Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 18, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-43


  Ilikuwa asubuhi na mapema, nikiwa najua leo ndio siku ya dhamana yangu, kiukweli usiku mmoja wa hapo ulikuwa mateso yasiyovumilika, sikuweza kulala kabisa,   Mara nikasikia nikiitwa, nikajua sasa ndio muda umefika, lakini mbona ni asubuhi sana, ni nani huyo kafika

Nikajitayarisha kwa haraka na kutoka nje baada ya mlango kufunguliwa

‘Kuna wageni wako…’nikaambiwa

‘Ni wakili wangu..?’ nikauliza

‘Hapana nenda tu utawaona mwenyewe, wanakusubiria…’nikaambiwa

Basi kwa hamasa nikaelekea sehemu ya kukutana na wageni, hata kabla sijawakaribia, nilianza kuangusha kilio,sikuweza kuvumilia..

Mama naye aliponiona alishindwa kujizuia, akaanza kulia, ikageuka kuwa kilio tena.. mama akanivamia na kunikumbatia, alitamani anibebe, tukalia mpaka hamu ikaisha,.. huku mama akinishika mashavuni, mwilini, kama kuhakikisha kuwa hakuna sehemu nilyoumia, halafu akasema;

‘Mwanangu upo salama kweli..?’ akauliza

‘Ni kama unavyoniona mama, nipo salama, japokuw ani hi mitihani tu mama, lakini msijali wazazi wangu haya yatakwisha tu…’nikasema

‘Lakini mwanangu kwanini hutaki kutuelewa sisi wazazi wako, ujue mzazi wako anaona mbali, tulishakuamba huyo mume wako hakufai, unaona sasa yanayokutokea hapa hata baba yako hajawahi ku-kufika, leo wewe umeanza, ni nuksi gani hii jamani...’akasema.

‘Mimi sitaki hata kukumbushia hilo, cha muhimu, ni jinsi gani ya kukusaidia utoke hapa, tuambie mumefikia wapi, maana tulitaka tufuatilie lakini nikaambiwa kila kitu kinashughulikuwa na wakili wako, sasa niambie mumefikia wapi...’akasema baba.

‘Wazazi wangu msihangaike, hilo linafanyiwa kazi, wakili wangu yupo huko, na taarifa za awali ni kuwa dhamana imeshakubaliwa, iliyobakia ni taratibu ndogo ndogo...’nikasema hivyo, japokuwa bado sikuwa na uhakika na hilo.

‘Tatizo lako ni hilo la kujiamini kupita kiasi, una uhakika kweli kuwa dhamana yako imekubaliwa, au unatudanganya sisi wazazi wako, ili kutupa matumaini, unafikiri mimi sizifahamu kesi za namna hii zilivyo, haijalishi wewe ni mtoto wa nani, kesi kama hizi ni ngumu…je una uhakika na hilo?’ akaniuliza.

‘Sasa mimi baba ningekudanganya , ili iweje, dhamana imeshakubaliwa, ka taarifa za juu juu, kilichobakia ni taratibu ndogo ndogo, hapa namsubiria huyo wakili aniambie wamefikia wapi, kwahiyo wazazi wangu....msiwe na wasiwasi, wakili analifanyia kazi hilo...’nikasema.

‘Lakini umeonaaeeh, tuliyokuambia kuwa tabia ya mtu huwa haijifichi, sasa unaanza kuonja joto ya jiwe, na kama hutakubaliana na sisi, utaone mengi zaidi ya haya, sio nasema hivi kwa kukuombea mabaya hapana, lakini ndio hali halisi ya watu kama hao..…tabia ya asili sio rahis kubadilika kirahisi, sasa sijui tukusaidieje binti yetu...’akasema baba.

‘Baba kwanini unakimbilia huko, una uhakika gani kuwa hayo yote ni kwasababu ya mume wangu..?’ nikauliza.

‘Mimi sio mtoto mdogo, usione nimekaa kimiya ukafikiria sifuatilii nyendo za maisha yako, hata kama unajimudu vipi…’akasema na mimi nikamkatisha na kusema.

‘Baba msijali, hizi ni changamoto za maisha yatakwisha tu, …’nikasema.

‘Binti yetu sio tunasema hayo kwa kutokupenda furaha yako, ..hatuna nia ya kuvuruga ndoa yako,lakini tunaangalia mbali, kipi kilicho bora, furaha ya muda, au furaha ya kudumu, eehe…?’ akawa kama anauliza

‘Ni ya kudumu baba..lakini…’nikasema

‘Ya kudumu hutaipata kwa hali kama hii,  haya yanayotokea hayafurahishi kamwe yanatutesa na sisi, jea upo tayari kuishi maisha kama hayo hadi unashuka kaburini, je huwaonei huruma watoto wako...?’ akaniuliza sasa mama.

‘Lakini wazazi wangu haya yanaweza kumpata yoyote, hata awe na mume kipenzi cha wazazi, bado, mitihani kama hii inaweza kumpata. Na sioni kwanini nikate tamaa na mume wangu kwa kufikiria kuwa kuna makubwa yanakuja..’nikasema

‘Sisi hatutaki wewe ukate tamaa, ila changamoto ndio hizo zimeanza, na maadui zangu wameshajua kuwa hapo kwako ndio kichaka cha kuniharibia mimi kisiasa na ndicho nilikuwa najaribu kukuweka au labda wewe hutaki nifanikishe malengo yangu ya kisiasa, unajua siasa ilivyo, kashfa ndio silaha ya adui yako..’akasema baba

‘Lakini baba, sijachunguza na kuamini kuwa hayo yaliyotokea ni kutokana na mume wangu, na sizani kama mume wangu anaweza kuhusika na kifo cha Makabrasha,  na hakuna mwenye ushahidi mpaka sasa kuwa mume wangu kafanya mabaya fulani yote ni tuhuma tu.., au sio…’nikasema

‘Kuuwawa kwa Makabrsha hilo tuwaachie polisi, sisi tunachokiongelea hapa ni tatizo la familia yako, ambalo linaweza kuwa ni chanzo cha yote hayo mengine, kashfa ndani ya familia yako inanigusa na mimi, sasa tusipoziba ufa tutazidi kukarabati nyumba, na haitadumu, hili mimi sitakubaliana nalo…’akasema baba

‘Baba ni sawa nimekuelewa, lakini yameshatokea eeh, sasa tufanyeje …maana mimi nimeshakuwa mke wake..je kama tatizo ni hilo, tatizo ni mume wangu,tufanyeje sasa, niachane naye, au nifanyejeje ?’ nikawa kama nawauliza.

‘Sisi hatuwezi kusema uachane na mume wako, hayo tulikushauri mapema sana, ukakaidi, hatua iliyofikia, sisi hatuna uwezo nayo, ni wewe na mume wako mtakavyoamua ,  lakini sisi kama wazazi ni wajibu wetu kukuonya na kukumbushia hilo…’wakasema

‘Lakini baba…’nikataka kusema na baba akaendelea kuongea

‘Mume wako, akishirikiana na huyo marehemu, ndio wamekufikisha hapa, na hatujui hatima yake itakuwaje, kwa vile walichotaka kukifanya wao ni kujenga kashfa dhidi yangu....’akasema

‘Sasa baba mimi sio mwanasiasa hayo yanafanyika kwa kukuharibia wewe au sio, ukiangalia kwa makini hilo linamweka mbali mume wangu na hilo, kwasababu, mume wangu akifanya hivyo kukuharibia wewe si ndio amejiharibia na yeye mwenyewe na familia yake, ina maana yeye hana akili hiyo ya kufikiria…’nikasema

‘Mume wako anatumiwa..huenda hata bila ya yeye kujua.., wamemchota, akawa anatoa siri za ndani, na siri za ndani ndio hizo zimetumiwa kisiasa,..sasa utasema chanzo hapo ni nani, sio, … mume wako..tuelewe hapo, mume wako angekuwa mkweli akasema ukweli,..tungelijua jinsi gani ya kumlinda…’akasema baba.

‘Je baba hayo yana ushahidi, maana kiukweli baba kukiwa na ushahidi hata mimi nitajua jinsi gani ya kufanya, mimi sitakubali hayo yafanyike kuniharibia familia yangu, lakini ushahidi upo…’nikasema

‘Ushihidi!!!... ina maana hata sisi wazazi wako tukikuambia jambo huwezi kutuamini mpaka tukupatie ushahidi..?’ akauliza mama

‘Sio hivyo mama, ..ushahidi sio kwa kutokuwaamini nyie, ushahid ni jinsi gani mimi nitaweza kupambana na mume wangu, .. kuna mambo yetu ya kifamilia tuyaliyaweka, na yatambana mume wangu, lakini ni lazima kuwe na ushahidi…’nikasema

‘Ndio huo mkataba..ulioibiwa na kuchezewa, hahaha, ..?’ akauliza baba na kucheka

‘Ndio baba, huo utanisaidia sana, kama nitapata ushahidi..’nikasema

‘Binti,… uwe makini sana…, kama bado hujaamini, basi subiria, lakini sasa yamegusa familia yangu, sitaweza kuvumilia tena, sitajali kama wewe ni binti yangu au huyo ni mkwe wangu.., walichokitaka kwa hivi sasa wamekikosa…lakini je wamejiandaaje baada ya hili kushindwa, kwangu mimi wameshanitangazia vita..’akasema baba kwa sauti ninayoijua , huwa akiongea hivyo hatanii.

‘Sawa baba nimekuelewa, lakini usichukulie jazaba, tafadhali na kuomba ....’nikasema na mama akasema;

‘Hebu tuambie, ukweli, ...rafiki yako, kazaa na nani?’ akaniuliza mama.

**************
‘Mama jamani hilo litasaidia nini kwa hivi sasa…?’ nikauliza na mama akauliza tena

‘Nauliza hivi rafiki yako kazaa na nani,..nakuuliza hivyo nikiwa na sababu zangu…?’ akauliza tena mama.

‘Mama, kiukweli hilo hadi hivi sasa, mimi sijajui, kwasababu hajawahi kuniambia ukweli...’nikasema.

‘Hajawahi wakati alikuwa mtendaji wako, na rafiki yako unayemuamini, hapo kuna kitu unatuficha,..lakini sasa hilo tunakuachia wewe kama homework, ukija kuligundua hilo inaweza ikawa mwanga kwako wa kujua hayo tuliyokuwa tukikuambia, na inaweza ikawa mwanga kwako, kuwa sio kila rafiki ni rafiki kweli,..’akasema mama


‘Sawa wazazi wangu nimewaelewa, ..’nikasema

Baba ghafla akabadili azungumzo tukawa tunaongelea maswala mengine nia ni kunifanya nisichoke sana kiakili, na kwa vile nimeshawaambia swala la dhamana lipo wazi hawakuwa na wasiwasi huo tena…baadae ikabidi waondoke, na wakati wanaondoka wakasema;

‘Kama unaona unahitaji msaada wetu tuambie, mimi nitafuatilia nihakikishe unapata dhamana, nina wakili wangu ....lakini hawezi kuingilia taratibu zako maana wewe una wakili wako, tusije tukaonekana watu wa ajabu, sio unajua taratibu zilivyo, au hata kama yeye anahitaji nguvu nyingine aseme tu...’akasema baba.

‘Msiwe na wasiwasi wazazi wangu, dhamana ilishakubaliwa, hapa nasubiria tu kuondoka...’nikawaambia, maana wakili wangu na rafiki wa mume wangu walinithibitishia hilo, kwahiyo sikuwa na wasiwasi na hilo japokuwa nilikuwa sijawa na uhakika wa moja kwa moja..

****************

 Wazazi wangu wakaondoka..

Saa zikawa zinakwenda, simuoni wakili au rafiki wa mume wangu,...hata wale maaskari nilizoeana nao, wanaonipa taarifa za mambo yangu sikuweza kuwaona, ilikuwa kama vile watu wameambiwa wasinikaribie,..na mchana huo, ukawa ukapita, ikawa inaingia jioni, simuoni mtu.

Bado niliendelea kutokuvunjika moyo, nikidhania labda kuna mambo bado yanafuatiliwa na watu wangu hao, hasa wakili, .

Ni wakati nimeshakata tamaa kabisa, nikiwa nahangaika kumtafuta mlinzi ili nimtume kwa wahusika ili angalau nijue ni nini kinachoendelea , mara nikasikia nikiitwa, na hapo nikajau ni muda wa kuondoka, dhamana imeshakubaliwa, japokuwa wamenichelewesha lakini sasa naondoka.

Hapo sasa nikawa najiweka sawa, kwani najua sitarudi tena kwenye hicho chumba, nilipokuwa tayari, nikatoka hadi chumba cha kupokea wageni.

Nilimkuta wakili wangu akiwa amekaa kwenye kiti, na aliponiona kama kawaida yake akasimama na kuja kunisalimia, nikamuitikia, lakini kwa jinsi nilivyomwangalia usoni, nikahisi kuna tatizo,… nilimuona kama hana raha, kanyong’onyea, nikahisi labda mzazi wake…nikatulia kusubiria taarifa, na yeye alipoona nimetulia akaanza kwa kusema;

‘Yaani hapa nilipo naogopa hata kusema kitu, maana huyo mkuu wa kituo, na yule mpelelezi anayeshughulikia kesi yako,  sijui wana dhamira gani,...ni aheri wangelianiambia mapema, lakini walichofanya ni kuchelewesha muda, kila nikiwafuta wananiambia subiri, subiri… na baadaye wakaja kuniambia kuwa mambo hayajawa safi....’akasema.

‘Unataka kusema nini?’ nikamuuliza nikiwa nimeshitushwa kwa kauli yake hiyo.

‘Wamekataa kukupa dhamana,...’akasema

‘Hakimu au wao..?’ nikauliza

‘Unajua haya mambo tulishaongea na hakimu, nahakimu alikuwa akisubiria taarifa zao hao watendaji, kauli yake inawategemea sana wao, sasa kumbe wao walikaa kikao, wanavyodai, ..kwenye kikao hicho, wakaona kuwa wewe huwezi kupewa dhamana…’akasema

‘Kwanini sasa mimi sina makosa, sijaua, ushahidi wanao…kwanini sasa, umeshindwa kazi…’nikasema kwa ukali

‘Sikiliza walioweka pingamizi hilo ni  mkuu wa kituo na huyo mpelelezi, wanasema kuwa, kupewa kwako dhamana kunaweza kukaharaibu baadhi ya mambo wanayoyafuatilia, wakasema wewe kwa jinsi wanavyokujua una watu wako ambao utawatumia waingilie kazi zao na kuweza kuharibu ushahid na kazi yao,..’akasema.

‘Hapana, hapana, ..wana nia gani na mimi, .....,halafu sasa ikawaje..?’ nikamuuliza, nikijua dhamani haiwezekani tena leo.

‘Baadaye tukaona twende ngazi za juu, ndio tukajipanga, docta, rafiki wa mume wako, na yule ofisa wa polisi, rafiki yake docta, wakasema wao wanakwenda kuonana na uongozi wa juu, na mimi nikawa naendelea kufuatlia mambo ya kisheria , tuligawana hivyo…’akasema

‘Wanasemaje hao waliokwenda huko..?’ nikauliza

‘Yaani ndio hapo naona kifo cha nyani… wenzangu tangu waende huko, hawajawasiliana na mimi, na cha ajabu kila nikipiga simu zao, hawapokei, zinaita tu..’akasema.

‘Mimi bado sijawaelewa, kwanini  mlipoona hivyo, hamkuja kuniambia mapema, mumesubiri hadi saa hizi, unafikiri mimi nitachukua hatua gani kwa sasa, kama mngelijuwa hilo limeshindikana mungelikuja hapa na kuniambia mapema, mimi ningejua ni nini cha kufanya, sasa muda kama huu, mnafikiria mimi nitafanya nini, ....au mnataka niendelee kusota huku jela, mnafikiri huku ni kuzuri sana  au...?’nikasema kwa hasira.

‘Sio kusudio letu, bosi, kila kitu kilikuwa kinakwenda vyema, na hatukutarajia kabisa kuwa kutatokea pingamizi kama hilo, mwanzoni tulijua kuwa wanafanya kupoteza muda tu, lakini dhamana ilishakubaliwa, ..’ akasema

‘Na hakimu au sio..?’ nikauliza

‘Ndio, hakimu yeye hakuona tatizo, kwa vile ushahid unaonyesha kuwa wewe huhisiki moja kwa moja, ila aliwapa tahadhari wajirizishe kwanza…’akasema

‘Sasa taarifa ya kukataliwa imekuja baadaye sana..jioni hii, kwahiyo tukaona tukimbilie ngazi za juu, na kiukweli dhamana ipo, lakini kwa leo...itakuwa vigumu, maana hawo viongozi wawili wenye pingamizi ambao ni muhimu sana kwenye kesi hii hawapatikani kabisa...’akasema.

‘Kwahiyo nyie mnataka nilale hapa tena, na huenda hata hiyo kesho ikashindikana, maana kama wameweka pingamizi, hata huko ngazi za juu watafanya nini, hawawezi kuwahini watendaji wao, au sio?’ nikauliza

‘Nimeona nije nikufahamishe hivyo, halafu mimi mwenyewe nitaende  huko ngazi za juu nionane na mwanasheria wao, kwasababu waliokwenda huko hawapokei simu, na hawajaweza kunipa yaliyotokea huko, na sheria inaona una haki ya dhamana, …’akasema

‘Sizani kama utafanya lolote kwa hivi sasa…’nikasema

‘Ningelijua kinachoendelea ningelijua nifanye nini….’akasema.

‘Mimi nahisi huko walipokwenda wamekwama, ndio maana hawataki kupokea simu yako...wanachofanya na wao,  ni kupoteza muda tu, ili wakija hapa, wasipate hata muda wa kuongea na mimi, hamna shida, nitasota tena hapa leo, lakini kesho nataka kuwasiliana na hizo ngazi za juu…nikasema

‘Wewe usijali , mimi kesho naamukia huko…’akasema

‘Utakavyoona, mimi sina imani na nyie tena..’nikasema.

‘Kulikuwa na jambo jingine nataka kukuulizia...’akasema.

‘Sitaki kuongea lolote na nyie tena, ninachotaka kusikia ni dhamana yangu imekubaliwa, basi, kama hakuna jibu kama hilo, sitaki kuongea na nyie, mumeshanivuruga akili yangu, wamefika wazazi wangu hapa wataniona  mimi kama mtoto mdogo, ...nitakuja kuwaambia nini,..’nikasema kwa hasira.

‘Wazazi wako nimeongea nao, na wao wakasema kama kesho itashindikana watafuatailia na wao waone tatizo lipo wapi, ...lakini nina uhakika kesho dhamana itapatikana....’akasema.

‘Hata kama umeongea na wazazi wangu,  haina maana tena kwangu, tumeshathibitisha kwao, kuwa hatuwezi kujitatulia mambo yetu wenyewe, mpaka wao wahusike, kitu ambacho sikutaka kabisa kitokee, ina maana wewe umeshindwa kazi, na wao watamuweka wakili wao, je unakubali hilo, mimi ninakulipa gharama zako za nini,kama kazi imekushinda....’nikasema.

‘Kazi haijashikana madam.., usiwe na wasiwasi, ...ni mbinu zao za kupoteza muda tu, wazazi wako wamenielewa, na sio kwamba watamuweka wakili wao, ...nitaendelea kufanya hii kazi, kama wakili wako, na hata kama wakili wao akifika hawezi kufanya miujiza, taratibu ni zile zile....hata hivyo, ... ‘nikamkatisha na kusema;

‘Ulitaka kuniuliza nini mwanzoni nisamehe maana akili yangu haipo sawa...’nikauliza huku nimesimama, nikiwa simuangalii, nimempa mgongo, niliona nimeongea kwa jaziba,na huyu ni wakili wangu natakiwa kumuheshimu.

‘Nilitaka kukuuliza je Mume wako alifika hapa leo kukuona?’ akauliza

‘Mume wangu, ...!!’ nikasema kwa kushangaga,

‘Ndio…’akasema

 ‘Hapana hajafika hapa…, mbona nasikia hali yake sio nzuri, ..?’ nikauliza

‘Ni kweli hali yake kuna muda ilibadilika, ikawa mbaya, unajua yeye ni mbishi sana, hataki kufuatilia baadhi ya mambo, sasa akaanza kudai kuwa anataka kuja kukuona, akakataliwa, na alipokataliwa akatoroka, na wakajua kuwa huenda amekuja huku kukuona....’akasema.

‘Katoroka,!!.. kwani kashikiliwa kama mfungwa, mimi ninavyojua yupo hapo hospitalini kwa ridhaa yake mwenyewe, ...’nikasema huku nikimgeukia na kumwangalia.

‘Ndivyo ilivyo, lakini kama mgonjwa akitaka kutoka nje,au kuondoka hospitalini kwa muda, ilibidi aondoke kwa kibali maalumu, kama ni lazima, na alipomuomba hivyo docta, akamkataliwa kutokana na hali yake ilivyokuwa, yeye akaondoka kwa siri, huko ni kutoroka, kavunja masharti ya hospitalini..’akasema.

‘Mimi nilishawaambia msimwambie huyo mtu, alitakiwa asifahamu kabisa kuwa kumetokea hivi, sasa mnaona, watamfanya sipone haraka…, sasa  katorekea wapi, yupo wapi, nyumbani au…?’ nikauliza.

‘Kesharudi, na hata mimi sijui ni nani alimwambia, nahisi, ni wazazi wako walipopata taarifa, labda walikupigia simu na ulipokuwa hupokei ndio wakampiga yeye, na hapo ndipo alipokuja kufahamu kuwa umekamatwa na hatimaye kueletwa huku Segerea, ’akasema.

‘Na sikukumbuka kuwauliza hilo wazazi wangu, na je wazazi wangu walipewa taarifa hiyo na nani..?’ nikauliza.

‘Sijui...labda rafiki ya mume wako, ....’akasema.

‘Hapana rafiki wa mume wangu tulikubalina naye kuwa wazazi wangu na mume wangu wasijue lolote kwanza, …hadi hapo muda muafaka utakapofika, na nilitarajia kuwaambia hilo baada ya kupata dhamana, kama ni lazima,..nahisi kuna kitu kimejificha hapa…kuna mtu anatuchezea akili akiwa na maana yake....’nikasema.

‘Mimi sioni kama kuna kusudio maalumu hapo, ni watu waliona kufanya hivyo, wanatenda wema, ...cha muhimu kwa sasa ni kutuliza akili zetu tuone ni jinsi gani tutalimaliza hili, na mimi nataka kuongea na mume wako, nina imani kuwa ninaweza kupata taarifa muhimu kutoka kwake, zitakazo tusaidia kwenye hii kesi,.....’akasema.

‘Kwa vipi wakati yeye ni mgonjwa, atakusaidije, hajui lolote utazidi kumuumiza tu?’ nikauliza

‘Kwa jinsi ilivyo, inabidi tuongee naye, hata kama ni mgonjwa, maana kila ukiangalia ni nani angeliweza  kuingia ndani kwako na kufungua  kabati, ...na kama ulivyosema hata ufungua wako, unao wewe mwenyewe…, na kule ofisini uliuficha mahali pa siri, hapa inaleta mashaka, maana kama ulivyosema wanaofahamu wapi unapoweka hata hiyo bastola yako ni wewe na mume wako tu, .....’akasema.

‘Kwahiyo unataka kusema nini hapo…?’ nikauliza

‘Inawezekana mume wako aliwahi kumwambia mtu mwingine, na huyo mtu mwingine akatumia mwanya huo kuingia na kuchukua hiyo bastola,...maana yeye ni mgonjwa, hatuwezi kusema kuwa yeye ndiye aliyefanya hivyo...’akasema.

‘Mimi bado sioni umuhimu wa kumuuliza mume wangu, tunaweza kufanya uchunguzi mwingine na kugundua ukweli hata bila kumgusa mume wangu,..tatizo nipo hapa jela, siwezi kufanya lolote kwa sasa, lakini kama ningelikuwa nje, ningelishagundua kitu...je kuna mtu kawasiliana na rafiki yangu, huyo msomi..,?’ nikauliza.

‘Ndio , mimi mwenyewe nilitaka kuongea naye, lakini muda niliompigia alikuwa yupo darasani, ufahamu aliondoka wakati wenzake wanaendelea na masomo, kwahiyo alipofika tu, akaingia darasani, ...bila hata kupumzika, sijaweza kumpata tena ila kuna muda aliongea na docta, rafiki wa mume wako, sijapata muda wa kumuuliza waliongea nini zaidi maana tulikuwa tunakimbizana na muda.’akasema.

‘Namfahamu sana rafiki yangu huyo ni mtu mwenye bidii sana, na akiamua kitu chake ni lazima akipate, na hayo masomo kwake ni muhimu sana, lakini kinacho nishangaza ni kutokunijali mimi, hafahamu kuwa hayo yote yasingelipatikana kama isingelikuwa ni mimi....nina hamu sana ya kuongea na yeye, na safari hii nataka anijibu maswali yangu yote kwa uwazi...’nikasema.

‘Mimi nahisi rafiki yako huyo, kaingizwa huko upande wa pili bila kupenda, kwani ninavyomfahamu ni mtu anayekuheshimu sana, isingelikuwa rahisi kuvunja uaminifu wake kwako,..lazima kuwe na kitu kikubwa cha msingi, kwake,..yule ni kama ndugu yako au sio, unafikiri anaweza kukusaliti...’akasema

‘Labda …kitu gani anaweza kunaswa nacho mpaka akubaliane nao, atakuwa mjinga basi, mimi sijui kwa sasa ila nitakuja kufahamu tu..’nikasema .

‘Kwa jinsi marehemu anavyojulikana, tunahisi, huyo jamaa alikuwa kwenye kazi zake za kitapeli, na huyo rafiki yako alikamatika kwenye jambo fulani, akapewa masharti kufanya hivi, usipofanya hivi, nitakuharibia, ni tabia ya marehemu pia kujishughulisha na biashara ya mlungula, ‘ blackmail.’.na hilo polisi wanalifanyia uchunguzi....’akasema.

‘Na kwanini tusubiri mpaka polisi waingilie undani wetu, nataka tufahamu ni nini kilitokea kabla polisi hawajagundua zaidi najua wawo wamerizika …ya kuwa mimi ndiye nahusika…, je unaweza kulifanyia kazi hilo ukagundua undani wake, kabla ya polisi, najua nakupa kazi ambayo sio yako?’ nikamuuliza.

‘Linaweza kufanyika kama wahusika watatoa ushirikiano, akiwemo mume wako, na rafiki yako,...nahisi hawo wanaweza wakawa ufunguo muhimu wa kulijua tatizo hili , chanzo chake na hatima yake...na nahisi kwasasa itakuwa ni rahisi kwao kuongea kila kitu, maana yule mtu waliyekuwa wakimuogopa, keshafariki, kama ndio yeye aliwashinikiza ...’akasema.

‘Kwahiyo unahitajia msaada gani kutoka kwangu?’ nikamuuliza

‘Msaada wako mkubwa ni kunipa ruhusu ya kuongea na mume wako, na ikibidi nitafanya uchunguzi nyumbani kwako, kwahiyo nahitajia ufunguo zako zote...’akasema.

‘Kwa hivi sasa nakuruhusu uongee na mume wangu, lakini kwa ufunguo, hebu kwanza subiria mpaka kesho kama nikitoka humu, mimi mwenyewe nitaifanya hiyo kazi, nikisaidiwa na wewe...kuna mambo nahitaji mwenyewe niyafanyie uchunguzi, sitaki yatoke nje, unanielewa hapo ...’nikasema

‘Sawa hamna shida…’akasema

‘Kama mna uhakika kuwa dhamana ni kesho, sioni kwanini nikupatie kila kitu,..na mengine nitakuambia hiyo kesho, kwahivi sasa fuatilia mambo ya dhamana yangu, na natumai kesho itapatikana , kama itakosekana, sitaki nikuone tena ukija hapa, na hao wenzako, waambie hivyo…umenielewa...’nikasema na kuanza kuondoka.

‘Kuna jambo jingine muhimu kabla hujaondoka, unahitajika kulifahamu...’akasema

‘Hilo jambo lisubiri kesho tafadhali...’nikasema.

‘Ni muhimu ulijue, ...kuna mtoto wa marehemu sijui kama unamfahamu, kaja kutoka nchi za nje…amekuja kwa ajili ya msiba wa baba yake anahitajia kuongea na wewe....’akasema

‘Kuhusu nini, kwanini anataka kuongea na mimi, kwa kazi gani, mimi sio ndugu yake hatuna mahusiano naye au anafikiri mimi ndiye niliyemuua baba yake..au mimi nitamshauri  mambo ya mirathi, baba yake hana mafungamani na sisi , kuwa labda alikuwa na hisa na mimi au....hapana sina haja ya kuongea na yeye, sitaki asije kunichanganya….’nikasema.

‘Anasema kwenye mirathi, aliyoachiwa na baba yake kuna mkataba unaoonyesha kuwa baba yake alikuwa na hisa kwenye kampuni yako na ya mume wako, kwa mume wako ni hisa nyingi kidogo, na kwako ni hisa chache tu, kwahiyo ni haki yake kulifahamu hilo...’akasema

‘Eti nini?’ nikasimama kama mtu aliyegusa na umeme.

‘Lakini hilo niachie mimi nitapambana naye nahisi ni kutokana na ule ubadhirifu wa ule mkataba wa awali, na sasa mkataba wao mpya unataka kuanza kuleta chokochoko, ..hilo niachie mimi hiyo kwangu ni kazi ndogo tu...’akasema.

This...oh,.... I can’t believe this,  its too much,....sitaki kusikia hayo maneno,...mwambie huyo mtu, asimchokonoe nyoka mwenye sumu shimoni, kama wanaishi kwa njia ya ulaghai, kama yeye ni sawa na baba yake, wasijidanganye kuwa wanaweza kufanya hivyo kila mahali...hakikisha unalimazliza hilo bila ya mimi kukutana na huyo mtu, sijui ana umri gani...’nikasema huku nikishika kichwa changu na kuvuruga nywele kwa hasira.

‘Huyo ni mtoto wake wa kwanza, ni mkubwa tu, mtoto huyo alizaliwa mapema sana, wakati marehemu bado anasoma, alimpa uja uzito binti wa watu..ambaye akaja kuwa mkewe,...kwahiyo ni mkubwa,. .’akasema

‘Basi ni mkubwa…sijawahi kumsikia..’nikasema

‘Mimi nilishamwambia kuwa kama ni maswala ya mikataba, anatakiwa kuongea na mimi, kwani mimi ndiye wakili wako, lolote linalohusiana na hiyo mikataba nalifahamu mimi, lakini kasisitizia kuwa anataka kuonana na wewe ili muelewane....’akasema

‘Tuelewane..ndio hayo siyataki,...naogopa kuwa ,nitafanya kitu ambacho sitapenda kukifanya, ...okey, tutaona naye hiyo kesho, ...fanyeni haraka nipate hiyo dhamana...’nikasema

‘Tutafanya hivyo madam…’akasema

‘Mimi sitaweza kuvumilia kubakia hapa ndani tena, ..ikishindikana nitatoka humu kwa nguvu..na wewe kazi hakuna...hii ni ahadi....’nikasema na kuanza kutembea kuondoka niliona wakili akitaka kuniuliza jambo jingien lakini sitakuata kusbiria tena…na wakati nafika mlangoni ili nigonge mlizi anifungulie mara kitu kikanigonga kwa nyumba kichwani, na giza likatanda,.....nikadondoka, na kupoteza fahamu.

NB:Ni nini tena hiki kinakuja....


WAZO LA LEO: Siku hizi kuna watu wanaishi kwa njia za ulaghai, uwongo, lugha za matusi, kejeli nk, watu wanaona ni kitu rahisi kuandika tu mitandaoni, hawajui dhamana yake na matokea yake kwenye jamii, ...hili ni changamoto kwetu, wakati huu jamii, zetu zinapojiunga kwenye kijiji kimoja cha utandawazi. Ni muhimu tukawa makini katika kutoa taarifa zetu, majina, anuani, namba za akiba zetu na maneno ya siri kwa watu, kwani huwezi kujua ni lini bahati mbaya itakuangukia.  Na kwetu watumiaji, tukumbuke kuwa maandishi(kalamu) ni hatari sana, ukishatuma kitu ujue hiyo taarifa ni kitu cha kudumu, ..leo kesho au baadae inaweza ikawa sumu kwako au kwa vizazi vijavyo, jiulize kwanza kabla ya kutuma, ninajenga au ninabomoa, ..


Ni mimi: emu-three

No comments :