Alikuwa ni baba….baba ananipigia simu…nikawa najiuliza kuna nini tena...kwa pale ilikuwa sio vizuri kupokea simu, labda nitoke nje, nikamuangalia docta, docta akawa haniangalii,...na simu ikaita mpaka ikaacha yenyewe...
Haikuita tena...tulishaingia chumba alicholazwa mgonjwa na...nikawa nasita kidogo, na docta, akanigusa begani, nikageuka kumuangalia.. akaniashiria nisogee, nitembee kuelekea kule kwenye kitanda….alipolala mgonjwa.
Mapigo ya damu yalikuwa yanakwenda kwa kasi, ni kama nina wasiwasi, au kuna kitu kinakuja kutokea, ...sijui kwanini niliwaza hivyo...
Mume wangu alikuwa kalala kwenye kitanda huku akiwa kanyooka
kabisa, na ilionekana kama kawekewa vyumba pembeni ili asitingishike,..lakini
tofauti na ilivyokuwa mwanzo, safari hii kitanda kilikuwa kimeinuliwa kidogo,
ili yeye kuweza kulala kama vile ameinuka sehemu ya begani na kichwani…
Nikasogea,…nilimchunguza, nikagundua kuwa, shingoni alikuwa
kavalishwa, plastiki la kuzuia shingo isicheze cheze, na jinsi alivyowekwa ni
kama mtu kakaa mwenyewe kimtindo. Na pale alipokuwa kalazwa, aliweza kuangalia
mlangoni, kwahiyo tulipoingia tu, alituona.
Rafiki wa mume wangu yeye akawa kasimama, nilijua alifanya hivyo,
ili kunifanya mimi nitangulie mbele yake, yeye akawa anakuja taratibu nyuma
yangu, huku akinigusa kwenye mkono, kuniashiria kuwa nisogee pale alipokuwa
mume wangu , na hata ilifikia hatua ya kuninong’oneza akisema;
‘Nenda pale kitandani kamsalimie mume wako,....mpaka
nikifundishe,..., na kumbuka niliyokushauri .....’ nikaelewa ana maana gani,
nilisogea huku macho yangu yakiwa yanamwangalia mume wangu.
Kwa pembeni karibu na ofisi ya docta, walisimama madakitari wawili
wakihakikisha kila kitu kinakwenda salama, na mmoja wapo alikuwa dakitari wake
bingwa wa maswala ya mifupa, alikuwa kashika makabrasha yake akimuelekeza
msaidizi wake ni nini cha kufanya baada ya hapo....
Mimi sikuwa na haja na watu hawo kwa muda huo, mawazo na
akili yangu ilikuwa kwa mume wangu, na
macho yangu yalikuwa yamelekea pale alipo mume wangu, na nikawa namsogelea huku
tumetizamana machoni.
Macho yangu na ya mume wangu yakawa yanaangaliana, kwanza niliona
usoni kama anashituka,au kama ananishangaa kuniona, na baadaye mdomoni
akaonekana kutabasamu, lakini niliona kama tabasamu la kulazimisha,..lakini
kadri tulivyokuwa tukimsogelea ndivyo lile tabasamu lilivyozidi kuongezeka, na
sasa likawa tabasamu halisi, na alikuwa wa kwanza kutamka neno.
‘Hatimaye mke wangu umefika...’akasema.
Na kauli hii ilinifanye
nigeuke kumwangalia rafiki wa mume wangu , ambaye alikuwa nyumba yangu kama
vile wafanyavyo walinzi, nahisi aliogopa nisije nikaongea jambo lisilotakiwa
kwa wakati huo.
Kiukweli sikuwa nimependa jinsi anavyonifanya, nakuwa sina uhuru
wa kuongea, lakini kwa namna nyingine niliona ni bora iwe hivyo, maana
ananifahamu vyema, sina uvumilivu wa kumezea jambo, kama ni jambo la kuongewa,
ni lazima litaongewa tu, sipendi kunyamaza nyamaza.
Nilimwangalia mume wangu huku nikitabasamu , lile tabasamu
la kimodo, ili tu mume wangu aone kuwa nampenda, namjali, na sina
kinyongi naye, kwakweli kwa hali ilivyo, tabasamu hilo lilikuwa kama la
kubandikwa mdomoni, lakini nilijitahidi kuliigiza ipasavyo…
Nilipogeuka kumwangalia rafiki wa mume wangu, nilimuona naye
akitabsamu, kama vile ananionyeshea kuwa na mimi nitabasamu hivyo hivyo,na
akawa ananionyeshea ishara kuwa nisogee mbele karibu sana na mume wangu. Nami
nikasogelea kile kitanda alicholala mume wangu , na kumuinamia..
Kwa ujumla mume wangu alikuwa amepungua sana, na hali hii ya
kupungua, kukonda ilianza kujitokeza hata kabla ya hili tatizo, na baada ya
hili tukio, nimeona kapungua kwa haraka sana, hali hii imezidi kumfanya akonde
zaidi, hata mashavu, yalishaonyesha kubonyea, moyoni nikasema akipona tu
nitahakikisha mashavu yanakuwa dodo...ni lazima nimrejeshe kwenye
hali yake ya kawaida....
‘Nimefika mume wangu unaendeleaje?’ nikamuuliza nikiwa
nimemkaribia, na kumuinamia nikambusu kwenye paji la uso, yeye akaguna kidogo
na kusema;
‘Mhh, hata sijui niseme nini, kuwa sijambo au naumwa, mwenyewe
unaiona hi hali niliyo nayo, maana hapa nilipo ni kama nusu mfu, mwili wote sio
wangu tena, kama unavyoona, mwili wote chini hauna kazi,ni kama sio mwili
wangu,....’akasema akionyeshea kwa ishara.
‘Utapona usijali..’nikaema
‘Unajua, eti wanasema ni swala la muda, lakini kwa hali kama hiii
....dakika,saa , siku ni kama mwaka, nateseka sana mke wangu,sijui hii ndio
adhabu yenyewe, mungu wangu nisamehe sana.., nimekosa, sitarudia
tena.....’akawa anaongea na mimi nikawa namwangalia tu.
Kiukweli macho yake yalionyesha huruma, na alivyokuwa akiongea,
hata ingelikuwa nani angelimuonea huruma, …pale nilipo huruma ilinishika, na nilihis machozi yakianza kunijia, nikakumbuka
maneno ya docta...
‘Hakikisha humuonyeshi mume wako kuwa anaumwa sana, zuia kulia,
jenga tabasamu la kumuonyesha kuwa hajambo...muonyeshe kuwa hali aliyo nayo ni
ya kawaida tu...’
‘Mume wangu mbona umeshapona tu, ..hatua uliyofikia ni kubwa sana,
maana ukiona hilo gari lako lilivyoharibika, huwezi kuamini kuwa kuna mtu
katoka hai, lakini mungu wako bado anakuhitajia uwepo dunia, sisi tunaokupenda
tunakuhitajia sana..namshukuru mungu kuwa upo salama, na hali uliyo nayo ni ya
kutia matumaini, cha muhimu ni kufuata masharti ya madakitari...’nikasema.
‘Eti masharti ya dakitari,..masharti gani hayo, hapa nilipo
nitafanya nini cha kuvunja hayo masharti, maana kama unavyoona mwili wenyewe
hausogei, nitavunja msharti gani, kinachofanya kazi hapa ni akili tu...kuwaza
tu, ..haya na huko kuwaza nitawezaje kujizuia, wakati nafahamu fika , kuwa haya
yote yametokana na dhambi ....nimewakosea watu.’akasema na hapo nikageuka
kumwangalia rafiki wa mume wangu, akanionyesha ishara ya kuwa makini.
‘Mume wangu hakuna dhambi hapa duniani isiyoweza kusameheka,kama
umetubu ..mimi nina imani kuwa kila binadamu anakosea, na wewe kama binadamu
huwezi kujiaminisha moja kwa moja kuwa utaweza kutenda kila jambo sawasawa,
....kama ulitetereka, basi ..imetokea na huna jinsi nyingine, cha muhimu ni
kujitahidi kutuliza kichwa chako na mawazo yako ukayaelekeza kwenye kupona, na
wamesema kupona kwako itategemeana na wewe mwenyewe...’nikasema.
‘Mmh, kupona kwangu itategemea na mimi mwenyewe, sijui kwa
vipi,...na wakati nimeshakuambia nimewakosea nyie watu wangu, ..nimewakosea
watu muhimu sana, katika maisha yangu..nimekukosea wewe mke wangu …nisamahe
sana...’hapo akatulia kidogo, na nilipomwangalia machoni, niliona kama
analengwa legwa na machozi, akasema;
‘Mimi nimeshakusamahe mume
wangu…’nikasema
‘Mke wangu umesema umenisamehe, kwanini ulikuwa huji kuniona mara
kwa mara, maana hata kama nilikuwa sina kauli, siwezi kuongea, lakini nilikuwa
naona kila kitu kinachotendeka…?’ akauliza na hapo ikabidi nigeuke kumuangalia
docta.
Docta aliniashiria niwe makini hapo, na kabla sijasema kitu,
akaendelea kusema
‘Unajua.., wote waliokuwa wakija nawaona, lakini wewe sikuweza
kukuona, , nilikuona mara moja tu, siku ile...hali hii inanipa shida na
kunifanya nisiamini kuwa kweli umenisamehe....hivi kweli umenisamehe mke
wangu..?’akasema na alikuwa kama analalamika, na hali hiyo ikanifanya nigeuka
kumwangalia tena rafiki wa mume wangu ambaye alijifanya kama haniangalii mimi,
alikuwa akisoma kadi iliyokuwa imewekwa mezani.
‘Mume wangu, mimi nilikuwa nafuata masharti ya madakitari, kwani
wao waliniambia kuwa huhitajiki kusumbuliwa, na ilitakiwa usikutane na watu
wengine zaidi ya madakitari wako, hadi zipite siku saba, ili uweze kutuliza
kichwa chako... ni masharti niliyopewa mimi, na ndivyo nilivyofanya, sikutaka
litokee jambo la kukufanya usipone haraka...’nikasema.
‘Sio kweli, kama ni hivyo mbona rafiki yako wa karibu mara nyingi
nilikuwa nikimuona akifika hapa...na aliniambia kuwa anaondoka na mtoto, kwenda
kusoma, kwanini aondoke na mtoto bado mchanga, hivi nyie mna akili kweli...’akasema.
‘Alifika akakuambia hivyo..?’ nikauliza nikionyesha mshangao.
‘Ina maana wewe hujui kuwa keshaondoka, ...usinidanganye wakati
wewe ndiye mfadhili wake, mimi sikuona umuhimu wa yeye kwenda kusoma kwa sasa,
wakati ana mtoto mchanga,nilimshauri asubiria kwanza, lakini hakunisikiliza,
nikajua mumepanga wote...’akasema.
‘Haina shida, huko Ulaya unaweza kusoma na mtoto, unaweza kusomea
nyumbani,...hilo lisikutie mashaka, anajua ni nini anachokifanya yeye sio mtoto
mdogo....’nikasema.
‘Kweli Ulaya ni ulaya, lakini mimi namuwazia sana mtoto, yule
mtoto bado mchanga bwana, wewe hulioni hilo..yeye angelisubiria angalau miezi
mitatu hivi, lakini haelezeki, htaaki kusikia, kaamua kaamua basi, rafiki yako
mnajuana wenyewe,....’akasema.
‘Yule niachie mimi, namfahamu sana, ni rafiki yangu, usiwe na
shaka na yeye, alishaambiwa huko mtoto hatakuwa na shida, kila kitu
wamemuandalia....’nikasema.
‘Mimi sina shaka na yeye nina shaka na mtoto, mtoto yule bado
mchanga, safari na hali ya hewa ya huko, mmh, mimi sijui....’akasema na
kutulia, na baadaye akasema;
‘Yeye alikuwa anakuja, anasimama pale mbele kwenye kiyoo,
ananiangalia kwa muda halafu anaondoka, mimi nilikuwa namuona…’akasema na mimi
nikageuka kuangalia kwenye hilo dirisha.
‘Nikawa najiuliza kwanini haingii ndani na mara ya mwisho nikaona niongee na dakitari
ili aruhusiwe aingie, inaonyesha alikuwa ana hamu sana ya kuniona, ..rafiki
yako ni mtu mnzuri, ila akiamua jambo, hapo humuelezi kitu, hajali tena hisia
za wengine..’akasema
‘Mhh, ndivyo alivyo…’nikasema maana naona imekuwa maongezi ni
kuhusu huyo rafiki tu, sikutaka kumkatili.
‘Ila kiukweli kauvunja moyo wangu…kuondoka na mtoto, unajua yule
tumeishi naye, tunamjali sana, kwanini hukumshauri wewe…lakini sawa mwache
aondoke, si atarudi,....’akasema
Hapo nikawa nataka kuongea
jambo, kuuliza maswali, lakini
nikaogopa, nikaona nikae kimiya,maana nilipomwangalia rafiki wa mume wangu
ambaye alikuwa kwa mbele, eneo la kichwani kwa mgonjwa, na alikuwa akiniangalai
moja kwa moja ninavyoongea, akaniashiria nisiseme neno.
‘Mke wangu, mimi inanipa shida sana naona kama wewe hujanisamehe
kiukweli, na nilikuambia ukinisamehe nahis hivyo,..siku ile kweli ulitamka na
ilionekana hivyo, ila kila hatua nahisi kama hujanisamehe..’akasema
‘Kwanini unasema hivyo mume wangu..?’ nikauliza
‘Kama hujanisamehe sizani kama mimi nitakuwa na amani, na huenda
nikarudi kuzimu , unajua nilikufa…ni maombezi tu, kuwa nirudi ili nimalizie
toba, nihakikishe kuwa kila kitu kipo sawa…sasa kwa hali kama hiyo, sioni
umuhimu wa haya yote...’akasema na mimi hapo nikashindwa kuvumilia nikajikuta
nimetamka neno ambalo lilimfanya rafiki wa mume wangu kuniangalia kwa sura ya
kunisuta;
‘Mume wangu mbona hujafanya kosa, kwani kuna kosa gani kubwa la
kukufanya usononeke kiasi hicho...nimeshakuambia kuwa nimekusamehe, japokuwa
sijui kosa gani ulilolifanya...’nikasema na nikaona akishtuka, na kunikazia
macho, nikaona kama anabadilika.
Docta rafiki , akahisi kwa haraka akatoka kule alipokuwa kasimama
na kunisogelea, sikuwa nimemuona, hadi pale aliponishika mkono, nilipogeuka
nikamuona yeye akinionyesha ishara ya kuwa makini.
‘Mhh, mke wangu…unasema nini, ..ndio maana nilikuwa na wasiwasi
sana, mungu wangu, ina maana kweli hujui kosa lako ni nini…mmmh,… hapana
usinichekeshe,..ina maana kweli kosa lenyewe hulijui, halafu umekubali
kunisamehe ..haah , kwahiyo ulikuwa wanichezea shere, unaigiza tu, nilijua tu…’akasema
‘Mume wangu mimi najua , kuwa umenikosea kwa yale mambo yetu ya nyumbani,
unakwenda unakunywa, unakutana na wanawake huko..sasa sijui huko mnamalizana
vipi, hiyo ni siri yako,..kama ni hivyo, basi
mimi nimekusamehe ilimradi umefahamu kosa lako ni nini, ila sipendi
kujua zaidi kama, ulipitiliza utajua wewe na mungu wako, ila mimi nimekusamahe,
ni wapiti njia au sio..…’nikasema
‘Oh…kumbe hata kosa lenyewe unasema hulijui, hapana sio wapiti
njia, mimi sikuwa na tabia hiyo…mimi nazungumzia kosa hilo jingine…kwahiyo sio
kweli, niambie ukweli..., au unajifanya tu kuwa hulijui kosa langu, kwa vile
kuna watu hapa, huyu ni rafiki yangu tu…’akasema akimuonyeshea docta.
‘Mume wangu haina haja, yamepita basi…’nikasema
‘Hayajapita, ni lazima unisamehe kiukweli, je hujaongea na mwenzako, mkakubaliana
jambo..au kwa vile hayupo leo hapa,…najua angelikuwepo hapa ingelikuwa ni bora
zaidi, ili alithibitishe hilo…lakini si atakuja tu, nitahakikisha anaongea kila
kitu, hata hivyo mimi sina muda, sijui muda wangu..maisha haya hayana
muamala..nataka niutue huu mzigo...’akasema na kutulia.
‘Mume wangu mimi nimekusamehe, na kwangu afya yako ni bora kuliko,
hayo ya kupita tu, amini kuwa nimekusamehe, nisingelipenda kujua mengine zaidi,
inatosha, unanisikia, wewe tuliza moyo wako ili upone haraka…’nikasema
‘Hapana mimi nataka kauli yako, nijue ukweli wako, je ni kweli
kuwa hulifahamu hilo kosa,… aah..pumzi inakata kwanini docta…ni lazima
niliongee hili leo hii,…niambie ni
kwanini usilifahamu wakati wewe ndiye uliyemtuma kwangu ..?’ akauliza
‘Kumtuma nani…?’ nikauliza na docta akaniashiria nikubali tu.
‘Rafiki yako…’akasema
‘Rafiki yangu …ok, ndio, mara nyingi
namtuma…alikuambiaje…’nikasema
Hapo mgonjwa, akatulia
akionyesha kama anawaza jambo halafu nikaona kama anabadilika, anapata taabu ya
hewa kitu kama hicho, mimi niligeuka kumuangalia docta, na docta wakati huo
alikuwa anashughulika na kitu kingine.
Nikageuka tena kumuangalia mume wangu, akawa yupo sawa, …ila ni
kama anajilazimisha,…akasema
‘Siamini kama hujui kosa langu,..nilijua tu , hukupenda, lakini
unajua tena ulevi..na hapo imekuwa sababu ya madhambi mengi tu….ooh, kwanini
hii hali haitulii, niongee na mke wangu…’akasema akijaribu kuinua kichwa
kumuangalia docta, na docta akamsogelea na kusema;
‘Kama hujisikii vizuri usijilazimishe…’akasema docta
‘Usiniingilie haya docta,..hata kwangu ni mhimu kwangu kuliko
chochote,..huenda nisipate muda tena…’akasema akimuangalia docta. Na docta
akawa kama anataka kumzuia asiendeleee kuongea lakini hakuweza, akaniangalia
mimi huku akionyesha wasiwasi, na kwa muda ule, mume wangu alikuwa akihangaika
kama hewa inamuwia ndogo, lakini aliendelea kuongea.
‘Mke wangu, unafikiri mimi nilipenda kufanya hivyo, ilikuwa kazi
kubwa sana kukubali hayo…, na nilikubali tu kilevi levi, lakini moyo haukutaka,
na ni kwa vile ni rafiki yako, na ni kwa vile kasema mliongea naye ukakubaliana
ila iwe siri,..hapo ukichanganya na ulevi, nikajikuta nimeingia kwenye mtego, ningelifanyaje
hapo mke wangu nakiri kuwa ni kosa maana sikutaka kuhakiki kutoka kwako…’akatulia
huku anaonekana anapata shida
‘Docta….’nikasema
‘Achana na …na huyo do-docta nisikilize mimi..unasikia ,
nisikilize mimi mumeo…’akasema, na mimi nikamuangalia, ndio akaendelea kuongea.
‘Ulevi, mawazo..na kauli
yake, ikanihadaa…unasikia, nasema haya kiukweli…nisamahe tu, najua nimekosea
sana, kwani sheria ya ndoa inanibana,…’akasema na nikaona akizidi kuhangaika.
‘Mhh…sikupenda mke wangu…ndio maana najuta sana, inaniuma sana,
sijawahi na sikutarajia kufanya hilo, nimekuwa mwaminifu kwako mke wangu, wengi
wakiniona nipo na mwanamke wanafikiri vibaya, lakini napoteza nao mawazo tu…’akasema
na kukokhoa, halafu akatulia na nilitaka niongee lakini akaanza kuongea yeye.
‘Rafiki yako, ananiliwaza, tunaongea ananipa faraja, nikamzoea
hivyo, lakini sikuwa na nia mbaya kwake…ila siku , oooh,…ikatokea , hata sijui
ilikuwaje, nashindwa kuelezea, kauli yake ikaniponza,, yaani inaniuma sana,
nilishindwa mke wangu, nikiri kuwa , ooh, nilitaka m-tttt.ooh wa-waaah, aaah..’akashindwa
kuendelea na hapo rafiki wa mume wangu alifika na kumuinamia akamwambia;
‘Rafiki yangu acha kuongeza zaidi, mke wako ameshakuelewa,
hukukusudia kabisa kujiingiza kwenye dhambi hizo, ulishawishika vibaya, kama
ulivyosema, unakumbuka nilivyokuambia, acha kabisa kuongea hayo mambo....ni kosa
na kama ni kosa limeshafanyika, ...basi’akasema…kukawa kimia, mimi nilikuwa
mwili umekufa ganzi
Muda kidogo,akafunua mdomo na kusema;
‘Mke wangu hana kosa,…wewe huna kosa nisitoe kisingizio kuwa kwa
vile..hapana, maana muda wote najizuia,…lakini rafiki yaka…alichosema, kilikuja kipindi
kibaya nikiwa sijitambui…kwahiyo kwa hali kama ile, basi ikawa hivyo, kwahiyo,
nisamehe tu mke wangu….’akasema
Docta akamwambia;-
‘Basi keshaelewa, tulia, sasa lala..au unataka ulazimishwe kulala
kwa madawa…’akaambiwa, mimi kiukweli akili ilikuwa sio yangu, nilikuwa kama
naota ..
‘Sogea pe-pembeni bwana,.. mimi nataka kuongea na mke
wangu…nisipoongea leo, sitaongea tena, unanielewa, nilifunga kuongea, nikiwaza
mengi, nikutubu, nikiwazia ya huyo rafiki yake, hataki kunisikiliza…sasa nipo
peke yangu ni bora kufa tu, maana sitaeleweka, nakutegemea wewe mke wangu, basi…baba
yako, hatanisikia, kampuni,…hata sielewi, ..’akasema.
Na hapo docta akageuka kule
walipo madocta, nahisi alitaka kuwaashiria kitu , lakini wale madocta walikuwa
wameinama wakiangalia kitu mezani.
‘Mke wangu unanifahamu sana, wakati wote nimekuwa nawajibika,
nimekuwa mwaminifu kwa kazi, tukirudi nyumba wewe na laptop na mimi na laptop,
hao ndio wapenzi wetu, haahaa…ni hivyo, basi mimi nikaongeza pombe, kumbe …ndio
imenifikisha hapa…’akatulia
Pale nilipo najaribu kufunua mdomo lakini siwezi, nimebakia
kimwili tu…na yeye akaendelea kuongea;
‘Mhh..sa-sa.., japokuwa wakati mwingine nateseka kama binadamu wa
kawaida, unatamani kitu, unataka mtoto…..unajua tena…inabidi uvumilie, ndoa ni
ndoa..mke yupo, lakini utafanyaje, nisingeliweza kumlazimisha mke wangu…’akasema
na hap akawa kama anaongeza kitu kichwani mwangu, natamani nianza kuonega kwa
jaziba, lakini siwezi.
‘Mke wangu ….kiukweli sikupenda, maana nakupenda sana mke wangu,
na sikutaka kukuumiza mke wangu, japkuwa nilikuwa naumia, natamani, ndio
nikaanza kulewa, kulewa ikawa ni shida, maana ndio imefanya akili ikaharibika…ila
simlaumu mtu, aah, najilaumu mwenyewe dhambi ni zangu, usiponisamehe, basi acha
nikaangamie, unasikia, nisimlaumu mtu, kabisa....’akasema
‘Mume wangu inatosha, sawa nimekuelewa, inatosha, mimi nimekosa,
samahani kwa hilo sitarudia tena sikujua kuwa nakuumiza hivyo, nisamehe mume wangu,
oh…ina maana haah, basi, ..hata, basi, hata..sielewi, inatosha mume wangu, basi
…’hapo sikuweza kujizuia, nikaanza kulia.
‘M-mke -wangu, usilie….najua hujakosea, sikiliza…’akawa
anahangaika kutaka kama kuinuka hawezi..
‘Ohoo, unafanya nini sasa wewe, utamuua mume wako, nilikuambia
nini..’akasema docta akijaribu sasa kufanya lolote kuidhibiti ile hali
‘Mke wangu…mke wangu nisamahe tu…nimeongea hayo kukuonyesha kuwa
sikutaka..ila nili..zidiwa, na kwa vile alisema mlikubaliana, upo radhi..basi, …’akatulia
‘Tulikubaliana nini..…’ hapo nikasema kwa ukali, mpaka docta
akashtuka na kuniangalia kwa macho yasiyoaamini,..haraka akanishika mdomoni
nisiendelee kuongea.
‘Ndio..alisema hivyo..ndio maana nikashindwa,...nikashindwa,....najuta
sana kukubali kufanya hivyo , kwanini nilishindwa kujizuia,mbona wakati wote
niliweza , kwanini safari ile nikashidwa ...nimeumia sana,…nisamehe sana mke
…mke…tamka neno kuwa umenisamehe, niwe huru na mateso haya, aah, aah, aah,….. ’
madocta wakawa wameshafika;
‘Nini tena, hebu,..hebu….’nikasukumwa pembeni, maana pale nilipo
sikuweza hata kuinua mguu.
‘Sogea, sogea, basi hatuwezi kumruhusu kuongea tena, ni vyema
ukatoka nje, ...ngoja tumpe dawa,
anahitajia kupumzika....’akasema
Hapo ndio nikagundua kuwa nimeharibu, nimeshindwa kuvumilia, kama
alivyonitaka docta, badala ya kujenga nimebomoa, nikajua sasa nimeua…mume wangu
akawa bado anajitahidi kuongea, nikasikia akilalamika,
‘Mbona sijamalizana na mke
wangu, sijamwambia, nilichotaka kumwambia...nipeni dakika mbili niongee na mke
wanguuu-uh...’akasema mume wangu, lakini maneno yake hayo ya mwisho yalikuwa
kama ya mtu aliyelewa, na akatulia, kumbe kuna dawa waliipitishia kwenye mpira,
ilikuwa dawa ya usingizi....
‘Mbona inachelewa….’akasema docta akiwa na maana ile dawa ya
kumfanya alale imechelewa kufanya kazi
‘Mungu wangu nimefanya nini....’nikajikuta nimesema hivyo, nikijua kuwa nilishindwa aliyoniambia
rafiki wa mume wangu nikageuka kumwangalia rafiki wa mume wangu, ambaye
alikuwa akibenua mdomo, kuashiria kuwa hakuna tatizo.
Nikageuka kumwangalia mume wangu ambaye alikuwa keshafumba macho,
na madaktari walikuwa wakiendelea kumkagua, na hapo kichwani nikaanza kukumbuka
maneno yake, maana muda ule wakati anaongea kuna muda akili ilikuwa kama
imeganda, sasa maneno yanaanza kujirejea kichwani;
‘Mke wangu, unafikiri mimi nilipenda kufanya hivyo, ilikuwa kazi
kubwa sana kukubali,...kwa vile ni rafiki yako, na kwa vile kasema wewe ndiye
uliyemtuma,
‘Oh, mungu wangu…’nikajikuta nimesema hivyo
Mimi ndiye niliyemtuma, ..aka-aka…sio hivyo, hatukukubaliana
hivyo, kwa mume wangu hapana, hili halipo, kwa shameji yake, nimtume mimi,
haiwezekani, sio kweli , sio kweli, labda kama …rafiki yangu aliamua kutumia
kauli hiyo kutimiza malengo yake…lakini haiwezekani sio rafiki yangu…
‘Au mume wangu hana maana hiyo, labda ana maana ya jambo jingine
labda sio hivyo, mungu wangu, mungu wangu sio kweli jamani…’maneno hayo
nikayasema kwa sauti , na docta akayasikia, lakini wenzake walikuwa
wakihangaika na mgonjwa..
Docta akaniashiria nitulie…hutaamini bado nilikuwa sijaweza kuinua
mguu, nipo pale niliposukumiwa na wale madocta, …miguu haiana nguvu
Na muda huo nahisi kama kuna vitu vimeingia kichwani, maneno ya
mume wangu yanajirudia rudia kichwani;
‘Mke wangu unanifahamu
sana, wakati wote nimekuwa nawajibika, nimekuwa mwaminifu kwako na kazi
yangu,nimekuwa nikijizuia kutenda dhambi yoyote, japokuwa wakati mwingine
nateseka kama binadamu wa kawaida...
‘Oh…mbona sielewi, kuna nini hapa, ina maana ni kweli,…’nikasema
kwa suti ndogo, kama namnong’oneza mtu..
‘Sio kweli, kachanganyikiwa tu mgonjwa sio kweli…’nikasema sasa kwa
sauti, mpaka wote pale ndani wakageuka
kuniangalia mimi.
Docta akanisogelea na aliponiangalia tu, akagundua kuwa
nimeshabadilika na muda wowote naweza kudondoka, ..akanishikilia nikaona
anamuashiria docta mwingine aje kusaidia..akawa anamuagiza kitu, sikuelewa ni
kitu gani.
‘Ina maana ni kweli, aaah, hapana sio kweli jamani …docta niambie kuwa
sio kweli..hana maana hiyo kabisa, eti docta ni kweli jamani...?’nikasema huku
nashikilia kifuani, kiukweli pale nilihisi maumivu makali yalikuwa upande wa
kushoto…nipo kama nimechanganyikiwa.
‘Mke -wangu,wakati mwingine kama binadamu wa kawaida natamani
nitende dhambi, lakini najizuia, naogopa, ...lakini safari ile nikashindwa,...nikashindwa,....najuta
sana kukubali kufanya hivyo , kwanini nilishindwa kujizuia,mbona wakati wote
niliweza , kwanini safari ile nikashindwa....’
Maneno hayo yalijirudia rudia kichwani...yakanifanya niishiwe
nguvu kabisa, kama isingelikuwa ni docta ningedondokea sakafuni, ..
‘Inatosha...haina haja, kumpiga sindano.’akasema docta akimwambia
mwenzake sikujua ana maana gani, na mimi nikawa naongea tu..
‘Umefanya nini na mume wangu, ...mumefanya dhambi gani wewe na
rafiki yangu, ina maana ni kweli ..ina maana ni kweli…hapana sio kweli jamani
haiwezekani kabisa,…
Nikamwamgalia mume wangu ambaye wakati huo alikuwa katulia, kalala,
na akili yangu pale ikanituma kuwa keshafariki…sijui kwanini niliwaza vile…;
‘Ina maana nimeongea vibaya, nimemuua mume wangu. Mume wangu usife
nataka niusikie ukweli wote, jamani…sio kweli jamani, sio kweli, kwanini hivi
jamani..mume wangu usife uje uniambie ni kwanini..’ sasa nikawa naongea kama
mtu aliyechanganyikiwa..
‘Hajafa, tulia, …ukiendelea kuongea hivyo ndio utamuua…’akasema
docta...na muda ule akawaashiria kitu, na mara nikahis sindani
ikipigwa..haikuchukua muda, giza litanda
usoni…lakini kabla sijafunga macho mlangoni nilimuona baba akiwa kasimama, kama
anasubiria kuambiwa aiingie, sijui alifika muda gani ….
WAZO LA LEO: Mambo yakijirudia sana mwishowe watu huja huamini, hata kama ilikuwa sio kweli. Ndivyo akili zetu zilivyo., ni wachache
sana wanaoweza kusubiria hadi ukweli uwe bayana hasa kwa mambo yanayokwanza
mioyo yetu. Tunaweza kujiaminisha kuwa ni kweli, kwa vile tu linaongelewa sana, kwa vile tu mtu mashuhuri kalisema, nk..lakini hatujiuliza kwanza, je ni kweli, je kama sio kweli itakuwaje, na tujiulize hivyo huku tukifanya tafiti yakinifu…bora ya kuwa na subira
kuamini jambo huku ukitafuta ukweli kuliko kukimbilia kuamini halafu ije kuwa sio
kweli..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment