Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, February 14, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-81




‘Je mume wa famalia, upo radhi wayasikie hayo mazungumzo yetu mimi na wewe, au utakubali makosa yako ili tusizidi kupoteza muda hapa…?’ akauliza mdada.

‘Wewe umekuja kutoa ushahidi, au sio, kutoa maelezo kwa ajili ya kujikosha, ili kurejesha hadhi yako, hajaitwa hapo, kumuhukumu mtu au kutoa maelezo ni nini mteja wangu afanye, timzi kilichokuleta hapo…’akasema wakili.

‘Na wewe umakuja kufanya nini, kujua ni ninikinachoendelea kwenye hiyo familia, na kukipeleka upande wa pili, au sio,..ushafahamika ndugu yangu, usipoteze muda wako wa maswali yya uchimbi…’akasema mdada.

‘Upande wa pili gani huo, usipoteze lengo..’akasema wakili

‘Unaufahamu sana, tatizo, nyie mnafikiri wote ni wajinga, hapa umeingia choo cha kike, kwa taarifa yako, na siku unaongea na bosi wako, siku ile nilikuwepo, hukuniona tu, hahaha…’akasema na kucheka, na wakili akawa namuangalia huyo mdada kama kumshangaa.

‘Hata sijui unachokiongea, tafadhali jibu maswali yetu na uache kupoteza muda, ndugu mwenyekiti, kwanini unamuachia huyu mtu apoteze muda…?’ akauliza wakili.

‘Kwani hayo aliyoyaongea mzungumzaji,sio kweli, tuambie umafuata nini humu..?’ akauliza mwenyekiti na wakili huyo sasa akashituka, na kugeuka kumuangalia mteja, kabla hajasema neno, na mume wa familia akasema;

‘Ndugu mwenyekiti huyu ni wakili wangu, nimemleta mimi mwenyewe, kwanini mnamzuia asifanye kazi yake..?’ akauliza mume wa familia.

‘Kwasababu wewe ni mjinga, hujui ni nini unachokifanya..’aliyeongea sasa ni mwenyekiti  kwa sauti ya hasira.

‘Mwenyekiti, tafadhali,…’akasema mume wa familia, na mwenyekiti akasimama, na kuja hadi pale nilipokaa, akaninongoneza jambo, na alichoniambia kikanifanya nianze kuingiwa na hasira na zaidi ni mashaka kwa mume wangu, nikageuka kumuangalia mume wangu,.alikuwa hajali kabisa, nikabakia kusikitika tu, sikusema neno, na baba akarudi kwenye kiti chake na kabla hajakaa vyema, ....

‘Kama hamtaki niwepo kwenye hiki kikao chenu mimi ninaweza kuondoka…’akasema huyo wakili

‘Hilo ni juu yako wewe na aliyekuleta hapa, sisi hatuna wasiwasi na hilo, ila ni kukuarifu tu, kuwa tunakufahamu, sio kwamba nilikuwa sikujui kabla, ila mzungumzaji amejaribu kuliweka hilo wazi mapema, kabla ya muda wake, sawa wewe fanya ulichotumwa, na waliokutuma, lakini ufahamu kuwa tunakufahamu wewe ni nani..’akasema mwenyekiti, na yule wakili akawa sasa anakusanya vitu vyake kutaka kuondoka.

‘Unataka kwenda wapi wewe, mimi ndiye niliyekuleta hapa, sio wao, wao wanafanya hivyo ili kukuvuruga akili yako, wewe hulioni hilo, ina maana wewe hujawahi kukutana na kesi kama hizi, mimi nilikuwa nakuaminia sana, mbona unanivunja uaminifu wangu kwako, usiondoke tafadhali..’akasema mume wa familia.

‘Tatizo ni usalama wangu, kama wanafamilia hawa hawaniamini, je likitokea tatizo hapa itakuwaje, utaweza kunilinda, huyu mdada keshawalisha sumu hawa wanafamilia dhidi yangu na wamemuamini, hawajui kuwa huyu dada ni ndumila kuwili tu, hamfahamu vyema, nimeshawahi kupambana naye kwenye kesi nyingi mahakamani, yeye ndio zake hizo,…’akasema wakili, na mdada akasema;

‘Unataka nitoe ushahidi kuonyesha mimi na wewe ni nani ndumila kuwili, ...hahaha, kume unanifahamu, kwenye kesi hizo ni nani huwa anashinda...nikuambie ukweli, hapo nilikuwa naanza tu, kuwaonya wanafamilia hawa, kuwa humu ndani yupo mzamizi, au ‘intruder,..’ kwa msisitizo,  mimi namfahamu sana huyu mtu, maana hiyo ndio kazi yangu, na pamoja na hayo yaliyotokea, mimi bado nawajibika kwa hii familia mpende msipende…’akasema.

‘Tuendelee na kikao chetu, hilo haliwezi kusimamisha sisi kuendelea na kikao chetu, hiki ni kikao halali na tunachifanya hapa ni halali, hatuna shaka, tuendelee…’akasema mwenyekiti, na mkewe akawa anamnong’oneza jambo mwenyekiti, na walipomaliza kuteta, mwenyekiti akasema;

‘Wakili unaswali la kumuuliza mzungumzaji, kabla hajaendelea na maelezo yake, usiwe na wasiwasi endelea na kazi yako tu, sisi ni watu wema, mambo ya kisiasa hayaweza kutufanya tuwe maadui, wewe ni mmoja wa wapiga kura wangu, lazima nikulinde, tuendee, ..’akasema mwenyekiti,

Wakili yule kwanza akamuangalia mwenyekiti kwa makini baadae akasema;

‘Sawa kwa vile bado mteja wangu ananitaka niendelee na kazi yangu, nitaendelea tu, ila nawaomba mnielewe, mimi ni wakili, na kazi yangu ni kwa mtu yoyote sijali kuwa huyu au yule yupo upande gani, ninaweza nikawa na watu wa kufanyia kazi , na watu hao wapo chama tofauti na huenda kisiasa ni maadui, mimi sitajali utofauti wao, ninachojali mimi ni miiko ya kazi yangu …’akasema

‘Sawa tumekuelewa, hamna shida…’akasema mwenyekiti

*************
‘Mimi bado nilikuwa na swali kwa mzungumzaji, ni kwanini hataki kuwataja, wale waliomshauri yeye kufanya hayo anayosema aliyafanya kwa mashinikizo, ikiwemo ushauri, kama nia ya familia ni kusuluhisha na kuweka mambo yawe sawa kwa kila mwanafamilia, basi ni bora kila mtu akafahamu makosa yake, kama wengine wataogopwa, sizani kama tutaweza kulifikia hilo lengo…’akasema wakili
‘Najua ni kwanini unataka niwataje …’akasema mzungumzaji
‘Vyovyote unavyojua wewe, lakini wajibu wangu ni kumtetea mteja wangu, yeye umemchafua sana kwa lugha tofauti, na yeye ana haki ya kujilinda, na kupambana na wale wote wanaotaka kumharibia jina lake, sasa ni kwanini hutaki kuwataja hao watu waliokushauri, unawaogopa, au kuna sababu gani..?’ akauliza wakili huyo.

‘Nimekuambia hivi, hapa nina ushahidi, na kuna ushahidi na mambo mengine yatatekelezwa baadae kama alivyosema mwenyekiti, kuwataja hao, ni kutoa ushahidi ambao bado muda wake,..na sio kwamba naogopa kuwataja, hapana ,mimi ndiye mtoa maelezo, na mimi ndiye ninayefahamu mpangilio wa malezo yangu , huwezi kunilazimisha niongee utakavyo wewe..’akasema rafiki yangu.

'Sio nitakavyo mimi, bali ni utaratibu wa kuelezana ukweli, ili kila mmoja ajibaini kosa lake, hatuwezi kumzonga mtu mmoja tu, kumbe na wengine wana makosa yao...'akasema wakili

Aliposema hivyo, wakili akamgeukia mwenyekiti, na mwenyekiti akawa kimia, alikuwa akiandika jambo, na kabla mwenyekiti hajasema neno, wakili huyo huyo akasema;

‘Haya endelea, ila umetufanya sisi tuelewe kuwa hapa kwenye hiki kikao, kuna watu wanaogopwa, hata kutajwa majina yao, kuna upendeleo, kuna shinikizo linatakiwa kufanyika dhidi ya mteja wangu, na yeye ana haki ya kujitetea…’akasema wakili

‘Endelea na maelezo yako mzungumzaji…’akasema mwenyekiti.

‘Samahani ndugu mwenyekiti, ningelipenda kukuliza hili, je nimekosea kuuliza maswali kama hayo ya kumtetea mteja wangu…?’ akauliza huyo wakili, na mwenyekiti akamuangalia kwa mshangao, halafu akasema;

‘Labda kwa kukusaidia tu, hapa nina mawakili wawili je umewaona  wakiuliza maswali…?’ akaulizwa na akageuka kuwaangalia hao mawakili, halafu akasema;

‘Mimi siwezi kufahamu ni kwanini wapo hapa..., labda mna utaratibu wenu, lakini mimi nimeitwa hapa na mteja wangu siwezi kukaa kimia,ni lazima nitimize wajibu wangu, je kwa kufanya hivyo nimekikosea kikao..?’ akauliza.

‘Hujakosea, …ila nilitaka kukuweka wazi tu, ..’akasema mwenyekiti

‘Sawa tuendelee, au sio mteja wangu…’akasema wakili sasa akimuangalia mume wangu ambaye alikuwa kainamisha kichwa chini, na hakumjibu wakili wake, akamuashiria, jambo, sasa wakawa wanateta, baadae mume wa familia akasikika akisema

‘Muulize swali huyo mdada anayejifanya kujua kila kitu, ..’akasema mume wa familia, na wakawa kama bado hawaelewani, na baadae wakili huyo akasema;

‘Nina weza kuuliza maswali mengine muheshimiwa mwenyekiti..?’ akauliza wakili.

‘Mimi naona tunapoteza muda, na kama ulivyosikia kwa mzungumzaji ana mambo mengi ya kutuelezea, na sisi tunajali maelezo ya kila mtu, ilimradi yawe na nia njema na familia hii, na labda tuendelee naye kwanza, nitamuongoza kwa swali hili ili kufupisha mambo mengine..’akasema mwenyekiti akimuangalia huyo mzungumzaji:

'Kwa ushahidi wewe mara nyingi umeonakana na mume wa familia, mkitembea naye, mkinywa naye na hata ukawa anafika kwako usiku, na hata kulala, halafu unakataa kuwa hakuwa mpenzi wako kabla...hapo sio kwamba kuna ukweli unatuficha sisi...'akauliza mwenyekiti

Na wakili akataka kuingilia hilo swali, lakini mwenyekiti hakumpa nafasi, akawa anamuangalia mzungumzaji

'Labda niwaelezee hivi, awali kabisa mimi nilikuwa namuogopa sana shemeji yangu huyu, sio kumuogopa kihasa, hapana nilikuwa namuheshimu, kama nilivyosema awali mimi awali nilikuwa naishi na familia hiyo..’akasema

‘Na kama shemeji, ni lazima nimuheshimu mume wa dada, mume wa bosi wangu, na kwa hiyo nikawa na mipaka yangu,…, sikuwa na ukaribu sana na yeye, yeye ndio alifanya juhudi hizo za kuondoka huo uwoga wangu, alikuwa anajitahidi sana kunifanya nisimuogope, na haya hayakuanzia nje, yalianiza hata nilipokuwa naishi nao...'akasema.

‘Inategemea na jinsi ulivyokuwa unajiweka, huenda tabia na mienendo yako ilimfanya afanye hivyo…’akasema wakili kabla hajaruhusiwa kuongea

‘Afanye hivyo nini..?’ akauliza mzungumzaji

‘Hivyo ulivyosema wewe, kuwa alijitahidi kuondoa uwoga huo, na ni kawaida mtu mkiishi pamoja, utafurahi wote wakiwa sawa, je kama angelikuwa mkali tu, ungelimfikiriaje, sema ukweli wako kuwa, hata wewe ulikuwa ukimtamani, na hilo sio nazusha, kwa kauli yako ulishasema, wewe ulikuwa ukiwapenda, waume za watu, hasa huyo shemeji yako…’akasema wakili na maneno hayo ya mwishi, ‘’hasa shemeji yako’ akayakazia zaidi.

‘Ukweli hauwezi kujificha, muulize mke wa familia, pamoja na haya yaliyotokea hatashindwa kuusema ukweli kuhusu tabia yangu nilivyokuwa nikiishi nao, je mimi nilivuka mipaka yangu ya ushemeji,…’akasema

Mimi sikuwa tayari kusema neno nikabakia kimia tu.

‘Yeye hawezi kukuchunguza wakati wote, je alipokwua hayupo, labda ndio ulikuwa unafanya hivyo kuigiza wema akiwepo, akiondoka wewe unakuwa mtu mwingine, ipo hiyo, na hayo yamejidhihirisha pale ulipopata mwanya, ulipoweza kuishi kwako, ukawa unamvuta mume wa familia, hadi mkawa mnakula wote, mnakunwya wote, je kama mwanaume unafikiri yeye angalifanya nini eeh,,kwahiyi bia na mienendo yako ndiyo kishawishi …’akasema wakili.

‘Labda nielezee hapo …maana umenipeleka sehemu ya mbali ambayo nilikuwa bado sijataka kuilezea…’akasema mzungumzaji

'Ujue kuwa ofisi yangu ninapofanyia kazi ipo karibu sana na ofisini yake na katikati yetu, kuna hoteli kwahiyo nikitoka kwenda kula chakula cha mchana, ninapita kwenye ofisi yake, sasa bwana huyu alikuwa kama ananisubiria, kila nikipita hapo yeye anakuja kwa nyuma, au tunaongozana naye… je ningelimfukuza, shemeji yangu,…eeh..'akasema

‘Endelea kuelezea, ulivyomnasa…’akasema wakili na hapo mwenyekiti akaingilia kati na kusema

‘Tafadhali wakili, tufuate utaratibu, tumuache mzungumzaji aendelee na ikifiki seehmu ya maswali tutakupatia nafasi, tafadhali muheshimiwa…’akasema mwenyekiti.

‘Sawa muheshimiwa mwenyekiti,..tupo pamoja…’akasema wakili, na wakawa wanateta na mteja wake, na mdada akawa anaendelea kuongea;

'Kwahiyo ukaribu huo, na kuonekana hivyo ndio maana watu wanafikia kusema mimi nilikuwa rafiki yake kabla na mimi kama mwanamke nilishamfahamu mapema huyo shemeji yangu ana lengo gani kwangu,..namuheshimu, na ni sheemji yangu,..hata hivyo mimi sikutaka kumzalilisha, au kujizalilisha kwake, nilimpa nafasi yake kiheshima...'akasema.

'Una uhakika kuwa, wewe hukulifanya hilo kama mtego, kuwa upate ushauri kutoka kwa watu wako wa karibu, na uutumie huo ushauri kama chambo, ili iwe kisingizio, baada ya wewe kuwa mumeshajuana na mume wa familia, na inaonekana mlikuwa na sehemu mnakuatana naye kwa kificho, kwa ndugu yako mmoja..ushahidi huo upo..'aliyeongea sasa ni mama, na mwenyekiti alitaka kumzuia lakini mama alishauliza hivyo.

'Najua hilo litakuwa limejulikana hivyo, na sio kweli kuwa sehemu hiyo tuliitumia kwa nia hiyo, hapana, yeye mwenzangu ndiye aliitumia sehemu hiyo baada ya kushindwa kila namna, akamtumia ndugu yangu huyo, ili yeye afanikishe mambo yake, hapo kwa ndugu yangu alipotumia kama moja ya mitego yake..’akasema

‘Tatizo ni kuwa, yeye hakufahamu kuwa kila wanachopanga na ndugu yangu huyo, ndugu yangu huyo alikuwa akiniambia, yule ndugu yangu ni mtafuta pesa, akajua hapo ni sehemu ya kuchuma, cha mjinga huliwa na nani...'akasema mzungumzaji

'Je tukimuita huyo ndugu yako akausema ukweli, huoni kuwa hayo yote uliyoongea yataonekana ni uwongo..?' akauliza wakili wa mume, na akaongeza kusema;

‘Samahani mwenyekiti imenibidi niulize hilo swali kuongezea swali la mama, natumai sijakosea..’akasema

‘Sawa…’akasema mwenyekiti.

'Muiteni huyo ndugu yangu, hamna shida kabisa,.., nashangaa kwanini hakuitwa hapa kama shahidi..tunao ushahidi wa kuwa sehemu hiyo ilikuwa ni sehemu ya mume wa familia, kufanyia madhambi yake na hilo mkitaka naweza kuwaonyesha sasa hivi, kuna mitego mingi humo, kuna ushaidi mwingi humo, na ndio maana nasema huyo mume wa familia hawezi kukwepa lawama hizo kuwa yeye ni Malaya, tofautio na anavyotaka kutuchafulia sisi …'akasema akimuangalia mwenyekiti.

'Huyo mume wa familia, ana mengi, waulizeni hata wahudumu wa hotelini na bar, alizokuwa akilewa, waulizeni watakuambia ukweli kumuhusu yeye, na sitashangaa nikisikia pia yeye ana mtoto mwingine na wahudumu hao..’akasema na watu wakaguna.

‘Mnaguna hilo, ina maana hamjui…hahah, akane tukamuite huyo mdada na mtoto wake, tatizo ni kuwa damu yake ni kali sana, haweza kujificha, nashangaa kama hilo nalo hamlifahamu, hahaha, huyo ni kidume cha mbegu, msione kampuni inafirisika mkazani ni maeni ya kikazi tu,…ameyataka yeye mwenyewe, ulizeni maswali zaidi ili niweze kufichua uovu wake...'akasema

'Inasadikiwa kuwa wewe lengo lako na mume wa familia ni kuhakikisha kuwa mkataba huo wa kugushiwa unafanikiwa ili wewe uje kuoana na huyu mume wa familia, na hata usipofanikiwa, unajua kuwa mume wa familia atavunja ndoa yake, na wewe utachukua nafasi ya mke wa familia na kuendeleza yale mliyoyaanza hilo ndilo lengo lako, maana wewe umshakiri kuwa kweli unampenda,  kweli si kweli..'akauliza mama

‘Hilo swali lilishajibiwa…’akasema mwenyekiti, lakini mdada akaendelea kuelezea

'Hiyo sio nia yangu, yeye ndiye alikuja kunitamkia hivyo, kama mnataka ushahid upo mtasikia kauli yake yeye mwenyewe, akisema hivyo kuwa lengo la mume wa familia nikuwa mkataba utampa yeye mamlaka, kwahiyo anaweza kunifanya mimi mke wake, kama mke wake atafiki mahali pa kutaka wao waachane, lakini nikaja kugundua kuwa hiyo ni moja ya lugha zake kwa wanawake wote anaowataka,...'akasema.

‘Kwangu mimi alikuja kwa mbinu hizo mapema, akinitaka, nikaona sasa amekwenda mbali, nikampasha ukweli, kuwa asinione mimi nipo karibu naye, na asinione mimi najipendekeza kwake kwa namna hiyo, mimi sio mhumi, nilimwambia wazi wazi kuwa mimi nawaheshimu sana waume za watu, na sitatembea na mume wa mtu abadani, muulize kama kweli anataka kusema ukweli…’akasema.

‘Na hata huko kulewa kupitiliza, alikuja kuniambia kuwa moja ya sababu inayomfanya alewe kupiliza ni kwasababu mimi nimemkataa na ananipenda kiasi kwamba hawezi kukaa mbali na mimi, na anapenda kila siku niwe naye, na zaidi angelipenda mimi niwe mkewe wake..’akasema na wakili akataka kuongea

‘Muulizeni yeye mwenyewe kwanza, asimtumie wakili, akatae yeye mwenyewe kwa kinywa chake..’akasema rafiki yangu akimwangalia mume wangu

Mume wangu hapo akainua uso wake na kucheka kicheko cha dharau, utafikiri linaongewa jambo la maana sana kwake, hakufahamu jinsi gani nilivyokuwa naumia.

‘Basi akawa analewa kiukweli, mwanzoni nilijua ni mbinu zake, tu, lakini akawa analewa mpaka anakuwa ni mtu wa kubebwa, na wakati mwingine tunakuwa pamoja naye, mimi sinywi kihiyo, kwahiyo ikawa tunafanya kazi ya kumbeba mimi na ndugu yake, na akilewa ndio anabwabwaja ukweli, kuwa kulewa kote ni kwasababu yangu,....anasema siku nikimkubalia tu ombi lake ataacha kabisa kulewa.

‘Hali hiyo ikawa na mimi inanitesa, kwani kimoyoni kiukweli, nilitamani nifanye hivyo ili aache pombe lakini sio kwa kuvunja udugu wetu,, na ibilisi ana nguvu sana, kuna muda nilitamani basi labda awe ni mpenzi wangu wa siri, au nyumba yake ndogo, kama alivyotaka yeye, lakini bado nafsi yangu ilinisuta…haya nayaongea kutoka moyoni…’akasema.

‘Nilijaribu sana kumfanya rafiki yangu anielewe kuwa mume wake yupo hivyo, kabdilika na kubalika huko kuna mengi, huenda chanzo kinaweza pia kutoka ndani yao wao wenyewe..kwa kujali kazi zaidi kuliko ndoa yao, lakini hata nilipotumia lugha ya busara kwake, niliona kama ananiona mtoto mdogo nisiyejua mambo ya mke na mume..’akatulia

‘Ina bidi hili niliongee hivyo, sio kwa kujitetea… samahani kwa hilo, ila ndivyo livyokuwa..’akasema

‘Hebu kidogo, unasema yeye alisema kuwa kaanza kulewa hivyo kupitliza kwa vile wewe hukuweza kumkubalia matakwa yake, kwahiyo kulewa kwake sio kutokana na mambo ya kifamilia…?’ akaulizwa

‘Jibu analo yeye mwenyewe, ila kwa kauli yake kwangu aliwahi kutamka hivyo, kuwa kaamua kulewa hivyo kwa vile mimi nimemkatalia..na atakuwa tayari kuacha pindi nikimtimizia matakwa yake…’akasema mdada

‘Wewe ni mwongo, sio kweli, kulewa kwangu kuliwa na mambo yangu mengi, ambayo hayakuhusu…’akasema mume wa familia.

‘Naona huko sasa kunatosha, …’akasema mwenyekiti alipoona wakili ananyosha mkono kuuliza swali

‘Inatosha, mzungumzaji, nataka uendelee, lakini sasa hivi ili tusipoteze muda, unaonaje ukituelezea ukweli hasa…maana uligusia kuwa mimba hiyo hukuipata kwa jinsi ulivyodhamiria, ilikuwaje.. hujatuambia uliipataje hiyo mimba..?’ akuliza mwenyekiti,…’akaambiwa

‘Sawa nilipanga kuja kuliezea hilo kwenye mpangilio wangu, …’akasema akimuangalia mwenyekiti, na mwenyekiti akaangalia saa, halafu akaniangalia na mimi, mimi nilikuwa kimia, nikiwaza hili na lile, na nilipoona mwenyekiti ananiangalia mimi nikasema;

‘Mwache aelezee, nataka kufahamu kila kitu..’akasema mama baada ya kuniona mimi nipo kimia

‘Ni kweli kwua tukio hilo lilikuja baada ya kupata ushauri kutoka kwa watu wangu wa karibu, lakini sio kwamba nilikuwa na dhamira ya kufuata ushahuri huo, sio kwamba ilikuwa ni moja ya mtego wa kulifanikisha hilo..mtakaoelewa vibaya shauri lenu.’akasema

‘Siku hiyo kulikuwa na sherehe, na mume wa familia kama kawaida yake akazinywa pombe kama anashindana nazo, na mimi siku hiyo sijui ni kwanini na mimi nikanywa tofauti na siku nyingine...’akasema na kumtupia jicho wakili akitegemea nen o kutoka kwake, lakini wakili hakusema kitu,

‘Ulevi ni mbaya jamani…hapo mojaikazaa jingine, tulijikuta tupo kwangu,...na usije ukasema nilipanga mimi iwe hivyo, hapana, na wala sikujua kuwa itatokea hivyo, na hiyo sherehe, mimi sikupenda kuwepo, kuna mambo yalitokea mpaka nikajumuika....ilikuwa hivi…

Baada ya kunywa kwenye hiyo sherehe na tukawa hata kutembea inakuwa shida, aliyefanya kazi ya ziada kutusaidia alikuwa mdogo wa mume wa familia, alituchukua hadi nyumbani kwangu, tulipofika kwa vile nimelewa, nikawa sijui ninachokifanya, nilitaka mimi nikalale wao waondoke…hawakutaka kufanya hivyo.

‘Japokuwa nilikuwa nimelewa lakini bado nilikuwa na ufahamu wangu, mimi sipo hivyo, siendekezi kulewa mpaka akili ibadilike, najiheshimu, najua ni nini ninachokifanya, …sasa kilichotokea ni kuwa nilipotoka kwenda kujisaidia, nilichelewa kidogo, kuhakikisha nimesafisha tumbo, najua jinsi gani y akufanya kuondoa ulevi mwilini,..nikarudi, sasa nikiwa sijambo

‘Una maana gani kusafisha tumbo..?’akaulizwa

‘Niliweka kidole kooni na kujitapisha, labda niseme hivyo mpate kunielewa, kwenye kazi zetu hilo linaruhusiwa, ili kufanikisha mambo…’akasema

‘Endelea…’akaambiwa

‘Nakumbuka wakati narudi, niliwaona ndugu wawili wakiongea jambo..’akasema

‘Ndugu wawili nani na nani…?’ akaulizwa

‘Mume wa familia na mdogo wake…yule ambaye yupo karibu sana naye,..’akasema

‘Ina maana siku hiyo wote walikuwepo…?’ akaulizwa

‘Ndio, ndugu zake wote wawili walikuwepo..’akasema

‘Duuh…’aliyesema hivyo ni mama watu wakacheka

‘Mama sio kwamba…’akataka kujitetea

‘Endelea,…mama hana maana hiyo..’akasema mwenyekiti

‘Waliponiona wakaacha kuongea, maana huyo ndugu yake alikuwa kakaa upande mwingine, akaondoka pale kwa kaka yake na kwenda kukaa sehemu ambayo likuwepo awali,… pale pale nikahisi kuna jambo, mimi kama mpiganaji nikahisi hivyo, nikaona nijihami..lakini kama unavyojua tena kilichopangwa kutokea kitatokea tu,..

‘Mimi muda ule, hata nilipofika pale sikutaka kuendelea kunywa pombe, nilikuwa nakunywa kinywaji cha kawaida, nilishawaambia mimi imetosha sitaki kunywa tena pombe

Wakati nakwenda kujisaidia, niliacha chupa nusu…kwa muda ule sikuwa na wazo baya kuwa inawezekana wakafanya hivyo, sikuwa na shaka na hilo, nilikuwa nawazia mengine kabisa, ya kujihami,..pale kwa taratibu nikamimina na kunywa maana hapo nilikuwa na kiu…nikanywa fundo moja, la pili, ndio nikahisi tofauti.

‘Hii soda ina nini…imeharibika nini…mbona haikuwa hivi kabla’nikasema nikitamani kutema lile fundo jingine lilikuwa mdomoni…

‘Umelewa wewe….’akasema ndugu wa mume, wakawa wanacheka na kunitania, hawakufahamu kuwa mimi nilishajipunguzia ulevi kichwani kiasi fulani.

‘Hapana nina shaka na hii soda…’basi nikaiweka pembeni, nikachukua nyingine, ilikuwa imefunguliwa pia, nikaanza kuinywa

‘Mbona zote zipo hivyo…’nikasema na wao wakawa wakinicheka, ikawa ni utani tena, .. tukatulia, sijui kwanini nikaendelea kuinywa ile soda, baada ya mazungumzo, utani, kucheka..ooh, nikahisi tofauti, mwili ukawa umelegea, …nikawa sasa sijatambui kabisa.

‘Nyie kuna kitu mumenif-fa-fa-nyia…’nikasema hivyo tu, yaliyofuata hapo ilikuwa kama ndoto kwangu…, ‘akasema

‘Una uhakika kuwa sio ulevi wa kawaida, uliokufanya hivyo…?’ akaulizwa

‘Hapana mama,…nilishajiflashi…nilifanya kama nilivyosema awali, na nilirejea pale niliwa sina ulevi..sio kwamba ulikwisha kabisa,lakini kwa kiasi kikubwa mimi nilikuwa nipo sawa,…’akasema

‘Oh, ikawaje sasa…?’ akaulizwa

‘Baada ya hapo nikawa hata kuinua mkono siwezi, akilini nikajua kabisa kuna kitu wameniwekea kwenye ile soda, na kiukweli kilichoendelea hapo ilikuwa kama mtu upo kwenye njozi ya ukweli,…ndio hapo wakafanikisha malengo yao..’akasema

‘Waka..ina maana wote..?’ akaulizwa

‘Mama, hapo sijui mimi, lakini sio wote kama ninavyosema ni ..ilikuwa kama ndoto, niliyemuona ni huyo mume wa familia, kwasababu walisaidiana kunibeba hadi chumbani kwangu,..nasemea hivyo, kwa vile nilipoamuka nilijikuta nipo chumbani kwangu…’akasema

‘Kwahiyo hukujua kuwa wao walikubeba hadi chumbani kwao..?’ akaulizwa

‘Sikujua,,..ila nilijua kuna kitu wamenifanyia…’akasema

‘Je una uhakika kuwa aliyekufanyia hivyo ni mume wa familia…?’ akaulizwa

‘Ninaweza kusema hivyo, kwa vile nilipoamuka nilimkuta kitandani tukiwa tumelala naye…’akasema

‘Swali una uhakika kuwa ndiye aliyekufanyia hivyo, maana hapo walikuwepo wote, na watoto wanafanana na ndugu hao, akiwemo mume wako, ndugu hao wote wanafanana..?’ akaulizwa

‘Uhakika huo,…kinjozi, nakumbuka ni yeye,…lakini siwezi ..’akatulia

‘Kwa ufupi huna uhakika,…’akasema wakili wa mume.

‘Lakini kwa mara ya pili nilikuwa na uhakika huo…’akasema

‘Ohoo, kumbe kuna mara ya pili, kumbe sasa ilikuwa ni fungulia njia, muonja asali sio..’akasema mama

‘Hapana sio kwamba baada ya hapo niliona ni jambo sahihi, au nilijilegeza kwake, hapana kiukweli baada ya tendo hilo, tulikorofishana sana, mpaka nikataka kuwashitaki, wao kwa pamoja walikuja kuniomba msamaha, …nikaona basi tena, ni ulevi yaishie hapo tu, ila baada ya kutokea mara ya pili, tulifka kubaya, waulize kama ni nini nilikifanya,…’akasema

‘Sio kwamba ulifurahia, ndio maana ikatokea mara ya pili…’akasema mama

‘Hapana mama, sio mimi…na sio kwa njia hio, hivi hapo kuna starehe gani, ..hakuna chochote cha kufurahia, ni kunizalilisha tu, na kama nilivyowahi kusema haya mambo yana mkono wa mtu wa tatu, sio bure, haya yalipangwa yafanyike hivyo, na kama mume wa familia atakuwa mkweli tunaweza kulithibitisha hilo…’akasema

‘Ok, ikawaje…?’ akaulizwa

 ‘Nilikuja kuzindukana usiku nahisi ilikuwa ni saa tisa hivi,…bado mwili wangu hakuwa sawa, lakini nikajitahidi, nikatafuta dawa yangu maalimu ya kuondoa sumu mwilini…nikainywa, nilitapika sana…baadae nikawa safi.

*************
 ‘Kwahiyo ulikunywa hiyo dawa ya kuondoa sumu wakati gani..?’ akaulizwa

‘Nilipoamuka tu, nikakimbilia chooni, nikanawa, na nilipoona bao sipo vizuri,nikaelekea sehemu ninapoweka dawa zangu za zarura kama hiyo nikanywa, na kurudi chooni,…’akasema

‘Ndio baadae nikarudi chumbani na kumkuta mume wa familia kalala kitandani,..’akasema

‘Alikuwaje…yaaani alikuwa kava au  yupo uchi…?’ akaulizwa

‘Yupo uchi…’akasema na watu wakacheka kidogo.
‘Kwahiyo ukawa na uhakika kabisa kuwa tendo lilifanyika,..?’ akulizwa

‘Ndio…’akasema

‘Utakuwaje na uhakika wakati ulikuwa hujitambui, je kumuona akiwa kalala hapo kitandani kwako kutawezaje kulithibitisha hilo…?’ akauliza wakili.

‘Nimekuambia mimi mwenyewe nilihisi kuwa nimefanyiwa jambo, pia usiku ilikuwa kaam naota nafanyiwa hivyo, ..nabakwa, au nisema hivyo…’akasema

‘Na nani..una uhakika ni nani..?’ akaulizwa walili

‘Unajua unataka nijibu utakavyo wewe…viashiria vyote vinaonyesha kuwa ni mume wa familia…’akasema.

‘Haya ikawaje…?’ akaulizwa

‘Nilipomuona huyo mtu kwanza niliogopa, nikawazia mbali, nikamuwazia rafiki yangu, kiukweli, nilihisi dhambi, nilihis kukosa, japokuwa wao walinifanyia hivyo bila idhini yangu…kwa haraka nikamuamusha, nilipoona hasikii nikachukua maji kumwagia, akazindukana, kwa hasira,..’akasema

‘Nilipandisha hasira, nikawa nafoka, mpaka mwenyewe akajua kweli nimekasirika, kwa haraka nikamwambia atoke chumbani kwangu…ili kuwa ni hasira kweli mpak ndugu zake wakaja kuamua ugomvi huo.

‘Hata hivyo hakutaka kuondoka, ikawa ni kazi kwa ndugu hao kumshawishi huyo mwanaume ili waondoke, wakaongea wenyewe baadae akakubali kuondoka, kwahiyo hapo nyumbani akachukuliwa na ndugu huyu mdogo sikujua kuwa ndugu huyu mwingine alibakia,..mimi nikarudi kulala, nikijua wote wameondoka, kumbe huyo mmoja alibakia , akaja kuingia chumbani kwangu, wakati huo nipo usingizini, nashtuka mtu huyu….

‘Unataka nini,..?’ nikamuuliza, akasema kaambiwa na kaka yake abakia kulinda usalama, wangu

‘Ondoka ndani kwangu haraka..’nilimwambia hivyo na jinsi alivyoniona nilivyoksirika, aliondoka.

Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza, kutendekea hilo na huyo mtu,  hata hivyo sijui kama ni shetani, au ndio ilipangwa hivyo, ikatokea tendo hilo siku nyingine, wakanitegea hivyo hivyo..nilikuja kugundua kuwa kumbe walikuwa wakiniwekea madawa fulani ya kulevya..ukiyanywa unaweza ukafanya mambo ukiwa hata usingizini, kama vile mtu anayeota huku anatenda jambo, na walisema yanaitwa phencyclidine, au jamii ya hizo…,’ akatulia.

‘Unasema ukinywa unafanya mambo kama unaota…mmh, kumbe, nakumbuka hali hiyo ilikuwa ikitokea kwa mume wa familia, naanza kupata picha…’akasema mwenyekiti…na akauliza swali jingine

‘Uligunduaje hilo…?’ akaulizwa

‘Niligundua hilo baada ya tukio hilo la pili, mimi nilichukua mabaki ya kinywaji kile na kwenda kukipima, na kilipopimwa, kinywaji kile kikaonekana kina madawa hayo ya kuelvya, nikaandikisha kumbukumbu kama ushahidi, siku zikaenda nikawa nimeyaacha hayo matukio kama yalivyo.

Baada ya mwezi kupita, na  nusu hisi nikahisi sipo sawa, nikajua ni malaria, nikatumia dawa, lakini ile hali haikuisha, nikaone nikamuone dakitari, sikwenda hospitali ninapojulikana, ndio nikaja kugundua nina mimba...’hapo akatulia na kumwangalia mwenyekiti ambaye alikuwa mara kwa mara akiandika kitu kwenye makabrasha yake kama vile ananukuu hayo yanayoongewa.

‘Sasa kwanini hukushitakia, ukijua kuwa madawa hayo ya kulevya ni haramu, hayaruhusiwi au wewe unatumia hayo madawa ya kulevya…?’ akaulizwa

‘Sababu kubwa ni kuwa nimepata kile nilichokitaka japokuwa sio kwa njia niliyoitaka..si ndivyo unavyotaka mimi niku jibu hivyo..’akasema na kuuliza.

‘Aaah, jibu unajua wewe mwenyewe, inavyoonekana ndio hivyo…’akaambiwa

‘Kiukweli kuwa na mimba nilikuwa nakutaka sana, lakini, tatizo ni jinsi gani nilivyoipata, sio njia sahihi, kiukweli ilinipa shida,…’akasema

‘Utakuwa na uhakika gani, kwani ina maana muda wote huo hukuwahi kutemeba na wanaume wengine..?’ akaulizwa

‘Mimi sina tabia ya uhuni, ni tofauti na watu waanvyoniona, kama nilivyosema awali ukiniona na wanaume nipo kazini, au napoteza muda tu..kwahiyo kipindi chote hicho sikuwa nimewahi kukutana na mwanaume yoyote, kwani baada ya matukio hayo mawili kulikuwa na kazi nyingi sana, …’akasema

‘Tutakuwa na uhakika gani..?’ akaulizwa

‘Uhakika kwa vipi…maana mimi ndiye ninayesema, na hapa ni ukweli mtupu n au uhakika gani mwingine mtoto si huyu hapa, muangalieni mniambie hii sura ni ya nani…’akasema

‘Labda ni hao wadogo zake mume wa familia, na pili ni kwanini hukushitakia, hapo kuna kitu umetuficha…’akaambiwa

‘Lakini mimi niliona hata nikisema bado nitaonekana mimi ni mkosaji, moyoni nikasema itakuwa siri yangu, na sikutaka tena kuwa karibu na hao watu nikajitenga na hao watu kabisa…’akasema

‘Hao, watu ina maana ulikuwa na wanaume wengu au sio…’akaambiwa

‘Wewe wasema,… nikisema hao watu, ni hao niliokuwa napenda kwenda kustarehe nao, akiwemo mlengwa, yaani mume wa familia..muulizeni, asema ukweli kama hayo hayakutendeka,..yeye mwenyewe  alifanya juhudi kubwa sana, lakini hakufanikiwa, na hata kuhamishiwa huko Zanzibar, ilikuwa moja ya mbinu zangu za kumkwepa…’akasema

‘Kipindi cha ujauzito kilikuwa kigumu sana kwangu, nilijitahidi sana kujizuia, na kujificha ili watu wasifahamu kuwa nina mimba, ukizingatia kuwa mimi sina mume, nilichofanya ni kuvaa manguo mapana, na kutokuonekana kwenye kadamnasi za watu..

‘Nashukuru pia kipindi chote hicho, cha ujazito wangu hakukuwahi kutokea kazi nyingi za nje ya ajira yangu, yaani kazi zangu na bosi wangu, na kama zilitokea niliweza kuwapa wasaidizi wangu, wakazifanya na kwahiyo sikuweza kukutana na mshauri wangu ambaye pia alikuwa ni bosi wangu, kwahiyo sikuwa na wakati mgumu, wa kujieleza, na siku zikaenda na hauchi hauchi , miezi nane ikafika,

Nilizaa nikiwa na miezi nane, na mambo yakaanzia hapo, na pamoja na furaha ya kupata mtoto, lakini ilifikia mahali nikaanza kujuta, kuwa kumbe nilichukulia mambo hayo kwa haraka, japokuwa sikuwa nimedhamiria hilo tendo liwe kama lilivyotokea,

‘Najua wengi watasema mimi ni mtu mzima, ningeliweza kupima kila jambo kwa uangalifu, ni sawa....lakini tuangalie na upande mwingine wa shilingi..je ni kweli mimi nilitaka litokee hivyo, ushahidi ndio huo, sikutaka , na lilifanyika kutokana na mbinu za huyo mwanaume…’akaniangalia mimi na mimi nilikuwa nimemkazia macho.

‘Sasa mimi na huyo mnayemuita mume wa familia ni nani Malaya, niambieni ukweli wenu bila kuficha, maana katuita sisi Malaya, je mimi nikimuita Malaya nina makosa, au lugha hiyo ni kwa wanawake tu. Pili mimi na yeye ni nani anayestahiki kuitwa msaliiti, tatu mimi na yeye ni nani mbakaji, mwizi, mdanganyifu,…’akasema na kuwaangalia wajumbe, halafu akamgeukia mwenyekiti alipoona watu wapo kimia

‘Najua wakili mtetezi ana maswali ya kuniuliza, ili aulinde mkate wake, je muheshimwa  mwenyekiti niendelee sehemu ya pili au tumuache muheshimiwa wakili  aniuliza maswali kwanza…?’ akauliza

‘Maana sehemu ya pili ndio itabainisha ukweli wa kifo cha Makabrasha, sasa hapo mwenyekiti utaamua mwenyewe, kwani hilo sio jukumu lako tena, ni jukumu la wenye mamlkaka, na mimi nawajibika kwa hilo, kama raia mwema natakiwa kuwasaidia watendaji na hapo sasa kila mtu ataubebe mzigo wake yeye mwenyewe…na mengine sistahiki kuyaeleza, labbda mwenyekiti aombe kibali..’akasema hivyo, na mwenyekiti angaalia saa, na mara akachukua simu, akawa anapiga namba, akaweka sikioni...

‘Unataka kumpigia nani mume wangu…’akauliza mama, akimuangalia baba kwa mashaka

Mwenyekiti akaashiria kwa mkono, kuwa mkewe atulie …

NB: Naona tushie hapa, kwa leo.



WAZO LA LEO: Ulevi wa aina yoyote ni hatari kwa afya zetu, ulevi, huondoa akili nzuri ya kibiadamu, na unaweza ukajikuta ukifanya jambo ambalo ukiwa na fahamu zako usingeliweza kulitenda, kama  ni hivyo basi kwanini tunakunywa  kitu ambalo kinatutoa utu wetu. Tutafakari kabla ya kutenda.
Ni mimi: emu-three
Ni mimi: emu-three

No comments :