kuvunja masharti makubwa ya ndoa, ni yale ya kibinadamu na kwenye mkataba tuliyaanisha hayo, yapo mapungufu ya kibinadamu, yanasameheka,....sio hayo aliyoyafanya yeye, ya kukiuka miiko ya ndoa, na kwenda kuzini nje, hadi kupata watoto, hawo watoto wanadai haki yao, kwanini walizaliwa hivyo, na wengine wanatelekezwa

Haya mnayaona mitaani au sio..haya ni kwasababu ya tamaa ya watu kama hawa wasio na maadili mema, hawa watu tutaishi nao mpaka lini, kwanini kusiwe na njia ya kuwawajibisha, eti jamani mimi hapo nakosea, ni lazima wawaji-...’nikasema na kumwangalia binti wa hiari wa wazee wangu, aliyekuwa mfanyakazi wangu wa ndani, alikuwa bado hajaondoka. Alikuwa analia…

************

‘Na nimesahau jambo moja la muhimu sana, huyu binti wa hiari, nimeamua kuwa nitamuajiri mimi kwenye kampuni yangu, nitaangalia jinsi gani ya kumsaidia,kabla hajapata hiyo ajira.

‘Naamua kuchukua dhima hiyo, kwa vile mimi ndiye niliyekwenda kumchukua kwa wazazi wake, yeye alikuwa katika mikono yangu na yote yalitokea kwenye nyumba yangu, mimi ndiye nabeba dhamana hiyo, mimi mwenyewe nitamsomesha na nina imani baada ya miaka mitatu atakuwa tofauti...namjenga rafiki mwingine mpya

‘Mimi...sitachoka kusaidia watu pale inapowezekana, nina imani baada ya muda huo, hatakuwa huyu binti tena....’nikasema.

‘Baada ya kusema hayo, ... ...,  kama ilivyoanishwa kwenye mkataba wetu wa hiari, na kutokana na ushahidi uliotolewa mimi nimeona ndoa yetu ifikie kikomo na kila mmoja aangalie ustaarabu mwingine, kwani hata bila kauli yangu hiyo ndoa ilishavunjika, au sio jamani…?’ akawa kama anauliza

‘Ndio hivyo hata kidini, kaulizeni mtaambiwa,..maana mkataba tulisaini wenyewe kwa hiari zetu tukiwa na akili timamu,…tukakubaliana mtu akazini…na ushahidi ukapatikana, adhabu yake ni nini… mungu ni shahidi yangu kwani kanisaidia kutoa ushahidi…, ni dhahiri kuwa ndoa haipo tena...

‘Mwenyekiti alisema kama mtu hajatenda hiyo dhambi ajitokeze, haya mimi hapa najitokeza sijawahi kuifanya dhambi,...mungu ni shahidi yangu, na hata kama watu waliniona nikiwa na docta, tulikuwa naye tukiongea tu, mimi na yeye hatukuwahi kuvunja amri hiyo kwenye mkataba wangu,...kwahiyo mimi nimetimiza wajibu wangu,…

Hapo mimi nitasemaje nawaombeni mnisaidia hapo…ni kweli mimi nilimpenda mume wangu lakini je kuna upendo wa sehemu moja….atasema ananipenda, je ni kweli ananipenda, upendo wa kuigiza, hapana asema ukweli wake tu,..na ukweli upi tena,...naombeni sheria ifuate mkondo wake....

 Na naombeni mnielewe, Maamuzi yangu ya kuachana na mume wangu, ni kuonyesha upendo wangu kwake, kuwa mimi najali hisia zake,...kuwa yeye ana mpenzi wake wanayependana naye sana, ..mpenzi wake wa asili…

Najua hata alipo anatamani awe naye, lakini kutokana na nakama za kimaisha, walishindwa, sasa wanazo mali, sasa wao ni matajiri, wanaweza kuishi kwa raha, nafiki ndoto yao sasa imetimia, au sio wenzangu...sasa wana mali, ...kwanini nisiwape nafasi hiyo,sitaweza kuwadhulumu kwa hilo, ndoa yangu na mume wa familia imekwisha, na nashukuru mungu kwa yote hayo, na sio nasema hivyo kuwa nina kinyongo tena, hapana nimeshawasamehe...

‘Ninachokifanya hapa ni kuwa sitaki kuwatendea dhuluma kwa vile walikuwa na hali hii au ile, nimechukua maamuzi haya magumu, kwa vile nampenda sana mume wangu, na nataka arikie na nafasi yake...’nikatulia kidogo.

‘Kama mlivyoona, mimi nilikuwa na mume ndani, nikijua kuwa mwenzangu yupo na mimi kumbe alikuwa akinivunga, na kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa....sasa muda umefika, yeye na mchumba wake wa asili wapo huru, baada ya taratibu zote za kuvunja ndoa yangu, talaka na kila kitu, wao watakua huru kuoana...hakuna kizuizi hapo,...’nikasema na kumwangalia aliyekuwa mke wa docta.

‘Lile swala la kuwa eti kwasasa kajifunza, hatarudia tena, mimi bado linanitia mashaka, na ninaona nisitumie mwanya huo kuwaharibia upendo wao na mpenzi wake wa asili, nilishaongea na mpenzi wake huyo na tumekubaliana mambo fulani fulani, ..

'Kwa ujumla mimi sioni kwanini wasioane, wanahitaji nini tena, sioni kwanini mpenzi wake huyo aende akaanza maisha ya kipeke yake huko kijijini, akae hapa, wafanye kazi, tumeshaliongea hilo na yeye japokuwa hakukubali moja kwa moja, lakini natumai wakikaa na mwenzake, watakubaliana kuhusu hilo..’nikasema na kugeuka kumwangalia mume wa familia halafu aliyekuwa mke wa docta.

 Docta alikuwa kashika shavu utafikiri hayupo kwenye kikao, naona alikuwa akiumia sana moyoni.

‘Sasa kazi ni kwenu wapendwa..ila cha muhimu, nawashauri tena na tena, kazi kwanza, hayo mengine baadaye, ni muhimu sana hilo, muhangaike, ili muweze kuuendeleza huo utajiri kwani haukuja kirahisi hivyo, unahitajika kuwajibika, msilale, fanyeni kazi kwa bidii, nina imani mtafanikiwa, na kama mkihitaji ushauri wangu mimi nipo, tutasaidiana pale mtakaponihitajia, lakini kwa nia ya kutoa ushauri tu.

‘Ama kwa yule aliyeitwa rafiki yangu, mimi sina kazi naye tena , nilichofanya  kwake ni kumsaidia, na kwa vile keshakuwa na anaweza kujichukulia maamuzi yake mwenyewe, basi, ....naona nimuache, kama nilivyoshauri, yeye apewe hisa kwenye hiyo kampuni,wanaweza kujiunga kwa pamoja wakajenga kampuni yao ikawa yenye nguvu.

Mimi nina imani nguvu hizo zikukutana kwa pamoja, kutakuwa na maendeleo makubwa sana..kwasababu nyote mnafahamiana, au sio...yeye sasa ana uwezo huo , hata wa kujiajiri yeye mwenyewe...sina wasiwasi na yeye, ...na nimemwambia kama atahitajia msaada kwangu mlango upo wazi

‘Hayo ndio maamuzi yangu, na sina zaidi naomba mawakili wetu wayaweke hayo sawa, na taratibu zote za kutalikiana zifanyike kwa amani, nataka hili zoezi lifanyike kwa amani ili baadaye tukikutana tukutane kama marafiki, hakuna chuki wala kununiana, au sio jamani…

‘Hayo ndio maamuzi yangu na hakuna kurudi nyuma, nawaomba wazazi wangu walipokee hilo , wakijua kuwa mimi sasa sio mtoto mdogo tena....’nikasema nikiwaangalia mawakili wetu na wazazi wangu, nilimuona mama akipitisha mikon usoni na kujifuta machozi....

‘Na kwa hivyo basi, ili kuweka mambo sawa, na kumhakikishia mume wa familia kuwa mimi sina kinyongo na yeye tema, nawaomba mawakili, wafanye taratibu za kisheria kuziondoa hisa zangu kwa kampuni ya mume wangu na kumumilikisha yeye, ...na pia waziondoe hisa za mume wangu kwenye kampuni yangu, na madeni ya kampuni y amume wangu yahamishiwe kwangu..

Na kwahiyo mimi nitamiliki kampuni yangu peke yangu, na yeye na wasaidizi kama watakubaliana wataangalia ni nani apate kipi ...nafahamu mume wa familia atakuwa na hisa kubwa kama mumiliki, ..wengine watakuwa na hisa zao ndogo ndogo, lakini sitawasaidia kwa hilo, hilo wakubaliane wao wenyewe...

‘Na kwa vile mume wangu ndiye mkosaji, mali nyingine alizozikuta zitabakia kama zilivyokuwa, kama alivyozikuta, ni mali yangu na watoto wangu ...ama kwa nyumba, ile nyumba,…nyumba aliyokuwa akikaa kwa sasa baada ya kutoka kuumwa na kifungoni , ile ni mali ya kampuni yake, basi itakuwa ni mali yake, sina haja nayo, ...’niliposema hivyo, mume wa familia akainua uso na niliona ukikunjuka na zile hasira alizokuwa nazo usoni zikayeyuka..

Akatabasamu…

‘Mnaona wenyewe, ni nini kilichokuwa kikitafutwa, natumai keshakipata, mimi namtakia maisha mema, na hili liwe fundisho kwake, na kwa wenzake,....mwenyekiti mimi naona nimemaliza....’nikasema huku machozi yakinilenga lenga. Mume wa familia alikuwa kavaa miwani, naona ni kwa ajili ya aibu ya hayo yaliyotokea.

*************
Ikawa kuna kuongea, kufurahi kucheka, baadae mwenyekiti akapiga makofi na kusema;

‘Basi  sisi kama wazazi, kama mumeriziana hivyo, natumai tulimalize hivyo,… au mume wa familia una la kuongea, je hujarizika bado?....maana bado wewe ni mume wa familia hadi hapo sheria itakapochukua mkondo wake...au nimekosea?’ akauliza mwenyekiti akiwaangalia mawakili,..

Mume wa familia akawa kimiya kwa muda, lakini baadaye akasema;

‘Sina la kuongea ndugu mwenyekiti…, nitaongea nini wakati maamuzi yameshapita....nimerizika…zaidi sina kwakweli..’akasema hivyo na kukaa kimiya huku akiwa kainamisha kichwa na ile miwani aliyovaa huwezi hata kufahamu anafikiria nini

Leo mume wa familia hakuvaa kama kawaida yake, .. leo alikuwa kava kinyumbani zaidi, kawaida yake kwenye vikao kama hivyo huwa anavalia suti safi..na tai shingni, huwa anajipenda sana…na hupenda kujionyesha kuwa yeye ni bosi fulani hivi, lakini leo,…akafika na t-shirt,…na suruwali ya jeans..alivalia kinyumbani zaidi. Nahisi alitarajia kuwa leo anakosa kila kitu.

‘Lakini ni vyema tukasikia kauli yako kama mume wa familia, hata kama mwenzako ameshaamua hivyo, je umerizika, muhimu ni hapo.. ...upo tayari kuendesha hiyo kampuni mwenyewe. Swala la talaka, mlishaongea wewe nay eye au sio.., na hapa ni kama taarifa tu, ....sasa hebu tuambie na wewe una kauli gani...’akasema mwenyekiti.

Hapo mume wa familia akainua uso na kusema….

‘Labda niongee tu, kwa vile mnataka kusikia kauli yangu..’akasema hivyo.

‘Mimi…, nasema hivi kama binadamu nina mapungufu yangu, hayo yaliyotokea ni kweli niliyafanya, lakini kipindi nayafanya nilijua natimiza wajibu wangu, hilo siwezi kuliacha kulisema maana ndio ukweli wenyewe, ulivyo kuwa..ndivyo nafsi yangu ilikuwa ikinituma hivyo…

‘Ndio wakati mwingine, nilizidiwa na kuyafanya hayo yasiyofaa, ni kweli ni hulka, siwezi kuikataa. Wakati unafanya unaona ni sahihi, ila matokea yake ndio yanakupa fundisho.....lakini nimejifunza, na nilikuwa tayari kujirudi,…nilishaahidi iwe hivyo, lakini mwenzangu hataki,....nitafanya nini sasa…

‘Sikuweza kujibishana naye, maana utasema nini, wakati mwenzako kashika mpini,..ni haki yake aamue hivyo, huenda tangu mwanzo alitaka iwe hivyo, lakini hakukuwa na mwanya huo,…aah, ndio mawazo yangu, si mumetaka niongee…’akasema hivyo aliposikia watu wakiguna.

‘Ndio hivyo… sasa mwanya umepatikana, na katimiza dhamira yake, sawa.....mimi nasema hivi kwa vile kaamua hivyo,…na kiukweli moyo wangu ulikuwa haujarizika, mnafahamu ni kwanini..lakini nianyeje, .. na iwe hivyo tu…, kama ningekuwa na njia nyingine ya kumshawishi kuwa sitarudia tena ningelifanya hivyo, lakini sina,...sina..japokuwa mke bado nampenda…hamjui tu..

‘Ni kweli, ...nilikuwa na hasira sana, nikiona nasota jela, ...mimi sijaua, mimi nilijitolea muhanga kwa ajili ya watu wengine,..nilikuwa sina jinsi, marehemu alishaniweka kati..nisamehewe tu, na yeye asamehewe huko alipo…ilikuwa niamua familia yangu au mimi…nilikuwa sina jinsi, nikaona ni bora nijitolee mhanga …sasa ni nani angeliamini hivyo, eeh..kiukweli inauma sana.....na ...sawa sitaki kulalamika sana na kwa vile yeye keshahitimisha,  basi sina jinsi..

‘Kwa vile keshamaliza, na maamuzi hayo ni hitimisho…, mimi nimekubaliana na maamuzi yake, nitajitahidi kufanya yale yote yanayostahili niyafanye, na kwa vile tuna mafungamano ya watoto, mimi na yeye bado tutakuwa karibu, hadi hapo atakapoona yeye, au hali ikisema hivyo...natumai hatanifukuza nikifika kuwaona watoto wetu...wale bado ni kuinganishi chetu…nawapenda sana watoto wangu…

‘Nimekubaliana na yeye juu ya watoto kuwa waendelee kuwa kwenye mamlaka yake, kwa vile kaona kuwa yeye anaweza kuwalea katika malezi bora, yeye kaona wakikaa na mimi labda wataharibika , labda wataniiga mimi na tabia zangu mbaya…mmh,...

‘Hilo kiukweli nalikana,..sio kweli kuwa mimi ni mbaya kiasi hicho, inapofikia kwenye malezi ya watoto…mimi kama mzazi nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuwalea watoto  kwenye maadili mema….hata hivyo, mimi sikutaka kupingana naye sana juu ya hilo, kwa vile kwa kufanya hivyo tunaweza kuwaathiri watoto wetu kisaikolojia,...nawaombea sana wapate malezi bora wawe kama mama yao…

‘Sawa,mimi  nimekubali, kwa vile nawapenda sana watoto wetu, na nia yangu ni wao waishi maisha mema, yasiyokuwa na tabia mbaya kama za kwangu..nimekubaliana na mawazo yake kuwa huenda nitaoa,..na hajui huyo mke nitakaye muoa,…atakuwaje…anaweza asiwapende watoto…mimi sijui hilo kwa kweli…na mimi nisingelikubali…hatahivyo sawa…hamna shida.

‘Ni kweli hata mimi nimeliona hilo, ...mimi kama mzazi nawapenda sana watoto, nisingelikubali mtu awatese, lakini kwanini tugombane kwa hilo, basi nimewaacha watoto wakae naye, sina kinyongo kwa hilo…kabisa kabisa…kwani nitakwenda wapi, bado nipo kwenye jiji hili, tutazidi kuwa pamoja tu.

‘Ama kwa kampuni…nashukuru sana kwa uamuzi wake huo..mzigo mnzito umeshaondolewa, madeni…kiukweli yalikuwa mzigo mnzito sana…

‘Hata hivyo, bado hata mimi,..nitajitahidi kuyalipa, sitaweza kuwamtumpia mzigo weote yeye peke yake…ndio maana nasema., mimi nitajitahidi kuiendesha hiyo kampuni kwa juhudi kubwa sana

‘Ni sawa…mimi nitakaa na wenzangu, kama alivyopendekeza yeye, mke wa familia, kuwa nishirikiane nao,…nitashirikiana na rafiki yake, kwani hata kabla , yeye alishakuwa msaada mkubwa kwangu… inabidi nifanye hivyo kwa vile pia ana damu yangu,  napia eeh, …mmh, nitamshirikisha,na,.. ..na....’hapo akasita huku akimgeukia mpenzi wake wa asili kwa aibu, na mimi nikasema;

‘Mpenzi wako wa asili....mke mtarajiwa’nikasema na watu wakacheka, na yeye akainama chini kwa kutahayari, lakini akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Na yeye pia ataingizwa kwenye kampuni, kwani anaweza…yeye na rafiki wa mke wa familia walikuwa wakifanya shughuli zao kwa pamoja…kwahiyo kwa pamoja, sote tutasaidiana..sijakaa nao, ila baada ya hapa tutakaa pamoja na kuona ni nini cha kufanya, natumai, hata wao wamejifunza mengi, na kwahiyo hatutafanya makosa ..kampuni hiyo itaimarika na kuendelea kama kawaida...hilo ninawaahidi.

‘Kiukweli mimi nimejifunza mengi , ni kweli namshukuru mke wa familia kanisaidia sana,...tena sana,...na kwa hivi sasa ninaweza kuiendesha hiyo kampuni bila ya kusaidiana na yeye, lakini kwa vile na wenzangu wana uzoefu wa kikazi, na wana haki hiyo, ...sitawatupa, nitakuwa na wao bega kwa bega...’akasema huku akiinua kichwa na kumwangalia mwenyekiti.

‘Na pia nawashukuruni sana wazazi, wakwe zangu kwa kunipigania na kunijali,..nafahamu kama ingelifuatwa sheria basi ningelikuwa sina changu tena...

‘Kiukweli sikutegemea kabisa kuwa mngelinifikiria na kunitetea hadi hatua hii ya mwisho, nilishawaona nyie ni maadui zangu, haah..kweli nimeamini kuwa nyie ni wazazi wenye hekima, sitawatupa, na sitawasahahu katika maisha yangu yote, nyie moyoni kwangu ni wazazi wa kweli...’akasema akimwangalia mama na baba yangu.

‘Hata hivyo sina  budi kukiri kuwa nimekosa, nimesikia kila mmoja akitaka mimi nikiri hivyo,… ni kweli moyoni nakubali hivyo, lakini mara nyingi kutoa kauli inakuwa na ugumu fulani kwa vile wakati mwingine unahisi hivyo kuwa hujakosa..ndio hivyo, niseme huo ukweli.

‘Sasa….’hapo akatoka na kusimama mbele ya watu, akapiga magoti..

‘Hii naitoa kutoka moyoni, kuwa mimi ni mikosaji,nimewakosea sana..hasa mke wangu, hasa wazazi wangu, na jamii kwa ujumla..naowaombeni sana mnisamehe kwa makosa hayo…sijui nifanye nini ili mjue kuwa mimi nimekosa na nahitaji msamaha wenu..nikifika hapa..aah, sijui nilitaka mke wangu,..lakini keshaamua tena nifanyeje…’hapo akashika kichwa

‘Oh…, sitaweza kuongea zaidi ya hapa…, ahsanteni sana...’akasema mume wa familia huku akionyesha huzuni fulani kama anataka kulia.

‘ Inatosha…kweli hapo nimeamini kuwa umekosa, na sisi , …mimi kwa niaba ya wote tumekusamahe……kama hakuna muongeaji, labda tufunge kikao,..’akasema mwenyekiti, wakati huo mume wa familia bado kapiga magoti.

***********

‘Mwenyekiti samahani kidogo naomba nifanye tendo hili kabla hatujafunga hiki kikao...’nikasema na kwa haraka nikatoka pale nilipokuwa nimekaa na kumsogelea mume wa familia,…nikamuinua maana alikuwa bado kapiga magoti.

Na yeye akawa kama kashikwa na butwaa, nikamuashiria aliyekuwa mke wa docta aje, na yeye bila kinyongo akasogea pale nilipokuwa, kwanza nilichofanya ni kumkumbatia mume wa familia, na nikawambia;

‘Ahsante kwa yote, mimi kwa moyo mkunjufu.. nimekusamehe, na nakutakia maisha mengine mema, ..’na yeye kwanza alisita kunishika na mikono yake, ikawa inatetemeka hivi..baadaye akainua mikono na kunishika tukakumbatia kwa muda, halafu tukaachana.

Baada ya tendo hilo,…mimi nikamsogelea aliyekuwa mke wa docta, na kumshika mkono, nikasema;

‘Nakuomba tafadhali uje hapa…’nikasema, alipofika huyo, aliyekuwa mke wa docta, nikamsogelea mume wangu na kusema;

‘Mume wangu kama nilivyokuomba…naomba utimize ile ahadi yenu, mliyowekeana kule kijijini, wewe na mpenzi wako wa asili… mpange siku gani mtafunga ndoa halali, ....sina shaka na uchumba wenu.., maana ilivyo, moyoni siku zote mlikuwa wachumba, au sio, sasa wadhihirishieni uma kuwa kweli mnapendana, kwa kukumbatiana...’nikasema

 Kwanza iliwashika kama butwaa…wakawa wamesimama huku wakiangaliana kwa hali ya kutahayari kidogo,  na baadaye, wakasogeleana na kukumbatiana, huku machozi yakiwatoka, kilichofuata hapo ni...vigelegele na shangwe vikatanda.

Baadaye na mimi nikamkumbatia aliyekuwa mke wa docta, na tukachekeana, nikampongeza, halafu ndio nikamgeukia mume wa familia,...nikamshika mkono na kumkaribisha kifuani kwangu, tukakumbatiana, kumbatio la mwisho,  kwa amani na kuagana, huku machozi yakinitoka, ilikuwa kumbatio la kwaheri.

Ni heri iwe hivyo..

Kulikuwa hakuna njia nyingine, ilibidi hayo yafanyike kwa masilahi ya wote, na namshukuru mungu, kuwa tulifikia muafaka, kwani baada ya kikao hicho, na kumbatio hilo la mwisho kama mume na mke wa familia, mawakili walifanya kazi yao vyema, ndoa ikavunjwa, talaka ikatayarishwa, na ikawa mwisho wa ndoa yangu na mume wa familia, yeye akaanza maisha yake na mimi maisha yangu.


MWISHO


NB: Mume wa familia kama ilivyotarajiwa baada ya miezi mitatu walifunga ndoa na mpenzi wake wa asili, ndoa tuliyoisimamia mimi na docta na wazazi wangu, na ilifana kwa kweli, ...mimi nikawa best woman wa mke wake, na docta akawa best man wake...

 Sio siri, yaliyopangwa na mungu hayapingiki, baada ya mvutano, na ushawishi mwingi wa docta, nilikubali turejeane urafiki wetu, na sisi mapenzi yetu ya asili yakarejea, nikakubali ombi lake kuwa tufunge ndoa, ahadi ikatimia, lakini ni baada ya miaka kama miwili hivi ya mvutano…

Nikaona haina shida…kwanini tujivunge…tukafunga ndoa, na sisi tukawa mke na mume.

 Na aliyekuwa rafiki yangu, yeye aliendelea kumlea mtoto wake, na alisema hataki kuolewa tena, sijui  kwanini, ...

Pengine hajapata anayemtaka, yote maisha,..yeye anadai alichokitaka keshakipata, yaani mtoto, na mdogo wake aliyekuwa mume wa familia yangu, alihamia Kenya na kuanzisha maisha yake huko, na yule mfanyakazi wa ndani sasa hivi ni mmoja wa mabosi ndani ya kampuni yangu..huwezi amini ukiutana naye …anamiliki gari lake na nyumba yake mwenyewe..

‘Hicho ndicho kisa changu mpendwa...’ akamaliza mdada


WAZO LA LEO: Mkioana na bahati mbaya ikafikia hatua ya kutalikiana na juhudi zote za kusuluhishwa zikashiniakana, basi achaneni kwa amani, kuliko kuishi huku mkiumia,fanyeni hivyo kwa amani na upendo, kwa masilahi ya watoto wenu, na mahusiano mema, ili mje kutembeleana kama marafiki wa zamani kwa upendo na furaha.

Natoa wazo hili sio kwamba napenda mawaza ya talaka, ila wakati mwingine inabidi iwe hivyo, kwani kuna mengine hayavumiliki, na hatuwezi kujidanganya kuwa tutaishi hivyo hivyo tu, ya mungu mengi, huwezi kujua ni nini kakupangia badili yake,hatuwezi kulazimisha kitu ambacho hakitakuwa na amani kwetu, tukaishi kwa maumivu na masononeko.

 Japokuwa kiukweli,kuachana si kuzuri, hasa mnapokuwa na watoto, mkifikia kuachana basi peaneni mikono na muombeni mungu wenu, kila mtu aje kufanikiwa katika maisha mengine…mola anajua zaidi.

NAWASHUKURU WOTE WALIKUWA NAMI TOKA MWANZO WA KISA HIKI, MUNGU AWABARIKI SANA, NA MAONI YENU MAOMBI YENU, MUNGU AYAKUBALI, HUENDA SIKU MOJA NA MIMI NITAWEZA.....kutengeneza kitabu, au hivi visa kuweza kuigizwa kwenye runinga, halikadhalika kupata wadhamini, maana haya yote nayafanya kwa gharama na muda,..lakini msijali ipo siko...

TUPO PAMOJA,.... 


Mwisho wa kisa hiki ndio mwanzo wa kisa kingine.
Ni mimi: emu-three

No comments :