Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, October 5, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-1


Ni kisa na mkasa, chenye mafunzo ndani yake, kinachotokana na ushauri wa kirafiki kati ya marafiki wawili. Ushauri uliokuja kuzaa mtafaruku hadi marafiki hawa wawili wakaja kuwa maadui makubwa wakutaka hata kuuana.

Ulikuwa ushauri wenye nia njema kwa mlengwa, lakini ….athari zake kwa wengine zinaumiza,…je hao wengine wakiwa ni wewe mshauri itakuwaje….

Hutapenda kuona rafiki yako akiteseka, utafanya kila hali ili aondokane na shida hiyo, njia mbadala zilishindikana, ikabakia wazo hilo...lililokujia akilini na kumshauri mwenzako, afanye tu, bila kuangalia upande mwingine wa athari zake….

Kisa hiki ni kumbukumbu za wale wanaoteseka, wenye shida mbali mbali, wenye mitihani ya maisha, wengine wakihitajia kuolewa lakini hawajapata wa kuoa au kuolewa, hawa wanahitajia ushauri, je tuwape ushauri gani…

Wapo wengine wakihitajia watoto, lakini mola hajawajalia,..au wapo wengine walitendwa na wenza wao, wakaachika, au kuachwa kwa namna moja au nyingine. Wapo waliovumilia..wapo walioshindwa kuvumilia,…, na wapo waliojikuta kwenye njia panda…je tuwapatia ushauri gani…

Kisa hiki hiki ni maalumu kwako wewe mtoa ushauri, na wewe mshauriwa…tuweni makini sana kwa dhamana hii ya ushauri! Ushauri sio kuongea tu kwa vile…sio wewe utayefanyiwa, sio wewe …hapana shauri ukijiweka kwenye hiyo nafasi , kama ingelikuwa ni wewe..ingelikuwaje…

Japokuwa unaweza ukatoa wazo hilo kwa nia njema kabisa, ukitaka kumsaidia mwenzako, lakini jiulize huyo atakayetendewa hataumia,…au kama ungelitendewa wewe ungakubali kutendewa, ….maana isije ikawa MKUKI NI KWA NGURUWE TU.

*************

Ilikuwa vigelegele vya shangwe, pale nilipofunga harusi yangu, kiukweli ilikuwa harusi kubwa, kutokana na hali zetu, na aliyesaidia kuhakikisha kila kitu kimekwenda sawa, alikuwa rafiki yangu kipenzi…

‘Rafiki yangu, mume wako ni bonge la handsome…hapo sitii kasoro, na nikuambie kitu, wewe usisumbuke kwa lolote lile, mwili wako na wangu  kila kitu niachie mimi, muhimu ni gharama, nipatie fungu, na wewe kaa, tulia, kama ningelikuwa na pesa, nisingelipenda wewe utoe hata senti moja, lakini nitajitahidi…’akasema

‘Ujitahidi kwa vipi, usije kutoa hata senti yako moja, pesa ya harusi hii ilishaandaliwa kwa kila kitu, wewe isimamie tu, na kila kitu nitakukabidhi wewe, nashukuru sana rafiki yangu, wewe ni mimi na mimi ni wewe, …wewe ni rafiki yangu tunajuana, kwa kila hali, nisingelipenda wewe kujiingiza kwenye madeni,… unasikia, ukifanya hivyo utaniudhi…’nikasema

Basi yeye akasimamia kila kitu, nikaja nikafunga ndoa na mume wangu..na maisha na rafiki yangu yakawa ni pale pale, ila alichojitahidi kwa hivi sasa yeye akawa hafiki mara kwa mara nyumbani kwangu, kama ilivyokuwa awali, yeye alifika akiwa na uhakika mimi nipo nyumbani…nilimuelewa, na sio kwamba nilimshuku vibaya hapana ni yeye tu, aliona isje ikajenga fitina…’akaendelea kusimulia.

 Masiku, miezi, miaka, ikaenda mimi nikajaliwa watoto, lakini rafiki yangu bado akawa hajaolewa , sio kwasababu kuwa hakupata wachumba, hapana, wachumba ni wengi waliotaka kumuoa, lakini yeye akawa hawakubali kutokana na sababu hii na ile, aliyoiona yeye. Na awali sikupenda kumuingilia sana kwa maamuzi yake hayo, maana ninamfahamu alivyo…ana msimamo wake.

Lakini siku zilivyozidi kwenda mbele ikabidi mimi niingilie kati, nakuumuliza yeye anataka mume wa namna gani, ..japokuwa nafahamu kwa jinsi tulivyokuwa tukiongea awali kabla ya kuolewa, kuwa yeye angelipenda mume wa namna hii na ile, na mimi nikawa namuelezea hivyo, lakini mimi nilipoolewa nikaja kugundua kuwa ndoto za akilini za kuwa utampata mume mwenye kila kitu unachokitaka ni ndoto tu, aghalabu kuwa kweli…

‘Nikuambie rafiki yangu ukweli, huyo  mwanaume unayemtaka wewe hajazaliwa, huwezi kumpata mume wa kila kitu unachokitaka wewe, vingine vitakuja huko mbele kwa mbele, na vingine hutaweza kuvipata hadi kufa kwako, ndivyo maisha yalivyo…’nikamshauri siku za mwanzoni,…

‘Usijali rafiki yangu, ipo siku nitaolewa tu, na mume ninayemtaka mimi, hilo la kuwa hajazaliwa halipo,..wapo, ninajua wapo…nitasubiri, ipo siku nitampata , hata hivyo, kuolewa, ni kuolewa, …mimi mwenyewe bado nina malengo yangu..nisingelipnda kukimbilia kuolewa kwanza…’akasema

Maisha yakaenda hivyo, na umri ukakimbia, umri hausemi, …unashangaa sura inabadilika, na majina yababadilika, kijana inageuka mtu mnzima, dada, inageuka kuwa mdada, baadaye…, mama,…mama bila mtoto, baba bila mtoto, mawazo yanaanza kuingia akilini, mawazo..

***************


‘Rafiki yangu nilimpenda sana, tulianza urafiki tukiwa shuleni, na hata tulipoanza kazi, ninafahamu kuwa mimi nina uwezo kuliko yeye kihali, maisha ya familia yangu yalikuwa juu, mwenzangu alitokea familia ya chini, ninaweza kusema hivyo…’ akaendelea kusimulia

‘Mimi nilijitolea kwa kila niwezavyo, rafiki yangu awe kama mimi, kila nilipoweza, akiniambia au hata kama hajaniambia, nilijikuta namsaidia mwenzangu, ilifikia muda kila ninachonunua namnunulia na mwenzangu, kwahiyo tulikuwa kama mapacha..

‘Unajua ilikuwa sifanyi jambo mpaka nishauriane na yeye kabla sijafunga ndoa, na baada ya ndoa, ikaendelea hivyo, japokuwa mengine ya ndani ya ndoa ilibidi nisimuhusishe sana,….kama ujuavyo sheria za ndoa zilivyo.

‘Lakini hata nilipoolewa, sikuacha hiyo tabia, ya kusaidiana na yeye..ila ikafika muda natakiwa kuwa na familia yangu na mume wangu zaidi, hii hali iliniuma pale rafiki yangu anapokuja ananikuta mimi nipo na mume wangu, yeye hana…iliniuma sana, nilitamani huyo mume awe wetu sote, lakini mmh…hapo pagumu.


 Baada ya ndoa mambo mengine yalijiweka yenyewe rafiki yangu, alianza kupanga muda wake, ni lini aje kwangu, au lini tukutane naye, hakupenda kuja nyumbani kwangu kama mimi sipo,…sio kwamba sikumiani kwa hilo…au hakupenda wakutane na mume wangu kupata chakula cha mchana bila ya mimi kuwepo, hadi mume wangu akaja kuniuliza ni kwanini;

‘Huyo rafiki yako, ni mwaminifu sana, unajua kuna siku nakutana naye, namuomba nimpeleke lunch, hataki, eti kisa hapendi ije kulete fitina , mkaja kukosana wewe na rafiki yako…, sasa mimi ni shemeji yake nitamfanya nini , eti hivi kweli inaweza mimi nikakusaliti wewe mke wangu, kwa rafiki yako kipenzi…’akasema.

‘Lakini nyie wanaume hamuaminiki,….mimi namuunga mkono kwa hilo,..hata hivyo mimi sina wasiwasi kamwe na rafiki yangu…’nikasema.

‘Ina maana mke wangu kwa kusema hivyo huniamini…?’ mke akamuuliza mke wake.

‘Sio swala la kuaminiana hapo, shetani ana mbinu nyingi, …na kwanini ujiweke kwenye rehani ya mitihani, kama unaweza kuikwepa ni bora kufanya hivyo, kuliko kujitwika mitihani hiyo,….’akasema mke

‘Ok, nimekuelewa sana mke wangu, lakini nikuulize kitu ni kwanini rafiki yako hakubali kuolewa, yeye ni mnzuri ana umbo la mvuto, anataka nini na umri unakwenda…?’ akaniuliza mume wangu.

‘Hata sijui, hajajaliwa bado, siku itafika, ataolewa, ni kweli umri umekwenda, na hata sijui nifanye nini ili ampate mume anayemtaka,…hata sijui…’nikasema.

‘Japokuwa yeye ni mnzuri, lakini umri unakwenda mshauri sana rafiki yako, leo anapendeza hivyo, kila mwanaume anamtaka, lakini itafika sehemu hatavutia tena, hayo ndiyo maumbile yaliovyo, atakuja kujijutia muda umeshakwenda…’akasema.

‘Najitahidi sana,…hata sijui nimfanyeje tena…’nikasema.

Kiukweli rafiki yangu huyo sikuwa na shaka naye hata kama ningelimkuta yupo na mume wangu, ninamfahamu sana kwa msimamo wake…anaogopa sana waume za watu, ….huwa akiahidi kitu kaahidi, na kwangu nilimuona kama sehemu ya ndugu zangu, na hata watu walimfahamu hivyo kwa msimamo wake huo, wa kutokujihusisha na rafiki ambaye ni mume wa mtu. Wanaume wengi walimjaribu wakashindwa kwa msimamo wke huo.

***************

 Kuna kipindi alimpata mwanaume mmoja wakawa wanakutana mara kwa mara nikajua huyo atamuoa, lakini baadaye nilipomuulizia, akanipa jibu la kukatisha tamaa.

‘Yule jamaa sitamkia tena,…hanifai, nilijua ni mtu mwenye msimamo, ..mtu wa matumizi, …lakini kumbe ni nguvu za soda, eti anakuja kunilalamikia kuwa anadaiwa hiki na kile, kwani nilimuambia akope….aah, nimeachana naye…’akasema

‘Hilo tu…?’ nikamuuliza

‘Wewe unaliona dogo hilo, achana naye, ..mengine sio lazima nikuambie,.hata kama wewe ni rafiki yangu, huyo nimeshambwaga…’akasema na sikutaka kumuingilia zaidi,..nafahamu msimamo wake ulivyo.

Kiukweli urafiki wetu ulikuwa ni dhati, na kila mmoja alijua msimamo wa mwingine na hilo ndilo litufanya tuwe hatuyumbi,…lakini ikatokea la kutokea, urafiki ukageuka kuwa shubiri, ukagubikwa na uadui wa kutaka hata kuuana….’akasema

‘Kwanini sasa, mimi nilijua marafiki kama nyie, mliojuana, hamtaweza kuachana…?’ nikauliza

‘Hapana, yule simtaki tena, hata kumuona simtaki hata aje nyumbani kwangu…,’ akasema wka hasira….kwa kauli hiyo nikawa na hamasa ya kutaka kujua kilichoajiri kati yao wawili,

Awali hakutaka kunisimulia undani wa maisha yao, hasa kilichosababisha hadi urafiki wako ukafa na kujenga chuki za kutaka kuuana, lakini baadae akaanza kunisimulia…kilichowafanya marafiki waliojulikana kuwa ni mrafiki wa kweli, marafiki ambao kila mtu alikuwa akitolea mfano kwao, lakini sasa ni maadui wakubwa….

***********

Miaka ikapita na mimi nikajaliwa kuwa na watoto wawili mapacha wa kike na rafiki yangu akawa akitoka kazini anakuja tunakuwa naye, ananisaidia kuwalea, kiasi kwamba watoto hawa walimuona kama mama yao. Na kwa ukaribu huo, watoto wangu walimpenda sana.

‘Nawapenda sana watoto wako, natamani niwe na watoto kama hawa, kwa sura, …natamani mume wangu anizalie kama watoto hawa…’akasema

‘Utawapata tu usijali…lakini muhimu uolewe, umri unakwenda, urembo wa msichana una kikono chake…’nikamwambia tukiwa tunaongea…

Kuna kitu ambacho anacho rafiki yangu,  alipenda sana kuchagua wanaume…sio kwa wanaume tu, hata vitu vyake akitaka kununua, yeye anachukua muda mrefu sana kufikia maamuzi, atachagua wee, atatoa kasoro wee….mpaka aridhike, itachukukua muda sana..kilichoniumiza ni kuona rafiki yangu haolewi, na umri unakwenda, yeye hakulijali hilo mapema na siku zikazidi kusonga mbele.

‘Rafiki yangu ukumbuke umri na urembo wa mwanamke, una kikomo, jinsi unavyozidi kukua, na urembo nao unapungua, ..na ujue mwenyezimungu anakupatia neema zake uzitumie, ukizipuuza, itafika muda atakunyang’anya, na hapo utaaanza kulalamika…’nikamwambia.

‘Usijali…ipo sku nitakuambia kusudio langu ni nini…unajua rafiki yangu sipendi nije kuumia,…sipendi nije kujutia,..muda utafika na wewe hutaamini…’akasema

‘Hapo sikuelewi, ina maana kuna kitu unanificha…?’ nikamuuliza

‘Hapana…wewe niamini tu, siwezi kukuficha kitu , wewe ni mimi na mimi ni wewe,lakini siwezi kukuambia kitu ambacho hata mimi sina uhakika nacho , bado sijawa na uhakika wowote kwa hivi sasa, ni nani na nani wa kunioa, nimtakaye hajaonekana na kila ninayempenda, nakuta keshawahiwa, nashindwa kuelewa ni kwanini…’akasema

**************

Siku zikaenda watoto wangu wakawa wakubwa, na wanaanza shule, hebu fikiria, miaka mingapi, kama kumi hivi, bado rafiki yangu hajaolewa,…

Siku moja mwenzangu huyu alikuja nyumbani kwangu, akanikuta mimi nipo na watoto wangu, huwa nikiwa nyumbani kama nimemaliza kazi zangu , huwa napenda kucheza na watoto wangu, najishusha nakuwa kama mtoto mdogo, tunacheza ile michezo niliyokuwa nikicheza nikiwa mdogo, basi ni faraja kwa watoto wangu.

 Rafiki yangu akaingia na akawa ananiangalia nikicheza na watoto, aliniangalia kwa makini sana,..nikahisi kama anataka kulia, siku zote huwa ana ujasiri fulani, akija kwa vile watoto wamemzoe kama mama yao, basi watamkimbilia, wataanza kucheza naye, na huku kucheza na watoto yeye ndio kanifundisha…

Lakini siku hiyo, haikuwa hivyo, alikuwa akiwa kanywea, hana raha kabisa, ule uso uliojaa ujasiri haupo tena,, watoto kama kawaida yao walipomuona wakamkimbilia, na akasalimiana nao, kiukweli watoto wangu walimpenda sana rafiki yangu huyu, hata yeye, na hakuchoka kuwasifia kuwa ni watoto wazuri, anapenda kuwa na watoto kama hao.

Siku hiyo hakuwa mchangamfu kabisa, nikajua kuna jambo, awali nilihisi labda anaumwa, lakini nilipomuuliza akasema haumwi,..nikaona kuna jambo jingine kubwa limemtokea, labda…, ikabidi niwatoe watoto ili nipate muda wa kuongea naye


‘Ok.. rafiki yangu vipi leo,…sio kawaida yako, hutaki hata kujiunga tukacheze na watoto kama kawaida yako.., unajua watoto wangu wakikuona wanahisi furaha sana, wanakuona wewe ni mama yao wa ukweli, kuliko hata mimi, vipi leo kulikoni…?’ nikamuuliza

‘Oh rafiki yangu jana sikulala, mawazo,….nahisi sio mimi tena,…sikuwa hivi kabla,….’ Nikaona machozi yakimlenga lenga.

‘Mhh, usilie bwana, niambie kuna tatizo gani…?’ nikamuuliza.

‘Unajua rafiki yangu mara nyingi huwa najipa matumaini, lakini kipindi hiki cha siku mbili tatu, nimekuwa nikiumia sana, nawaza kupitiliza, na hata kujiuliza, ni kwanini, unajua alipo…nitenda yule mwanaume, kunikasaliti wakati nilishapanga yeye ndiye wa kunioa, namkuta na mwanamke mwingine ndani, …imenivunja sana nguvu…’akasema

‘Lakini wapo wengine au sio..keshaoa, achana naye….’nikasema

‘Kwanini sasa inatokea hivyo, kile ninayempenda, tunakwenda vizuri, baadae hali inageuka, inatokea jambo tunakosana na huyo mwanaume ama awe msaliti, au awe na imani nyingine ya dini, na siwezi kuacha imani yangu ya dini, sasa nifanyeje jamani…yaani hata sielewi, inafikia muda siwaamini tena wanaume, kwanini nisimpate mwanaume kama huyo wako….’akasema

‘Utampata tu rafiki yangu, wewe subiria muda utafika…’nikasema

‘Yaani hata kwenye ndoto nimeota nakuona wewe upo na watoto wako na mume wako mnafurahi, mimi nipo peke yangu porini, mkiwa, ..oh, mara nikajiukuta nipo kati kati ya bahari nachukuliwa na maji, napiga ukelele, wa kuomba msaada, hakuna wakunisaidia, nikawa nawaita nyie, mje kuniokoa lakini mkawa hamnisikii, nikawa nazama, nikashtuka …’akatulia

‘Hiyo si ndoto tu, au…?’ nikamuuliza

‘Ni ndoto ndio..lakini nahisi imetokea kwa vile jana niliwaza sana,..mara nyingi najipa matumaini, nikirudi nafanya hiki na kile siwezi sana, lakini jana, sijui ilikuwaje, hawa watu wamenitibua kweli, ..ndio maana sitaki kuolewa…’akasema

‘Akina nani tena…?’ nikamuuliza

‘Si hawa wanaume..inafikia sasa wananiringia mimi, …kuna mmoja kanibwatukia mpaka hamu yake ikaisha, akafikia kusema, nitaishia kuzeeka bila mwanaume..sawa, labda ana ukweli wake, lakini haya ndio maisha yangu, kama anataka anioe, anioe basi, yeye anasema anataka kunipima kwanza, kunichezea, hapana hilo siwezi kabisa…’akasema

‘Kwahiyo, umeshakata tamaa au sio…?’ nikamuuliza

 Hapo akakaa kimia akiwa kashika shavu ile ya kusononeka, kiukweli kama rafiki yake ilinuma sana, nikamsogelea na kumkumbatia, hapo akalia kweli, hadi alipotulia, nikamwambia akae , najua sasa ile hasira yake imekwisha

‘Unajua rafiki yangu, ndio maana nilikushauri awali uolewe na yule mwanaume wa kwanza aliyekuwa rafiki yako, ukamkataa, na hawa wengine ilikuwa sio bahati yako, ni wao walikusaliti, sio kusidio lako, tumuachie mungu tu…’nikasema

‘Mhh..ni kweli rafiki yangu sasa kweli naona nimechelewa, maana hata waume nao siwaoni kabisa wanaonifaa, wa umri ninaoutaka mimi hawapo tena, ninaokutana nao, ndio hao wanaotaka kuuchezea mwili wangu, kitu ambacho sikitaki,..natamani atokee mume wa kweli, alete posa, simuoni..wale niliowataka ndio hao wameshaoa…kiujumla kwa sasa sina raha tena…’akasema


‘Sasa unatakaje, maana hata mimi sipati usingizi nikikuwazia wewe. Tumejadiliana na mume wangu tuone jinsi gani ya kukusaidia, lakini wanaume tulio-waona wanakufaa, ndio hao wameshaoa, kama ulivyosema, lakini bado wapo wengine, na wewe huwataki, kwasababu zako…na tulijua yule mliyekuwa naye angekufaa, sasa unasema hamuelewani tena,…sasa, tukusaidieje..?’ nikamuuliza.

‘Kiukweli, nikikuona hivi, wewe upo na watoto wako, nawazia mbali kabisa, najua nilishakosea, na umri ndio huu umeshakwenda sana....naona jinsi gani ulivyo na raha na watoto wako,....nikiwaona watoto wako najisikia kukosa kitu muhimu sana katika maisha,…’akasema

‘Utawapata tu…’nikampa matumaini hayo, lakini moyoni najiuliza kwa vipi.

‘Nitawapataje sasa…?’ akauliza

‘Kwanini unasema hivyo rafiki yangu, kuwapata utawapata tu, ukiolewa au sio, kwanza muhimu ndio hilo,kuolewa, mkubali mmojawapo akuoe, sasa sio muda wa kuchagua tena…’nikasema hivyo na siku hiyo ikaishia hivyo, na masiku yakazidi , miezi, miaka, rafiki yangu hajapata mume wa kumuoa.

Na siku nyingine ambayo naikumbuka sana, akafika kwangu, akiwa hana raha, zaidi ya siku nyingine, nikajua ni yale yale…moyoni nikawa najiuliza nitamsaidiaje, nifanyeje, ningelikuwa na ndugu yangu wa kiume ningelimshinikiza amuoe, lakini sina,, ningekuwa sina wivu, ningemshauri aolewe na mume wangu, lakini nina wivu wa kufa mtu

 Hata mume wangu hataki kuoa wake wawili alishaniambia,…kwani siku moja nilimtania tu, akaniambia niache kabisa mawazo hayo, yeye hana uwezo wa kuoa mke zaidi ya mmoja, huyo mmoja kwake, anaona ni kazi…ni mwanaume wangu namfahamu hivyo, kweli hawezi, na hataki..sina shaka na hilo

Sasa nitamsaidiaje rafiki yangu….na katika maongezi ndio likanijia wazo….wazo ambalo lilikuwa ni kisu cha kunichoma mimi mwenyewe…

Ni wazo gani hilo


WAZO LA LEO: Urafiki mwema ni ule wa kujaliana kwa shida na raha, na mkikutana mnashauriana mambo ya heri, mambo yenye tija, na hakikisha kuwa pale unapotoa ushauri  kwa mwenzako  unampatia ushauri ambao hata wewe ungeliweza kuufanya au kufanyiwa. Usije ukamshauri mwenzako kwenye jambo ambalo kama utakuja kufanyiwa wewe hutakuja kupendezewa nalo.
Ni mimi: emu-three

No comments :