Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 15, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-95



Kazi imeanza….

Nikaenda sehemu wanapohifadhia picha za video  ambazo zilikuwa zinaonyesha mtu aliyefika kwenye hicho chumba karibu, nikajiona ni mimi peke yangu nikaifuta hiyo kumbukumbu, halafu nikatafuta sehemu ya kuzuia kamera za humo ndani zisichukue matukio hadi itakapokubaliwa tena ,nikaiweka OFF.

Ina maana kuanzia hapo hadi hapo mtu mwingine atakapokuja kuikubali kuonyesha matukio, kutakuwa hakuna kitu kitakachoonyeshwa, nilipoamaliza nikatoka kwa haraka, na wakati natoka tu, genetaror likaanza kunguruma na umeme ukarudi.

‘Oh huyo mtu kaniwahi, lakini bado…’nikasema kimoyo moyo

Nikatoka mle ndani kwa haraka nikawa natembea kuelekea ofisini kwangu, mara bosi huyu hapa…

‘Ulikuwa wapi wewe nakutafuta sehemu zote,..naona mitambo ya usalama humu ndani imezima, sio kawaida, hata umeme ukizimika inaweza kuhimili hata saa nzima, ..kuna tatizo,....’akasema Makabrasha huku akielekea kwenye chumba cha usalama, lakini baadaye akatoka huku akiongea peke yake.

‘Naona kuna tatizo kwenye mitambo ya usalama, ..siwezi kuingia kwenye komputa ya usalama, sijui huyu mtoto kafanya kitu gani,..kabadilisha neno la siri...kwanini anafanya hivyo bila kunipatia mimi taarifa, sasa tutafanye hapa..’akawa anaongea huku akinipita na mimi nikamwambia.

‘Mimi sijui, lakini tunaweza kujaribu pamoja huenda tukagundua jinsi gani ya kuingia, tukiwa wawili…’nikasema.

‘Hapana huko wewe huhusiki kabisa, ni mimi na yeye tu…’akasema

‘Kama yeye hayupo na hali kama hii imetokea itakuwaje…?’ nikamuuliza

‘Subiri wewe,…haya hayakuhus,  ngoja nimpigie simu huyu mwanangu, japokuwa leo tumekorofishana, lakini hili ni muhimu, ni lazima afike, kwa hraka…’akasema sasa akishika simu kumpigia mwanae nikaona nimpoteze mawazo kwanza…

‘Mbona alishafika hapa…’nikasema
Ina maana kumbe alikuja kuzima na kubadili …kwanini lakini huyu mtu ni muhuni sana, ana nini leo..’akasema kwa hasira.

‘Nahisi kuna kitu, alitaka kufanya, labda anataka kurekebisha, nilisikia akisema kuna matatizo kwenye mitandao..ooh, unajua mimi sijui mambo zenu…’nikasema

‘Alitakiwa aniambia mimi, yeye ni mwanangu tu, haya mambo humu ni yangu sio yake, naona anataka kunipanda kichwa, …ni lazima niongee naye, au ni kweli labda kuna kaliona, ikabidi afanye hivyo, alitakiwa aniambie au sio…’akasema kama ananiuliza

‘Kapatiwa,…subiria si atakuja….’nikasema

‘Unajua leo sijisikii vyema, sipo hivi kabla, mwili wangu una afya tele, lakini leo, ooh, nahisi natakiwa baadae nioane na dakitari…halafu nahisi ....kama kuna tatizo kama kuna kitu kibaya kinata kutokea,.tokea jana  hali haipo sawa..’akasema

‘Unaumwa, inabidi umuone dakitari, wewe si unaweza kumuita mmojawapo akaja kuutibia hapa nyumbani….’nikasema

‘Hapana mimi siumwi,…unajua jana nilikorofishana sana na huyu kijana wangu, namuona kabadilika ghafla,..mama yake anamfunza vibaya, sio yule mwanangu wa zamani ambaye alikuwa akinitii kila kitu…’akasema

‘Kwani mama yake karudi..?’ nikauliza

‘Ndio,…huyu kila mara akiwepo inakwua hivi..nilishamuambia kijana wangu asimsikilize mama yake…kwani mama yake hana nafasi kwangu, ilitokea bahato mbaya tu nikazaa naye, sina ….mahusiano naye kabisa…’akasema

‘Lakini si umezaa naye, huo ni uhusiano pia….wewe ulipozaa naye ulitegemea nini..?’ nikamuuliza

‘Wewe hujui tu…na…unajua akili yangu haipo sawa, nahisi kuna kitu ambacho sio cha kawaida humu ndani, huwa mimi ninakuwa na hisia kabla ya tukio…na hili limeanza pale tu nilipokorofishana na huyu kijana..maana aliondoka kwa hasira,  ndio maana hajafika mpaka muda huu..’akasema

‘Mbona alifika halafu akaondoka, kwani mlikorofishana nini tena na mtoto wako kipenzi?’ nikamuuliza

‘Unafahamu hawa vijana  wana tamaa sana, wao wakiona kitu kipo, hawajiulizi kimefika fikaje hadi hatua hiyo, hawafahamu kuwa sisi wazazi wao tumetumia miaka mingapi hadi kulifanikisha hilo, hawajui jinsi gani tulivyojijenga..unaona …’akasema.

‘Mimi hapo sikuelewi, nijuavyo mimi, wewe na huyo kijana wako mumekuwa naye bega kwa bega kwenye maendeleo yako, na kama yeye anataka jambo, basi ana haki, na nimegundua kuwa yeye ni mshauri wako muhimu sana..’nikamwambia.

‘Pamoja na hayo, kuna mambo mengi kayakuta, na sio kwamba tumeshirikiana naye, hilo ndio anakosea, yeye, mengi kayakuta, …na kwa vile nilimuona ni mtu anayefanana na mimi, ndio nikawa na mshirikisha, lakini sio kwamba, yeye ni sawa na mbia wangu, hapana…’akasema

‘Kwani tatizo lipo wapi…?’ nikauliza

‘Unajue yeye anataka mengi kwa muda mrefu, ana tamaa zaidi yangu..’akasema akiwa kasimama karibu yangu.

‘Kwani yeye anataka nini?’ nikamuuliza na akataka kuondoka, lakini akageuka na kuniangalia machine  akasema;

‘Huyu kijana analalamika, ni kwanini nimeamua kubadili mirathi, kwanini sasa hiv nimeamua kumweka mwanangu huyu mkubwa kuwa mrithi wangu wa kwanza, nay eye sasa nimemfanya kama mtu wa pili..anadai yeye ndio ana haki ya kuwa mrithi wangu kama nilivyofanya awali..

‘Mimi sielewi, …’nikasema.

‘Unajua yeye  hafahamu mawazo ya kikubwa, mimi nimtu mzima natizama mbele zaidi yake,nimefanya hayo baada ya kufikiria sana, hali imebailika, maisha yamebadilika sasa hivi mimi sio yule mtu wa jana…’akasema

‘Umetajirika au sio…?’ nikauliza

‘Ni kweli hilo siwezi kukuficha, ndio maana nimeona huyo mtoto wangu mkubwa ndiye anayeweza kuja kuendeleza kila kitu nikiwa sipo..na sio kwa vile naandika hayo ndio najitabiria kifo…mbona hayo yalikwepo toka awali, kama wakili hayo ni muhimu yawepo kwenye familia yangu…’akasema

‘Unahisi ni kwanini anaona yeye ndiye anastahiki kuwa mrithiw ako zaidi ya huyo mtoto wako mwingine aliyemkubwa…?’ nikamuuliza
Ni tamaa tu,..na mwanagu huyu hakuwa hivyo, nahis kuna kitu mama yake kambadili,..hajui kwanini mimi nimefanya hivyo…haya kaona, sasa anakuja juu, ni kwanin nimefanya hivyo, yeye hana haki ya kuingilia maisha yangu..’akasema

‘Leo hii unasema hivyo, mimi nakumbuka ulikuwa ukitamba kuwa huyo mtoto wako ni kila kitu au sio…?’ nikauliza.

‘Nimeona mbali,..unajua japo huyo kijana yupo mbali, lakini mimi nafuatilia maendeleo yake kwa karibu, ….anajitahidi sana, kielimu, na…anafaa kuwa kiongozi wa hii wa familia..na ukumbuke huyo ndiye mtoto wangu wa ndani ya ndoa, unaona eeh, ...’akasema

‘Lakini kihalali, …hata ingelikuwa mimi ningedai hivyo hivyo, kwasababu huyo kaka yao yupo nje, hajui chochote kinachoendelea hapa, na nakumbuka uliwahi kuniambia huyo mtoto wako wa huko Ulaya hampatani kabisa, hakujali…, na aliondoka na kukuambia hana haja na mali yako ..sasa kwanini unajipendekeza kwake....?’ nikamuuliza

‘Wewe hujui mambo ya wazazi na watoto, hata kama mtoto hampatani kwasababu kadhaa, lakini yeye atabakia kuwa mtoto wangu wa kwanza, na yeye nilimzaa na mke wangu wa ndoa, ana haki zote itakuwa sio halali kumfanyia hivyo, niliandika awali ile mirathi kwa hasira tu. …’akasema

‘Na huyu je…mbona ndiye anakutumikia kwa kila hali…?’ nikamuuliza

‘Huyu niliye naye hapa nimemzaa kwenye nyumba ndogo,..nilimsomesha na kumuandikisha kama watoto wangu wengine, na nimeona anastahili kuwa karibu na mimi,  na ndio maana nimemuweka nafasi ya pili, atakuwa chini ya huyo kaka yao anayeishi huko Ulaya, kuna tatizo gani hapo....’akasema.

‘Kwahiyo wewe na mtoto wako mkaishia wapi?’nikamuuliza

‘Yeye alikuja na mipango yake, uone jinsi mtoto huyu alivyo balaa, kakaa sijui na mama yake, wakapanga mambo mengi tu, jinsi ya kugawanya mali  eti keshaandaa na mikataba ya kifamilia, kama vile mimi ninakufa karibuni, kwenye mikatba hiyo, ambayo ni kama urithi, , ...na yeye awe ni mrithi wangu , yaani kiongozi wa familia,..’akasema kwa hasira

‘Wanataka mimi nife au sio..si ndio maana yake hawa watu hawana akili kabisa…, nimemwambia huo uchuro siutaki, kama ni mikataba ya urithi, mimi nimeshaupanga na ninafahamu ni nani awe kiongozi wa familia, kama mimi nikifa..lakini sijafa, na sitaraji kufa leo...siumwi,, sina tatizo la kiafya..kwanini anakuja na mipango hiyo, wana matatizo sana hawa watu....’akasema akijiangalia.

‘Lakini  kufa sio lazima uumwe, wewe kama ulivyo, kutokana na mambo yako unayoyafanya,una maadui kila kona, wakija kuku-ua watu, hata hivyo kuandika mirathi, sio lazima mtu afe, ni katika kuwekana sawa kimajukumu au sio..vyovyote iwavyo ni muhimu kila mwanafamilia afahamu nafasi yake au sio....’nikasema

‘Kweli hilo ni la kuangalia sana,..nahisi maadui wananitafuta… ndio maana umeme ulipozimika, nimeshituka sana, sitaki uzembe huu utokee tena, ...unanisikia, ....sasa nisikilize kwa makini, kesho huyu mpenzi wako anakuja, nilishakumbia hilo, au umesahau au uliona naongea tu, tafadhali kwenye kazi iwe ni kazi tu ...’akasema

‘Mpenzi wangu gani, mimi ni mke wa mtu.?’ Nikamuuliza

‘Hebu acha utoto, nikisema mpenzi unanielewa ni nani, ..nimeshamweka sawa anakuja kuweka sahihi yake kwenye hiyo mikataba ambayo itanifanya mimi, niwe na haki ya kumiliki kila kitu…’akasema

‘Mhh..’nikaguna tu.

‘Nilishawaelezea hilo..sio nafanya hivyo kwa kupenda,..amelipa mdeni yangu kupitia kwenye hisa zake..ni halali kabisa,…kwahiyo wewe na wenzako mlitambue hilo, ...na tatizo ni huyu mtoto wangu anakuja na sera zake za ajabu ajabu, anataka na yeye awe na hisa,...anataka kunikorofisha, haya mambo hayajakaa sawa, keshaanza kugombea mali, ni uchuro huu…I don’t like this...’akasema kwa hasira

‘Mimi ninawashangaa kweli kweli, yaani mumeshaanza kugombea mali za watu, hata kabla hamjazipata, mumeshaanza kumiliki hata kabla humajamilikishwa, kweli akili zenu wote ni za  kishetani wewe na mtoto wako,  na mimi nahisi hamtafanikiwa kwa hilo, na mkifanikiwa mtakuja kupigana baba na mtoto wake, hiyo ni hatari....’nikasema

‘Kama mimi nipo hai, hakuna cha mtoto wala mama yao atakayeweza kunitawala, mimi, unasikia…mimi  ndiye mwenye amri ya mwisho.., wote wanalifahamu hilo, najua kabisa huyo mtoto anaendeshwa na mama yake, na mama yake nilishamwambia simtambui tena, tulishamalizana mimi na yeye…’akasema

‘Kazi unayo, mali ya dhuluma kamwe haiwi na amani, nakuambia ukweli..’nikasema

‘Sikiliza,..usitake kunifanya mimi ni mdhalimu, nimemdhulumu nani hapa, umeona mwenyewe sera zangu, na nimejaribu kukuelimisha dhamira yangu, umeona jinsi gani ninavyoitumikia jamii…na hili la mpenzi wako, ni lazima lifanyike, ili na mimi niweze kuendelea kuwa juu…wakubwa huko wananisakama…’akasema

‘Wakubwa gani..?’ nikauliza

‘Sitaki niyaongee haya mara kwa mara, wewe unafahamu ni nani nawaongelea, sasa …huyo mtoto natakiwa nimuweke sawa, aacha upuzi wa kumsikiliza mama yake, mama yake hana nafasi kwangu, na zaidi mimi na mama yake...hatukuwahi kufunga ndoa naye…yeye alikuwa mpenzi wangu wa kupita tu, nikampa mimba ndio akapatikana huyo kichaa.’akasema kwa  hasira.

‘Aaah, kumbe, una wangi sana, kazi yako ni kuzalisha tu, huyo alikuwa mpenzi wako wa zamani, nahisi wapo wengi wa namna hiyo, huyo wakati huo ulimuona mpenzi, sasa hafai, au ni kwa vile kazeeka,au?’nikamuuliza

‘Namfahamu sana huyo mwanamke, ana tamaa sana, hatuivani kabisa, na mtoto wake kachukua tabia zake zote, na kama ataendelea na hiyo tabia sizani kama tutaivana, na...namuona atakuwa  kikwazo katika mipangilio yangu ya kimaisha kinyume na nilivyotarajia, kabadilika kabisa, hajui mipangilio yangu mingine..ni lazima niwe makini sana...’ akatikisa kichwa kusikitika halafu akaendelea kusema;

‘Sawa mimi nakushauri hivi, kwa hali ilivyo ni bora make muongee mkubaliane au sio, yeye ndio kama mlinzi wako au sio…yupo nawe wakati wote,..’nikasema

‘Ni kweli unayoyaongea,..mimi najiuliza tu ni kwanini siku hizi  hanisikilizi mimi, na anakuwa akimsikiliza sana mama yake, ujue huyu mtoto mimi ndiye nimefundisha ujanja wa kimaisha , alipomaliza kisomo chake akataka kufanya kama alivyosoma, nikamwambia dunia hii, ina utaratibu, lakini ndani ya hizo taratibu kuna njia za mikato,..unaona eeh..’akasema

‘Kumbe ni wewe ulimuharibu…’nikasema

‘Sio kumuharibu,..hivi niambie kiukweli kwenye hali za maisha yetu kuna mtu anaweza kuinuka akawa tajir bila kufanya magendo,…sasa ni lazima nimfundish, ujanja wa dunia hii…ukijifanya unasubiria mshahara tu, utakufa masikini..ndio hivyo nikamuelekeza jinsi gani ya kuishi, kaiva sasa ananigeuka…’akasema

‘Ndio maana nawaambia dhuluma itawaandama hadi kaburini…’nikasema

‘Mhh..na wewe bwana, mbona hunielewi,…kwa namna nyingine upo sahihi, kuwa kuna kitu kama hicho, lakini tufanyeje sasa, wakati wakubwa wameamua kujitajirisha wao wenyewe, angalia hizi foleni za magari,  makodi mengi yasiyomjali mtu wa chini, ..utafanaje kazi namna hii, angalia tatizo la umeme, kweli unaweza kuwekeza hivi, wao wakitaka kupita njia zinasafishwa, kwao umeme haukatiki…utafanyeje…’akasema

‘Ni hayo tu…?’ nikauliza

‘Natolea mfano kidogo kuwa ili ufanikiwe katika nchi yetu, huna budi kupita njia za mkato, ukitaka njia sahihi utaumia, kuna watu wanakuwa ni vikwanzo..hebu anza kufuatilia hati za kiwanja uone…au ..mifano ipo mingi… utasubirishwa wee..kumbe ni namna tu inatakiwa, bado sana….kwahiyo ilibid nimfundishe kijana aelimike…’akasema

Na sio hilo kazi..siku hizi watu binafsi, ukifanya kwao, eeh,…ujue utanyonywa kupitiliza, usipo kuwa mjanja utaishia kuwa masikini…umeonaeeh,…haki nyingi za mfanyakazi wanazikwepa, chunguza sana hili utaliona, sasa mimi kama Makabrsha nataka hawa watu niwakomoe kihivyo, nyie hamjui tu…’akasema

‘Hutafanikiwa, …maana unatumia njia hiyo kujitajirisha huku ukitafuta visingizio, hujui kiasi gani unawaumiza watu,….maana unatutumia sisi watu wa chini kwa ajili ya visasi vyako kwa watu wa juu…’nikasema

‘Naona wewe hutanielewa, ni kwanini lakini…nilitaka wewe unielewe ili umsaidia huyu kijana, umuelemishe ili tufanye kazi pamoja, wewe uwe mtu wangu wa karibu pia..’akasema.

‘Tatizo wote wawili hamuaminiki, mtoto kama baba yake...au kama wanavyosema  mtoto wa nyoka ni nyoka..’nikasema kwa dharau huku nikijifanya kutabasamu .

‘Huyo haniwezi kabisa na hataweza kunifikia mimi, yeye anachukulia mambo kwa pupa, mimi natumia ujanja, hekima na akili, ndio maana unaona nimefanikiwa kwa kiasi hiki kikubwa, unaona jumba hili, ni nani anaweza kujua nimelijenga mimi kwa vipi,..ni akili, ..usione watu wana majumba, utajiri, ukfikiria ni kirahisi hivyo…’akasema sasa akiangalia juu.

‘Dhuluma tu hiyo..’nikasema

‘Sio dhuluma jamani, nielewe…, ni kutumia akili, na ujanja, lakini dhumuni kubwa ni kuwasaidia wanyonge, humu nimewekeza, angalia ajira kiasi gani nimezifufua hapa, unakula, na huku unasaidia, siwezi kusahau dhumuni langu, hapa nina mpango wa kuwajengea wazee sehemu yao,…ambapo wataweza kuwekeza, kila mtu na ujuzi wake, ngoja haya mambo yawe safi, wewe utaona tu..’akasema.

‘Kwahiyo yote hayo umemfundisha mtoto wako?’ nikamuuliza

‘Tatizo yeye hataki kutuliza kichwa, yeye anataka mambo kwa pupa, ana tamaa za haraka, hata sijui kwanini ameweza kufaulu masomo yake ya uanasheria, kazi hii hataiweza kama atakuwa na tabia ya namna hiyo, ya pupa, na ninavyomuona hatafika mbali..’akasema

‘Mhh..haya bwana..’nikasema

‘Sio nataka wewe unielewe, ili mkikaa kuongea umuelimishe…, hebu angalia, anataka kunirithi nikiwa hai...sijui kwa hali kama hiyo, tunaweza kukaa pamoja,....lakini mimi kama baba, nitamdhibiti tu, nimeshamfahamu vyema anakotaka kwenda, sasa ataona vipi baba livyo mjanja, haniwezi kabisa...’akasema.

Na mara simu yake ikalia, akaipokea bila kuiangalia, na mara akakunja sura ya uso wake na kuonekana kukasirika, akasema kwa sauti ya juu ya hasira;

‘Kwanini unasema hutafika leo, wakati unafahamu umuhimu wa wewe kuwepo leo, nataka uje hapa haraka,...kwanza kuna matatizo kwenye mitambo ya usalama, na pia ni wajibu wako kuwepo hapa, ili tukamilishe kazi , achana na tamaa zako hizo, nasema mimi kama baba yako uje hapa haraka,.....’akasema

‘Unasema nini, unanijibu mimi hivyo, kuwa hutafika,mpaka nikubaliane na matakwa yako, ina maana unanilazimisha kufanya unavyotaka wewe, hivi unaelewa unaongea na nani...unasema nini, ina maana umeshaota mapembe sasa eeh,...’akawa anaongea huku mwenzako naye anaongea, maana sauti ya huko nilikuwa naisikia, wakazozana hapo mwishowe akasema;

‘Sikiliza wewe mtoto, kama nimekuzaa mimi, utakuja hapa, kama una baba yako mwingine usije , usijione kuwa umekuwa sasa,...na kujiona hunihitaji tena,  hujui ninaweza kukufanya lolote ukasahaulika katika hii dunia..’akasema na kusikiliza simu kwa muda halafu akaibamiza simu chini , na simu hiyo ikapasuka vipande vipande, na kusema;

‘Mwanaharamu mkubwa wewe...tutaona,....’akageuka na kuelekea ofisini kwake, ukumbuke hapo tulikuwa tunaongea kwenye varanda, nilipokutana naye wakati natoka huko kufanya mambo yangu,..hapo mimi nikachekelea kimoyo moyo, nikisema ‘mipango inakwenda sawia…’ ukitaka kumshinda adui , wagawanye, wasiwe na masikilizano..utwashinda kirahis sana..mimi huyoi nikurudi chumbani kwangu, sikutaka kumfuata huko ofisini kwake, kwani nilijua kwa hali aliyonayo hatutaweza kusikilizana.

Mimi kwa hali kama hiyo , ilikuwa kama vita vya kunguru, faraja kwangu, nilitaka watu hawa wawili wawe hivyo, ili mipango yangu iweze kufanikiwa,..na kimoyomoyo nikijua sasa sehemu muhimu imekamilika…

Mpaka hapo nilijipa moyo hivyo, hata hivyo, sikuwa nimeamini kabisa kuwa huyo mtoto wa marehemu hatafika, namfahamu sana, yeye na baba yake hawaeleweki, wao ni waarabu wa pemba, wanajua sana, utaona wamegombana hivyo baadae kidogo wapo pamoja wanajadili mambo yao,…kwahiyo nikachukua tahadhari,..

Nilikwenda kuongea na mlinzi mmoja ninayemuamini , nikamwambia , kama huyo mtoto wa bosi akija , anipigie simu kwa haraka,...kwani sehemu kubwa ya mitambo ya kunasa matukio ilikuwa haichukui picha, kwahiyo ningeliweza kufanya lolote bila kujulikana, kwa kiasi fulani nilikuwa na amani kidogo, nikasuburia muda muafaka, wa kumalizia kazi ambayo nilishaianza.

Nilikuwa najiamini maana sasa nina silaha, na nikiwa tayari , au nikisikia kuwa huyo jamaa kafika nitakwenda kuichukua, sikuwa na haraka nayo sana, nikatembea kuelekea  ofisi ya siri ya Makabrasha, nikafungua, na kulitafuta kabati maalumu anapoweka nyaraka zake, nikachukua kile ninachokihitajia, na kurudi chumbani kwangu.

Kabla sijafika huko nikakumbuka kazi nyingine ya kufanya, kwani siku hiyo niliipanga iwe siku ya mwisho ya kukaa kwenye hilo jengo, nikaelekea sehemu ninapoweka vitu vyangu muhimu ambavyo nimevihifadhi mbali na chumba changu, sikutaka waje wavikute chumbani kwangu, kama ikitokea kuvitafuta, nikaviweka sawa, halafu nikarudi chumbani kwangu,sasa nikijiandaa kwenda kuichukua silaha yangu, sikutaka iwe mbali na mimi na wakati nafika chumbani kwangu, simu yangu ikaita, alikuwa mtoto wa Makabrasha,

‘Unasemaje?’ nikamuuliza kwa sauti isiyotaka kuongea,

‘Samahani sitaweza kufika kwenye shule niliyokuahidi, lakini ombi langu lipo palepale,na kwanini mitambo hapo haifanyi kazi,  ...umeingia tena humo ndani?’akasema na kuniuliza

‘Umesema hutakuja, ina maana mkataba huo umekufa, labda useme kuna jingine..na kuhusu swala la mitambo hayo unayafahamu wewe, wewe ndio mtaalamu, huenda ulifanya hivyo makusdi kumuonyesha baba yako kuwa wewe ni zaidi au sio..?’nikasema kama namuuliza

‘Wewe nimeshakufahamu, wewe unajifanya ni mjanja, lakini ujue kuna wajanja zaidi yako, kuna kazi naifanya ikimalizika nitaangalia, kama nitakuja au la, ..lakini kwa vile hatujaafikiana na mzee ninaweza nisifike, na kama nikifika, nitahitaji maelezo ya kina kwanini umezima mitambo, na kwasasa siwezi kuona chochote kinachoendelea hapo, utakuwa ni wewe tu...na hilo litakufanya utimize ombi langu, la sivyo, mimi nitakuumbua kwa mzee ...’akasema

‘Una uhakika gani na hilo..na je nikimuambia mzee wewe unanitongoza,..nia ushahid hujui kila nikiongea na wewe nakureodi kwenye simu…hahaha, mimi ni mjanja kama wewe…au nimuambie?’ nikamuuliza

‘Utaona....mimi huwa sichezewi, mimi ni mtaalamu, nafahamu sana hiyo mitambo, na kawaida yangu, nikitaka jambo ni lazima nilipate, muulize baba atakuambia, ndio maana nipo naye karibu, ananifahamu sana,…’akasema

‘Mbona sasa kampa urithi kaka yako, ina maana wewe hufai, huna akili iliyotulia, sema wewe una tamaa, utawazaje mambo ya urithi wakati baba yako yupop hai, mna mipango gani wewe na mama yako…’nikasema

‘Nini..nimekuambia nini wewe…’akasema kwa hasira

Nakuulize wewe, maana baba yako kakasirika, sijawahi kumuona akiwa na hasira kiasi hiki, nisikilize mimi, pamoja na yote mzazi ni mzazi kumbuka ulipotoka..’nikasema kama kuuma na kupuliza.

‘Wewe hutujui…na kwa hili ni lazima nipiganie haki zangu, mfano tu, je mzee kama hayupo, unafikiri huyo kaka yangu atanijali,..yeye na mimi hatuivani kabisa,… je huyo kaka yangu anafahamu wapi tulipotokea, ni kwanini tumefika hapa tulipo, sema ukweli wako,..’akasema na kukatiza nahisi alikuwa akiongea namtumwingine.

‘Sasa…eeh ukiangalia hiyo mikataba aliyotayarisha baba, yeye kanisahau mimi nimejaribu kumtayarishia mikataba mizuri tu, nikimkumbushia wapi tulipotoka, yeye anakimbilia kumuingiza mama kwenye mazungumzo yetu.., eti mama ndiye  ananiharibu…’akatulia kuna sauti ilikuwa kama inamsumbua.

‘Unajua nikuambie kitu , mama yangu masikini ana nini na yeye, alimpachika mimba yangu eeh, akamtelekeza, mama kaishi maisha magumu hadi anajifungua mimi…siwezi kusikia vizuri mtu akimuongelea vibaya, huyu ni mama yangu na mama yangu ni kila kitu kwangu,…sitajali ni nani, kama mtu anataka kuwa asui yangu amuongelee mama yangu vibaya,..sipendi…najua yeye ni baba yangu namuheshimu kwa hilo, lakini pia awe akinisikiliza na mimi,..’akasema lakini akawa kama anakatiza.

‘Ni nani huyo mpo naye, ni Malaya zako nini…?’ nikauliza

‘Hahaha…acha hayo, sio kweli…’akasema, na nikasikia akiongea na mtu, baadae akasema;

‘Sory, nipo na mtu karibu, ….sio kama unavyofikiria wewe…’akasema

 ‘Hahaha..mtoto kama baba, umalaya, na sasa mnagombea mali ya dhuluma eeh, nina uhakika kuwa dhuluma hiyo itawapeleka pabaya...na mwisho wake umeshafika, ..wewe njoo nakusubiri kwa hamu..’nikasema

‘Nini…!!1,…ina maana kweli unanitaka eeh, unasikia sikutaka kuja huko, lakini kama kweli utanitimizia ombi langu, mimi naweza kuja kwa ajili yako tu, sio kwa…na sikiliza kama unataka nije kwa ajili ya kupambana na wewe..hilo mimi hunitishi, sikiliza nina uhakika ni wewe umezima hiyo mitambo, sasa..ngoja tuone,….’akasema tamaa zake za mwili akazitanguliza mbele, na alipogundua kuwa mimi nina maana gani ndio akasema hivyo.

‘Ni hivi  baba yako ameshakushitukia, kuwa wewe unanitaka na mimi, pili wewe una tamaa, na tatu, hufai kwenye uongozi wa familia, kwahiyo kuanzia sasa ujue wewe huna chako ....’nikasema

‘Nini,..haa, unasema nini, tutaona…’ akasema sasa kwa hasira, nikasikia sauti ya kike ikisema;

 ‘Kuwa makini…’

‘Ndio hivyo…sasa uje usije, huna maana kwake kwa sasa…’nikasema na mara  nikasikia akikata simu kwa hasira huku akisonya.

NB: Je huyo jamaa alifika?  na kama alifika kulitokea nini na je ombi lake lilitimizwa,ni nini kitatokea kwa Makarasha, tuonane kwenye sehemu ijayo ya shahdii huyu muhimu aliyekuwa karibu na Makabrsha..ambaye ni marehemu!


WAZO LA LEO:Tuwe makini na malezi ya watoto wetu, kama tunafanya shughuli zisizo na manufaa kwa watoto wetu kwa maisha yao ya badaye, ni bora tusiwahusishe. Tuwajengee watoto wetu misingi mema ya maisha yao ya baadaye, tukikwepa makosa tuliyoyafanya, ili wao waweze kuishi maisha bora, na kujenga kizazi bora cha baadaye.


Ni mimi: emu-three

No comments :