Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, December 14, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-40



Sikuamini, sikutarajia kuwa siku moja na mimi nitaionja jela, mtoto wa muheshimiwa, familia ya kitajiri,  pamoja na elimu yangu yote, pamoja na ujanja wangu wote…, pamoja na sifa ya familia yangu, hayo yote hayakusaidia kitu, ...nikajikuta na mimi naingia ile sehemu niliyoifahamu mimi kuwa ni sehemu ya wahallifu, ....

‘Jela….’

‘Siwezi kwenda jela mimi, kwa kosa gani, ..’nakumbuka siku moja nilikuwa nabishana na rafiki yangu  nikamwambia hivyo, ....ilikuwa tunaongea mambo yanayofanana na  maswala ya jela, na yeye akaniambia, katika dunia hii huwezi kujithibitishia moja kwa moja kuwa huwezi kuingia jela, maana hujafa hujaumbika lolote laweza kutokea

‘Kwanini niende jela wakati natii sheria, nijiepusha na makosa, maana mpaka mtu uende jela, ina maana umetenda makosa makubwa, au sio…’nikajitetea hivyo.

‘Unaweza ukajitahidi hivyo, unaweza ukajihakikishia hivyo, lakini ukumbuke una watu wapo chini yako, wenye kaliba tofauti tofauti, pia wewe mwenyewe unaweza ukajitolea kufanya jambo kwa huruma zako,.., kumbe unajipeleka kwenye makosa bila kujijua...’akasema

‘Lakini hapo sheria si ipo, nitajieleza, au sio…?’ nikasema

‘Inaweza ikatokea bahati mbaya sio wote waliopo kifungoni wana makosa kwa asilimia mia..wengine ni hiyo bahatio mbaya tu, au dhuluma tu za watu wenye masilahi yao…’akasema

‘Mhh, mungu aniepushia na hiyo bahati mbaya....’nikasema.

**********


‘Unashikiliwa kwa kosa la mauaji ya Makabrasha…’sauti hiyo ilijirudia sana kichwani mwangu

‘Mimi sijamuua Maka-brasha…’nilijitetea lakini haikusikilizwa.

***********

Nikakumbuka jinsi polisi walivyonikamata…

‘Simama, upo chini ya ulinzi….’ilianzia hapo, wakati huo natetemeka nimeshikilia mdomo kukwepa nisiendelee kupiga kelele..

Waliingia askari polisi wakafanya upekuzi wao, baadae wakanijia na kusema;

‘Tuambie ilikuwaje..’akaanza huyo askari

‘Mimi sijui, niingia hapa kama nyie, nikamkuta hivyo hivyo..’nikasema

‘Ulikuja kufanya nini usiku, huu ni muda wa kazi..?’ akaniuliza, na mimi nilitaka kumjibu kijeuri kuwa kama sio muda wa kazi yeye alikuwa akifanya nini ofisini, lakini muda kama huo ilitakiwa niwe mpole.

‘Kuna mtu nilikuwa namtafuta, na niliambiwa yupo hapa, nilipofika ndio nikamkuta huyo mtu yupo hivyo..’nikasema

‘Madam inabidi tukushikilie kwa utaratibu wa kipolisi, wewe utaisaidia polisi kwa vile umepatikana hapa kwenye tukio, kwahiyo unakuwa mshukiwa namba moja wa kifo cha Makabrasha....’nikaambiwa

‘Eti nini, ....’nikang’aka!

‘Ndio hivyo, tafadhali tulia pale, kila maelezo yako hapa yatachukuliwa kwa mujibu wa sheria…’nikaambiwa sasa kwa sauti kama vile mimi ndiye muuaji.

‘Mimi sio mhalifu, kwanini hamtaki kunielewa, nimeshawaambi kuwa nilifika hapo ofisini kwa Mkabrasha, nikimfuata rafiki yangu, ambaye nilihisi yupo matatani, na nilipoingia humo kwenye ofisi ya Makabrasha nilikuta kama mlivyomkuta nyie,sijui lolote zaidi, tusipoteze muda, mhalifu anapata mwanya wa kutoweka ..’nikasema

‘Sawa, hatupotezi muda hapa, tunafanya kazi yetu, na sio sisi tu wapo wengine wanafuatilia kila mahali kuhakikisha mhalifu aliyefany akitendo hiki anapatikana, kama ni wewe au yoyote yule..’akasema

‘Mimi nina ushahidi waulizeni walinzi, huko chini nilipita bila hata silaha, walinzi wake walinikagua, mimi sijui aliuwawaje huyu mtu, kama ni kosa lianzie kwa hao walinzi, silaha ilipitaje ...’nikajitetea.

‘Usiwe na shaka hayo yote yatafuatiliwa,…’akasema na mara akatupa macho chini akaiona ile bastola, mimi nilishaiona , niliiona wakati ndio wanaingia na kuamrisha kuwa niweke mikono chini, lakini sikuweza kufanya kitu, bastola ilikuwa karibu na migu yangu imefunikwa kidogo na kitu sio rahisi kuiona kwa haraka, na hata wakati wanakagua walikuwa hawajaiona, sasa kaiona huyu polisi.

‘Hii bastola ni ya nani?’ akaniuliza akinionyesha ile bastola, ikiwa karibu sana na miguuni yangu, wengine wakaiona wakaja wakapiga picha,...baada ya tukio hilo, polisi akiwa na tahadhari, akaichukua alikuwa kavaa kinga, akaikagua na wakati anafanya hivyo na mimi ndio nikapata mwanya wa kuikagua..!

Pale pale nilihis moyo ukilipuka , bastola, ilionekana kama yangu,..lakini nina uhakika bastola yangu ipo kabatini, sizani kamaa hiyo silaha ni yangu;

‘Mimi sijui..itakuwa labda ya huyo mhalifu au ya huyu huyu marehemu, ni kwanini unaniuliza hivyo, mimi sikuingia na silaha humu ndani..’nikasema

‘Hii bastola ilikuwa miguuni mwako, au sio, ina maana uliidondosha wakati tunaingia au sio..wewe unamiliki bastola..?’ akaniuliza

‘Ndio…namiliki bastola lakini mimi sijafika na bastola humu ndani,..’nikasema

‘Hebu iangali vizuri hii silaha, haiwezi ikawa ni yako..?’ akaniuliza

‘Kwanini unaniuliza hivyo, mimi sijaingia na bastola humu ndani, na …nimeiona wakati maningia, sikuwa nimeiona kablsa..’nikasema kwa ukali.

‘Nimekuona ulivyobadilika baada ya kuiangalia hii bastola, na hisia zangu zinanituma hivyo, kuwa hii silaha unaifahamu, tuambie ukweli, hii bastola ni ya nani..?’ akauliza kwa sauti ya ukali

‘Nimkuambia mimi sijui…usinilazimishe kwa kitu ambacho mimi sikijui,..’nilisema Kiukweli ningekuwa nimeiona mapema, nisingelisimama karibu yake, au ningeipiga teke iende mbali na migii yangu..na mbona hiyo bastola inaonekana kama yangu wakati bastola yangu ipo nyumbani.

‘Na kwanini umevaa hizo gloves mkononi..?’ akaniuliza

‘Ni kawaida yangu, hata nikiwa ofisini wakati mwingine unaweza kunikuta hivi hata nyumbani kwangu ni hali niliyojijengea ya kujihami, kiafya..’nikasema.

‘Umesema unamiliki silaha, …si ndio?’ akaniuliza

‘Ndio…’nikajibu

‘Na una uhakika kuwa silaha hii sio hiyo silaha yako unayomiliki…maana tutakwenda kuhakiki…?’akasema

‘Mimi nina uhakika kuwa silaha yangu ipo nyumbani..’nikasema

‘Silaha yako ni aina gani..?’ akauliza akiwa kaishikili hiyo bastola sasa wakihifadhi kwenye mfuko wa plastic, ni baada y akupiga picha sehemu ilipokuwepo na baadae wakaipiga picha bastola yenyewe ikionyesha namba zake.

‘Ni bastola..nikama hii..lakini…’hapo nikasita nikiichunguza vyema, lakini sikuishika

‘Aaah, kumbe unajua eeh, huku unajifanya hujui, kumbe hii ni bastola yako eeh, ....’akasema.

‘Nimesema inafanana..’nikasema

‘Sisi ni lazima tuchukue maelezo yako yote haya, na uweke sahihi …’akasema

‘Siwezi kufanya hivyo, kwa vile mimi nina wakili wangu, sitafanya lolote kwa hivi sasa mpaka afike hapa ..’nikasema

‘Wewe umesema huna kosa, wakili wa nini..?’ akaniuliza

‘Ni haki yangu kufanya hivyo, ..wakili nimemuajiri wa nini..’nikasema

‘Hebu muweke pingu…’akasema huyo askari, akimuarisha mwenzake.

‘Kwanini mnanivalisha pingu, mimi sio mhalafu, niacheni ..siwezi kuvaa hiyo pingu mnanielewa ...’nikalalamika, na yule kiongozi wao, akaniangalia kwa makini na kuonyesha uso wa kushangaa, halafu akasema;

‘Mwacheni msimtie pingu, nimeshamfahamu huyu mwanamke, wewe si ndio yule tajiri wa kampuni ya…, ile kubwa inatwaje vile...na baba yako ni…ok, ni wewe eeh?’ akaniuliza huku akijaribu kufikiria na mimi sikutaka kujulikana kwa watu,nikasema;

‘Nimeshawaambia kuwa mimi sijui lolote kuhusiana na hili, ....’nikasema huku nikikwepa kuangalia pale alipolala Makabrasha, na niliona nisipokuwa mwangalifu , nitazalilika, tajiri mkubwa, …

Tajiri mkubwa, leo kakamatwa kama mhalafu, je vyombo vya habari vikifahamu hili itakuwaje, nikajaribu kuwazia jinsi gazeti litakavyoandika, kwa maandishi makubwa wakikolzea uwongo, ili tu gazeti linunuliwe, ...na kama wakiniona nina pingu mkononi, watanipiga picha na kuiweka ukurasa wa mbele, hapana, ....hapana....

‘Twendeni huko kituoni kwenu mimi nitaongea na mkuu wenu....’nikasema kwa kujiamini.

‘Hamna shida mama, huko tutakwenda lakini kwa hivi sasa tuna kazi ya kufanya, kama hutaki matatizo, subiri hapa, tumalize kazi yetu, ukileta matata, tutakufunga pingu...’akasema huyo kiongozi wao, na mimi nilikaa pembeni nikiangalia wanavyofanya,nikatulia kimiya hadi walipomaliza kazi yao, na kuanza kunihoji tena..

‘Mimi siwezi kuongea lolote mpaka wakili wangu awepo, na mtu ninayeweza kuongea naye ni mkuu wenu ,sio watu kama nyie...’nikasema kwa nyodo.

‘Sawa madam, hakuna shida utaenda kuongea naye...’wakasema na kunichukua hadi kituoni cha polisi.., bila ya kufungwa pingu. Nashukuru kuwa nilipotoka pale nje, sikuonana na watu wengi, nilijitahidi kuficha uso wangu, ..sizani kama kuna mtu anayenifahamu au kuona sura yangu.

*********

 Nilionana na Mkuu wa hicho kituo kesho yake, alikuja  na kuniambia kuwa kiutaratibu inabidi nipelekwe Segerea kwa vile mimi ni mshukiwa wa mauaji, na hapo kituoni kwao, sio sehemu ya kuweka washukiwa wa uhalifu mkubwa kama huo, wa kesi ya mauji.

‘Lakini mimi sio muuaji, na wakili wangu bado hajafika..’nikalalamika.

‘Sisi kwa utaratibu inabidi tukushike, kama mshukiwa , hadi hapo tutakapothibitisha ukweli wa mauaji hayo, kama huhusiki, utaachiwa huru, kama unahusika, basi sheria itachukua mkondo wake, hizi ndizo taratibu zetu, na kama unasema huwezi kuongea lolote mpaka wakili wako afike, basi utakutana na wakili wako huko Segerea , hatuwezi kukuweka hapa....’akasema mkuu wa kituo ambaye nilipopelekwa hapo kituoni usiku huo niliomba nionane naye, nikijua kuwa yeye ataweza kunisikiliza, lakini wapi...

‘Hamuwezi kunipeleka huko kabla sijaonana na wakili wangu…’nikasema

‘Lakini mwenyewe nasikia umekiri kuwa bastola iliyoonekana mle ndani, ni mali yako,..na hiyo bastola ndiyo iliyotumika kwenye mauji..na pia kuna kumbukumbu za kurekodiwa zilizogunduliwa, zilizoachwa na marehemu zilizokuwa zikonyesha kuzozana kati yako na Marehemu ukimtishia usalama wake, uzuri ni kuwa yeye alikuwa na tabia ya kutembea na vyomvo vya kunasia sauti , na hii itatusaidia sana kama ushahidi.....’akasema mkuu wa kituo.

‘Hayo yalikuwa ni mazungumo tu, unaweza ukaongea kwa hasira, huyo jamaa alikuwa kifanya hivyo kwa mbinu zake, za kuwatishia watu, lakini sivyo kama mnavyofikiria nyie, kama mngelimfahamu vyema huyo mtu, msingalijisumbua kumtafuta muuaji, huyo mtu ana maadui wengi...’nikasema.

‘Kila raia ana haki yake, hata kama ni jambazi, bado atalindwa na sheria hadi hapo itaapothibitika kuwa ni mhalifu,....hayo tuachie wenyewe, ila wewe kama mshukiwa, unastahili kutendewa mambo kadhaa, ili sisi watendaji wa vyombo vya usalama, tuweze kufanya kazi yetu vyema....na kama ulivyosema huenda alikuwa na maadui wengi, na mmojawapo anaweza kuwa ni wewe kutokana na ushahidi tulioupata....’akasema.

‘Kukamata watu wasio na hatia ndio mnajisifia kutenda kazi yenu vyema, muda ule mngahangaika huku na kule mngeliweza kumkamata huyo mhalifu, nyie, mnakimbilia kunishika mimi, na mnampa mhalifu mwanya wa kukimbia mbali au kujificha kabisa...’nikasema.

‘Nikuulize tena, Je silaha iliyopatikana mle ndani, ni silaha yako au sio yako?’ akaniuliza.

‘Sio silaha yangu silaha yangu ipo nyumbani,…’nikasema

‘Unaweza kunitajia namba za silaha yako…’akasema

‘Sijaikariri kwa kichwa…’nikadanganya hivyo, wakati hiyo silaha naifahamu namba yake kwa kichwa.

‘Silaha yako nyumbani inaiweka wapi, ..?’ akaniuliza

‘Naiweka kwenye kabati, na nina uhakika itakuwa huko huko,…’nikasema.

‘Hebu iangalie vizuri hii silaha, , ...na namba yake siunaikumbuka namba yake,..hii hapa iangalie vizuri, ni silaha yako au si yako?’ akaniuliza, na mimi nikaiangalia kwa makini, ilikuwa ni silaha yangu, kulikuwa na alama yangu, hakuna ubishi, nikasema;

‘Inaonekana kufanana na silaha yangu,  lakini ili nirizike mpaka nifike nyumbani ....kwani inanipa mashaka, ni nani aliyeweza kufungua kabati langu la siri, na kuichukua hiyo silaha,...siwezi kuhakikisha hilo, mpaka nifike nyumbani nione wa macho yangu...’nikasema.

‘Mama, kila mtu anapopewa silaha, wengi wanazikariri nambe zake, nah ata kuweka alama ya siri, hii silaha ni yako au sio ya kwako?’ akaniuliza.

‘Jibu langu ni hilo hilo, inaweza ikawa ni silaha yangu, siwezi kukataa, maana namba japokuwa sikumbuki vyema, lakini inakuja kuja kama namba yangu, sina uhakika…’nikasema

‘Tungelipenda utoe ushirikiano, kama kweli wewe sio mhaifu, ukizidi kutudanganya ndivyo utakavyozidi kushukiwa, hata kama huenda sio wewe uliyefanya hayo mauaji..’akasema

‘Nimesema hivi, hiyo silaha inafanana kama silaha yangu, lakini silaha yangu ilikuwa kwenye kabati, naona ajabu imefikaje hapo, hiyo sio silaha yangu, ni kufanana tu….’nikasema na huyo mkuu akacheka kuonyesha kuwa mimi najaribu kudanganya.

‘Kama ni silaha yako, imefikaje kwenye tukio la uhalifu,..hebu tuambie ni nani mwingine anayefahamu wapi unapoiweka hiyo  silaha yako?’akaniuliza.

‘Mume wangu, lakini yeye ni mgonjwa...yupo hospitalini.’nikasema.

‘Na kwahiyo anabakia wewe mwenye kuweza kujua wapi silaha ilipo na kuichukua na kuitumia, kwa hali kama hiyo inabidi tusikuachie, na dhamana yako itakuwa ngumu kupatikana...’akasema

‘Mnafanya kama kunikomoa au..?’ nikauliza

‘Kwanini tufanye hivyo,…ila usijali sana bado tunafanya uchunguzi wa kina, kuthibitisha hilo, kama risasi iliyomuua marehemu imetoka kwenye hiyo bastola, kwa ujumla mama una kesi ya kujibu, ...’akasema kwa upole

‘Niitieni wakili wngu, siwezi kuongea zaidi..’nikasema

‘Ni kwanini ulikuwa umevaa kinga za mikononi,…?’ akaniuliza

‘Ni kawaida yangu kuvaa hivyo, ninapokwenda sehemu nisiyokuwa na uhakika nayo, kiusalama na kiafya..’nikasema

‘Ni kawaida yako…ina maana una uzoefu na mambo hayo…’akasema kwa upole

‘Kwahiyo nyie mlitaka niseme uwongo, kuwa silaha sio yangu au?’ nikawauliza kwa ukali.

‘Ukweli wako ndio unaoonyesha kuwa wewe unaweza kuwa mshukiwa wa maujai hayo..na vielelezo vilivyopatikana kwa muda mfupi vinathibitisha hivyo, ili kuokoa muda, ungetuambia ukweli wote kuwa wewe ulimuua huyo jamaa kwasababu kadhaa, kama hasira au kisasi, na sisi tutaona jinsi gani ya kukusaidia,....’akasema huyo mkuu wa kituo, na wakati huo alikuwepo mpelelezi aliyenikamata

‘Sijafanya hivyo hamnielewi, sikuwa na haja  yoyote ya kumuua Makabrasha, na sikuwa na silaha ningelimuuaje, angalieni na muda wa mauaji , mimi nilifika yameshafanyika, ...nyie naona hamtaki kujisumbua kumtafuta huyo muuaji, na naona hamtaki kunielewa,  naona tumsubiri wakili wangu, sitaki tena kuongea lolote....’nikasema.

‘Sawa lakini mwisho wa siku ukweli utadhihiri...’wakasema.

******

Baadaye alifika mkuu wa upelelezi akawa anaongea na mkuu wa hicho kituo, na huyu mpelelezi, wakawa wanaonyeshana vidhibiti, ikiwemo hiyo silaha, na soksi za mkononi,…na ushahidi wa vyombo vya kunasia sauti walivyovipata kwenye nifa vya Makabrasha, na baadaye wakasema kuwa inabidi mimi nipelekwe Segerea huku uchunguzi ukiendelea kufanyika.

‘Mimi Siwezi kwenda huko Segerea kwa kosa gani....?’nikalalamika.

‘Utakwenda tu …hakuna ubishi, sisi tunatimiza wajibu wetu ....’akasema huyo mkuu wa kituoa. Na hapo nikawa sina la kufanya,ikabidi nitii amri, na baadae wakaniingiza kwenye karandinga, eti kama mshukiwa wa mauaji, hadi huko Segerea.

Ndio ikawa mara ya kwanza kuingie jela…usiombee hili likukute jamani jela sio seehmu ya mchezo, hata ukiitwa mahabusu,…sikuona tofauti ya mahabusu na mfungwa wote tulichanganywa humo..

Itakuwaje sasa

WAZO LA LEO: Ni kweli Jela ni kwa wakosaji, lakini je ni wote wanafikishwa huko wana makosa. Kuna ambao wanafikishwa huko kwa sababu tu ya kutetea haki, wengine kwa chuki binafsi, je hawa ni nani atakuja kuwalipa haki zao. Huu ni mtihani mkubwa sana kwa wanaoshika dhamana hii, na mtihani zaidi kwa yule aliyekutanika na adhabu hii ambayo hakuitenda, na mtihani tena sana kwa wanafamilia wa huyu mhanga.Tumuombe mola atuepushie na mitihani hiyo na wale waliofikwa na mitihani hiyo mola awape subira na awajalie waweze kuishinda mitihani hiyo na haki iweze kutendeka. Aamin

No comments :