Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, January 16, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-59


‘Haloo, afande unasemaje…’nikauliza baada ya kuiweka simu hewani

‘Nilikuwa nyumbani kwako nimeambiwa umeelekea hospitalini, basi kama utakuwa na nafasi nataka kuongea na wewe, sijui…kesho labda…’akasema

‘Kuhusu nini..?’ nikauliza

‘Kuna muendelezo mpya wa upelelezi kuhus kifo cha Makabrasha, kuna maswali mawili matatu nilitaka kukuuliza…’akasema

‘Bado mnanishuku mimi…?’ nikamuuliza

‘Hapana,..ni kuhus mumeo…’akasema

‘Kafanya nini..?’ nikauliza

‘Nitakuambia tukikutana mimi na wewe,..kama hutojali…’akasema

‘Kama ni kuhusu mume wangu msubiria apone, labda kama linanihusu mimi, na kama linanihusu mimi pitia kwa wakili wangu, ingelikuwa ni bora zaidi…’nikasema

‘Hamna shida..’akasema na kukata simu

*********

 Nilipofika hapo hotelini, sikuweza kumkuta huyo mtu, nikasubiria kidogo, nikawa najiuliza nifanye nini sasa maana sina namba yake…nikasubiria robo sasa ikapita, nusu saa ikapita….nikaona sasa napoteza muda wangu na muda huo natakiwa niwe hospitalin, nimeshaanza kuchelewa,..

Ni wakati naingia kwenye gari langu, sasa nimeshaamua kuondoka, ndio ukaja ujumbe wa maneno, kuwa yeye ameondoka hapo kwasababu za kiusalama, atanijuliasha baadae ni kwanini;

‘Mjinga sana wewe…’nikasema hivyo tu

 Nikaondoka hapo nikiwa nimeanza kuchelewa kufika huko hospitalini, huku akili yangu ikiwa na hasira kuwa maandalizi yangu yote ya kumnasa huyo mtu yamekwenda bure;

Nikafika hospitalini…

‘Mgonjwa yupo na docta wa magonjwa ya akili, kasema ukija uwafuate huko chumba cha uchunguzi…’nikaambiwa na kwa haraka nikaelekea huko kwenye chumba maalumu

‘Tumekusubiria sana …’akasema docta

‘Foleni za dar, lakini hata hivyo nimejitahidi sana…’nikasema

‘Hukuonana na huyo jamaa?’ mume akaniuliza, swali lake likanipa mashaka, nikabakai kumuuliza

‘Jamaa gani…?’ nikamuuliza kwa mshangao, na yeye akaniangalia kwa mshangao, na baadae akasema;

‘Ok,.. basi samahani, hata sijui, …, tuendelee…’akasema hivyo, na docta akaingilia kati na kusema

‘Tuendelee mgonjwa au umechoka…’akasema

‘Hapana sijachoka wewe uliza maswali yako tu…’akasema mume wangu

Huyo docta akawa anamuuliza mume wangu  maswali mengi nikiwepo hapo hapo, yeye mwenyewe anajua ni kwanini anamuuliza hivyo, na mengi ya hayo maswali yalijibiwa kuwa ‘hakumbuki’ ‘hana uhakika’…au ‘hajui’

‘Hata kilichotokea usiku…hukumbuki…?’ akaulizwa

‘Kiukweli sikumbuki, na nawaza sana kuhusu hilo,..lakini sipati jibu…’akasema

 Baadae akaulizwa maswali mengine mengi ya nyuma, hadi ikafikia kuulizwa maswala ya historia yake, kuhusu maisha yake, na baadae akaulizwa kama ana kitu anakitafuta kinampa mawazo je anahisi labda ana mtoto wan je au aliwahi kufanya jambo gani baya, docta akawa na maswali mengi akitafuta jambo

Hata hivyo majibu mengi ya hayo maswali yakawa yale yale ‘hakumbuki’ au ‘hajui’ au ‘hana uhakika..’

Basi hatua ya pili ikatakiwa mume wangu akapimwe kipimo cha ubongo, na uti wa mgongo,…docta alitaja vipimo hivyo, kama CT scan, na PET scan, …akachukuliwa kuelekea huko

‘Baada ya hivyo vipimo ndio nitaweza kutoa taarifa yangu kwa ukamilifu…’akasema huyo docta..Baadae nilikaa mimi na huyo docta, wakati huo mume wangu yupo huko kwenye vipimo, na docta akaanza kunihoji na mimi.

‘Hebu niambie kuna kitu gani kigeni kimetokea kwa mume wako?’ akaniuliza

‘Kwanza namuona kabadilika kabisa sio yule mume wangu ninayemfahamu, sasa sijui ni kwasababu ya hayo matatizo au anaiigiza, maana simuelewi,..., kitabia, na hata kimatendo ni tofauti na zamani, na zaidi anakuwa msahaulivu,...’nikasema

‘Hiyo ni kawaida...nionavyo mimi ni kwasababu ya hilo tatizo,...na ushukuru kuwa yeye haikumuathiri sana, ....na hali yake sio mbaya,....yanayotokea ni matatizo ya kawaida tu. Nina uhakika kuwa akitoka hapa safari hii hali itakuwa njema kabisa,...Je kuna jingine lolote uliloligudua ambalo hakuwa nalo kabla?’ akaniuliza na mimi nikatulia kidogo akili ikiogopa kusema tukio la jana, sikutaka lijulikane na watu wengi, nikasema;

‘Eti docta kuna mtu anaweza kuamuka usiku akafanya kitu na akiamuka asubuhi hakumbuki kabisa?’ nikamuuliza

‘Kwa vipi,..je mtu huyo anaamuka akiwa na fahamu zake, au anakuwa amelala..?’ docta akaniuliza

‘Hata sijui nisemeje..’nikasema hivyo

‘Nakuelewa, ila nataka uhakika kidogo, ....maana kuna ugonjwa wa namna hiyo, lakini mtu wa namna hiyo anakuwa amelala, anaamuka akiwa usingizinini, na kutenda matendo akiwa usingizini,..hajijui hapo, yeye hapo anaota, japokuwa ndoto za namna hiyo muotaji hazikumbuki ....’akasema.

‘Mhh, ndio hivyo..’nikasema hivyo nikiwa sina uhakika kabisa na hilo.

‘Ni hivi mtu wa namna hiyo, anakuwa kwenye ndoto, lakini tofauti ya ndoto yake na ndoto za kawaida ni kuwa, yeye anatenda yale matendo kivitendo, ....’akasema.

‘Sasa mimi siwezi kujua kama alikuwa usingizini au alikuwa anaigiza…’nikasema

‘Ili umfahamu huyo mtu vyema, mchunguze machoni, na jinsi anavyotembea,..macho yake yanakuwa na weupe kile cheusi hukioni,…pili kutembea kwake ni kama kwa kunyata,...hivi…’akasema

‘Oh, mume wangu alikuwa hivyo hivyo, ulivyosema…’nikasema

‘Basi ndio tatizo hilo la kuota huku unatenda kwa vitendo…na hebu nikuulize je tatizo hili lilianza lini…?’ akaniuliza

‘Mimi naona ni baada ya hii ajali, maana mimi sijawahi kumuona hivyo kabla ya hapo…’nikasema

 ‘Inaweza ikawa hiyo ajali imesababisha hayo, maana ubongo ni kitu nyeti (delicate )sana, kikipata mtikisiko wa namna kama hiyo ya ajali, unaweza ukaharibu mfumo mzima wa mawasiliano mwilini, akili, ikawa sio yako tena, ndio maana unakuta watu wanapooza viungo, wanapoteza kumbukumbu na wengine wanaharibikiwa kabisa...’akasema.

‘Oh…’nikaguna hivyo

‘Lakini pia tatizo kama hilo linaweza kuwa ni la kurithi, huenda familia hiyo kuna mtu mwenye tatizo kama hilo, baba,mama, au wazee wao, lakini hili la mume wako, litakwisha tu maana kwa silimia kubwa tunaona ni kutokana na hiyo ajali iliyomkuta, na kama ni la kizalia ndio limejitokeza sasa, tutajua jinsi gani ya kulidhibiti..’akasema

‘Kwahiyo anaweza hata kufanya mambo mabaya bila kukusudia?’ nikamuuliza

‘Ndio... wengine wanafiki hata kuua, ukisoma visa vingi, huko Ulaya imetokea hivyo, hata hapa kwetu mhh.., tatizo huku kwetu hatuna kumbukumbu za kulithibitisha hilo, lakini wenzetu wanakuwa na kumbukumbu za kudumu za kitaalamu ...’akasema

‘Oh, sasa utawezaje kuishi na mtu kama huyo..je akija kunigeuka na kunidhuru mimi mwenyewe au watoto…?’ nikauliza

‘Cha muhimu ni kufahamu chanzo cha matatizo hayo, je tatizo la kuzaliwa. Labda karithi kutoka kwenye ukoo wao, au ni kutokana na majanga kama haya ya ajali,...baada ya hapo kuna utaratibu wa matibabu,...cha uhakika kujua historia yake ni kujua kutoka kwa watu wanaomfahamu toka utotoni, au hata mke, kama ilishatokea ukiwa naye, lakini pia kutoka kwa wazazi wake, je wao, wana tatizo hilo au kwenye jamaa zao….je mume wako amekuwa na tabia kama hizo kabla, ni muhimu sana hilo..’akasema

‘Kabla hapana, tangu tuoane sijawahi kuliona hilo kabla…’nikasema

‘Hiyo jana ilikuwaje…?’ akauliza

‘Hiyo jana kama nilivyosema, alitoka kitandani akaenda sehemu nyingine, akafanya matendo , na akarudi na bahati mimi nilikuwa sijui , nikamshitua, akadondoka akapoteza fahamu...sio kupoteza fahamu …sio hivyo.., ila alionekana kama kalala tena,...pale alipodondoka...’nikamwambia.

‘Mtu wa namna hiyo haitakiwi kushutuliwa kabisa..,ukimuona mtu wa namna hiyo wewe unachotakiwa kukifanya ni kumfuatilia taratibu kimiya kimiya, ili kuhakikisha usalama wake, kwani atafanya kile kitu anachotaka kukifanya na baadaye anarudi kulala kama kawaida, ukimshitua, unaweza ukamsababishai madhara mengine...’akasema.

‘Oh, ...sasa kama ni hivyo, mbona inanitisha docta....’nikasema

‘Usiwe na wasiwasi, mimi matatizo hayo nayafahamu sana, ndio ujuzi wangu, hilo tutaliangalia kwa makini, kuna jinsi ya kumpima, na tutagundua ukweli zaidi, usiwe na hofu, ..kama ni kutokana na ajali litakwisha lakini kama ni kutokana na kizalia, tutaweza kuliangalai kwa namna nyingine zaidi...’akasema

‘Oh, haya docta huyo ni mgonjwa wako sasa…’nikasema

‘Unajua mara nyingi tatizo hilo linahitajia muda sana kulitatua, hasa kama ni la kizalia, na wewe mke utakuwa na kazi ya kutusaidia, ili tujue hatua kwa hatua maendeleo yake, kwa hivi sasa tunahitajia tukae naye, tumchunguze, tuone tatizo lipo wapi zaidi...na tuta-mu-hypnotize…ndio matibabu yake makubwa’akasema

‘Mhh, sijui kama ni kizalia,....maana haijawahi kutokea hivyo kabla, labda kwa vile sikuwa makini na hali kama hiyo, umesema kitu gani..?’ nikauliza maana alitaja neno sikulielewa, na hata baada ya kumuuliza hakulifafanua  kuwa maana yake ni nini...

‘Basi hiyo kazi tuachie sisi, tunafahamu jinsi gani ya kuligundua,lakini hata hivyo ningelihitajia niongee na watu wake wa asili, kuna ndugu yake yoyote wa kuzaliwa naye, baba au mama ninaweza kuongea nao kidogo, kwani hilo linaweza kutupunguzia muda, kama hakuna tutajua jinsi gani ya kuligundua kitaalamu zaidi?’ akaniuliza

‘Yupo mdogo wake lakini sizani kama anafahamu lolote kuhusu historia zao, mimi nahisi kuwa tatizo hilo limetokana na ajali....’nikasema.

‘Kama limetokana na ajali lingejitokeza mapema,tungeliligundua siku za mwanzoni kwenye uchunguzi wetu...hata hivyo, kwa vile yupo kwenye mikono yetu, tutaliangalia kwa mapana yake, usijali....’akasema

‘Sawa docta nitafurahi kama nitapata taarifa zake, na ni kitu gani mumekigundua, kama ikiwezekana mapema zaidi, kama itawezekana, vinginevyo, mimi nawategemea nyie ...’nikasema.

‘Hamna shida tutawasiliana...karibu sana..’akasema na mimi nikaondoka kurudi kule alipolazwa mume wangu,…alikuwa kaka kitandani,

‘Unajisikiaje..mume wangu?’ nikamuuliza naa alionekana kama anataka kulala, labd ni dawa au kuchoka

‘Mhh..mimi sijambo, ni usumbufu wao tu, maswali mengi, vipimo vingi, lakini mimi sioni kama ninaumwa mahali..ila hapa nahisi kutaka kulala..’akasema.

‘Lakini ni vyema ukafuata ushauri wao ili kuondokana na tatizo hilo kabisa….’nikasema

‘Sawa…hamna shida nitafanya hivyo..’akasema

‘Kuna lolote zaidi maana nataka kuondoka muda wa kuona wagonjwa umeshapita, wamenisaidia tu kwa dharura…’nikasema

‘Mke wangu unaweza kwenda tu, usiwe na wasiwasi na mimi kabisa, mimi hapa sina tatizo, sihisi tatizo kwa sasa, na ningependekeza kuwa wewe haina haja ya kuja hapa mara kwa mara kuniangalia, mdogo wangu anatosha, yeye nitakuwa nikimtumia kama nitahitaji kitu, wewe hangaika na shughuli za kikazi, hasa kwenye kampuni unayoihudumia wewe, au sio...’akasema

‘Hamna shida...wewe angalia afya yako, hakikisha unafuata masharti ya dakitari, tafadhali, usije ukatoroka, hayo maswala ya kazi usiyafikirie kabisa, afya ndio muhimu, ukiwa huna afya hata kazi haina maana tena au sio…mimi nitajitahidi kufika kazini kwako nione kama naweza kufanya lolote..’nikasema

‘Kwanini nitoroke,...’ akasema hivyo akiniangalia, na mimi sikusema kitu hapo

‘Mke wangu mimi sijawahi kutoroka hospitalini, mimi sio kichaa, au mfungwa,...nimekuja hapa kwa hiari yangu mwenyewe, na nitafuata kila kitu, usiwe na wasiwasi na mimi kabisa..’akasema

‘Sawa hamna shida, ..muhimu ni kujali afya yako, na nikutakie afya njema, kila-laheri...’nikasema na kuagana naye, kabla sijaondoka akasema

‘Na kazini kwangu pasikusumbue sana, kuna mtu nikiwa hivi yeye anafanya shughuli zote,…’akasema

‘Sawa hamna shida…’nikasema

Wakati natoka mlangoni, niligeuka nyuma, nikamuona akipiga simu, aliponiona nimegeuka kumuangalia akairejesha simu kwa haraka kama kuficha ili nisijue kuwa alikuwa akipiga simu, sikuelewa kwanini anafanya hivyo…

********

Nikarudi nyumbani, na kumuita fundi ambaye nilimuagiza abadili vitasa vyote vya makabati, ....nikasimamia hilo zoezi mpaka likamalizika, halafu nikahakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, sikutaka kuangalia ndani ya makabati, japokuwa nilikuwa nataka kupitia pitia kabati la mume wangu, lakini nikaona huo sio wakati muafaka, kwani nilijua hakuna kitu cha zaidi ndani ya kabati hilo.

Wakati nataka kuelekea bustanini , kwani napenda sana kupumzika kwenye bustani yangu, mara nikasikia gari linaingia getini, alikuwa mdogo wa mume wangu, alionekana kuwa na haraka, alisema kaja kuchukua baadhi ya vitu vyake alivyokuwa akivifanyia kazi usiku,  nikamwambia hakuna shida mimi nipo bustanini, akitaka kuondoka  aniambie.

‘Sawa, na kuna vitu kaka kaniagiza,nije kuvichukua, kanielekeza wapi pa kuvipata ....’akasema

‘Sawa wewe mchukulie…kama kuna kingine hutakiona au unakihitajia kwa ajili yake wewe niambie tu….halafu ukishakuwa tayari kuondoka, nataka tuongee kidogo....’nikasema.

‘Sawa lakini nina haraka kwani kaka anahitaji hivyo vitu vyake kwa haraka, kaniambia nisichelewe...’akasema

‘Sawa sitakuchelewesha sana…’nikasema

Baadaye alikuja bustanini, na kuniambia anataka kuondoka, na alionekana kama ana wasi wasi fulani, nikamuuliza keshachukua hivyo vitu alivyomuagiza kaka yake;

‘Ndio, lakini kuna kitu kaniagiza kaka, ...sasa hilo kabati alilonielekeza  halifunguki..’akasema.

‘Kabati gani hilo na ni vitu gani?’ nikamuuliza

‘Basi hakuna shida, ....labda ufunguo sio wa kwake, lakini...’akasema akiangalia ufunguo aliokuwa nao mkononi.

‘Hivyo vitu ni vitu gani na ni kabati lipi hilo?’ nikamuuliza

‘Kwenye lile kabati kubwa kule maktaba kwenu...’akasema huku akiwa na wasiwasi

‘Ina maana umeingia chumbani kwangu bila kuniambia kwanini usingelianiambia nikaenda kukuchukulia, ni kitu gani unakihitajia ?’ nikamuuliza

‘Mhh, niliona nisikusumbue, niliingia mara moja, kwenye kabati la kaka, kanipa ufunguo wake, kanielekeza kuwa kuna kitu kwenye hilo kabato kubwa, ni makaratasi yake ya kazini, na makabrasha tu.... ’akasema

‘Makaratasi gani ya kazini, wakati dakitari kasema hahitajiki kujishughulisha na jambo lolote la kumfikisrisha, hebu niambie kwa uhakika  ni kitu gani alichokutuma,...na kwanini hakuniambia mimi, wewe unamua kuingia kweye chumba changu hadi maktaba bila ya mimi kujua?’ nikasema kwa ukali nikamuon aakinywea.

‘Samahani shemeji, niliona nisikusumbue tu…’akasema

‘Nilishakufundisha tabia njema, kuomba kitu, kuomba msamaha, salamu nk, hivyo ni vitu vidogo tu lakini vina thamani kubwa sana kwa mpokeaji,..au ni kaka yako alikuambia uchukue bila ya mimi kufahamu au sio…?’ nikamuuliza nikaona anasita sita, halafu akasema.

‘Kaka kaniagiza nikamchukulie, na alisema nitaviona, kwahiyo sikuona haja ya kukusumbua shemeji, hebu nielewe hapo, kusudio langu halikuwa baya...’akasema

‘Akakuambia kuwa uingie bila kuniambia mimi, ?’ nikamuuliza

‘Hajasema hivyo...’akasema, na mimi nikaona nisiendelee na hayo malumbano, nikaona nimuingie kwa njia nyingine.

‘Hebu niambie jana mlipoondoka na kaka yako mliongea nini?’ nikamuuliza na hapa akaangalia saa kuashiria kuwa namchelewesha.

‘Mambo ya kawaida tu ya kimaisha…unajua kaka akielewa anaongea sana mambo mengi…na kwa vile alishachanganyikiwa mengine niliona hayana umuhimu…’akasema huku akionyesha kutaka kuondoka, na mimi sikujali nikaendelea kumuuliza

‘Mimi nataka kujua, nina maana yangu, nimetoka kuongea na dakitari, na maelezo yako yanaweza kusaidia sana..sasa niambie aliongea nini, usijali umuhimu wake..’nikasema;

‘Ni yale yale ya kuchanganyikiwa, kuwa anahisi ana mtoto wa kiume, na tunahitajika kumtafuta, na kulinda haki zake..pia anataka mimi nijibidishe kwenye kazi..ni mambo hayo ya kama ananihusia vile..ni hivyo tu shemeji…’akasema

‘Ulisikia jana mlio wa risasi..?’ nikamuuliza na hapo akashtuka na kusema;

‘Ndio hivi ilikuwa ni nini, maana nilisikia kama mlio wa bunduki, au bastola, kuna muda nimemuliza kaka, yeye anasema hajui kama kuna kitu kama hicho kilitokea…mimi mwenyewe nilishapitiwa na usingizi lakini nikashtuka, na nilipokuja ukasema hakuna tatizo basi sikulichukulia maanani…’akasema

‘Yote hayo aliyafanya kaka yako, ..ndio maana nataka kufahamu jana mlipoondoka wewe na yeye mliongea nini…kuna umuhimu mkubwa kulifahamu hilo, usione kama nakupotezea muda, sio jambo rahisi kama unavyofikiria wewe…’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka, na kusema;

‘Tulichongea ni hayo niliyokuambia shemeji, mengi ni mikakati yake ya maisha kuhakikisha kampuni yake imekuwa kubwa, ana ndoto za kuwa tajiri, na vitu kama hivyo, amesema kuwa sasa hivi kaamua kutimiza wajibu wake, kwani sasa ana kampuni zaidi ya moja, na yeye ndiye msimamizi...’akasema

‘Kakuambia kampuni zake, kwani yeye ana kampuni gapi nyingine unayoifahamu wewe..?’ nikamuuliza

‘Mimi hapo sijui…ndio maana nikasema mengine alikuwa akiongea tu, kwa kuchanganyikiwa kwake..’akasema

‘Ndio akasema sasa hivi anataka kutimiza wajibu wake kwa vipi, kwani huko nyuma ilikuwaje? Nikamuuliza na akaangalia saa tena.

‘Anasema huko nyuma, alikuwa hajajitambua kuwa ana majukumu makubwa, kiasi hicho, sasa hivi kashajitambua kuwa ana majukumu makubwa kama baba wa familia, kama mtendaji mkubwa wa makampuni yake, kwahiyo inabidi abadilike, hataki kuja kulaumiwa...’akasema

‘Je mliongea lolote kuhusu mkataba?’ nikauliza na hapo akashituka na kugeuka kuangalia sehemu nyingine, nikahisi hapo kuna jambo, kwanini nilipotaja mkataba ameonekana kama kutahayari….akakaa kimia akiangalia saa

‘Unajua shemeji muda umekwenda..mengine utamuuliza mwenyewe, tafadhali shemeji..’akasema

‘Umenisikia swali langu, nililokuuliza...?’ nikasema.

‘Sijui unazungumzia mkataba gani, maana sielewi mambo yenu na kaka’akasema

‘Una uhakika na hilo, ...kuwa huelewi lolote kuhusu mkataba, wakati jana niliongea na kaka yako akaniambia yote, kuwa wewe unafahamu kila kitu, wewe ndio yeye, au nimekosea...’nikasema

‘Kaka alisema hivyo?..haah shemeji unajua Yule mtu kachanganyikiwa anaongea tu..’ akauliza kwa mshangao

‘Ndio kaongea hivyo, ...sasa niambie ukweli, jana mlipokwenda na kaka yako hamkuongea lolote kuhusiana na mkataba, maana kama kakuambia kuhusu makampuni yake, huenda kafungua kampuni nyingine mimi siijui, huenda hayo yapo kwenye mkataba uliotengenezwa na yeye na marehemu, hilo unalifahamu sana, kweli si kweli,?’ nikamuuliza

‘Lakini shemeji umesema, kuwa mliongea na kaka kama mliongea naye kwanini unaniuliza mimi tena, na shemeji ni vyema hayo mambo yenu mkayamaliza nyie wenyewe, hayo ni mambo yenu ya ndani, na mimi sifurahii kuwekwa mtu kati…’akasema kwa hali ya kama kukasirika hivi lakini hakuionyesha hiyo hali, maana kiukweli jamaa huyu ananiheshimu sana na mara nyingi anakuwa kama ananiogopa japokuwa sasa ni mtu mwenye mke wake,....’akajitetea

‘Kama ni mambo yetu ya ndani kwanini kaka yako anakutuma wewe mambo ambayo unajua ni mambo yetu ya ndani ya mimi na mume wangu, wewe unayafanya tena kwa siri bila ya mimi kufahamu..?’ nikauliza na yeye akakaa kimia

‘Na ni kwanini wewe uwepo kwenye huo mkataba usifahamu kuhusu huo mkataba,halafu  kwanini kaka yako akakuambia mkaongee naye huko mlipokwenda jana , na kwanini anakuita wewe ‘Jembe lake’  hayo yote nayafahamu mimi sasa niambie ukweli?’ nikamuuliza na y eye hapo akawa kama hataki kusema lolote,akaniangalia mara moja na kusema;

‘Shemeji naomba unielewe, nafanya hayo kwa vile kaka ananituma, na mimi kama mdogo wake, ninawajibika kumtii, lakini ...sina  haja ya kuingilia mambo yenu ya ndani, sitaki kabisa kufanya jambo ambalo wewe litakuumiza…’akatulia na kuangalia sasa

‘Usiangalie saa hili tunaloongea hapa ni muhimu sana…’nikasema

‘Shemeji ..kaka kaniambia nisichelewe …’akasema

‘Utamwambia nilikuchelewesha mimi…unasikia…’nikasema

‘Nikimwambia hivyo itamkwaza sana, sitamuambia lolote kama tulikaa tukaongea, mimi na wewe kumhusu yeye, najua itampa shida sana kuwaza, natumai unanielewa na kuniamini kwa hilo..na pia kwa vile…’akakatiza hapo kuongea na kujifany akuangalia saa.

‘Kwa vile alikutuma na kukuambia usiniambie kuwa kakukutuma kitu, ujifanye unakuja kuchukua vitu vyako au sio…?’ nikauliza

‘Shemeji mimi namtii kaka yangu, kama ninavyokutiii wewe, kwangu mimi nyie watu wawili ni muhimu sana kwangu, na-na-waheshimu sana..sitaki kumkwaza kaka , na halikadhalika wewe, wakati mwingine nafanya mengine ili tu kaka asije kukasirika akahamanika na hilo docta kasema tulichunge sana....’akasema

‘Hebu niambie ni jambo  gani ulilowahi kulifanya kwa vile kaka kakuambia tu, lakini wewe hukulitaka kulifanya umelifanya ili kaka yako asije akaathirika?’ nikamuuliza na hapo akatulia kimiya, nikaona nisimpotezee muda .

‘Kuna kitu nataka nikuonyeshe na kama usiponiambia kile ninachokuuliza inabidi niwaite polisi, maana naona yeye sasa anashirikiana na watu wa nje , ukiwemo wewe, ili kuja kunifisdi, na tukio la jana limenithibitishia hilo, nyie mnataka kuniua, na sijui lengo lenu ni nini baada ya mimi kufa...’nikasema.

‘Shemeji, hayo yametoka wapi…?’ akaniuliza akionyesha uso wa mshangao.

‘Ushahidi upo,..sio kwamba naongea tu kutoka hewani, sasa kama kweli ulivyosema wewe ni kweli kuwa unanijali, na mengine unayafanya kumrizisha tu kaka yako japokuwa wewe hutaki kuyafanya hayo….sasa nataka kulihakikisha hilo..na huu ushahidi umenifungua macho, kuwa nyie wawili mna njama na mimi…’nikasema

‘Shemeji ushahidi gani huo, na kuna nini…kinachoendelea shemeji, mimi sitaki kabisa kushiriki kwenye mambo yenu, hata hilo la mkataba, nililikataa kata kata.., lakini kama nilivyokuambia, mengine nayakubali ili tu kumrizisha kaka…’akasema

‘Kwahiyo uliitwa kuweka sahihi tu au ulikuwepo kwenye hicho kikao chao…?’ nikauliza

‘Niliitwa kuweka sahihi tu,..na nilipojaribu kukataa, nikaonywa, …sasa shemeji usinilazimishe mimi niongee mengi, hebu jiweke wewe kwenye nafasi yangu, ungelifanyaje…’akasema

‘Na kwasababu hiyo, kama umekubali kushirikiana na matepeli, wezi, walaghai na wewe utakuwaje? Ee niambie..! Sasa mimi nataka nilione hilo, kama kweli hutaki kushirikiana nao…nataka unionyesha, na mimi nitakulinda, nakuhakikishia hilo, lakini kama hutajitoa kimatendo, basi nitachukulia kuwa na wewe ni miongoni mwao, na sitasita kuchukua hatua,..na sio kusita hatua zimeshaanza kuchukuliwa…’nikasema

‘Shemeji kwni kuna nini..mbona mnaniweka kwenye wakati mgumu…’akalalamika

‘Je jana hamkupanga kuja kunimaliza, na labda hukupenda lakini ulifanya kwa vile kaka yako alitaka kulifanya hilo, niambie ukweli..?’ nikamuuliza

‘Shemeji, mimi hiyo kauli siitaki, nakuheshimu sana shemeji yangu, wewe ni sawa na dada yngu mkubwa, nimeishi nawe hapa ukanisaidia sana, lakini hilo unalolizungumza sasa hivi limevuka mpaka, kwanini mimi nifanye hivyo, kwanini…’akasema sasa akionyesha kukerwa.

‘Sikiliza …’nikasema

‘Hapana shemeji mimi naona niondoke, maana haya mazungumzo yatanikosesha adabu, na mimi silitaki hilo litokee nitajilaumu sana, hapana shemeji ngoja niondoke tu…’akasema, lakini sikumpa muda huo, nilijua leo ni leo tu.

‘Nimekuambia nina ushahidi na hicho ninachokisema, sisemi kwa kukisia tu, na hapa najipanga jinsi gani ya kuongea na askari, atafika hapa muda wowote, sasa nilitaka kujua ukweli kutoka kwako, kama hutaki kusema ukweli, basi wewe utausema yote mbele yao, watajua jinsi ganu ya kukufanya uongee..’nikasema na hapo akatulia, na akaonekana kuwa na mashaka

‘Kwani kulitokea nini shemeji…?’ akauliza sasa akionekana limemgusa
Nikachukua ile mashine ya kuchukua kanda ya video zamatukio nikaweka sehemu ambayo anaweza kuona, nilitaka kumuonyesha sehemu ndogo tu, ili niweze kumchota mawazo, na najua kuna ukweli mkubwa anaufahamu lakin anaogopa kumchongea kaka yake....

‘Haya angalia ushahidi huo…’nikasema nikimuacha aangalie

‘Oh shemeji....mbona, ...oh, inaonyesha anampiga mtu, sio wewe ulikuwa umelala hapo...mbo-mbona ....’akawa hamalizii

‘Sasa niambie ukweli jana mlipotoka wewe na kaka yako, mliongea nini au mlipanga nini maana ushahidi umeuona,..polisi wanakuja, na wewe ni mzima, kaka yako ni mgonjwa, kwahiyo wewe utahusika kwa hili moja kwa moja

‘Shemeji..mimi sijui-ki-kitu…’akasema sasa akiangalia kule getini, aliposikia gari linapita akajua ni polisi hao wanakuja

‘Unakumbuka asubuhi nilikuambia nini,…’mbona unashtuka kuniona, unakumbuka..?’ nikamuuliza

‘Mhh..akaguna hivyo

‘Sio kweli kuwa uliponiona ulionekana kama unashtuka,..sasa hivi wajifanya hujui,..ulishtuka nini, ni baada ya kuniona mimi nipo hai, au sio… au unajifanya hujui mlichokipanga wewe na kaka yako, au niambie kaka yako alisema anataka kunifanyia nini mimi…?’ nikamuuliza hapo kwa ukali…

NB: Tutaendelea na sehemu hii uone mdada alivyoliweka hilo jambo, na hatimaye ikawa ni sehemu ya kupiga hatua kuishinda hiy mitihani inayomkabili


WAZO LA LEO: Asili ya nafsi ya binadamu ni ubinafsi, na usipoweza kuidhibiti nafsi yako, tamaa huchukua nafasi, na shetani anakuwa ndiye rafiki yako mkubwa, na hapo ndio unajikuta hujali kufanya maasi, dhuluma inakuwa ndio jadi yako, na ukifika hapo hutawajali wanadamu wengine,  hutakuwa na huruma...imani ya ucha mungu kwako inakuwa ni hadithi. 
Ni mimi: emu-three

No comments :