Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, August 2, 2017

DUWA YA KUKU...27


Matatizo yaliingilia familia za wakina mama hao, hasa hao wawili, yule aliyenitoa kijijini, na huyu anayeishi na mdada, ila huyu ninayeishi naye kwasasa hayakuwa makubwa sana, zaidi ya migogoro yao ya kifamilia hasa kati ya baba na mkewe, mkewe alikuwa hataki kabisa mimi niendelee kuishi hapo, hata kurudi kuishi hapo, ilitokea pale wenzake walipomshauri kuwa nirudi kwake niishi kwa muda.

‘Mlishakubaliana, aje aishi kwako, huku akitafutiwa chumba, basi wewe endelea kufanya hivyo, nakuomba sana , maana kama unavyosikia, kwangu hakuna amani, mume wangu kawa kama mtu aliyechanganyikiwa..kijana wangu naye haeleweki…’yule mama mfadhili wangu wa kwanza akamwambia mwenzake huyu alipopigiwa simu kuhusu mimi.

Walikuja wakakutana na kukubaliana aendelee kunivumilia.

Basi ikakubaliwa hivyo, nikawa naendelea kuishi hapo, lakini kwa makubaliano kuwa niishi hapo kwa muda, lakini alisema hatakubali mimi nikae hadi nijifungulie hapo kwake….

Tuendelee na kisa chetu…

************

Baada ya tukio hilo, mimi niliendelea kuishi kwa yule mama niliyepelekwa kwake, kwa masharti kuwa nindoke hapo kitakapopatikana chumba, ili nihamie na kuanza maisha yangu mapya, na mtu wa kunitafutia chumba alitakiwa awe mume wa yule mfadhili wangu wa kwanza.

Siku zikaenda na mimba inakuwa, na hali yangu ilikuwa leo mzima kesho mgonjwa hoi kitandani, na nikiumwa ndio makelele matusi, mimi nipo hapo kwa ajili ya kula na kulala tu,…ikabidi nivumilie hivyo hivyo nitafanya nini.

Sikuweza kuwalamu wafadhili wangu wa kwanza, kwanini hawanitafutii chumba kwa haraka, kwasababu sikujua kuna tatizo gani huenda bado wanahangaika na matatizo ya familia yao, maana baada ya kutoka siku ile, huyo mama alipopigiwa simu kuwa mume wake kachanganyikiwa, mimi sikuweza kuonana naye tena, nasikia tu, kwa kupitia kwa huyu mama ninayeishi naye kuwa hali ya yule mume imekuwa ya utatanishi.

 Siku moja nikakutana na mdada, nilipokwenda sokoni, tukapata mwanya wa kuongea kidogo, na ndipo akaniuliza nimefikia wapi na mpango wa chumba

‘Sinilisikia kuwa wanakutafuti chumba, imefikia wapi…?’ akaniuliza

'Mimi hata sijui, kila kukicha wanandoa hao wawili, wanakimbilia kwenye shughuli zao, jioni wakikutana ninachosikia ni ugomvi, mama mwenye nyumba analalamika, mimi nitawekwa humo mpaka lini, na mimba ndio hiyo inazidi kukuwa na kila siku siishi kuumwa umwa.

'Na mzee anasemaje, baba mwenye nyumba?’ akaniuliza

'Yeye anasisitiza kuwe na mke wake azidi kuwa na subra, kwani hawataweza kunirejesha kule kwa familia ile nyingine kwa hivi sasa kutokana na matatizo yanayoendelea huko, kunipelekea mimi huko kutaizidisha matatizo zaidi, na mpangop wa chumba haujakamilika….’nikasema

‘Lakini chumba kiwe ni tatizo kupatikana, mimi hili siamini, nahisi kuna jambo jingine , labda baba yule kutokana na hali yake, na kazi ya kutafuta chumba na kukuhudumia kakabidhiwa yeye..si ndio hivyo..?’ akasema na kuuliza

‘Ndio hivyo…’nikasema

‘Kwahiyo huyo mama anatakaje, kuwa uondoke, uende wapi, urudi kule au iweje, kama ni hivyo, kwanini yeye asisaidie kutafuta hicho chumba…?’ akaniuliza

‘Huyo mama kasema hayo ni mambo ya wanaume waliosababisha hayo yote ,kwahiyo kama ni chumba, waume ndio watafute, ili waweze kuwajibika, wanachoogopa ni kuwa wakitafuta chumba wao, waume wao hawatawajibika ndio makubaliano yao, na zaidi kinachoniuma ni kauli yake tu….’nikasema

‘Kauli gani…?’ akauliza

‘Hiyo ya kuwa mimi nikizaa shetani, ni nani atahangaika nalo…’nikasema

‘Lakini ndivyo alivyosema marehemu au sio, wote wawili hilo walilisema, na hata yule rafiki wa marehemu alilithibitisha hilo, japokuwa yeye ni mganga tu wa miti shamba, lakini si alisema ukiwa na matatizo umpigie simu, atakutafutia dawa…?’ akauliza

‘Ndio, lakini huyo mama ninayeishi naye, kasema hataki kuhangaika na mambo ya kishirikina, kama ni shetani, niondoke nalo, nikazalie huko huko…’akasema

'Hayo waliongea lini…maana majuzi walikutana kwenye kikao chao…?’ akaniuliza

'Hata wiki haijapita, walizozana kweli, hata usiku sizani kama wamelala kwa amani…maana asubuhi waliamuka kila mtu kanuna, …’akasema

'Basi hao akina mama  walikutana kwenye kikao chao, wakashauriana kuwa sisi turejeshwe kijijin na kukabidhiwa kwenye familia za hao marehemu maana sasa familia zao hazina amani tena, na tukiendelea kuwepo, matatizo hayataisha…’akasema huyo mdada

'Aaah mimi hilo sikubali, kama hawanitaki, waniache tu, nitahangaika hapa dar, na najua nitaweza kuishi, lakini sio kunirejesha huko kijijini…’nikasema

'Haya wakikitupo huko mitaani ndio utaishije, hebu niambie, una mipango gani ya maisha..?’ akaniuliza

'Mungu mwenyewe atajua, ….’nikasema

‘Mungu mwenyewe atajua, ndio mipango yako hiyo, mimi sipendi hata kuongea na wewe, maana huna ubunifu, huna akili ya kufikiria, mungu atajua, ukiwa umekaa hivi hivi tu…’akasema huyo mdada

‘Sasa unataka mimi nifanye nini, elimu yangu imeishia hivyo…sina ujuzi zaidi ya kufagia na kusafisha vyombo, na kuomba omba mitaani, nitafanya kazi gani…?’ nikauliza

'Tatizo wewe….hata nikikushauri jambo ni kama nampigia gita mbuzi, wewe ulivyo, huwezi kuishi na mimi, wewe huwezi  kupambana na mambo ya mitaani…mimi mwenzako ni mjanja, nione hivi hivi tu…’akasema

'Mungu atanisaidia, najua mungu anajua fungu langu, kama ni hapo hapo au hata wakinifukuza, ipo siku nitafanikiwa tu, lakini siwezi kufanya mambo nisiyokuwa na ujuzi nayo…’nikasema

'Mimi ninachokuonea huruma, wewe una mzigo tumboni, na baya zaidi hatujui huo mzigo ulio nao tumboni upoje, ushaambiwa sio mimba ya kawaida, je ukizaa shetani, hebu niambie kutakalika kweli…’akaniambia

'Mimi sipendi hiyo kauli, kwanini nizaie shetani, …kwani wengine wanazaaje, mbona hospitalini wanasema ni mimba ya kawaida tu…’nikasema.

'Hiyo ndio kauli yako,mungu anajua, mungu anajua, haya kaa na kauli yako hiyo tuone kama mungu atakusaidia kama wewe mwenyewe hujisaidii,..kiukweli mimi nilikuwa na mpango, lakini kila nikiongea nawe naona ni majanga tu, hutaweza kuniunga mkono, na sana sana, utaniharibia, naogopa kukushirikisha kabisa…’akasema

'Mpango gani huo…?’ nikamuuliza

'Niapie hutasema kwa mtu, kama nikikuambia kuhusu huo mpango wangu, maana ni…..’akatulia kama kshtuka jambo, akageuka kuangalia kule sokoni, na mimi nikaangalia huko huko kuwaangalia wenzangu niliokuja nao.

'Niambie kwanza, ndio niape siwezi kuapa kitu ambacho sikujui, je kama ni dhambi…’nikasema

'Hawa akina mama si wanajifanya wajanja, hawajui kuwa bado wamekalia bomu….’akasema

'Bomu gani hilo…?’ nikamuuliza

'Si yale mazindiko, umesahau, kwani walifanya juhudi gani kuyaondoa, wamepuuza, angalia yule mama kule tulipokuwa awali anavyopata shida, kwanini hawaelewi,…’akasema

'Si walishahangaika wakaambiwa yameondolewa, na hayo yanayotokea hivi sasa  yawezekana ni mambo ya kawaida tu, mimi hata sijui, …’nikasema

'Thubutu, kila siku majanga, nimesikia wakiongea, mume wa kule tulipoanzia, siku nyingine anakutwa yupo nje uchi, anaweza akawa anatembea hata hajui anakwenda wapi, usiku amaanuka, anatembea, anafanya kazi, hivi hayo ni mambo ya kawaida…’akasema

‘Lakini docta alisema huo ugonjwa upo, na kutibika kwake hakuhitajii haraka, …’nikasema

‘Na huyo kijana wao, umesikia vituko vyake…’akasema

‘Amekuwaje na yeye…?’ nikauliza

‘Hahaha, mimi niliwaambia, huyo kijana wao, ana matatizo, wakaniona namchukia, naingilia mambo ya kifamilia, na unajua mimi walishanichukia mapema hata kabla y ahayo matatizo, kisa namsingizia mtoto wao, eti mambo asiyoyafanya, wanamdekeza sana yule kijana, sasa wameshaanza kuipata joto ya jiwe, watanikumbuka…’akasema

‘Amekuwaje kwani…mbona siyajui hayo?’ nikauliza

‘Sasa na hilo utasema ni ugonjwa,…hilo sio ugonjwa, pamoja na mengine, mtoto wao ana matatizo, na ukionamtu anakushauri msikilize, yule mama ni mwalimu, msomi mnzuri, lakini sijui kwanini mambo mengine anayafumbia macho, hasa yakihusu mtoto wake..yeye alitekwa na akili kuwa mimi huenda natembea na mume wake, akashindwa kuangalia mambo mengine…’akasema

‘Mhh,…sijui kwanini alikuwa akifikiria hivyo, kwanini lakini, mimi wala sikuwa na mawazo hayo…’nikasema

‘Hukuwa na mawazo hayo, ushahidi si unao tayari….’akasema akicheka.

‘Naona wewe unaleta utani, mimi niliwahi kutembea na mume wake…’nikasema

‘Sasa ndio hapo, wangetuliza kichwa, wakaangalia kiundani zaidi, tatizo, sio sisi tu, huenda matatizo hayo yameanzia hata kabla yetu, mzee, kijana,…na ni kweli kuna mamabo yamewekezewa, nayo walitakiwa wayafukue, lakini kwanza wamejiangalia wao wenyewe, mle ndani kuna tatizi zaidi ya tatizo,…’akasema

‘Mhh..au wewe unahusika….’nikasema

‘Hahaha, watamtafuta mchawi, na hawatampata, maana mchawi keshafariki, yaliyobakia, ni masalio yake, na hayo masalio, watapata shida sana kuyamaliza, ... waache wahangaike, mwisho wa siku watatutafuta, ila mimi sijui kama nitaendelea kuishi na hawa watu…’akasema

‘Kwanini wanasema hivyo watatutafuta,…?’ nikauliza

‘Hivi unafikiri utaishi na wao milele…na we ngoja tu,…mimi sio mjinga, najua kuishi na watu, kwanza nilipofika hapo kwa madamu, nikafanya utafiti, kuna mtu kanifundisha jambo, mjue mtu unayeishi naye anataka nini…nikamtafit madamu nikajua anataka nini na nini..nikamtafuti mzee, nikajua anapenda nini na nini…mzee wake hata habari na mimi kabisa…hilo nimelifurahia, tatizo ni mama…’akasema

‘Lakini si kawaida…mama ndiye mlinzi wa nyumbani…’nikasema

‘Sasa huyo mama kuna siki atanitafuta….’akasema

‘Utakwenda wapi…?’ nikamuuliza

‘Wewe kaa hivyo hivyo, ngoja niondoke, wasije kurudi hao mabosi, madamu wangu nampenda lakini ..unajua kuna kipindi tunakaa naye ananisimulia mambo mengi, ..lakini kuna kipindi haeleweki, kila unachokifanya hakionekani…akiona mume wake akinitupia jicho, basi keshabadilika, ni nani kasema anamtaka mume wake mzee yule..mimi nina mipango yangu, …hahahaha,.’akasema akicheka kwa dharau

‘Lakini wewe si ulisema, wanakusifia kuwa wewe ni jembe, unafanya kazi sana,…’nikasema

‘Ndio hivyo, kwa hilo, kila mtu ananisifia, sio madamu, hata mzee mwenyewe,  lakini kazi ukimaliza, hawakosie cha kunisema, mara mimi ni muhuni, mara mimi napendelea mambo ya kishirikina, , mara tumeleta matatizo kwenye familia zao, yaani karaha,kashfa, sasa mimi sio mtoto mdogo, nayasikia, yananiuma, mpaka lini…kwa kifupi maisha kaa haya, hayana uhakika, na alishaniambia, siku yoyote atanitimua kama hanijui…’akasema

‘Lakini angalau kwako kuna unafuu, sio kama kwangu…yaani kuna muda nafikiria kukimbia, niondoke kabisa, unaweza ukajitahidi kufany akila kitu, lakini watoto wa pale ndani, wale mabinti, wanaharibu, wanachafua, maana wao wanataka kula na kulala, ..ndio maana hawaolewi. Na mama yao anawatetea, sasa hata mimi hali kam hiyo inanikwaza, lakini ndio maisha utafanyaje, hata hivyo, hata mimi nitakimbia, nitaondoka hapo nyumbani…’nikasema

'Sasa ukimbie na hali kama hiyo uende wapi …?’ akaniuliza akinikagua tumbo

'Popote,…ipo siku, mungu atanionyesha njia, yaani hata sijui, hakuna anayenionea huruma kazi zote nafanya mimi, nachoka sana, kuna muda nahsi kizungu zungu , kutapika, nakimbia kujificha mpaka hali hiyo inakwisha, najua wakiniona nipo hivyo, itakuwa njia ya kunifukuza, aah, ni shida kwakweli …’nikasema

'Umeonaeeh,….ndio hayo matatizo yanayonikuta mimi, ila kwako, haaah, unalo….nilikushauri awali uiotoe hiyo mimba ukakataa, sasa kazi unayo…sasa sikiza nikuambie mpango wangu….’akasema

'Mpango upi huo…usiwe mpango mbaya, mimi sitaki matatizo…?’ nikamuuliza na yeye kwanza akaangalia kule sokoni kama ana mashaka fulani, , halafu akaniangalia na kusema;

'Unauliza eti mpango gani, …’akasema na kuaniangalia

‘Sawa nimekuelewa, niambie sasa…’nikasema

‘Nikuambie kitu, hawa watu, hata ufanye kazi kama punda, hata uwe mnyenyekevu kama malaika, hata uwe mtiifu kama …sijui nani, hawatakutahamini kamwe, unanisikia, hawa watu watakutumia, na wewe hivi wanakulipa shilingi ngapi, aheri ya mimi mwisho wa mwezi nakinga japokuwa ni kidogo…’akasema

'Hawanilipi chochote, wanadai mimi sina mkataba na wao,…mimi hapo nakaa kama nimefadhiliwa tu, kama mgeni, na siku ikifika nitaondoka, yule mama mchungu wa pesa, kila kitu anakupigia mahesabu, na ole wako usirudishe chenji, kwahiyo maisha ninayoishi anayejua ni mungu peke yake….’nikasema

‘Sasa sikiliza nikuambie huo mpango, lakini ole wako ufungue domo lako , huu nimeshaufanyia kazi na utafanikiwa, ni wewe tu,….’akasema

‘Sawa niambie…’kabla hajaongea mara nikaitwa, na nikiitwa, nawafahamu watu wangu, wanataka niwepo mara moja, ikabidi niachane na huyo mdada, kuwakimbilia watu wenzangu, na mdada akanipungia mkono akisema

‘Kwaheri ya kuonana….’akaondoka

Niliwaendea watu wangu na nilipowafikia tu mama mwenye nyuma akaniuliza

‘Ulikuwa wapi muda wote huo,tunakutafuta hatukuoni, ..?’ nikaulizwa

‘Nilikuwa naongea na yule mdada wa kule…’nikasema

‘Mumeanza kudanganya tena eeh, sawa, ongeeni tu, na huyo mwenzako ni mjanja njanja, ngoja akudanganye uhadaike, shauri lako…’akasema

‘Hakuna kitu kibaya mama, nilikuwa naongea naye tu.

‘Sawa ongeeni tu, na nilikuwa sijakuambia, ujiandae, safari yenu ya kwenda huko kijijini inaiva, wewe na yeye mtandoka, sasa kama mlikuwa mnaliongelea hilo mlipange vizuri, safari hii hakuna kurudi nyuma, ukazalie huko kijijini kwenu mlipoyatoa hayo mashetani…’akasema huyo mama

‘Mama kwanini unamuambia hivyo….’mtoto wake akasema

‘Kwani uwongo mwenyewe anafahamu tumboni kabeba nini, na akijifungulia hapo nyumbani, mtaambukizwa na nyie, na hatujui hilo shetani litakuwaje,…kama ni shetani kweli, si itakuwa ni balaa…’akasema huyo mama

‘Mungu anajua,…’mimi nikasema hivyo tu, siku hiyo kiukweli sikuwa na raha kabisa, nikawa kama mgonjwa, kumbe safari imeshapangwa, sasa nitafanya nini…akilini nikajipanga niende kuonana na huyo mdada, niusikie mpango wake, kama ni kutoroka tutoroke wote, sasa sijui tutakwenda kuishi wapi.

Basi siku hiyo ikapita, na nyingine na siku ya tatu sasa, nikiwa nyumbani, wenzangu walitoka, nilikuwa sijisikii vyema, na nikiwa ndani, mara nikasikia wanzangu wakirudi, na kabla sijatoka nje kuonana nao, mara, wakaja askari,

‘Kuna tena jamani…?’ wakaulizwa

‘Tunamuhitaji huyu mfanyakazi wenu wa ndani…’akasema

‘Kafanya nini…? Huyo mama akauliza

‘Atuambie mwenzake yupo wapi, …’wakasema

‘Mwenzake yupi…?’ mama akauliza

‘Yule mfanyakazi wa yule rafiki yako,….’akasema huyo askari, huku akinikabili mimi, pale nilipo nilihis mwili ukinisha nguvu miguu ikawa kama imekatika kwenye magoti.

‘Kafanya nini huyu mfanyakazi …?’ akauliza huyo mama.

‘Kaondoka hapo nyumbani, tangia jana, …na kuna kiasi kikubwa cha pesa hakionekani, inaonekana ni yeye kazichukua hizo pesa na vito vya thamani vya huyo mama, na rafiki yake mkubwa ni huyu mfanyakazi wako, tunataka tukamuhoji huyu mfanyakazi wako kituoni…’wakasema hao askari.

‘Lakini mna uhakika gani kuwa huyu anajua wapi huyo mwenzake alipokwenda…?’ akauliza huyo mama

‘Tuna uhakika, kwa mara ya mwisho , walionekana wakiongea hawa wawili kule sokoni,

NB: Majanga 


WAZO LA LEO: Tuweni makini kwenye ushauri tunaopewa na watu wengine, kuhusu mikakati ya maisha, tusikubali kwanza, kabla hatujafiria matokeo ya hiyo mikakati, kuna watu wengine ni wepesi wa kubuni na kupanga mambo hata kama ni ya shari, na kuwashikirisha wengine, nia ni kuingiza kipato. Jiulize kwanza kipato hicho ni cha halali kinapatikana kwa njia ya halali, kama kuna mkono wa shari epukana na mipango ya namna hiyo. Tumuome mola wetu atupe njia ya heri, na kupata riziki za halali
Ni mimi: emu-three

No comments :