Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 13, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-25



Sikutaka kuondoka kabisa siku hiyo hapo hospitalini, lakini baada ya ushawishi mkubwa wa madocta ilibidi niondoke, maana walisema hata nikikaa hawataniruhusu nionane naye kwani hawajui ni kwanini ilitokea hivyo baada ya kuniona mimi.

Basi baada ya kurejea nyumbani, nikapiga simu kwa rafiki yangu, kabla hata sijamuuliza yeye akatangulia kusema kuwa ile kazi hajaikamilika, kuna vitu bado hajaweza kuvipata kwahiyo nimpe muda zaidi, na mimi sikuwa na cha kumwambia maana mawazo yangu kwa wakati huo yalikuwa mume wangu.

‘Mume wangu hali yake sio nzuri…kwahiyo sawa,…kama wahitaji muda, ..sijui wataka mpaka lini,… ila jitahidi, nakupa siku moja ya ziada,  ufanye haraka iwezekanavyo, maana huo uchunguzi ni moja ya mambo ya kumsaidia yeye mgonjwa..’nikasema

‘Kwani kazidiwa tena zaidi, si ndio hiyo hali ya kutafuta kumbukumbu au…?’ akauliza

‘Hivyo hivyo tu, unasema kumbukumbu, ulipata wapi taarifa hizo…?’nikasema na kuuliza

‘Atapona tu…ilimradi yupo na madakitari…’akasema bila kujibu swali langu, na sikutaka kumuuliza tena.

‘Ndio hivyo, ila kuna kitu kinamsumbua, mimi sijajua anasumbuliwa na nini hasa, hata madocta hawajui tatizo ni nini hasa…walitarajia mimi nitaweza kusaidia..hata sijui nifanye nini,…, ndio maana nilitaka hiyo kazi uimalize kwa haraka iwezekanavyo, unielewe hapo rafiki yangu ni muhimu sana kwangu na kwa mume wangu, nashindwa mimi nifanye nini sasa…’nikasema

‘Sawa nimekuelewa,…ila kiushauri wangu, hata ikikamilika hii taarifa ni bora ukasubiria apone kabisa, kuna mambo mengi, yatamsumbua kichwa ukianza kumhoji ni kwanini, ni kwanini..unanielewa hapo lakini.., hasa ya kazini kwake, na mengine ni wewe na yeye, hakuna zaidi ya hapo, mengine ndio haya sijapata uhakika nayo…’akasema

‘Mimi nikiipata hiyo taarifa nitajua kipi ni kipi cha kuongea naye..je huyo mzazi aliyekuwa akimfuatilia umeweza kumtambua ni nani, maana siku hiyo ya ajali nasikia aliondoka kwenye kikao, akiaga kwenda kumuona mzazi, …sasa ni nani..?’ nikamuuliza

‘Mhh, nani kuambia hayo..ok,…hapo kuna utata, ndio kuna mzazi alijifungua siku hiyo, siku ambayo na mimi nilijifungua, lakini sio mfanyakazi mwenzao, sasa hakuna uhakika wa moja kwa moja kuwa ndio yeye,..unaona hapo, na ni kweli, kuna kipindi cha nyumba mume wako alikuwa karbu na huyo mama,…sasa huwezi kuchukulia hilo kama kigezo, ndio maaana nasema kuna mambo kidogo hayajakamilika hapo

‘ Ni nani huyo…Je huyo mzazi anaweza kuwa mpenzi wa mume wangu , ndio huyo shetani ninayemtafuta mimi au, nataka majibu hayo haraka iwezekanavyo, umenisikia, ..?’ nikauliza kwa ukali kidogo

‘Bado sijaweza kupata uhakika, maana kama nilivyosema sio mfanyakazi mwenzao…lakini sasa, huyo mwanamke ana mchumba wake,…nilitaka...niende kwake,..lakini nimesikia kasafiri jana….ooh, hebu subiria kidogo,..’akasema na kutuli baadae akasema

‘Kuna kitu nafuatilia, ….ujumbe uliingia, lakini sio muhimu,…sasa ni hivi subiria kidogo,leo nahis nitafikia sehemu, nitakuambia …mambo mengine naogopa kutumia watu, kwasababu za kiusalma na siri zetu, unanielewa hapo…’akasema

‘Ok….sawa, nimekuelewa,…mimi  nakusubiria wewe…maana leo nilitakiwa kuonana na baba, kuna mambo ya kuongea naye, muhimu sana..na nilipomueleza hayo mabadiliko ya afya ya mume wangu, akaona tuahirishe hicho kikao, ..na kasema kuna mambo zaidi kayagundua, sasa sijui ni mambo gani…’akasema

‘Kagundua nini, hakusema ni mambo gani hayo, mmh…?’ akauliza

‘Mimi kwa hivi sasa akili haipo sawa, siwezi kujua, hakusema….labda yanaweza kuwa ya kazini kwa mume wangu au hata sijui, nahisi anaona namficha jambo, kawa mkali sana..’nikasema.

‘Unajua baba yako nilionana naye, bahati nzuri sikuwa na mtoto, na kukutana kwetu ilikuwa ni bahati mbaya tu, sio kwa kupanga ilitokea tu, nikiwa nafuatilia jambo fulani nikiwa na haraka kurudi nyumbani, na hakutaka hata kunisalimia, akakimbilia kuniuliza maswali ….’akasema

‘Maswali gani…?’ nikauliza

‘Kwanza alisema kwanini nimeamua kuzaa bila kuolewa,…nikamwambia ni bahati mbaya tu,…akaniuliza haya baba wa mtoto ni nani, ..nikamwambia hilo ni siri yangu,..akaniuliza mambo mengi-mengu tu mfululizo…, nahisi anajua kitu….sijui kajulia wapi mambo mengi ambayo hata sikutagemea kuwa atayafahamu,…rafiki yangu…, tusipokuwa makini, baba yako anaweza kuchukua hatua ambayo hukutarajia, maana keshafahamu kila kitu…’akasema

‘Ndio maana nilikuambia ufanye juhudu za haraka, ili uwahi kuziba sehemu zote nyeti, lakini wewe ukalichukulia taratibu, sijui ulijiamini nini, ujue mimi nina mipaka yangu, na kama kuwajibika kama  baya likitokea, sawa, nitawajibika kama mtendaji, lakini huyo ni baba yangu hawezi kunitupa moja kwa moja lakini nyie je nitawasaidiaje, na ina maana juhudi yangu yote ndio ifike hivyo, inaniumiza sana, kama watu niliowategemea, na lakini sawa....’nikasema

‘Nimejitahidi nilivyoweza, nikaziba sehemu nyingi tu…lakini baba yako kama umjuavyo anaweza kufika kokote bila vikwazo, hata hivyo,..hawajafanikiwa kuupata uhakika wa baadhi ya mambo, ndio maana aliniuliza maswali mengi, kuashiria kuwa hana uhakika,…unajua …mimi nimeshaamua, liwalo na liwe, sasa nitafanyaje .…’akasema

‘Una maana kusema hivyo, liwalo na liwe…?’ nikauliza

‘Sasa rafiki yangu yaliyotendeka, yameshatendeka, utafanyaje sasa hapo…eeh, hebu niambie, wakati mwingine tuangalie mbele, tukirudi kinyume nyume kwa kujiuliza, tutajikuta tupo kwenye lawama sote …na lawama hizo zinaweza kutufikisha kubaya, kama tutajiangalai nafsi zetu tu…na kumbe ilikuwa ni dhamira nzuri tu..lakini sawa, mimi nitakukamilishai huo uchunguzi na uamuzi utakuwa mikononi mwako…’akasema

‘Nataka kufahamu tu, je wao wameshagundua lolote kuhusu baba wa mtoto, maana hilo linaweza kuleta picha mbaya kwangu,..kama..lisemwalo lipo sijui nitauweka wapi uso wangu, lakini kama sio kweli..nataka kumkosha mume wangu..awe huru na shutuma hizi..’nikasema

‘Kwani …mmh, mume wako si yupo, waache apone atasema mwenyewe, kwanini ulaumiwe wewe…’akasema

‘Baba anasema kagundua mambo mengi ambayo kama angelifuatlia awali yasingelitokea na hili limempa fundisho…sasa mimi sipendi hiyo hali ya kuingilia mambo ya mume wangu, …ndio maana nilitaka ukweli kutoka kwako…na hilo la baba wa mtoto wako, lisiwe kama wasemavyo, itakuwa heri sana kwangu, na kwa mume wangu, vinginevyo, sijui baba atachukua hatua gani…’nikasema

‘Unajua hizo shuku shuku zao kuhusu mtoto kama nimezaa na nani…nimemwambia baba yako wazi wazi hayo ni maisha yangu, hayawezi kuingiliana na biashara zake, akifanya hivyo anakosea sana..kwani vyovyote iwavyo hakuna nitakayemwambia baba wa mtoto wangu, na sina lawama na mtu, kuwa labda nitambebesha yoyote majukumu ya ulezi, kwahiyo sipendi watu kuniuliza-uliza hayo maswali …’akasema

‘Sawa , kwa baba unaweza kuongea hivyo, lakini kila kauli yako anaichukulia kwa uzito wake, maana naye sasa hivi keshasikia mengi, …mimi nakupa angalizo tu, uwe makini sana ukiongea na baba, usimchukulie juu-juu, ana lengo lake, unaweza ukajikuta kubaya sana, na anajua ni nini anachokifanya, hawezi kuingilia mambo ya watu bila sababu maalumu…’nikasema

‘Namafahamu sana…najua ni vipi niongee naye, na wapi ikibidi na mimi niwe mkali, maana na mimi nina haki zangu,kiukweli ndio baba yako ni mkali, lakini mimi siwezi kumuogopa tu, ..ninachoogopa ni hatua zake, kuwa labda anaweza kuchukua hatua mbaya zikaumiza wengine bila kujali, na visingizio vije kwangu, hapana kama ni langu aniumize mimi mwenyewe….’akasema

‘Baba anachoangalia ni heshima yake, pili bishara zake, maana heshima ndio inamletea wateja na biashara, na mambo ya kisiasa, hataki kashfa mbaya …Na hilo litakuwa ndio ajenda kubwa kwenye hicho kikao, watakuwepo wakurugenzi wote wa vitega uchumi ambavyo ana hisa navyo,…kwahiyo sio kikao kidogo, ni kikao cha maamuzi,..sasa haya mambo ni mengi na yanatokea kipindi hiki, na wewe ulikuwa msaada wangu mkubwa, sijui, umekuwaje sasa…’nikasema

‘Niliponana na baba yako, alikuwa na mdogo wa mume wako…’akasema

‘Oh yupo yule aliyesafiri au huyu mwingine….kwahiyo wameshaongea, huenda kabanwa na kusema ukweli wote au…?’ nikauliza

‘Ndio, lakini huyo mtu nilishaongea naye kabla na kumuweka sawa, sizani kama anaweza kufungua bakuli lake, nina mambo mengi yake mabaya ninayoyafahamu, anajua kabisa akinisaliti nitamuumbua kwa mkewe.., kaahidi hatasema loloye baya dhidi yangu, usiwe na wasiwasi na huyo mtu….’akasema

‘Una uhakika hataweza kusema ukweli, maana nilipanga kuonana na mke wake…?’ nikauliza

‘Hawezi kusema chochote, …mambo yangu yatabakia kuwa yangu, nina uhakika, hilo litabakia sirini kwangu, hakuna nitayakemuambia nimeshaamua hivyo, mpaka hapo muda muafaka ukifika, , kama ikibid kusema, nitasema…, lakini sizani kama kuna mtu atafahamu siri hiyo,..na unasema unataka kuongea na mke wake unataka kuongea naye nini, …usije ukaharibu…’akasema

‘Hapana…kuna mambo yangu mengine na huyo mwanamke..mambo ya akina mama, unajua nimewekeza huko pia, kwa akina mama, sasa yeye ni mmoja wa wahusika wakuu, na nilitaka nijue yeye anasemaje kuhusu haya yanayoendelea hasa kuhusu huyo mtoto wako,je hamshuku mumewe …’nikasema

‘Hata sijui….lakini kwangu nimehakikisha kila kitu kipo sawa, …mimi nakushauri wewe hangaika na mume wako, haya mengine yaache kama yalivyo,..hiyo taarifa itakusaidia kidogo tu…sizani kama ina lolote jipya…’akasema

‘Unajua nilipokuwa naongea na docta, docta alisema mume wangu anaonekana kama  anataka kuonana na wewe…?’ nikasema, nikahis kama kashtuka na akahema kidogo na kusema

‘Kuonan na mimi, aliongea hivyo au…?’ akauliza

‘Docta, rafiki wa mume wangu ndiye anahisi hivyo…’nikasema

‘Mhh, kuna nini kilitokea mpaka ahisi hivyo, lakini eeh, hata hivyo ni wajibu wangu kumuona au sio , nyie ni kama ndugu zangu, tumeishi nanyi, tumeleleana, shemeji namuona kama ndugu yangu pia, japo,…haya yanayotokea sasa yanaleta kigugumizi, ila …sijui nitafikaje na mtoto,. Si unajua tena, …’akasema

‘Wewe fanya mpango uje uonane na yeye, kama itasaidia,..huyo mtoto isiwe kisingizio, huyo unaweza kuja naye…maana kutokana na docta kuna muda akiwa anaweweseka, alitaja mtoto, kama ingelikuwa ni watoto wake, angelisema watoto, lakini katamka ‘mtoto’…hizi ni hisia zinajengeka, na kumfanya docta ahisi kitu…’nikasema

‘Mtoto, katamka hivyo mtoto, mtoto wa nini, hapana, labda kamsikia vibaya, na hiyo sio sababu ya kuhisi mtoto wangu…sema kwa vile kuna kitu kinatakiwa hapo, lakini hilo lisikusumbue kichwa, ni langu, najua jinsi gani ya kupambana nalo…’akasema

‘Docta analifuatilia hilo kwa karibu na anajaribu kuwa karibu na mume wangu, kusikia kama atapata chochote kutoka kwake…je hamjawahi kuonana na docta ukiwa na mtoto wako…?’ nikamuuliza

‘Hajawahi, labda, ..sina uhakia maana huyu ndugu yangu anayekaa na mtoto angeliniambia…kama aliwahi kuja nikiwa sipo, na mimi sijamuacha mtoto wangu kwa muda mrefu na huyo msaidizi wangu…’akasema.

‘Unajua kila hatua, naanza kuingiwa na mashaka..anyway, mimi nina imani hujanificha kitu,..sijui, maana, umeshasema huwezi kumuambia mtu kuhusu baba wa huyo mtoto wako.., ikiwemo mimi, na kauli hiyo inanifanya nianza kuwaza mengi, ni kwanini hadi mimi unifiche, najiuliza sana…’nikasema

‘Ndio maana naona bora iwe hivyo,…kama mwenyewe umeshaanza kubadili imani yako kwangu, unaanza kupinga hata kauli zako, basi hata mimi naingiwa na mashaka, je mimi rafiki yako naweza kufanya jambo kinyume na kauli zako, aah, kwa hali hiyo, hata safari, sijui itakuwaje….na huenda nikaondoka haraka iwezekanavyo…’akasema

‘Huwezi kuondoka kabla sijaufahamu ukweli. Ujue hiyo safari nimeidhamini mimi mwenyewe, sasa usije kuharibu kila kitu…Hilo la kuujua ukweli, nitalijua tu, nimeahidi hivyo…, umesikia, kupitia kwako au kwa njia nyingine, nitamfahamu baba wa huyo mtoto, umesikia, na nina maana yangu kufanya hivyo…’nikasema.

‘Haah , sawa…lakini ….hebu kidogo…’ na simu ikakatika, nilishtuka kwa kitendo hicho cha kukata simu kabla sijamalizana naye…, sio kawaida yake kukata simu, kihivyo

Kwa vile nilikuwa na haraka, sikutaka kumpigia tena simu, …lakini kitendo icho kilinikwanza kweli kweli….

***********

 Nilifika hospitalini, na nilihitajika kuonana na docta kwanza kama naruhusiwa kuonana na mume wangu.

‘Sawa unaweza kuonana naye, ila docta, jirani yako, yupo huko anaongea naye… NA kumpatia mazoezi kuna huduma nyingine tunataka kumfanyia kidogo huenda ikasaidia..’akasema

‘Kwahiyo sasa anaongea vizuri…?’ nikauliza

‘Ndio ila, kumbukumbu hazijakaa vyema kabisa…kuna muda anajichanganya, na siku ya leo amekuwa akikuulizia wewe, ni mnyonge sana, nahisi wewe utaweza kumsaidia, jaribu sana kuwa naye karibu…’akasema

‘Haya ngoja nikaonane naye, kwahiyo unahisi ana tatizo jingine kubwa…’nikauliza nikiwa na hamasa ya kwenda kuonana na mume wangu.

‘Hakuna zaidi ni hilo, …mengine hatuwezi kuyafahamu kwa sasa, maana hatua kwa hatua anaanza kuimarika, usiwe na wasiwasi kabisa…’akasema

 Basi nikaondoka na kuelelea huko alipolazwa mgonjwa, nilipoingia nilimkuta docta akimfanyia mume wangu mazoezi, nilishangaa kuona hata ile kukaa kama kwanza hawezi, …sikutaka kuwashtua kwanza nikatulia kuwaangalia.

‘Sasa naona upo tayari,…unajua ni muhimu ukajitahidi mwenyewe ungelifanya kama ulivyojitahid kipindi kile ungelipona haraka tu…’akasema docta

‘Hata sijui ilikuwaje, kwani nilijitahidi vipi…?’ akaliza suti yake ilikuwa ya kinyonge ya mgonjwa aliyekata tamaa.

‘Uliweza kukaa mwenyewe kitandani…’akasema

‘Mimi, nilikaa mwenyewe, ….sikumbuki. maana hata mwili siuhisi ni kama vile sina mwili kabisa….’akasema

‘Utakumbuka tu kidogo kidogo,…’akasema docta

‘Hivi unasema kweli ..kuwa Mke wangu aliwahi kuja kuniona, mbona mimi sikumbuki kumuona…’akasema

‘Mbona kila siku anakuja kukuona…’akasema docta

‘Mmhh, kweli nahisi hataki kuja kuniona kwa hayo niliyomtendea, nimemkosea sana, sijui kwanini, nahisi mimi ni mtu mbaya sana, na huyo rafiki yake mhh…’akasema hapo akatulia hakuendeleza neno

‘Usijali,..kosa ni kosa, na ukikosa, ukatubu basi kosa linafutika, ila ukirudia kosa, ujue wewe ni mkosaji…’docta akasema

‘Nimerudia kosa mara nyingi sana..ndio maana nipo hivi…sijui atanisamehe kabla hajchelewa… unahisi atanisamehe, nataka nafsi yangu iwe huru, nina imani akinisamehe, basi, nitapumzika kwa amani, atakuja leo…?’ akauliza

‘Atakusamehe, kwani hujafanya kosa kubwa la yeye kushindwa kukusamehe, makosa ni kawaida ya mwanadamu au sio…’akasema docta

‘Wewe hujui tu…nahisi moyo mwake ananichukia sana, tena sana, sijui kwanini ilitokea hivyo, lakini, hata sijui, nilifanya nini…’akasema

‘Kwani anafahamu kosa ulilomtendea, ni kosa gani kubwa hivyo..?’ akaulizwa

‘Ndio maana hataki kuja kuniona, nahisi keshafahamu, ni kosa kubwa sana, tena sana, lakini sikumbuki, tatizo, nahisi nimekosa, lakini haaa, mbona sikumbuki kitu…’akasema

‘Kosa gani…lakini utakumbuka tu usijali…si hukumbuki, basi ni kosa dogo tu, au sio..au unalikumbuka, ni kosa gani…?’ akauliza na hapo akageuka, wakaniona, na kimia kikatawala.

 Mume wangu aliponiona akaonekana kutokuwa na raha, akawa katulia, nikamsalimia, akaitikia kwa unyonge sana, nikamuuliza anaendeleaje akasema sasa hajambo.

‘Sasa ni kujitahidi kula na mazoezi, na nitajitahid kuja kukufanyisha mazoezi mwenyewe, maana walinikataza awali, sasa najua upo tayari, au sio..?’ nikamuuliza

‘Sawa, lakini ..ulishanisamehe…’akasema hivyo

‘Kukusamehe, mume wangu usiwe na wasiwasi mimi ni mke wako, tunakoseana sana, au sio, kwani wewe si ulishasamehe au sio..’nikasema

‘Lakini wewe hujanikosea kitu mke wangu, wewe ni mke mwema, nimeliona hilo, wewe ni mwema,…’akasema

‘Mh, mume wangu nimeshakusamehe kabisa…’nikasema, nikimtupia jicho docta na docta akaashiria kukubaliana na kauli yangu japokuwa sikufahamu ni kosa gani analolisemea mume wangu.

‘Najua hujanisamehe, niona nafsi yako…unanichukia sana, nakuomba uondoke tu, kama hutaki kunisamehe…’akasema na kunifanya nishtuke na kugeuka kumuangalia rafiki yake.

Docta..alipoona vile..kwanza alitulia, kama ananisubiria mimi niseme neno la kumsihi au kitu kama hicho, na aliponiona nipo kimiya yeye  akamsogelea mume wangu pale alipolala, akamwiinamia na akawa anamsemesha sauti ya chini-chini

‘Rafiki yangu nimeshakuambia, ukitaka usipone haraka, uendelee kujitesa na hayo mawazo yako, mke wako hana kinyongo na wewe kabisa,…. anafahamu kuwa kila binadamu anakosea, na kutenda kosa sio kosa, bali kurejea kosa, wewe kama uliteleza, uliteleza tu kama binadamu wengine,..na umeshafahamu kosa lako, umetubu, au sio ...hiyo inatosha kabisa..mimi nimeshaongea na mke wako, yeye kasema ameshakusamehe.....’akasema.

‘Wewe huelewi tu, .....ninachotaka ni kauli ya mke wangu kuwa amekubali kunisamehe, kutoka moyoni mwake, nafsi yake bado haijanisamehe, naiona kabisa, usimsemee…’akasema

‘Nafsi yake umeuonaje wewe…’akasema docta

‘Naiona,…naiona, naiona. Naiona…’akawa anaongea hivyo mfulululiza mpaka docta akamgusa begani ndio akanyamyaza

‘Mimi najua tu, mimi ni mtu wa kuangamia tu, maana hajanisamehe, ninajua mimi sio mtu kuishi tena, nimepewa muda wa toba, kabla sijafa, niwe nimesamahewa, na mke wangu, lakini mke wangu, hajanisamehe, anaongea tu mdomoni, yeye na baba yake ni kitu kimoja, wanataka niangamie tu,, ....’akasema na kauli hiyo ikanishitua, nikajikuta nikisema.

‘Wewe mume wangu unakazania nikusamehe, nikusamehe,  kwa kosa gani,mume wangu mbona hujanikosea kitu, kama ni yale ya nyumba nimeshakusamehe, lakini sijui kama una makosa mengine,labda uniambia makosa gani hayo,na hilo la baba yangu linatoka wapi,,,.?’ nikauliza na rafiki yake akasema.

‘Tulishaongea hilo na mke wako, kwake sio kosa kubwa sana, ni mambo yanatokea, hasa kwa wanadamu, baba yake alikuja hapa akasema yeye yupo tayari kuangalia unapona haraka, na kama kuna lolote limekwama aambiwe, sasa unataka nini tena..’akasema docta

‘Baba yake au mwingine….hahaha, na akisikia hayo madhambi, si ndio, atanifukuza kabisa,…najua keshayafahamu ila anasubiria kuwa nitapona ili aje kuniumbua, hatawahi kabisa, ila mke wangu, nisamahe jamani, naangamia mwenzako…’akasema kwa sauti ya uchungu kama anataka kulia.

‘Kiukweli pale nilitaka kuongea kwa ghadhabu, maana sijui ni kosa gani, na nimetamka kuwa nimeshamsamehe bado ananisihi, …docta akaingilia kati na kusema

‘Mkeo anakupenda sana, muda wote yupo na wewe, kaacha kila kitu kwa ajili yako, sasa unataka nini tena hapo, keshakuelewa, muhimi ni wewe kupona hayo ya kufikiria kufa , kila mtu atakufa hata akiwa mnzima au sio....’akasema docta na kunigeuka akaniambia kwa sauti chini chini

‘Toa kauli yenye udhabito kuwa umemsamehe, umeshafahamu kila kitu,..tusipoteze muda, kwani hali yake, itaboreka haraka akiwa na moyo wa matumaini,..vinginevyo,…huyu mtu atachanganyikiwa… ‘akatulia kwani dakitari wawili na nesi waliingia wakiwa na vifaa, vikiwemo vyuma, nikashangaa hivyo vyuma vya nini tena .

NB: Mambo ndio hayo, msichoke, maana hapo hospitali ndio tutagundua mengi.

WAZO LA LEO:Fadhila , baraka na rhema kutoka kwa mola wetu ni nyingi sana, je tunazikumbuka, je tunamshukuru, au tunasubiria mpaka tuanza kuwa na hali mbaya ndio tuanze kusema ‘ooh mungu wangu…. tumkumbuke mola wetu tukiwa wazima, tukiwa na uwezo wetu, tukiwa vijana, ..naye atatukumbuka tukiwa na shida.

Tumuombe mola wetu tuwe na imani hiyo, Aamin.
Ni mimi: emu-three

No comments :