Ilikuwa ni muda wa usiku, nahisi ilikuwa ni saa sita na nusu hivi,
kwani niliangalia saa ya ukutani, tatizo, siwezi hata kugeuza kichwa, lakini
niliona ni saa sita, mshale unaonyesha hivyo.
Cha ajabu mwili hauna nguvu, na pumzi ilikuwa ndogo sana, nipo
wapi hapa, ni jela au ni chumba gani hiki hakina hewa…nikajiuliza, nikijaribu
kugeuza kichwa siwezi, lakini naona, kwa hisia
Mara ghafla mishughuliko, kama kuna kugombea jambo..sijatahamaki mara mkono ukanishika shingoni, unanikaba, na mwingine , na mwingine..ikawa inakuja mikono mingi kunikaba, lakini simuoni mtu ila nahisi ni mikono ya watu inanikaba kila
nilipojaribu kugeuza kichwa au kujitetea, sikuweza, mwili ulikuwa haukubali
ilikuwa kama mtu aliyenyweshwa madawa ya kulevya au nusu kaputi.
Akili ilikuwa inaona, au nahisi hivyo, kuwa kuna mikono mingi
inanikaba, tena ya kiume..na pia ya kike, ni nani hao, wanataka kuniua,..wote
walikuwa wamenishikilia na kila mmoja akiapiza kivyake, kuwa ananiua kwa
vile..hiki na kile, na sauti hazisikiki vyema, ila sasa mmoja ndio akasema
‘Nataka ufe kwa vile unakuwa kikwazo kwetu…ila tunakupenda, na
kukupenda huko, ili usihangaike ni bora ufe tu…’ilikuwa suti ya kike, iliyochanganyikana na sauti ya kiume kama wanaongea kwa pamoja.
Mikono hiyo mingi iliendelea kunikaba, na mara kwa mbali,
nikamuona mtu…anakuja taratibu, akatabasamu, na kusema;
‘Nilikuambia mimi ndiye rafiki yako wa ukweli, sasa nikuokoe au
nikucha wakuue..?’ akauliza hivyo, na mimi nikawa najitahidi kujiokoa, sitaki
huyo mdada aniokoe namuona kama mnafiki kwangu ,ananihadaa tu, ananivunga, nikawa nataka
nijiokoe kivyangu,..hapo sasa pumzi ndio kama inishia, sasa nataka kukata roho.
Yule mtu, ni mdada, lakini mrefu..akaniuliza tena..tena,
'Hutaki,
nikuokoe unajua wewe ni rafiki yangu, nakupenda sana,na kila kitu nafanya kwa
ushauri wako,wewe ndiye ulinijenga, akili yangu ikawa inakuwaza wewe, usemacho
kwangu ni kama askari anayepewa amri,..ua, naua, kamata , nakamata , sasa iweje…sasa
niambie nikuokoe au niache ufe..'
‘Mna-na-fiki wewe…’nikajaribu kusema hivyo, kinafsi niliweza, lakin mdomoni siwezi hata kufunua mdomo mkavu,..kwa sababu ya kukabwa, ulimi umetoke nje...na Yule mdada, akainua mikono, kama
vile na yeye anataka kunikab au kunikoa, mimi nakataa, sitaki afanye anachotaka kukifanya,…,
Ni wakati huo nimeshakata
tamaa, namuomba mungu anisamehe makosa yangu ili nife kwa amani,…sasa sina
uwezo tena hata wa kuongea, kauli imeshakata,..mara kikaja kitu kama mwanga,
kikanipiga usoni, nikashituka,...nipo wapi, .. ooh, kumbe ilikuwa ni ndoto.
‘Ndoto mbaya hii…ooh..’nikasema sasa nikijaribu kuweka fikira
zangu vizuri, mwanga ulikuwa ukitokea dirishani,ni mwanga wa taa za nje...!
Jasho lilikuwa linanitoka, haraka nikainua mikono yangu na kushika
shingo, sikuona dalili yoyote ya maumivu, ya kukabwa,..na nikageuka huku na
huku kunyosha shingo, sikuhisi kuumia, na wakati huo macho bado mazito
kufunguka, naogopa nitayaona haya majitu.
Baadae nikafungua macho…nipo chumbani kwangu , kitandani,…hapo nikajitahidi
na kujiinua kidogo, nikajikuta nipo sawa, nikajinyosha, halafu nikageukia ubavu
wa pili, upande ule aliolala mume wangu,
Hakuna mtu!!
Mume wangu hayupo kitandani, na nina uhakika alikuja usiku ule
tukalala naye, japokuwa alikuwa kalewa, sikuweza kumkatalia, kwa ile hali,
lakini awali sikuweza kupata usingizi hadi niliposikia anakoroma kuashiria kuwa
kalala, na ndipo usingizi ukanishika,, sasa mume wangu hayupo kitandani
‘Labda katoka kidogo,..’nikajipa matumaini
Usiku ule walipofika na mdogo wake, niliongea naye kumuuliza hali
ya mgonjwa, maana ni mgonjwa sasa, ..
‘Shemeji yupo safi tu, ila anaongea sana…’akaniambia
‘Sawa sasa ni usiku sana, ila kesho kama nilivyokuambia,huyu ni wa
hospitalini…’nikasema
‘Amekataa, anasema yeye haumwi, sijui tutafanyaje…’akasema
‘Basi nitamuita rafiki yake docta, aone atatusaidiaje, ila kwasasa
ukalale naye..’nikasema
‘Hapana, shemeji,..kasema anataka kulala na wewe kwa vile wewe ni
mke wake, nilimuambia hilo wakati tunakuja, kakataa katakata…kasema ukimkitaa,
atakufanya kitu ambacho hutamsahau…’akasema
‘Atanifanya nini..?’ nikauliza
‘Kasema hivyo tu…’akasema
‘Oh,…sasa akileta vurugu usiki itakuwaje..?’ nikauliza
‘Wewe shemeji usijali, hakikisha simu yako ipo karibu, akifanya
fujo, au hali ikiwa mbaya, wewe nibeepu tu, weka namba yangu tayari, na mlango
usifunge kwa kubana,…’akasema
Kwahiyo tukaishia hapo, na
kweli nilifika na kumkuta mume wangu ameshatangulia kitandani, na sasa kalala…
‘Sasa kaenda wapi huyu
mtu..?’ nikajiuliza hali ya ndani kulikuwa kimia kabisa, husikii kitu …nikakaa
kimiya kidogo, nikisubiria huenda kweli katoka kujisaidia, lakini hakutokea
kabisa, moyoni nikahisi ni yale yale, nilikuwa nikiogopa, na nikikumbuka hiyo
ndoto ndio nikawa na mashaka kabisa
Uzuri watoto walikuwa hawapo, wapo shule za bweni, kwahiyo upande
huo nilikuwa na amani nako, sasa ni mimi na mume…na shemeji yupo chumba
kingine.
‘Uwe makin na huyo mtu, hata ukilala usilale kupitiliza…’nikakumbuka
ushauri wa docta rafiki wa mume wangu.
Nilipokumbuka hilo kwa haraka, akili ikanijia, nikaona nifanye
jambo , jambo ambalo niliwahi kuliona kwenye sinema, lilinijia hilo wazo tu.
Taa ya ndani ilikuwa inawaka, lakini sio ile ya mwanga mkali, huwa sipendi
kulala na giza,
Kwa haraka nikaamua nifanye hivyo, sijui kwanini niliamua kufany
ahivyo, ila nilifanya hivyo tu, sijui…
Kwa haraka nikachukua mto wangu wa kulalia,na mashuka ya akiba
nikayaweka pale nilipokuwa nimelala, nikayafunika kama mimi niliyelala, na mimi
mwenyewe nikatafuta sehemu ya kujibanza, nikajaribisha na kuona ninaweza
kujibanza hapo bila ya yoyote kuniona.
‘Najihami tu…’nikasema hivyo.
Nilikaa pale kwa muda bila kuona mtu akitokea, nikawa najiuliza je
ni kweli ninavyowaza au ni wasiwasi tu.
‘Ngoja kwanza nikahikishe labda jamaa kaenda kulala chumba cha
maongezi,..’nikajisema moyoni, kwahiyo taratibu nikafungua mlango na
kuchungulia huko…hakuna mtu…nikasikia kitu kama kimegonga, kwa haraka nikarudi
kwenye maficho yangu na kutulia, kukapita muda, hakuna mtu aliyetokea
Nikakumbuka jambo,…kila kitu kinahitajia ushahidi au sio, ngoja
niweke ushahidi kama kuna lolote laweza kutokea.
Kuna video, niliyokuwa nimeweka chumbani, ni katika kutafuta
ushahidi tu, lakini baade niliizima, ni videi inayochukua matukio…nikasogea
kwenye lattop yangu nikaisha na kuiweka hai, ili ichukue matukio yote humo ndani.
Mara nilisikia kitu kimegonga upande ule wa makitaba, ...oh, kumbe
mume wangu yupo huko, huenda aliamua kwenda kupoteza muda, nikataka kwenda
huko, lakini nikaona ngoja nitulie kama dakika tano hivi, huenda kuna kitu
anakitafuta, nikasikiliza lakini sikusikia tena…nikatoka mafichoni, na sasa
nataka kwenda huko maktaba
Mara ....nikasikia kama mchakato, wa mtu kutembea, na niliposikia
hivyo, nikakimbilia ile sehemu yangu ya maficho. Huwezi jua, huenda ana lake
jambo ngoja nione anataka kufanya nini.
Nikawa najiuliza kama mume wangu alikwenda tu kupoteza muda,
...akaja akaikuta ile hali, anaweza kuniona simwamini...hapana nitamtania
tu kuwa nilikuwa namfanyia mzaha. Nikatulia, huku nikiwazia mataayrisho
ya kesho kuwa kesho ni lazima nimtafute fundi, abadili vitasa vyote vya makabati,
na hata ikibidi nyumba nzima, maana hakuaminiki tena...
‘Bastola...’ oh nilipokumbuka hivyo mwili mnzima ukazizima, woga!!
‘Mungu wangu , kwanini sikuiondoa pale…’nikajilaumu
Hapo moyo wangu ukawa
unanienda mbio, sijui kwanini nilisahau, kwani nilipanga, kuja kuiondoa ile
bastola kwenye kabati na kuificha sehemu nyingine, lakini kutokana na mishughuliko,
na hayo mambo ya kufuatilia, nikawa nimesahau kabisa,
Nakumbuka mume wangu walipoondoka na mdogo wake hawakuchukua muda,
walirudi, wakiwa wanaongea kwa furaha, na nilipopata muda wa kuongea na shemeji
yangu, yeye alisema kaka yake muda wote walikuwa akiongea kwa furaha,
hakukuonekana tatizo lolote...
**********
‘Inabidi kujihami tu...’nikasema kujipa moyo nikiwa bado mafichoni
Kila hatua nilihis nipo
hatarini, na kila nikitaka kumbipu shemeji, nahis kama nitaonekana muoga,
simuamini mume wangu, basi nikaona niache tu, nione kwanza mwisho wake ni nini
Muda ukawa umepita sikuona dalili za mume wangu kutokea.
‘Au kaenda kulala na shemeji au kule kwenye chumba chake kingine…anapolala
akiwa kalewa…’nikasema hivyo kimoyo moyo
Nilipoona muda unakwenda nikataka kutoka na kumfuata mume wangu
huko huko kama ni chumbani kwake au kwenye maktaba yetu, na mara mlango
wa maktaba ukafungulia!
Mume wangu akajitokeza…akiwa na pajama la kulalia, mkononi kashika
kitu,
Kwanza sikuweza kukiona hicho kitu alichokishikilia, kwa jinsi
alivyokishikilia usingeliweza kuona na pale nilipo ikawa siwezi kujisogeza,
na kwa vile nilikuwa nimesimama kwa muda, mwigi kwenye shemu ndogo, miguu
ilishaanza kuuma, lakini hata hivyo niliogopa kijitikisa sikutaka mume wangu
ajue kuwa nipo pale.
Mume wangu akawa anakuja ule muelekeo wa kitanda, alikuwa
akitembea mwendo ule wa kunyata,yaani utafikiri ule mwendo wa kwenye picha wa
kunyata, taratibu, na kila hatua ilikuwa kama mtembeaji anahakikisha kuwa mguu
umefika pale alipopataka,..akasogea hadi karibu na kitanda, na hapo nikaona
kashikilia nini,...moyo ulinilipuka, nikawa nahisi kuishiwa nguvu..
Yale yale niliyokuwa nikiwaza, na hapo nikazidi kujilaumu,
kwanini sikufanya kama nilivyoambiwa, haya mambo ya kuzarau, sasa naona
matokeao yake ...huwa kila anachoniambia rafiki wa mume wangu nimekuwa na tabia
ya kukizarau, na nimejikuta nikipatwa na matatizo na baadaye ndio najiona
nimefanya makosa, ni aheri ningelimsikiliza ushauri wake.
Tatizo huyu rafiki wa mume
wangu, ni mtu anayejitahidi sana kunisaidia, japokuwa ni mume wa mtu, lakini
bado anaonyesha ile hali ya kunipenda, hata wakati mwingine najisikia vibaya
kutokana na matendo yake. Na kuna wakati anajisahau kabisa kuwa yeye ni mume wa
mtu na anataka kufanya yale tuliyokuwa tukifanya tukiwa wapenzi, kwakweli kwa
hilo sikutaka upuuzi huo.
Sasa kupuuzia yale
anayonishauri matokea yake ndio haya...
Wakati huo mume wangu alikuwa ameshafika eneo la kitandani na hapo
akainua kile alichokishikilia na sasa kikawa kinaonekana dhahiri,
Bastola…!!
Sasa akawa kaishikilia bara bara, japokuwa mikono yake inakuwa
kama inatetemeka,..sasa anailenga ile bastola pale nilipokuwa nimelala, niliona
mikono yake ikitetemeka, sijui kwanini
Kwa haraka nikamchunguza kwenye macho yake, awali alipokuwa
kasimama nisingeliweza kuyaona vyema, kwani mwanga wa taa ya ndani ulikuwa ni
hafifu, ila aliposogea karibu na kitanda pale aliposomama sasa ndio nikamuona
na ni kutokana na mwanga wa taa nje.
Taa ya nje ilinipatia nafasi ya kumchunguza vyema machoni alikuwa
kafungua macho, ila ukiangalia kwa makini macho yake yalikuwa meupe,...sio ya
kawaida, nikakumbuka zile hadithi za watu wanaofanya kazi wakiwa usingizini,..
Kweli mume wangu hapo hayupo sawa, na ilivyo, hutakiwi kumshitua,
..unaweza ukamsababishia mshituko wa moyo, na hata kusababisha kifo, kwahiyo
nikatulia kimiya, nione ni jambo gani anataka kulifanya,..
**************
Mume wangu hajui kutumia
vyema bastola, niliwahi kumfundisha lakini hakupenda kabisa kuitumia, nahisi
ndio maana mikono yake ilikuwa ikitetemeka,..ila nilimfundisha jinsi gani ya
kuweka risasi na kutoa, kwahiyo yawezekana atakuwa keshaweka risasi kabisa
kwenye hiyo
‘Hii imepangwa itokee, ili iwe fundisho kwangu...’nikasema kimoyo
moyo.
‘Jembe njoo huku...’sauti ikatoka mdomono kwa mume wangu, ilikuwa
kama ya kuwewesa..na anaongea kama mtu aliyelewa hivi.
Huyo jembe ni nani..?’ nikajiuliza, nikakumbuka ..jembe ni mdogo
wake, lakini hapo hayupo, mbona anamuita kama vile yupo naye karibu.
‘Jembe, ..nakutegemea wewe....lakini hili ngoja nilifanye mimi mwenyewe,
sitaki wewe uje kuingia matatani, na kama unaogopa ondoka....’ikatoka ile
sauti, ni kama ya wale wanywa madawa ya kulevya. Niliweza kuisikia kwa
shida, hapa nikuelezea kwa vile nilivyoelewa, lakini alivyokuwa akiongea ni
maneno ya kutafuta.
‘Na-na-taka ku-ku-limaliza hi-li ka-ka-bisa, tuwe huru...’akasema
huku akisogeza ile bastola palen nilipoweka mto, na kama angegusa kwa mkono
angeligundua kuwa hakuna mtu, lakini nikamuona akisogea nyuma, akapiga magoti.
‘Oh, Jembe nisaidie jamani.. , nashindwa kufanya hili....nashindwa
kumaliza hii kazi, namuonea huruma, lakini jembe , nisipofanya hivi tutakosa
kial kitu,...kazi yangu yote na juhudi zangu zote zitapotea bure, mtaishije,
nitaishije,..nirudi kuwa masikini hapana, sikubali, ni bora nimfuate
Makabrasha, ....’akatulia.
‘Unasikia eti, wana-se-sema Makabrasha ka-fa…yu-le, afe…hapana, kama ni
hivyo, basi hata mimi nataka kumfuata huko huko…najua hata mimi ndio njia yangu…nitakufa,
lakini abla ya kifo changu, nataka niachie familia yangu jambo la kunikumbuka.
‘Sitaki ubaguzi..ooh, mtoto wan je..nani kasema hayo..sasa ili
huyo mtoto wa nje naye atahaminiwe, basi nataka huyu kizuizi aondoke,… Jembeeh,
unanisikia,..sasa nisaidie tumalize hii kazi, mbona husogei, sogea huku...mkono
hauna nguvu kuvuta hiki kiwashio…traigaaaaa..’akasema.
‘Oh, wewe sasa unaogopa eeh,,..ngoja mimi nimalize hii kazi
mwenyewe, maana wiki imeshapita, kinachofuata hapo ni nini....ni mkataba wa
zamani, ukipatikana huo, mimi sina changu, hivi huo mkataba wa zamni ni upi,...ananishangaza
kweli, kweli mke wangu kachanganyikiwa, mimi siujui huo..sija—labda makarasha
atanisaidia, mimi sijui....’akatulia
‘Sikiliza jembe, tusipolimaliza hili, tutakosa kila kitu,
tukilimazlia hili, tutakuwa huru, na mimi nitamfuata Makabrasha, nimekutana
naye, kasema huko alipo kuna amani…yupo wapi huyu mtu…’akatulia
‘Ananiita, unasikia, suti yake hiyo, ananiita…hahahah..ngoja
nimalize hii kazi, anasma nimalize hii kazi halafu nimfuate huko alipo…’akatulia
kama anasiliza
‘Mke nakupenda lakini …wewe ni kikwazo..bora nije kuishi na huyo
mwingine, hana shida,..kwanza …anadai yeye ndiye kanizalia dume, hivi ni kweli
eeh, yawezekana ni yeye,..hahaha, kanizalia dume, kama ni kweli, basi kweli ananipenda,
tofauti na wewe mke wangu ambaye anaogoma kunizalia dume..Tatizo wewe mke
wangu,..unathamini tu mali, wazazi wako, familia yako..na kunifanya mimi bweeege.’akasema
Pale nilipokuwa nimejificha, nilihisi hasira, nikahisi
nijitokeze nikafanye lolote , lakini mwili ulikuwa kama umekufa ganzi,
nikabakia kuumia ndani kwa ndani, kumbe....kumbe, ni kweli mume wangu ana
mwanamke mwingine nje na huyo mwanamke anampenda kuliko mimi, sasa ni nani,…ni..ni…hapana
mbona hamtaji!
‘Ni mwanamke gani huyo…?’ nikajiuliza
‘Tatizo mwanamke wewe unayenipenda sikuoni…upo wapi…ni nani
wewe..mbona inakuwa kama jinamizi, nashindwa ku-kumbuka, ni nani wewe..nakuwa kama
mtu anayempenda shetani, ..jini mahaba, asiyeonekana, umekwenda wapi wewe…je ni
kweli ni wewe ulinizalia jembe…’akatulia
‘Ni kweli maana ni kwanini mke wangu alitaka kumtupa mtoto ..kwa
vile hana uchungu naye..yaah, nimegundua, mke angu hanipendi, kama hampendi
mtoto wangu hata mimi hanipendi, sasa nakuua…ufe,..ufeee...na hii silaha yako…na
mimi,…hahaha’
‘Sasa jembe mimi namaliza kazi, nikimaliza kazi, kinachofuata
tukamtafute mtoto wetu, ...tutakuwa na jembe jingine, dume la kazi....ukiwa na
jembe ndani ya familia raha, watoto wote nawapenda, lakini wa kike watapendwa
na wengine zaidi, watachukuliwa, nitabakia na nani sasa....mungu kanisaidia
nimepata mtoto wa kiume, eti nimuachie hivi hivi..hapana, ni lazima ..ni
lazima, tukamchukue, sasa jembe mimi namaliza kazi ..
‘Wewe sihutaki kunisaidia eeh ...mimi naifanya hii kazi peke
yangu, wewe ....unisaidie jambo moja, nikikamatwa, unilelee watoto, nikifa,
halikadhalika, nakuachia kila kitu kikiwa sawa,...hata nikifungwa, wewe chukua
jahazi, najua kwa sasa kila kitu kipo makini, ahsante Makabrasha, nakuja
nisubirie, nakujaa.....’akasema
Akasogea karibu kabisa sasa na pale nilipoweka kanyaboya
akaelekeza ile bastola kwenye mto, akaisogeza karibu sana, na kusema;
‘Samahani sana mke wangu ...nalifanya hili kwa vile sina namna
nyingine, na nikimaliza hili na mimi nikiona vipi nitajimaliza mwenyewe, kwa
manufaa ya familia…’akawa sasa anakaza kidole cha kuvuta kiwambo cha bastola
‘Najua..nitapatilizwa na kusakamwa sana..lakini kama wanavyodai
wamemfanya hivyo Makabrasha, kwanini hililisifanyike , na kuna shida gani maana
kila kitu sasa kipo makini, kila kitu kipo makini au sio best Makabrasha,
nakushukuru sana...’akasema na kuisogeza bastola karibu kabisa na mto....
‘Kila kitu kipo makini....’akawa anayarudi hayo maneno mara kwa
mara sasa, nikawa najiuliza hayo maneno yana maana gani, kwanini ameyependa
kuyarudia, amejihakikishia vipi kuwa kila kitu kipo makini, nikawa najiuliza
huku nikimwangalia mume wangu, nikiwa pale nimejibanza,
‘Makabrasha kafa…nani kasema kafa, wehuu nyie…, basi kama kafa
nimemuua mimi, mwenyewe, hivi hivi….hahahha. Kama nimemuua rafiki yangu
aliyenithamini, kwanini nishindwe kukua, wewe…hahahaha, kwaheri…
Mara mlio ukasikika, ...mlio ulitetemesha ndani,....na mlio ule
ulimshitua hata huyo aliyeusababisha, na yeye akadondoka chini, na mimi pale
nilipokuwa ilikuwa kama mtu kaniziba masikio ghafla,.
Hata hivyo nikajitahidi, maana ni lazima nifanya jambo, kwani
huenda mlio huu umesikika hadi huko nje, itakuwa ni kashifa,...nikatoka pale
nilipokuwa nimejificha, na kwa haraka nikaenda pale alipodondokea mume wangu,
alikuwa amedondoka sakafuni, sasa kalala, ..ametulia....anahema kwa mbali, na
sauti kama ya kukoroma, ya kuashiria
kuwa mtu yupo kwenye usingizi,...
Nikaiangalai ile bastola ipo wapi ilikuwa imemtoka mkononi na
kudondokea kitandani, na hapo nilitaka kuichukua lakini nikatulia, kwani
nilisikia mlangoni ukigongwa.
‘Shemeji kuna nini huko....’alikuwa mdogo wa mume wangu, na mara
simu ikaanza kuita….
NB: Kwa leo naishia hapa, naogopa na kuogopa,
WAZO LA LEO:
Tuwe ni wenye kuhurumiana, na kusaidia, hasa pale tunaposikia kuwa mwenzako
yupo kwenye mitihani ya maisha huo ndio upendo wa kweli. Mitihani ya maisha ipo
mingi, lakini mtihani wa maradhi ni mgumu sana, kwa mgonjwa mwenyewe na
muugazaji, Ni wangapi wanakuwa wepesi kusaidia mtu akiumwa, ni vigumu sana
kuwaona,..lakini mtu huyo huyo akisikia mwingine kafa, hata kama ni nauli
atakopa,..najiuliza tu, je twawapenda watu wakiwa maiti zaidi ya wakiwa
wagonjwa! Najiuliza sana sana hili. Tupo pamoja..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment