Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, December 16, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-42‘Na je mume wangu ana taarifa?’ nikauliza.

‘Sina uhakika na hilo, sijaongea na mume wako bado, ..’akasema.

 ‘Wakili wako atakuwa  keshafika, mtaonana naye leo hii hii…

Alikuwa docta rafiki wa mume wangu , na baada ya hapo akaondoka, na mimi nikawa mikononi mwa askari wa Magereza…

Tuendelee na kisa chetu….

*************

Nikaingia jela, na kuonyeshwa hiyo sehemu niliyoambiwa ni ya usalama zaidi na kuahidiwa kuwa hapo sitasumbuliwa na kitu chochote…

‘Nataka nionane na wakili wangu haraka iwezekanavyo…’nikasema

‘Akija utaonana naye hakuna shida, lakini hata akija dhamana sio rahisi kupatikana kutokana na kosa lenyewe..’nikaambiwa.

‘Dhamani ni haki yangu, sina kosa, hata nyie mnalifahamu hilo, mnafahamu kabisa mimi sijaua, mnachofanya ni kunizalilisha tu mimi, hamjui na nyie ipo siku mtazalilishwa hivi hivi, …’nikasema

‘Sisi hatujui hayo, hapa kazi yetu nikuhakikisha tumekupokea kama mfungwa, mengine hayatuhusu, muhimu tii sheria za hapa, kuna kitu kingine unahitaji,..maana tumeambiwa tuhakikishe upo salama, na nakuhakikishia hutapata tatizo lolote hapa,.. …’akasema askari mmoja.

‘Sihitaji kitu…’nikasema na mlango ukafungwa nikabakia peke yangu.

*******

Nilibakia mle ndani, kiukweli niliwekwa mbali na wafungwa wengine,lakini hakukuwa na amani, akili iliteseka, na unawaza mambo ambayo hayana mtu wa kukusaidia, huna vitendea kazi, huna simu…inabakia kuwaza tu.

Hata hivyo, niliona sina jinsi, nikubali ukweli kuwa sasa nipo jela, ..je nifanye nini, kwanza nikaanza kuliwazia hili tukio kiundani,  nakujiuliza je nimekosea wapi, tatizo ni nini hasa, ni mimi au ni walimwengu,…au ni mume wangu…na ni kwanini nafikwa na mitihani hii yote,..nilijiuliza hadi kichwa kinauma, maana awali nilikwuwa nawaza tu bila mpangilio

‘Ni kwanini wamemuua Makabrasha..?’ hapo nikatulia na kujaribu kupata usingizi. Hakukuwa na usingizi baadae nikagundua kuwa mtu mwingine kaletwa upande mwingine wa chumba, naye alikuwa akihangaika kivyake, hakutaka hata kuniangalia….yeye baadae nikamuona kalala, ni kama mzoefu vile

‘Ni nani kamuua Makabrasha..?’ ilikuwa ndilo swali langu la mara kwa mara

 Huenda haya mauaji yanatokana na matukio ya nyuma, ...ambayo yameanzia kwa mume wangu, au kwangu, mtu akayafuatilia na baadae akaona huu ndio muda muafaka wa kulifany ahilo , ili kuichafua familia yangu, sasa ni nani huyo

‘Ni adui zake…’ ndivyo polisi wanavyoamini hivyo, na adui za Makabrasha wanavyoona polis kwa ushahidi ni mimi….

‘Kwa mume wangu haiwezekani kwa maana kuwa  Makabrasha alikuwa rafiki ya mume wangu, na ndiye anamtumia kufanikisha malengo yake, kama hiyo mikataba na…hapana kwa mume wangu haiwezekani, kwanza mtu mwenyewe yupo hospitalin, na sizani kama ana watu anaoweza kuwatumia, pesa ya kufanya hivyo ataipatia wapi..’nikawa naongea kwa kimoyo moyo.

‘Je ni mambo ya kisiasa…’nikasema na kuinua kichwa, nikagundua kuwa yule mtu mwingine alikuwa kalala, lakini sasa anakuwa kama ananichunguza kinamna fulani, sikumjali,…nikaendelea kuwaza.

Kutokana na maelezo ya rafiki yangu hili jambo limekwenda zaidi na kuingiza siasa ndani yake, kwahiyo haya yanaweza yakawa yamepangwa kisiasa, lakin kwa vipi, ili iweje, wakati huyo ni mtu wao muhimu sana, hapana kwa upande huo sizani kama wanaweza kumuaa, sasa ni nani...

‘Huyu Makabrasha kama anatumiwa, na hao wanasiasa ni kwanini wamuue…?’ nikajiukuta nimeongea kwa sauti mpaka nikajishutikia, na niligundua yule mtu mwingine upande ule alikuwa kama ananisikiliza

Nikamzarau na sasa nikawa makini ili nisiongee kwa sauti, ..jamani ukiwa mahali kama hapo, unakuwa kama umechanganyikiwa fulani hivi, usiombe kukaa sehemu kama hizo, hakuna mawasiliano na wanadamu wenzako.

‘Mkataba…eeh’ nikasema na kukuna

‘Kuna huo mkataba wa pili, wa huyu rafiki yangu aliotakiwa yeye kuweka sahihi, je huo mkataba ulikuwa malengo gani, kwanini uwe wa kulazimishana,...ili iweje, kwa manufaa ya nani, kama ni Kwa Makabrasha kwanini wakamuua, na kama Makabrasha alikuwa jembe la wanasiasa kwanini wamuue…hapa ina maana gani, ..kuwa aliyemuua Makabrasha sio hao wanasiasa, ni watu ambao hawana umuhimu naye sasa ni akina nani’

‘Hapo ndio wewe unaingia..na kushukiwa kuwa huenda ndio wewe ulifanya mauaji hayo…’ nilikumbuka kauli ya docta rafiki wa mume wangu.

‘Hapa kwa vyovyote iwavyo, rafiki yangu anafahamu mengi yanayohusiana na huu mkataba,..namfahamu ni mjanja sana, atakuwa keshafahamu kitu, …na huenda na yeye ni muhusika mkuu, na anaweza akafahamu lolote kuhusiana na huyo mtu aliyekuwa akiongea na Makabrasha, na huyo mtu ndiye muuaji, sasa ni nani huyo…’nikawaza kimia kimia.

‘Rafiki yako hahusiki kwa vile aliondoka  kwa Makabrasha..akatoweka, ushahid upo kuwa alikuwa uwanjani kajificha,…mmh, kajificha wapi…

‘Hayo mauaji  yalifanywa baada ya yeye kuondoka kwahiyo yeye hahusiki kwa hayo mauaji, labda awe katuma watu wake waje kufanya hivyo...na watu wake ni akina nani,...watu wake wengi nawafahamu,...nitaongea nao,....lakini kwa vipi ...hapa si mpaka mimi nitoke humu, lini... na muda ni muhimu sana...’nikajikuna kichwa huku nikiwaza.

Nikasimama, na kujinyosha, niliona yule jamaa kule akijiinua kuniangalia, mimi sikumjali..nilijinyosha nikachukua mazoezi kidogo, ilimradi mwili ufanye kazi, hadi nikachoka na kujilaza.

‘Ni nani mwingine anaweza kuhusika, labda docta, rafiki wa mume wangu, lakini kwa nini ahusike, ana nini na huyo mtu, hapana, huyu haweze kabisa, ..sasa  ni nani….mhhh, ?’ nikajiuliza bila majibu.

Kichwa sasa kimechoka kuwaza, nitaka kama nipate dawa ya usingizi, nitaipataje, maana kwa hali kama hii nitawehuka…nikasimama, nikakaa, nikasimama nikaaa..yaani kiukweli akili ilikuwa sio sawa..baadae nikajilaza tena na wakati nataka kupata usingizi..mara…

 Nikasikia nikiitwa, na kuambiwa wakili wangu ameshafika, na wamemruhusu nikaongee naye kwa muda mfupi tu, kwani muda wa kuongea na watu wa nje ulishapita ila nimepata upendeleo tu..

Kwa haraka nikasimama na mlango ukafunguliwa, nikatoka hadi sehemu ya kuongea na wageni, nikamkuta wakili wangu akinisubiria, na aliponiona tu akaanza kuongea;.

‘Samahani sana, ilibidi kwanza nihakikishe kuwa mzazi wangu yupo sehemu stahiki, si nilikuambia anaumwa, kwahiyo kutokana na hili tukio, ikabidi tubadilishe mipangilio yetu yote,..ikiwemo kumchukua mgonjwa, nije naye huku Dar, hili halikuwepo kwenye mipangilio yetu.

‘Anaendeleaje..?’ nikamuuliza

‘Ni hivyo hivyo, na uzee nao..lakini uzee sio tija ya kuwa mtu aumwe, ni maradhi tu, na kwa vile mwili ni mzaifu, madawa yanachukua muda kufanya kazi yake, tunapambana, huku tukimuomba mungu..’akasema

‘Poleni sana…’nikasema

‘Ilikuwa ni kazi kubwa sana kumshawishi hadi akakubali tuje naye huku, hakunielewa ni kwanini najali kazi zaidi, hakuelewa umuhimu wa hili tukio, lakini mwisho wa siku akakubali,

‘Haya...., sasa tuingie kazini, maana nimejitahidi kupitia kwa watu wote muhimu, kuanzia kwa wale  waliokukamata,…mpaka nimefika eneo la tukio…nikaongea na watu mbali mbali mle kwenye lile jengo, nikaja kuongea na wapelelezi nia ni kupata picha na hali halisi, na mtizamo wa watu kabla sijafika kwako ....’akasema.

‘Wamekudanganya nini hao watu?’ nikauliza.

‘Kiufupi ni kesi ngumu..’akasema

‘Lakini mimi kiukweli sijaua, siwezi kukuficha hilo…’nikasema

‘Najua, hujaua, polisi bado wanahisi unaweza ukawa umefanya hivyo, unajua kazi ya polisi ilivyo, ni mpaka wajirizishe, shuku shuku ni moja ya kazi zao ili kumpata muuaji, na kukushikilia kwako ni njia moja wapo ya kumpata muuaji,..’akasema

‘Kwanini wanitese mimi,maana huku nikutesena, napata hasara kiasi gani,..nazalilika, familia yangu inaingie kwenye kashfa, hawalioni hili...’nikasema

‘Ushahidi mkubwa wanao kuwa wewe unaweza kuhusika,...lakini kinachowachanganya, ni muda wa muaji,..muda ndio imekuwa kikwazo kwao, kukuweka wewe kuwa mtuhumiwa mkuu…’akasema

‘Wanajua hilo..’nikasema

‘Sasa kutokana na hilo wanakuja kukuona huhusiki moja kwa moja na mauaji hayo, ila wanafikiria kuwa wewe utakuwa ulimtuma mtu, ayafanye hayo mauaji , na ulifika hapo kuchukua nyaraka fulani hapo ofisini ndio wakakuwahi…swali kwanini ujipeleke mwenyewe…’akatulia.

‘Nilijipeleka, mimi nilikuwa sijui lolote ni waongo hao…’nikasema

‘Pili, silaha yako ndiyo iliyotumika kwenye hayo mauaji, japokuwa hakuna alama zozote za vidole kwenye hiyo silaha, ya kwako au ya mtu mwingine, silaha haina alama yoyote, na wewe walikukuta umevaa kinga za mikononi.

‘Kwahiyo, swali ni kwanini ulivaa kinga,…na silaha haina alama za vidole , ina maana ulifany ahivyo makusudi…’akasema

‘Wanasema pia ulipofika ulisema una miadi na marehemu…lakini kwenye kumbukumbu cha kitabu cha marehemu haupo, yeye ana kitabu cha kumbukumbu cha watu alitakiwa kukutana nao, hakuna jina lako, na imegundulikana kuwa ukurasa wa siku hiyo umechanwa, na hawajaona ukurasa huo mahali popote huenda ingesaidia jambo…’akasema

‘Kwahiyo bada ya kumtafuta muuaji, wanahangaika na mimi au sio…’nikauliza

‘Wanasema kwa wadhifa wako unaweza ukawa uliwatuma watu wako, ukawapa silaha yako, na huenda kilichokupeleka hapo ni kuharibu ushahidi pamoja na kuchukua nyaraka ambazo alikuwa nazo Makabrasha, swali ni kwanini uende mwenyewe wakati..umeagiza mauji yafanyike, na kwanini ukadanganya kuwa ulikuwa na miadi na huyo mtu, …’akasema

‘Unaona eeh, wao wanajikanyaga tu kutaka kuniharibia jina langu, kama wanatumiwa basi wataumbuka wenyewe…’nikasema

‘Swali jingine ni kwanini uliwadanganya kuwa ile bastola sio silaha yako…wakati silaha yako unaifahamu…hapo wakahisi kuna kitu unawaficha..’akasema

‘Lakini ni kweli, mimi nilikuwa sina uhakika bado, maana silaha yangu niliicha kabatini…’nikasema

‘Uliposema silaha yako ipo kabatini walikwenda kuhakiki,  wakaona kabati lako limefungwa, hakuna dalili zozote za uvunjwaji, kwa maana huyo mtu aliyeichukua hiyo silaha yako ana ufungua, ni nani mwingine mwenye ufunguo wa hilo kabati unapoweka hiyo silaha..?’ akaniuliza.

‘Hakuna mwingine…nakala zote ninazo mimi, mume wangu hakuwa na haja ya ufunguo wa kabati hilo…’nikasema.

‘Kwahiyo huyo mtu aliyeichukua hiyo silaha yako,ndio huyo huyo, aliyeweza kuiba mikataba,..yawezekana mtu huyo anafahamu siri zako za ndani, sasa ni nani huyo, unaona hapo, kwahiyo ni lazima wawe na shaka na wewe..’akasema

‘Kiukweli hata mimi mwenyewe nashindwa kuelewa hapo, ni nani huyo..?’ nikawa kama namuuliza wakili

‘Ndio hapo polis hawataki kukuachia....’akasema wakili.

‘Zaidi ya mume wangu ..hakuna anayejua kuhusu hizo funguo, hata rafiki zangu hawajui hilo, ..wafanyakazi wa ndani hawafiki huko, huko nafanya usafi mimi mwenyewe…na mume wangu ni mgonjwa, asingeliweza kulifanya hilo, japokuwa hajambo lakini bado hajaweza kutembea vyema, na asingeliweza kutoka hospitalini wasimuone….’nikasema

‘Na hii inafanya jambo hili liwe gumu kidogo, kwani watu tunaowafahamu waliopo karibu na wewe na wanaoweza kufahamu nyendo zako ni mume wako, mwingine kwa mbali ni rafiki yako, ambaye yupo mbali sana na tukio lenyewe, kiushahidi, maana muda wote alikuwa na watu wanaoaminika, mwingine ni nani unayemuhisi....?’ akaniuliza.

‘Sana sana ni docta, rafiki wa mume wangu, ambaye hawezi kuhusika kabisa....’nikasema.

‘Kwasasa kila mtu anaweza kuhusika, cha muhimu ni kukusanya ushahidi, ...lakini kwa sasa, kwa vile nimepewa muda mchache tu, ngoja nikafuatilie kuhusu dhamana yako kwanza, na kwa hivi sasa unatakiwa kukumbuka kila kitu,  ili  tukikutana tena, uniambie kwa uwazi, usinifiche chochote, ni muhimu sana kwa sasa...’akasema wakili.

‘Nasikia dhamana imekataliwa...ni kweli…?’ nikauliza.

‘Mimi ni wakili wako, kama imekataliwa nitakuambia mimi mwenyewe, usiwasikilize watu wengine, na kwa tahadhari, usiongee na mtu mwingine yoyote kwa hayo yaliyotokea, zaidi yangu mimi,  unanielewa hapo..tukishirikiana vyema.., hili litakwisha japokuwa lina ugumu wake kidogo...’akasema na kutaka kuanza kuondoka.

‘Ni ni kweli kuwa haya mambo yamekuwa ya kisiasa zaidi….?’ Nikauliza

‘Yawekana ikawa hivyo, ila kwa hivi sasa ni mapema kulisema hilo, maana kwangu mimi natakiwa niwe na ushahidi unaoweza kumtosheleza hakimu, sio maneno ya kusikia ..unanielewa, nia ni kukuondoa kwenye makosa kisheria, sio kupambana na makundi…’akasema

‘Inasemwa hivyo kuwa huenda ni maadui wa baba yangu wa kisiasa wanatumiwa mwanya huo kujenga kashafa,kwa vile baba yupo kwenye siasa, ..’nikasema

‘Nikuambie kitu, hadi hivi sasa upande huo wana kundi limeundwa kwa ajili ya kutafuta ni nani kamuua mtu wao, ..Marehemu alikuwa mtu muhimu sana kwao, na wametumia pesa nyingi kumgharamia , kwenye masomo nk..haiwezekani wao, wakamuua..lolote laweza kutokea, ..kama ni kisiasa, lakini kiushahdi haina mshiko..’akasema

‘Kwahiyo…?’ nikauliza

‘Kwa hivi sasa acha nifuatilie mambo ya dhamana yako kwanza, ni muhimu sana hilo,  kabla siku haijaisha, .., mengine yanaendelea kufanyiwa kazi, unasikia wewe kwa leo nakuomba tu, utulie kwanza, najua upo kwenye wakati mgumu lakini kwa kosa kama hili, hatuna ujanja wa kulazimisha mambo, niamini mimi,…’akasema

‘Nakuomba kitu kimoja, usije ukamwambia mume wangu, najua wazazi wangu wameshafahamu lakini mume wangu ni mgonjwa, haya mambo yatazidi kumchanganya,...’nikasema.

‘Wote hawo wanashafahamu, wazazi wako walinipigia simu, japokuw mtu wa kwanza kunipigia simu alikuwa ni mume wako, niliongea naye na yeye , na akaniomba sana niweze kukusaidia upate dhamana haraka iwezekanavyo...’akasema

‘Haiwezekani, ni nani alimuambia mume wangu kwa haraka hivyo alijuaje, kwanini watu wanachukua mambo kwa haraka hivyo, hwafahamu kuwa huyo mtu ni mgonjwa, na docta, amesema hakuwahi kuongea naye leo, ni nani huyo..?’ nikauliza.

‘Ndio hivyo, ili ujue kuwa, dunia sasa hivi haina dogo....wa kwanza kunipigia simu alikuwa ni mume wako, na baadae ndio wakanipigia wazazi wako, wazazi wako ndio walionifanya nihangaike kumchukua mgonjwa nije naye…’akasema na kuondoka.

Nb: Tulikuwa tunamalizia sehemu hii, ilikuwa ndefu kidogo, ndio tukaigawa sehemu tatu, tukijaliwa tutaingia sehemu nyingine, kufichua utata huo, ni nani kamuua Makabrasha na kwa nini.... 

Swali,: bashiri ni nani anaweza akawa kamuua Makabrasha, kati ya wahusika hawa: Mdada(mke wa mgonjwa), mgonjwa (mume wa mdada), Rafiki wa mdada(anayesafiri masomoni), Docta rafiki wa mume, wanasiasa ili kujenga kashfa...toa maoni yako, na ni kwanini unaona hivyo.

Tuzidi kuwa pamoja.


WAZO LA LEO: Ukiona mtu anafurahia madhila na taabu za wengine , na anatamani watu hao hata wafe, watu ambao wasio na hatia, wanateseka, wazee , akina mama na watoto ambao hata hawajui kinachoendelea, wewe unafurahia, unatoa maneno ya dharau, chuki, unadhihirisha ile chuki yako ya ndani…eti kwa vile sio wenzako, ujue mtu huyo ana roho ya shetani ndani yake.

 Haijalishi mtu huyo anayeteseka, anayedhulumiwa haki yake yupo kwenye kundi gani, ilimradi hayo yanayompata sio stahiki yake, na hakuna hukumu kisheria iliyopitishwa dhidi yake, ilibidi watu wapaze sauti ya kuwatetea,…lakini watu wanafurahia, wengine wakiuwawa, wakiteseka, wakidhulumiwa, utafikiri hao wanaofurahia hivyo wataishi milele,..hakuna atakeyeishi milele, marejeo yetu ni kwa yule aliyetuumba, na siku itafika hukumu ya kweli itatimilizwa.

Tukumbuke sisi sote ni wana-wa -Adamu, na chanzo chetu ni kimoja, sasa iweje damu ya ndugu yako inamwagwa, watu wanadhulumiwa haki zai, sisi tunafurahia, kwa kisingizio cha makundi, bado tunaiona ni wacha mungu…hapana huo sio ucha mungu,na wenye tabia hiyo, sio mtoto wa Adamu, na kama wewe sio mtoto wa Adamu, utakuwa mtoto wa nani..

No comments :