Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, February 20, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-84


.....huyo bint ndio yeye aliyesema kuwa anashirikiana na usalama wa taifa…?’

‘Hapana, unasikia ….’akatulia kama anawaza jambo

‘Yule binti aliyekuwa mfanyakazi wa nyumbani yeye aliondoka kwa sababu zake binafsi, aliiba pesa, na pesa hizo nilikuwa nimezichukua kwa mke wangu, kwa kazi maalumu ya zabuni kubwa ya kibiashara, sasa huyo binti akazikomba zote, na sikupenda hilo jambo mke wangu alifahamu kabisa, nikatafuta njia ya kuzirejesha kivyangu..’akasema

‘Kwanini sasa, kama mtu kaiba, kwanini wewe ubebe gharama zake, hiyo sio kweli, niambie ukweli, huyo binti aliondoka hapo nyumbani kwenu kwa sababu gani, nahisi kuna kitu ulimfanya huyo binti, na huenda ni uzinzi wako, na ndio maana ukalipa hizo pesa, na hukutaka mkeo afahamu, hiyo ndio tabia yako, na leo hii unataka mimi nikusaidie, hayo ndio maisha yako au sio...’nikamwambia.

‘Sio kweli yule ni mwizi, na akirudi tena hapa Dar, tunamweka ndani, tatizo hajulikani wapi alipo…’akasema

‘Wewe sikuamini, au nikusaidie kumtafutahuyo bint alipo, nipe hiyo kazi japokuwa sina muda, mimi nitamleta hapa na atausema ukweli wote…’nikasema

‘Hapana achana naye, huyo nilishamalizana naye, muhimu ni hili tatizo lililope mbele yetu, mbona hulitilii maanani, hivi, ..’akasema

‘Sizani kama tutaelewana kwa hali kama hiyo…’nikasema

‘Sasa kama huniamini mimi utamuamini nani,..ndivyo ilivyokuwa,..na mimi ndiye muhusika,…’akasema

‘Sasa sikiliza, mimi nikionana na huyo mtu atakayetusaidia, kama mambo yatakwenda vyema nitakuja kukuambia, vinginevyo, kama unaona huwezi kunisaidia, au tusaidiane, haya,…lakini hili tupo wote..hatari niliyo nayo mimi haina tofauti na yako…na hao jamaa inavyoonekana, lengo lao ilikuwa kupata pesa kote kote, ila wameshindwa…’akasema

‘Mimi siwezi kukubaliana na wewe mpaka nifanye uchunguzi wangu nihakiki haya mambo, siwezi kukubali upuuzi kama huo, mimi sio kama unavyonifikiria wewe, na ole wenu nikiwagundua kuwa mna njama zenu za kitapeli, .....’nikasema

‘Hakuna utapeli hapa..unielewe hivyo…’akasema

‘Miminilivyo eeh, nipo tayari hata hizo picha zifike kwa mkeo lakini nitahakikisha nalisafisha jina langu kuwa hata mimba wewe ndiye sababu, nyie ndio mlifanya mbinu zenu na sijui mlikuwa na malengo gani, mlitumwa, au…sawa usiposema ukweli hili litakuwa lako,....’nikamwambia.

‘Ukinitisha mimi utajisumbua bure, sijui lolote, hata mimi najiuliza ni kwanini, sijui kitu, wakati mwingine nahisi kuwa sipo sawa sawa..lakini haya niliyokuambia ndio ukweli wenyewe…na hata kuamua kuja kwako, nilijua tutaweza kushirikiana , sasa wewe unazidi kunichanganya tu hapa’akasema

‘Niambie huyo Makabrasha mlijuana naye kivipi, ndio umesema mlikuwa wote kijijini sawa…, je ilitokeaje mpaka mkawa na usuhuba wa karibu kwenye mambo yenu ya kazi, na haya…, ?’ nikamuuliza

‘Usiweke hivyo …usuhuba na huyo mtu ni mpaka kuwe na masilahi kwake, ..’akasema

‘Ni kusema kabla ilikuwaje …’nikataka kuongea na yeye akaanza kuongea

‘Kujuana kabla, ni hivi, yeye mwenzangu alitangulia kidunia na kimaisha, ni mkubwa kuliko mimi, na aliwahi kufika mjini muda mrefu tu, na kutokana na kisomo chake, alikuwa akifahamu mambo mengi sana...nilipenda sana tabia yake ya kujua kila kitu, akawa kama mwalimu wangu...akija kule kijijini, ananisimulia mengi, na alipenda sana kusoma vitabu, na moja ya mambo aliyokuwa akinisimulia ni kama hayo...’akasema

‘Mambo gani hayo, unayosema kama  hayo…?’ nikamuuliza ili kujua zaidi

‘Yakusomea sheria, na kuja kupambana na watu matapeli, kama hao, ambao kazi yao ni kutaka kupata pesa kwa matajiri kwa njia hii, ya kuchukua picha mbaya na kuwatishia matajiri, na wanatoa pesa ili siri zao zisivuje yeye alisema anataka kuwakomesha hao watu...’akasema

‘Kwahiyo akakufundisha na wewe jinsi gani wanafanya, au anafanya, au alipenda kufanya, na wewe sasa ukaamua kunifanyia mimi, au sio?’ nikamuuliza

‘Kukufanyia wewe…!!! Hapana, alikuwa akinihadithia hivyo visa tu, mimi nilikuwa nikimsikiliza tu, ikatokea nikamuoa mke wangu, na akalifahamu hilo kuwa nimemuoa mke mwenye uwezo, na hapo ndio akaanza kunifua fuata, kwanza alikuja na ajenda ya kunilaumu kwanini nimekimbilia kumuoa mke mwingine nikamuacha mchumba wangu,…’akasema

‘Mchumba wako!!! Ina maana ulikuwa na mchumba wako, mwingine, kabla ya kukutana na huyu mkeo ?’ nikamuuliza

‘Kila mtu anakuwa hivyo, au sio, unakuwa na wachumba wengi lakini mwisho wa siku unaamua kumuoa mmojawapo, ni kweli nilikuwa naye, sikuwa na mwingine zaidi yake, wengine walikuwa wakupotezeaan muda, kila mtu alijua hilo, hilo kiukweli siwezi kukudanganya…’akasema

‘Ok…nimekuelewa hapo…, sasa lakini bado najiuliza, kwanini huyo wakili akulaumu kwa hilo..?’ nikamuuliza

‘Unajua yeye, alitaka awe wakili wetu, lakini sikupendelea awe hivyo kwa vile namfahamu sana tabia yake, hata hivyo alivyozidi kunifuatilia, nikaona bora niongee na mke wangu niona kama ataweza kunikubalia tumpe kazi hiyo, lakini mke wangu akasema tayari yupo wakili wake anamuamini sana.

‘Sasa kwanini azidi kuja kwako, bado haijaniingia akilini, kwanini wewe, asiwe mwingine, sawa yawezekana ni katika kutafuta wateja au sio, lakini kwako…mmh, kuna sababu au sio…’nikasema

‘Yeye nahisi alikuwa na ajenda zake za siri, maana baadae alikuwa akija kunishawishi nifanye mambo fulani ili huyo wakili wa mke wangu aonekane hafai, ili yeye aje kuipata hiyo nafasi, unaona ilivyo… ina maana alikuwa na jambo anataka kulifanya, na mimi sikumkubalia ..’akasema

‘Kwahiyo…kwahiyo…sizani kama ni ajira tu alikuwa anataka kwako, kuna msukumo hapo,..kwanza lawama, pili ajira, na tatu….niambie ukweli?’ nikauliza

‘Tukawa hatupatani,  lakini kuna muda tunaelewana, nikiwa na kazi fulani za haraka unajua tena hizi kazi zetu za biashara, sio kila kitu kinakwenda kwa mkono wa sawa, inabidi wakati mwingine upindishe mambo, basi huwa namtafuta yeye, na yeye hashindwi kitu, anajua njia zote za kupindisha pindisha mambo na siku zinakwenda, unafanikiwa kile ulichokitaka ndio maisha..’akasema.

‘Nimjuavyo Makabrasha katika uchunguzi wangu, alijengwa, hata kusomeshwa na yule mwanasiasa mpinzani wa baba mkwe wako, …na sasa kuona anataka kujiunga upande huu, …tatizo lako hutanielewa,…huyo Makabrasha ana zaidi ya hilo unalolifikiria wewe…’nikasema

‘Hayo ni mawazo yako, maana pia mimi nilimuuliza hilo, akasema yeye ni kama taksi dereva, abiria wake wote ni sawa, haijalishi wapo kwenye imani au chama au kabila gani, muhimu wanamlipa ujira wake…’akasema

‘Ukaamini hivyo..hahaha, huyo mtu yupo kwenye orodha ya watu wasiofaa, nikisema hivyo nina maana yangu, …na siwezi mimi kuwa naye chungu kimoja, hatutakuja kuelewana kamwe, na anaifahamu….ila kwasasa anahisi kanipata, hajanipata bado, haweza kuja kuonana na mimi uso kwa uso…ndio maana anakutumia wewe…’nikasema

‘Mimi hayo siyajui, kama mna uadui ni wenu nyie wawili, mimi yule ni ndugu yangu rafiki yangu, tunaivana sana, …kama ana ajenda ya siri, labda ni ya kimasilahi, lakini nina imani kubwa, kuwa hawezi kunitupa..’akasema

‘Hahahaha…sasa hebu subiri, usiondoke, ..’nilisema hivyo nilipoona anataka kuondoka.

‘Huyo mchumba wako na Makbrasha, wana ukaribu gani, udugu labda hivi..maana ni kwanini akaja kukulaumu  wewe kwa hilo, kuwa umemuacha mchumba wako na kukimbilia kumuoa mchumba tajiri..?’ nikamuuliza

‘Unajua alichonilaumu mimi, sio kwa vile tu nimemuoa binti tajiri na kumuacha huyo mchumba wangu, wa awali, yeye alisema nimemuoa mke tajiri, lakini siwezi kuwa na akili ya kuona mbali, siutumii huo mwanya kujiimarisha na kuwa kama baba mkwe wangu ….’akasema

‘Kama baba mkwe wako…unakuja taraibu, au sio…’nikasema

‘Kwani, ..ndio hivyo…yeye alisema hivyo, na pia mimi nimekuwa kama mtumwa fulani hivi wa mke wangu..siku hiyo tulikosana naye, anafikia kuniambia eti mimi ni mjinga, mtumwa wa mke wangu.. sio kweli…’akasema..

 ‘Ngoja, ngoja..hapo hapo,.. nikuulize kwani kwa mkeo unakosa nini, mbona mkeo ni mtu mnzuri tu, hajali kuhusu maisha yako, una kampuni yako, na hiyo kampuni imetokana na baba yake,..?’ nikamuuliza

‘Unajua tena, wakati mwingine nayawazia mawazo ya huyo rafiki yangu kuwa huenda ni kweli naweza kufanya hivyo na mimi nikawa mtu mwenye mamlaka yake, ni ndoto za kimaendeleo au sio, hata kama utaharibu hapa, lakini kwa vile mwisho wa siku utafanya jambo kubwa la maendeleo, hakitaharibika kitu, ndio hivyo…sasa sikiliza, ngoja mimi niondoke…’akasema nikahisi kuna kitu ananificha na mimi sijamalizana naye.

‘Subiri mimi sijamaliza na wewe,…hili neno la kutaka wewe uwe kama baba mkwe wako, ni lako, ..au lilitoka kwa Makabrasha..?’ nikamuuliza

‘Mhhh, yeye ndio alianza kuniambia, lakini hata mimi nilikuwa na wazo hilo…’akasema

‘Kwanini hakukuambia uwe kama yule mpinzani wa baba mkwe wako, na yule si mtu mkubwa, tajiri…eeh, kwanini…huoni kuna kitu hapo, au akili yako bado inafikiria hapa tu…?’ nikamuuliza

‘Tatizo wewe unakuza mambo, …unataka kulifanya hili la kisiasa au sio, makabrasha na siasa wapi na wapi…’akasema

‘Yeye si mbwa wa bwana, anatumwa, anaelekezwa, tatizo wewe humfahamu makabrasha kwenye uwanja huo…wewe unamfahamu kwa mahusiano ya karibu, mimi namfahamu kitaifa na kimataifa, huyo mtu sio mchezo, anajua kuingia anaga zaote na akafanya uaharibifu..ni mtu hatari, kuliko unavyofikiria yeye, akiwa vitani hana udugu,…nakuonya hilo ulifahamu…’nikasema

‘Wasiwasi wako tu, mimi namfahamu sana, ni mtu wa kijijini, tumeishi naye sana..sema mud mwingi alikuwa huku mjini…’akasema

‘Ok…najua naongea na mtu …ok…  nikuulize kwanza, ina maana wewe ulimuoa mke wako kwasababu ya utajiri au ulimpenda eeh,..?’ nikamuuliza na hapo akacheka, na kutikisa kichwa, na kuonyesha furaha fulani hivi…akasema;

‘Unajua swali lako hilo ni kama kunitega, lakini nikuambie kitu hata rafiki yangu huyo ananilaumu kwa hilo na hata kufikia kusema kuwa mimi sikustahiki kumuoa mke tajiri, eti sijui jinsi gani ya kuendeleza huo utajiri, na mke akaniamini, eti mimi nilitakiwa nimuoe mpenzi wangu huyo wa siku nyingi, maana yeye tunaendana, lakini mimi sio kuwa nimemuoa mke wangu kwa vile ni tajiri tu, pia nampenda …’akasema

‘Unampenda pia, hahaha… sasa kwanini umemsaliti, au mapenzi kwako yana maana gani..?’ nikamuuliza na hapo, akawa kimia kama anawaza jambo, na nilipoona hataki kujibu swali langu hilo nikamuuliza swali jingine;

‘Huyo mpenzi wako unaweza kumlinganisha na mkeo, mkeo ana kila kitu, kwanza yeye ni mzuri, mpenzi wako anaweza kumfikia mkeo kwa uzuri, zaidi ya hayo yeye ni msomi ana pesa, amatokea kwenye familia yenye uwezo,....kwanini hutulizani na yeye mkasonga mbele, sasa angalia ulichokifanya, haya yasingelitokea kwasababu ya tamaa zako?’ nikamuuliza

‘Usinilaumu kwa hilo….kwanza haya yameshatokea, lawama haisaidii…,najua nimekosea, lakini sio kwa kupenda, unajua mengine nikikuambia hutanielewa, ndoto yangu kubwa, ilikuwa kumpata mtoto wa kiume,  na pia hiyo ya kutaka na mimi nijikweze, niwe mtu wa kuheshimiwa, kama mume wa familia,…’akatulia

‘Una uhakika kwa kufanya ulivyofanya unaweza kulifanikisha hilo…?’ nikamuuliza

‘Ndio kitu …nilitaka kukifanya, haya mengine yamtokea na kuharibu kila kitu,..haya sio ajenda yangu, …hapana, ndio maana nasema wakati mwingine nahisi kama sipo sawa sawa, ..kuna hali inanitokea na kuwa kama nimechanganyikiwa,…na sijui, kuna dawa nilipewa zinanisaidia saidia..’akasema

‘Unahisi…haupo sawa kiakili..una tatizo la akili labda, au ..kwani ulipimwa hospitalini..?’ nikamuuliza
‘Hospitalini walisema ni mawazo tu…nikaonana na jamaa yangu mmoja akaniambia hata yeye ana matatizo hayo, kuna dawa anatumia zinamsaidia…’akasema

‘Rafiki, sio docta, wewe…si umesoma wewe, halafu dawa za matatizo ya akili..?’ nikamuuliza

‘Unajua ukitegemea hospitalini, unaweza ukapata shida, kwanini hamuamini dawa za kienyeji..’akasema

‘Kwahiyo ni madawa ya kienyeji ulitumia…ya miti shamba au sio..?’ nikamuuliza

‘Ya kienyeji lakini ya kitaalamu..yapo kividonge hivi…’akasema

‘Ni nani huyo docta, au huyo rafiki yako ni docta..?’ nikamuuliza

‘Kwanini unaiuliza hivyo, nimeshapona, inatokea tu , sio tatizo sana, ila kuna muda inatokea, ikitokea natumia hizo dawa…’akasema

‘Hebu kwanza,..hili la afya yako tuliweke pembeni…. unajua mimi siwezi kufanya jambo bila kufahamu kiini chake, kukuhoji hivi ni kutaka kufahamu kiini cha haya yote,..unasikia, sasa twende kwa huyu rafiki wako wa zamani…’nikasema

‘Wanini, huyo achana naye, hana tatizo kabisa, usimuhisi vibaya, huyo namuamini sana, na …sitaki mtu amsema vibaya,…’akasema

‘Kwasababu unampenda sana au sio…?’ nikamuuliza hivyo

‘Hahaha, sio hivyo, ndio kumpenda ni sawa tu, kwa vile alikuwa mtu wangu, na ndio hivyo, hata hivyo, kwa hivi sasa yeye ana mume wake, na mimi nina mke wangu, hayo yalipita, japokuwa tumetoka naye mbali, sio kwamba kwa vile sijamuoa, ndio nimseme vibaya, hapana, huyo …hapana, ..sipendi kwanza kumuongelea vibaya, kabisa kabisa..’akasema, na mimi nikamuangalia moja kwa moja usoni na kusema;

‘Kwangu mimi ili nikusaidie hili, itabidi umuongelee, nimfahamu, kuna kitu nahisi anahusika,…’nikasema

‘Wewe unahusikanaje, uwongo kabisa, ungelimfahamu huyo binti, hana tatiz na mtu…’akasema

‘Sikiliza mimi ukiniambia ukweli kumuhusu yeye, basi mimi nitafahamu kama kweli anahusika au hahusiki, unielewe hapo, hebu niambie ukweli kuhusu huyo mpenzi wako wa siku nyingi, ni kitu gani maalumu kinakufanya umpende sana?’ akaniuliza

‘Mpenzi wangu wa siku nyingi nampenda sana, na yeye anafahamu hilo, lakini mke wangu ana kitu cha ziada, ana mali au sio, hata wewe unalielewa hilo,. Kwahiyo hivi ni vitu viwili huwezi kuvilinganisha kama unavyotaka wewe.’akasema

‘Hujanijibu swali langu bado..’nikasema

‘Huyo mpenzi wangu wa zamani, yeye kwa kulinganisha na mke wangu, yeye kiukweli, anayafahamu mapenzi ya kweli, na penzi letu mimi na yeye ni la kutoka moyoni,…nilishakuambia ni penzi la asili, hilo halitaweza kufutika moyoni hta ukimuuliza yeye, …lakini eeh, mtaishije, maisha yanahitaji kujiongeza, au sio..? hamuwezi kulala njaa, huku mnasema mnapendana, au sio, ilibidi iwe hivyo, baada ya kumpata huyu mke wangu  basi tena, ikawa ni bahati …’akasema

‘Kwahiyo,eeh,..ngoja kwanza, ulipompata huyo mkeo, maana sio kazi rahisi kama nijuavyo, kwenye swala la mapenzi,…sasa wewe uliwezaje kumshawishi huyo mpenzi wako hadi akakubaliana na wewe au wewe ulimsaliti tu kivyako, maana nakuona ndio tabia yako …?’ nikamuuliza

‘Hapana mbona tulikubaliana tu kwa wema tu.., tulikaa tukaongea ,tukakubaliana iwe hivyo..unajua ilitokea bahati, yeye naye alimpata mwanaume mwenye uwezo,…na..alimpenda kwa hali kama ilivyo yangu, tukaona tusiziachie hizo bahati, unaona eeh,  nakuelezea haya, kwa vile nakuamini,sikutaka kumwambia mtu mwingine haya yalikuwa baina yangu mimi na yeye tu...’akaniambia hivyo.

‘Hahaha, mnanishangaza sana, ..yaani muache kuoana nyie mnaopendana kiukweli, mkakubaliana muachane ili mpata wenye mali, ajabu kabisa,, sasa hauoni kuwa mlijidanganya..’nikasema

‘Kwa vipi…?’ akaniuliza kwa mashaka.

‘Sasa wewe huoni, ndio maana hutosheki kwa mkeo, wewe hulioni hilo..?’ nikamuuliza

‘Hapana…sio hivyo,..sisi wawili tulielewana, na hakuna atakayeweza kutuelewa kamwe, ndio maana nasema huyo mpenzi wangu wa zamani muache kama alivyo, hahusiki na lolote,..na isingelikuwa uyu mtu , aliyekuja kutughasi baadae, sisi tulishamalizana,..’akasema

‘Aliyewaghasi ni huyo Makabrasha au sio..?’ nikauliza

‘Ndio,…, maana hakuishi kwangu tu, alikuwa akienda hadi kwa huyo… kumsumbua..’akasema

‘Anamsumbua kwa lipi sasa..?’ nikamuuliza

‘Eti na pia huko yeye awe wakili wao wa familia, yeye alitaka apenyeze mambo yake kila mahali, lakini hakuafahamu misimamo yetu sisi wawili, na akija kwangu anajaribu kunishawsishi kwa maneno yake ya kunikera kuwa mimi sio kama mume, mimi ni kama nimeolewa na mambo kama hayo, ni maneno ya kuniumiza moyo tu…’akasema.

‘Kwani ni kweli, kuwa wewe upo upo tu, sio kama mume…?’ nikamuuliza

‘Aah, hayo tuyaache bwana, kwani yanasaidia nini kwa hili…’akasema

‘Sikiliza unajua hapa najaribu kutafuta ukweli, inawezekana huo ukweli ukawa na sababu na hili tukio, mimi kwanza simuamini huyo rafiki yako, nahisi anahusikana na hili jambo, nimeshaanza kuhisi hivyo…, kuna mambo kidogo bado sijaelewa, nikielewa tu, nitakuambia ni kwanini simuamini huyo rafiki yako…’akasema.

‘Mambo gani hujaelewa, sikiliza haya ni mambo mawili tofauti, niamini mimi…’akasema

‘Sikiliza, mimi kazi hizi za upelelezi nazifahamu sana, sisi huwa tuna hisia zetu, hisia ya tatu,..kama kuna jambo linahusiana, akili hucheza, na mara nyingi, ikitokea hivyo, inakuwa kweli..hisia ya tatu, usiifanyie mchezo na hisia ya tatu,.. mashaka kidogo yanakutuma kwenye sehemu ambayo hutegemei, na huko huko ndio unaupata ukweli, mimi nahisi huyo mpenzi wako, ana kitu na Makabrasha..sasa niambie ukweli, …wewe kuna kitu unanificha, au …’nikasema

‘Unataka nikuambie nini sasa…?’ akaniuliza

‘Kila kitu, ..mfano, Huyo Makabrsaha alikushauri nini, baadae, ..?’ nikamuuliza

‘Ushauri wake, ni kuwa yeye anaweza kunisaidia, nikawa mume mwenye nguvu, nikaweza kuzitawala hata mali zetu za ndani..vitu kama hivyo…’akasema

‘Kuzitawala…!!! Mhh..kwa vipi sasa…?’ nikamuuliza, nikiwa bado na maswali mengi kwake.

‘Unajua mimi na mke wangu tuna mkataba,…’akasema

‘Mkatabaeeh, ..yapu huo ndio unakuweka roho juu, je huyo rafiki yako aliwahi kukusaidia ukaukwepa huo mkataba, au sio…’nikasema

‘Ndio… sikutaka kukuambia hili…, kuna kipindi ilitokea nikamjaza binti fulani mimba ..’akasema na kushtuka akakatiza , hakuendelea kuongea.

‘Mwingine huyo,au yule yule…?’ nikauliza

‘Sikiliza sasa,…ilikuwa ni bahati mbaya, huyo binti akaja juu, anataka kunishitakia, ..sasaa liyenisaidia kwa haraka ni  huyo rafiki yangu, na ndio hapo akagundua kuwa mimi na mke wangu tuna mkataba,..na ndio akaniomba aupitie huo mkataba, aona kama kuna kitu cha kunisaidia…’ akasema

‘Duuh, kwahiyo ndio hapo huyo jamaa akafahamu kuhusu mkataba wenu, kumbe alishalifahamu hilo…sasa huoni hapo, huyo jamaa alishakutega, alishajua siri zenu, na sasa keshakuweka kiganjani,…’nikasema

‘Sasa ningelifanya nini, maana asingelikuwa yeye, mimi ningelichukulia haya mambo kiubabe, na binti angelienda mahakamani, ina maana mke wangu angelilifahamu hilo, na mkataba wetu ungelinifunga, hebu wewe angalia hilo, ndio maana namthamini sana huyo rafiki yangu…’akasema

‘Na wewe huoni kuwa huyo rafiki yako alingojea nafasi kama hiyo, na sasa imetokea, ndio maana anatumia mbinu za namna hiyo, hivi sasa keshakunasa, ana kila ushahidi wa kukuweka kubaya..ndio maana akalifanya hili..hapo alichokifanya  ni kutafuta mtu mwingine, kumbe huyo mtu mwingine wamepangana naye, hizo ni mbinu zake tu…’akasema

‘Huyo jamaa haamini watu bwana kwenye kazi zake, sijaona msaidizi wake zaidi ya binti mmoja anyechapisha barua zake,  mimi ninamfahamu sana, achana na mawazo hayo..’akasema

‘Kwahiyo kwa kifupi, huyu rafiki yako kakushauri nini kwenye hilo, atakusaidiaje, si lazima mlijadili afanye hiki na hiki, au sio..?’ nikamuuliza

‘Anasema kuna jambo alitaka alifanyie kazi likifanikiwa sitakuwa kwenye matatizo tena, ila ni gharama sana, zaidi ya gharama, …lakini yeye hana tatizo, hata kama ni gharama hawezi kunifanya nilipe kwa mkupuo, atajua jinsi gani mimi nitamlipa…’akasema

‘Hajakuambia ni kiasi gani..?’ nikamuuliza

‘Hajasema , si mpaka afanikishe hilo jambo,…’akasema

‘Hapo sijakuelewa, hilo ni pamoja na hizo picha au hilo ni jingine…?’ akauliza

‘Hilo ni jingine  bwana, hili la picha ndio imekutana naye leo tukajadili , ila kasema hata hili la picha ataweza kulimaliza, kwa huo mpango anaoufanya, ukifanikiwa basi mimi nipo huru, maana picha zikifika kwa mke wangu, ina maana ni ushahid tosha au sio..kwahiyo akasema nimpe muda alifanyia kazi….’akasema.

‘Kwahiyo hilo la kulifanyia kazi lilitokea lini, kabla ya hili tuko la picha au sio..?’ nikamuuliza

‘Kabla, ndio…na sasa tulipokutana ndio akasema ule mpango uharakishiwe maana utasaidia hata kwenye hili tatizo la picha..muhimu ni mimi nihangaike kutafuta pesa, maana inahitajika pesa nyingi sana..’akasema

‘Hahaha, wajinga wakubwa nyie…hapo nimekunasa kilaini, ..haaa, sawa bwana, ngoja tuone…’nikasema, na yeye alikuwa bado hajanielewa, na sikutaka anielewe, kwa muda huo,  ila kwangu mimi nilishagundua ni nini kinachoendelea

‘Umeninasa kwa vipi..?’ akauliza, na mimi nikasema

‘Kwahiyo wewe sasa unataka kufanya nini, kwa hivi sasa, maana mwenzako kakutega, na kwa hili umeshaingia kwenye mikono yake, sasa nikuulize ni kitu gani hicho alitaka kukifanyia kazi, ..?’ nikamuuliza

 ‘Hakuniambia, …cha muhimu kwangu ilikuwa ni jinsi gani ya kuikoa ndoa yangu,..’akasema

‘Yeye alikuambia hichoakikifanya ataiokoa ndoa yako, ..?’ nikamuuliza

‘Hicho kitu, kitasaidia mambo mengi tu, pamoja na hilo…’akasema, na kuendelea kusema
‘Kiukweli mimi na mke wangu tunapendana, na sitaki kuja kumuumiza mke wangu, sitaki watoto wangu waje kupata shida, wakiulizia baba yao yupo wapi, ni bora nife kabisa nijue moja…’akasema

‘Ni nini maamuzi yako mpaka sasa tusipotezeana muda hapa, maana nakuona akilini hufikirii mbali, hapo kila kitu kipo wazi,..?’ nikamuuliza

‘Mimi nina uhakika huyu rafiki yangu atanisaidia, alishanisaidia sana, na hili hawezi kunitupa,atapambana na hao watu, sasa tatizo ni pesa…’akasema

‘Sawa tatizo ni pesa, na wao lengo lao kubwa ni kupata pesa, na wameshakuambia pesa unazo unazikalia, sasa inuke wazichukue, hahaha, unajua wewe ni mjinga sana, unajua nikuambie, usipende kujifanya mjanja, kwa hili utaumbuka sana, hapa wameshakushika kubaya, utoe wakitakacho au wakuumbue, na kwa hali yako hiyo, huna ujanja…’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka

‘Kwanini unasema hivyo..?’ akaniuliza

‘Sio kitu…’nikasema nikiwaza kidogo, na yeye akasema;

‘Unajua huyo rafiki yangu aliwahi kuniambia mimi nakusaidia sana, lakini ipo siku utanikumbuka, utayakumbuka maneno yangu kuwa matajiri hawana wema, na ukiwa nao bora ujue njia ya kuwekeza mapema kabla hawajakufukuza, kwani kukuchoka kwao ni rahisi sana , na wao wana mbinu za kukutega, ili wakikuchoka tu wanakutema kirahisi…’akasema

‘Una maana gani hapo sasa, sijakuelewa mbona..?’ nikamuuliza

‘Hebu angalia hili tukio, unafikiri likifika kwa mke wangu itakuwaje, ina maana ndoa yangu hakuna tena, na mimi sina changu, maana kutokana na huo mkataba wetu wa kifamilia, ikipatikana ushahidi, hata kampuni yangu nitanyang’anywa, nitabakia mikono mitupu, na makosa ni ya kibinadamu tu,..wote tunakosea, mbona mimi nafahamu kuwa yeye ana mpenzi wake wa siku nyingi, lakini sina ushahidi,..’akasema hivyo

‘Kwa mawazo ya rafiki yako huyo, wewe uliyafanyia nini,maana unavyoongea ni kama  uliyakubali mawazo yako, ukamruhusu afanye anachotaka kukifanya bila kujali ni kitu gani,.. au sio,…sasa wewe ulichukua hatua gani..?’ nikamuuliza nikitaka nimfahamu zaidi.

‘Awali mimi sikumjali sana rafiki yangu, ..lakini siku zilivyozidi kwenda, naona ni kweli, matatizo yanazidi kuniandama, kila nikifanya kosa , najikuta kwenye wakati mgumu,..unajua kitu kingine huyu rafiki yangu hafanyi kazi bure bure, nina madeni mengi kwake, sijamlipa,...’akaniambia hivyo

‘Linaongezeka jingine la madeni,…hahaha,….kuna kitu anakufanyia kazi na hicho kitu kikikamilika hutakuwa hakuna tatizo tena, ni kitu gani hicho…wewe unasema hukijui, au sio, na huku una madeni mengi kwake, nab ado yanaongezeka, nab ado hujaelewa,…mjinga sana wewe…mimi sio mtoto mdogo, unasikia, sasa sikiliza..nijibu haya maswali yangu halafu nitakuambia ni kitu gani hicho…’nikasema

‘Maswali gani hayo tena…?’ akauliza kwa mashaka.

************

‘Hebu nikuulize huyo jinsi gani huyo mpenzi wako wa zamani, alikukubalia umuoe huyo binti tajiri?’ nikamuuliza mume wa familia tena hilo swali , sijui kwanini, nilihisi kuna maungano fulani hapo.

‘Alikubali, kwa shingo upande, tulikuwa hatuna jinsi, lakini alifanya hivyo, kwa vile, na yeye alishampata mwanaume mwenye mwenye nazo pia, kwahiyo tukaona tukubali ili na sisi tuyajue maisha ya kitajiri,  mimi nikamuoa binti mwenye hali nzuri, na yeye akaolewa na mume mwenye nafasi yake, na maisha yakaendelea nikijua kuwa pesa ni kila kitu...’akaendelea kunisimulia mume wa familia.

‘Kwahiyo kwa kauli hiyo inaonyesha kuwa huna raha na mke wako?’ nikamuuliza

‘Raha ya kipesa ninayo, lakini kwa mapenzi..mmmh…, yale ninayoyataka mie, unajua mke wangu ni mtu wa kazi, hana muda wa starehe, ndio maana nahangaika na watu kama nyie, ..lakini sio tatizo sana,  …tuyaache hayo, maana , kila mtu na uwalakini wake, ...unafahamu mke wangu hajali kuangalia hisia za wenzake, ndio tatizo lake jingine, yeye anaona utajiri ndio mapenzi yake,...’akaniambia

‘Nikuulize kitu, ina maana wewe na mpenzi wako wa zamani, huwa, mnakutana, mnaonana, au ulipo-oa mkakata wenu wa mahusiano…ndio mkawa hamuonani tena,ili kulinda heshima zenu, ili msije mkagundulikana kuwa mlikuwa wapenzi na bado mnapendana?’ nikamuuliza

‘Hili swali gani, hilo siwezi kulijibu, maana huko unakokwenda una nia ya kunichimba,huko unapokwenda hakuna maana usiniulize maswali ambayo hayatatusaidia kitu, sanasana ni kuniumiza moyo wangu, mengi yamepita na haya yaliyopo mbele yangu,yataharibu kila kitu,sema utanisaidia au niondoke, .?’akaniuliza

‘Mimi ninakuuliza hilo swali nikiwa na maana yangu muhimu, inawezekana huyo jamaa anashirikiana na mpenzi wako wa zamani, atakuwa anakufanyia hivyo kwasababu maalumu, ’nikawambia.

‘Hiyo hoja yako haina mshiko, yeye anifanyie hivyo ili iweje, ...ili nikose, nimuache mke wangu,  nikikosa yeye yeye atapa faida gani kumbuka tuliacha kuoana mimi na yeye kwasababu gani, ..na mali aliyo nayo yeye iende wapi, hapo umakosea, hiyo hoja yako haina mshiko...’akasema

‘Binadamu anaweza kukutwa na jambo, au kushawishika na jambo akilenga jambo fulani, na nyie mnaonekana akili zenu ni fupi…, au hata mume wake anaweza kumtumia kwa masilahi fulani, huwezi jua, ufahamu wewe upo kwenye sehemu ambayo kila mtu anaimezea mate, na kwa ajili hiyo, utegemee maadui wa nje na ndani...’nikamwambia lakini yeye akatingisha kichwa  kutokukubaliana na mimi.

‘Hapana yule hawezi kunifanyia hivyo hata siku moja, ananipenda sana, hawezi kuniumiza, kama ilivyo mimi, …tumeamua iwe hivyo, na tunaaminiana kihivyo, kwa vile tunafahamu wapi tulipotoka, kila mmoja ana mipango yake ya kimaisha na mwenza wake,tulishawekeana ahadi kuwa tusiingliane...’akasema mume wa familia.

‘Ina maana ulivyoniambia mimi kuwa unanipenda ulikuwa unanidanganya..?’ nikamuuliza na hapo akatulia ni swali ambalo hakulitegemea

‘Ok, sawa nimekuelewa, wewe ulitaka mtoto wa kiume, na sio mtoto wa kiume, bali hilo ni kizingizo, kuna zaidi ya hilo, ...na kwahiyo kwangu mimi, kwasasa kazi yako imekwisha, naomba tusijuane…umenisikia..’nikasema kwa ukali

‘Sio kwamba sikupendi, mimi nakupenda, lakini kila mmoja nampenda kwa nafasi yake, mke wangu nampenda kwa nafasi yake ya kwanza…, na ni mtu muhimu sana kwangu, ndio maana sitaki nimkose kwa hali na mali, na wewe nakupenda kwa nafasi yake, lakini mpenzi wangu wa zamani penzi lake ni la asili, siwezi kuliweka sawa na wengine…’akasema

‘Penzi lake ni la asili kwa vipi..?’ nikamuuliza

‘Hahaha, tatizo lenu hamfahamu mapenzi, penzi la asili kamwe halifutiki moyoni, hata iweje,..penzi hilo huwezi kulilinganisha na kitu chochote, na kama ikiwezekana, kama ikiwezekana zunguka kote lakini mwishowe mtakuja kukutana…’akaniambia

‘Kiukweli ulivyonieleza hapo, haya ya ulevi, kujifanya hupati mapenzi, kuhangaika huku na kule ni kwa vile akili yako bado ipo kwa mpenzi wako huyo wa zamni mpenzi mwenye penzi lako la asili, au sio..wewe ulikuwa unatafuta upate ili baadae mje kukutana na kurejesha mahusiano yenu, na wengine wakawa wanawatumia kufanikisha mambo yao..au sio?’ nikamuuliza

‘Kwani hayo, yatasaidia nini kwenye hili tukio, hivi hujafahamu hatari tuliyo nayo, hulioni hilo…’akasema

 Nilikaa kimia kiukweli mimi akili yangu ilishazama kumuwazia huyo mpenzi wake wa asili, sijui kwanini alitokea kumpenda hivyo, na kwanini akawa karibu na Makabrasha, na kwanini..nikahisi hawa watu wana kitu muhimu sana, na kupitia kwao nitaweza kugundua jambo, ambali litamaliza haya matatizo..

Sasa akawa anataka kuondoka, na kabla hasogeza hatua mbili, nikasema

‘Hebu subiri kwanza, ili tuelewane..nataka uniambia ukweli wako,..Ni nani huyo mpenzi wako wa zamani?’ nikamuuliza.

‘Siwezi kukuambia,…’akasema sasa akiwa anaondoka.

‘Sikiliza wewe si unataka tusaidiane kwa hili, kama kweli una nia hiyo, niambia huyo mpenzi wako ni nani…akili yangu inanituma huyu mpenzi wako wa zamani ana jambo na huyo wakili , ukiondoka hapa bila kuniambia hilo usirudi tena hapa, ..NI NANI HUYO MPENZI WAKO WA ASILI…

Hapo akasimama…taratibu akageuza kichwa kuniangalia.....

NB: Ni nani huyo mpenzi wake wa zamani, tukutane sehemu ijayo mungu akipenda tuombeane uzima na changamoto za kimaisha.WAZO LA LEO: Wapo wana ndoa wapo kwenye ndoa kwasababu ya mali, lakini ndani ya nafsi zao wana wapenzi wao wa zamani, waliowapenda sana, hata wakifany ajambo, wanakuwa kama wanalinganisha,.., hilo ni kosa kubwa sana, huko ni kumsaliti mwenza wako, tukumbuke kuwa mapenzi ya kweli yanatoka moyoni, tukijidanganya kuwa tunapenda eti kwasababu ya pesa, au mali, ipo siku hivyo vitu vyote vitakwisha, je ndio mwisho wa mapenzi yenu. Kama mumeamua kuoana kwasababu ya mali, au sababu fulani, basi jifunzeni kupendana kiukweli. Mungu atawasaidia na mapenzi yenu yatakuwa na baraka.
Ni mimi: emu-three

No comments :