Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, January 18, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-60


‘…Jana asubuhi uliponiona ulionekana kama unashtuka,..kweli si kweli kwanini ulikuwa unashutuka, si ina maana hukutegemea kuniona nikiwa hai, au sio… au unajifanya hujui mlichokipanga wewe na kaka yako, vinginevyo uniambie ukweli…mlipanga nini wewe na kaka yako,…?’ nikamuuliza hapo kwa ukali…

‘Shemeji hapana, hatujapanga kitu kama hicho, na wala sielewi kwanini kaka alifanya hivyo....kwanini tupange kuku-ua shemeji, mimi nakujali sana, kuwepo kwako ni muhimu sana kwangu…, ’akalalamika huku akishika kichwa akionyesha masikitiko.

‘Sasa mimi nimeamua, nichukue hatua, nakuambia wewe kwa vile kaka yako ni mgonjwa, na kwa vile wewe ni mzima, na inaonekana mpo shirika, basi wewe utaisaidia polisi ili ukweli uweze kupatikana,…kwasababu mimi nimeyavumilia haya mambo mpaka watu wananiona mimi ni mjinga…’nikasema na mara simu yangu ikaita

Shemeji akawa ananiangalia kwa mashaka, akihisi labda ni polisi wananipigia na nilipoitizama hiyo namba nikaona ni ya yule mpigaji asiyejulikana, nikaiweka hewani na kusema;

‘Niambie…?’ nikasema

‘Polisi wananitafuta sana ili niongee nao, na naogopa nitaongea nao kabla sijakutana mimi na wewe, nahisi ni wewe umewaambia, sasa litakalo tokea mimi sina lawama …’akasema

‘Sasa kwanini huongei nao, mimi siwezi kukulaumu, kama una ushahidi huo kawape polisi, si una uhakika nao, kwanini unaogopa kuwaopatia polis, lakini kama nia yako ni kupata masilahi, kwangu hupati kitu…’nikasema

‘Tatizo wewe hujui kitu gani nilicho nacho,..sawa…kama unasema hivyo, sawa, lakini namuonea sana mume wako huruma, na zaidi nashangaa kwanini mke wake hana huruma naye, huyo akienda jela atafia huko, ndio unalolitaka au sio…’akasema

‘Hayo ni maneno yako na hisia zako, hayawezi kubadili sheria za nchi…’nikasema

‘Unajua madamu, mimi nilitarajia leo ningewakabidhi kila kitu, ili mjua wenyewe jinsi gani ya kufanya, lakini mpaka sasa naona muda unakwisha tu..sipati marejesho…’akasema

‘Marejesho gani, kutoka kwngu, mimi na wewe tulikubaliana kitu gani, wewe ulisema tukutane unionyeshe huo ushahidi, mara eeh, unatafutwa na polis, kumbe na wewe ni mhalifu unatafutwa na polis, eeh, sasa kajisalimishe huko na huo ushahidi wako…’nikasema

‘Mimi nimeongea na mume wako nikamuelezea yote , na pamoja anadai kuwa hakumbuki, lakini ushahidi kidogo niliomuonyesha kakiri kuwa yupo matatani, hata kama anaumwa,…na kasema nimuachie huo ushahidi, akasema kuna mtu atamtuma,…ili nimkabidhi…’akasema

‘Sawa kama mumeongea na mume wangu basi mtamalizana naye, mimi sihitaji sana kuongea na wewe, kwani msimamo wangu ni ule ule, na huyo mtu ni nani..?’ nikamuuliza sasa nikimtupia macho shemeji yangu akawa ananiangalia kwa mashaka.

‘Anamfahamu yeye mwenyewe huyo mume wako…’akasema

‘Alishawahi kutumwa kwako kabla, au umesahau kuwa wewe ulikuwa tarishi wa marehemu, ….au sio..’nikasema

‘Sawa tuyaache hayo, ila nilifanya hivyo kwa manufaa yenu, kama umefikia kunidharau hivyo, basi mimi nitawakabidhi polisi, itakwua usumbufu kwako mkurugenzi mnzima ukishitakiwa wewe na mume wako, maana huo ushahidi unaonyesha kama nyie wawili mlishirikiana …’akasema

‘Kwa vipi…?’ nikauliza

‘Yeye alifika akamaliza kazi, na wewe ukaja kuhakikisha,..bahati mbaya wewe ukakamatwa, lakini mume wako bado yupo mafichoni, kwa maana ya kuwa polis bado hawajamtambua, …wameshatambua hilo, ila wanahitajia ushahdi zaidi na shahidi muhimu ambaye ni mimi…’akasema

‘Sawa nimekuelewa sasa unataka nini..?’ nikauliza na mara yeye akakata simu.

************

Niligeuka kumuangalia shemeji yangu aliyekuwa akisikiliza kwa makini, akasema

‘Nahisi ni….nilijua ni polisi..’akasema

‘Ni mtu wenu huyo…nahisi kaka yako alitarajia kukutuma kwake kumpelekea pesa ili asitoe ushahidi kuwa kaka yako anahusika kwenye mauaji ya Makabrasha, na inaonekana kazi yako ndio hiyo ya kutumwa na kaka yako, au sio….’nikasema

‘Sasa shemeji ngoja mimi niondoke…’akasema

‘Nimekuambiaje..maana hata ukiondoka sasa hivi utakutana na polis njiani, ..’nikasema

‘Kwani mimi nina kosa gani…?’ akauliza na kabla sijamjibu simu ikapigwa tena

‘Hebu subiri kuna huyu tena anapiga simu…’nikasema na kuipokea hiyo simu, ilikuwa namba ambayo sijaiweka kwenye kumbukukumbu zangu.

‘Halloh nani mwenzangu..?’ nikauliza

‘Ni mimi yule mtoto wa marehemu…nilikuwa nauliza kama upo tayari ya kikao chetu, ni kesho au sio…?’ akauliza na kabla sijamjibu akaendelea kuongea

‘Japokuwa baba mdogo, nikiwa na maana mumeo kalazwa, lakini sizani kama hilo litasumbua kitu au sio maana tulishaongea iliyokuwa imebakia ni sisi kurejesha maelezo kutoka kwa mawakili wetu..je kesho upo tayari..?’ alikuwa Yule mtoto wa Marehemu ambaye ni kiongozi wa familia.

‘Mimi sina shida ya hicho kikao , ila msimamo wangu ni ule ule, je mumeupata ule mkataba wa zamani…?’ nikauliza

‘Hilo ni tatizo madam , hatujaweza kuupata huo mkataba unaosema ni wa zamani.., ni kama vile haupo..’akasema

‘Sasa tutajadili nini, iliyobakia ni mimi nifuate sheria, ili ijulikane kabisa kuwa mkataba huo mlio nao ni wa kugushi..’nikasema

‘Mimi nataka kuondoka, na ..natarajia kukaa na familia yangu, ili majukumu yote niyaache kwa huyo msaidizi wangu siwezi kuendelea kusubiria…’akasema

‘Mimi sina shaka, yoyote Yule nipo tayari kukabiliana naye, ilimradi tu, huo mkataba wa awali uwepo..’nikasema

‘Kiukweli madamu, kwa hilo, itakuwa ni vigumu sana, maana wakili wetu amefanya jitihada zote ameshindwa kuupata huo mkataba unaosema ni wa zamani, sasa tufanyeje..?’ akaniuliza

‘Hilo ni swali ambali unatakiwa umuulize wakili wenu au sio..’nikasema

‘Yeye kashauri hivi,  wewe ukubaliane na huu mkataba tulio nao sasa, maana swala sio kuufuata, swala ni kuhakikisha kuwa haupo tena, na kuufuta ni lazima taratibu za kisheria zifuatwe…umeliona hilo…’akasema

‘Kwangu mimi siwezi kufanya hivyo, huo mkataba siutambui, na najua dhumuni la hayo yote, kwahiyo msimamo wangu bado ni huo huo…’nikasema

‘Basi hilo nitawaachia nyie mpambane na huyo msaidizi wangu… , kiukweli siwezi kuendelea kusubiria tena, hata mama naye anataka kurudi huko kijijini, akahangaike na shughuli zake,…, ngoja nikae na wanafamilia, ili hili jambo sasa liwe bayana kwa wanafamilia wote, kitu ambacho sikukipendelea, unajua kila mmoja anamtizamo wake…’akasema

‘Hilo ni juu yenu nyie kama wanafamilia..ila ninacho kushauri, hata mkikaa na wanafamilia usije kuwaficha kuwa huo mkataba ni batili, unasikia..vinginevyo, hata kama utakwenda huko unapokwenda, ujue unaweza kuitwa kama shahidi kwenye kesi nitakayoiwakilisha mahakamani…’nikasema

‘Sawa..ngoja tuone, nitakujulisha baada ya kikao cha wanafamilia..’akasema na kabla hajakata simu nikasema ;

‘Nikuulize kitu, ulisema wewe kwenye ile video ya matukio kwenye ofisi ya Makabrasha uliona Yule aliyemuua baba yako, au sio..?’ nikamuuliza

‘Sikumuona, nilikuambia sura haikuonekana,..alitokeza kichwa tu, na kichwani alivaa kitu kama soksi, ya kuziba uso na kichwa kizima akaacha macho na pua..’akasema

‘Na wakati anamlenga marehemu risasi, mume wangu alikuwa amekaa mbele ya huyo marehemu au sio, sambamba, au sio ,..?’ nikauliza

‘Ndio walikuwa wamekaa wawili mmoja huku na mwingine kule, meza imewatenganisha, kama ilivyo kwenye ofisi…sio sambamba ya kukinga..lakini walikuwa wanaangaliana na huyo mpigaji alipiga risasi akiwa mlangoni, akimlenga marehemu, naelewa unachotaka kukisema hapo,  kuwa labda isingeliwezekana mtu akiwa mlango kumlenga marehemu…angalia mlango ulipo, na meza ilipo, na muuaji ana shabaha..’akasema

‘Kwahiyo kwa vyovyote vile, kutokana na huo ushahidi mume wangu hawezi kuhusika na hayo mauaji au sio…?’ nikamuuliza

‘Hawezi kuhusika,..hao ni polisi wanatapa tapa tu, nimelisikia hilo, kuwa wao wana ushahidi wa kutosha kuwa mume wako kahusika, ni waongo..au kama wana ushahidi mwingine mimi siujui..ila nilio nao ndio huo, na kama mume wako angelihusika mimi mwenyewe ningehakikisha anakwenda kuhukumiwa…’akasema

‘Kwanini sasa hutaki kuwaonyesha polisi huo ushahidi ulio nao wewe…?’ nikauliza

‘Kwasababu utamtia hatiani mume wako kwa jinsi unavyoonekana , kwa namna moja au nyingine, ataonekana anahusika, ama kwa kushirikiana na hao watu, au kujua ukweli halafu akauficha, halafu nimeshachelewa kufanya hivyo, nikifanya sasa unajua ni nini kitatokea, its too late! …’akasema

‘Lakini kwenye maelezo yako ya mwanzo hukusema hivyo…’nikasema

‘Nilisemaje..?’ nikauliza

‘Ulisema hutaki kuonyesha huo ushahidi kwa polisi kwa vile unaogopa kuwa polisi watajua kuwa mume wangu alikuwepo kwenye hicho chumba kwahiyo atashukiwa,..ni kitu kama hicho..’nikasema

‘Ndio,… hiyo pia ni sababu moja wapo, na hilo la kuwa mume wako alionekana hapo ofisini, bado halina nguvu, hakuna mtu wa kulithibitsha hilo, …’akasema

‘Una uhakika na hilo kuwa hakuna mtu anayefahamu kuwa mume wangu alikuwepo huko…?’ nikauliza

‘Aaah, uhakika gani, mimi nilijaribu kuulizia, hata mpelelezi wangu alijaribu kufanya uchunguzi , hakuna mtu aliyewahi kumuona mume wako hapo kwenye hilo jengo, pili hospitali wanatambua kuwa mume wako alikuwa mgonjwa, alilazwa, na hali yake isingeliwezesha yeye kufika huko..’akasema

‘Sawa nashukuru..’nikasema na kukata simu.

 Nikageuka kumuanga shemeji yangu , na alionekana akitabasamu kidogo

‘Umefurahi nini..?’ nikamuuliza

‘Nimesikia kama umesema kaka hahusiki, ni kweli itakuwaje, mtu alilazwa hospitalini angeliwezaje kufika huko…’akasema

‘Wewe ungeliweza kumsaidia, wewe si jembe lake..wewe si anakutuma mara kwa mara kumfanyia kazi zake…’nikasema

‘Nini ..!!’ akasema akionyesha mshtuko

‘Wewe sio jembe lake, wewe si ndio anakutuma mara kwa mara, na akitaka kufanya jambo anakuita wewe, je siku hiyo sio wewe aliyekuita ukampeleka huko, ..?’ nikauliza

‘Wapimwishowe nimeona ni muhimu kuwafahamisha watu wa usalama, ili baadae nisije kualaumiwa,unaona, ..wao wanakuja, ..sijui kwanini hawajafika mpaka muda huu, na wewe watakiwa kuonana na kaka yako…’nikasema

‘Shemeji, kwanza nimeshachelewa, kaka atakuwa ananiulizia huko…’akasema

‘Huwezi kuondoka, mpaka uonane na polisi,…acha akupigie simu, na polis watajua jinsi gani ya kumjibu, wanajua kuwa kaka yako yupoje...kwani wakati anakutuma, ilikuwaje, alikupigia simu au..?’nikauliza

‘Mimi sijui lakini yeye alinipigia simu niende hospitalini, kuna kitu anataka kunigaiza, ndio nilipofika akaniagiza nije kuvichukua hivyo vitu…’akasema

‘Ni kimojawapo ni mkataba, au sio mkataba ambao bado anahangaika nao, mkataba wa kugushi, mkataba ambao utampa mamlaka ya kumiliki mali ili na wewe ufaidike au sio?…yeye anafikiria kuwa huo mkataba utamsaidia..na kingine ni nini alichokuagizia…?’ nikauliza

‘Ni hizi nyaraka tu za ofisini kwake…’akasema na kunionyesha, sasa alionekana kuwa huru kufanya ninavyotaka, na ndicho nilikitaka,…nikachukua zile nyaraka na kuanza kuzikagua, nikakuta kuna mkataba wa kuuza gari…

‘Kwanini anataka kuuza gari…?’ nikauliza

‘Mimi sijui, yeye wakati ananituma alisema, kuna mkataba wa mauzo, anatakiwa aufanyie kazi haraka maana kuna watu wanahitajia pesa kwa ajili ya kuimaliza kesi ya mauaji, hataki wewe usumbuliwe  tena…na asipowalipa hizo pesa wanazomdai, unaweza kufungwa..’akasema

‘Mimi au yeye…?’ nikauliza

‘Yeye alisema ni wewe…’akasema
‘Kwanini mimi nifungwe wakati sihusiki na hayo mauaji..?’ nikauliza

‘Mimi sijui…’akasema

‘Kuna jingine alikuagiza..?’ nikauliza

‘Hapana…’akasema kwa kusita

‘Una uhakika, hakuna kitu kakuambia uweke…au uchukuze zaidi ya hivyo…kama anavyokuagiza kila mara , hujawahi kuagizwa kule ofisini kwangu kuchukua kitu..?’ nikamuuliza

‘Hakuna shemeji…zaidi ni karatasi za madeni,hakuna,..hapana shemeji, ofisini kwako, hapana, mimi kama niliwahi kufika huko, ni wakati upo ofisini, sijawahi kufika wewe ukiwa haupo …’akasema

‘Wewe unahisi hizo pesa anataka kumlipa nani..?’ nikauliza na hapo akaniangalia kwa mashaka, halafu akasema;

‘Hapo sijui…lakini jana nilisikia wakati anaongea ovyo, kuwa una mtu kasema asipomlipa pesa anaweza kutoa siri, siri ambazo zinaweza kukufunga na hata yeye anaweza kuwa hatiani…, nikamuuliza siri gani, akasema ni  vyema mimi nisijue itakuwa bora kwangu….’akasema

‘Unahisi kweli kaka yako hajaua..huoni kama vile kafanya yeye hayo mauaji ndio maana anajaribu kuuficha ukweli…na kama hajaua kwanini ahonge, unaona eeh, na wewe unaingizwa kwenye janga hilo…’nikasema

‘Lakini atauwaje na wakati alikuwa mgonjwa, mimi nahisi anaongea kwa kuchanganyikiwa…’akasema

‘Kuchanganyikiwa mpaka leo, si sasa hivi ni mzima, ana akili zake sawa sawa, mbona analikumbuka hilo, …kwanini kakuagiza huu mkataba, kwanini analikumbuka hilo la huyo mtu, anayedai pesa, kuwa ana ushahidi..? ..na docta kasema mara nyingi mtu akiwa kwenye hiyo hali anaweza asikumbuke alichokifanya akiwa kachanganyikiwa, hebu acheni hayo maigizo..?’ nikamuuliza

‘Lakini shemu yawezekana ni kweli…maana alivyoongea leo sio sawa na alivyoongea jana usiku…’akasema

‘Leo kaongea vipi…?’ nikamuuliza

‘Nilipofika, nilimkuta kama yupo kwenye dimbwi la mawazo, halafu akaniuliza, jana nilifanya nini..mimi sikutaka kumuambia, ukweli wote,  halafu akasema hivi,..leo kuna mtu kampigia simu, kuwa ana ushahidi ambao akiwaonyesha polisi yeye na wewe mnaweza kuwa hatiani, lakini hakumbuki huyo mtu ni nani, akasema kwa kuepusha shari ni bora ampe huyo mtu akitakacho na ili huo ushahidi upatikane uharibiwe,..…’akasema

‘Mbona hukuniambia awali hivyo, mpaka nimekubana kwa njia hiyo, wewe kuna kitu unaficha,..unamficha nani,…sikiliza mimi sitaweza kukubeba kwa hili, unasikia…kama hutaniambia ukweli wote, basi, …’nikasema

‘Ukweli upi tena huo shemeji…’akasema kama kukereka

‘Hapa unaona nakukera, lakini polis ni mara ya ya hapa, watakuuliza kitu kile kile, hadi wakuchanganye kichwa, na mwisho wa siku wataubaini ukweli wanaoutaka, sasa niambie, jana aliongea nini…?’ nikamuuliza

‘Shemeji nimeshakuambia jana alikuwa anaongea mambo mengi tu, ovyo ovyo, wakati mwingine anachanganya mada, …’akasema

‘Kwahiyo unavyohisi wewe ni kweli hajui alichokifanya jana…nataka useme ukweli ili tuweze kumsaidia kaka yako, na pili ili tuweze kumshika huyo tapeli anayetaka kupata pesa kwa njia isivyo hali, wewe huoni kuwa kaka yako anatumiwa tu…’nikasema

‘Mimi namfahamu kaka vizuri sana, …anavyoongea leo, sio kama ilivyotokea jana, mengi nikimuuliza hakumbuki kabisa…anahisi kama likuwa anaota tu shemeji….’akasema

‘Ngoja polisi waje natumai wakija wewe utakuwa na habari nzuri ya kuwaeleza, wao ndio watayapima hayo maelezo yako, lakini kwa kukutahadharisha tu, hayo maelezo yako yanaweza kukufunga, unageuza geuza maneno, hata mimi naanza kukushuku kuwa wewe una mpango mmoja wewe na kaka yako…’nikasema

‘Mpango gani shemeji, ..mimi siwezi kufanya hivyo,….ninachofanya sasa ni kujaribu kumsaidia kaka ili aondokane na haya mambo, kiushauri pia..ili muishi wawili kwa amani…’akasema

‘Wewe na kaka yako, mlipanga jana kuniua,..hilo huwezi kulikwepa..hata kama …lakini kaka yako alikuwa na nia hiyo…’nikasema

‘Sio kweli shemeji, hilo …nakuapia, mimi siwezi kufikiria hilo,na kama ningelifahamu kuwa kaka anataka kufanya hivyo, ningekuarifu…’akasema

‘Na hayo mauaji mengine..?’ nikauliza

‘Mauaji gani, ..shemeji, hivi kweli mimi naweza kumuua mtu…’akasema

‘Umeshirikiana wewe na kaka yako kulikamilisha hilo..hata kama wewe hujafanya, ila unafahamu hizo njama kwahiyo mumeshirikiana naye…’nikasema

‘Hapana…mimi sijui lolote ..’akasema

‘Haya, nakupa muda wa kuliwazia hilo, hapa hapa, kabla polisi hawajafika, maana wao wakifika utawaelezea vyema, kwanini kaka yako alitaka kuniua hilo lazima watakubaba mpaka useme,  …’nikazidi kumshinikiza kwa hilo, nia ni kumjenga hofu ili aweze kuja kuniambia kila kitu ninachokitaka

‘Pili, kaka yako nashukiwa kuwa kashiriki au ndio yeye kamuua Makabrasha, aliwezaje kwenda huko wakati anaumwa, ni lazim akuna mtu alimsaidia, ni nani, kama sio wewe jembe lake, kwahiyo alikuita ukampeleka au sio…?’ nikamuuliza na hapo akashtuka na kuangalia kule getini.

‘Sema ukweli shemeji, …ukweli ndio utakusaidia..’nikasema

‘Kaka alikuwa mgonjwa, huenda ugonjwa wake ndio uliomfanya akafanya hivyo, mimi sijui lolote utanionea bure tu shemeji…’akasema

‘Haya…, kama ni ugonjwa, angwezaje kufika huko….ni lazima kuna mtu alimsaidia,…hapo huwezi kukwepa…’akasema

‘Shemu mimi naomba tafadhali..usiwaambie polie lolote kwa hivi sasa, subiria kaka apone kwanza…’akasema

‘Haya ni lazima yawekwe kwenye kumbukumbu za polisi, kuna leo na kesho, je ikitokea akafanikisha dhamira yake,..kutapatikana wapi ushahidi wa rejea…hapa ni kauli yangu na yako, ni lazima watu wa usalama wawe na habari hizi..’nikasema

‘Hapana, sio vyema shemeji, na kwanini mimi nihusike hata hivyo..?’ akauliza

‘Kwasababu hata wakati anataka kuniua, alikutaja wewe, na kakiri kuwa wewe ndiye jembe lake…, kwanini akutaje wewe kuwa umsaidie hebu jiulize hapo…’nikasema

‘Mimi sijui labda ni kuongea tu, …’akasema

‘Docta anasema mengine anayafanya kutoka na kumbukumbu alizokuwa nazo kichwani, na moja ya kumbukumbu zake ni wewe. Mlivyoongea , mlivyopanga…ndio maana nakutilia mashaka, hata polis wanakutilia mashaka, ndio maana wanataka kukutana na wewe, mimi nimetaka kukusaidia, lakini hutaki kuniambia ukweli, basi nanawa mikono...’nikasema

‘Shemeji mimi jana nilipokuja nilienda chumbani kwangu, kweli si kweli, na kiukweli mimi nilichelewa kulala , kwahiyo hata usingizi uliponishika nilala fofofo, ndio nikaja kuamushwa na huo mlio wa bunduki, sikujua kabisa ni nini kimetokea, na nilipoamuka ndio nikakimbilia kuja kuwaona, nilijua kua mtu kaumizwa, nilipokuona upo sawa, ndio nikashikwa na butwa, nikijiuliza huo mlio wa bastola ulikuwa wa nini,.....’akasema

‘Kwahiyo kwa kauli yako hapo, ulijua kaka yako kaniumiza..au kaniua…?’ nikamuuliza

‘Kaka nimemuona yupo vile, hajaumizwa, hana jeraha, kwahiyo iliyokuwa imebakia ni wewe..ndio nilipokuona nikawa na hiyo hali, unayosema ni ya kushangaa…’akasema

‘Haya sawa, kuna jambo nataka uniambia maana ukitoka hapa, hutakuwa na mimi tena, utakuwa mtu wa polisi, huyo mwanamke aliyezaa na kaka yako ni nani, umesikia akisema kuna mwanamke wake, huyo mwanamke anampenda sana kwa vile kamzalia mtoto wa kiume, jembe jingine…, ni nani huyo mwanamke?’nikamuuliza.

‘Mimi simjui huyo mwanamke,  ...naona alikuwa anaongea tu kama mtu aliyechanganyikiwa...huoni hata sauti yake inasikika kama mtu aliyelewa, kama teja, kama mtu yupo usingizini, na shemeji kwanini unasema hutakuwa na mimi, nitakuwa na polisi kwa kosa gani...?’akasema sasa akijua simtanii…

‘Kila kitu nikikuuliza mimi unasema hujui, …nitakusaidiaje eeh, hebu niambie,na wao wanataka kukutana na wewe, kukuhoji..kuujua ukweli,..na kwa maelezo yak ohayo, ni nani atakuamini, unaichanganya…wewe...utakwenda kulala jela...’nikasema sasa nikichukua simu yangu, hapo akawa ananiangalia huku akionyesha kuogopa

‘Shemeji mimi nina uhakika , kaka anakupenda sana asingeliweza kufanya kitu kama hicho akiwa sawasawa, mimi nahisi kafanya hivyo, kutokana na kuchanganyikiwa...na unataka nikuambie kitu gani ili uniamini, ..mimi sijui zaidi ya hayo, msubirie tu kaka akipona utamuuliza’akasema

‘Ngoja polisi waje…, naona wamechelewa sijui kwanini..natumai ukiwaona ndio utajua kuwa wewe upo matatani. Kwa maelezo yako tu, mimi nimethibitisha kuwa kuna kitu mpo ushirika na kaka yako, na haya yaliyotokea na wewe unahusika, sasa..wewe utaweleza  yote jinsi gani unavyofahamu wewe, ili ibakie kwenye kumbukumbu zao, unasikia....’nikasema.

‘Shemeji, acha usiwapigie simu polisi…,’akasema

‘Nikiwapigia, nisiwapigia ni hali moja, wewe utahojiwa na wao, na wao walisema watakuja hapa,..na nimeoa ni bora wakuhojie hapa, kuliko kukupeleka kituoni, ili nisikie wanachokuhoji…’nikasema

‘Shemeji, nisaidie, na msaidie kaka..huyo ni mume wako, kwa hili utamtia hatiani, ..kama kuna kitu kingine niulize tu, nitakuambia kila kitu utakavyo, lakini waweke mbali polis na kaka,, utamchanganya kichwa kabisa ..’ akasema na mimi nikawa tayari nimeshampigia simu ofisa mmoja wa upelelezi ninayemfahamu..

NB: Sehemu hii nimeandika kwa haraka haraka, naweza nikawa nimerudia rudia, naomba ipite hivyo, ili tusonge mbele.WAZO LA LEO: Moja ya rehema za mwenyezimungu, ni mapenzi kati ya mume na mke, kuhurumiana na kujaliana.        Wawili hawa wanakuja kujenga familia , na huenda walikutana tu bila hata kujuana, ni nani alijua wewe utamuoa huyo uliye naye au kuolewa naye, ni kwa rehema za mola wetu….sasa kwanini tunakuja kuliharibu hilo, watu wanakuwa hawaelewani tena, ndoa zinakuwa ndoana. Tumuombe mola wetu azijalie ndoa zetu, ziwe za upendo, na furaha, na wale ambao hawajajaliwa kuwa na ndoa, mola awajalie walifanikishe hilo, kwa rehema zake. Aamin. 

Ni mimi: emu-three

No comments :