Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, January 19, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-61


Nilishaanza kumshuku shemeji yangu kuwa anafahamu mengi, na siku ya leo niliona ndio siku pekee ninayoweza kumbana , na kusema ukweli wote, lakini sikutaka niongee naye peke yangu, nilishaongea na watu wa usalama, ambao nafahamiana nao,na niishawaeleza ni nini lengo langu, na nikaona niwaite watu hao waje kunisaidia ...

Endelea na kisa chetu

*********
Shemeji yangu huyo alipooa nafanya kweli akageuka huku na kule akitaka kukimbia, na kabla hajafanya hivyo nikamuonyeshea ishara ya kumuonya..., akatulia nikamaliza kuongea na huyo ofisa upelelezi, ambaye nilishamgusia kuhusu hayo mambo yanayoendelea katika nyumba yangu  na yeye akaahidi kuwa atalifuatilia hilo tatizo kwa karibu.

‘Shemeji ...ina maana unataka sisi tufungwe?’ akauliza shemeji yangu huyo sasa akionyesha ile sura adimu ya chuki, sura kama hizo kwa wengine ni nadra kuonekana.

‘Ukweli wako ndio utakaokusaidia wewe na kaka yako, nilishawapa muda wa kutosha, sasa wakati umefika, kama kweli  unataka kumuokoa kaka yako na wewe mwenyewe sema ukweli, niambie kila kitu nitakachokuuliza kabla huyo jamaa hajafika..’nikamwambia.

‘Lakini shemeji mimi nitakuambia nini, nimeshakuambia kila kitu ninachokifahamu mimi, mengine sina uafahamu nao, sio kila kitu kaka alikuwa akiniambia, ananiita ananituma na kama hilo tukio, ..mimi nilikuwa sijui kitu..shemeji kiukweli hivyo sio sahihi kabisa..’akasema.

‘Sawa ...basi kama umeshaniambia kila kitu ngoja hawo polisi wafike, wao wana utaalmu zaidi yangu mimi, baada ya hapo, najua sitakusumbua tena, unasikia,.tatizo wewe unafikiri mimi ninatania ..’nikasema na mara mlinzi akaja, na kutuambia kuwa kuna jamaa wamefika wanataka kuonana na mimi.

‘Ni watu gani?’ nikauliza.

‘Wanasema wao ni watu wausalama, wamenionyesha vitambulisho vyao...ni kweli ni watu wa usalama…’akasema huyo mlinzi, na hapo shemeji yangu ambaye alifikiria nafanya utani, akasimama na kushika kichwa, na mimi nikamwambia huyo mlinzi.

‘Waambia waje huku bustanini’nikasema huku nikiweka ile mashine yangu vizuri, sikutaka mazungumzo hayo yaishie hewani.

‘Shemeji umafanya makosa makubwa sana, kaka akilisikia hili, na hayo matatizo yake sijui kama mtaweza kuishi nyumba moja,...ina maana kweli ni wewe shemeji, sasa unataka kaka afungwe,...aheri hata mimi mnzima nikifungwa haijalishi kitu , lakini mume wako ni mgonjwa..huo ndio ukweli wenyewe, kama ana matatizo…’akawa anasema kama anataka kulia.

‘Muda wa utani umekwisha ndugu zanguni, , maana mimi wakati nawaonea huruma nyie mnafanya kweli..hamnionei huruma na mimi, hamfahamu kuwa hata mimi ni binadamu,.., sasa ngoja na mimi nifanye kweli tuone mwisho wake utafikia wapi, nina ushahidi wa kutosha wa kukuweka wewe na kaka yako ndani ..’nikasema.

‘Ina maana hata kaka, mumeo humpendi tena,...unataka umweke ndani hujali kuwa anaumwa, siamini hilo shemeji?’ akauliza.

‘Wewe ndio utakwenda ndani kuisaidia polisi, ....kaka yako atasubiri hadi hapo atakapopona, mjue mna makosa mengi ,kwanza kwa kuniibia, pili kwa kugushhi mikataba halali, tatu kwa mauaji ya Makabrsha , nne kwa wizi, na jingine hilo la jana la kutaka kuniua,..na mengine mengi...’nikasema na mara hawo jamaa wakafika mmoja akiwa na pingu tayari mkononi kuonyesha yupo kazini.

************
‘Mungu wangu kumbe ni kweli…’akasema hivyo sasa akionyesha ule uwoga wa dhahiri, sikufahamu kuwa shemeji yangu ni muoga hivyo mpaka nikamuonea huruma, lakini hiyo ndio njia pekee ya kuupata ukweli.

‘Wakaribishe huku…’niliona wale wageni wakiaka kuingia ndani, ikabidi niwaite kwa sauti, watuone kuwa tupo huku bustanini..

‘Shemeji, mimi sitaki kwenda jela, kwasababu sihusiki kabisa, yote niliyafanya kwasababu ya kaka..kwasababu ya kumsaidia kaka, angalia ali yake ilivyo, ...muhurumie kaka, shemeji...’akasema sasa akininong’oneza, na mimi sikumjali.


`Ukitaka usalama wako ongea ukweli, maana mengi yanafahamika, wao watakachofanya ni kupima ukweli wako,...sema yote unayoyafahamu, ukipindisha na kusema uwongo, jela inanukia, jela sio mchezo, isikie hivyo hivyo, mimi nimeionja na niliwekwa sehemu wanayosema ni nzuri, lakini taabu niliyipata siwezi hata kusimulia....’nikasema na wale jamaa wakafika

Kwanza walijitambulisha na wakaonyesha vitambulisho vyao. Mimi nikajifanya navikagua, halafu nikasema

‘Karibuni sana, niambieni shida yenu, maana mnatutisha, silaha,..pingu, ni mimi mhalfu tena..’nikasema nikijifanya kunyosha mikono kujisalimisha, na wao wakacheka kiogo, na kusema;

‘Haaah, hapana sisi tupo kazini, ni kweli..kazi yetu ni hiyo kuwatafuta wahalifu, sasa tutashukuru na sisi tukisikia utambulisho wenu…’akasema mmojawapo, na mimi nikajitambulisha na kumtambulisha shemeji yangu.

‘Sawa karibuni..’nikasema

‘Kwanza tunachohitajia hapa ni ushirikiano wenu, tupate ukweli kwa hayo tutakayoyauliza, …’akasema

‘Sawa ..’nikasema

‘Mama mwenye nyumba,..wakati, umeshikiliwa kituo cha polisi, na hata kupelekwa Segerea, ulisema kuwa nyumbani kwako kulitokea upotevu wa vitu, kweli si kweli..?’ akauliza

‘Ni kweli…’nikasema

‘Je hebu kwa kutukumbusha tu, kulipotea vitu gani…’akasema mwingine.

‘Ni kweli, kuna vitu vilipotea, na ni vitu muhimu sana, mojawapo ni mikataba wangu halali, na zaidi hata silaha yangu...’nikaanza kuongea , japokuwa nilishaongea naye, lakini sikutaka shemeji yangu afahamu kuwa nawafahamu hawo watu.

‘Una maana ile silaha iliyotambulikana kuwa ndiyo iliyomuua Makabrasha?’ akauliza huyo ofisa usalama.

‘Ndio ..’nikasema.

‘Kwahiyo kumbe kwa kupitia hivyo vitu tunaweza sasa kumpata muuaji halisi wa Makabrasha,  ..’akasema huyo mwingine

‘Na huyu umesema ni shemeji yako..?’ akauliza

‘Ndio…’nikasema na shemeji yangu alikuwa kanywea kweli kweli haamini kinachotokea.

‘Huyu hapa ni shemeji yangu, kiukweli ni mtu niliyeishi naye hapa namtambua vyema, ni mtu mwaminifu sana..’nikasema.

‘Hebu tuambie ndugu, ujue tunachokiuliza hapa tumekifanyia kazi, na hatutaki kupoteza muda mwingi hapa…wewe na kaka yako mnaelewanaje..?’ akaulizwa swali.

‘Ni..ni..kak yangu, tunaelewana tu…’akasema

‘Kwahiyo shughuli zake nyingi unazifahamu…?’ akaulizwa

‘Zile anazoniambia, nazifahamu…’akasema

‘Sasa kutokana na uchunguzi wetu, wewe ni mtu wa karibu sana na kaka yako, kuna mambo mengi sana mumekuwa mkishirikiana naye…huwezi kutuficha, lakini tunahitajia kauli yako kukupima je unahusika au huhusiki…’akasema mmojawapo

‘Kuhusika kwa lipi..?’ akauliza shemeji, naona kaamua kujikakamua.

‘Wewe ndiye uliyekuwa ukitumwa na kaka yako, kuchukua vitu mbali mbali, na katika upotevu wa vitu, kama alivyosema shemeji yako, makabati, au nyumba haikuvunjwa, ina maana kuwa mtu aliyefanya hayo yote ni mtu wa nyumbani,…kama kaka yako alikuwa hospitalini mtu mwingine anayeweza kuifanya hiyo kazi ni wewe…’wakasema

‘Kazi ipi…?’ akauliza


‘Sikiliza sisi hatuja kupoteza muda, tunakuuliza kitu amacho hata wewe unakifahamu, unasikia, tuna namna nyingi za kukufanya useme ukweli wote, lakini kwanza tunahitaji ushirikiano wako,… hapa tunamstahi shemeji yako tu, lakini tukifika huko utaimba yote kama wimbo unaoufahamu sana..’akaambiwa.

‘Sasa mnataka niseme nini?’ akauliza huku akijaribu kujitutumua, naona alishaniona sio mtu wake tena, alishaniona mimi ni msaliti wake.

‘Kwanza kuna mkataba wa shemeji yako uliibiwa, je upo wapi?’ akaulizwa

‘Mimi sijaiba huo mkataba,...muulizeni kaka....’akasema.

‘Kwahiyo kaka yako ndiye anafahamu wapi huo mkataba upo, au sio..?’ akauliza

‘’Mimi sijui…’akasema

‘Ok, shemeji tunaomba tuondoke na huyu mtu, sisi tunakuhakikishia tukifika naye huko atataja kila kitu, sisi tulishamchunguza nyendo zake kwa kirefu, tuna ushahidi wote kuwa anahusika kwa kiasi kikubwa sana,kuna mambo mengi anayafahamu,na ameyafanya sasa hatuna muda wa kupoteza tena ...’akasema

Na mimi nikamuangalia shemeji yangu huyo ambaye alikuwa kama kamwangiwa maji. Alikuwa hataki hata kuniangalia, nahisi chuki dhidi yangu zilikuwa kubwa, lakini sikuwa na njia nyingine.

‘Shemeji hiyo ndio nafasi yako ya mwisho, kama unamjali kaka yako sema ukweli, kama unaona kukaa kimiya ndio kutamsaidia kaka yako haya, mimi nitawaruhusu muondoke nao, na unafahamu ni kitu gani kitakukuta huko mbele, unamkumbuka yule rafiki yako aliyejifanya anaweza kuvumilia mateso ya huko, alikuambia nini kilichompata,....kama wewe unajiamini zaidi yake niwaruhusu muondoke ....’nikasema na  yeye kwanza akaniangalia kwa jicho lenye chuki, halafu akasema.

‘Haya  mimi nitawaambia ukweli lakini naombeni mumuache kaka yangu , kaka yangu anaumwa, na mengi aliyafanya bila kujitambua..’akasema

‘Hiyo sio kazi yako, sisi tunalifahamu hilo ndio maana tunakuuliza wewe, hatujakwenda kumuliza kaka yako kwasababu anaumwa,...kama tungelikuwa hatulitambui hilo, kaka yako sasa hivi angelikuwa jela. Sasa  kwa vile wewe ni mzima huna matatizo unahitajika  utuambie ukweli, kwani wote lenu ni moja....’akaambiwa, na akatulia kimiya kwa muda kama anawaza, halafu akasema;

‘Haya ulizenu maswali yenu nitawajibu, kwa kile ninachokifahamu...’akasema

‘Swali la kwanza, tuambie mkataba wa wanandoa hawa wawili ulioibiwa upo wapi?’ akaulizwa.

‘Mimi sijui huo mkataba ulioibiwa ni upi, ...’akasema

‘Wewe unafahamu mikataba mingapi?’ akaulizwa

‘Mimi nilishaiona mikataba zaidi ya mmoja, sasa sijui upi ni upi?’ akasema.

‘Kwa hivi sasa wewe una mikataba mingapi?’ akaulizwa

‘Nina huu mmoja alisema nimpelekee huko hospitalini....’akasema

‘Ulishawahi kutumwa kuchukua mikataba kama hiyo kabla?’ akaulizwa

‘Ndio…’akasema

‘Ulipotumwa hukuambiwa ni kitu gani, …?’ akaulizwa

‘Niliambiwa nikachukue nyaraka, imeandikwa mkataba…wa hivyo na hivyo, na upo mahali fulani, na ufunguo huu hapa, mimi namtiii kaka yangu, nafanya hivyo…’akasema

‘Kwahiyo ulipochukua hiyo mikataba ulimpelekea nani..?’ akaulizwa

‘Kaka…’akasema

‘Kulikuwa na mkataba uliokuwa nao wewe , ambao haujaonekana mpaka sasa, mkataba huo ndio shemeji yako anaoutafuta, kwa uchunguzi wetu, unao wewe, tunahitajia huo mkataba ambao ni ule wa mwanzao uliotumwa kuuchukua, sisi tunao ushahidi kuwa unao wewe...’akasema huyo ofisa.

‘Nimesema nilishamrudishia kaka....’akasema na kukatisha

‘Sema ukweli, ilivyoupata huo mkataba, uliingiaje kwenye nyumba ya mtu , na ukifahamu mwenyewe yupo, ....ina maana uliuiba au sio?’ akaulizwa.

‘Kaka ndiye alinituma niuchukue...mimi sijaiba, kaka ni mwenye nyumba pia...’akasema.

‘Ehe, uliwezaje kufungua makabati, ya shemeji yako?’ akaulizwa.

‘Nilipewa ufunguo na kaka, ....’akasema

‘Hebu tuonyeshe hizo ufungua’akaambiwa, na akatoa zile ufunguo alizo nao akazionyesha kwa hawo watu, waliziangalia tu, kwa mbali bila kuzigusa, halafu wakauliza

‘Kwahiyo hizo ufunguo zote ulizo nazo, alikupa kaka yako, na zinaonekana ni za kuchonga?’ akauliza

‘Ndio alinipa kaka, lakini mimi sijui kama ni za kuchonga,...’akasema.

‘Alikutuma pia ukachukue na ule mkataba uliokuwa huko ofisini kwa shemeji yako?

‘Ukazipeleka wapi hizo mikataba, ulizotumwa

‘Nilimpelekea kaka..’akasema

‘Kuna mkataba mmoja unakosekana, wewe bado unao,..tunauhitajia huo..usitupoteze muda…’akaambiwa na hapo akasita kidogo

‘Kaka yako ndiye alikutuma hiyo mikataba sio..wa nyumbani, na wa ofisini, au sio../’ akaulizwa

‘Ndio…’akasema

‘Kwa ujumla nakala za mikataba yote uliichukua wewe, baada ya kutumwa na kaka yako…kweli si kweli…?’ akaulizwa

‘Ndio alinituma yeye, kwanza huo wa nyumbani alikuwa nao yeye mwenyewe, alikuwa na nakala mbili, sikujua kuwa mmoja ni wa shemeji, baadaye, akaniambia nizipeleke kwa Makabrasha...’akatulia.

‘Nilipofika kwa Makabrasha akaniambia nihakikishe kuwa hakuna nakala inayobakia, mimi nilikuwa nimeshaficha nakala moja,...bila kaka kujua,..’akasema

‘Kwanini ulifanya hivyo?’ akaulizwa.

‘Nilitaka nitoe nakala nyingine, kwani nilihisi baadaye inaweza ikahitajika, kaka huwa anachanganyikiwa, baadae anaweza kuhitaji nakala au kumbukumbu, huwa naan ahivyo kwa akiba…ila kiukweli mimi sikuwa nafahamu malengo yao ni nini....’akasema

Ulijua lini malengo yao....?’ akaulizwa

‘Kuna siku waliniita kwenye kikao wakaniambia kwanini wameamua kuziharibu hizo nakala zote...’akasema

‘Walikuambiaje , lengo lao ninini?’ akaulizwa na hapo akaa kaa kimia, na hapo yule ofisa akauliza swali jingine.

‘Na kule ofisini uliwezaje kuingia , wakati muda wote kuna walinzi?’ akaulizwa

‘Niliingia muda wa kawaida tu, yule mhudumu alikuwa hayupo, na mimi niliwaonyesha kibali kuwa nimetumwa na shemeji, nikaweza kuingia kwasababu nilikuwa na ufungua, alionipa kaka....’akasema.

‘Kibali gani hicho, ina maana ulikwenda kwa shemeji yako ukamuomba hicho kibali?’ akulizwa

‘Aliwahi kunipa kibalia kabla,,...nikawa naendelea kukitumia..kuna siku nafika kwa ajili ya matengenezo ya ofisi yao’akasema.

Hicho kibali hakina tarehe?’ akaulizwa, na kukaa kimiya, na yule ofisa akauliza swali jingine.

‘Ina maana uligushi tarehe....?’akasema huyo mpelelezi

‘Kilikuwa hakijaandikwa tarehe....’akasema

‘Kwahiyo kumbe kaka yako alikuwa ana ufunguo zote za ofisini na za makabati ya mke wake?’

‘Mimi sijui, hilo swali ingelifaa mumuulizeni yeye mwenye kaka, yeye alinipa ufunguo akanituma niende ofisini akanielekeza wapi pa kuipata hiyo nakala ya mkataba, mimi nikafanya kama alivyoniagiza....’akasema.

‘Wewe kwanini hukumwambia shemeji yako ?’ akauliza

‘Kwanini nimuambie, kama kaka angetaka nifanye hivyo angeniambia nimwambie, kaka kafanya hivyo kama mume wake, na mume wake ana haki kwenye kampuni za mkewe, kuna ubaya gani hapo eeh , ‘akasema na kuniangalia mimi , na mimi nikawa nimemkazia macho, akaangalia pembeni.

‘Ohooo, kwa vile yeye ni mwanaume, sio…safi kabisa, mlishalipana hilo, ..’akasema mmojawapo.

‘Kaka aliniambi ahivyo…’akasema

‘Kuwa yeye ana mamlaka popote, hata kama kampuni sio yake,wewe hujui kuwa kampuni hiyo uliyokwenda kuchukua huo mkataba ni ya shemeji yako sio ya kaka yako ...huoni kuwa ni makosa?’akaulizwa

‘Hayo muulizeni kaka yeye mwenyewe , mimi nimejitolea kuwaambia yale ambayo hata kaka hakutaka niwaambie, ...najua nimefanya makosa sana kuwaambia, kaka hatanisamehe kwa haya, lakini sina jinsi...’akasema kwa uchungu.

‘Swali jingine, je kaka yako ndiye aliyekutuma kuchukua bastola kwenye kabati la shemeji yako?’ akaulizwa na hapo akatulia kidogo, halafu akasema.

‘Lakini kaka sio yeye aliyemuua Makabrasha, ...’akasema

‘Una uhakika gani na hilo?’ akaulizwa na kukaa kimiya, na huyo ofisa hakutaka kumshinikiza kwa hilo, kwa vile wao wanafaahmu zaidi, wakauliza swali jingine

‘Kama sio kaka yako basi ni wewe uliyemuua Makabrasha?’ akaulizwa

‘Sio mimi wala sio kaka..’akasema

‘Unaposema sio kaka yako au wewe, ina maana unamfahamu muuaji, ni nani aliyefanya hivyo?’ akaulizwa

‘Kwakweli mimi sijui,....’akajibu na kutulia na yule ofisa akatabasamu na kutikisa kichwa, halafu akauliza swali jingine

‘Tuambie ilikuwaje siku hiyo ambayo Makabrasha aliuwawa,, maana usipotuambia ukweli , ujue hapo wewe utakamatwa kama muuaji, wewe na kaka yako’akaambiwa.

‘Mimi sio muuaji, ..sijamuua Makabrasha, japokuwa ni kweli mimi ndiye niliyekwenda kuichukua hiyo bastola kwenye kabati la shemeji, ...nilifanya hivyo nikiogopa kuwa shemeji kwa jinsi alivyokuwa na hasira , angeliweza kuitumia kumuua kaka, nikaona bora niichukue hiyo silaha nikaifiche mbali kabisa na wao’akasema

‘Kwahiyo hukutumwa na kaka yako kuichukua hiyo bastola?’ akaulizwa

‘Hapana kaka hajanituma kuchukua hiyo bastola, niliichukua mwenyewe baada ya kuiona hapo, siku aliponituma kurudisha hiyo mikataba mipya...wakati nafungua kabati la shemeji nikaiona hiyo silaha, na najuta kwanini niilichukua hiyo silaha’akasema

‘Ulipoichukua hiyo silaha uliipeleka wapi?’ akaulizwa

‘Niliificha ofisini kwetu, na siku moja, nikaichukua kwenda nayo porini kuitupa...’akasema na huyo ofisa akatabasamu, na kumwangalia mwenzake, ambaye alitikisa kichwa kama kukubali kitu.

‘Kwanini ufanye hivyo?’ akaulizwa

‘Kwa wazo hilo hilo kuwa ikiwemo mle ndani inaweza kuleta majanga, na bora niitupe mbalii kabisa,..’akasema

‘Ikawaje sasa, ...?’ akaulizwa

‘Nikiwa ndani ya gari, nikiwa naelekea huko porini , nilifika mahali gari likawa halina mafuta, ....kituo cha mafuta kilikuwa karibu tu, lakini gari lilikuwa haliwezi kufika hapo, kwahiyo nikaona nichukue galoni niende kununua...’akasema .

‘Unaweza kutuambia ni kituo gani hicho, na una risiti na mafuta uliyonunua siku hiyo, kama ushahidi?’ akaulizwa

‘Mh,hata sikumbuki, na hata jina la kituo, sikumbuki, na nakumbuka sikuchukua risiti...’akasema

‘Ehe, ikawaje?’ akaulizwa

‘Niliporudi kwenye gari langu sikuuona  ule mkoba wangu uliokuwa na silaha, ulikuwa haupo,....inaonyesha kuwa kuna watu walikuja kwa haraka wakafungua kiyoo, wakauchukua, sikuwa makini kufunga viyoo vya gari, ningelijua ningelifunga hivyo akasema

‘Endelea…’akaambiwa

‘Nahisi kuna mtu alikwua akanifuatilia, kwasababu ni nani angelijua kuwa ni na vitu kama hivyo,...nilijaribu kuangalia huku na kule lakini sikuona dalili ya mtu, nikajua nimeibiwa, na silaha ya watu imeshachukuliwa, sikujua nifanye nini, nikaamua kukaa kimiya, ..hadi hapo niliposikia kuwa hiyo silaha ndiyo iliyofanyia hayo mauaji,..huo ndio ukweli wenyewe, ..’akasema

‘Hiyo hadithi yako hukuipanga vyema, inabidi ukaipange vyema, hiyo hadithi yako haina vina wala mizani, itakutia matatani, usiposema ukweli,..’akaambiwa.

‘Ndio ukweli wenyewe huo....’akasema

‘Sema ukwei ni nani uliyempa hiyo silaha, ujue ulichukua silaha ya watu inayomilikiwa kisheria, na silaha hiyo ikatumiwa kufanyia mauaji, na muuaji mpaka sasa hajapatikana, kwanini wewe usikamatwe kwa kosa hilo, tuambie ukweli ulivyo..’akaambiwa.

‘Ukweli ndio huo, sina ukweli mwingine, ...’akasema

‘Inavyoonekana ni kuwa kaka yako alikutuma hiyo silaha, ili ukampe mtu fulani, ambaye ndiye aliyemuua, 
Makabrasha,  sisi tunafahmu kuwa ni wewe uliifanya hiyo kazi, ulitakiwa uifanye  wakati kaka yako anaongea na marehemu....’akasema

‘Hapana,kaka hajawahi kunituma hiyo silaha, kaka kipindi hicho anaumwa, hajui kabisa kuhusu hiyo silaha, ....na mimi sijaua mtu, na siwezi kufanya hivyo..kwanini tumuue mtu kama yule ambaye anatusaidia sisi, hilo hamlioni jamani, Makabrasha alikuwa ni mtu wetu wa karibu,....’akasema akiwa na wasiwasi.

‘Anaweza akawa mtu wenu wa karibu lakini mkaona hawafai tena, akifa yeye, hisa zake mtazichukua nyie, kwasababu akiendelea kuwepo, hisa zote mtazipoteza kwa vile alikuwa anawadai pesa nyingi sana, na madeni yake alipanga yalipwe kwa hizo hisa,..hiyo ndio mipango yenu,...’akasema huyo mtu wa usalama.

‘Hapana hatujamuua Makabrasha, sijui ni nani aliyefanya hivyo...tunasikitika sana kwa kifo chake...’akasema

‘Ni nani aliyemchukua kaka yako kutoka hospitalini hadi kwa Makabrasha?’ akaulizwa

‘Ni mimi, alinipigia simu kuwa niende kumchukua,...kwani ana mazungumzo  muhimu na marehemu’akasema

‘Kwahiyo alikutuma pia ukachukue hiyo silaha, umpe mtu mwingine kama unakataa kuwa sio wewe na huyo mtu mwingine ni nani,..usipomtaka huyo mtu ni wewe, nakuuliza haya ukijua sisi tunafahamu kila kitu, lengo ni kukupima yawezekana haya uliyafanya kwa kumsaidia kaka yako  ...’akasema kabla hajamaliza shemeji akamkatisha na kusema;

‘Mbona mnanitungia uwongo, sijafanya hivyo, hata silaha yenyewe sijawahi kuitumia,...’akasema.

‘Unaweza usiweze kuitumia ukabahatisha,kwani ina ugumu gani , yoyote anaweza kutumia, kama anafahamu jinsi ya kufyatua risasi, hata hivyo hatujasema wewe ndiye uliyemuua, kuna mtu uliye mpa hiyo silaha, ndiye aliyefanya hayo mauaji, na unamficha, na kwahiyo wewe utashitakiwa kama ndiye uliyefanya hayo mauaji ...’ akaambiwa.

‘Mimi nimeshawaambia huko ukweli, na kwanini tumuue Makabrasha wakati ni mtu anayetusaidia?’ akauliza.

‘Hilo swali unatakiwa ujibu wewe,...’akaambiwa.

‘Mimi nimeshawaambia ukweli,....’akasema.

‘Hilo litajulikana baadaye, kama unasema ukweli, sisi tumeshaujua ukweli, nia yetu hapa ni kukupima, na ukweli ndio utakao-kuokoa wewe...’akasema.

‘Nimeshawaambia ilivyokuwa,...mnataka niseme ukweli gani zaidi ya huo’akasema.

‘Hujatuambia ni nani uliyempa hiyo silaha, ...hilo unatuficha, ili hali sisi tumeshamfahamu, ’akaambiwa.

‘Mimi nimeshawaambia hiyo silaha sijampa mtu...’akasema.

‘Ehe, ulipomchukua kaka yako wewe ulikwenda wapi..hebu elezea hapo…maana ni lazima umfikishe pale, wewe ulipomfikisha ulikuwa wapi ukimsubiria kaka yako....?’ akaulizwa.

‘Mimi nilimsubiria nje, barabarani..’akasema.

‘Ni nani aliyekuona ukimsubiria,maana hapo usipokuwa na ushahidi wa kutosha, utaingia matatani...’nikamwambia.

‘Yule mlinzi wa nje wa hiyo hoteli iliyopo karibu na lile jengo, nilicheza naye drafti, hadi kaka alipokuja, na tukaondoka naye...’akasema. Na huyo jamaa akaandika jambo kwenye karatasi yake, na kusema.

‘Hilo nilishalifuatilia, ni kweli...ulionekana ukicheza drafti na huyo mtu, lakini kabla ya hapo...mhh, sawa hilo tuliache hivyo kwanza au sio mwenzangu..?’ akasema akiangaliana na mwenzake..

‘Yap, weka akiba..’akasema mwenzake.

‘Lakini bado hatujamalizana na kipengele hicho, kuna ukweli mwingi unatuficha hapo, na hatujui kwanini unafanya hivyo, tutakuja kuuliza sana sehemu hiyo muda ukifika....’akasema na kukatisha.

`Swali la tatu, hiyo nakala ya mkataba wa zamani uliokuwa nao wewe upo wapi?’akaulizwa

‘Niliurudisha kwenye kabati la kaka.....’akasema

‘Lini?’ akaulizwa.

‘Leo asubuhi...wakati shemeji walipompeleka kaka, mimi nilibakai nyuma, nikaurudisha ..kimia kimia, niliuweka pale ulipokuwa,...’akasema.

‘Kwanini ulifanya hivyo?’ akaulizwa

‘Niliogopa kuwa kaka akifahamu nina nakala nyingine ya huo mkataba atagomba, kwani wao walitaka nakala zote ziharibiwe, ..lakini pia nilisikia kaka akihangaika kuutafuta huo mkataba wa zamani,na pia nimesikia shemeji akiuulizia huo mkataba, nikaona jambo jema kuondoa hili tatizo nikuuweka huo mkataba wa zamani, ili kaka akija akiuona, aurudishe kwa shemeji mambo yaishe...’akasema

‘Hapo pia kuna kitu unakificha, kama wewe uliona kuwa mkataba huo ni tishio kwenu, hasa kwa kaka yako, na mkakubaliana kuwa mikataba yote iharibiwe, ibakie hiyo mipya, ni kwanini ukaamua kuurudisha hapo tena,....kuna nini kilikusukuma kufanya hivyo, au ulitaka kuuficha hapo kwa muda ili baadaye uje uuchukue, maana ulishajua kuwa kule kwako hakuna usalama tena,..’kaulizwa

‘Mimi niliamua kuurudisha kwa nia njema kabisa…,kama nilivyowaambia...’akasema

‘Kwahiyo huo mkataba kwa sasa upo wapi?’ akaulizwa

‘Nimefika leo kuuangalia, nimekuta kabati halifunguki, kwahiyo sijui kama upo hapo hapo, ila nina uhakika niliuweka hapo hapo....’akasema

‘Swali kubwa hapo ni kwanini uliurudisha?’ akaulizwa

‘Nilitaka kaka aje auchukue mwenyewe,...., sikutaka tena kuendelea kujihusisha na mambo ya familia, na niliona nafanya makosa, na nilitaka kaka na shemeji waje waelewane....’akasema.

‘Waelewane, kwani walikuwa hawaelewani…kwasabababu ya mkataba au kwasababu ya matendo ya kaka yako…?’ akaulizwa na kukaa kimia.

‘Ina maana huo mkataba hadi hivi sasa upo kwenye hilo kabati...?’ mimi nikamuliza na akaniangalia akionyesha uso wa kunikasirikia , akasema;

‘Ndio upo humo kwenye kabati..., lakini kabati halifunguki kabisa, kama vile kitasa kimebadilishwa, kama likifunguka mtauona, upo .... maana mimi ndiye niliyeuweka leo asubuhi,...na kuna kitu changu kingine, sijui kama kipo humo au vipi....’akasema na mimi kwa haraka nikainuka na kuomba niende kwenda kuuangalia kama kweli ndio huo mkataba wetu wa zamani.

‘Nenda kahakikishe, halafu uje, tuendelee, maana huyu mtu asipotuambai ukweli, leo tunakwenda naye..’aaksema huyo ofisa.

‘Mimi nimeshawaambia ukweli, naomba niende nikamuone kaka, yeye ndiye aliyenituma… na jinsi ninavyochelewa nampa mashaka, na wasiwasi, na hivyo vitu havitakiwi kwa afya yake...’akasema

‘Yeye ndiye aliyekutuma nini, huo mkataba, au sio…kuna mengine kakutuma hujatuambia…au sio?’ akaulizwa

‘Ndio alinituma huo mkataba na vitu vingine,....’akasema

‘Shemeji wewe nenda kahakikishe hilo,..huyu haendi mahali, hadi hapo kitakapoeleweka, kuwa tunakwenda naye kituoni, au anafunguka ukweli wake wote, na ukweli wake ndio utakaomfanya sisi tumwamini, na akifanya hivyo basi sisi tutakuwa upande wake, kumlinda..’akasema huyo ofisa.

Mimi nikawa nimeshaanza kutembea kuelekea ndani , moyoni nikiwa na hamasa kuupata huo mkataba wa zamani, …mkataba utakaoleta haki ndani ya familia yangu,…na huku nyuma nikasikia shemeji akiniambia;

‘Shemeji ...ukiona kitu changu ndani ya huo mkatana nakuomba tafadhali, unipatie, nahisi nimekiacha ndani ya huo mkataba...’akasema na mimi sikumjali nikaharakisha kwenda kufungua hilo kabati na wale watu wa usalama wakiendelea kumuhoji, hawakujua kuwa nimeacha mshine ya kurekodia matukio, ikiwa inafanya kazi....

NB Ni hayo kwa leo, natumai leo mumefurahia sehemu hii kama mumefurahia,naomba comments nyingi sana..



WAZO LA LEO: Katika maisha yako jifunze kuwa mkweli, kusema ukweli na kutenda yaliyo haki, hiyo ndio njia ya kuiweka nafsi yako huru, kujiamini na na kutokuwa na wasiwasi…na matokea yake huwa ni chanya,…na hutajuta katika maisha yako yote, kinyume chake ni mashaka, na mwisho wake ni kuzalilika tu.
Ni mimi: emu-three

No comments :