Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, October 18, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-10


‘Huyo aliyeingia alikuwa ni nani, si huyo shemeji au…huyo aliyekufanya sasa una mtoto, si ndio huyo, hutaki kuniambia lakini mimi nimeshamfahamu...si ndio huyo, mdogo wa mume wangu au sio?’ nikamuuliza

‘Hapana....'akasema

'Ni nani sasa.mbona sikuelewi...?' nikamuuliza

'Alikuwa mdogo wa huyo jamaa,…'akasema

'Mdogo wake...!!!'nikasema kwa mshangao

'Ndio, na tena kaingia huku kafunga taulo, kiuonini, …na tabasamu tele mdomoni, kama vile nilikuwa naye usiku kucha,....na sasa ana...yaani mimi  nilihisi kama kutapika, nikawa na hisia za ajabu,..nikawa nahisi huenda walinifanyia kitu kibaya hao watu…’akasema

‘Mbona sielewi, na  huyo..unayemuita shemeji...alikwenda wapi, ina maana watakuwa walishirikiana hapana hawawezi kufanya hivyo, sio watu wabaya kiasi hicho au…?’ nikauliza

‘Kwa muda huo akili ilikuwa hivyo, inadhania hivyo....sikuelewa kitu kwa muda ule, si unajua tena ukiamuka kutoka usingizini, , …hapo ilivyo, akili yangu ilinifanya nielewe hivyo kuwa walishirikiana,...'akasema

'Lakini sio kweli...'nikasema

'Mhh...ngoja niendelee...maana hadi sasa nahisi hasira,...kama ilivyokuwa siku ile, nilipomuona huyo mtu, akili yangu ikajawa na ..., hasira chuki, ..nahisi kuzalilika,..na hasa pale nilipogundua kuwa nipo kama nilivyozaliwa, nikarudi kitandani na kunywea, na huku akilini nikijiuliza kulitokea kitu gani..na kama kuna kitu kilifanyikabasi watu hao, watakuwa wametangaza vita na mimi,….mimi sio mtu wa kuchezewa hivyo…’akasema

‘Kaka ameshaondoka, ,…alisema nije nikuangalie kama umeshaamuka..na kama unahitajia lolote uniambie niweze kukusaidia, ..’akasema na sikumjibu kitu, na jamaa akataka kusogea kuja pale kitandani, nikainua kumuangalia kwa chuki, akasimama, hakusogea tena.

'Eeeh, imekuwa hayo...'nikajiukuta nimesema hivyo.

'Nilimuambia kwa ukali, kwa ishara ya mkono,....

'‘Naomba utoke humu ndani kwangu  kwa haraka…’nikasema, kwa msisitizo

‘Oh,….imekuwaje sasa…ok.ok…hakuna shida,… ila nilitaka kuhakikisha tu kuwa upo salama, mimi nitaondoka tu,…sina nia mbaya, kwanza hata mimi nahitajika nyumbani haraka, si unajua tena…’akasema

‘Na ole wenu,….kama mlinifanyia chochote kibaya, mtanitambua kuwa mim ni nani….’nikasema

‘Kibaya, ....!!! Hapana,...shemeji.... yote yaliyofanyika kwa ridhaa yako, …na ok, mtaongea na kaka, mimi ngoja nikavae, niondoke , hamna shida, ….’akasema akirudi kinyume nyume karibu ajigonge mlangoni

‘Kwa ridhaaa yangu….’nikajikuta nimesema hivyo, na wakati huo mjamaa alishatoka ndani kwangu,

Nilijikagua,....kiukweli, sikuwa na hali mbaya....ila nilisi vibaya tu...na nikaona iliyo bora ni kwenda kuoga...basi nikaenda nikaoga, huku nikiwaza na kuwazua,,,, kilichotokea jana ni nini,...je sijafanya mambo ya aibu...

Na maji yalipomwagika mwilini ndio nikaanza kumbukumbu, ...akili ikianiz  kwenye sherehe,....oh, nikahema, ...nikawa najidadisi, je sikufanya jambo la aibu mbele ya wafanyakazi wenzangu pale ukumbini...hapana....hilo nalikumbuka vyema, je  baada ya hapo….

‘Oh mungu wangu…’nikajikuta nikisema hivyo na kurudi kitandani,...kujilaza, uzuri siku hiyo ilikuwa ya mapumziko...na nilipotulia vyema ndio taswira ya tukio nzima ikaanza kunijia akilini…

**********

 Nilianza kukumbuka, kuwa nilikunywa kupitiliza, na hata  tulivyofika nyumbani ilikuwa ni kwa shida, kama isingelikuwa huyo mdogo wake shemeji sijui ingelikuwaje, japokuwa nay eye alikuwa kalewa pia, lakini sio sana, …

Tulipofika nyumbani, gari likisimama , kwa muda ule sikujua tumefika, nikawa nafoka, kwanini kasimamisha gari, dereva ambaye ni mdogo wa shemeji akasema tumeshafika, …basi nikawa najitahidi kutoka kwenye gari, ni mshike mshike..hata nilipotoka nje,..mmh, sikua vyema nayumba.

Hapo nikajua wataondoka wataniacha …nilianza kutembea kuelekea ndani huku nayumba, shemeji naye huyo, akawa keshateremka kwenye gari...akawa ananifuata naye hivyo hivyo, anayumbe, akanishika nikawa najaribu kumkatalia asinishike,..uhimili wa miguu yetu ukahindwa,... sote tukaserereka chini.

'Hahahaha...kama nilikuwepo....'nikacheka

‘Sasa wewe vipi…’nikasema, nikimuambia shemeji, hapo kanilalia, .. tukaishia kucheka, hapo tumelala chini, na mdogo wake shemeji ndio akaja kutusadia kusimama mmoja mmoja..., haya…mzobe mzobe hadi ndani kwangu...pombe mbaya jamani, narudia tena kauli hiyo...'akasema

‘Haya ondokeni…’nikasema tulipoingia ndani…

‘Haondoki mtu hapa….leo tunalala hapa hapa…’akasema na mdogo mtu akashangilia, ujue wote hao wana wake zao, wanafamilia zao...

  Kwa muda huo hata sikutaka kubishana nao...macho manzito, yanatamani kulala tu..., mimi nikakimbilia chumbani kwangu…nashangaa mjamaa naye huyu hapa, kaniganda, na tukajikuta tupo kitandani kwangu…kilichotokea hapo,..aaah, hata siwezi kuongea, maana ilikuwa kama sinema fulani …’akasema.

‘Hongera,…ikawaje sasa maana mlilewa, iliwezekana siku hiyo...sizani , maana mlikuwa bwiii..au ilikuwaje...?’ nikamuuliza

‘Mhh, kwani hapo nakumbuka, siwezi kukuficha, sikumbuki sikumbuki ndio maana hadi sasa najiuliza.., …..ila kumbukumbu za baada ya hapo zipo,…'akasema

'Unanificha...'nikasema

'Kunaaaah, ....muda, ndio... nahisi ilikuwa usiku sana, nilishituka,…akili kidogo zilikuwa zimerudi, kichwa kinaniuma kweli..,..najikuta kuna mtu kalala pembeni yangu…hapo natamani,..sijui kutapika, kichwa, kichwa...’ akasema

‘Hahaha…pole sana nyie mwafikiri pombe ina mema, ..ni shida, sijui kwanini mnaendekeza kunywa..haya ikawaje..?’ nikauliza

'Kichwa, kichwa kinauma,...'nikalalamika, na jamaa akajizoa zoa, na kwenda kuniletea maji, akaniuliza nina ..dawa ya maumivu,...nikamwambia ipo ...akanichukulia nikanywa, nikatulia kwa muda, baadae kikapoa kidogo.

‘Hapo...., akili zimesharudi, nikamwambia aamuke aondoke..lakini akasema hawezi kuondoka usiku huo,…nikatoka kujisaidia, vyoo ni ndani kwa ndani,  lakini , nikawa na wasiwasi, nikaelekea varandani, ..nashangaa kuna mtu kalala kwenye sofa.

Nikaanza kukumbuka pale ilivyokuwa, hapo hapo nikamuamusha mdogo mtu, ili waondoke.., lakini shemeji hakukubali, akasema hawezi kuondoka usiku huo hata hivyo alishamuambia mkewe atalala kazini…nikaona isiwe shida, ..sijui ilikuwaje, nakumbuka nilisikia kiu, nikataka kunywa kitu…nikasikia shemeji akisema

‘Bwanamdogo mpe kinywaji atulie…’akasema

Kweli mdogo mtu akaniletea kinywaji,  nikanywa, …haikuchukua muda,...nahisi kama kilevi kilikuwa sio cha kawaida, maana nililegea ..hata sijui ilikuwaje,ila nahis kuna mambo yalifanyika tena hapo..sina uhakika, …ukumbuke hapo ilikuwa varandani, sasa naamuka asubuhi, najikuta nipo kitandani kwangu, nimelala, nipo kama nilivyozaliwa, je ilitokea nini..na hapo sikumbuki vyema imekuwa mtihani kwangu,…’akasema

‘Ikawaje sasa, tuache hizo pazia unazoweka, hazina maana kwangu, ilikuwaje…?’ nikauliza

‘Ikawaje, ikawaje, ikawaje... ..ndio hivyo, asubuhi, huyu mdogo mtu nikamuambia aondoke, nikabakia peke yangu….’akasema

‘Mhh,… wanaume hawa bwana, …nakumbuka siku moja mume wangu alikuja na mdogo wake, naye akiwa amelewa bwii, sikutaka hata kuongea naye, nikamwambia alale huko huko sebuleni,….sikutaka shida, …kama huyo yupo hivyo, achana naye, ilimradi kakupatia mtoto basi inatosha, mwanaume mlevi ni tatizo, anaweza kukuleta magonjwa…’nikamwambia.

‘Nikuulize kitu samahani lakini..kwani shemeji ana tatizo gani?’ akaniuliza. swali lake lilikuwa kama kitu cha kushitukiza ni kitu sikutarajia kuulizwa, nikawa kama nimeshtuka, nikajikuta nikisema;

‘Nani shemeji, mume wangu kakuambia nini…?’ nikaamuuliza

‘Ndio mume wako..., naona kama …ana matatizo, wewe ni rafiki yangu, na lako ni langu, niambie ukweli …kuna tatizo gani kati yenu wawili?’ akaniuliza

‘Matatizo ni ya kawaida tu..leo hili kesho lile mimi nimeshajizoelea tu, kwani umemuonaje, sizani kama alipokuja hapa mliongea kitu, au kwanini unaniuliza hivyo…?’ nikamuuliza

‘Hapana,....mmh, ... mimi si ninaona tu…alivyo, sio yule shemeji niliyemzoea, anaonekana hana raha kabisa…nahisi kuna tatizo kati yenu wawili , niambie ukweli....’akasema

‘Ungemuuliza yeye kwanza,...maana mpaka unauliza hivyo si ina maana mlikaa mkaongea au...na ni  shemeji yako,..kwanini hukumuuliza...'nikasema

'Aaah, ina maana hutaki mimi kukuuliza mambo yako...'akasema

'Sijakuambia umefanya vibaya,.... mimi nimemuuliza anasema yupo sawa,..hebu jiuliza  kama wewe mtu baki umemuona hivyo, je mimi ninayeishi naye,…kiukweli mimi sitaki kujisumbua tena kichwa changu, maana nina mengi ya kufanya,..hayo nakuomba tuyaache tu nitayamaliza mimi mwenyewe, kwa muda wake,..., nashukuru kwa kuliona hilo…’nikasema

‘Mhh, nahisi kuna tatizo kubwa sana linalomsumbua shemeji..., jaribu kuwa naye karibu, sio vizuri rafiki yangu, mimi nawajali pia...’akasema rafiki yangu huyo.

‘Unafikiri,....mbona nalifanyia kazi...nimeshaliona hilo, na yeye,...nimeshajaribu kumdadisi,... hasemi,... sasa nifanyeje, na sitaki hata kumuuliza zaidi, …kwa hivi sasa nimeamua akili yangu yote kwenye mambo ya kimaendeleo , kwa ajili ya familia yangu basi, muda utafika nikiona mambo yamekaa vyema nitalijadili, na yeye aniambie kwanini hataki kusema ukweli, ana tatizo gani…’nikasema

‘Kama ni hivyo huyo mtoto wa kiume mtampataje…?’ akaniuliza swali ambalo, pia lilitoka na kunifanya nishtuke, sio kwamba ni swali la ajabu, lakini nakumbuka kauli hiyo aliwahi kuitamka mume wangu, wakati tunazozana, ilinijia tu hivyi, lakini sio kwa kudhania ubaya...

Nakumbuka katika kuzozana zozana na mume wangu, kuna kipindi alitoa kauli hiyo...

‘Mke wangu, hivi kwa hali kama hii, ..tutapataje huyo mtoto wa kiume,…kila siku uko na kazi nyingi, umechoka,…unanifanya nifanye hata nisiyodhamiria kuyafanya,…’akasema

Kiukweli kauli hiyo ilinifanya niwe kwenye wakati mgumu, kama binadamu, kama mwanamke, nilihisi kweli nimekosea, lakini hata hivyo kama mwanamke nilihitajika kubemebelezwa, sio kwa vile mimi ni mke wake basi iwe hivyo, ni mambo ya ndani sitaki kuyasema zaidi,, lakini kiukweli  …hayo niliwaza tu, sio kwamba niliongea na rafiki yangu.

Pale mimi nikasema;

‘Achana naye…kama yeye kaamua hivyo..., na kaona hiyo ndiyo starehe yake ya kulewa, na pombe  ndio kila kitu basi aendelee, sitaki tena kumuingilia, sana muda utafika lakini sio kwa sasa, kwa sasa kuna mambo yananiumiza kichwa...'nikasema

'Hilo ni muhmu sana rafiki yangu....'akasema

'Nikuambie kitu, mimi sio mtoto mdogo, ...kulikuwa na wakati wa hayo....sasa hivi sisi ni watu wazima, lazima tuwe ni kipaumbele cha kujali ni nini baadae,...sasa nikimueleza mwenzangu haelewi, sawa, ana mambo yake..lakini...hajayatilia maanani kihivyo....'nikasema

'Lakini ulisema kuwa anajitahidi kwa kazi, ndio maana kafungua ofis yake...'akasema

'Sasa hiyo ni baada ya kuongea sana..na akicheza atashindwa,...kama ataendekeza pombe, najua yeye ulevi wake ni pombe, sizani kama ana ulevi mwingine,...kwa hivyo, basi...naona ni sterehe yake, nimemuacha  aendelee nayo...'nikasema

'Aakirudi inakuwaje...mnalala pamoja...?' akanuliza swali jingine lililonifanya sasa nicheke sana.

'Hahaha, wewe sasa nona unataka kuvuruga ajenda yetu,....hahaha, kwanin unaniulza hivyo...nikuambie tu kwa vile wewe ni rafiki yangu...kwa muda sasa.., nimeamua kumsusa hata kulala naye tuna muda, hata tunaishi hivyo hiyo ni siri yangu nakuambia wewe tu kwa vile ni rafiki yangu,…na nilishamwambia akirudi kalewa, asilale na mimi chumba kimoja, sipendi harufu ya mipombe…na siku akiwa safi, aaha, hamna shida anakuja tunalala, lakini ndio hivyo, tupo tupo tu,….’nikamwambia.

‘Rafiki yangu hilo ni tatizo, jaribu kumuuliza vyema, kwani tatizo ni nini,..nahisi mume wako ana tatizo, mimi kama rafiki yngu nakuomba ulifanyia hilo kazi kabla hujachelewa, sizani kama unataka uwe na mke mwenza….utakuja kujuta, ukiwa umechelewa, hali kama hiyo sio nzuri.., utampoteza mume kwa hali hiyo, huenda ana tatizo linamsumbua na mtu wa kumsaidia ni wewe mke wake...’akaniambia

‘Hahahaha,unanichekesha, eti mke mwenza, hahaha..ajaribu..kama ni kuoa, aoe, mbona nilishamuambia hilo, ila asifanye siri...nikaja kugundua,...na leo, kweli umenichekesha, Hivi nikuulize, unajifanya unafahamu saana  maswala ya ndoa, wewe ngoja utakuja kuolewa, utakuja kuyaona haya wewe mwenyewe, ..ndoa nyingine ni ndoa,kuna matatizo chungu mbovu, ...., lakini sisi wanawake tunavumilia mengi,.we yaache tu..’nikasema

‘Hata kama sijaolewa, lakini mengi ni ya kibinadamu , nayafahamu tu…’akasema

‘Unafikiri mimi sijafanya juhudi, nikuambie kitu, ndoa..sio ..yeye akiwa na hamasa zake aje akuvamie tu, mimi ni mwanamke, nahitajia kubembelezwa, nahitajia, hali itakayonifanya nisahau mengine ya kikazi,..na hilo halianzii,..kitandani tu…’nikasema

‘Mhh..hapo unanitisha ...ok, labda nikuulize hapo... unataka kusema nini, mbona shemeji mimi namuelewa sana, nakumbuka ulishawahi kuniambia, umempata mwanamume anayejali, anayejua kubembeleza, au ulikuwa ukinidanganya…’akasema

‘Ilikuwa…ghafla, mambo yalipojiongeza, majukumu ya hapa na pale, unaelewa, hali nayo ikabadilika,…tukurudi nyumbani kila mtu na laptop yake, shughuli mtindo mmoja, ..mengine ni uhalisia, hata hivyo, ..siwezi kumlaumu au yeye kunilaumu, lakini pia, yeye anawajibika, kulibadili hilo…’nikasema

‘Mhh..mnatakiwa muwajibike wote, ..rafiki yangu shemeji ni mtu mnzuri sana, …anajali, nahisi wewe ndio hutaki kulifahamu hilo, au kwa vile unacho, ukiwa nacho unaona ni kitu cha kawaida tu..’akasema

‘Unajifanya unamuelewa sana kuliko mimi au..ni kweli, unalolisema, alikuwa hivyo, lakini sio hivi sasa..nahisi keshonja kwingine, na mimi sina muda wa kupoteza kumdadisi, ila nilimuambia, …kama atakuja kufanya jambo kinyume na ndoa yetu, ajue tumeshamalizana….’nikasema

‘Una maana gani…?’ akaniuliza
‘We tuyaache hayo, ….muhimu nataka nihakikishe jambo lako limekwisha, halafu nitayamaliza ya kwangu nionavyo ni sahihi…na najiuliza sana, kwanini umefikia kuniuliza haya yote..maana hayahusiani na tatizo lako au sio…?’ nikamuuliza

‘Nimeuliza tu…kwa vile nimemuona alivyo, na sizani nimekosea kukuulizia hayo, kaam uanavyonijali mimi, ndivyo ninavyokujali wewe…’akasema

‘Ni kweli,..ila yasikuumize kichwa, mimi mwenyewe ni mipangilio yangu, kuna haya mambo ya kikazi yakikaa sawa, nitatafuta mtu wa kuyafanya, na mimi nitakuwa kariu na familia yangu, hilo nimeshaliona, lakini kwa sasa, ngoja, nione ni kitu gani anakihitajia,..ila, siku nikigundua ana kimada nje,..ohooo..huyo na yeye nitakachowafanyia, watakuja  kunikumbuka….’nikasema


‘Mhh, kama ni hivyo utanifanya mimi niogope kuolewa, na hilo litawafanya wanaume wengine wapate mwanya wa kutoka nje ya ndoa…mpaka hapo naogopa, na hata …sizani kama nahitajika kuongea zaidi…’ akaniambia.

‘Usiogope, kuolewa kwa vile umesikia hayo kutoka kwa ndoa za watu , ndoa za watu hazina utaratibu maalumu kuwa yule akiwa hivi na wewe utakuwa hivi, kila mmoja ana utaratibu wake wa kuishi, na mwsho wa siku wote wawili mnakubaliana na hali halisi iliyopo, muhimu msifichane, msiwe na ajenda za siri, zinazovunja ndoa....’nikasema.

‘Lakini mimi nina imani nikiolewa nitahakikisha kuwa mimi na yeye kwanza tunapeana masharti  ya jinsi gani ya kuishi, na kama nikihisi kuwa kuna tatizo nitamuuliza mpaka aniambie, kwani sitafurahi aje kutembea nje ya ndoa, na chanzo kiwe ni mimi....vinginevyo, nisijue …. ’akasema.

‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa mimi ninaweza kuwa chanzo, kuwa mimi ndiye nimemfanya mume wangu alewe , awe hivyo, au.. ..kama ana tatizo angeliniambia basi, moja kwa moja, mimi si mkewe, kwanini aone uzito kuniambia, eeh,.., ukiona anaficha kitu, ujue hataki kukuambia, mimi namfahamu sana,…vinginevyo mimi siwezi kumuingilia maisha yake aliyoamua kuwa nayo, muhimu mimi mwenyewe naweza kuishi maisha yangu...’nikasema.

‘Mhh, haya bwana, kama ulivyosema ndoa kila mtu na utaratibu wake, na mimi nimejifunza kutoka kwa wenzangu sizani kama nitafanya hayo makosa,...maana mengine hayavumiliki, ...na wasiwasi wangu najiuliza kama likitokea tatizo hapo ni wa kulaumiwa, na je ni nani wa kuumia, kama sio sisi wanawake, hebu lifikiria hilo rafiki yangu....’akasema..

‘Achana na mume wangu, hebu tuendelea na hili tatizo lako, likimalizika la kwako litanipa nafasi ya kuendelea na mambo mengine, …ilikuwaje baada ya hapo,...?’ nikamuuliza.

‘Yaliyoendelea ni kama unavyoona, ....kwanza baada ya tukio hilo tulikaa kama wiki hivi hatuonani, na tulipoonana akawa ananionea aibu,..na mimi halikadhalika, na hatukuweza kubahatika kuliongelea hilo tukio hata siku moja, na ikawa kama vile tukio hilo limetushitua, sote wawili…’akasema

‘Mhh, lakini ulisema ilitokea mara ya pili au…?’

‘Ya pili, si ilikuwa siku ya pili yake, nikawa nahisi kuumwa, kumbe ni hiyo mipombe, akaja akaniambia dawa twende kunywa tena,..nikagoma, akanisihi mpaka nikakubali, ikaja kutokea kama vile…aliyetusaidia ni huyo huyo ndugu yake…’akasema

‘Una hatari wewe…’nikasema

‘Basi baada ya hapo,…nikaona atanizoea vibaya, nikaanza kumkwepa, akipiga simu sipokei, nikawa sasa siendi kula chakula cha mchana,nikingia ofisi nakuja a chakula changu, sitoki hadi jioni, na nikitoka najivunga kutoka na mmoja wa wafanyakazi ninaofanya nao....siku zikaenda...’akasema.

‘Mara nikaanza kuhisi mabadiliko...nikashituka, mwezi wa kwanza wa pili sijaona siku zangu, nikaona oohoo,… ngoja nikapime, kupima, nikaambiwa hongera..una mimba.....’akatulia.

‘Oh…ikawaje…?’ nikamuuliza

‘Ikawa hivyo hivyo, namkwepa kuliko, awali, lakini ikafikia muda, hali inanivuta natamani kuonana naye, ..lakini sitaki nionekane na watu, nahisi aibu fulani hivi…basi siku moja akanitumia meseji kuwa hana raha,…bila kuniona hataweza kwenda nyumbani kuna kitu anataka kuniambia

‘Kitu gani….?’ Nikamuuliza

‘Mhhh…nilishindwa hata kumuelewa, kumbe alikuwa na ajenda ya siri, …na sijui kwanini ilitokea hivyo, ndio maana rafiki yangu nakukanya,..ndio mimi sijaolewa, ndio mimi sina uzoefu wa ndoa, lakini wanaume wengine wanafikia kufanya mabaya kutokana na jinsi tunavyoishi nao, tunawajenga,..tunawafanya wafanye hivyo,…tuweni makini sana…’akasema
‘Hebu niambia alitaka kukuambia nini, maana mimi nataka kuondoka, naona unanifanya nijihisi siwajibiki, wakati wewe hujui mengi ya ndoa,..ipo siku nitakueleza, sio kweli kuwa mimi nimefikia kuyafanya hayo bila sababu, lakini mambo mengine ya ndoa, …hayazungumzwi….’nikasema

‘Basi kwa vile hali hiyo ilinizidi, nikawa natamani nimuone tu, awe karibu yangu, awe akiongea, awe kinibembeleza…yaani nakuwa na raha, na kuwa na amani, na akuiondoka, nakuwa muogoa, naogopa, ni hali tu ilinitokea hivyo…basi, nikamkubalia siku hiyo aje, …na hiyo ikawa imekaribisha mimi na yeye kuwa karibu tena

‘Sasa alipokuja siku nyingine ndio, akaniambia lake la moyoni….na hilo ndilo likafanya ajue kuwa mimi nina uja uzito….’akasema

‘Alikuambia nini…?’ nikamuuliza na yeye, akasimama maana mtoto alikuwa akilia, na mimi simu yangu ikawa inaita…

‘Alikuambiaje…?’ nikamuuliza nikiangalia ni nani anayenipigia, kumbe, … alikuwa ni mume wangu, nikamwambia rafiki yangu;

‘Tafadhali kidogo…niongea na shemeji yako…’nikasema

Nikawa sasa naongea na mume wangu , huku rafiki yangu akiniangalia kwa makini, ni kama ana shauku kufahamu naongea nini na mume wangu

‘Njoo nyumbani haraka…’ilikuwa sauti ya mume wangu kwenye simu

‘Kuna nini…?’ nikauliza, na mume wangu akakata simu…kutokana na sauti yake hiyo, nikajua kuna tatizo, kwahiyo sikutaka tena kuendelea na rafiki yangu, nikasema

‘Rafiki yangu, tutaendelea baadae , nataka kufahamu, alikuambiaje, au ..alikuambiaje…ok..ngoja niondoke….tutaongea siku nyingine si bado upo,….?’ Nikamuuliza

‘Kesho naondoka…’akasema

‘Basi nitakuja, …nahisi nyumani kuna tatizo…’nikasema na kukimbilia nje, kuondoka..

NB: Naishia hapa kwa leo,

WAZO LA LEO: Ndoa ina siri zake nyingi sana, na iliyo wajibu,  ni wanandoa wenyewe kujaribu kuzikabili changamoto zao, na kufiachiana siri zao, kwa kadri wawezavyo, kwani siri nyingine ni mtihani mungu anawajaribu…ni changamoto za kuvuka daraja…


Ni vyema kwa wanandoa, mkawa kitu kimoja kwa kuyajadili matatizo yenu, ni aibu kama wanandoa kama mtakuwa mkilalamika kwa watu wengine kuhusu mambo yenu ya ndani, ambayo mengine ni siri za ndoa, kwanini msiulizane, mkaangalia tatizo lipo wapi…kumbe yawezekana ni kitu kidogo tu… Tuweni makini kwa hili. Tumuombe mola azilinde ndoa zetu atuongoze tuwe kizazi chema.
Ni mimi: emu-three

No comments :