Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 20, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-11


Basi niliondoka hadi nyumbani, namkuta mume wangu kazidiwa shinikizo la damu, ikabidi nifanye jitahada nyingine za kumuita docta, hakutaka nimpeleke hospitalini, akaja docta, akasema kweli shinikio la damu lipo juu, kwahiyo apate dripu…

Baadae hali ikawa shwari, ikabidi nikae naye kumuhoji hili na lile, nilichelea kuongea naye maswali yanayoweza kumtatiza hata docta alinionya kwa hilo, lakini kuna swali lililokuwa kichwani mwangu;;

‘Nikuulize kitu samahani lakini..kwani shemeji ana tatizo gani?

‘Ndio mume wako, naona kama …ana matatizo, wewe ni rafiki yangu, na lako ni langu, niambie ukweli …?

‘Hapana, mimi si ninaona tu…alivyo, sio yule shemeji niliyemzoea, anaonekana hana raha kabisa…’akasema

‘Mhh, nahisi kuna tatizo kubwa sana linamsumbua, jaribu kuwa naye karibu, sio vizuri rafiki yangu, mimi nawajali pia..

Kumbukumbu hizo ziliuteka ubongo wangu, na kiukweli sikuwa na amani kabisa..,Japokuwa mpaka hapo sikuwa na wazo baya dhidi ya rafiki yangu…ila nilianza  kuamini kweli mume wangu ana matatizo..na hilo ndilo nililipa kipaumbele, vipi nitaweza kumsaidia mume wangu, maana hiyo hali iliyojitokeza ikiendelea hivyo, kweli naweza kumpoteza mume, …niliwazia zaidi kwenye afya yake

Basi nilipoona mume wangu katulia, na anaongea vizuri, nikamuuliza

‘Hivi mume wangu,  hebu niambie,…. kuna tatizo gani linalokusumbua…?’ nikamuuliza

Mke wangu matatizo ni ya kawaida tu, …tulishayaongea haya,…na mimi  sitaki ukwazike kwa hilo, na sijui kwanini leo hali yangu imekuwa hivi,..nijitahidi isitokee tena, lakini kuna mambo mengi yamenizonga, lakini yataisha tu, nitayamaliza kwa vyovyote iwavyo…’akasema

‘Huo ni ugonjwa, halafu unasema utajitahidi isitokee tena, na tatizo hilo, ninavyoona sio bure, nahisi kuna kitu kinakusumbua,…sasa usipotaka kunishirikisha mimi, eeh, hebu niambie,…ni nani mwingine anaweza kukusaidia, zaidi ya mkeo …’ nikamwambia.

‘Usijali mke wangu,…wewe endelea na kazi zako tu, najua una mipangilio yako mingi sana, …, na sitaki mimi niwe sababu ya kukukwamisha…’akasema

‘Hujanisaidia kwa hilo, maana sasa sitaweza kufanya kazi zangu kwa amani, nitakuwa na mashaka muda wote, usiponiweka wazi…utanifanya na mimi nianze kuumwa.

Basi nikaanza kuwa karibu na mume wangu na kumuomba samahani kama mimi ndiye chanzo cha hayo yote, na siku moja akaniambia;

‘Mke wangu, uwe na amani, najua yametokea mengi, ambayo huenda hata mimi sikupenda yatokee, lakini isiwe sababu ya wewe kukatisha shughuli zako, muhimu ufahamu sijapenda yatokee, na kuumwa kwangu hata mimi ninaanza kuogopa, inabidi nibadilike..’akasema

‘Ni kitu gani kinachokusumbua, hebu niambie kwanza…?’ nikamuuliza

‘Kifupi hakuna…nimeshazoea, na…hakuna tatizo, …’akasema na sikuweza kuwa na amani tena…hasa nikikumbuka zile kauli za rafiki yangu, na sasa ninaona kweli mume wangu ana matatizo,…

Kwasababu ya hayo matatizo, nikawa sina muda wa kumfuatilia rafiki yangu tena, kumbe alishaondoka kwenda Zanzibar.

Na siku baadae nikamtembea rafiki yangu, katika kupoteza mawazo, na katika kuongea tukajikuta kwenye yale mazungumzo yetu, tukafikia pale pale…nikamuuliza

‘Unajua siku ile tulipoongea ukanipa ushauri kuwa niwe makini naweza kumpoteza mume wangu, imenifanya nianze kujirudi, nimewaza sana, naona kweli nitakuja kuumiza mume wangu…’nikasema

‘Nilikuambia lakini…sasa kwanini unaendelea kufanya hivyo, na je mume wako anaendeleaje…?’ akaniuliza

‘Hajambo hajambo kabia…na  huwezi kujua ni yule siku ile nilimkuta kitandani akiwa kama kapoteza fahamu, ..shinikizo la damu ni baya… siku ile hata mimi niliogopa, maana alikuwa kama anataka kukata roho…’nikasema

‘Oh,… lakini ni nini tatizo…?’ akaniuliza

‘Mpaka leo sijafahamu…na hata sielewi, unajua kuna kauli alisema…lakini sio sababu nahisi kuna jingine..lakini hizo kauli zimenifanya niwaze tu, …japokuwa sizani kama zinaweza kuwa ndio sababu..’nikasema

‘Kauli gani hizo mbona huzitaji…?’ akaniuliza

‘Unajua kuna kitu, …mume wangu anatamani sana, kimojawapo ni hicho, ya kuwa anatamani kupata  mtoto wa kiume…na kingine ambacho hatusikilizani, yeye bado, anapenda ujana ujana,….hajui kuwa umri umekwenda…hilo sijui wanaume wengi kwanini haalioni…mzee mzima bado upo na mambo ya vijana.., mimi namemuambia sina muda huo…’nikasema

‘Mhh kwanini unafanya hivyo, unafanya makosa, maana mume wako ni mwenza wako mwatakiwa mshirikiane, mfurahishane, sasa kama anataka hivyo akaende wapi, ndio maana wanakimbilie mitaani, ..hili hulioni wewe…?’ akaniuliza

‘La kujiuliza ni hili mambo hayo, eeh yana faida gani kwetu, kwa umri huu…sawa kama ni watoto tutapata tu,….mungu akipenda, … ila nilitaka nimalizane na mipangilio yangu ili tukianza kuzaa, nisiwe na hangari hangari nyingine ndio mpangilio wangu, nimejifunza kwnye mimba hiyo ya kwanza, …na hilo nilishamuambia…’nikasema

‘Ina maana hilo ndilo la kufanya usiwe karibu naye,…hilo ndilo linakufanya  usitimize haki za ndoa, ambazo ndio msingi wa ndoa au …’akasema

‘Unasema nini.., nani kakuambia kuwa sitimizi haki za msingi za ndoa..?’ nikamuuliza kwa mshangao.

‘Nakuuliza sio nasema mimi, nakuuliza wewe, na …’akasema na kabla hajamaliza nikasema;

‘Umeyajuaje hayo,….!! Kwani aliwahi kukuambia hivyo, kuwa sijamtimizia hayo…aah, naona sasa unaingilia mambo yasiyokuhusu…’nikasema

‘Lakini rafiki yangu rejea mazumgumzo yetu tuliyofanya siku  ile, kwani hukuwahi kunigusia hilo,…. au unafikiri mimi nakuzulia au urafiki wetu una mipaka sijakuelewa, …’akasema

‘Ok,…ok… basi labda niliwahi kukudokezea hilo.., sawa, nimekumbuka nilikuambia …hata hivyo hilo mimi nimeshaliona, na nilikuwambia nitalifanyia kazi, kwahiyo lisikuumize kichwa, umenielewa…’nikasema

‘Sawa, ….ni heri ulifanyie kazi, na kiushauri, kama kuna yaliyotokea yakakukwaza, au kama kuna kitu, jaribu kukiweka kapuni, kitupe… nakuomba uyasahau yote mabaya ya nyuma,…hali umeshaiona, hali hiyo inaashiria kuwa ,  sasa hivi uwe karibu naye, na…nahisi inaweza ikaleta heri ukifanya hivyo.., tusameheane tu, maana mengi yanafanyika ili tu, kutimiza adhima…’akasema

‘Nimekuelewa,…’nikasema

‘Unajua nilitaka nikisafiri niwe na amani, niwe nimeacha kiula kitu ni shwari..nisiwe na kitu moyoni mwangu kwako, na wewe kwangu…’akasema

‘Hilo lisikutie shaka, hebu kwanza nikumbushe, siku ile tuliishia wapi…’nikasema

‘Siku ipi tena….mmh, yale tuachane nayo bwana…ndio maana nataka tuhakikishe tumeridhiana, hakuna …jambo la kuumizana kichwa, na ukweli wote, nshakuambia au sio…’akasema

‘Hapana hujambia,..ukweli wote.., maana nakumbuka siku ile ulisema…, alipokuja kwako,…kuna kitu alikuambia ndio kikafanya yeye agundue kuwa una mimba, ni kitu gani miliongea…?’ nikamuuliza

‘Hahaha, na wewe bwana,….hahaha, unajua wakati mwingine nacheka, lakini wakati mwingine najiuliza hivi hili jambo litafikia mwisho tusahau , isije kuleta matatizo huko mbeleni,…na ikileta .. itakuwaje…maana nimejaribu kila njia unielewe, lakini sizani kama utanielewa, kwa hali kama hii…unakuwa mdadisi kwa kitu ambacho ulikanya wewe mwenyewe kuwa jambo hilo liwe siri….sasa labda mimi naona nikuambie kila kitu iwe iwavyo…’akasema

‘Sawa lakini hapo …kuna kitu sijakuelewa…’nikasema

‘Rafiki yangu, hebu nikuulize kwani unataka nini zaidi,..unataka matatizo, unatakaje ili iweje, …wakati mwingine naona ni bora tukae kimia, wakati mwingine naona ni bora niweke kila kitu kwenye meza, ..lakini sitaki  kuumizana , sipendi kabisa…’akasema

‘Kwa hivi sasa bora uniambie kila kitu tu, maana ukiacha ndio utanipatia shinikizo la damu, maana nimekuwa nikijiuliza, na…nilitaka hata niende kuonana na mdogo wa shemeji ili niwe na uhakika fulani, kuna maswali yana nijia, na mimi nataka nimuulize, lakini siwezi kufanya hivyo mpaka nipate ridhaa yako,…wewe huelewi tu, …wewe ni kama mdogo wangu lazima niwe na uhakika na ulichokifanya, ili likitokea la kesho,  niweze kuwa na majibu, ukumbuke kuna leo na kesho…’nikasema

‘Kwahiyo unataka nini hasa, na upo tayari kwa …mimi siwezi kuwa na uhakika na wewe, maana hili linaweza likawa sababu, na mimi sitaki, unielewe hapo, eeh, mmh…nasita kidogo hapo…’ akasema

‘Swali lipo pale pale… ikawaje, usitake tuzunguke,…. huyo shemeji alifahamu vipi kuwa wewe una mimba, na ni kauli gani ilikyokufanya hata wewe ufikie kumwambia, au ilikuwaje…unajua, nimeanza kuandika kitabu changu, natunga true story ya maisha yetu mim na wewe vyema…hahaha, huwezi amini mengi yaliyotokea kati yangu na wewe nimeshayaandika…’nikasma

‘Unasema kweli…?’ akauliza

‘Ndio..ni pale ninapokuwa sina kazi,..akili imetulia huwa naandika, yale yaliyotokea kama hadithi fulani hivi,…sasa hivi nipo kwenye hilo tukio, naona lina maswali mengi yasiyokuwa na majibu, na sehemu hiyo nimeiita, ‘ukweli baada ya ushauri kwa rafiki yangu..’.

‘Mhh, ushauri kwa rafiki yako, ambao umeleta matatizo au, itakuwaje sijui….’akasema

‘Matatizo aah, nani kasema, hakuna kitu kama hicho, ni ushauri ulioleta matunda ya kuleta faraja…huoni sasa una mtoto, usiseme hivyo….’nikasema

***********

‘Kama nilivyokuambia, kuna muda nilikuwa natamani yeye awe anakuja, au nimpigie simu tuongee naye, nikifanya hivyo, nikasikia angalau sauti yake, kama hakuweza kufika, najihisi raha, nakuwa na amani fulani… lakini wakati huo sikutaka hayo yajulikane na watu.., sikutaka watu wanione nikiwa naye tena, naona aibu kuliko wakati wote, nilihisi kama watu watanigundua kuwa ndio yeye…’akaanza kusimulia

‘OK…sawa endelea…’nikasema

‘Siku hiyo alifika akiwa hana raha, nikamuuliza tatizo nini…akasema hakuna kitu ni mambo ya kawaida tu,..ni mambo ya kifamilia zaidi…’akasema

‘Kama huniambii, sitakuwa na amani, siku hizi sijisikii vizuri, nataka wewe ukija uwe na furaha, na kama huna furaha ..ni bora usije ,..na usiponiambia tatizo lako, ni bora uondoke..’nikasema na moyoni nijiuliza hivi kweli akifanya hivyo si nitaumia sana, na mimi nataka awe karibu yangu.

‘Ina maana muda huo mimba bado imejificha,..bado mapema au sio..?’ nikamuuliza

‘Kitumbo bado ile yasana,… ila kimeshaanza kutuna, na mimi sijui kwanini, nilianza kuvaa nguo pana mapema, ..kama  Madera…kitu ambacho wengi walianza kunihoji nakawa nawapa majibu yao, na nikazoeleka hivyo kuwa nimebadilika, siku hizi sio yule mdhungu tena…ilinisaidia, hata dalili zozote zisionekane mapema, na siku baada ya siku …tumbo likaanza kukua…’akasema

‘Safi kabisa, ulicheza hapo maana hata mimi sikuwahi kukushuku awali…’nikasema

‘Nataka unizalie mtoto wa kiume…mjamaa alipofika alisema hivyo…’akasema

‘Mungu wangu alikuambia hivyo…?’ nikauliza nikihema, muhemo, kama vile kauli hio inanihusu mimi.

‘Ndio alisema hivyo na mimi kauli hiyo ilinishika kwa mshangao, lakini sikutaka kujionyesha, nikacheka kweli

‘Kwanini unacheka, akaniuliza…?...’akasema

‘Unanishangaza, ina maana kukuita hapa, umenifanya mimi kama hawara wako,..nilishakuambia yaliyotokea siku ile, mimi sikuyataka na yaninipa wakati mgumu sana, na..na..kwanza ole wenu nilitaka kuwashitaki, mlichonifanyia wewe na ndugu yako, sitaweza kuwasamehe..’nikasema

‘Kitu gani, mbona sikuelewi…?’ akasema

‘Tuyaache hayo…na umesema nini…?’ nikauliza kama vile sijasikia

‘Natamani wewe unizalie mtoto, lakini awe wa kiume..’akasema

‘Nikuambie kitu, hilo kamwambie mkeo, sio mimi…’nikajifanya kuwa mkali,

‘Sikiliza,..najua hata wewe unataka mtoto, nimesikia hivyo..,..unatamani uwe  angalau na mtoto, hata mimi naliunga mkono, maana umri unakwenda au sio, sasa hebu tulia basi…’akasema na mimi muda huo nilikuwa nasimama nahisi kichefu chefu

‘Ni nani kakuambia upuuzi huo…’nikasema nikigeukia upande wa pili leso mdomoni.

‘Wakati mwingine wanawake mpo hivyo, kama hujaolewa kwa muda..umekaa na unahisi umri utakusuta..na sio siri kila mtu anatamanikuwa na mtoto, hata wewe itakuwa hivyo,…hilo lipo wazi, sasa nisaidie na mimi nikusaidie…’akasema

‘Nikusaidie..wewe si mume wa mtu jamani, unataka nini…?’ nikamuuliza na mengi yakaendelea hapo ikawa tena hatuelewani…’akasema

‘Mengi yapi..?’ nikauliza

‘Tulibishana sana kuhusu hilo la mimi kumzalia mtoto, eti tena wa kiume,…hivi hilo si alitakiwa aongee na mkewe…anyaway, tulibishana hapo, na sijui ikatokeaje, nikaanza kujisikia vibaya, kutapika, nikakimbilia washroom, kumbe alinifuatilia kwa nyuma, sasa wakati natapika, ikafikia muda, nikasema;

‘Kama mimba ni hivi, bora …nizae mapema tu..hiki kikombe kinipite…’nikasema na huku nyuma yangu nikasikia akisema;

‘Kumbe una mimba…’akasema,..nilishtuka, karibu nizimie, na akaja haraka kunishika ili nisidondoke, na alipohakikisha nipo salama akasema;

‘Oh, sasa niambie ukweli,…kumbe una mimba , kumbe ni kweli…mmh, nishathibistha inatosha, sasa niambie ukweli  ni yangu au kuna mwingine…’akasema

‘Mimi sio Malaya bwana…’nikasema

‘Ndio maana nauliza isije kuleta matatizo..najua mimi nimeshatembea nawe, sina uhakika na mwingine je ni ya kwangu au kuna mwingine…?’ akaniuliza

‘Mimi sijui, maana mlichokifanya wewe na ndugu yako siku ile mimi sijui, mimi sijui na sitaki kujua, niache, ushaiharibu siku yangu  , ondoka…’nikasema

‘Basi natosha, ninachoomba kwa mungu awe mtoto wa kiume…’akasema hivyo, na hakutaka kukaaa sana, akaondoka akiwa anaonekana ana furaha usoni , sio kama alivyokuwa amekuja.

‘Kwahiyo hebu kwanza nikuulize kuna jambo nilitaka niwe na uhakika nalo..hivi ulipogundua kuwa una mimba, ulikwenda kupima wapi, maana nataka mambo haya yawe kwenye kumbukumbu zangu, hapo kasema, ‘kumbe ni kweli’…’nikasema.

‘Kwanini unauliza hivyo…ina maana kweli kuna kitabu unatunga, au unataka jambo kama ushahidi fulani, ushahidi wa nini…?’ akaniuliza.

‘Nimeshakuambia naandika tu  kujifurahisha, nilianza kama mzaha tu, lakini kadri siku zinavyokwenda naanza kufurahia,… na hasa hii kadhia, kuna muda.. inaniacha kwenye maswali mengi ya kutaka kujua zaidi,..unajua tena…na hata hivyo ni kawaida yangu kuwa na kumbukumbu, na  usinifikirie vibaya, kwanini nafanya hivyo, au hupendi, niwe naandika, kama hupendi nitaacha tu…’nikasema

‘Ok.. nilikwenda kupima kwenye  ile hospitali iliyopo karibu na kazini,…na nilifanya hivyo kwa vile sikuwa na amani, nilikuwa sijisikia vibaya vibaya, hali ambayo sijawahi kuihisi kabla, huko kupoteza siku zangu , inatokea mara kwa mara kwahiyo haikuwa ni sababu…hata hivyo wakati naenda kupima, nilikuwa kama siamini, maana …kama tukio lilivyokuwa ilikuwa kama ni ndoto…na sikuweza kuwa na uhakika, niweke hivyo tu…’akasema

‘Hukuwa na uhakika gani kuwa ni nani kati ya hao ndugu wawili au si..…au hukuwa na uhakika kwa vile..haiwezekani ulisema ..kitendo kilikuwepo au sio, … hapo usinidanganye kitu…mpaka hapo nahisi kuwa kuna kitu unanificha, halafu unajinasa mwenyewe  hiyo kauli ‘sikuwa na uhakika..’nikasema

‘Nimekumbuka kitu…siku ile nilipokwenda kupima nilikutana na docta ambaye nafahamiana naye, naye kuna kipindi tulikuwa naye karibu baadae ndio akaoa, nikaachana naye,…sasa nikuchekeshe kitu,....’akasema.

‘Nichekeshe…’nikasema

‘Kumbe yule docta ni best sana wa shemeji….’akasema

‘Shemeji,…una maana huyo bwana’ko…?’ nikauliza

‘Na wewe bwana…sio bwanangu huyo..,..mwishowe utazoea hiyo kauli, mimi siipendi…’akasema

‘Samahani, naongea hivyo kwa vile tupo wawili wala usiwe na shaka…’nikasema

‘Sasa nahisi..au nilihisi huenda waliwahi kuongea kuhus mimi, kuwa nina mimba, nahisi hivyo kwa vile siku nilipokwenda kupima,..jana yake, au siku baada yake, nakumbuka,  mjamaa aliniuliza…. , japokuwa hakuwahi kuniambia kuwa kagundua kuwa nina mimba..na nijuavyo aligundua hilo baada ya siku hiyo wakati alipokuja, na kuanza kuongea hayo kuwa anataka nimzalie mtoto…’akasema

‘Mhh, ...mambo ya huyo shemeji  hayo….yanafanana sana na mambo ya mume wangu, , unajua hata wakati naandika, nikawa najiuliza huyo mtu  ni nani,  sura ya mtoto inafanana na familia yangu, ina maana huyo baba yao, eeh, atakuwa anafanana na mume wangu, …na na…hili tena,….unajua mume wangu ni rafiki mkubwa wa huyo docta wa pale…walisoma wote…’nikasema.

‘Ndio hivyo….mmh, sasa…mmh, unajua  yote haya ni kutokana na ushauri wako, nisingelifikia hatua hiyo, wakati mwingine nafikia kujilaumu ni kwanini nilikusikiliza, ….usinielewe vibaya hapo kuwa sikuupenda huo ushauri wako.., ila nasema haya kwa vile naona kila hatua kuna mtihani fulani na naona inaweza ikafikia sehemu…hata sijui itakuwaje……’ akasema

‘Ni wasi wasi wako tu….unafikiri, unajua hayo yote nayafahamu na …kukushauri kwangu sikuwa na nia mbaya, nilijua haya yanaweza kutokea hivyo..na mimi nitayapokea kwa jinsi yalivyo, siwezi kukulaumu kwa lolote lile, unasikia,.., kwahiyo, wala usiwe na shaka kabisa…’nikasema

‘Kwahiyo unataka kusema nini hapo.., kuwa unajua ni nani, na huna shaka lolote kwa hilo…yaani hutanifikiria vibaya , tukaja kukosana…?’ akaniuliza

‘Hebu nikushauri kitu,  hebu kwanza nihakikishie kwa huyo shemeji ni nani , ili niweze kupanga jinsi gani ya kumweka sawa, mimi nataka nije kuonana naye, ili niliweke hili jambo sawa, sawa..’nikasema

‘Mhh..kumbe bado…’akasema

‘Ni hivi…ninachoogopa ni wewe unaweza ukavuruga huu mpango kabisa…, wewe unachukulia hili jambo kirahisi tu, hujui ni jinsi kwenye mwenye mume atakavyojisikia akiligundua hilo, unataka mim nije kujuta kwanini nilikushauri, sitaki itokee hivyo kamwe, unasikia,...sasa nataka uniambie ukweli huyo shemeji ni nani?’ nikamuuliza.

‘Na wewe bwana , hapa nilijua unasema umeshamfahamu, na ulijua kitu kama hicho kinaweza kutokea,…ulikuwa na maana gani,..mimi naona haya tuyaache tu, yasije kukutia presha?’ akasema

‘Mimi nishakuambia ..kwa hisia zangu ni huyo mdogo wake mume wangu, kwasababu nyingi tu, kuanzia kufanana watoto na tukio zima kama ulivyoliezea, na , naaeeh…sioni mtu mwingine anayefanana na hivyo,… labda uniambie wewe, ni nani huyo, na kwanini…eeh,  unaona ugumu kunihakikishia kuwa ni yeye, …mimi siwezi kufanya lolote, maana hanihusu kwa sana, japokuwa ni mume wa mtu,…hawa wanaume jaman…’nikasema.

‘Lakini…mbona umesahau kuwa ulinishauri hivyo, ukisema hawa waume jamani, unanishutumu na mimi au…’akasema

‘Ndio hivyo, ila …ukweli upo pale-pale, inauma sana, tena, sana, sijui ikitokea kwangu kama nitaweza kuvumilia, mimi aah, ..mimi siwezi,…ndio maana nilitaka nimfahmu huyo mtu ili madhara yasizidi kuendelea, umenielewa hapo…nataka niongee naye,nitajua jinsi gani ya kumweka sawa,…haya niambie ni nani huyo mtu….?’ nikamuuliza


‘Ni shemeji jamani…nimeshakuambia ni shemeji’akasema, na kusimama, kama anataka kuondoka,…sijui kwenda wapi,  akageuka kuniangalia na mimi nikawa nimemuangalia, tukawa tunatizamana…


Kiukweli  mpaka hapo bado mimi sikuwa na tashwishwi yoyote mbaya, maana kwa hilo neno ‘shemeji’ ndivyo alivyo kuwa akimuita huyo jamaa yake tangia awali, na nikajua anamuita hivyo kutokana na mimi, kuwa ni mdogo wa mume wangu…lakini bado naona kama anaogopa kunibainishia hilo, na kwa namna hiyo akazidi kunipa hamasa.

‘Hahahah, nilijua tu, kwahiyo sasa umenihakikishia, kuwa ndio yeye, au sio….marafiki wawili wana waume kutoka familia moja, japokuwa…wewe unapita tu, hahaha…kiukweli, nimefurahi, japokuwa,…mmh, namuonea huruma sana mke wake….’nikasema na mara ujumbe wa simu ukaingia kwenye simu yake, akausoma, na mara kwa haraka akasimama, akiangalia kule mlangoni, sikusikia sauto ya gari…kwahiyo sikuwa na mashaka kuwa kuna mtu kaja…

‘Unajua, …kuna mgeni anataka kuja, na sikutaka akukute hapa, wewe au mtu mwingine, na huyu mtu kawahi kabla ya muda,ujuo wako sikuwa na …..sasa sijui kwanini, mbona hivi…’akasema akijaribu kupigia simu, nahisi kwa huyo mtu,  lakini naona simu ilikuwa haipokelewi..

‘Kwani una nini, mbona huna amani , ni nani huyo mtu…?’ nikamuuliza

‘Hata sijui itakuwaje…na nilishamuambia asije hapa mpaka nimpe nafasi, au aniambie kabla, sasa anajileta tu, mbona huu mtihani.’akasema sasa akiangalia mlangoni


‘Kwanini, mimi si rafiki yako…na huyo shemeji,…niambie ukweli..’nikasema

‘Ndio yeye….’akasema

‘Safi kabisa, …hilo sasa niachie mimi, wala usiwe na shaka,…na kwa vile mume wangu hajui kuwa nipo hapa, ..nitamtumia ujumbe kuwa nimepitia mahali, sitamwambia kuwa nipo hapa, nataka hili jambo tulimalize leo hii, au sio…’nikasema

‘Ina maana mume wako, hajui kuwa upo hapa, umekuja huku bila kumuambia, kwanini lakini,  …?’ akaniuliza kama ana hamaki

‘Nilikuwa na kikao na muwekezaji mmoja, na bahati kikao hakikufanyika kwahiyo yeye anafahamu nipo kazini..mimi kwa hasira…maana huyo muwekezaji kanipotezea muda wangu maandalizi, halafu analeta ujumbe mwishoni kuwa kaahirisha kuja..ameniboa kwa kweli,…’nikasema

‘Mhh….’akasema akiangalia simu yake naona alitarajia kupata majibu fulani lakini hayaji.

‘Sasa sijamfahamisha mume wangu kuwa nimetoka, ngoja…nimtumie ujumbe…’akasema akiandika ujumbe kwenye simu…akatuma na kusema

‘Leo simu ya mume wangu haipo hewani, kulikoni…’nikasema

‘Labda kwa vile…’akasema na kusita….kwani mlango uligongwa


‘Huenda ni shemeji,...mungu wangu…’akasema

Nikiwa natabasamu tele mdomoni macho yangu yakaelekea kule mlangoni, nimuone huyo shemeji, akilini kwangu najua ni huyo huyo, mdogo wa mume wangu….shemejiiiii…

Nikamtupia jicho la pembeni rafiki yangu  nikamuona akiwa anahangaika hana amani kabisa, sikuelewa ni kwanini, labda ni kwa vile hakutaka nikutane na huyo shemeji, lakini kwa muda huo sikujali, nilijua nitalimaliza nikikutana na huyo mtu, sasa nilimuona kama anataka kwenda kule mlangoni,...huku mkono mmoja kashikilia mdomoni…!!!


WAZO LA LEO: Tunapopeana ushauru, au tunapotoa ushauri tuhakikishe hicho tunachokifanya tuna uhakika nacho, kiimani ya kweli(kwenye dini zetu), au kiutarataibu uliokubalika na jamii zetu,  ili matokeo yake yasije kutuathiri sisi wenyewe au kuonekana watu wa ajabu katika jamii zetu. Lakini muhimu tuangalie je mola analiridhia hilo, je ningelifanyiwa mimi ningerizika nalo… 

Ni mimi: emu-three

No comments :