Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, March 17, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-97Leo ni leo….nikaingia kwenye mapambano…nikiwa peke yangu!

Nikiwa nimetulia ofisini kwangu nikimalizia kazi mbali mbali, na mara nyingi unapoanza kazi za mahesabu,kuweka kumbukumbu za mahesabu kwenye komputa, na kutayarisha  taarifa mbali mbali, masaa yanakwenda haraka bila hata yaw ewe mwenyewe kujitambua, nikawa nimesahau kabisa wajibu wangu mwingine.

Nilipoangalia saa, ndio nikagundua hilo….nilikuwa nimetumia muda mwingi sana,...hapo hapo nikaacha kila kitu, na kujiandaa kutoka mle ndani, niende chumbani kwangu ikibidi nikachukue silaha, ili nikaweza kuwavamia Makabrasha na mume wa familia.

Kwanza nilitaka kuhakikisha kuwa hawo jamaa bado wanaongea, au mume wa familia keshaondoka maana muda mwingine ulishakwenda, nikachukua simu kutaka kupiga, lakini kitu kikanizuia, sikupiga simu.. nikawa sasa nataka kutoka mule ndani,…hapo ndio nikasikia king’ora cha polisi kwa mbali,

Muda huo moyo wangu unadunda sana,…na ikitokea hivi kama nipo kwenye mapambani ni ishara ya hatari…na niliposikia hicho king’ora cha polisi ndio ikawa ni zaidi,…hata hivyo mwanzoni nilijua ni polisi wanapita tu.., lakini kilipofika maeneo ya kwenye jengo kikasimama hapo, na  mimi nikashituka, nikajua kuna kitu ..kuna jambo, na sio jambo dogo.

Nilichofanya kwa haraka nikumpigia simu mlinzi kumuuliza kuna nini, na mlinzi akasema hana uhakika

‘Huna uhakika, hilo sio gari la polis limesimama huko, limafuata nini…?’ nikauliza

‘Ndio na mimi nafuatilia madam…’akasema.

Hapo sasa sikujali nikampigia boso yaani Makabrasha..simu ikawa inaita bila kupokelewa,…moyoni nikajua kuna tatizo limetokea ofisini kwa makabrasha, nilitaka kumpigia mtoto wake kwani ndiye mlinzi wa baba yake, lakini sikupenda afike kwanza, nilijua akifika kila kitu kitaharibika.

Nikawa bado nipo mle ndani, moyo haunitumi kutoka nje…., nikapiga simu kwa walinzi kama mtoto wa Makabrasha keshafika, huyo mlinzi akasema hana uhakika, kwani yeye alitoka, na kumuachia mwenzake ulinzi, na huyo mwenzake  ameshaondoka.

Baada ya dakika chache, nikapiga simu tena  kwa walinzi kuulizia kuna nini, wakaniambia kuna tatizo kubwa limetokea ndani ya ofisi ya Makabrasha, na polisi wameshafika,..

‘Polisi!, tatizo gani la kuwahusisha polisi?, wamekuja kufanya nini?’ nikauliza maswali mengi kwa haraka bila kujua nauliza nini.

‘Makabrasha kapigwa risasi na hali yake ni mbaya sana, sijui kama atapona...’akasema huyo mlinzi na aliposema hivyo

‘Kapigwa risasi na nani…!’ nikauliza

‘Hatujui madam…’wakasema

‘Hamjui , huyu mtu aliingiaje ndani na silaha, bila kujulikana…’nikasema nikiwa nimesahau kila kitu kuwa kama ni wa kulaumiwa ni mimi, niliyezima mitambo ya kugundua vitu kama hivyo.

Pale mawazo yangu yalinipeleka kuwa liyefanya hivyo ni mume wa familia, japokuwa Makabrasha siku hiyo nzima alikuwa akikutana na watu mbali mbali, na wa mwishi ndio alikuwa mume wa familia kutokana na ratibba yake

‘Kama ni yeye amepatia wapi silaha, na aliingia nayo kw vipi, yawezekana..mungu wangu…’nikajikuta nikisema hivyo…

Nikampigia tena mlinzi mwingine kumuulizia,..sasa nikiwa na sauti ya kutaka kulia, nikasema;

‘Na nani kafanya hivyo, maana muda mfupi uliopita nilikuwa nikiongea naye, kwenye simu,haiwezekani..ngoja nikahakikishe....’nikasema na kukata simu.

Nilitoka mle ndani, nia nikuelekea huko, ili kama mume wa familia yupo hapo niweza kutoa msaada,lakini nilikuwa nimechelewa, kwani nilipotoa kichwa kuangalia kwenye korido, nikawaona maaskari. Wanakuja kuelekea chumba cha Makabrasha.

Kumbe maaskari walishafika, nikarudi ofisini kwangu kwa haraka kabla hawajaniona,na kujifungia, sikutoka kabisa, na sikutaka kufanya lolote maana sikujua nikikutana na hao polisi nitasema nini.

Nikawa namuomba munu wangu hayo yanipitilie mbali maana nikihojiwa, nikasema ni mimi nilizima mitambo ya kuonyesha matukio, nitakuwa hatarini, kwanini nilifanya hivyo, nk…

Maombo yangu yakajibiwa,…ajabu kabisa siku hiyo hakuna polisi aliyekuja kunihoji. Walikagua ofisi zote lakini ya kwangu wakaisahay,…baadae ndio nikasikia kuwa, wameshampata muaaji,...

‘Ni nani huyo..?’ nikauliza, wakanitajia sifa za huyo mtu aliyekamatwa, na jina lake,..oh...

‘Huyu mdada alifikaje hapa…., alikuja muda gani?’ nikauliza, na walinzi wakasema alifika hapo muda kabla polisi hawajafika, na inaonekana ndiye aliyemuua  Makabrasha, na polisi wameshamshika, yupo chini ya ulinzi.

‘Aliingiaje na silaha..?’ nikauliza

‘Hata sisi hatuji Madam, maana mlinzi wa mlango wa kuingilia anakiri kuwa alimkagua na hakumkuta na silaha yoyote, na mitambo ya hatari haikuwahi kulia…’akasema na alipotaja mitambo, moyo wangu ukakumbuka jambo, hapo hapo nikauliza

‘Je yule mgeni wa Makabrasha, mwanaume aliondoka muda gani?’ nikauliza.

‘Alipoondoka tu ndio huyu mdada akaja…baadaye ndio hapo ikagundulikana kuwa Makabrasha amepigwa risasi...’akasema.

‘Ni nani sasa aligundua hilo?’ nikauliza.

‘Hatujui, hata sisi tuliona ajabu, maana hakuna mlio wowote wa hatari uliosikika, ina maana mitambo huko juu haifanyi kazi..na akti yetu hakuna aliyewahi kupanda huko juu, mpaka sasa polisi hawajasema ni nani aliwapigia simu…!’ akasema.

‘Sawa…tutajua tu..’nikasema

Wazo la haraka ni kwenda kuwasha mitambo ya kunasia matukio, …amoja na uamkini wangu, siku hiyo nilichanganyikiwa, maana…mawazo yangu yalikuwa kwa mume wa familia je yupo salama…

‘Je polis wakigundua hilo, kuwa ni mimi nilizima hiyo mitambo itakuwaje..’hilo nalo lilinisumbua sana…hapo sina ujanja, moja kwa moja nitashikwa kwa kuhusika na hayo mauaji, hapo nikawa na wakati mgumu. 

Nikatafuta upenyo, hadi nikaupata nikatoka pale haraka na kwenda chumba cha mitambo ili niweze kuweka ile mitambo ON, niliingia kile chumba kwa haraka, nikaendelea ule mtambo...nilipotaka kugusa pale, nikagundua ipo ON tayari.

Unajua nilishituka,..ni kama vile mtu kaona kitu cha kutisha,.. ina maana kuna mtu alikuja akabadili, ...ni nani huyu, hakukuwa na muda wa kufikiri, ni kitendo cha haraka, kama ipo ON, ina maana matukio yote yatakuwa yapo bayana..

Hapo nikavutika nione kilichotokea kwenye ofisi ya Makabrasha, kwa haraka nikavuta droo ya ile komputa, laptop...ila nataka kuivuta mara....nikasikia kitu au mtu, hapo nikageuka kwa haraka kuangalia huku na kule, nilihisi ni mtoto wa Makabrasha kaja,..lakini hakukuwepo na mtu, hata nilipojaribu kuangalia kila sehemu sikuona mtu..ila nina uhakika huyo atakuwa ni mtu tu...

Nikaacha, kile nilichotaka kukifanya, sasa nikawa na wasiwasi kuwa hata polisi wanaweza kunikuta hapo, na ninaweza kuonekana kuwa nilikuwa natafuta njia za kuficha ukweli,...na wakatu nawaza hilo, mara nikasikia watu kama wanakuja mueleko huo nikajua ni polisi…nikatokeza kichwa.

Ni kweli walikuwa ni polis wanazunguka, hapo, nikaona hakuna usalama tena…nilipoona kuna upenyo nikatoka kwa haraka na kurudi ofisini kwangu, na kutulia kuwasubiri polisi wakija kunihoji, nilijua ni lazima watafika kunihoji...lakini hilo halikutokea kabisa siku hiyo.

 Muda ule nipo hapo ofisi peke yangu, nikawa namuwazia Makabrasha, sikuamini kuwa huyu mtu anaweza kufa,..ina maana uhai wa mtu ndio hivyo, muda mpo naye ghafla keshapotea, ndio basi tena...nikamuwazia sana, zile tambo zake..kuwa yeye hawezi kufa hivi karibuni maana ana afya..., hata hivyo, kuna muda nilijikuta nikimuwazia kuwa huenda atapona hajafa...lakini kama alipigwa risasi, sijui sehemu gani, na huyo muuaji alidhamiria kumuua, sijui kama atapona!.

Unafahamu mtu hata awe mbaya vipi, linapomfika jambo kama hilo, la ugonjwa au umauti, hata kama ni ugonjwa tu, huwezi tena kumtakia mabaya, huruma itakuja tu, labda wewe uwe na nfasi mbaya, hapo mimi nikawa naombea apone tu, asife...sio dhamira yangu mtu huyo afe, mimi nilitaka akamatwe afungwe tu, ili haki itendeke, lakini sio kufa...

Kiukweli pamoja na mengine, kuwa alikuwa ni adui yangu na ilifikia muda natamani hata kumuua, lakini mtu huyo alikuwa na mazuri yake, ukiwa naye, ..na hata kwa jamii,..na kiukweli pamoja na hayo, alishakuwa mtu wangu wa karibu, sasa nikifikiria kuwa sitamuona tena, hapo kiukweli sikuweza kujizuia, nililia sana..kumbuka hapo nipo peke yangu…

 Sikumbuki nilikaa muda gani nikilia hivyo,…kuangalia saa muda ukawa umepita sana, kupo kimia, na ile hali iliyozoeleka muda huo huwa nje kumechangamka, lakini siku hiyo ilikua kinyume chake, watu waliondoka, waliobakia ni wachache tu..

Hapo nikapiga simu kwa askari ili nijua kinachoendelea, askari huyo ndiye akaniambia kinachoendelea huko njem...kuwa Makabrasha kakimbizwa hospitalini...

'Ana hali mbaya sana..?' nikauliza

'Sijui Madam, hakuna aliyeweza kumuona, polisi hawaruhusu...'akasema

'Oh, basi, huenda atapona..'nikasema

'Sijui...'akasema huyo askari, na kukata simu

Nikawa hata sijui nifanye nini...kila ninachoshika hakishikiki, ule ujasiri wangu wote ukaondoka, ..nikachukua simu kumpigia mume wa familia, simu haipatikani, nikampigia docta wake ninayemfahamu simu haipatikani, nikampigia simu mume wangu halikadhalika....ikawa n ajabu kwangu, kwanini watu hao muhimu hawapatikani.

Sasa nimetulia, mara simu ya huyo askari niliyekuwa nampigia simu ikaita, nikapokea kwa haraka

'Nipe habari..?' nikauliza

'Makabrasha hatunaye tena duniani..'akasema

'Nini, una uhakika...?' nikauliza

'Ndio ukweli wenyewe, kafariki kwa jeraha la risasi,..uchunguzi bado unaendelea,…’ akasema huyo askari.

Shahidi huyu alipofika hapo akatulia kidogo kama kukumbuka kifo cha mtu huyo. Hata mume wa familia alionekana kuwa mbali zaidi maana sasa alikuwa kashika kichwa kwa mikono kichwa kimeegemea mikono.

Nilipopata taarifa hiyo, sasa akili ndio ikaanza kufanya kazi, sasa nikaona nitoke hapo haraka nirudi huko chumbani kwangu, niliangaza nje, nilipoona hakuna dalili ya askari haraka nikatembea hadi sehemu ya kushuka chini kulekea chumbani kwangu, karibu nionekane na askari, lakini hakuniona.

Wazo langu kwa muda huo ikiwezekana, nitokea kabisa kwenye hilo jengo nipotee kabisa, usiku kama huo angaliona nani,..na asubuhi na mapema nisafiri hadi huko kwetu kijijini, maana hata hapo watu humo jengo wananifahamu kwa sura ya bandia, sio ile sura yangu ya asili, kwangu ingelikuwa ni rahisi kutoka na ingelichukua muda watu kunigundua kuwa ni mimi nilikuwa nafanya kazi humo.

Nilishajipanga hivyo, lakini nisingeliweza kuondoka haraka hivyo,...bado kuna mambo ya kufanya, kwanza...hapo ndiop nikakumbuka ile silaha...nikawa sasa nipo chumbani, kwa haraka nikainua lile godoro....nilishikwa na butwaa...

Bastola haipo...!

‘Nani kaingia humu na kuichukua bastola…’ nikajikuta nikijiuliza mwenyewe, hapo nikainua godoro kabisa na kuliweka pembeni, hakuna kitu…

Mawazo ya haraka yakaniambia, bastola hiyo ndio imechukuliwa kufanyiwa mauaji…miguu yote ikalegea, nikajikuta nakaa sakafuni,..sina la kufanya, nikaiona jela ilee…

Maana hapo utajitetea nini..ni mimi niliyezima mitambo, bastla iliyoua nilikuwa nayo mimi, ni kwanini nilikuwa na bastola…nitasema nini kwa polisi…’hapo akatulia kwa muda, na aliyemzindua ni mwenyekiti,…

‘Bastola haipo imekwenda wapi…hapo tuambie ukweli, nahisi kuna kitu unatuficha?’ aliyeuliza swali hilo ni mwenyekiti…

‘Mimi sijui mwenyekiti sikujua imekwenda wapi….’akasema msimuliaji

‘Hapo kwakweli sisi hatukuelewi, Ina maana unataka kutuambia kuwa  sio wewe uliyemuua Makabrasha…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Mwenyekiti huo ndio ukweli anu, haya niliyosimulia ndivyo ilivyokuwa,…’akasema

‘Kiukweli inavyoonyesha hadi hapo, ni kuwa wewe na mpenzi wako ndio mlioshirikiana kumuua, makabrasha,…hadi hapo tu, huna cha kujitetea,…’akasema mwenyekiti

‘Mwenyekiti ndio maana nikaamua kuwaelezea ilivyotokea, nafahamu hilo, kuwa haya maelezo yangu ambayo ndio ya ukweli, yanaweza kunifunga, na mimi nitaonekana kuwa ndiye niliyeua,…lakini huo ndio ukweli, mkweli hana lawama..’akasema shahidi

‘Hebu nikuulize, hapo ulipokuwa kwenye ofisi na ofisi ya Makabrasha kuna umbali gani…?’ akauliza
‘Ni ofisi zilishikiana, yaani ni sema ni vyumba viwili vya karibu, sema ofisi ya Makabrasha ni kubwa, sio kama ilivyokuwa yangu…’akasema

‘Kwahiyo chochote kinachofanyika ofisi kwa Makabrsha hukuweza kukusikia..?’ akaulizwa

‘Huwezi kusikia kabisa,..alivyoitengeneza ofisi yake ni ‘sound proof..’ akasema

‘Lakini ungeliweza kutoka kwenye chumba chako kwa haraka na kufanya mauaji na kurejea ofisi kwako,…au sio…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Ungeliweza…siwezi kusema huwezi maana …..ila nasema hivi, mim sijafanya hivyo,…’akasema

‘Polisi wanasema, wewe ndiye uliyezima mitambo ya kuonyesha matukio, wewe ulikuwa na bastola, bastola hiyo alikuelekea mdogo wa mume wako kwa siri..mdogo wa mume wako kalithibitisha, hilo…kwanini ulihitajia silaha mdogo wa mume wako kasema hajui…’akasema mwenyekiti.

‘Hawezi kujua hilo, maana hakuna aliyemuambia…alichosema ni sahihi..’akasema shahidi

‘Hadi hapo, sisi kama wanafamilia, unafikiri tunaweza kukuamini..?’ akauliza mwenyekiti

 ‘Nakumbuka, tangu mwanzo, kabla sijaongea mimi, wewe ulikuwa ukiamini kuwa aliyefanya hivyo ni mume wa familia na mdogo wake, au sio , sasa iweje kwa haraka uamini kwua ni mimi nimeyafanya hayo mauaji,…?’ akauliza shahidi.

‘Ni kutokana na maelezo yako…’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo ukweli wangu ndio unaokufanya nionekane mimi ni muhalifu, au sio..kwahiyo mimi nimefanya kosa kuwaelezea huo ukweli,  jinsi ilivyokuwa…?’ akauliza shahidi

‘Kutokana na maelezo yako toka mwanzo, inaonyesha ni wewe, kwasababu silaha iliyotumika kumuua Makabrasha ulikuwa nayo wewe hadi hatua ya mwisho, na wewe ndiye uliyafahamu wapi silaha hiyo ipo, na wewe ndiye ulizima mitambo ya kuonyesha matukio, kweli si kweli..?’ akauliza

‘Ndio…’akasema
 na wewe umekiri kuwa ulishafikia sehemu upo tayari hata kumuua, kutokana na hali aliyowatendea, na..zaidi ulikuwa tayari kufanya lolote kumlinda mpenzi wako, na zaidi wewe unafahamu kutumia silaha vizuri, kuliko mpenzi wako
..huoni huo ukweli, hapo huwezi kukwepa hilo,..sema ukweli wako, ili tulimalize hili...’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti,..hayo niliyowasimulia hadi hapo, ndivyo ilivyokuwa, huo ndio ukweli, wa siku hiyo,...kama mliambiwa vinginevyo ni uwongo, maana mimi nilikuwepo humo ndani, tatizo, ni kuwa, ni kweli ni mimi nilizima kitufe cha kuonyesha matukio…’akatulia]

‘Subiri kidogo..ulisema ulipokwenda kuwasha uliona kipo ON…?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio..ndio maana nataka muwe na subira, kwasababu bado nina maelezo zaidi ya hayo, mkifanya haraka mtauharibu ukweli na nyie ndio ndugu zangu, mnahitajika muufahamu ukweli kabla sijaingia mikononi mwa polisi..’akasema

‘Sawa sisi tutakusikiliza tu, lakini hadi hapo, hata sisi tuna wasiwasi na wewe…’akasema mwenyekiti..

‘Wasiwasi wako hadi hapo, unakujaje, kuwa mimi ndiye niliweka hicho kitufe OFF, kwanini usiwe na wasiwasi kuwa NINANI, aliyekuja kuweka ON, na kwanini..na aliweka muda gani…?’ akauliza shahidi..

‘Hapo sijui, labda utuambie wewe…’akasema mwenyekiti.

‘Ndio nawakata msiwe na pupa,…maana kumbe baada ya hapo, huenda, huyo mtu alikuja kuweka ON, baada ya kumaliz hiyo kazi, au sio, kwanini matukio hayo yasionekana, hadi leo,..je polisi wanayo taarifa ya matukio yaliyotokea siku hiyo…?’ akauliza

‘Mimi sijui…’akasema mwenyekiti

‘Hawana, ukweli ni kwamba kuna mtu alikuja akaiba video, ya amtuki ya siku hiyo, ina maana kama ingelikuwepo, ingelionyesha yote yaliyotokea baada ya kuwekwa ON, nina imani,..kuna kitu hapo…’akatulia

‘Kwanini unasema hivyo…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Sikiliza,..mimi niliweka OFF,..akaja mtu mwingine, huyu mtu mwingine hajui kuwa mimi nimeweka off…ukiwaja kwa haraka, usipoangalia kwa makini unaweza kuweka ON, ukijua mwenzako kaweka OFF, au ukaweka OFF, ukijua mwenzako kaweka ON, na ndivyo ilivyotokea…’akasema

‘Una maana gani..?’ akauliza mwenyekiti.

 ‘Ndugu mwenyekiti…baada ya kufikiri sana na kupata taabu ya kuliwazia hilo tukio lilivyokuwa, nikaona ni bora niseme huo ukweli ulivyokuwa, lakini nikijua kabisa, nikielezea huo ukweli kwa polis kwanza nitakwua mshukiwa namba moja , achilia mbali polisi,yoyote nitakayemuelezea huu ukweli,  jinsi ilivyokuwa hataamini kuwa sio mimi niliyemuua Makabrasha,

‘Hata mimi…’akasema mwenyekiti

‘Ni sawa, sio kosa lako mwenyekiti,sio kosa la yoyote aliyepo humu ndani, lakini mimi ninaamini ukweli ndio silaha ya mtu yoyote yule…’akatulia

‘Sawa tuelezee ukweli wote, ndio tunataka sisi..kama wanafamilia..’akasema mwenyekiti

‘Ukweli wangu ndio huo, nyie ndio kwa mara ya kwanza nimweza kuwalezea kila kitu kilivyokuwa, bila kukwepesha jambo, maana hapo ningeliweza kukepesha, hebu jiulize kwanini hadi leo polisi hawajaweza kunikamata…?’ akauliza

‘Walitaka kukukamata mimi ndio nimewazuia…’akasema

‘Sasa ndugu mwenyekitu huo ndio ukweli, ni wajibu wenu, kuukubali kama ulivyo, au kuungana na polisi, siwezi kuwazuia kwa hilo, lakini ukweli halisi ndio huo, na sikuwaficha kitu hata kimoja,…ndio maana nilitaka nielezee hatu kwa hatua…,kama nimewaficha kitu mungu pekee ndiye anayejua zaidi….siwezi kukumbuka kila kitu au sio…’akasema

Aliposema hivyo mwenyekiti akakuna kichwa kidogo ile yakufikiri halafu akasema;

‘Mhh,… mimi sijui, lakini nionavyo mimi polisi wakisikia hayo maelezo yako , moja kwa moja wewe utakuwa mshukiwa namba moja, je hujatuficha kitu, mimi naomba uwe mkweli ili wakili wetu aweze kukutetea, nipo tayari kumtoa wakili wangu kwa ajili hiyo…?’ akaniuliza mwenyekiti.

‘Mwenyekiti, pamoja na hayo mimi nimeshaongea na polisi, lakini nilijua jinsi gani ya kuwaambia..niliwaambia yale niliyoyafanya kama mfanyakazi wa Marehemu lakini sikuwaambia kuhusu bastola au kuzima mitambo, ili nipate muda wa kukamilisha upelelezi wangu, ni muhimu sana ili haki iweze kutendeka...’akasema.

Mwenyekiti akaangalia saa yake, na alionekana na maswali mengi ya kumuuliza huyo shahidi, lakini kabla hajamuuliza huyo shahidi, huyo shahidi akasema;

‘Mimi imenichukua muda  kuliwaza hilo, lakini moyo unanisuta, na kila nikiwaza sana naona sijatenda uadilifu, na watu wengine wanakamatwa ovyo, wakishukiwa kwa hayo mauaji,…wakati sio kweli,… na imekwenda, inafikia hali kama inafifia hivi, kwanini..ina maana kuna mtu anafichwa, ukweli sasa unaanza kubatilishwa, na kuna watu wengine, wanatarajiwa kukamatwa..na ni baada ya propaganda potofu..’akatulia

Na wasiwasi wangu ni huo kuwa atakayefuata kwa hivi sasa ni mume wa familia na mdogo wake, ambaye keshausema ukweli ..na huo ukweli kama kausema ulivyo, mume wa familia yupo matatani, mimi ndio naanza kuingizwa sasa....ndio maana nikaona sasa inapokwenda ni kubaya, ni bora nijitokeze mimi mwenyewe, wasiwasi wangu ni kuwa bado sijamaliza kazi yangu,....'akasema.

'Kwahiyo umeamua kujitokeza kwa vile sasa inaelekea kumgusa mpenzi wako wa asili..kwahiyo kwa hivi sasa upo tayari kufungwa kwa ajili yake…?' akauliza mwenye huku akitabsamu kwa utani.

'Hapana, ....mimi kama mpelelezi, hilo nilikuwa nalifanyia kazi, nilikuwa kwenye uchunguzi binafsi, kumjua ni nani hasa aliye-yafanya hayo mauaji, maana nashindwa kujua, ni nani mwingine angeliweza kufika hapo na kuchukua silaha hiyo, ..’akatulia

‘Kwanza kabisa kwenye shuku zangu nilimuwazia mtoto wa Makabrasha, lakini ukumbuke hadi walinzi walithibitisha kuwa mtu huyu hakuwahi kufika eneo la jengo hilo…wapo walinzi ninaowaamini sana,… na yeye pamoja na kukosana na baba yake asingeliweza kumuua baba yake, anampenda sana baba yake, sasa ni nani mwingine angeliweza kulifanya hilo...'akatulia kidogo, halafu akasema;

'Kiufupi, sikutaka kusema huo ukweli, kabla sijamaliza uchunguzi wangu, ila ninachotaka kuwaambia hapa ni hivi, ...mimi sijamuua Makabrasha huo ndio ukweli...na sikuwa na mipango huo, mimi nilikuwa na mipango yangu mingine kabisa ya kumnasa huyo mtu na kumfikisha kwenye vyombo vya dola, nikiwa na ushahidi ambao ulikuwa unafichwa na Makabrsha..ili iwe ni mwisho kwa mtu huyu, na kundi lake haramu, maana yeye anatumiwa tu....’akasema

‘Ushahidi huo unao sasa…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Siwezi kukujibu hilo swali kwa hivi sasa…’akasema shahidi

‘Kwanini…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Nina maana yangu kama mpelelezi, niamini kwa hilo…’akasema hivyo

‘Sasa kama sio wewe uliyemuua Makabrasha ni nani basi,…maana kwa muda huo, mweye silaha, na aliyekuwa humo ndani ni wewe?’ akauliza mwenyekiti.

‘Kama mtaniruhusu ninaweza kuongea nionavyo mimi,kutokana  na uchunguzi wangu kiogo nilioufanya, ningelipata muda zaidi eeh, nikaweza kumalizia uchunguzi wangu, ningelimaliza kazi..lakini naona haraka haraka za polisi zitafanya nisifanikiwe, na nafahamu ni kwanini..’akasema

Mwenyekiti alisita kumuuliza ni kwanini, akawa anaangalia nje, halafu shahidi akasema

‘Japo sio sahihi, hata mimi sipendi, je ndugu mwenyekitu upo tayari niutoe ushahdi mwingine wa ni nani kamuua Makabrasha, kitu ambacho hata polis hawajaweza kukigundua,..?’ akauliza

‘Hayo ..kwanini usiwaambie polis wenyewe, maana wanasubiria huko nje…?’ akasema mwenyekiti na watu wakageuka kuangalia huko nje, na kweli askari walionekana wakiranda randa nje, kuhakikisha hakuna mtu anayetoka.

Shahidi akainamisha kichwa chini, kama anamuomba mungu wake, halafu akasema

‘Mwenyekiti wewe ndiye unayweza kulisawazisha hili, na ukweli ukapatikana, wewe ndiye waliyekuamini, au sio…mimi nasema hivi, fanya kile unachoona ni sahihi, lakini kwangu mimi, …bado nilikuwa na mengi ya kufanya,..unaonaje… yao…’akasema nakusita, alipoona mwenyekiti akisoma ujumbe wa simu yake

 Ilionekana Mwenyekiti yupo kwenye wakati mgumu. Baadaye  mwenyekiti akachukua simu yake akitaka sasa akitaka kupiga , huku akimwangalia huyo shahidi, na shahidi akageuka pembeni kumuangalia mume wake, alijua hadi hapo hakuna jinsi, ni lazima mwenyekiti atimize aajibu wake, hata hivyo nafsi mwake alijua bado hajakamilisha kazi yake. Shahidi huyo sasa akaniangalia mimi, nahisi alihitajia msaada wangu…

NB: Ni nini kitaendelea.WAZO LA LEO: Dhana mbaya haitakiwi, hii ni pamoja na kusengenya, kuwateta watu wengine vibaya,..hivi vitu sasa hivi vinaonekana ni vya kawaida tu! Watu kutetana, kuandikana mambo ya aibu, kupiga picha mbaya na kuziweka mitandaoni, kuzusha uwongo, au propaganda,..au jambo halijathibiti,a u kuruhusiwa kuongea wewe unakuwa wa kwanza kulitangaza... nia wakati wmingine ni kuharibiana majina. Hii ni dhambi kubwa, hebu fikiri kama ni wewe ungelifanyiwa hivyo ungelifurahi, ukijua kuwa ni uwongo. Inaumiza sana..je utawezaje kulilipa hilo jeraha la mtu aliyeumia moyoni kutokana na dhana hizo potofu..Tujiepusheni na tabia hii jamani.

Ni mimi: emu-three

No comments :