Ilipofika asubuhi, nikiwa
nimechoka, macho yana usingizi, maana ilikuwa hakuna kulala…mjamaa yeye alikuwa
anakoroma tu, usingizi kwa kwenda mbele. Hata asubuhi ilikuw kazi sana
kumuamusha.
‘Leo sijisikii vizuri mwili umechoka sana…’akasema
‘Ndio maana tunataka twende hospitalini…’nikasema
‘Hapana wewe nipe zile dawa zangu, leo hata kazini nitachelewa
kwenda ..’akasema
‘Sikiliza…’nikasema na kabla sijaendelea kuongea yeye akasema;
‘Kuna ndoto mbaya niliota
usiku.., lakini sikumbuki ni ndoto gani,...sikumbuki kabisa, lakini ilikuwa ya
kutisha inavyoonekana, sitaki…hata kuikumbuka maana sio nzuri, muhimu
nimegundua ni ndoto tu....’akasema huku akijaribu kukumbuka
‘Uliotaje..?’ nikamuuliza
‘Yaani najaribu kukumbuka lakini haiji akilini….na bora
nisiikumbuke tu..’akasema
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Ni mbaya…’akasema akiniangalia mimi kwa macho yaliyojaa wasiwasi,
ni kama haamini, au…
‘Nikuulize hukumbuki kabisa kilichotokea jana..?’ nikamuuliza
‘Jana..hapana..sikumbuki zaidi ya ndoto mbaya, hata hiyo ndoto
haiji akilini, …’akasema
‘Jana wewe hukuwahi kuingia maktaba usiku ukachukua kitu?’
nikamuuliza
‘Kitu…! Kitu gani…hapana, mimi sijaingia huko kabisa, hilo
usinidanganye, nakumbuka nilipotoka matembezi na mdogo wangu, ila kuna sehemu,
nakumbuka kuwa nilitoka na mdogo wangu, mdogo wangu yupo..?’ akauliza
‘Ndio..hilo unakumbuka sio..?’ nikauliza
‘Sasa hapo sijui..ni ndoto ama ni kweli, kama mdogo wangu yupo
basi, inawezekana ikawa ni kweli, lakini mengine sitaki kukumbuka…’akasema
‘Na ulipolala hukuwahi kuamuka hata kwenda kujisaidia hata mara
moja?’ nikamuuliza
‘Nilala kama gogo, nahisi nilikuwa nimelewa,ni kama nililewa, hivi
nilikunywa, kwanini hukunikataza....’akasema.
‘Basi kuna tatizo, kama hukumbuki uliyoyafanya jana basi ujue
unahitajika kwenda kumuona docta hakuja jinsi hapo...’nikasema
‘Kwani kuna nini kimetokea mke wangu..?’ akaniuliza akionyesha
mashaka sasa
‘Nakumbuka kama ulitoka nje, ukaenda maktaba...ukachukua
kitu’nikasema
‘Mke wangu hapana…nakumbuka niliporudi kazini nililala ..hata hiyo
kunywa pombe mimi sikumbuki kabisa..ila kuna kitu nahisi kuwa mimi nilikuwa na
mdogo wangu, hapo sina uhakika…’akasema
‘Hakuna shida, wewe jitahidi sana kutuliza kichwa, ili uweze
kukumbuka vyema, na ili akili yako iwe sawa, inabidi twende hospitalini
wakafanye uchunguzi wa kina maana hali kama hiyo sio nzuri…’nikasema.
‘Mimi siumwi mke wangu hali kama hiyo walisema inaweza kutokea ,
na itapita, usiwe na wasiwasi, ilimradi tu, nikumbuke, maana hata ukinirudisha
hospitalini, itasaidia nini, itaisha yenyewe tu...’akajitetea.
‘Ulitakiwa mara kwa mara uwe unakwenda kiliniki, hujaenda, na
ukumbuke kuwa uliambia kukitokea jambo lisilo la kawaida pia uende haraka
ukamuona dakitari, na unaona hali uliyo nayo, unapoteza kumbukumbu, unafanya
mambo usiku na hukumbuki kuwa ulifanya, ....ni muhimu tukamuone dakitari, hilo
halina mjadala...’nikasema.
‘Oh…kwanini lakini, haya bwana, kama unaona hivyo ni vyema,
tutakwenda tu mke wngu,.....’akasema.
‘Na utakwenda huko ukafanyiwe uchunguzi wa kina, ili tuone tatizo
ni nini, kwahiyo unajiandaa kwenda kukaa huko kwa muda...’nikamwambi na hapo
akashituka na kusema;
‘Hapana, kwenda tutakwenda kw vipimo, halafu tunarudi nyumbani, ...siwezi
kupoteza muda wangu huko, kuna mambo mengi ya kushughulikia, bila kuyamaliza
hayo mambo, sitakuwa na amani...’akasema.
‘Wewe unasema hivyo, lakini mimi niliyeshuhudia mambo ya usiku,
siwezi kukubali, ukalala hapa nyumbani tena.. ni lazima ukafanyiwe uchunguzi wa
kina, kwa hiari , au...’nikataka kusema neno lakini yeye akakatiza na kusema
‘Sawa mke wangu nimekuelewa, nitakwenda,...nitafanya yote
wanayotaka wao, sitaki mke wangu uishe kwa mashaka,..na kukosa amani kwa ajili
yangu, mengine nitayafanyia huko huko hospitalini, . nakupenda sana mke wangu
...’akasema huku akionyesha kutokufurahishwa na uamuzi huo....
‘Ujitahidi sana, kufuata msharti ya dakitari...’nikamwambia
‘Sawa mke wangu, usijali, nitajitahidi sana,....maana nataka
kuondokana na hii hali,...unajua mke wangu niliacha kwenda kiliniki nikijua
kuwa sina tatizo tena,...najua docta atanilaumu sana, lakini ...aah, hata hivyo
najiona nimepona. Mke wangu nataka nipone kabisa tuchape kazi kama zamani.
Tukae tufanya kazi, sitaki nije kuonekana sijui kulea familia yangu...’akasema.
‘Hamna shida, siku ukikumbuka yote yaliyopita ukaniambia ukweli
moja baada ya jingine, ndio nitafahamu kuwa kweli umepona, na hutarudi hapa
nyumbani mpaka nihakikishe hilo...’nikasema.
‘Kwani sijakuambia kila kitu mke wangu, sizani kama kuna jambo
sijakuambia, eti mke wangu kuna kitu sijakuambia kweli, kuhusu nini hasa,
...?’akauliza akiniangalia kwa mshangao
‘Kwa swali lako hilo inaonyesha bado haupo sawa,… hujapona,
ukipona utakumbuka kuwa hujaniambia ukweli wote, na ni muhimu sana kwangu, ni
muhimu sana kwa ajili ya familia hii, umesikia, ukweli wote ndio kibali cha
kuwa wewe umepona vinginevyo, utadumu sana huko hospitalini...’nikasema.
‘Mhh, kweli , hakuna shida...’akasema na tukaondoka kuelekea
hospitalini.
**************
Baada ya mume wangu kufikishwa hospitalini nikarejea nyumbani na
kwanza kabisa nilihakikisha kuwa kila kitu kipo kama kawaida, na ule mto na
shuka lililotobolewa na risasi nilivikunja vizuri, na kuvihifadhi mahala
salama, kama vitahitajika kama ushahidi. Hata ile bastola, mimi nilihakikisha
siugusi bila soksi ya mkononi, vyote hivyo nikavihifadhi sehemu salama.
Nilijua kabisa sauti ya mlio huo wa bastola itakiwa imesikika kwa
majirani, na nilishapanga jinsi gani ya kuwajibu, niliwaambia hakuna
tatizo,....sikutaka kuwaambia lolote, kwani kila kauli utakayotoa, inaweza kuwa
ushahidi baadaye, japokuwa wengi walipoona mume wangu akitoka na kufuatili na
kuona tunaelekea hospitali walijua ni hayo matatizo ya mume wangu ...
Docta jirani yetu ambaye alinipigia simu , nilimuambia kuwa ni yale
yale matatizo ya mume wangu..
‘Lakini nimesikia sauti ya mlio wa bunduki, ..kulitokea nini..?’
akauliza
‘Ni utundu wake tu, ina maana hukuiondoa hapo ilipokuwa...’nikasema
‘Nilikuwa mbioni kufanya hivyo, lakini si unajua mambo
yalivyofungamana…’nikasema
‘Utakuja kukumbuka ushauri wangu, sasa umeamuaje…?’ akasema na
kuuliza
‘Kama nilivyokuambia, hali yake bado, kwahiyo asubuhi tunampeleka
hospitalini…’nikasema
‘Akibisha, wewe niambie nitajua la kufanya..’akasema
‘Sawa nitafanya hivyo…’nikasema
Dunia haina dogo, hata mwandishi mmoja wa habari jirani, alifika
kutaka kujua zaidi nikamwambia hakuna cha zaidi, hakuna tatizo, na ole wake
akiandika mambo ya kizushi...na wananifahamu hakuna lolote lililoandikwa kwenye
magazeti.
Tuendelee na kisa chetu....
*****************
Kutokana na afya ya mume wangu kubadilika hivyo…, mimi ilinibidi
nianze kufikiria mipangilio mingine. Kuna muda nilitaka niachane na haya mambo
kabisa, lakini kwa vipi…maana kuna mambo ya kisheria ndani yake, na hata
nikisema niache yabaki kama yalivyo, nigange yajayo…lakini, hali halisi ikawa
inanisukuma nifanye hata yale nisiyoyataka kuyafanya.... Ndio nikakaa kwenye
kiti na kuanza kuandika…
‘Afya kwanza…’ mkataba wa asili ulitaka hilo, lazima nitimize hilo
kwa ajili ya mume wangu, na hata wakili wangu alinisisitizia hilo, hata hivyo,
hata bila mkataba kiubinadamu, nilitakiwa kuwajibika kwa mume wangu japokuwa mengi yalishajitokeza
yaliyonifanya nianze kubadilika kinafsi,..chuki ilishaanza kugusa nafasi yangu.
‘Lakini lazima hili tatizo liishe, ..’ hiyo ilikuwa fikra ya pili,
kuwa pamoja na hayo, lazima nifikirie namna gani ya kulimaliza hili tatizo
kabisa ili maisha yaendelee sasa kwa vipi
‘Kwa vipi…’nikatulia kuwaza
‘Ehee..hapa kuna mambo mawili…’nikasema
‘Jambo la kwanza…labda mimi nikubali yaishe.. na je nikikubali hilo,
je kutakuwa na madhara gani…?’ nikaandika kwenye laptop yangu…
Je nikikubali …mkataba wao
unasemaje....?’ nikajaribu kukumbuka mkataba wao unavyosema, japokuwa sikutaka
kabisa kuugusa huo mkataba, nikakumbuka kama nilivyowahi kusoma
‘,…kwenye mkataba wao, kama nitakubali yaishe inabidi nikubali
maamuzi ya mume wangu,..kwanza kuwa kakosa na mimi nimeshamsamehe, na kwa maana
hiyo moja kwa moja ninakubaliana na yale waliyoyapitisha kwenye mikataba yao
mingine eti kwa masilahi ya familia, na yaliyomo humo…
-Mume kama mume anashika hatamu…’sio mbaya mimi sikatai,yeye
ashike hatamu tu, lakini kwa msingi gani, sasa…wa haki , au wakutumiwa yeye kwa
masilahi yaw engine, maana hapo anatumiwa tu, halijui hilo…
-Haki za watoto, ikiwemo huyo mtoto wa nje, na kwa vile ni wa
kiume yeye atakuwa kiongozi wa familia…: Mhh, haiwezekani..hili haliwezekani
hata kidini, …siwezi kulikubali, lakini lipo kwenye mkataba, na nikikubaliana
na mume wangu hili linapita bila kupingwa…
-Nikikubali pia, ina maana nimekubaliana na mkataba wao mwingine
ambao mume wangu ndiye anausimamia kama kiongozi wa familia, kwenye huo mkataba
mwingine ambao moja kwa moja unafungamana na mkataba wa asili wa familia,
umewapa watoto wa marehemu hisa, kutoka kwenye urithi wao…
Hawa watu wana kichaa…sitakubaliana na hili.
‘Njia ya pili ni ya kwenda mahakamani, na ikifikia hapo, ndoa,
hakuna…uadui mimi na mume wangu….’
Simu ikaingia ujumbe wa sauti….
Tuendelee na kisa chetu…
*******
‘Mimi ni Yule jamaa mliyekutana naye kule uwanja wa
ndege,..nilikuambia tutakuja kuongea, na sababu kubwa ni kuwa polisi wamenitaka
kunihoji, na pia nasikia wanahitajia mimi niwe shahid kwenye kesi…’akasema
‘Kesi ipi…?’ nikamuuliza
‘Najua madam wewe ni mkurugunzi, unamiliki hisa kubwa kwenye
familia yako, lakini humo pia kuna hisa za watoto wa marehemu, hilo halipo
wazi, na..kutokana na ushahidi nilio nao, hilo litakuja kuwa wazi..achana na
hilo, lakini pia, watoto wa marehemu wanastahiki kumiliki kampuni ya mume
wako..kwa wingi wa hisa walizo nao, na mume wako, hana pesa ana madeni, kwahiyo
uwezo wa kufany alolote hana
‘Na zaidi anakabiliwa na kesi ya mauaji, mimi ninao ushahidi wa
kutosha wa kumweka ndani,…ni swala la mimi tu kukutana na huyo mpelelezi wao,
lakini huyo mpelelezi wao, sipatani naye…ndio maana nikaona nioane na wewe,
tuone tutasaidianaje..’akasema .
‘Mimi kwa ushauri wangu wewe kama raia mwema unawajibika
kushirikiana na polis, na haki itajulikana au sio..kwahiyo kwani kuna ubaya
gani ukiutoa huo ushahidi polisi…?’ nikasema
‘Ina maana upo tayari kuacha mume wako afungwe, maana ushahidi
wangu ni kumfunga mume wako, lakini pia upo tayari kuachia hisa zako ziende
mikononi mwa watoto wa marehemu…mimi nina ushahid kuwa wao, hizo hisa
wamezipata kimagendo, je hutaki nikusaidie kwa hilo,…’akasema
‘Ushahidi gani ulio nao, wa kusaidikisha hayo…?’nikauliza
‘Nina ushahid hapa nikiutoa mume wako anafungwa,..na wewe pia
utaonekana kama mlishirkiana hilo ni lakwanza lakini pia nina ushahidi wa kuwa
hisa zao, japokuwa zipo kwenye mkataba, lakini unaweza kuutumia kuhalalisha
kuwa hazikupatikana kwa haki,..je hutaki nikusaidie kwa hilo, na pia nimsaidie
mume wako..huyo wakili mtoto wa marehemu ananitafuta sana, lakini hatujaweza
kukutana mimi na yeye, sasa kabla ya kukutana na yeye, ..nimeona nikupigia simu…’akasema
‘Nimekuuliza huo ushahidi upoje…?’ nikauliza
‘Tukikutana utaweza kuuona, haina shida kabisa, mimi nawajali,
sitaki mume wako ambaye ni mgonjwa asumbuane na polisi, na bila huo ushahidi
ambao polisi wanautafuta kwa hivi sasa, bado hawataweza kumkamata mume wako,
lakini cha muhimi ni wewe kuliweka hili liwe siri, ukilivujisha basi mimi sina
budi, itabidi niwasiliane na polis, unaona ilivyo, kwahiyo iwe siri…’akasema
‘Kwani mume wangu ni muuaji, hajaua bado, alikuwa mgonjwa,
nilikuambia hilo, …’nikasema
‘Huo ushahid utasema…hakuna shaka na hilo….’akasema
‘Kwahiyo unataka nini…?’ nikamuuliza
‘Nitakupigia…’akasema na kukata simu.
Alipokata simu, kwanza nikatuliza kichwa, kitu kilichonishtua ni
kuhusu huyo wakili, kijana wa marehemu…kama huyu mtu atakutana na huyu mlinzi
wanaweza kujenga ubia ambao unaweza ukawa mbaya sana wa kunisumbua mimi, sasa
nifanye nini
Hapo hapo nikashika simu na kuwasiliana na wakili wangu:
‘Kuna swala hili la familia ya marehemu, siku zinakaribia,
natakiwa kukutana nao ili kumalizana kuhusu huo mkataba wao, unaodai kuwa wao
wana hisa kwenye kampuni ya mume wangu, ..na seehmu kwenye kampuni
yangu..’nikasema
‘Hilo niachie mimi….’akasema
‘Lakini ni muhimu nikutane nao, maana waliniona kirafiki..kuacha
huyo ndugu yao mwingine…’nikasema
‘Nitaongea na wakili wao kuhusu, hilo, ili niende mahakamani
kuweka pingamizi, ili twende kisheria…’akasema
‘Lakini..hapo huoni nitakuwa sikuwasikiliza, maana wao walikuja
kwangu wakasema wapo tayari kuridhia makubaliani, bila ya kwenda mahakamani…’nikasema
‘Wao wamesema hivyo, kama ukikubaliana na mkataba huo, au sio,
huoni kuwa wamekutega, kwa namna moja kwa njia ya kumsaidia mume wako,..hulioni
hilo..hata hivyo, huo mkataba upo kisheria, ni lazima sheria ndio iutengue, na
huwezi kuutengua bila kupitia kwenye haki za kisheria, na hapo inabidi mimi
nikutane nao…na ili uoekane huo ni batili, ni lazima twende mahakamani…’akasema
‘Kwahiyo tufanyeje…?’ nikauliza
‘Kwa hivi sasa wewe subiria kwanza, wao waanze, maana wao ndio
wanadai mirathi, ni wajibu wako kwenda mahakamani kudai wanachostahiki
kukidai..’akasema
‘Sawa….lakini kuna kitu kingine ambacho kinanifanya nitaharuki…’nikasema
bado nikiwa sina uhakika kama kweli hilo ninaweza kumuambia wakili wangu au
la..lakini wakili wangu ndiye kila kitu kwa mambo hayo
‘Kitu gani…?’ akauliza
Huyu mlinzi sasa ananiweka
roho juu, sio tu kwa ajili ya mume wangu lakini kwa namna moja anataka kugusa
haya ya mikataba, na hayo wanayodai
wanafamilia hawa, kuwa wana hisa ndani ya kampuni zetu, inatakiwa
kumdhibiti huyu mtu mapema, kwani akiungana na wakili mtoto wa marehemu itakuwa
ni vita nyingine, ..nikasema
‘Kuna mtu mmoja ananitishia kuhusu mume wangu, muda hivi kanipigia
simu anataka kuonana na mimi, nataka na wewe
uwepo, japokuwa kasema kuwa hataki mtu mwingine awepo, ila nataka uwepo wako
usiwe wazi, …’nikasema
‘Anadai nini kwani…?’ akaniuliza
‘Anataka eti nimfunge mdomo, ili asiwe shahidi kuwa mume wangu,
kwani ana ushahidi wa kubainisha kuwa mume wangu alikuwepo siku ya tukio…na
huenda akawa anahusika kwa hayo mauaji ya Makabrasha…’nikasema
‘Kwani mume wako kashitakiwa tayari , au kuna dalili hizo za
kushitakiwa kuwa anahusika…?’ akauliza
‘Hapana , lakini kuna tetesi kuwa itafanyika hivyo,…’nikasema
‘Ili mimi niingilie kati, ni lazima kuwe na mashitaka, mimi
nakushauri hivi, kama anataka kuongea na wewe usimkatalie kama una nafasi, kama
huna nafasi, haina haja kabisa kusumbuka naye..’akasema
‘Wasiwasi wangu ni kuwa anaweza kumtumia mume wangu kama kitega
uchumi, na hali aliyo nayo mume wangu akitaka pesa, nitafanyeje…na docta kasema
hali aliyo nayo sitakiwi kumkwaza..sasa je akimuendea mume wangu kwa kumrubuni
itakuwaje..na..?’ nikauliza na kabla sijaendelea wakili akasema
‘Kwani ni nani huyo…?’ akauliza na nikamtajia, kuwa ni mlinzi
kwenye jengo alilofarikia makabrasha, na nikamtaja jina lake
‘Huyo mtu ni hatari…yeye ndiye anashukiwa kama mtumiwaji wa
Makabrasha, aliwahi kuwa mtu wa usalama akafukuzwa, akaenda kuajiriwa nchi ya jirani
na huko nako akafukuzwa, na hata kufukuzwa kwake hakupo wazi sana kuhusu kosa
lake, ila walisema kwa usalama wa kikazi…inatilia mashaka, ni mjanja
sana…’akasema
‘Sasa nifanyeje…?’ nikauliza
‘Natamani sana kukutana na huyo mtu kwenye uwanja huo wa sheria,
nione huo ujanja wake …’akasema wakili
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Watu wakorofi kama hao wananipa changamoto kwenye kazi yangu,
sasa wewe subiria, akikupigia simu tena, fanya kama nilivyokuelekeza nitakuwa
hewani, nikiona alama ya kuwa mpo naye, sawa..mengine yatafuata kuanzia
hapo…’akasema
************
Basi siku hiyo ikawa
inakwenda salama, na kabla sijajipanga kwenda
kumtembelea mume wangu hospitalini, mara simu yangu ikaita,…nilipoangalia nikaona
hakuna jina au namba (anonymous) ..ina maana muitaji ni mtu asioyefahamika.
Kwa haraka nikaweka simu yangu kwenye kurekodi, mazungumzo, na
kuiweka hewani
‘Nipitie Maringo hoteli, ukienda kumuona mgonjwa, nitakusubiria
nje ya hoteli….’akakata simu.
‘Kajuaje kuwa nakwenda hospitalini…?’ nikajiuliza
Kwa kukisia tu anaweza
akawa ndio huyo jamaa, lakini sikuwa na uhakika, na nisingeliweza kumpigia simu
maana namba ya simu haisomi..nikawaza kiusalama nifanye nini.
‘Docta, nakwenda kmuona mgonjwa, je tunaweza kuongozana..?’
nikampigia docta jirani yangu
‘Mimi nipo hospitalini kwangu, kama ni muhimu kuja huko
nitakuja…’akasema
‘Basi hamna shida..’nikasema,
‘Huyo mtu ni
hatari…yeye ndiye anashukiwa kama mtumiwaji wa Makabrasha, aliwahi kuwa mtu wa
usalama akafukuzwa…, ni mjanja sana…’nikakumbuka maneno ya wakili akimuelezea huyo mtu
‘Hata kama ni mjanja mimi ni mjanja zaidi yake…’ nikasema kimoyo
moyo, kwanza nikaegesha laptop yangu ambayo ipo nyumbani, ambayo inatumia waya
za hewani, iwe na mawasiliano na simu zangu za mikononi, na chombo kingine
nitakachokuwa nacho,..kwahiyo nikiwa naongea na huyo jamaa, tukio hilo
litachukuliwa moja kwa moja kwenye laptop yangu, japokuwa ipo nyumani…,
Nikaseti nywele zangu na kuchukua kibanio maalumu, na kuzibana
nywele zangu, hicho kibanio, sio cha kawaida….
Pia nikachukua simu zangu mbili zote zinauwezo wa kuchukua matukio
ya sauti zikiwa na chaji ya kutosha, na kwenye begi langu nikaweka kitufe
kingine chenye kazi hizo-hizo…hicho huwezi kukibaini kwani kinalengeshwa kwenye
mkanda wa hilo begi..…
Nikatoka nyumbani na kuingie kwenye gari langu…kuelekea
hospitalini, lakini nikikumbuka kuwa natakiwa kupitia Maringo hoteli, ili
kukutana na jamaa huyo mwenye ushahidi na wakati nipo kati kati ya bara bara,
nikapigiwa simu
‘Nani mwenzangu…?’ nikauliza
‘Mimi ni wakili wa familia ya Makabrasha..’ akasema
‘Unataka nini..?’ nikauliza
‘Kijana wa marehemu kanipigia simu, kuwa anataka kuonana na wewe
na mimi nikiwepo, ana mambo muhimu ya kifamilia, …na kwa vile mume wako
anaumwa, anataka wewe uwajibike nayo, kwani muda wa kuwakilisha mirathi
unakaribia…’akasema
‘Siwezi kuliongelea hilo, kwa vile mambo yote alikuwa
akiyashughulikia mume wangu, na yeye kutokana na hali yake hawezi kuongea
kisheria ikakubalika..’nikasema
‘Katoka kuongea na mgonjwa muda mfupi uliopita, na mgonjwa kasema
kutoa na hali yake kuwa mbaya, anashindwa kufanya lolote, lakini kwa vile wewe
upo, basi unaweza kuongea naye…’akasema
‘Kaongea na mgonjwa, ni nani kamruhusu kuongea na mgonjwa,…?’
nikauliza
‘Mgonjwa mwenye ndiye alishinikiza kuwa anataka kuongea na huyo
jamaa, sijui ilitokeaje mpaka ikafikia hapo…’akasema
‘Madocta wana akili kweli..’nikasema kwa hasira
‘Ilibidi, huwezi kuwalaumu madocta, unajua mume wako akitaka kitu
hataki kukataliwa, na kwa hali aliyokuwa nayo haikuwa na jinsi…lakini waliongea
kwa amani tu.., hata madocta wanasema baada ya huyo jamaa kuongea na mgonjwa, imesaidia sana, kwani hata shinikizo la damu
limetulia…’akasema
‘Sawa nimekusikia..’nikasema hivyo tu nikijua hapo kuna jambo
linatengenezwa
‘Tatizo jingine polisi wanataka kuongea naye…na mimi nimewazuia..’akasema
‘Kuongea na nani..?’ nikauliza
‘Na mgonjwa…’akasema
‘Kuhusu nini tena…?’ nikauliza sasa nikianza kuhisi kichwa
kikiniuma
‘Kuhusu mauaji ya Makabrsha…’akasema
‘Kwani mume wangu anahusika nini na hayo mauji..?’ nikauliza
‘Wanadai wana ushahidi mkubwa wa kuonyesha hilo, kuwa mume wako
anahusika…’akasema
‘Wameupatia wapi huo ushahidi..?’ nikauliza
‘Mimi sijui..ila wanasema wanao huo ushahid na sasa wanahangaika
kutafuta mashahidi wa kutosha, na wana uhakika safari hii ni lazima huyo muuaji
atahukumiwa kwa kosa la kuua, kuna shahidi mmoja tu bado hawajampata nasika
yeye, alimuona muuji kabisa..’akasema
‘Ni nani huyo, shahidi…?’ nikauliza kwa hamasa
‘Sijui..nasikia hata mtoto wa marehem kaniambia anamtafuta huyo
shahidi ili haki itendeke, kasema atashirikiana na polisi kuhakikisha huyo mtu kapatikana..’akasema
‘Hujanitajia huyo mtu…’nikasema
‘Watu wanahisi labda ni mmojawapoo wa walinzi, kuna mlinzi mmoja
kachukua likizo, hapatikani, hayupo yumbani kwake, wanahisi labda kasifiri
kijijini kwako, polisi wanamtafuta…’akasema
Hapo nikakata simu...kwani
kuna simu nyingine ilikuwa inataka kuingia…ilikuwa ya mpelelezi
anayeshughulikia kesi ya mauaji ya Makabrasha…
WAZO LA LEO: Anayepitia uchungu ndiye anayeweza kuhadithia
uchungu huo ulivyo;
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment