Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, February 22, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-85‘Sikiliza wewe si unataka tusaidiane kwa hili, kama kweli una nia hiyo, niambia huyo mpenzi wa zamani ambaye unasema mna mapenzi naye ya asili,…?’ nikamuuliza

Ilikuwa ni kama kitu kimemusa moyoni, akasimama, na taratibu akageuka kuniangalia, akasema;

‘Kamwe siwezi kukuambia ni nani, hata hivyo nimekuambia mengi ambayo sikuhitajika kukuambia, tulipatana mimi na yeye mapenzi yetu ya nyuma yawe ni siri kubwa sana,…kumuongelea hapa, ni kama kumsaliti..kwaheri…’akasema na kuondoka zake.

 Tuendelee na kisa chetu

************
 Siku zikazidi kwenda na mimi nahitajika kwenda kusoma, na hali ya hatari inazidi kuniandama, na kama nisipokuwa makini hata huko kusoma sitaweza kwenda kusoma tena, na nikikwama hilo, basi malengo yangu ya mbeleni yangelikwama kabisa.
 Kilichokuwa kikinikwaza ni kuwa  bosi wangu yaani mke wa familia, anataka nimuambie ukweli kuwa huyo mtoto nimezaa na nani, nahisi kuna kitu kilikuwa kinamsukuma hivyo, huenda, ameshanishuku.

Siku rafiki yangu ananitamkia kuwa siku akimgundua mtu anayetembea na mume wake atamkamatisha kwa wale wahuni hatajali kuwa ni ndugu yake au ni rafiki yake ndio siku aliyofunga kauli yangu ya kumuambia ukweli, …hapo nikaomba zoezi la kwenda kusoma lifanyika kwa haraka.Nilichofanya ni kuongea na wale watu wanaosimamia mchakato huo mnzima wa masomo yangu ili uwe tayari iwezekanavyo. Ilikuwa ni kazi rahisi kwangu.

‘Ninachoshukuru, pamoja na yote hayo , mke wa familia hakuwa akilifuatilia hilo, ilikuwa kama kalisahau, kwahiyo mipango yangu ya kusoma ikawa inakwenda vyema, japokuwa sikuwa na amani,…na nilishukuru mungu kuwa muda ulipofika tu, nikaondoka kwenda kusoma.

Sasa kabla sijaondoka, nilitaka nifanye mambo fulani ya kuniweka kwenye amani, kwanza kuna huyo mdudu mtu, ambaye alishaingilia maisha yangu, sikutaka hili la picha liishe hivi hivi, japokuwa mume wa familia alishasema kazi hiyo keshampatia Makabrasha, lakini ni nani huyu Makabrasha,..ni mtu asiyeaminika!

Ukumbuke kabla sijaondoka, rafiki yangu au bosi wangu, mke wa familia aliwahi kunipatia kazi, kuwa nimtafuta mtu anayemzuzua mume wake, kwani kasikia kuwa mume wangu ana mwanamke, ambaye anamfanya asiwe na amani, ..na anasikia kuwa huyo mwanamke kazaa na mume wake…sasa hiyo kazi nilitakiwa nimpatie mume wa familia kwa haraka.

‘Atakuwa ni huyo mpenzi wake wa asili…’ niliweka mikakati ya hivyo, ndio maana nilitaka kumfahmu huyo mpenzi wa asili wa mume wa familia, nilijua nikimfahamu tu, mizigo yote ataibeba yeye, tatizo ni hilo, la kuwa kazee na yeye, je kama hana mtoto,..lakini muhimu ni kumfahamu huyu mtu ..maana asipopatikana yeye, basi huyo mwanamke atakuwa ni  mimi..’nilijisemea hivyo.

Mikakati ya kwanza na muhimu kumpata huyo mpenzi wa asili,..mikakati ya pili, kumpata huyo mdudu mtu, hapokuwa kwa akili yangu ya haraka, nilishaanza kumshuku huyo Makabrasha

 Hapo nilikuwa na siku moja ya kuyafanikisha hayo, sio kazi rahisi, nikaona kwa vile mikakati ya safari imeshakamilika, hiyo hakuna wa kuzuia tena, labda mdada, bosi wangu kama angeliamua, kufanya hivyo, angeliweza, lakini ingemchukua muda,…
 Usiku huo nikapanga jambo,  ...
 Usiku huo, nikawaza sana, na hatimaye nikaona haina budi, ni lazima nimpate mtu, ninayemuamini, nikaanza kuwachuja rafiki zangu ninaowatumia kwenye kazi zangu, nikagundua kuwa kuna mtu wangu mmoja wa karibu sana ambaye nikimpa hiyo kazi anaweza kuifanya bila matatizo.

Tatizo la huyo mtu wangu wa karibu, yeye, kikazi ni mtu kivuli, huwezi kufahamu kabisa kuwa anafanya kazi na mimi,  napenda sana kumpa kazi huyu mdada, nilishafanya kazi naye za siri, alitokea kuipenda hiyo kazi, lakini alikwama kusonga mbele, mimi nikamuwezesha kisiri, ..na kiukweli huwezi kujua kabisa kuwa huyu mtu anafanya kazi hizo, kabisa,…tatizo yeye alishaniambia kuwa hataki tena hizo kazi,…

‘Mimi hizi kazi sitaki tena, nataka kutuliza maisha yangu na familia yangu, sitaki kujipa presha…’siku moja aliniambia hivyo.

‘Lakini kazi ninazokupatia ni zile ambazo, huwezi kujulikana kabisa, muhimu iwe hivyo hivyo, siri ndio ufunguo wa kufanikisha hilo, usije kulogwa kumuambia mtu kuwa uanafanya hizo kazi, unasikia, sasa niambie ni kwanini unaogopa kuendelea kuzifanya, ina maana juhudi zangu hadi kukusomesha hazina maana tena..?’ nikamuuliza

‘Nina maana yangu kubwa, na sitaki mtu afahamu hilo, hata wewe, haya nayafanya kwa ajili ya maisha yangu ya baadae, mimi nataka kuwa mke wa familia muadilifu, na hili litakuwa linavunja uaminifu wngu kwa mume wangu…’akasema

‘Sio bosi wangu kakushauri uache kazi hizi au sio , kwa vile bosi wangu keshaanza kunichukia mimi..,?’ nikamuuliza

‘Hapana , wala mimi sina ukaribu naye, unajua kazi zetu zilivyo, sizani kama yeye anafahamu kuwa nafanya kazi kama hizo, ukumbuke hili ulinionya wewe mwenyewe, na ndivyo nilivyo, …’akasema na kweli nilimuamini.

Unapofanya kazi kama zangu unaweza ukawa na watu wako, hata muajiri wako asiwafahamu hata kama huyo mtu ana mume wake , huyo mume wake pia anaweza asijue kuwa mke wake anafanya kazi kama hizo…inakuwa baina yangu mimi na yeye, na yeye anafahamu ni kwanini inatakiwa iwe hivyo. Na malipo yake sio mchezo.

Huyu msaidizi wangu ni mdada, na sio mchezo, kwenye kazi kama hizo namuaminia, anaijulia kazi, anajua mbinu za kila namna za kupata siri fulani zilizojificha, na ni msiri mkubwa sana, na kilichonipa nguvu na kumuamini, ni kuwa kweli hata mume wake alikuwa hajui kuwa mke wake anfanya hiyo kazi.

 Siku aliponiambia hataki hizi kazi , nilipata shida sana,maana ni mtu niliyekuwa nikimtegemea kwenye kazi zangu za namna hiyo, sio kwamba sikuwa na watu wengine,lakini huyu nilimuamini sana kwenye hizo kazi, na hata aende wapi nikimuita atafika hapa mjini hata bila kujulikana, akafanya kazi, na akatoweka bila mtu kumfahamu kuwa alikuwa hapa jijini, ni mbinu zetu za kujibadili.

Nilipomkumbuka hapo hapo nikamtafuta kwenye simu, nikampata,  nikamwambia,namuomba anisadie kazi mbili muhimu sana, akaniuliza kazi gani, hakusema nilishakuambia sitaki kazi, nikajua huenda sasa hivi huyo mdada hana pesa.

Mimi nikamwambia, moja kwa moja bila kuficha, kuwa kuna mtu anatakiwa yeye  amchunguze, kwa ukaribu nahisi huyo mtu anataka kuingilia maisha yangu..

‘Mtu gani bosi, unajua nilishakuambia…’akataka kujitetea

‘Ni Makabrasha, …’nikasema kwa haraka

‘Mungu wangu, huyo mtu tena…’akasema

Hilo neno ‘tena’ nikahisi lina jambo, lakini sikutaka kumdadisi zaidi, mimi nikasema;

‘Sizani kama unamuogopa huyo mtu, ni saizi yako kabisa, mimi nakuaminia,..nafahamu kuwa watu wanamvumishia ujasiri ambao hana, wewe ni jasiri zaidi yake, unaweza kuzivunja nguvu zake kwa siku moja tu, au umeshalainika, na mume wako, usiniangushe, nakuamini kwa kazi hiyo..’nikasema

‘Kwanini unamtaka huyu shetani....’akasema, na alivyotamka hilo neno ‘shetani’ nikahisi kweli kuna jambo kati yake na huyo Makabrasha. Mimi nikamwambia kwa kifupi;

‘Huyu mtu anataka kuniingila kwenye maisha yangu binafsi,…usiniulize ni kwa vipi, muhimu kwako, ni kumfuatilia, kumchunguza, na utakuja kugundua ni nini kipo anakifanya ili kutaka kuangamiza maisha yangu, na ni ni lengo lake, hakuna mtu ninayemuamini kwa kazi hii zaidi yako wewe, malipo yatakuwa zaidi ya unavyofikiria…’nikamwambia.

‘Nilijua tu, ....huyu mtu anataka kumjaribu kila mtu, nahisi anataka kufanya jambo kubwa sana,… na kinachonishangaza ni kuwa hata polisi wanashindwa kumkamata huyu mtu, ana ulinzi gani huyu mtu, kiukweli yeye, ni… ni mjanja kupita maelezo, lakini …mimi naona hapo alipofikia kavuka mpaka, kuna haja ya kumuwahi kabla hajafika mbali...’akaniambia.

Hapo nikajua kweli nimelifikisha kwa mtu ambaye huenda naye katendwa, huenda alishaingizwa kwenye mitego ya huyo mtu, na jamani sio kwamba namteta vibaya marehemu, huyu mtu alikuwa mbaya sana, na kama angeliendelea kuwa hai, sijui tungelizunguza nini leo,  alishafikia kubaya…’mzungumzaji akaendelea na maelezo yake.

‘Kwahiyo unasemaje, upo tayari kuifanya hiyo kazi, ...au?’ nikamuuliza

‘Umesema kuna kazi mbili, hiyo ni ya kwanza , hiyo kazi nyingine ya pili ni ipi, na unataka niifanyeje, na kwa hiyo ya kwanza, umesema unataka nimchunguze, kuwa kuna jambo kakufanyia, au anataka kukufanyia, au niwekezeje nguvu zangu kwa hiyo kazi …?’ akauliza na hapo nikajua kakubali hiyo kazi.

‘Kumchuza nyendo zake, na kujua ni nini kakifanya dhidi yangu, nahisi kuna kitu anakitaka kwangu, sasa wewe fuatilia ujue ni kitu gani,na kwanini anafanya hivyo, je ni kwa ajili yake au kuna mtu kamtuma,  mengine utajua mwenyewe lakini nataka iwe siri…’nikasema

‘Toka lini kazi zako kwangu zikawa sio za siri, najua kabisa kila kazi ukinipa ni ya siri, au sio…’akasema

‘Hii ni ya siri zaidi…’nikasema

‘Upo wapi Dar, au Zanzibar, na lini utasafiri…?’ akaniuliza

‘Nipo Dar, natarajia kusafiri kwenda kusoma hivi karibuni, ila nitakuwa nikiwasiliana nawe, wewe ndiye utakuwa mawasiliano yangu, nilitaka nikuachie majukumu yangu lakini wewe haupo ofisini ulishaacha kazi, ila kwa kazi hii inabidi nikuachie…’nikasema

‘Ile safari yako…, imeshafika sio umeweza kuruka vihunzi,..sawa nenda kasome uje uanzishe kampuni yako, uachane na hizo kazi za kutumwa…huenda huko baadae , lakini sijui, nimechoka na hizi kazi, …naweza kuja kwako kuomba kazi,… lakini sio kwa sasa…’akasema

‘Usijali, wewe ni mtu wangu ninayekuamini sana, ni wewe tu kukimbilia kuacha kazi ngoja nimalize masomo, utarudi tu..’nikasema

‘Najua..hilo usiwe na shaka kabisa…nataka tu unielewe, siwezi kukuambia hili, kuacha hizi kazi nina maana yangu kubwa, kwahiyo unasema tutawasilianaje sasa…’akasema na kutulia

‘Unajua hii kazi inahitajia uharaka fulani, mimi nitakupatia namba ya kuwasiliana na mimi, ikifanikiwa haraka nitashukuru zaidi, na  malipo yake kama kawaida yetu..’nikasema

‘Swala la malipo sio tija, wakati wote nikiwa na shida, ni wewe unanisaidia, hiyo nitaichukua kama kulipa fadhila tu…ila msimamo wangu ni ule ule, kwa hivi sasa sitaki ajira, sitaki kazi za mikataba, nitafanya kimia kimia, na tutamalizana hivyo hivyo…’akasema

‘Usijali, ni lazima nikulipe…’nikasema

‘Na hiyo kazi ya pili ni ipi…?’ akaniuliza

 ‘Huyo mume wa familia, mke wa bosi wangu, eeh, ana mpenzi wake wa zamani, kabla hajaoa, walikuwa naye huko kijijini, nakata unitafutie huyo mpenzi wake alikuwa ni nani,..’nikasema

‘Unasema nini, mmh, kwanini unataka kumuingilia bosi wako, kuna nini, ..?’ akauliza kama hajasikia vyema, na ilinipa mashaka huko kuitikia kwake, kama kushtuka, na maswali yake hayo

‘Unitafutie huyo mchumba wake alikuwa ni nani, ni muhimu sana kwangu kumfahamu, ilikuwa siri kubwa,, hakuna aliyelifahamu hilo, nimelifahamu lakini sijamfahamu huyo mchumba wake ni nani..’nikasema

‘Subiri kwanza kuna mtu ananisumbua hapa…’akasema na kukata simu, basi nikasubiria na baadae nikampigia simu, simu yake ikawa haipatikani. Nilimpa muda, kama masaa mawili nikampigia tena..

Alipokea na nikamuuliza kwanini alikata simu, akaniambia kuna mtu alifika, na hakutaka asikie anaongea nini na mimi, mimi nikamuelewa maana kiukweli kazi zangu mimi na yeye ni za siri kubwa.

‘Ni hivi, mimi nataka umtafute huyo mtu ni nani, na nimegundua jambo, kuwa mume wa familia, (hapo nilimtaja jina lake) ana ukaribu na Makabrasha, nataka kufahamu ni kwanini wapo na ukaribu hivyo, na pia, nahisi huyo mchumba wa huyu mume wa familia, anaweza akawa na ukaribu na huyo Makabrasha, nataka kufahamu ni kwanini, na je kuna kitu mume wa familia kafanyiwa, sasa sina uhakika kama ni Makabrasha au kuna mtu mwingine..’nikasema.

‘Sikiliza rafiki yangu, bosi wangu, mara nyingi mimi napokea kazi zako bila masharti, nikijua ni nini ninachokifanya, ila hii kazi, sio sitaki kuifanya, ila …inanipa ukakasi, huyu mtu anayeitwa Makabrasha sio mtu mwema, nilishamchunguza kabla, huyu mtu haaminiki , pili inaonekana ni kazi ndefu, maana hapo umeshamgusia hata mume wa familia, ni zaidi ya watu watatu hapo, natakiwa kuwachunguza, no, wanne...’akasema

‘Kwahiyo utazifanya hizo kazi mbili nilizokupa, au ndio unanikatalia hivyo..kwangu mimi ni muhimu sana, na wewe ndiye mtu wangu wa karibu wa kazi zangu za siri, na nilitaka chochote utakachogundua kiwe siri kati yangu mimi na wewe, unasikia..?’ nikamuuliza

‘Siwezi kukukatalia, lakini …mmh, kumchunguza huyu mtu, ni kunitaka mimi nihatarishe maisha yangu na familia yangu, nilishakorofishana naye na akanitegea, si unajua mambo yake,…’akasema

‘Mambo gani yake..?’ nikamuuliza

‘Huyu mtu anaendesha biashara za mlungula(blackmaili), na akitaka akupate kwa jambo fulani, atafanya kila hila ili akuingize kwenye biashara hiyo, na ..bila kukuficha alishanitega kwa hilo…’akasema

‘Mhh, ndio maana unaogopa..hujamalizana naye ?’ nikauliza

‘Sio kwamba naogopa, ila nakuelezea ni kwanini nasita kuifanya hiyo kazi..mtu kama huyo kumalizana naye sio rahisi, kila akikutaka atatumia vitisho, …si unajua biashara hiyo ilivyo,…ila nitapambana naye nione mwisho wake ni nini.’akasema

‘Sasa utaifanya hiyo kazi au hutaifanya…maana kumbe ulishaianza au sio?’ nikamuuliza

‘Bosi unajua , sitaki kufanya kazi hizo tena, nilishakuambia, lakini pia sipendi kukukatalia, na nikikutolea udhuru, ujue kuna sababu ya umuhimu...’akasema

‘Na mimi ukiona ninakupa kazi hiyo wewe peke yako ujue ina umhimu sana kwangu, tafadhali, ..huwa wakati wote natoa amri kwako, lakini hii ninakuomba, ni muhimu sana kwangu..’nikamwambia.

‘Mhh,.... ama kwa Makabrasha, hiyo kazi ninaweza nikaifanya,..kwa vile… lakini sio kwa hiyo kazi nyingine, ya kumchunguza huyo mchumba wa mtu, naona huko kuna safari, kuna mambo mengi, na sitaki kushikilia kazi zaidi ya hii, na hii ni kwa vile inanigusa na mimi..’akasema hivyo na kunifanya nishangae kidogo.

‘Kwahiyo kumbe kuna kitu kakufanyia,..ok, huwezi kuniambia ni kitu gani…au umeshaingia kwenye ajira yake nini…?’, nikamuuliza .

‘Hapana sina hisa naye kabisa, lakini sitaki kuchukua kazi mbili kwa sasa, nina majukumu mengi, na..nimekubali hiyo moja tu , kwa vile wewe ni rafiki yangu, na unanidai sana, fadhila zako kwangu ni nyingi sana…vinginevyo sina sababu nyingine ya msingi, ya kuikataa kazi hiyo ya pili, na zaidi ya kwanini, siwezi kukuambia, unielewe tu…’akasema.

‘Hizo kazi zote mbili kwangu ni muhimu sana, unajua mimi nakwenda masomoni, sitakuwa na muda wa kufuatilia, na wewe ndiye unyeweza kuzifanya kazi  hizo kwa uamakini na kwa siri kubwa,..Nakuomba sana...’nikajaribu kumsisitizia, na yeye akasema;

‘Sitaweza kukufanyia kazi zote mbili hiyo moja sawa, maana Makabrsha namfahamu na nilishawahi kuifanya kazi inayomuhusu, lakini hiyo nyingine hapana, sitakuwa na muda huo, nielewe hivyo,...’akasema.

‘Kwahiyo hiyo kazi kumuhusu Makabrasha, utaifanya, lakini kwa kunisaidia kumtafuta huyo mtu mwingine, ndio umesema hutaiweza, unanipa mashaka ujue, je nikikuambia uiache hiyo ya makabrsha uifanye hiyo nyingine je…?’ nikamuuliza, na yeye akasema.

‘Hiyo ya makabrasha nitaifanya tu kwa vile nimeona huyo mtu na mimi namtafuta sana, nataka nimfahamu vyema, nije kulipiza kisasi kwake,,...japokuwa kwa ujumla sikutaka niifanye kazi zozote za namna hii tena, lakini kwa vile na wewe una muhitaji, basi ndio nikaona niichukue hiyo, ...’akasema.

‘Kwani kuna nini kikubwa huyo Makabrasha alikufanyia mpaka utake kulipiza kisasi kwake niambie ili nijue huenda ni yale yale..?’nikamuuliza.

‘Unaona, ....sitaki mtu kuniingilia hayo mambo yangu, kama unataka niifanye hiyo kazi, sitaki kuniuliza-uliza maswala kunihusu mimi binafsi, nitakuambia yale unayoyataka kuyafahamu kwenye kazi yako, ya kwangu niachie mimi mwenyewe, nina maana yangu na sitaki mambo yangu yaje kuwaumiza wengine...’akasema

‘Mhh, safari hii nakuona mwenzangu unaniacha njia panda, sijui kuna nini kinaendelea kwenye maisha yako, ujue mimi nipo tayari kukusaidia, tusaidiane ndio urafiki wa kweli ...’nikasema.

‘Kwa hili huwezi, hutaweza kunisaidia, haya ni maswala binafsi tu sipendi yakumguse mtu mwingine, sipendi…’akasema

‘Haya sawa nimekuelewa…’nikasema

‘Wewe nenda kasome, kwa kazi inayomuhusu huyu jamaa, anayejiita wakiliw a kujitegemea wa kimataifa, nitaifanya..ila nimjuavyo mimi huyu mtu ni mbaya, na hatari,kuliko unavyofikiria wewe, hata hivyo, siwezi kukuambia lolote mpaka nimalize uchunguzi wangu, na sikutaka niyaongee haya kwenye simu na kwa mtu yoyote, mpaka nimalize kazi yangu...’akasema

‘Ok, itakuwa vyema, kama ulishaianza…’nikasema

‘Saana, niamini kwa hilo, utapata taarifa nzuri tu…’akasema

‘Basi ukiwa tayari kuhusu huyo mtu tutaongea ili nijue tufanye nini, ni muhimu sana kwangu,..na nakuomba ulifanyie kazi hilo kwa haraka iwezekanavyo, na kwa huyo mtu mwingine nitajua ni nini cha kufanya, hata hivyo nina ombi moja kwako zaidi...’nikamwambia

‘Ombi gani hilo...’akaniuliza

‘Nina mikakati ya kazi kubwa baadae…, nina mipanglio mingi ya kimaisha, nikimaliza elimu yangu huku nataka tuwe wabia mimi na wewe.,.kwahiyo ninakuomba ujiandae kwa hilo, weka kumbukumbu za kazi zetu za zamani, kusanya ukweli wa kusaidia kwenye kazi zetu, tengeneza maktaba fulani yenye kumbukumbu za kesi na matukio, hasa za watu mashuhuri, nk..si unajua ninachotaka kukuambia..’nikasema .

‘Hilo halitawezekana..hujanielewa mimi sitaki tena hizi kazi,..nilikuambia ukija utaniajiri awali nilikuwa nasemea tu, nataka kubadilika, kuwa mtu mwingine kabisa, kama uhai bado upo, kiukweli kazi hizi sio nzuri, zinamuweka mtu mashakani muda wote, mimi sitaki kujishughulisha na haya mambo tena, kwa manufaa yangu ya baadae...’akasema.

‘Sawa nimekuelewa, lakini mimi nina imani kuwa tupo pamoja, hata kama kuna mambo yametokea ya kukwaza, bado tuna mafungamano ya kikazi, unafahamu kazi zetu hizi zilivyo, unaweza ukasema humuhitaji mtu, baadaye ikatokea jambo ukamuhitajia sana mtu wako wa zamani, usitupe mti na jongoo wake..’nikamwambia

‘Kwa maisha haya ninayopambana nayo, sizani kama kuna mashikamano na mtu kwenye kazi kama hizi, naomba tuishie hapo ,na ni vyema usitake kujua mengi zaidi kunihusu mimi, usiniulize tena , samani sana....’akasema akitaka kukata simu

‘Sawa kama unataka iwe hivyo…’ nikasema

‘Kiukweli nataka iwe hivyo..’akasema

***********v
Ndugu mwenyekiti ili uweze kuipata hii picha vyema, nawarejesha kidogo nyuma, nilishaliongelea hili kabla, awali, jinsi gani nilivyoweza kurejea nyumbani kwa dharura, lakini kuna mambo sikuweza kuyaongea awali, kwasababu za msingi.

Sasa hivi nitafichua yale yaliyojificha kwenye kurejea kwangu, ambayo sikuyaongea awali , hayo ninayoongea sasa yanafichua ukweli mwingine ambao utahitajika sana kama nilivyogusiwa, sitakiwi kuingilia maswalaya mauaji ya Makabrasha, nitajaribu kufanya hivyo.…’akasema.

‘Sawa endelea, lakini ni muhimu ukalichunga hilo, swala la mauaji halipo kwenye kikao chetu hiki, hilo swala lipo mikononi mwa polisi….’akasema mwenyekiti

 Siku nilipokuwa masomoni, wakati najiandaa kufanya mtihani fulani muhimu, nilipokea ujumbe kama huu… ‘

‘Utahitajika  ‘’Dar kwa haraka, kusaini mkataba wa hiari, dhidi yako na mzazi mwenzako, lakini bado ninamdai pesa nyingi sana, kama itatokea sitalipwa pesa zangu, sitakuwa na jingine bali kuwakilisha hizi picha kwa rafiki yako,…’’ ule ujumbe ukaambatishwa na picha, mojawapo ya picha mbaya, ambazo zilionyesha yale niliyokuwa nikifanya na mume wa familia, hiyo ikiashiria vitisho, kuwa nisipofanya hivyo, picha hiyo itafikishwa kwa walengwa.

Nilipopata huo ujumbe nikampigia simu huyu mtu wangu wa karibu, nikamwambia anifanyie uchunguzi, ni kitu gani kinachoendelea kati ya Mume wa familia na mke wa familia,  na hapo mtu wangu huyo, akaniambia hilo ameshalifanyia kazi, na kusema;

‘Mume wa familia kaingia kwenye mtego na adui yetu,..’akasema

‘Una maana wakili Magumashi..’nikamwambia
‘Huyo huyo, …. kwahiyo inabidi afanye kila anachotakiwa kukifanya , na mengi ni kwa ajili ya masilahi ya huyo adui yetu, ikiwemo kukubali kuingia na adui yetu kwenye mkataba unaoidhinisha adui yetu kupata hisa kwenye makampuni ya bosi..’akaniambia.

‘Haiwezekani...ooh, mbona hilo ni  gumu sana…unauhakika na hilo..?’nikasema kwa mshituko mkubwa.

‘Ndio hivyo, kuna mengi yamefanyika, na mshika usukani ni huyo adui yetu, inavyoonekana ni kuwa huyu adui yetu kaingilia mambo mengi, lakini nia na lengo lake ilikuwa kuingiza makucha yake kwenye mali za bosi wako…’akasema

‘Una uhakika na hilo…?’ nikauliza

‘Zaidi ya uhakika… na ukumbuke kuwa bosi wako na mume wake hawapo kwenye mahusiano mazuri, hawajui yote hayo yalipikwa na huyu adui yetu, ingawaje hadi sasa wana ndoa hao, wapo kwenye kutimiza wajibu wa kibinadamu, kutokana na huo wajibu, itawabidi waendelee kuwa wanandoa, vinginevyo, kitu kinachoitwa ndoa ni kama hakipo...’akasema.

‘Hali gani hiyo ya kibinadamu?’ nikamuuliza.

‘Mume wa familia  kutokana na hiyo ajali,  kuna matatizo mengi yanazidi kutokea, kuna dalili za maradhi ya kuota kwa vitendo, kuna kuchanganyikiwa, …unaona..na inaonekana hali aliyo nayo sio ya kupona leo, na mke kama mke hatakiwi kumtelekeza mumewe kwenye hali kama hiyo.., nahisi kama isingelikuwa huo ugonjwa sasa hivi tungeliongea mengine...’akasema.

‘Kuna nini kikubwa ulichokigundua, kilichosababisha  hadi hiyo ndoa iingiwe na tatizo kubwa kiasi hicho, ni mambo yao ya ndani kwa ndani au kuna msukumo mwingine kutoka nje...?’ nikamuuliza.

‘Hayo unayafahamu sana wewe, sioni haja ya mimi kukuambia, japokuwa kuna mbinu zilizotoka nje, zilizojengwa kitaalamu sana na wajanja, ili ionekane hivyo ilivyo, kwa muda niliofanya uchunguzi wangu, nimegundua mengi, kumbe hata wewe upo kwenye mchakato huo, sikutegemea, kumbe unanipa kazi ambayo unaifahamu ...’akasema

‘Mimi kwa vipi..sielewi kitu ndio maana nikakupa hiyo kazi..niambie kwa vipi?’ nikamuuliza

‘Hahaha..usijali, ..japokuwa imeniuma sana, kuwa kumbe nafanya kazi kwa mtu ambaye ni mmoja wa watu wanaonichoma kisu moyoni mwangu...’akasema akiongea kwa sauti yenye huzuni.

‘Una maana gani, ‘mimi kukuchoma kisu..’ ?’ nikauliza

‘Usijali, utakuja kujua , lakini sio sasa…’akasema

‘Ni kwanini sasa hutaki kuniambia ukweli...nimekufanyia nini mimi kibaya , niambie ukweli, kama kuna jambo nimekukosea, ni bora uniambie, huenda kuna sababu ya msingi ya mimi kufanya hivyo, ila wewe hufahamu’ nikamuuliza na kujaribu kumuelezea, ili nifahamu ni jambo gani hilo, nililolifanya hadi mwenzangu afikie kuumia kiasi hicho.

‘Ukweli unaoufahamu wewe unatosha, na nakushauri ufanye kama wao walivyotaka, na watakavyotaka, kwa hivi sasa…hakikisha umefika huku nyumbani bila kukosa,…, ufanye kama watakavykuambia, baada ya hapo, mengine yatafuata, kwa hivi sasa wameshikilia mpini, ukikosea kidogo utakuja kujuta,..’akaniambia.

‘Ina maana hata wewe upo kwenye huo mchakato au umeligundua hilo kutokana na ule uchunguzi niliokuambia…?’ nikamuuliza

‘Hata siku moja siwezi  kushirikiana na hao mashetani, hili ninalokushauri ni kutokana na uchunguzi wangu, nifanyavyo kazi zangu hutaweza kunielewa, lakini mwishi wa siku nitakupatia taarifa yako..’akasema

‘OK…’Nikasema hivyo, halafu akasema

‘Siku nikimaliza hii kazi, kila kitu kitakuwa hadharani, na nitahakikisha kuwa kama kuna kundi, kama kuna njama, basi zitafikia kikomo chake...kama ni kundi, nikitoka kwa huyu mtu, basi nitamuendea  mwingine, mpaka nihakikishe nimemaliza kazi...’akaniambia

‘Unaposema kundi, au watu wengine ni akina nani, inaonyesha umeshawagundua hao watu au sio?’ nikamuuliza

‘Mhh, ,,kwa hivi sasa siwezi kukuambia kitu, nipe muda kidogo, cha muhimu ni kuhakikisha kuwa hili jambo nimeliweka sawa, nataka kuhakikisha kuwa hawa wananitesa moyo wangu, wanasambaratika, na hakuna kitu kama hicho tena, na kama ni njama, zinazofungamana na mwenza wangu, nitahakikisha nazifahamu, na kama yeye anahusika,…oh, hata yeye mwenyewe atajuta kufanya hivyo, ..’akasema

‘Mhh, sasa hapo unazidi kunichanganya, na huyo mwenza wako ndio nani tena, ndio huyo mume wako ?’ nikamuuliza

‘Usinidadisi sana kuhusu hilo, ila yeye ndiye moyo wangu, unasikia, ni, ni....’ simu ikakatika, na ilikatika kama vile mtu kapatwa na tatizo, ikanibidi nipige simu, kwa mtu wangu mwingine, yeye ni msaidizi wake, katika mambo yetu ya utendaji, nikamhoji,

‘Unamuulizia bosi, mbona alishaacha zile kazi zetu…’akasema

‘Yupo salama ..ebu mfuatilie hata kwa simu tuone kama yupo salama..’nikasema na ikachukua muda, halafu akawa hewani na kusema

‘Yupo salama bosi..’akasema

‘Je kwa hivi sasa anafanya kazi gani..?’ nikamuuliza

‘Hajulikani sana bosi, nahisi yupo nyumbani…’akasema

‘Kwahiyo hana kazi yoyote yupo nyumbani tu, au ana kazi gani maalumu anaifanya kwa sasa y akumuingizia kipato..?’ nikamuuliza

‘Si kwamba yupo nyumbani, si unajua alivyo, anaweza kuacha kazi hii, kumbe ana kazi nyingine, kuna sehemu anafanya kwa muda,…anakwenda huko mara chache chache, ila mara nyingi anaonekana yupo peke yake, yaonekana kuna jambo linamtatiza, anakuwa kama kachanganyikiwa hivi..’akasema.

‘Kwa mtu gani huyo anapoonekana akifanya kazi ...unamfahamu huyo bosi wake mpya?’ nikamuuliza

‘Ndio namfahamu huyo bosi wake, japokuwa awali alifanya ni siri, lakini nilimfuatili mpaka nikaja kugundua wapi anapofanyia hiyo kazi, japokuwa sio kwa siku zote,...’akasema

‘Au labda anafanya kazi hapo kwa ajili ya kupata taarifa, ..?’ nikamuuliza

‘Mhh, sizani,…hapo sina uhakika bosi …’akasema

‘Ni kwa nani hapo anapofanyia kazi, nipe taarifa kamili, sio unanipa taarifa kama unaogopa, ni kwa mtu gani anapofanya kazi kwa sasa?’ nikamuuliza kwa hasira

‘Ni kwa Makabrasha bosi, ...mara nyingi anaonekana ofisini za siri za kwa Makabrasha, inaonekana kaajiriwa na Makabrasha, au kuna kazi maalumu anaifanya kama ulivyosema, sina uhakika na hilo...’akasema na hapo hapo nikakata simu.

Sikupoteza muda nikapanda ndege na kuja Dar,ndivyo ilivyokuwa kuja kwangu Dar, kwa ghafla .... na sasa safari yangu hiyo iligundua nini, na ukumbuke ndicho kipindi Makabrasha aliuwawa, ukumbuke ndipo kipindi mume wa familia anaumwa…kuna mambo mengi hapo yamejificha…akatulia pale alipoona mwenyekiti akiongea na simu

‘Niendelee mwenyekiti…’akaulizaWAZO LA LEO: Mambo yanayohusu imani za watu , hisia za watu, upendo wa watu…, mambo hao ni nyeti sana, ni vyema, ukikutana na vitu kama hivi uwe makini sana kuviingilia. Mtu akiamini, akapenda, huona vingine vyote havina maana, anaweza hata akafumbia macho elimu yake, na akafanya mambo ambayo kwa elimu yake, hastahili kuyafanya hayo. Ndio maana wanasema, mwenye kupenda haoni, hata akiona kibaya kwake, ni kizuri, akiona chongo ataita ni kengeza.
Ni mimi: emu-three

No comments :