Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, December 15, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-41


 Usiku sikulala,.nilimuomba sana mola....hadi kunapambazuka macho mazito, usingizi hakuna, lakini macho yanataka kulala...akili haitaki..na hatimaye kukapambazuka, na kama ilivypangwa...baada ya muda, gari likaja huyo ..ikawa safari ya kwenda Segerea..sikuamini..lakini ndivyo ilikuwa

Tuendelee na kisa chetu...

************

Nilipitiwa na usingizi njiani, tahamaki nikafikishwa Segerea.,!

Tulipofika huko nikashangaa kuona gari la docta rafiki wa mume wangu, limeshafika, hapo nikajiskia faraja kidogo, japokuwa nilikuwa kwenye wakati mgumu, na kujutia kwa nini nilimkaidi, nilifahamu maneno gani yatamtoka huyu mtu, nikamuanza  mimi kuongea pale aliponisogelea;.

‘Sasa ndio umefuata nini, muda wote ulikuwa wapi, umeacha mpaka naletwa Segerea, kwanini hukufika mapema nikiwa kituo cha polisi,....huku unasema unanijali, eti unanilinda?’ nikaanza kumlaumu.

‘Wewe hujui tu, tulivyohangaika, kwanini ulikuwa hupokei simu..?’ akaniuliza na mimi sikuwa na la kusema nilitaka kusikia tu kuwa labda wamefanya jambo lolote ili nisilale hapo Segerea.

‘Ina maana mlikuwa mnafahamu kuwa Makabrasha kauliwa?’ nikauliza.

‘Nilijua baadae sana…yaani we acha umetupa wakati mgumu sana, sasa hata sijui lakini ngoja tuone…’akasema

‘Ina maana…’nikataka kusema

‘Niliamini kuwa utakwenda nyumbani kwako maana muda ulishakwisha, japokuwa bado nilikuwa na mashaka moyoni, lakini bahati akaja mgonjwa, ikawa nipo kwenye heka heka za kumhudimia,..nilipata mwanya nikakupigia ukawa hupokei, yaani mpaka namalizana na huyo mgonjwa, muda umekwenda, ndipo napokea simu kutoka kwa watu wangu wananielezea kuhusu hilo tukio..’akasema

‘Aaah, hata sijui …’nikasema na yeye akanikatisha kwa kusema;

‘Lakini hayo tutaongea baadaye, ila nahisi hawa watu wa usalama hawakutaka nifahamu wapi ulipo mapema…, kwani nilipopata taarifa usiku huo huo, nilianza kukufuatilia mimi mwenyewe, nikafika hadi hapa ulipokuwa umeshikiliwa nikaambiwa haupo…’akasema

‘Kwanini walifanya hivyo..?’ nikauliza

‘Sijui…usiku huo huko nikaenda hadi makao makuu ya polisi, ...nashukuru jamaa yangu, alipopata hiyo taarifa, alifuatilia na kugundua kuwa upo huko nilipotoka, nikarudi tena hapo sikuruhusiwa hata kukaribia hicho kituo....’akasema.

‘Ok, ok…Sasa niambie umefikia wapi au umechukua hatua gani?’ nikamuuliza.

‘Kwanza niliwasiliana na mkuu wa upelelezi wa anayeshughulikia kesi yako, na akasema kuwa kiukweli vithibitisho vilivyopatikana vinaonyesha kuwa wewe ni mshukiwa muhimu, na sio rahisi kukwepa hilo, na hata dhamana inaweza kuwa ngumu kupatikana, ....’akasema

‘Kwanza nikuulize wewe ulifahamu muda gani kuwa huyo mtu alishafariki, ..?’ nikauliza

‘Nilifahamu baada ya kupigiwa simu na watu wangu wakati huo umeshakamatwa…’akasema

‘Kwanini sasa ulikuwa ukinipigia simu, ni kama vile unafahamu kilichopo mbele yangu au sio..?’ nikauliza

‘Ulipotoka hapa nikapata huyo mgonjwa nikawa bize, na nilipopata nafasi ndio nikawa nakupigia simu, kuhakikisha kama umefika nyumbani na muda huo nilikuwa sijajua lolote, unielewe hapoa..’akasema

‘Sasa mtafanya nini, mnakubali mimi nilale huku Segerea..?’ nikauliza

‘Polisi wanadai bado wanafanya uchunguzi, kujirizisha kuwa kweli wewe ni mshukiwa muhimu au kuna watu wengine, wanasema wanaogopa ukipewa dhamana utatumia utajiri wako kuharibu ushahidi, ....na kinachowatatiza  ni muda wa hayo mauaji....’akasema.

‘Muda…eh, wanasemaje hapo , najua hapo nitawashinda, ..hawataki kufany akazi yao vyema, mimi nilifika mtu keshauwawa…hata damu zinaonyesha …zilikuwa kama zimeganda…sikuweza kutazama vyema lakini ndio hivyo..na kama vipimo vyao vipo sahihi wataligundua hilo..’nikasema

‘Vipo sahihi…wameshaligundua hilo…’akasema

‘Na hapo ndipo inaonyesha wazi mimi wamenishika kimakosa...na kama wanalifahamu hilo kwanini wanileta huku, …aah, sijui ni nani kafanya hayo mauaji, kaharibu kila kitu, kaniharibia …hata sijui nisemeje,  aheri ningelifahamu,...au unafahamu lolote kuhusiana na huyo muuaji.?’nikamuuliza  nikimwangalia, nay eye akatabasamu na kusema.

‘Wanasema kuwa ni kweli wewe ulifika wakati Makabrasha keshauwawa, hata hivyo, wao wanadai kuwa inawezekana wewe ndiye uliyetuma mtu au watu kufanya hivyo, na wewe ukafika hapo kufuatilia ili kuthibitisha, au kuchukua baadhi ya nyaraka,ulizozitaka..’akasema

‘Hawo watu wana wazimu, nyaraka gani nilikuwa nazifuatilia mimi, wakati nilikuwa nakwenda kumuangalia rafiki yangu, kama nilivyokuambia nahisi yupo kwenye matatizo, ni wema na huruma vimeniponza, ooh ...’nikasema kwa ukali na kabla hajajibu kitu nikasema.

‘Yah, wema na huruma zako, pole…’akasema

‘Wakili wangu hajafika maana wewe sikuoni kama utaweza kunisaidia lolote kwa hivi sasa..?’ nikauliza.

‘Tatizo wakili wako hayupo hapa Dar, ila keshapigiwa simu, anaweza akafika leo hii, kaambiwa apande ndege ili awahi kufika sasa sijui maana anauguza mzazi wake, si unalifahamu hilo…’akasema

‘Sasa wanaposema nilifuata nyaraka , nyaraka gani hizo…?’ nikauliza

‘Wanasema kuna Mikataba miwili ilionekana juu ya meza, mmoja ni mkataba kati yako na mume wako, na kuna mkataba mwingine, huo mkataba mwingine hawakutaka kuusema unamuhusu nani, wanasema kwa hivi sasa itakuwa siri yao, kwani unaweza kutumika kama ushahidi mahakamani ...’akasema

‘Ni siri yao kwa vipi..?’ nikauliza

‘Kwa mtizamo wao wewe huenda ulikuwa ukitafuta hiyo mikataba au mambo yanayohusiana na hiyo mikataba. Na kuna vielelezo wamevipata vinavyoonyesha kuwa wewe na marehemu mlikuwa hamuivani,…’akasema

‘Vielelezo gani hivyo..?’ nikauliza kwa haraka maana askari alionekana kuja kunichukua.

‘Ni vielelezo vya kurekodiwa,  ni kazi ya Makabrasha, yaonekana alishajiandaa vyema kukuharibu, kuna ushahidi mwingi, wa sauti yako ukigombana nay eye, na wewe ukitoa kauli za vitisho dhidi yake, na kuna CD siunajua tabia yake ya kurekodi mazungumzo ya watu, kwenye mkoba wake ana mitambo hiyo ya kurekodi, anatembea nayo....’akasema.

‘Ni kweli niliona hiyo mikataba pale mezani wakati naingia kwa Makabrasha, lakini sikupata muda wa kuisoma, ila nahisi mmoja kati ya hiyo mikataba ni ule mkataba waliouchakachua,....sikupata ujasiri wa kuusoma kwa haraka.., kwani kwa muda huo ndio niligundua damu, zikiwa zimatuama juu ya meza, kuashiria kuwa Makabrasha kauwawa...........’nikasema.

‘Na ni wakati wanaingia hawo maaskari polisi nahisi kuna mtu aliwapigia simu waje..na wakati wanaingia ndio nikaona bastola ipo karibu kabisa na miguu yangu, imefunikwa kidogo na kiti, ilikuwa sio rahis kuiona mpaka ufike pale niliposimama…’nikasema

‘Wakaionaje sasa..?’ akauliza

‘Kwa muda huo watu wao walikuwa wakichunguza, na muda wote walikuwa hawajafika pale niliposimama, unajua pale nilikuwa kama nimeganda, siamini ninachokiona…kashfa, kashfa…ni mpaka pale aliponisogelea huyo askari wao, ni kiongozi wa hilo kundi lililofika, akaanza kunihoji…

Wakati anafanya hivyo ndio akaiona hiyo bastola..’nikasema

‘Una uhakika hukuwa nayo silaha yako wakati unafika hapo kwenye tukio..?’ akaniuliza na mimi nikamuangalia kwa jicho baya.

‘Ina maana huniamini, sijamuua, mimi…silaha sikuwa nayo bwana, ..’nikasema

‘Sio sikuamini, unaweza ukawa ulitembea nayo, au sio, si ulisema kuwa kutokana na hali ilivyo usiku utakuwa unatembea na silaha..?’ akaniuliza

‘Sijawahi kuichukua tokea siku ile nilivyokuambia, niliongea tu,..na silaha yangu muda wote ipo kabatini, nimeifungia hapo, na mimi ndiye mwenye ufunguo wake…’nikasema

‘Je mume wako hana nakala ya ufunguo huo wa kabati..?’ nikauliza

‘Hapana kuna makabati yeye hana nakala ya funguo zake…, na hilo nimojawapo, lakini yeye anafahamu , akitaka kulitumia mimi huwa ninampatia ufunguo..mara nyingi hana kazi yoyote na hilo kabati, maana vitu vilivyopo ni vyangu vya kike kike tu, unasikia…, hana haja na hilo kabati kabisa, hata hivyo yeye yupo hospitalini, anaumwa, huwezi kumshuku kwa hilo…’nikasema

‘Na ndio hapo inapokuwa kesi ngumu kwako, na inakuwa vigumu kuwathibitishia viginevyo, vipi funguo unazo, kabati lifunguliwe na..…’akasema

‘Hapo hata mimi sijui kwakweli..’nikasema na niliona kama docta ana mashaka na mimi.

‘Ulipofika chumba cha Makabrasha, uliiona hiyo silaha kabla polisi hawajaingia au ilikuwa wapi, ..?’ akaniuliza

‘Ilikuwa sakafuni, nilishtuka naikanyaga wakati huo polisi wameshaingia na kuniamrisha niweke mikono juu, ndio hapo na mimi nikaiona hiyi silaha, muda wote nilikuwa sijaiona,..ilikuwa hapo sakafuni, karibu kabisa na mguuni kwangu, yaani hapo ndio nguvu zikaniishia ....’nikasema

‘My, my….miguuni mwako na usiione wakati wote,…hapo inaashiria nini, kuwa muuaji, alifanya hivyo, akaiacha hiyo bastola hapo ili polisi waione, lakini sasa mbona ilikuwa miguuni mwako…’akasema

‘Mimi sijui..nilikuwa natembea kumshtua marehemu nilijua kalewa, kulikuwa na chpa kubwa ya pombe mezani na gilasi mbili..’nikasema

‘Mhh …uone hapo sasa, ilikuwaje ikawa miguni mwako,…hapo itaonekana ulikuwa nayo, ukaidondosha sakafuni, kwa kuchanganyikiwa.....’akasema.

‘Mbona unakuwa kaam huniamini jamani, kama wewe huniamini polisi itakuwaje…’ nikasema sasa nikichezesha chezesha miguu kitoto vile..

‘Mimi nataka kufahamu ukweli ..na kudadavua jinsi gani ya kuweza kusaidia…siokwamba sikuamini, mimi ninaamini unachoniambia ndio ukweli, au sio…’akasema

‘Najiuliza  ni nani ambaye alifahamu kuwa nitafika huko, zaidi yako wewe, maana hata watu wangu sikuwahi kuwaambia?’ nikamuuliza.

‘Kuna mtu utakuwa uliongea naye kwenye simu labda au alikuwa akikufuatilia, bila ya wewe kufahamu, …au…’akasema na mimi nikamkatili kwa kusema;

‘Mtu niliyeongea naye ni rafiki yangu, nilimtumia ujumbe wa maandishi, hakuna mtu mwingine niliyemwambia kuwa nakwenda huko, kwa Makabrasha ...na sijui labda simu yake ilikuwa mikononi mwa hao watu, hususani marehemu, kama alikuwa nayo.....’nikasema.

‘Kabla hujafika kwangu uliongea na rafiki yako..?’ akaniuliza

‘Ndio, …ndio yeye alinielezea kuhusu kuibiwa mtoto wake, na baadae wakampigia simu kuwa mtoto wanaye wao, na …katika kuhangaika wakaukubaliana na hao kuwa atimize matakwa yao, akaletewa mikataba aweke sahihi na kukubaliana nayo…’nikasema na hapo nikakumbuka jambo

‘Mkataba..mkataba gani huo…?’ akaniuliza

‘Mim sijui maana sijawahi kuuona na…ndicho kilinisikuma sana nifike nionane na huyo rafiki ili nifahamu kinachoendelea…’nikasema

‘Hebu kumbuka vyema wakati unaongea na huyo rafiki yako aliongea ni ni zaidi cha kusaidia labda…?’ akaniuliza

‘Unajua nimekumbuka kitu wakati naongea na huyo rafiki nilisikia mtu kama anamkatiza kuongea jambo, ni sauti ya mtu yaonekana alikuwa karibu yake,…ndio hapo simu ikakatika…’nikasema

‘Huenda atakuwa ni huyo huyo Makabrasha, kama walikuwa naye karibu au kama kulikuwa na mtu kamshikilia..hilo bado halisaidii kitu..’akasema

‘Mimi nahisi  kuna mtu mwingine,alitokea wakati unaongea nami, hakuzima hapo hapo, nikawa nasikia wakiongea mambo, lakini sikuyasikia vyema,..baadae ndio akazima hiyo simu ...’ nikasema.

‘Hiyo yote yawezekana ikawa ni geresha tu ya rafki yako, mimi bado sijamuamini kihivyo..’akasema

‘Lakini hapo ilikuwa mapema sana, kwenye saa kumi na moja hivi....sina uhakika sana ilikuwa ni saa ngapi, ila ilishaanza kuingia jioni...na muda huo huyo muuaji anaweza alikuwa hajafikia, kama ni mtu aliyekuja baadaye kufanya hayo mauaji..’nikasema

‘Mauaji yalifanyika baadae…usiku..wanasema ni kati ya saa moja hadi saa mbili hivi, saa mbili na nusu…na hili linakuweka mbali kidogo na hayo mauaji, lakini hoja hiyo bado haitii nguvu kukuweka mbali na kadhia hiyo kwani wanakushuku bado ni wewe unahusika kwa namna moja au nyingine..’akasema

‘Mimi nahisi mle ndani kulikuwa na mtu alikuwa akiongea na Makabrasha, maana nilikuta gilasi mbili..sasa huyo ndiye anaweza akawa ndiye kafanya hayo mauaji, je polisi wanasemaje kuhusiana na hilo,..?’ nikauliza

‘Hilo hawajaliongelea..sijasikia hilo.nahisi mengine wameyaweka kama akiba yao…kwanza ni kuthibitisha kuwa je wewe ndiye muaaji au la..akiba yao nyingine kama sio wewe ni nani mwingine,..kwahiyo hizo gilasi, ..yawezekana ni wewe ulikuwa naye, mkinywa wanaweza kuhisi hivyo..’akasema

‘Mimi sikuwa naye, na wala Marehemu hakujua kuwa nitafika hapo, japokuwa niliwadanganya walinzi kuwa nina miadi naye, je hizo..gilasi hazina alama za mikono za watu…?’ nikauliza

‘Hilo litafuatiliwa, lakini kama ni muuaji mwenye ujuzi atakuwa kazifuta..vinginevyo polisi wangekuwa wameliongelea hilo, kukaa kwao kimia ina maana halina nguvu, mle ndani kila kitu wamechukua alama za mikono, wamepiga picha kila kitu …’akasema

‘Kama ni hivyo basi kwanini wananishikilia mimi, sina makosa, unaonaeeh, hawana nguvu ya kunishikilia mimi, pambana nipate dhamana yangu nitajua jinsi gani ya kujitetea mwenyewe…’nikasema

‘Aaah, sema sio kukulaumu, ungelipokea simu yangu,..kwanini hukupokea..’akauliza akiniangalia

‘Kupokea,..sikuwa na wakati mnzuri, nilikuwa napambana na muda…ooh, nimekumbuka kitu..’nikasema

‘Sema umekumbuka nini..?’ akaniuliza

‘Nimekumbuka..kuna mtu nilikutana naye akikimbia ehee, kwanini nilipitiwa na hili, yaani hata polisi walipokuwa wakinihoji sikulikumbuka kabisa hili,.., kuna mtu jamani, atakuwa ndio yeye muuaji, kabisa kabisa ndio yeye..’nikasema

‘Mhh…alikuwaje..?’akaguna hivyo na kuuliza.

‘Anaweza akawa ndiye yeye muuaji, ooh, sasa nimekumbuka ndio yeye, tena alikuwa kavalia kofia pana kuficha sura yake, kuna muda aliinu au uso, kunitizama, kiukweli sikumuangalai vyema, lakini, nikimuona tena nitamkumbuka ndio yeye bwana..’nikasema

‘Anaweza akawa sio yeye pia…’akasema na kunifanya nishikwe na mshangao

‘Kwanini..?’ nikauliza

‘Wewe ulimuona sura yake vyema..?’ akaniuliza

‘Hapana..’nikasema

‘Polisi umeshawaambia kuhusu huyo mtu..?’ akaniuliza

‘Hapana, yaani hilo lilinitoka kabisa ndio nakumbuka sasa hivi, nitawaambia,...lakini sasa kiukweli sikuiona sura yake vyema, yule mlinzi atakuwa anamfahamu bwana..hawezi kutoroka kihivyo.....si lazima atakuwa kpitia hapo..kaandikisha au...kwa taratibu za pale huwezi kukwepa, hata ukiandikisha jina la uwongo, sura je... atakuwa ndio yeye, wakambane yule mlinzi vyema…’nikasema

‘Kama watakuhoji tena, sawa waambie tu, ila sizani kama ndio yeye …’akasema na kunifanya nishtuke tena na kumangalia docta kwa mashaka

‘Kwanini…?’ nikauliza

 ‘Kama rafiki yako angelikuwepo, ..tungelisema mengine,kuwa yeye ndiye kafanya hivyo, au katuma watu kufanya hivyo, ...’akasema na nilihisi hasira kwanini haniungi mkono hoja yangu ya huyo mtu niliyemuona anaongea kitu kingine.

‘Huyo mtu bwana ndio yeye,…, anaweza kuwa ndio yeye…kwanini husemi lolote kumuhuu huyo mtu, au..mbona kama vile unamkwepa huyo mtu.., mbona sikuelewi au unafahami kitu hutaki kuniambia…?’nikasema

‘Wewe unasema hukumuona sura yake sio…ukiwaambia polisi kwa sasa watasema unatunga , wewe utamuambia wakili wako huyo mtu alikuwaje...sawa muembie kila kitu..., na yeye atajua jinsi ya kulifuatilia hilo, hata mimi nalifanyia kazi, unanielewa, kwa hivi sasa huna haja ya kuwaambia polisi chochote zaidi ya wakili wako, umenielewa hapo…’akasema

‘Mhh huanimbi kitu kwangu huyo mtu anaweza akawa ndio yeye,...kwanini nililisahu hilo,...'nikasema

'Sawa kumbuka kila kitu, ..jaribu kukumbuka sana...'akasema

'Unajua niliwaambia polisi wanapoteza muda, mhalifu anaweza kupotea hivi hivhi, hapo ningelikumbuka hilo, lakini cha ajabu sikulikumbuka hilo kabisa,..unajua wangelimkamata huyo mtu kwa haraka iwezekanavyo..., tatizo pale nilikuwa nimeshachanganyikiwa ..nikasahau..ooh, atakuwa ndio yeye huyo, polisi wakinipa nafasi mimi nitampata huyo mtu....’nikasema

‘Hiyo ni kazi yao, wala huwezi kuiingilia, kesi kama hii ni ngumu sana, tunatakiwa kuwa wangalifu sana...'akasema

'Lakini umeniamini, eeh, kuwa ndio huyu mtu, au sio..'nikasema

'Yawezekana,..au kuna mtu mwingine pia, huyo mtu kama ndio yeye, unasema alivaaje...?' akauliza.

'Nguo za khaki khaki hivi kichwani kavaa kofia pana..ana mwili wa kishujaa,..kama askari askari hivi...'nikasema

'Umeonaeeh...huyo mtu alifika wakati Makabrasha ameshauwawa, na yawezekana ndio yeye alitoa taarifa polisi..lakini sina uhakika kama ndio huyo uliyemuona wewe, vyovyote yawezekana , muhimu ni kulielezea hilo kwa wakili…’akasema

‘Kasema kuwa yeye alifika kabla ..ndivyo alivyosema na polisi wakamuamini, kwanini wamuamini na mimi wasiniamini...hapa kuna kitu maana yeye alifika kabla yangu au sio...basi yeye awe ndio mshukiwa muhimu, na wala sio mimi..vinginevyo , atakuwa ndio yeye, kwanza wamuhoji, na natamani niwepo wakimuhoji,.’nikasema

‘Ndio hivyo, ila kwa akili ya haraka haraka sio yeye…kama angelikuwa ndio yeye, angelishakamatwa, polisi watakuwa na habari naye,..lakini ngoja tuone,..kila kitu kwa sasa ni muhimu sana...’akasema

‘Sikukutana na mtu mwingine zaidi ya huyo mtu…unasikia, ndio yeye, vinginevyo waniambie ni kwanini wananikamata mimi na huyo mtu anaonekana hahusikia...’nikasema

'Wewe unakamatwa, kwa sababu kwanza ulipatikana kwenye tukio, pili, silaha iliyotumika tatu, vielelezo vilivyopatikana...wana vigezo hivyo, na ya kuwa kama hata sio wewe  wa moja kwa moja, lakini unahusika kwa njia nyingine , wanahis wewe unaweza ukawa kiongozi wa tukio zima..hayo ni maelezo ya mpelelezi, huyo rafiki yangu...'akasema

'Hapana...kuna kitu wanaficha...wana lao jambo, kuna mtu wanambeba, na ningelipata nafasi ya kutoka hapa ningelifahamu hilo...ninawezaje kuwapata watu wangu sasa..'nikasema

'Watu wako mimi siwajui, na..kwa hili, wala usiwahusishe, maana utawafanya wajulikane, au haijalishi wakijulikana..?' akauliza

'Inajalisha, sitaki wajulikane,..ok, nimekuelewa...'nikasema

‘Kwangu mimi,akili yangu inamshuku sana rafiki yako, lakini najiuliza ni kwanini afanye hivyo, kama Makabrasha ni mwenza wake, wa kukamilisha hicho kilichomrejesha huku, unajua yeye, ndiye kamsaidia mambo mengi hata hiyo njia nyingine ya kumpata mfadhili mpya, mikataba ..nk....kwahiyo Marehemu alikuwa msaada wake,...'akasema

'Msada wa masharti, kiukweli sio kumsemea vibaya marehemu, lakini hakuwa na rafiki wa kudumu, rafiki kwake ni yule anayekidhi haja zake kwa muda huo, nina mashaka hara rafiki yangu atakuwa kaingizwa huko kwa kushinikizwa kinamna fulani,...'nikasema

'Sasa ni hivi kwa taarifa za uhakika rafiki yako alitoweka mapema, na watu wake wanathibitisha hilo…’akasema

‘Alitoweka kwa vipi na akaenda wapi..?’ nikamuuliza

‘Alikuwa kajificha humo humo ndani ya uwanja wa ndege mpaka anaondoka, alikuwa na watu wa usalama aliwaambia kuna watu wanataka kumdhuru, kwahiyo wakamuwekea ulinzi , kwahiyo yeye ana ushahdi kamili kuwa hahusiki, ...’akasema

‘Hata mimi siwezi kumshuku yeye, mimi akili yangu kwa huyo mtu niliyemuona , kwanini alikuwa akikimbia , tena alionyesha kuwa ana wasiwasi , akawa kama anataka kuongea na mimi, akaghairi, ni nani huyo..?’ nikauliza

‘Sio yeye, alitaka kukutahadharisha tu..’akasema

‘Wewe umejuaje hayo..?’ nikauliza

‘Nimekuambia kuwa nimeongea na mpelelezi, anafahamu yote hayo, huyo sio yeye, alifika muda mchache kabla yako na huyo ndiye kakuokoa usishikwe moja kwa moja kama muaji, ila umekamatwa kama mshukiwa wa kufanikisha mauaji hayo, unanielewa sasa, huyo achana naye kabisa,…’akasema

‘Lakini yeye ni nani..?’ nikauliza, na docta akaonekana kama anakerwa na hiyo hali yangu ya kumshinikiza huyo mtu ndio akasema;

‘Ni polisi…ni mtu wa usalama…’akasema

‘Mhh…mbona hukiniambia, ..kwani yeye hawezi kuua...?'’nikaguna bado nikiwa sijarizika na hilo jibu, lakini nikaona niachane nalo ndio nikamuuliza docta;

‘Je rafiki yangu wakati yupo huko na watu wa usalama alikuwa na mtoto wake…?’ nikauliza.

‘Kwa muda  huo hakuwa naye,… mtoto aliletwa uwanja wa ndege baadae sana, kwa kificho, watu wa uwanja wa ndege wamelithibitisha hilo pia....’akasema.

‘Watu wangu hawakuwahi kumuona …alikuwa kajificha wapi..?’ nikauliza

‘Mhhh,...ndio hivyo, yule sio mwenzako hizo ndio anga zake,..na..na.. kwahiyo, inaonyesha kuwa mtoto wake alikuwa sehemu nyingine, na hayo yote ya kuwa mtoto alikuwa ametekwa inaweza ikawa sio kweli...'akasema

'Kwanini..?' nikauliza

'Mimi nahisi alifanya hivyo ili watu wasimuone huyo mtoto, ...unaonaeeh, anajitahidi sana kumficha huyo mtoto na ndio akaamua kutumia mbinu hiyo...kuwahadaa watu, hasa wewe na wengineo wanataka kumuona huyo mtoto…’akasema

‘Mhh kwanini sasa…?’ nikauliza.

‘Hivi wewe hujawafahamu hawa watu, kuna mchezo walioucheza, na huenda mtoto sasa anatumiwa kama chambo cha hayo yote mengine, huwezi jua, ....ila ninachoshindwa kufahamu ni kwanini wamemuue Makabrasha ..’akasema

‘Mhh..’nikagua na yeye akasema

‘Hapo kuna mawili, moja ni usaliti, au kuna kutokuelewana hapo, au pili, kuna maadui wa makabrasha waliona watumie mwanya huo kum-maliza kabisa..labda kwa ajili ya masilahi fulani, lakini ni akina nani hao, hao maadui zake ni akina nani,...maana ukisema maadui zake basi unakwenda kwingine, na hapo ndipo wewe unapoingia kutokana na ushahidi uliopatikana ...’akasema.

‘Mimi ndio naingia, …acha huo utani, mimi sijui lolote na sihusiki, sikuwa na hata na lengo la kumdhuru huyo mtu , kabisa kabisa, japokuwa nilikuwa namchukia…’nikasema

‘Tunajaribu kudadavua tu, najua wewe huhusiki, lakini ni lazima tuone njia zote jinsi ya mtizamo wa polisi, na jinsi gani ya kuzivuka hizo hisia zao, na hasa mbele ya  muhehimiwa hakimu…’akasema

‘Hapo hata sielewi kitu naona kama unanichanganya tu, na hata hivyo hayo yote yatanisaidia nini mimi kwa hivi sasa, muhimu kwangu kwa hivi sasa ni kutoka hapa, kukwepa kwenda jela, sitaki kulala humo ndani, na yaani usiku huo mmoja kwangu ilikuwa kama mwaka,..je huku sasa itakuwaje.…nitachanganyikiwa, naweza kupoteza fahamu…’nikasema nikuna kuna kichwa changu kilikuwa kikiniwasha kwa mawazo.

‘Nakuomba tena sana jitahidi kuwa mvumilivu, nafahamu hali unayopitia, lakini hakuna jinsi, mimi nitajitahidi kadri ya uwezi wangu, ..utatoka tu…vuta subira..’akasema

‘Nivute subira, unajua hali niliyopambana nayo usiku wa jana, sasa sijui huko ninapokwenda kulala leo kupoje, mimi sistahili kukaa sehemu hii, mimi sio mhalafu, na hadhi yangu inaharibika, jingine la kufanyia uchunguzi wa haraka ni kuhusu silaha yangu ilifikaje hapo,au ...'nikasema

'Hilo ndio swali hata polisi wanajiuliza, na ndipo unapowekwa wewe matatani.

'Mimi nahisi huenda wamefanya mbinu tu,..wameua kwa silaha nyingine na hiyo wakaja kuileta baadae, huyo huyo mtu wako unayesema wa usalama labda alitumwa kuja kuiweka,...'nikasema

'Vipimo vitalithibitisha hilo..'akasema

'Kama muuaji sio huyu aliyekuwa akikimbia, basi, ..kuna mtu, kuna mtu kuna mtu, kuna mtu ku-ku......’nikasema huku nikirudia rudia hayo maneno mpaka docta akanishika.

‘Hii inaonyesha kuwa muuaji ni mtu wa karibu sana, anayekufahamu, na anayefahamu wapi unaweka silaha yako, na anafuatilia nyendo zako mara kwa mara...sasa ni nani mtu mwingine anafahamu mambo yako?’ akaniuliza.

‘Mimi sijui, kama angelikuwepo rafiki yangu ningelisema ni yeye, lakinji huyo yupo mbali kabisa na tukio hili, au sio, mwenyewe umelithibitisha hilo, sasa anayebakia ni nani, ni mume wangu, hapana, mume wangu ni mgonjwa...sasa ni nani mwingine,labda nikushuku wewe...’nikasema.

‘Hahaha, nishuku tu, ....lakini...mimi nina ushahidi na wala usipoteze muda wa kunifikiria mimi,, ...anyway, tuyaache hayo kwasasa, muuaji atapatikana tu, ila cha muhimu kwa sasa ni dhamana yako....hili ndilo tulipe kipaumbele, na unafahamu mambo ya nchi yetu, ikishindikana, tutatakiwa kupenyeza rupia, hilo ujiandae nalo....’akasema.

‘Utaweza hilo,...mimi sijali gharama, ila kuwe na uhakika na kila unachokifanya isije ikawa janga jingine, sitaki kufanya makosa juu ya makosa,..kama huwezi hilo nimtafute mtu mwingine wa kukusaidia, nina watu ninaweza kukuelekeza wakatoa huo msaada hadi dhamana ikapatikana, angelikuwepo rafiki yangu hii ingekuwa kazi rahisi sana....’nikasema

‘Nimejaribu kila njia, hayo unayoyafikiria wewe nimeshayafanya, nimeshakuambia nina rafiki yangu wa kushibana, yupo ndani ya mtandao wa serikali, hana shida, na kama kuna uwezekano wowote angelianiambia, nimeongea na mkuu wa upelelezi, na  huyo mkuu wa kituo ambaye anafahamiana sana na baba yako, wamesema kwa leo hutaweza kupata dhamana, maana hayo ni mauaji, ila watahakikisha unakaa sehemu salama, ..’akasema.

‘Eti nitakaa sehemu salama, toka lini Jela kuna sehemu salama.....nikitoka humu, nitahakikisha huyo muuaji namtafuta mimi mwenyewe, na wote wanaohusika na hili nitahakikisha nawawajibisha,...siwezi kuingia matatani kwa sababu ya tamaa za watu wengine, najua kabisa haya yote ni kwasababu ya mali zangu, kwanini wasitafuta mali zao....’nikasema kwa hasira.

‘Pole sana mpendwa,…ni zaidi ya hilo unalolifikiria wewe, lakini kwa hivi sasa sio rahisi kujulikana kirahisii hivyo, na hata likijulikana, sio rahisi kulitetea kiushahidi..ila nakuahidi kitu kuwa mimi najitahidi sana, na nitahakikisha kesho hulali hapa, ila kwa leo, nakuomba uvumilie tu…, tuliza kichwa chako...’akasema.

‘Huna maana kabisa, kulala hapa ni kuniharibia afya yangu hadhi yangu na hii sasa ni kashifa, ndicho wazazi wangu walikuwa hawakitaki…nasikia waandishi wa habari wameshaipata taarifa na walitaka kuja kunihoji,…sitaki kuonana na hao watu kabisa…’nikasema

‘Nitajitahidi kuwaeleza walizuie hilo, mengine niachie mimi..’akasema

‘Na jingine nisingelitaka wazazi wangu pia waje huku, ..nafahamu hili limeshafika kwao, fanya ufanyavyo wao wasije hapa kabisa, na je mume wangu ana taarifa?’ nikauliza.

‘Sina uhakika wa hilo, sijaongea na mume wako bado, ila nijuavyo mimi hali yake inandelea vyema tu.., lakini kwa wazazi wako, …ni vigumu kidogo, hawawezi kukaa tu, ngoja tuone..hayo niachie mimi..’akasema.

‘Kama mume wangu atataka kuja huku kuniona mzuieni kabisa, sitaki kuonana na yeye, kiujumla sitaki kuonana na watu wangu wa karibu,...zaidi ya wewe na wakili wangu, basi...’nikasema.

‘Wakili wako atakuwa  keshafika, mtaonana naye leo hii hii…’akasema

‘Sawa huyo ni muhimu kwangu…’nikasema na docta akaondoka akionekana mnyonge zaidi hata zaidi ya mimi. Na hapo nikajua hali sio rahisi, hali iliyopo mbele yangu ni ngumu,..sijui itakuwaje kwa wazazi wangu, ikizingatiwa kuwa baba ndio yupo kwenye kampeni..


WAZO LA LEO:  Tunaweza kujitahidi kuwa na tahadhari za kila namna, za majanga, za kashfa za maradhi na mitihani mingine tu, lakini kwa lile lililopangiwa kukupata, hata ufanyeje, litakupata tu,..muhimu tukumbuke mola ndiye mpaji, na ndiye anayefahamu ya ghaibu, mengine ni kujitahidi tu. Lilipangwa kukupata litakupata tu. Tumuombe mola atulinde, atusaidie, atuongeze kwenye njia sahihi, na kutuepusha na mabaya yote kwa mapenzi yake.

Ni mimi: emu-three

No comments :