Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 19, 2018

MKUKU KWA NGURUWE-83‘Ni wakili mmoja hivi wa kujiegemea,..sio muhimu kumfahamu jina lake kwa sasa…’akasema

‘Kwangu ni muhimu sana…’nikasema

‘Unajua cha muhimu  ni wewe kukubaliana nami, halafu mengine niachie mimi, maana hili janga bila mimi kushirikiana nawe, halitaweza kufanikiwa, na ujue lolote baya likitokea halitaniathiri mimi tu,…’akasema

‘Kwanza nikuambie kitu, siogopi majanga, hayo ni sehemu ya maisha yangu, sawa naweza kukubaliana na wewe kwa vile kuna huyo mdudu mtu kaingilia maisha yangu, na mimi hilo ni changamoto, …nataka kumfahamu huyo mtu ni nani..’nikasema

‘Ndio hapo nikaona tushirikiane, ili tuweze kumnasa huyo mtu…’akasema

‘Achana na huyo mtu, mimi nataka kumfahamu huyo wakili ambaye yupo tayari kukusaidia ni nani…?’ akauliza

‘Sijakubaliana naye baddo kwahiyo siwezi kukuambia…’akasema

‘Ok, kama hutaki kuniambia tuachane tu, ondoka zako…’nikamwambia

‘Sikiliza nitakuuambia nikirudi huko nilipoitwa, nina uhakika , haya mambo yalivyo, yanahitajia mtu kama yeye, yeye huo ni uwanja wake, hutaweza kumchukua wakili wa aina nyingine akakubaliana na sisi, na kwa hili, hatutakiwi kwenda polisi, unaona eeh, maana ukifanya hivyo, nyuma yake utakutana na waandishi wa habari..’akasema

‘Ok, so unataka mimi nifanye nini…?’ nikamuuliza

‘Kwanza unakubaliana na mimi kuwa kuanzia sasa hili la mtoto iwe siri, hakuna wa kufahamu baba wa mtoto ni nani, na rafiki yako asijue hili kabisa ..unanielewa hapo, maana akifahamu hilo, sio mimi tu, hata wewe utakuwa umejiharibia…’akasema

‘Sawa…hilo halina shida, tangia mwanzo hili nilitaka liwe langu tu, tatizo ni huyo kidudu mtu, na nakuonya, kama wewe upo nyuma ya hilo jambo, utanitambua mimi ni nani, unanifahamu sio…’akasema

‘Kwanini huniamini…nisingelipoteza muda wangu kuja hapa kwako,…sasa ngoja mimi niende, nikaonane na huyo mtu, nikitoka kwake nitakuja kukufahamisha  ni nini tulichoongea naye ,sawa ilimradi wewe umeshakubaliana na mimi ..’akasema akitaka kuondoka

‘Pamoja na hayo, sitaki uwe unakuja hapa kwangu, pili..tusizoeane kihivyo, mimi sio mpenzi wako na haitatokea kuwa hivyo, maana tangia awali sijataka mahusiano na wewe, wewe ni mke wa mtu,..na kwa hili imetokea bahati mbaya, na tatu, msimamo wangu ni ule ule, huyu mtoto ni wangu peke yangu, hana baba…’akasema

‘Usiseme hivyo kuwa hana baba,..hata hivyo, hayo tutakuja kuongea, kwasasa sio ya muhimu, tusianze kugombea mtoto, au sio…umenielewa hapo, muhimu ni kuona jinsi gani ya kulikwepa hili, hivi wewe huoni hatari iliyopo mbele yetu…naogopa sana mkwe wangu akija kulifuatili,a yule mtu ni hatari, …’akasema na kuanza kuondoka.

Na alipoondoka tu, simu yangu ikaita, alikuwa ni rafiki yangu anasema yupo njiani kuja kuniona, hapo nilihisi mwili ukinicheza, maana kuja kwake nilishamuahidi kuwa nitamuambia kila kitu, lakini kutokana na haya yanayoendelea sizani kama nitaweza kumuambia.

‘Nduguzanguni,  …naongea haya ili muone kipindi hicho jinsi nilivyokuwa na wakati mgumu , mnaponilaumu kwanini sikusema mapema, baada ya tukio hili, yaonekana kabda mimi nilifanya makusudi,..hapana kulikuwa na changamoto zake.

‘Na pia naomba mnivumilie kwa mahojiaono yatakayo kuja kuendelea baadae nia ni kuja kuwafichulia kile kilichokuwa kimejificha ndani yake, hili tukio sio rahisi kma lilivyo, kuna mambo yamepangwa,..na huenda hata wahusika wengine hawalifahamu hilo..’akasema bila kuonyesha hao wahusika wengine ni nani.

*********

Baadae alikuja rafiki yangu tukawa tunaongea na hoja yake ikawa ile ile ya kutaka kufahamu ni nani baba wa mtoto wangu, sikuweza kumwambia, nikijua kuwa kuna huyo mdudu mtu, ni lazima nimpate, pili, ni hali halisi ambayo, nahis nikimuambia rafiki yangu ndio urafiki utakufa kabisa,  na kwahiyo sitaweza hata kwenda kusoma kabisa.

Sasa wakati rafiki yangu yupo hapo, simu yangu ikaingia ujumbe wa maneno, na nilipoangalia, kabla sijaufungua nikahisi ni hao watu, kwa jinsi ujumbe wenyewe ulivyokuwa kuwa kuna kitu kimebebeshwa kwenye huo ujumbe na ni picha au video…sikuweza kuisoma ile simu nikapotezea.

‘Mbona huangalii , nahisi kuna ujumbe umetumiwa, akaniambia rafiki yangu, na kwa haraka nikaufungua huo ujumbe, maelezo, kidogo tu, halafu, fungua hizo picha kama ushahidi, nikafungua, mamamamah!….nilitamani niirushe hiyo simu chini, nilibadilika kwa haraka, lakini akili ikanicheza, kwa haraka pale nikasimama kupotezea, nikasema;

‘Vipi kuna nini…?’ akauliza rafiki yangu

‘Mhh..kuna mtu ana mzigo wangu kasema niende sasa hivi, ni mzigo muhimu sana, na muda umeshapita,… samahani dada, sio nakufukuza, ila ni muhimu niende..’nikasema

‘Na mtoto…?’ akaniuliza

‘Usijali, nipo na ndugu yangu hapa, …’nikasema na rafiki yangu akanielewa akaondoka, na alipondoka nilishukuru mungu, maana nilichotumiwa kwenye simu, kilitaka nipoteze fahamu, ni picha zile zile, lakini hii ilikaa vibaya zaidi..kwanza sikuifuta kwa haraka, nikampigia mtu mmoja wa studio, ili anisaidie, nikamuelezea kuwa kuna mtu ananichezea je unaweza kugundua kuwa picha hii ni kweli au ya kutengeneza

‘Akasema anaweza…na sikupoteza muda nikaenda kwake, akaichunguza akasema picha hiyo ni ya kweli na imechukuliwa kwenye kamera za kujificha, haina shaka,..

‘Unaweza kugundua ni kamera za namna gani ..?’ akasema

‘Hii ni mitambo ya kisasa, inaweza ikawekwa sehemu yoyote, ikachukua matukio, ni kidude kidogo tu, …’akasema

‘Nawezeje kugunduaje kama bado kipo ndani ya nyumba yangu..?’ nikamuuliza

Akanielekeza jinsi gani ya kukigundua kwa kutumia simu yangu tu ya mkononi, akaniwekea program fulani kwenye simu yangu, ambayo itanisaidia kugundua hicho kifaa, basi nikarudi nyumbani, nikajaribu kufanya kama alivyonielekeza, lakini sikuweza kukigundua hicho kifaa, ina maana kilishaondolewa.

‘Sasa ni nani huyu mtu…’nikajiuliza na kabla sijapata jibu mara simu yangu ikaita, kuangalia nikagundua kuwa ni mume wa familia,

‘Unasemaje…?’ nikamuuliza nikiwa naona kama ananipotezea muda tu

‘Umetumiwa ujumbe wowote..?’ akaniuliza na hapo nikashtuka, yeye kajuaje hilo, nikasema hivi tu

‘Na nani…?’ nikauliza

‘Mimi nimetumiwa ujumbe hapa wenye picha, wakasema na wewe wamekutumia, unaona hizo picha zilivyo, wanataka tuwalipe pesa nyingi, na mimi sina pesa za kutosha, tufanyeje..?’ akaniuliza
‘Ni nani hao…?’ nikamuuliza

‘Hawajajulikana bado…’akasema

‘Kwahiyo unaniambia mmi nifanye nini, mimi sina pesa, unafahamu fika mimi  namtegemea mke wako, anilipe mshahara na kazi hiyo ya ajira pesa yake ndio kiduchi hata sisemi ni kiasi gani…’nikasema

‘Sikiliza mwambie rafiki yako umekwama, una tatizo kubwa sana, kama anaweza akukopeshe milioni kumi hivi…’akasema

‘Milioni kumi!!.Wewe una wazimu kweli mimi sio kama wewe unayemiliki kampuni pesa kama hiyo kwako ni ndogo au sio…, kwangu mimi ni pesa nyingi sana.siwezi kufanya kitu kama hicho, hata rafiki yangu atanishitukia..’nikasema

‘Umesoma huo ujumbe kwenye hizo picha, ulivyosema..?’ akaniuliza

‘Mimi sijali, wafanye watakavyo, mimi sina hizo pesa…siwezi kujiingiza kwenye mtego kama huo…’nikasema ila kiukweli moyoni nilikuwa na wakati mgumu, yaonekana huyo mtu alishajipanga, na sio rahisi kumnasa kwa njia rahisi, iliyobakia ni kushirikiana na huyo huyo mume mtu.

‘Kwenye hizo picha kweli kulikuwa na ujumbe wa vitisho, uliandikwa hivi;  je unataka kwenda kusoma, je unataka urafiki wako na rafiki yako udumu, je rafiki yako akiziona hizi picha utafanikiwa hayo…tutawasiliana nawe baadae..’’ wakamaliza hivyo

‘Ninakuja kwako nataka kukuelezea nilichokutana nacho huko nilipokwenda…’akasema, sikuwa na ujanja, nikakubaliana naye tu . ila nikampa tahadhari kuwa asije na gari lake..

Baadae kweli alifika:

‘Unajua kuna mambo ambayo huwezi kuamini..’akasema

‘Kwanini..?’ nikamuuliza

‘Unafahamu sikuamini hata mimi,…sikutarajia unajua nilikwenda kuonana na huyo mtu, na nikafuata maagizo yake, ni kwenye mgahawa fulani hivi, mara akaja mtu, akaniambia naitwa niende sehemu nyingine humo humo, nafika nakutana na mtu ambaye sikutegeemea kukutana naye hapo…

‘Mtu gani huyo, …?’ nikamuuliza

‘Makabrasha…’akasema

‘Makabrasha anahusikanaje na hili..?’ nikamuuliza

‘Hahusiki, lakini ilikuwa ni bahati kukutana naye hapo…’akasema

‘Kwa vipi..?’ nikamuuliza

‘Kwasabau ndiye wakili niliyepanga nionane naye …’akasema

‘Wewe, ina maana huyo wakili uliyesema anafaa, ndio huyo,.. hahaha, wewe kweli huna akili , kama ndio huyo mimi simo…?’ nikamuuliza

‘Sio kuwa ni yeye anahusika, hapana, yeye anasema kaniona nikiingia akawa anataka tuongee mambo mengine nikamkatiza kuwa mimi nipo matatani, ..nilishampigia simu awali, akasema niende ofisini kwake, lakini nilimuambia hilo jambo sio la kiofisini..’akasema

‘Mjanja huyo ndio huyo huyo kakufanyia hivyo…’akasema

‘Hapana sio yeye, yeye alikuwepo hapo kwa mambo yake tu, ndio ikaabidi nimuambie, maana bado nilikuwa sijamuambia tatizo lenyewe..’akasema

‘Akasemaje sasa…?’ nikamuuliza

‘Nimpe yeye hiyo kazi ya kukutana na huyo mtu, na yeye atajua jinsi gani ya kulimaliza hilo tatizo, maana watu wote wenye kazi hizo anafahamina nao,…nikaona basi nimemaliza tatizo…’akasema

‘Ukakubali…kirahisi hivyo…?’ nikamuuliza

‘Sasa ningelifanya nini,kwa hali kama hiyo, unajua nilichofanya kweli nlikubali,nikasema sawa kama ana nia kweli ya kunisaidia anisaidie, na kama ana nia mbaya, nitamgundua tu,… sikuondoka kwa haraka.

 Nikajifanya nimeondoka pale, lakini sikuondoka nilikwenda kwenye duka moja na nikanunua nguo za haraka nikabadili na kuvaa mawani ya kuficha sura, nikarejea pale na kujificha sehemu ambayo ningeliweza kuiona ile sehemu niliyotakiwa kukutana na huyo mtu…’akasema

‘Basi kweli,…kwasababu Makabrasha alikaa sehemu ile niliyopanga nikae mimi, na huyo jamaa akaja kwenye ile meza, unajua,….. ndio maana nasema sio kweli, jamaa alipogundua kuwa aliyepo hapo ni Makabrasha…kwa haraka akasimama kuondoka,

Makabrasha akajua jinsi gani ya kumweka sawa, wakaongea na mwishoni wake nikaona wakikubaliana kwa kushikana mikono, …’akasema

‘Walikubaliana vipi…?’ nikauliza

‘Baadae Makabrasha akanipigia simu ndio akaniambia kuwa kaongea na hao watu, na wao wamekubali kuachana na hizo picha kama watapata mafaso yao, na gharama za huo mradi, wamesema mradi huo umewagharimu pesa nyingi, kwahiyo wao, kwa haraka wahitajia hisa kwenye kampuni yangu, asilimia kumi na ishirini, akashushana nao hadi kumi na tano, ndio mwisho…na pesa taslimu, milioni hamisini…’akasema

‘Mungu wangu, mbona ngumu hiyo kwanini hisa za kampuni, huoni hapo ni mtego, na watu kama hao huwezi kuingiana nao makubaliano ya hisa, watakuja kuua kampuni…’nikamwambia,

‘Ndio hapo, siwezi kwakweli, lakini sasa nifanyeje…kiukweli hapo nimechanganyikiwa, hata sijui nifanyeje…’akawa kweli anaonyesha kuchanganyikiwa, mimi sikuweza kumsaidia kwa hilo, nikasema;

‘Mimi sitaki upuuzi wenu, huyo makabrasha ndiye anakuchezea akili, wewe hujui tu, mimi hado hapo nimeshaiona hiyo picha, ni swala la kupata ushahidi tu…’nikasema

‘Sio yeye bwana, yeye hawezi kunifanyia hivyo, yeye pamoja ya kuwa ni rafiki yangu lakini pia yeye ni kama ndugu yangu tumetokea kijijini kimoja, kama angelitaka kitu kama hicho angeliniambia, na yeye mbona tunafanyiana kazi mara kwa mara ...’akasema.

‘Sasa sikiliza umeshanifahamisha hilo, sasa ankuomba, niachie hilo jambo, mimi nitafanya kivyangu, lakini kwangu hapati hata senti moja, wewe fanya ufanyavyo, wewe si una pesa, …tumia pesa zako, na hisa zako, shauri lako,..mimi nitatumia mbinu zangu, huyo mtu kaingia kubaya..’nikasema

‘Ndio maana nimekuja kwako, na nakufahamu wewe ni askari, unaweza kupambana na mtu kama huyu, kwa mbinu zako za uchunguzi na mimi nitatumia kila hali, pesa , na kila njia, ili tuweze kupata mwanya wa kumshinda huyu mtu na mambo mengine yaenda kama kawaida,...’akaniambia

‘Hili sio swala la uaskari, huu hapa ni utapeli, wa kishenzi, na mbinu kama hizi mwisho wake ni mbaya, sipendi kabisa kujiingiza huko, najua ni nini kitatokea baadaye, ...tamaa ya namna hiyo inaweza kugharimu maisha ya watu, na ukiingia huko, ukanaswa kwenye mitegi yao, kuja kujinasua itakuwa vigumu sana, ..haya baada ya hapo mkakubaliana nini?’ nikamuuliza

‘Mimi sijakubaliana naye bado, maana walichokitaka ni kikubwa sana kwangu, kwa hivi sasa kwanza sina pesa, pili kampuni ina madeni mengi, na ukumbuke baba mkwe anafuatilia kila kinachoendelea kwenye kampuni kwa vile kampuni hiyo imeanzishwa kwa mkopo wake,…..’akasema

‘Hujapanga kitu na yeye unakuja kwangu, mimi sina pesa, mimi kwa hivi sasa nipo maternity, na zaidi unajua mke wako kaniganda kama ruba, unataka mimi nifanye nini..?’ nikamuuliza

‘Nafikiri hunielewi na huniamini, nimekuambia kila kitu nimekiacha mikononi mwa huyo wakili, kaongea naye wakaja na makubaliano hayo, sasa, mimi nashindwa la kufanya,..na huyo wakili anasubiria jibu langu, nilitaka ushauri wako hapo, nifanyeje…?’ akaniuliza

‘Ushauri wangu eeeh, waambie, ‘go to hell’ unasikia, najua unafahamu kiingereza sawa sawa,….unanielewa waambie wafanye wanalotaka, mimi siwezi kukushauri jambo hapo, huwezi kuwapa hisa nyingi hivyo, bado wanataka pesa kiasi hicho, kama unazo wape..’nikasema

‘Basi, ngoja nikikutana naye tena nitajua la kufanya, huyo wakili atanisaidia tu, anafahamu njia ya kupambana na hao watu, atawafanya washuke shuke, kwa hisa sikubaliani nao kabisa…’akasema

‘Umesema kuwa uliwahi kufanyiwa hivyo, na aliyekusaidia ni huyo huyo wakili , alikusaidiaje… ?’ nikamuuliza

‘Nikuambie ukweli, yaani sasa nachanagnyikiwa, kwani siku za nyuma, kama miezi kadhaa nyuma..yawezekana mwaka sasa, sina uhakika.., nilitakiwa kumlipa binti mmoja pesa nyingi tu, baada ya vitisho vinavyofanana na hivi, sikuweza kufahamu ni nani, ila huyo binti aliniambia kuwa  huyo anayeshirikiana naye ni mtu wa usalama wa taifa...’akasema

‘Mtu wa usalama wa taifa!, hapana wewe, ulijuaje kuwa huyo mtu ni mtu wa usalama wa taifa?’ nikamuuliza

‘Ndivyo alivyoniambia hivyo huyo binti...’akasema

‘Usiwe mjinga, ni huyo huyo wakili wako anakuchezea, keshaonja asali sasa anataka kuchonga mzinga, naona hapo kuna jambo, nahisi wewe unafahamu zaidi ya hayo...je huyo binti ni nani?’ nikamuuliza

‘Mhh, ni binti mmoja muhuni tu, haina haja kumfahamu, si unajua zangu, pombe zikinitinga nakuwa sio mimi tena, ilitokea bahati mbaya tu...’akaniambia

‘Au ni yule binti wenu wa ndani mliyesema katoroka..hivi kweli ilikuwaje, sijamsikia kabisa, sio yeye kweli?’ nikamuuliza na yeye akageuka pembeni,na kukaa kimiya.

‘Sikiliza, kama unataka kushirikiana na mimi kwa hili, hunabudi kuniambia ukweli wote je huyo binti ni yule binti wenu wa ndani, na kwanini alitoroka?’ nikamuuliza.

Hapo alikaa kimia, nikahisi kuna jambo hapo na hapo naweza kugundua mambo, na huenda huo ndio mchezo wao, na sasa anataka kunitumbukiza na mimi kwenye huo mtego.

‘Sikiliza unafahamu mimi ni mpelelezi, na kwa hilo naweza kulifanyia kazi na kuligundua, ..ninaweza kumtafuta huyo binti na kuufahamu ukweli wote, sasa ili tusipoteze muda niambie ukweli kilichotokea kwa huyo binti..?’ nikamuuliza

‘Wa nini huyo binti, sitaki kabisa kumuona tena huyo binti, maana nikimuona nitamweka ndani..hata hivyo yule binti ni wa kijijini tu.., anahusikanaje na hili…’akasema

‘Una uhakika na hilo…sio yeye uliyempachika mimba ndio akaanza kudai mapesa mengi…, niambie ukweli au nianze kazi ya kuwapigia simu watu wangu,wanaomfahamu huyo bint..?’ nikamuambia

‘Unataka nikuambie nini kumuhusu yeye…?’ akauliza sasa akionyesha wasiwasi fulani. Hapo nikakumbuka kipindi fulani nilizoeana na huyo binti, ikawa mara fulani akiwa na nafasi ananitembelea, na hapo akilini mwangu ikawa inaniuliza ni nani angeliweza kufika kwangu kwa uhuru na kuweka vifaa kama hivyo, ni shuku shuku tu.

‘Kila kitu…ilitokeaje mpaka akatoroka, maana yawezekana ni yeye kaamua kukuchezea huo mchezo, ili kukukomoa, je ilitokeaje kwa huyo binti, je ndio yeye aliyesema anashikrikiana na usalama wa taifa, ..na huyo usalama wa taifa ni nani, nikipata majibu hayo nitaweza kusema neno…’nikasema

Akaa kimia kama anawaza na baadae akaanza kuongea;…

NB: Ngoja niishie hapa kwanza, maana hapa kuna maelezo marefu msichoke kwanza, lakini hapa hapa mtagundua jambo muhimu kwenye hiki kisa…


WAZO LA LEO: Dunia ya sasa ilivyo, sio vyema kumuamini kila mtu, watu wengine wanapenda kuwaingiza watu wengine kwenye biashara haramu, hasa wakishaona mtu mwingine yupo kwenye hali ngumu. Halingumu zetu, maisha magumu yetu, mitihani mbali mbali ya isiwe ni sababu ya kujitumbukiza kwenye biashara haramu, tukauza utu wetu na heshima zetu,..tukaja kuachana na familia zetu, kwa kutumbukizwa jela au kupoteza maisha,…Tuwe na subira kwani mapito hayo, kwani mitihani hiyo maisha, ni ya muda tu, muhimu ni kujaribu kutafuta njia halali za sababu ya kupata riziki na pato halali, tukumbuke baada ya dhiki hiyo, itakuja faraja.
Ni mimi: emu-three

No comments :