Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, October 24, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-13



‘Ajali….’ Ilikuwa kauli yangu ya awali pale nilipozindukana, sijui kwanini hali hiyo ilinitokea,..kupoteza fahamu,…mmh.. nilijiuliza pale bila kujua sababu ni nini,.. labda ni kuchoka tu, mambo yamekuwa mengi kupitiliza…, niliinua uso na kuwaangalia watu , maana walishafika kuangalia kuna tatizo gani, …haikuchukua muda mrafu hiyo hali.

Bahati nzuri, nahisi ni dakitari, alikuja kutokea hapo kwenye hilo jengo la soko-duka, alikuwa kavalia nguo za kidakitari, hilo jengo ni kubwa lina ofisi nyingi na mojawapo ni dispensary. Na kuwa huo  alikuwa kachuchumaa karibu yangu, na akawa ananiangalia tu, huenda alishanichunguza nikiwa nimepoteza fahamu

Mimi kwa haraka nikajaribu kusimama,…nikajikuta narudi chini,.. nilihisi kizungu zungu kidogo, huyo docta akanishika mkono, kunisaidia, nikaa vyema, nikawa najifunika vizuri, kushusha gauni vyema….

‘Upo ok.., unajisikiaje sasa..?’ akaniuliza na mimi nikawa kimia, nikitafakari, kuvuta fikra.

I hope so, nipo ok…’nikasema

‘Mhh, unahitajika kutulia kwanza, naona hali yako bado haijawa sawa, unahitajika mapumziko kidogo, sijaona tatizo lolote kubwa kwako, lakini ni vyema, ukafika hospitali kwa uchunguzi zaidi, hapo ndani kuna zanahati, nahudumia hapo, kama hutojali unakaribishwa...’akasema huyo docta?’ akaniuliza

‘Nipo ok…nahisi hivyo, natumai, hunidai kitu…’nikasema

‘Hamna…sijafanya lolote, nilikukagua tu  Je utaweza kuendesha gari mwenyewe…, au tumpigie mume wako simu,au jamaa yako, simu yako hii hapa, tukusaidie kumpigia…?’ akauliza huku akiwa kashikilia simu yangu, nahisi waliichukua wakitafuta namba ya jamaa yangu yoyote.

‘Hapana….niko ok..’ Ni alipotaja kuhusu mume wangu, ndio akili ikafunguka, nikakumbuka ile simu niliyopigiwa  na hapo hapo kwa haraka nikaingia kwenye gari…

‘Ahsante sana kwa huduma yako,….’nikasema

‘Hamna shida, uwe mwangalifu tu, na nazidi kukushauri fika hopsitali, usizarau hilo laweza kuwa chanzo cha tatizo , na huwezi kulijua mpaka ukapimwe…’akasema huyo docta na mimi nikawasha gari na kuanza kuondoka.

Niliendesha gari langu kutoka eneo hilo, na muda huo sikuwa na wazo la kuangalia vitu vyangu kama vipo salama,..sikuwa na wazo la kuangalia simu yangu ambayo, alinikabidhi huyo docta niliweka pembeni ya kitu,..kumbe simu yangu …ilikuwa imezima..watu wananipigia wanipati.

Nilipokaribia eneo la nyumbani kwangu ndio nikakumbuka kuwa dakitari alisema nipitie kwake,… lakini niliona haina umuhimu kwa muda huo,  kwanza nifike nyumbani kwangu, nijue kinachoendelea,…maana mpigaji simu, nakumbuka  alisema,..

‘Kuna ajali, gari la mume wako limepata ajali, lakini hayupo….haonekani…. , tunahisi huenda kaimbilia nyumbani kwake… watu wanamtafuta haonekani sijui wapi alipo….’nilikumbuka hiyo sauti.

‘Ajali halafu yupo nyumbani, haonekani wapi alipo…?’ nikajiuliza tu, hata sijui nifanyeje, lakini muhimu nikaona nifike nyumba kwangu kwanza, nianzie hapo.

Ndio nikakumbuka simu yangu, nikaichukua na kuiwasha sijui kwanini ilizimika, maana chaji ipo ya kutosha, nia yangu nikujaribu kumpigia mume wangu… lakini ujumbe nyingi zikaanza kuingia, kuashiria kuwa watu wengi walikuwa wakinitafuta, nikapokea simu iliyokuwa inaita kwa muda huo.

Alikuwa ni docta jirani yangu….

 ‘Upo wapi…’ akaniuliza kwa haraka hivyo

‘Nipo , ndio nafika kwangu…’nikasema,

‘Ok sasa ni hivi, fika hapa kwangu mara moja ni muhimu sana, mume wako yupo hapa,…’akasema

‘Yupo salama lakini…?’ nikauliza

‘Ndio…anaendelea vizuri…mengine utayajua ukifika hapa….’akasema.

‘Haya…nakuja…’nikasema

Nikarudisha gari nyuma, maana sio mbali na kwangu, tunatenganishwa na bara bara na ukuta…

‘Umeshafika…’akanipigia tena docta, nilishangaa kwanini kapiga tena kwa haraka, nikaanza kuhisi kuna tatizo kubwa.

‘Nimeshafika eneo la getii ya nyumba yako....vipi kuna maendeleo gani…maana huyo mtu aliyenipigia simu, alisema kaona kama gari la mume wangu limepatwa na ajali, …lakini sizani kama ni yeye, kwani ninafahamu yupo kazini, yupoje mume wangu, ni yeye, kaumia, …’nikasema.

‘Sawa ingia ndani, tutaongea ukifika, hajambo….’akasema.

‘Nataka kujua ni kweli docta, niambie yupoje..?’ nikauliza.

‘Mume wako ni kweli kapatwa na ajali..…, na yupo hapa nyumbani kwangu, ...’akasema

‘Kwanini hajaenda hospitali, …?’ nikauliza

‘Ukifika tutaongea, kama ni kwenda hospitali..au la…wewe ukifika unaweza kusaidia hilo, maana mwenyewe hajataka kwenda hospitalini ...’akasema

‘Mhh..haya nakuja…’nikawa najiuliza imekuwaje, nijuavyo mume wangu alikuwa kazini, sasa hiyo ajali ilitokeaje, na wapi…nikawa najiuliza.

Basi nikaingia nyumbani kwa docta


************
‘Oh, shemeji bora umewahi kufika, naona uliendesha kwa mwendo usio wa kawaida, msifanye hivyo....’akasema jirani yetu huyo mmoja, ambaye nahisi aliniona wakati naingia na gari kwa mwendo wa kasi.

‘Mumeo ni kama unavyomuona kapatwa na ajali mbaya sana, kwa jinsi nilivyoambiwa na watu, …na ameponea kwenye tundu la sindano,hapa tumempatia huduma ya kwanza , hata hivyo alitakiwa awepo hospitalini kwa hali jinsi ilivyo...cha ajabu mumeo amekataa kata kata tusimpeleke hospitalini,…’akasema

‘Kwanini jamani, hili sio swala la kuhitaji yeye kukubali au la, docta, rafiki yako huyo, unambembeleza kwa hilo…?’ nikauliza

‘Yeye alisema afikishwe hapa nimpatie huduma ya kwanza, anahisi hana tatizo,..’akasema

‘Kwahiyo..?’ nikauliza

‘Muhimu afikishwe hospitalini haraka iwezekanavyo,  ...’akasema docta.

Mimi sikuelewa, kwanini mtu apatwe na ajali ya gari, watu badala ya kumpeleka hospitali, wanamleta huku nyumbani kwa docta,...labda, au sijui alikuwa na maana gani kutibiwa nyumbani.

‘Shemeji kwa hali ilivyo, tunahitajika tumuwahishe hospitalini, hatuwezi kumsikiliza tena yeye, na kwa vile wewe upo, utawezesha hili, tulishapigia simu gari la wagonjwa linakuja,,....’akasema docta.

‘Haya, mimi sioni kwanini tusubiria hilo gari la wagonjwa, si tunaweza kumbeba hadi kwenye gari langu,au…?’ nikauliza

‘Gari la wagonjwa linakuja na kitanda cha kumlaza, …isije kuleta matatizo mengina lakini kwa vile limechelewa, basi tumbebe tu, awahishwe hospitalini…’

Nilimuangalia pale alipolala, shati ni vipande vipande…uso umevimba, na michubuko…

‘Sasa hivi kapatwa na usingizi kwa dawa nilizompa…’akasema docta

‘Basi abebwe hivyo hivyo, afikishwe hospitalini…’nikasema

‘Ni kweli, lakini lazima atazindukana, na ataweza kuhisi maumivu kwa sasa , alikuwa kama kachanganyikiwa alivyoletwa hapa…’akasema

‘Kwahiyo aliletwa kumbe…?’ nikauliza

‘Kuna mtu alikuwa anamsaidia, alikuja naye, wakati mimi nataka kutoka nje..kiukweli alikuwa akitembea kwa shida sana, na muda huo hajaanza kusikia maumivu bado, nahisi sasa ataanza kuyasikia, nimempa dawa za kutuliza maumivu zitasaidia kidogo…’akasema

‘Mhh, ...huyu mtu ana hatari kweli…angelifika hospitalini kwanza, kwa hali hii jamani anakuja kutibiwa nyumbani kama mhalifu…’nikasema,

‘Hayo hayana maana kwa sasa, hakuna haja ya kusubiria hilo gari la wagonjwa,  tulionelea kama gari la wagonjwa lingelifika mapema, tungeliweza kumfikisha hospitalini bila kukwazika na foleni, na kuzidi kulete athari mwilini.’akasema docta.

 Docta akatoa kitanda chake ca kukunja, wakasaidiana kumweka mume wangu kwenye hicho kitanda, sasa alikuwa kilalamika maumivu., wakamtoa nje na kumlaza kwenye kiti cha nyuma cha gari langu, na tukaanza safari ya kuelekea hospitalini.

Ndani ya gari pamoja na docta alikuwepo mtu mwingine na jirani mmoja, na hapo ndio nikaanza kusikia jinsi ilivyokuwa, lakini akili haikuwa sawa kusikiliza wanachoongea….

‘Nimeambiwa hiyo ajali ni ya aina yake, ukiambiwa kuna mtu katoka hapo huwezi kuamini…’akasema

‘Kwahiyo ilikuwaje, uliona ilivyotokea…?’ akaulizwa

‘Hapana , mimi nililiona hilo gari, halina thamani tena…’akasema

Sikutaka kusikia wanachoongea, kwani wanavyozidi kuongea hivyo, ndio nazidi kuogopa, nilitamani kuwaambia wanyamaze..sijui ilikuwa, wakanyamaza hadi tunafika hopsitalini.


Kila nilipokuwa nikimtupia macho mume wangu, wakati sasa anatolewa kwenye gari kuweka kwenye vitanda maalumu vya wagonjwa, ndivyo nilivyoanza kuona kuwa kweli mume wangu yupo kwenye haali mbaya, hali yake ilishaanza kubadilika, alionekana kama anazidiwa, na hapo wasiwasi wangu ukazidi, na hadi anaingizwa  hospitalini,sikuwa na amani, nilimuona kama kapoteza fahamu..

 Mwili uliniisha nguvu kabisa, lakini nikajitahidi kutembea hadi sehemu ya kusubiria…nilijiuliza tatizo ni nini hasa, ..maana  docta alisema mume wangu hajaumia sana. Hapo sikuwa na sababu za kuvumilia, nikamuendea docta, muda huo alikuwa akiongea na simu.

‘Docta kuna nini tena kwa mume wangu....?’ nikamuuliza, na yeye akaniangalia machoni, na hakusema kitu hapo hapo, lakini baadaye akasema;

‘Tutajua baada ya uchunguzi, hivi sasa siwezi kusema lolote, lakini kila kitu kitakuwa sawa....ngoja wakamchunguze na kumpiga x-ray. Na utra sound, tutakuja kufahamu hilo…’akasema, sasa hakusubiria akaelekea huko alipopelekwa mume wangu, chumba cha wagonjwa mahututi.

‘Docta…’nikamuita, nilitaka kumuambia asichelewe kunipa taarifa, sijui kama alinielewa, yeye alinionyeshea ishara kuwa nitulie, nisijali kwa mkono,


**********

Dakitari huyu pamoja ya kuwa ni jirani yetu,pia ni rafiki mkubwa wa mume wangu na alikuwa mpenzi wangu wa awali kabisa ,kabla sijakutana na huyu mume wangu na wazazi wangu walitaka sana niolewe na yeye, lakini mimi nilipingana nao kwani hakuwa ndio chagua langu. Wazazi wangu waliona yeye ndio hadhi yangu, kiuchumi na kielimu.

Kuna sababu za msingi, zilinifanya nisioelewe na yeye,  mojawapo ni kuwa mimi nilikuwa nimempenda huyu mume wangu bila kujali hali yake ya kiuchumi. Nilikuwa na sababu zingine tu ambazo hazina umuhimu wa kuzitaja hapa kwa sasa.

 Tulikuwa nje sasa tukisubiria,..mimi pale sina amani kabisa…na haraka nikataka nipate angalau mtu wa kuongea naye angalau niwe na amani, ndio nikampigia rafiki yangu simu, nikamwelezea kuhusu ajali iliyompata mume wangu..

‘Unasema nini kapatwa na ajali saa ngapi…?’ akauliza, kama vile haamini, na mimi nikamuelezea jinsi nilivyosikia.

‘Oh, labda…ilitokea muda ule, na kumbe ndio hiyo watu wanaiongelea, kuwa hajapona mtu kwenye hilo gari, ..nahisi sio hiyo maana wanasema hawezi mtu kupona kwa jinsi gari lilivyo…oh, kwanini aliendesha kwa mwendo kasi, kiasi hicho…’akasema

‘Hata sijui, maana mimi najua alikuwa kazini, na muda ule ni wa kikao, kwasababu niliongea na mtu mmoja alikuwa kwenye hicho kikao chao, hata mpaka natoka pale kwako, najua yupo kwenye kikao, sasa  …alitoka saa ngapi..hapo sijui…’nikasema


‘Oh ..na ile kona ni mbaya…’akasema

‘Kona gani…?’ nikamuuliza

‘Acha ile kona ya kutoka kwangu , unaipita hadi ile kona ya bara bara inayokwenda kuelelea kwenu…ndio nimesikia hiyo ajali imetokea hapo, lakini sizani kama ndio hiyo ya she- , …ya mume wako…’akasema, nilisikia mtoto analia, akawa anakat akata maneno.

‘Oh, mungu wangu wakati napita hapo niliona watu wamekusanyika, sikutaka kuangalia, maana nilikuwa na haraka, ina maana…sasa huko alitokea wapi, …mbona kupo kinyume na barabara ya kutokea kazini kwao…?’ nikauliza

‘Labda…alipotoka….hata sijui…hilo tuliache tu…’akasema

‘Hapana,..tuliache kwa vipi, …yaani, muhimu ni kujiuliza huko alifuata nini, na….oh, mungu, ….mungu amjalie apone tu..,..maana hali ilibadilika ghafla tulipofika hapa hospitalini, naogopa kweli rafiki yangu…’nikasema

‘Mhh…muhimu ni hali yake,…hiki kitoto kinasumbua, nakiogesha hapa,…basi, usijali rafiki yangu,  mengine hayana  tija, atapona tu kwa uwezo wa muumba, …’akasema

‘Ni kweli,…mengine sijui yapi hayo…haya,  ndio hivyo rafiki yangu, ni siku  ambayo sitaisahau kabisa, maana njiani napo nilikutwa na mikasa, nikiwa soko-duka, nilipoteza fahamu ghafla..’nikasema

‘Ulipoteza fahamu…!!!, ilikuwaje tena jamani… pole, na wewe umezidi kujiongezea mawazo, mengine yaache yatajipa yenyewe, ukitaka kufahamu kila kitu unaweza kuathiri ubongo wako…Haya utanipa taarifa kinachoendelea…’akasema

‘Sawa nitakujulisha..’nikasema na kukata simu.

*************

Baadae docta mmoja akaja, akasema wameshaondoa ile hali mbaya, hakuna matatizo tena, hakuna athari za ndani, kwahiyo mume wangu atapelekwa chumba cha kulazwa wagonjwa wa kawaida, baadae kweli akatolewa huko ICU,

‘Hii ina maana kuwa hana tatizo kubwa…’akasema docta jirani yangu, aliyekuja baadae

‘Kwahiyo tunaweza kwenda kumuona….?’ Nikauliza

‘Ndio..sizani kama kuna kikwazo…’akasema

Tulipofika kwenye hicho chumba alicholazwa mume wangu, tulimkuta kama kalala, kafumba macho, kalala kaangalia juu, nilimkagua kichwani kafungwa fungwa, umebakia uso,..na shingoni kavaliwa dude kuashiria huenda kuna hitilafu shingoni….hiyo ni dalili kuwa kweli alikuwa kaumia, japokuwa alijikaza kuonekana kinyume chake..

Baadae akafungua macho, nikamsogelea nilimuangalia mume wangu pale alipolala, nikahisi machozi yanataka kunitoka…kalala huku kaangalia juu, hakutaka hata kugeuza kichwa kuniangalia, labda hawezi kugeuza shingo,..nikamsogelea pale kitandani, na hapo akajitahidi kuniangalia, kwa kugeuza macho, nikaona machozi yanamtoka…akasema

‘Pole sana mume wangu, mungu ni mwema utapona tu…’nikasema

‘Nisamehe sana mke wangu, ni-sa-sa- mehe…’akasema huku machozi yakiendelea kumtoka, nikachukua leso yangu na kumfuta, sikuelewa, nahsi ni hiyo hali,…hata mimi pale machozi yakawa yananilenga lenga, nampenda sana mume wangu, na kumuona kwenye hiyo hali, niliumia sana, mawazo yalinipeleka mbali sana.

‘Usijali utapona, tu…mume wangu…’nikajitahidi kusema hivyo.

 Sasa akafumba macho, akawa anahema taratibu, na hilo lilinipa moyo, kuwa kufumba macho huko sio kwa ubaya, nikasema

‘Mume wangu utapona tu..tuzidi kumuomba mola…, umenielewa eeh, docta amesema hakuna tatizo kubwa…’nikasema, lakini akilini nikawa najiuliza ni kwanini kakimbilia kusema; nimsamehe…labda,…kawaida mtu akiumwa hujua hatapona ndio anaomba msamaha kwa watu, labda…

‘Atapona tu…’nikasema hivyo

‘Ndio atapona docta kasema ni athari ndogo za kuteguka …na ngoja tusubiria vipimo halisi havijatoka kwanza…’akasema docta huyo jirani yangu.

Baadae mume wangu akapitiwa na usingizi, na tuliambiwa tumuache alale, sisi tutoke nja, tukafanya hivyo.

Na wakati tupo nje, ndio nikajaribu kuwauliza watu walikuja nasi, yupo docta , na jirani mwingine na mfanyabiashara aliyenipigia simu, yeye alishafika, wengine yule mwingine tuliyekuja naye alishaondoka, huyu mfanyabiashara anasema yeye alishuhudia hiyo ajali,…

‘Kwani ajali hiyo imetokeaje..?’ nikauliza

‘Imetokea ile kona ya kutoka barabara kuu, kuingia barabara ya mitaa inayoelekea kwako, mume wako alitokea mitaa ya kutokea Uzunguni, mimi nilikuwa barabara kuu naelekea kwingine, nikasikia huko nyuma paaah, mlio wa kuogonga, unajua nilikuwa naendesha sikuona ilitokeaje, nikasimamisha gari, na kutoka nje…’akasema

‘Ina maana ni huu mtaaa wanaouita ‘Uzunguni..’..huko alitokea wapi, …huko si ndipo anapoishi rafiki yangu, mbona mimi nilikuwa maeneo ya huko…, sijamuona ….?’ Nikasema na kuuliza

‘Ndio hivyo..yawezekana alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi, nahis alikuwa akiwahi jambo, au angelikuwa mhalifu tungelisema anawakimbia polisi…’akasema huyo mfanyabiashara

‘Mhh, hata sielewi, na hana tabia ya kuendesha gari kwa mwendo kasi..sio kawaida yake…’nikasema

‘Mimi nilijua mlikuwa naye labda…akawa anawahi kitu nyumbani, ..kama ulikuwa maeneo ya huko…’akasema jamaa mwingine.

‘Oh, hata sijui…sikumuona kabisa maeneo ya kule…hakuna mtu aliyemuona,.., labda kwa vile nilikuwa  ndani naongea na rafiki yangu..labda kuna kitu alikuwa akikifuatilia, akapitia njia hiyo..akitokea wapi sasa…mmh, hata hivyo ni kwanini akimbize gari hivyo…’nikasema.

‘Ni ajali tu…’akasema docta

‘Kiukweli ana bahati sana, maana ukiliona hilo gari, utasena hakuna mtu aliyetoka humo ndani, halitamaniki, alikuwa kwenye mwendo kasi sana, ..na gari lenyewe baadae liliwaka moto, na hata watu walipouzima, lilikuwa limeshateketea kabisa…’ akasema jirani.

‘Oh, ...niliona ajali hapo njiani wakati nakuja, lakini sikujua ndio hilo ya gari la mume wangu,....,’nikasema

‘Sasa mimi nawashangaa huyo mtu aliyemleta hapo nyumbani kwako docta,  badala ya kumkimbiza hospitalini, alikuambia ni kwanini alifany ahivyo?’ akaulizwa docta.

‘Nahisi alichanganyikiwa, na labda hakutaka ijulikane ajali hiyo imetokea wapi, labda maana tunajisema wenyewe tu kuhisia,..sabbu kubwa ni kuwa  alichanganyikiwa maana haina maana hapo…, gari si lipo, kama ni wazo hilo, la kuficha kuwa ajali ilitokea wapi…’akasema yule mfanyabiashara.

‘Unajua watu walipofika kwenye hilo gari, walijua wanafika kutoa maiti tu..mimi mwenyewe nilishashika kichwa nilipogundua kuwa ni gari la mumeo…lakini watu walipofika hapo, wanashangaa kuona ndani ya gari hakuna mtu…ina maana huyo mtu alitoka kabla ya kugongana au alirushwa nje ya gari…’akaelezea

‘Na walipoona hivyo hakuna mtu, wasamaria wema wakaanza kuhangaika kutafuta dereva yupo wapi, lakini hakuonekana kabisa…mimi mwenye nahangaika kukupigia, simu inatumika, mara hupatikani mara…baadae ikawa haipatikani kabisa….’akasema huyo mfanyabiashara.

‘Mimi hata sijui….mume wangu jamani, apone tu,..sikujua kuwa ni gari lake wakati napita pale, nilikuwa na mawazo mengi, na kama ni ajali nilitegemea kwingine kabisa sio njia hiyo...’nikasema

‘Gari halithaminiki, hakuna kumbukumbu yoyote ndani,..maana lilikuwa bado haliingiliki, baadae mimi kwa vile nalifahamu ni la nani, taratibu bila kuwaambia watu lolote, nikaanza kufuatilia, kukupigia simu ukawa hupokei, baadae mimi wazo likanijia...

Nikaamua kwenda nyumbani kwanu, na nimefika pale haupo, na mumeo hayupo,,…nikaona hapa, isije ikawa mtu kaungulia ndani ya gari hatukuona vyema, nikataka kurudi tena kuhakikisha,…sasa wakati natoka pale kwenu,  ndio nikakutana na jamaa mmoja rafiki yangu, akaniambia, kuwa kakutana na mumeo, yupo kwenye hali mbaya, …kaingia nyumbani kwa docta.

‘Mhh, hapo kwa haraka nikahisi aliruka alipohisi ajali, lakini mmh, yatakiwa uwe mzoefu kweli kama askari, sijui…yaani hapo ni kitendawili mpaka mwenyewe ajae kutuambia…’akasema

‘Hata hatujui alifikaje kwa docta,…..rafiki yangu mmoja alikuwa anapita na gari lake, ndio akamuona yupo nje ya mlango wa docta akiwa kasimama, kashikilia mlango, ..yupo hoi,..kama aliyepatwa na ajali, ana damu, shati limechanika,..ikabidi asimamishe gari kuja kuangalia kuna tatizo gani, ndio akamuona yupo kwenye hali mbaya,… akamsaidia kuingia naye ndani,kwani aliadai aingizwe humo ndani kwa docta.

 ‘Nikamuuliza alimuachaje …hali yake vipi, maana siamini, mtu katokaje kwenye hilo gari…’akasema.

‘Akasema kumbe docta huyu jirani yenu yupo likizo, walimkuta yupo hapo ndani, basi ikabidi aanze huduma ya kwanza, akaniambia kuwa kamuacha huko ndani akimuhudumia, lakini anaonekana hayupo vibaya, ila ni kama kachanganyikiwa…’akasema

‘ Mhh… mungu mkubwa…’nikasema hivyo. Na mimi ndio nikaingia na kumkuta docta akimuhudumia na kwa muda huo hata docta hakujua kilichotokea, ndio nikamuelezea, nilichokiona huko nilipotoka, na ndio akajaribu kukupigia, naona simu yako ina matatizo,…simu yako haina matatizo kweli…?’ akauliza huyo mfanyabiashara.

‘Haina matatizo, lakini kuna muda ilizima…’nikasema hivyo, sikutaka kuongea zaidi, pale nilikuwa na hamu nirudi ndani nikamuangalia tena mume wangu.

Nikamsogelea docta kumuomba akaombe ili niweze kuingia ndani, nikamuone tena mume wangu.
‘Sawa, hamna shida…’akasema na kuniambia tuongezane, basi tukaenda naye hadi pale alipolazwa mume wangu


Nilipomchungulia mwili wake, nilihisi mwili wangu ukisisimuka sikujuwa kwanini, kwanini kanyoka tu vile…, na muda ule alikuwa kafungua macho, sasa hataki hata kuniangalia machoni, mwili wangu hapo ukafa ganzi, nikawa nasubiria tu hiyo taarifa ya docta nisikie kama ana tatizo au hana...

Pale docta akaongea nilipomuuliza ni kwanini alikuja kwake…


‘Yeye ndiye aliyenipigia simu, na namba tofauti, nahisi alimuomba mpita njia mmoja, mtu wa bajaji…kwa bahati nzuri nipo likizo, kwahiyo nilikuwa hapo nyumbani, nikijua ni tatizo dogo, ndio hivyo  akaletwa, kiukweli nilimshauri aende hospitalini, lakini alisema ni muhimu atibiwe hapo nyumbani tu, na nilion akachanganyikiwa, anasema hataki ijulikane kuwa kapatwa na ajali, ..ni kuchanganyikiwa tu huko...

‘Kwanini hataki, wakati keshapata ajali, mmh…?’ nikamuuliza

‘Atakuja kukuambia mwenyewe, ndivyo alivyosema…’akasema docta

‘Kiukweli nilipomfanyia uchunguzi wa haraka haraka na kufanya kile kinachowezekana, sikuona tatizo kubwa la nje, ila…ajali ni ajali, unaweza kwa nje usione kitu, tatizo likawa lipo kwa ndani, na unaona, kumbe kuna athari kwenye uti wa mgongo na shingoni, ngoja tusubiria taarifa za madocta,.. ’akasema huyo docta jirani yangu

‘Uti wa mgongo…umeathirika..mungu wangu ina maana gani sasa ina maana hataweza kutembea tena,..’nikasema nikishika kichwa

‘Usiwe na wasiwasi, …yupo kwa wataalamu..ngoja tusubirie uchunguzi wa mwisho….’akasema docta kunipa faraja


NB: Ndivyo ilivyokuwa hivyo...., 



WAZO LA LEO: Mwili wa binadamu una uvumilivu wake, tunahitajika kuutunza sana, na unapouzidishie mambo juu ya uwezo wake, ukiulazimisha sana mwili, hasa kimawazo, tunaweza kujikuta tukipatwa na athari za kiafya. Mazoezi ni muhimu sana ili kuwezesha miili yetu, na akili zetu kubeba mambo kwa mpangilio. Lakini pia tusipende kuulazimisha kupita kiasi…hasa mawazo, mawazo yakizidi sana huja kuleta matatizo.

Ni mimi: emu-three

No comments :