Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 23, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-12



Mlango wa geti la nje uligongwa ndio,…!

Sio mlango wa nyumba yenyewe, maana hiyo nyumba imezungukwa na geti, , nina uhakika ni geti hili la nyumba anayoishi  rafiki yangu…nikamtupia jicho rafiki yangu huyo,….nikamuona, akitoa macho kuangalia kuelekea kule mlangoni…

Ni kweli atakuwa huyo mgeni wa rafiki yangu, maana nilisikia sauti ya mlango wa geti ukilia,…geti linafunguliwa, sasa kuashiria kuwa huyo mtu kaamua kulifungua hilo geti yeye mwenyewe hapo ina maana gani, kuw huyo mtu kazoea kufika hapo, anapajua vyema.

Hapo ikawa kama kamchokoza rafiki yangu huyo,  nahisi rafiki yangu hakutaka kabisa huyo shemeji tuonane naye mimi, kwa jinsi nilivyomuona akihangaika, na kwa jinsi alivyobadilika sura, usoni alionekana kutahayari…, mpaka nikamuonea huruma,…lakini nikawa sijali, kwanini …mimi sina nia mbaya, hanielewi tu…

‘Kwanini unapata shida hivyo, mkaribishe mgeni…’nikasema lakini rafiki yangu alibakia akiwa kashika kichwa, akiniangalia kwa macho yenye huruma, au…kama anataka kulia…


‘Hapana, sio leo jamani..sijajiandaa kwa hili, nahisi imekuwa ni haraka sana, …nahisi hatari…unasikia, rafiki yangu, wewe pitia mlango wa nyuma uondoke, sitaki matatizo hapa nyumbani kwangu, najua kabisa itakuwa hivyo….’akasema akishika kichwa.


‘Kwanini…mbona sikuelewi…’nikasema nikimuangalia kwa macho ya kujiuliza na yeye akawa ananikwepa kabisa kuniangalia machoni.

‘Tafadhali fanya hivyo….nitakuja kukuambia ni kwanini…lakini kwa hivi sasa ili kuepusha shari..ili , nisivunje uaminifu..unajua aliniomba tena sana nisije kumsema kwa watu, hadi muda muafaka ufike,…na nikifanya hivyo, ..na yeye…unanielewa hapo, haya nenda pitia mlango huo wa nyuma…’akasema

‘Mimi siendi mahali, lao nataka hili jambo lifikie mahali na mimi, niwe na amani , nahisi kuna …sijui nisemeje, unanifanya nianza , kama nilivyokuambia nitunge kitabu, sasa ni kwanini, maana matendo yako, kauli, zako zinanihamasisha nifenye hivyo, kifupi nahisi kuna kitu unaficha, ambacho ni zaidi ya hilo tulilokubaliana, sasa ningeliomba umkaribishe huyo mgeni, najua tutayamaliza,….’nikasema

‘Hapana, nielewe nina maana yangu kubwa sana, najua itafika muda hili itabidi liwe hivyo, lakini sio kwa leo, sio kwasasa…nakuomba mimi ni rafiki yako, niamini ninalokuambia…yanayotokea, na kauli zako…hapana, na iwe hivyo tu..ila nitakuja kukuelezea kila kitu..unajua, nitaumia sana ikifikia mahali pabaya….’akasema na mimi nikataka kusimama

‘Unataka kufanya nini sasa ?’ akaniuliza

Mimi nikamtizama kwa macho ya kujiuliza, akilini nilishadhamiria kitu, lakini sina uhakika nacho, na alipoona kweli nataka kuchukua hatua akasema

‘Rafiki yangu, ndugu yangu sivyo kama unavyofikiria wewe, tulia kwanza unataka kwenda wapi…nielewe maana hata mimi nilivyokuwa nikitegemea, imekuwa sivyo kabisa, nahisi nahitajia muda zaidi wa kulitafakari hili nisije kuleta hatari…..!’ akasema akiwa kasimama mbele yangu kama kutaka kunizuia


Mimi pale nilishikwa na butwaa, sikumuelewa kabia, ni kwanini anafanya hivyo,..nikabakia kumuangalia, uso ukiwa na maulizo mengi, kujiuliza kwingi,  ..baadae nikasema

‘Mhh..hatari…hatari gani….mbona  unanichanganya, au hatupo sawa tena,nieleze rafiki yangu kama kuna kitu kibaya kimetendeka nielewe mapema, hivi unanitesa kabisa, wewe hujui tu,…hapana mimi bado nakuamini, mimi bado nipo na wewe, usiwe na wasiwasi bwana…achana na mafikira potofu,…nikuambie ukweli, mimi nina hamu sana ya kumuona huyo shemeji yangu..’nikasema

‘Utamuona…kwanza ushamuona sana..ila kwa sasa naomba nipo chini ya miguu yako tafadhali…’akasema akiashiria kutaka kupiga magoti.

‘Unajua sijakuelewa, kwanini..…kila siku ni …shemeji, shemeji, nataka nimuone huyo shemeji, hata kama yupoje, labda unahisi hadhi yake haiendani na wewe labda, kama kweli sio huyo ninayefikiria mimi,… labda umekuja kutembea na mtu, asiyekustahili labda hivyo..mim hilo sijali kabisa , ilimradi kakupa kile ulichokitaka na mimi ndiye msiri wako…’nikasema

‘Hapana, sio hivyo…ninasababu nyingine kabisa, ya nia njema, …nielewe hivyo tu…’akasema

‘Mhh..mimi hapo sitakuelewa kabisa.., leo…eeh, hakuna jinsi, lazima nimuone huyo mtu, kama kaja yupo huko nje, mwambia aingie ndani, tuyamaliza hapa hapa…’nikasema na yeye akabakia kimia

‘Sasa unaogopa nini, mtu yupo huko nje, anasubiria, unajua naanza kuingiwa na wasiwasi, kitu ambacho sikuwa nacho dhidi yako, na hizi eeh…kauli zako zinanipa mashaka, ..kwanza najiuliza kuna hatari gani, kuwa itakuwaje, kuwa nitatoa hii siri nikimfahamu au..hahaha, mimi nimeshamfahamu, muite tuyamalize leo hii, ili na mimi niwe na amani..’ nikasema

‘Siwezi kufanya hivyo, for the sake of our friendship….kwa minajili kwa kuwa hata yeye mwenyewe hataki, na kama angelijua nipo na mtu asingelifika kabisa,…alishaniomba na akafikia kunitisha, kuwa ni..iwe siri yetu,…’akasema

‘Kukutisha kwa vipi….?’ Nikamuuliza

‘Bwana wewe liache kama lilivyo… na sijui kwanini unang’ang’ania hivyo, wakati hata wewe mwenyewe  ulitaka iwe hivyo…hapana, acha tu, iwe hivyo hivyo.., nakuhakikishia muda utafika kila kitu kitakuwa bayana, ikibidi….’akasema na mimi nikatikisa kichwa kukataa.

Hapo akageuka kuangali mlangoni, …uzuri mlango ulifungwa..kuna namna ukifunga mtu wa nje hawezi kufungua, mpaka mtu wa ndani labda uwe na ufungua…sasa sikujua kama aliuegesha tu,…

Nikawa naangalia kule mlangoni nikitamani huyo jamaa aingie, lakini nahisi alikuwa kasimama, anasubiria mwenye atoke, au kahisi kuna …na mara nikasikia sauti ya viatu vya mtu kukaribia mlangoni …ka-ka-ka-ka..huyo mtu kavaa viatu vinavyotoa sauti,

Nakumbuka kuwa hata leo mume wangu wakati anaondoka kwenda kazini alikuwa kavaa viatu vinavyotoa sauti ukitembea, nikamwambia hivyo viatu vinavyotoa sauti sio vya kisasa, abadilishe, lakini hakutaka, siku ya leo alisema alivitamani kuvivaa viatu vyake maana vinamkumbusha mbali.

‘Bebii…upoooh…’nikasikia sauti ikasema kutoka nje…..

Bebii…..’nikajikuta nikisema hivyo, akili ikanipeleka mbali kabisa, hivyo ndivyo mume wangu alizoea kuniita, kipindi hicho, mambo hayajawa mambo, na sikumbuki tena kuniita hivyo,…na, mbona hata sauti ni kama …hapana…mmh,

Unajua nilihis moyo ukinienda mbio nikishindana na nafsi yangu, sikupenda kamwe nafsi inishinde, ..lakini hata hivyo, hata huyo mdogo wa mume wangu ana sauti kama hiyo, isipokuwa ya kwake inakwaruza-kwaruza hivi, hiyo imetoka sawa sawa naya mume wangu.

 Na hata kufikiria hivyo, sio kwamba nilihisi kuwa ni mume wangu yupo huko nje, hapana siwezi kudanganya, akili yangu ilinizidi kunipa tashwishwi ya kumuona huyo mtu anayefanana mambo mengi na mume wangu.

‘Mume wangu yupo ofisini sio…’nikajikuta nasema hivyo kwa sauti ndogo.

Rafiki yangu akanitupia jicho aliposikia nikiweweseka hayo maneno, na ni kweli..nilikuwa na uhakika kuwa mume wangu yupo ofisini kwao, ana kikao muhimu sana, asingeliweza kuja huku,…ndio maana alizima hata simu yake kuchelea kusumbuliwa.

Sasa kwanini moyo wangu ukashtuka hivyo, niliposikia sauti hiyo, inayofanana nay a mume wangu, na kwanini kauli hiyo neno hilo, liwe sawa sawa na neno alilopenda kulitumia mume wangu enzi mapenzi yamepamba moto....hapo nikagwaya...

Lakini atakuwa ni shemeji tu huyo….

**************
‘Kumbuka ahadi yetu, kumbuka kuwa wewe ndio uliyenishauri hivyo, na naomba iwe hivyo ...nataka tukubaliane, ili lisije kuleta shida baadaye…’.

 Nikiwa nasubiria rafiki yangu amkaribishe mgeni wake, nikahisi maneno hayo yakijirudia rudia kichwani mwangu kama onyo…na mara mtoto akaanza kulia,…na muda huo rafiki yangu yupo mlangoni, anataka kufungua mlango,

Mtoto alipolia akageuka kumuangalia, na akaniona mimi nasimama kwenda kumuhudumia, akawa na amani akashikilia kitasa kunyonga mlango ufunguke

 Mimi mtoto alipolia kwa haraka nikasimama na kuelekea pale alipolazwa huyo mtoto, alikuwa kwenye kitanda chake chandarua , nikamkagua na nikaona kakojoa, kwa haraka nikaanza kumbadilisha, na kuwa muda huo akili ikawa kwa mtoto sikuwa na muda tena wa kuangalia kule mlangoni, ila nilisikia sauti kwa mbali ikisema;

‘Upo peke yako, …sijakuelewa, nauliza upo peke yako…mbona hunikaribishi ndani..?’ sauti hiyo niliisikia kwa kuunga unga, sikuweza kubahatisha vyema, maana kulikuwa na kelele za tv,na kulikuwa na kitu kama upepo nje, ulikuwa unapita, sikuweza kusema hiyo sauti inafanana nanni, sio ..kama ile ya awali alipotamka neno bebii, …na mara kukawa kimia.

Mtoto akawa kalala , basi mimi nikasimama sasa, sasa namuangalia rafiki yangu, sisikii wanachoongea kama wanaongea itakuwa ni sauti ya chini sana,…hapo nikatamani nisikie wanachoongea, nikatembea taratibu kuelekea huko mlangoni

Nikasogea taratibu, hadi nikakaribia mlango, na nilipofika , kwanza nilikuwa na nia ya kuwaingilia, na kumkaribisha huyo mgeni, lakini nilipofika hapo nafsi ikataka kusikia wanachokiongea,..na kwa muda huo rafiki yangu alikuwa kazama kwenye mazungumzo na huyo mtu, na nilichoweza kusikia kwa muda ni haya maneno, yalikuwa ya kuwewesa zaidi kiasi kwamba huwezi kuyasikia vyema, alisema ;

‘Kama upo peke yako unaogopa nini…’ni sautiya chini sana….kiasi kwamba sikusikia alichoongea zaidi

‘Wewe nenda, siku ya leo sio nzuri, muhimu unielewe, …ondoka haraka sana,..mimi hapa nipo peke yangu, lakini muda wowote anaweza kufika mtu, nielewe hivyo, kwaheri…oh..’akasema rafiki yangu na kutaka kuufunga mlango, na sasa akageuka, na kunikuta nipo nyuma yake, alishtuka, ..na kunitolea macho yenye dalili ya uwoga fulani hivi

‘Oh, ulikuwa unani…sikiliza…?’ akauliza kwa mashaka

‘Vipi, mbona haingii…’nikasema, na akiniashiria nikae kimia, kwa vidole, akisema,
Sshiii…huku akitikisa kichwa, na mkono mmoja bado umeshikilia mlango ina maana hataki huyo mtu huko nje ajue kuwa kuna mtu ndani…lakini mimi nikajifanya sijamsikia, nikasogea karibu sasa nikitaka kufungua huo mlango.

‘Haya baadae nitakuja,…’sauti huko nje ikasema, hiyo sauti nikaisikia, sauti hiyo iliyonifanya nishtuke kidogo, lakini sio saana, maana haiwezi ikanihakikishia nilichokifikiria kwa muda, nikajikuta nikisema;

‘Mhh..ni nani huyo anaongea sauti kama ya mume wangu..?’ nikauliza

‘Ni shemeji…’akasema rafiki yangu akionekana kuwa na wasiwasi, na sasa akawa kasimama kati kati ya mlango kunizuia nisiweze kufungua mlango na kutoka nje.., huku akiniangalia machoni kwa yale macho ya mtu aliyetoka usingizini, au alikuwa analia, …au mashaka…hivyo!

 Mimi nilimuangalia kwa mashaka, ...na sasa kitu kama hasira zilianza kujijenga, ni kwanini rafiki yangu mwenyewe ana nifanyia hivyo, kwa vyovyote iwavyo rafiki yangu hataki nimuone huyo mtu, ni kwanini… na inawezekana ikawa sio huyo shemeji…, na kama sio shemeji atakuwa ni nani..au anaweza akawa ndio yeye, lakini hataki tuonane naye uso kwa uso..ni kwanini…, labda kutokana na jinsi walivyoelewana. Hata hivyo, ..

Kwanza nilitaka nirudi, niyaache kama yalivyo, lakini nafsi ikasema, kwanini ..kwanini niyaache , hapana, ni lazima nihakikishe huyo ndiye kama ninavyofikiria, na kwanini nisimuone, ni  kwanini nisimuone tukaongea naye, haya mambo niyaweke sawa yaishe tu, nina imani nikionana naye nikaongea naye, yataisha tu..nataka nimuone huyo, she-she…shemeji….

Hapo sikuwa na simile, nikasogea na kuubandua mkono wa rafiki yangu pale mlangoni, na kumpiga kikumbi cha kumsukumiza pembeni…, ili asogee, na hakulitazamii hilo, akapepesuka na kutaka kudonoka chini, mimi hilo sikujali, nikavuta mlango, ukafunguka…

Nje…hakuna mtu…lakini hisia zinanifanya nihisi kuna mtu, ila simuoni..yupo wapi..!nikageuka huku na huku , sioni mtu…

‘Mhh…haya..’nikasema hivyo tu

**********

‘Mbona hivi rafiki yangu, imekuwa ugomvi…’akasema sasa yeye akiwa kasimama mlangoni, akinitizama kwa mashaka,..

Muda huo ndio naangaza huku na kule kumtafuta huyo mtu kwa macho lakini huyo mtu haonekani,…haiwezekani huyo mtu ayeyuke hivi hivi, haiwezekani kwa muda huo mfupi awe keshafika getini na kutoka nje,..hapo nikataka kuhakikisha, nikatembea hatua chache kuelekea getini, lakini sikuona mtu.

‘Amekwenda wapi huyo mtu uliyekuwa ukiongea naye…?’ nikauliza

‘Nani, …keshaondoka bwana…?’ akaniuliza  na kusema hivyo, sasa akionyesha uso wa kunishangaa mimi. Nikamtizamaa weeh, na kutikisa kichwa.

‘Hahaha, haiwezekani, …huyo mtu anapaa au….yupo wapi huyo shemeji….nataka nionane  naye…kakimbije haraka hivyo na kutoka nje, haiwezekani, yupo wapi…’nikasema na nikaona kama uso wa rafiki yangu ukinawiri, ni kama vile alitarajia nitaongea kitu kingine kibaya, lakini akakuta nimeongea kitu ambacho hakikumkwaza, akasema;

‘Utamuona tu ndugu yangu..subira huvuta heri, njoo ndani tuongee , tumalizane, maana leo sina amani, natamani niondoke leo hii hii nikakae huko Zanzibar, mpaka siku yangu ya kuondoka kusoma ifike.., lakini haiwezekani, mambo ya visa bado hayajakamlika…lakini sikufukuzi, njoo ndani tafadhali…’akasema

‘Kweli ni bora niondoke zangu, huna maana wewe kabisa…yaani leo, sijui hasira zangu zimekwenda wapi..haya bwana fanya utakavyo, naona …aah, sijui kwanini,…mimi ninavyokujali na kukupenda malipo yake ndio haya, baya bwana…lakini…hiyo lakini iweke moyoni, ipo siku nitaimalizia,..’nikasema sasa nikitaka kuondoka

Nikakakumbuka kuwa nimeacha mkoba wangu ndani,…uone mambo ya mweneyzimunu yalivyo,..nikarudi ndani kwa haraka, muda huo nishakasirika nataka niondoke tu hapo.

Mimi kwa haraka nikarudi kuelekea ndani, ila haraka, uso umeshakasirika, hata nampita rafiki yangu anaonekana kuogopa labda nitafanya kitu..yeye kasimama kwa tahadhari,, akionekana hana amani…mimi sikutaka hata kumuangalia machoni.

 Nilipofika ndani, mtoto alikuwa kaamuka, nikamuona anavyochezesha-chezesha vimkono vyake pale alipolazwa, nikavutika kumuangalia…unajua tena ukiwa na hulka ya kupenda watoto…, keshaamuka  macho yake yamefunguka, ananitizama, kama vile ananiona na hapo hapo taswira za watoto wangu wakiwa wadogo zikanijia akilini.

Kila ninapomuangalia huyu mtoto , nawaza mengine ambayo siyataki, nahisi kama ni mtoto wangu, nahisi..kufanana…na… lakini hainijii akilini, na naishia kuhitimsha kuwa baba wa huyu mtoto atakuwa mdogo wa mume wangu…hivyo tu na kujiaminisha kwa msimamo wangu huo. Mungu mwenyewe ndiye anajua..

Nilisimama pale kwa dakiki kadhaa nikimkagua huyo mtoto kwa macho, kabla sijageuka kuondoka, na mara huko nje nikasikia sauti ya viatu kama mtu anakimbia, tatatatata…sauti ya viatu…ni sauti ile ile…atakuwa ni huyo jamaa kumbe alikuwa hajaondoka, atakuwa alijificha sehemu kwanini sikuwa makini kukagua upande wa nyuma wa hiyo nyumba,

Hapo, hapo…nikamuangalia rafiki yangu kwa macho yaliyojaa hasira, na kwa haraka nikawa nimeshauweka mkoba wangu mkononi, na sasa najiandaa kuelekea mlangoni, ili niweze kumuwahi huyo mtu, na rafiki yangu alikuwa hajaondoka pale mlangoni, malngo upo nusu wazi, lakini kaushikilia, na aliponiona akajua nataka kufany anini, akaufunga mlango na kuendelea kuushikilia…, kasimama kati kati ya mlango.

Nikamsogelea nikiwa na haraka nataka kutoka lakini safari hii alikuwa kajizatiti, akawa hasogei, hata baada ya kumsukuma anipishe nipite..na huko nje nilisikia mlango wa geti ukifunguliwa na najua atakuwa keshaondoka, kiukweli kitendo hicho  kilinikwanza kweli……sasa ikawa kama shari, tunasukumana, na bado hataki mimi nitoke…baadae nikafanikiwa nikamtoa pale mlangoni, nikafungua mlango na kutoka nje,…nilishachelewa.

‘Kwanini unanifanyia hivi lakini, kwanini, ..?’ nikamuuliza sasa akiwa kasimama pale mlango akiniangalia tu kwa mashaka..baadae akasema

‘Ni bora nusu shari kuliko shari kamili, ni bora tu, iwe hivi, ili nisije kuharibu…najua utakuja kunielewa baadae, ..samahani sana rafiki yangu, nakuomba unielewe hivyo, sina nia mbaya kabisa, natimiza masharti yetu tuliyowekeana, na ahadi niliyoweka na huyo mtu, haitapendeza kabisa, nikifanya kinyume chake, nielewe hivyo tu, samahani sana rafiki yangu…’akasema

‘Kwahiyo kumbe ni kweli…eeh,’nikasema huku nikitikisa kichwa changu

‘Kweli kuhusu nini..nimeshakuambia huyo ni shemeji, hutaki kunielewa,sasa bora iwe hivyo hivyo tu…., na ukweli ndio huo, nimetimiza kile tulichokipanga, ni wewe sasa unayetaka kuharibu, sijui kwanini unataka kujisaliti mwenyewe…’akasema

Shemeji ..shemeji,…, hata mimi ninao wengi tu… haya kaaga na huyo shemeji yako na sitaki tena kumuona, ila ole wako, litokee tatizo, unasikia, ole wako…si unanifahamu nilivyo, na usifikiri nimekata tamaa, …nitamfahamu tu, huwa sishindwi jambo  …haya kwaheri…’nikasema na kuanza kuondoka..

Nikageuka nyuma, nikamkuta rafiki yangu kasimama mlangoni mwa nyumba anapoishi,..bado ananiangalia kwa mashaka, ..mimi nikatikisa kichwa kama mtu anayesikitika, sikusema kitu zaidi…nikaanza kutembea kuelekea kwenye geti na hapo simu yangu ikaita.

Nilipoangalia mpigaji, nikagundua ni namba ya docta , huyu ni jirani yangu, sikutaka kuipokea kwa muda ule.., sijui kwanini. Docta ni mtu ninayejuana naye sana, na mara nyingi hunipigia simu tunaongea naye sana, huyo kwa viwango naweza kumweka kwenye nafasi ya marafiki zangu ninaoaminiana naye sana.

Kwa muda ule sikutaka kuipokea simu yake maana mara nyingi akinipigia tunaishia kuongea mengi sana yaliyopita, kutaniana…kwahiyo nikadharau, kwa vile akili yangu haikuwa sawa, nikakata simu

Baadae alipopiga tena, nikajua kuna jambo, nikapokea

‘Upo wapi zilipendwa…’ akasema kiutani, najuana naye kiukweli

‘Acha utani wako, nipo kwenye …jambo muhimu, tutaongea baadae, naelekea nyumbani…’nikasema, yeye akasema niende kwake.

‘Nije kwako kuna nini…?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Pitia hapa ni muhimu tuonane…kama unaelekea nyumbani…’akasema

‘Sawa…’nikasema , lakini sikuwa na shauku , na moyoni nilipanga nisipitie kabisa, namfahamu , tumezoeana kihivyo …nitakuelezea baadae ni kwanini nimezoeana naye hivyo

Nilielekea pale nilipoweka gari langu na kumlipa huyo kijana ambaye ninamuamini sana, nikaingia kwenye gari, na wakati nataka kuondoka, yule kijana akasema

‘Shemeji naye alileta gari lake, nilisafishe … , lakini hakusubiria nimalizie kusafisha, anaonekana ana haraka sana, ameondoa gari kwa haraka sana, sio kawaida yake….’akasema

‘Shemeji gani…?’ nikamuuliza na mara honi ikapigwa nyuma ya gari langu, kulikuwa na gari lilikuwa linataka kuingia, basi,…sikuweza kuongea na huyo kijana, ikabidi nisogeze gari langu mbele kwanza, na nilipomaliza, nikafungua kiyoo cha gari, kutizama nje, kumtafuta huyo kijana, nikamuoana anaongea nawateja wake, nikaona isiwe taabu…nikapandisha kiyoo changu kuanza kutoka nje ya eneo lile.

Nikabakia kwenye kitendawili,..ni nani shemeji, ..ni kwanini rafiki yangu ananificha, kuna nini hapa….akili ilikuwa bado imefungwa kabisa….huwezi amini, ilikuwa hivyo…

Wakati nakaribia nyumbani, nikaona nipitie supermarket, ninunue vitu fulani,…lakini nilihisi moyo wangu ukiwa hauna amani, sijui kwanini,..hata hivyo nikasema labda ni hayo mawazo, ya rafiki yangu…nikasimamisha gari…,lakini akili ikawa haitulii…

‘Huyu kijana kasemaje, ‘shemeji naye alileta gari..’ naye shemeji, rafiki yangu shemeji..shemeji, shemeji….si alisema shemeji, au sikumsikia vyema, huyu shemeji atkuwa ni nani, ni mume wangu, hapana, mume wangu yupo kazini,…ana kikao muhimu sana, hawezi kutoka, aliniambia, hatatoka kazini mapema..

Nikataka kumpigia simu mume wangu, ili nihakikishe,…lakini nikaona nitamsumbua tu, sasa hivi atakuwa kati kati ya mikutano yake…nikaachana na wazo hilo, nikaingie hapo, sokoni-duka, na kununua vitu nilivyovitaka.

‘Oh, nimekumbuka , huyo atakuwa ni shemeji… mdogo wa mume wangu ..’nikasema kwa suti, niliwazia hivyo kwasababu huyo kijana kipindi fulani nilifika akawa analisafisha gari langu na mara mdogo wa mume wangu akafika, na aliponiona akasema

‘Shemeji kumbe umeniwahi, basi ngoja amalize, na mimi nitafutia, vipi shemeji hatuonani…’akasema na tukawa tunaongea, na huyo kijana alipomaliz kusafisha, akafika na kusema

‘Shemji zamu yako…’alipotamka hivyo sisi tukacheka,…basi akawa kila akionana na huyo shemeji yangu anamuita hivyo shemeji…sasa sijui kuwa alikuwa na maana ya huyo shemeji au la…mmh, shemeji, shemeji..hapa kuna kitu, kimejificha, nah ii itakuwa ufungua wa kuupata ukweli.

Sikuwa na tabia ya kumdhania mtu vibaya,… hasa mume wangu, au huyo rafiki yangu, niliwaamini sana, kutokana na jinsi tulivyoishi,…mume wangu ni mwaminifu sana, na namuamini kwa hilo,sikuwa na shaka naye hata kidogo, licha ya tabia hiyo ya kulewa, ambayo ilianza baadae tu…hata sijui ni kwanini,  lakini binadamu bwana….

Kiukweli hadi hapo sikutaka kuingia na dhana mbaya dhidi ya mume wangu, wala rafiki yangu…ndivyo nilivyokuwa, utaniona ni mtu ajabu lakini , sijui nisemeje, na ilinisaidia sana kuwa na tabia hiyo kipindi , hadi lilipotokea hili tukio.


Mimi mwenyewe ili kulimaliza hilo akilini, ili nisije kuingiwa na shetani mbaya wa dhana chafu,  nikahitimisha kichwani kwangu kuwa, huyo aliyefika pale nyumbani kwa rafiki yangu atakuwa ni mdogo wa mume wangu, na kwa kujiridhisha tu, nitarudi kwa huyo kijana tena kumuulizia vyema au nitakwenda kwa shemeji, yaani mdogo wa mume wangu. Hilo nikalimaliza hivyo kichwani. Lakini bado nikasema;

‘Huyu rafiki yangu kuna kitu ananificha..na hicho kitu ni zaidi ya tulivyokubaliana, na nafsi yangu haitatulia mpaka nikigundue, nitakigundua tu,..’


 Wakati huo naendesha gari kulekea nyumbani….mara simu yangu ikaita, na kuangalia nikakuta ni mmoja wa wateja wangu , nikaipokea simu, muda huo ndio nataka kuingia kwenye gari,

‘Unasemaje,…nini, ajali, …wewe una….hapana, sijasikia,…ndio naelekea huko, wapi lakini…’ nikahisi kitu kama kikigonga kichwani, kizungu zungu,…sikujitambua, baadae nafungua macho najikuta nipo nimelala chini, watu wamenizunguka.

‘Ajali….!!!’ Nikajikuta nimesema hivyo, kwa haraka nikainuka kutaka kuingia kwenye gari langu.



WAZO LA LEO: Ni kweli tunahitajia kitu, ni kweli tunataka kupata lakini je ni sahihi kupitia njia ambayo sio sahihi, kwa vile tu, muda umekwenda, kwa vile upo kwenye shida, kwa vile tu…je unauhakika utakipata na kuishi muda wa kukifaidi hicho kitu…..tuwe makini na mambo tunayotenda huku tukiangalia uwepo wetu hapa . Tumuombe mungu atupe hekima ya kutafakari mambo kabla ya kuyafanya Aamin.
Ni mimi: emu-three

No comments :