Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, August 31, 2017

DUWA LA KUKU.....44


Kwa vile kuna kipindi nilizama kwenye mawazo, nikapotea kabisa kifikra, sikusikilia alichokuwa akisimulia yule mbaba, kwahiyo nikamuuliza mama Ntilie anihadithie walichokiongea, hadi wawili hao wakafikia kusameheana mtu na mke wake,… lakini haikuwezekana kwa muda huo yeye kunisimulia kwani walifika wateja wakihitajia huduma na siku hiyo ikapita, na siku ya pili ikawa hakuna kazi nyingi sana, na tulipopata muda na ndio nikaweza kuelezewa na mama Ntilie, kabla hatujaingiliwa na ugeni mnzito….


Tuendelee na hitimisho la kisa hiki….



**********
Ni siku ya pili yake baada ya hicho kikao changu na baba na mama , wafadhili wangu ambao waliondoka baada ya mimi kuhakikishiwa kuwa kweli wamesameheana, nashukuru mungu kuwa kweli, kwa hali ilivyojionyesha watu hao sasa ni mke na mume wema.

Kila muda nilikuwa najiuliza nilipitwa na nini hapo kati, maana sikumbuki jinsi walivyofikia hapo, ndio ikafikia muda nikamuuliza mama Ntilie..
‘Hebu niambie ilikuwaje siku ile..?’ nikamuuliza mama Ntilie.

Mama Ntilie akasema;…

‘Unajua nilikuona ukiwa umezama kwenye mawazo, sikutaka kukusumbua, nikakuacha tu, nikawa mimi nasimama badala yako, wakikuuliza swali nakujibia, na ndipo ikafika ile hatua ya wao kuja kukupigia magoti, nikawaambia…

‘Mngelijua moyo wa huyo binti ulivyo, hapo yupo kwenye imani na mungu wake, hapo yupo na mola wake, mimi naona msijisumbue kumpigia magoti,  ni nyie tu, kwanza mumuhakikishie kuwa mumeshasameheana, vinginevyo hataweza kuwa na amani, na kama mlivyosema hatima yenu itategemeana na huyo binti kwa vile yote yalitokea kutokana na hayo aliyofanyiwa,…’nikawaambia hivyo.

‘Oh….ina maana ni hivyo tu…?’ nikaguna na kuuliza.

‘Ndio nakuanzia, sijui wewe ulianza kupotea wapi, ila nikirudia hapo, baada ya kuwaambia hivyo, mume mtu akauliza

‘Ina maana mke wangu asiponisamehe, na yeye msamaha wake hauna maana au sio, sasa mke wangu muambie kilichopo moyoni mwako, je umenisamehe kiukweli…’akasema.

‘Ndio, aliniambia kuwa msipofanya hivyo, yeye atamlilia mola wake mpaka musamaheane na hapo anamlilia mola wake, mimi namfahamu sana…’nikasema wakati huo moyo wangu una mashaka, ni kwanini upo hivyo, unalia, huongei….’akasema.

‘Mke wangu unasikia…’akasema mbaba.

 ‘Mhh, wewe tatizo lako hunielewi, isingelikuwa ni wazazi wangu sijui kama ningelikusamehe, lakini nimekusamehe, kwa ajili ya familia yangu…’akasema.

‘Sasa tumuonyeshe binti yetu,…lakini kwanini anaendelea kulia tu…’akauliza huyo mbaba akiniangalia mimi, na hao nikasema;

‘Tumpe muda bado yupo kwenye kumlilia mola wake….’nikasema
‘Unajua mama Ntilie, tangia tunafika hapa, nilishafikia uamuzi fulani,..maana huko nilipotoka ilikuwa shughuli kubwa, mimi  nilikutana na wazazi wangu, nikiwa nataka ndoa ivunjwe, lakini cha ajabu sasa wazazi wangu hawataki ndoa nivunje …’akasema mke mtu.

‘Kwanini…?’ nikamuuliza wakati huo wewe upo kama ulivyokuwa machozi, huongei…

‘Wazazi wangu wamasema  wao sasa wanakiri kuwa wamefanya makosa, na mitihani wanayokutana nayo kwa hivi sasa inaweza ikawa inatokana na wao kuwa mbali na watoto wao, hususani mimi na mume wangu…’ akasema.

‘Kiukweli niliwaonea huruma sana wazazi wangu..na nikawaza sana, nikaona kweli inabidi tusahau yaliyopita tugange yajayo, ni vigumu lakini utafanyaje…ndio ikabidi nimtafute huyu mwanaume, sikumuambia nilichoongea na wazazi wangu..nilitaka nisikie kauli yake ya sasa na ukweli wote,na kama angelificha safari hii,…, nisingelimsamehe, safari hii alikiri yote tofauti na yaliyotokea kipindi kile kabla hajachanganyikiwa…’akasema.

‘Kwani kipindi mlipoitwa na baba yako ilikuwaje…?’ akaulizwa.

‘Siku ile niliumia sana, kwani alipokuja baba, baba akiwa kajiandaa kumsamehe, yeye aliendelea kuficha ukweli, mbele ya kijana wetu ambaye alikuwa anafahamu kila kitu, siku ile…baba alikuja, akatuuliza kuna tatizo gani kwa kijana wetu mbona kuna kitu kinamsumbua.

‘Kijana huyu achana naye, nitamalizana naye, ni tatizo dogo tu... Nilishaongea naye, tatizo hanielewi, unajua watoto wa siku hizi walivyo, …’akasema mume mtu.

‘Eti kijana kuna tatizo gani…?’ akaulizwa, na kijana sasa alionekana kuwa na wasiwasi, akawa kidogo anamuangalia baba yake kwa mashaka na mara nyingi anaangalia chini. Halafu alipoona anasubiriwa yeye kuongea akasema;

‘Mimi nataka baba aongee yeye mwenyewe, kama hataki kuongea …mimi siwezi kuongea tena…nimeamua bora yaishe …nitajua la kufanya mwenyewe…’akasema.

‘Kwanini,… si ulisema utaongea kila kitu…sasa hiki kikao kina maana gani…’akaambiwa.

‘Hapana nimewaza sana, nikaona ..baba ndiye angelipaswa aongee au seme ukweli..lakini kama hataki kuusema ukweli,… basi, mimi nitaamua la kufanya mimi mwenyewe…’akasema
‘Auseme ukweli gani sasa…ina maana sisi tumekuja hapa kupoteza muda wetu, tukitarajia kusikia hilo jambo, ambalo lilikupeleka hadi kwa babu yako, ..na hiyo bahasha yenye ujumbe ipo wapi..?’ akauliza huyo mzee.

‘Mhh..mimi sijui…’akasema akimuangalia baba yake.

‘Haya baba mtu hebu tuambie kuna tatizo gani hapa nyumbani kwako…?’ akaulizwa na baba mkwe.

‘Hakuna tatizo mzee, matatizo ni ya kawaida, kama ujuavyo maisha yalivyo, kunatokea mitihani ya hapa na pale, sasa haikuwa na lazima wewe uje, kama ingebidi hivyo, sisi wakubwa tungekuita rasmi,…, unajua vijana siku hizi wamepata simu, wana mitandao, wanahisi kila kitu ni kupiga video, hawajui madhara yake,…nimeongea naye najua keshajirudi..’akasema baba mtu.
`
‘Una uhakika huna cha kuongea…?’ mama mtu akamuuliza kijana wake, na kijana akainua uso kumuangalia baba yake halafu akasema;

‘Baba kama hataki basi…’kijana akasema.

 Mimi hapo nilikuwa na ajenda yangu kichwani sikutaka kusema lolote, nilijua nikisema kitu baba atachukua hatua mara moja, sikujua baba ana kitu gani moyoni,..na pia nilitaka kusikia mume wangu atasema kitu gani, hakujua kuwa mimi nilishagundua ukweli wote…’akasema mke mtu.

‘Ukweli wote uliupataje huo ukweli..?’ akaulizwa na mama Ntilie.

‘Mimi nilishaupata huo mkanda wa kijana wangu, na ni ule alioupeleka kule kwa babu yake…’akasema na kila mtu akashikwa na mshangao

‘Kwa vipi…ina maana muda wote huo ulikuwa nao…?’ akaulizwa.

‘Siku ile wakati huo mkanda unaletwa kule nyumbani kwa wazazi wangu, nilikuwepo, nilifika kule kwa mambo yangu, na wakati kijana anaingia na kuonana na mlinzi nilikuwa dirishani namuangalia, sijui waliongea nini na mlinzi, ila niliona kijana akimkabidhi huyo mlinzi bahasha,….kwa muda ule nikajua labda mlinzi alipomuambia kuwa mimi nipo ndani, kijana akaona aondoke, labda alikuwa akinikwepa,  lakini kumbe mlinzi hakumuambia mimi nipo humo ndani…

Nilitaka nitoke nje kwa haraka nimuite huyo kijana tuongee naye, lakini hakusubiria, hata wakati natoka nje alikuwa keshaondoka,..alikuwa anaendesha piki piki lake…na muda huo mlinzi alikuwa kashika hiyo bahasha wakati natoka, kwahiyo mlinzi hakupata muda wa kuikagua vyema…mimi kwa haraka nikaona jina la baba juu ya ile bahasha…sikuwa na shaka nilijua ni mzigo wa baba,..lakini nikajiuliza ni kwanini aulete huyo kijana…na kabla sijamuuliza mlinzi , yeye akasema;

‘Kijana wako kaleta bahasha hapa, kaniambia nimpatie babu yake mkono kwa mkono, lakini mume wako alisema kama kuna mzigo utaletwa hapa na kijana au mtu mwingine yoyote, nisimpatie baba yako, kwani una makosa, inahitajiak urejeshwe nyumbani, alinisisitizia sana, je ndio huu, au kuna mwingine…?’ akaniuliza
‘Ni kweli, wewe nipe nitampatia, kama ndio wenyewe…’nikasema akilini mwangu nikihisi kuna jambo, kwanini kijana alete huo mzigo, na kwanini baba yake asema hivyo, akili ikachanganua na kuhisi kuna jambo, na hapo hamasa ya kuchunguza hiyo bahasha ikanijia…’akasema
‘Unajua nimekumbuka kuna kazi nilimuachia mume wangu, nahisi ndio hii, ngoja nione kama kuna cha kubadili nitafanya hivyo, haina haja mpaka yeye aje kuuchukua, ngoja, nitaongea naye kwenye simu..’nikamwambia huyo mlinzi
‘Lakini mume wako…’akalalamika
‘Nitampigia kwani una wasiwasi gani, kwani alikuambia nini kuhusu huu mzigo…?’ nikamuuliza
‘Alinisihi nisimpe mtu mwingine mpaka yeye aje kuuona mwenyewe….’akasema
‘Alikuambia huo mzigo ni kwake unakuja hapa kwa baba, atauleta huyu kijana..?’ nikamuuliza
‘Ndio….’akasema
‘Basi haina shida..nitaongea naye ikibidi nitamsubiria, huenda yupo njiani anakuja, tutakutana naye hapa…’nikasena na yeye akakubali shingo upande, na hali hiyo ikazidi kunipa hamasa, nahisi kuna jambo kati ya mume wangu na kijana wangu, na kuna kitu nyuma ya pazia. Nikaingia na hiyo bahasha ndani, nikaichunguza ndio nikagundua kuwa video.
Kwa haraka nikaenda kwenye deki,, bila kujali kuwa huenda ni mzigo wa baba, huenda ni kazi fulani kijana alipewa kuifanya na baba, …nikaona kwanza niondoe mashaka moyoni mwangu, nikaiweka kwenye deki na kuanza kuiangalia, kiukweli nilihamaki..nilikasirika, na kama …sio subira…nashukuru hata baba hakuwepo..’akasema.

Basi nikawaza sana, nikaona ngoja kwanza nione huu mchezo mwisho wake ni nini, ndio nikatoka nje nikamsomesha mlinzi anisaidia jambo moja, na hayo aliyoyafanya mlinzi ni yale niliyomuelekeza mimi..na wakati huo nikapata muda wa kuatafakari haya mambo vyema, na mpaka hapo nikawa nimejua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba yangu.

Kiukweli hadi hapo nikawa nimeazimia uwe mwisho wangu na huyu mwanaume,  tuachane tu kwani hayo niliyoyaona sio ya mtu wa kawaida, hayo ni ya mchawi…na nitaishije ndani na mchawi, ndio, kuna namna inaonyesha kuwa sio dhamira ya huyu mwanaume kufanya hivyo, lakini kwanini..kama ni tatizo kwanini asiniambie…na nilipoona ile sehemu ambayo niliipeleka kule kwa yule mtu anichunguzie, ndio hapo nikazidi kutishika zaidi, kuwa kumbe naishi na shetani ndani ya nyumba….sasa sina jinsi, kwani ushahidi ninao, lakini moyoni, nikasema ngoja nimpatie nafasi ya mwisho huyu mtu, unajue tena mumeshazaa naye, watoto wakubwa, kuna mambo yanakusuta…’akasema mke mtu..

‘Ndio ikaja hicho kikao chako na baba yako au sio…?’ akauliza mama Ntilie
‘Ndio, lakini hicho kikao sikuitisha mimi, hicho kikao ni cha kijana kutaka kusema jambo na alishaongea na babu yake kuwa ana jamabo la kutaka kuongea, na nilion ajabu ni kwanini tena kijana akaghairi, na sizani kama aliongea na baba yake akatishiwa, nahisi kuna kitu aliogopa, na sikuwahi kumuuliza..…na cha ajabu mume wangu hakutaka kusema ukweli, hapo nikajua kweli huyu mwanaume ana tatizo…’ akasema

‘Ni kwanini hakukubali kusema ukweli, ni ili hali hakuwa na uhakika kuwa hiyo bahasha iliyotumwa huko kwa baba ipo kwa mlinzi, au baba yake ameshaipata…?’ akaulizwa

‘Hakukubali, akijua kuwa siri hiyo haijajulikana, yeye alikuwa na uhakika bahasha hiyo bado anayo mlinzi, na nilimuambia mlinzi amuambie hiyo bahsha bado anayo,… na walishapanga na mlinzi kuwa alipe kitu kidogo, apewe hiyo bahasha, kwahiyo akajiona yeye bado yupo salama, …

‘Unajua mtu kama huyu mpaka mabaya yamkute ndio anaweza kukubali ukweli..sasa utaona yaliyotokea baadae, ambayo yalimpa fundisho, hebu atuelezee mwenyewe ilivyokuja kutokea adhabu kutoka kwa mola mwenyewe…’ mkewe akamgeukia mumewe.

*****************
Hapo ndio mume mtu akaanza kuelezea ilivyokuja kutokea baadae….

‘Ni kweli, tulikuja kukutana na baba mkwe akiwemo kijana…na nilishangaa mzee alipokuja alikuwa na sura tofauti na siku nyingine,…alinisalimia kwa unyenyekevu, badala ya mimi kuanza kumsalimia, ..mzee huyo ni mkali, hana utani kwa watoto,

‘Watoto wangu nisameheni sana,..nahisi nimekuwa mkaidi kwenu….na naona sasa nahatarisha ndoa yenu mpaka kijana anakuwa hana raha…na nimegundua bila ya mimi kutoa idhini yangu kwenu hamtaweza kuishi kwa amani, nimeliwazia hilo sana, kwahiyo kuanzia sasa nipo radhi na nyie, nimeikubali ndoa yenu, lakini kabla ya hilo nataka jambo moja kutoka kwa huyu mkwe wangu..je upo tayari kubadilika na tabia yako hiyo mbaya…?’ akasema

‘Tabia mbaya, baba nina tabia gani mbaya,..sawa labda mimi nina kiburi, labda…basi kama ni hivyo  mimi nikubali nitabadilika,  nipo tayari kubadilika….!’nikasema hivyo.

‘Je upo tayari kubadilika, na kuacha hayo mambo unayoyafanya yasiompendezesha mungu na ndoa yako..?’ nikaulizwa na mke wangu.

‘Mke wangu mambo gani yasiyompendezesha mungu…ambayo mimi nayafanya..?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Mume wangu…unajua hapa yupo baba, hapa yupo kijana, na kijana ana mambo anataka kuyasema …ambayo yamekuwa yakimkera, ana ushahidi, bado wewe unaendelea kusema huna tatizo, je huo ushahidi ukitolewa utakuja kusema nini…?’ nikauliza

‘Ushahidi gani jamani..eti kijana wangu una ushahidi gani kuwa mimi nina tabia mbaya, nimefanya kitu gani, sema ..au utoe huo ushahidi wako…mmi nipo tayari…na sijui kwanini haya yote mimi sina tatizo, sijamkosea mtu yoyote na kama nimemkosea basi..nisamaheeni…’akasema huku nikiwa na mashaka mashaka.

‘Umesikia binti, huyu mume wako hajabadilika..umesikia mwenyewe, nilikuambia kama kweli kabadilika basi mimi nitakwua radhi na nyie, lakini kwa hili, bado…bado, sikiliza binti yangu, mimi nipo tayari kuwapa idhini yangu, lakini nahisi bado, siwezi kukutelekeza binti yangu kwa mtu ambaye ninajua ana matatizo, kama utaniamini haya, kama hutaniamini haya,..sisi tutazidi kumuomba mungu, kama upo ukweli wa haya aje autoe, sina zaidi, labda tumsikia kijana atasema nini…’akasema baba, na mke angu hakukata tamaa akaniuliza tena..

‘Mume wangu kwanini unanilazimisha nifanye nisicho kipenda, kwanini hutaki kutubu, ukajirudi, tukapata baraka za wazazi wetu..mume wangu wewe hadi kijana kasema una mambo unayoyafanya usiku, sasa unafanya nini, tuambie tukusaidie, kwanini upo hivyo…?’ mke wangu akaniuliza.

‘Nani mimi..oh,…hahaha, hivi mke wangu hayo yametoka wapi,..hivi wazazi wangu wangelikuwepo hapa  wakayasikia haya, wangehisije, kuwa mim kijana wao ni mchawi, au si hivyo unavyotaka kusema...sio vizuri jamani, mnanifanya nijishi mpweke baba na binti yake mnanisingizia mambo ambayo sio kweli…’nikasema
‘Na kama ni kweli, ujue utapata mabaya makubwa sana, maana sisi tunamuomba mola atusaidie, awasaidie na nyie muondakane na hayo yanayowasumbua, na kama upo ukweli, aje audhihirishe, utakuja kuumbuka mkwe,…’akasema baba mkwe

‘Nasema ukweli hakuna kitu kama hicho, mimi sijawahi kufanya hayo unayoyasema baba, au mke wangu kijan huyu hapa aseme mwenyewe, ..hao waliotaka kufanya hivyo ndio hao wamelipiliziwa mimi wala sijui walikuwa wakitaka nini…wamekufa , wangekuwepo mungeliwauliza wenyewe…’nikasema na baba alipoona sijabadilika akasimama kutaka kuondoka, kijana wangu akasema;

‘Baba kwanini hutaki kusema ukweli..?’ aliponiuliza kijana hivyo, hapo nikashtuka…nikajua sasa kijana anataka kuusema ukweli. Nikamwangalia kwa kumkazia macho, kijana wangu toka utotoni anajua sura yangu ikiwa vipi nipo na hasira hapo anakuwa makini na hata kuogopa kuongea, naona hadi sasa kawa mkubwa anajua hulka yangu,

‘Sikiliza kijana hujui haya…nilikuambiaje mambo ya wakubwa usiyaingilie litakalotokea utakuja kujuta mwenyewe.., kaa pembeni,…usipende kuingilia mambo ya watu wakubwa, wewe tabia yako ya unga ndio imekuharibu, acha tabia hiyo,… mimi sijafanya hayo unayoyafikiria wewe, wewe ni mzushi, ni unga wako unakupeleka kubaya, na tabia yako hiyo mbaya, uiache mara moja, unasikia, sitaki tena kusikia kijana wangu anatumia unga, iwe mwisho leo……’nikasema kwa ukali…

Kijana alitulia kwa muda, machozi yakawa yanamlenga lenga…kijana wangu sio mdogo, angeliamua la kufanya hapo angelifanya, lakini nahisi kuna kitu kilimpata au kuna mtu kamshauri akaona awe hivyo.


‘Basi mimi naondoka kwenye hii nyumba, maana sasa naonekana kuwa mimi nii mzushi, maana sasa kila mtu ananionyeshea kidole mimi kuwa nilitunga uwongo, na mambo yangu yote niliyoyaweka kama ushahidi umeyaharibu, sasa…naonekana mimi kama mzushi, na hata huku kuumwa nazusha tu…, haya, mimi naondoka zangu, nitajua mwenyewe la kufanya….’akasema na kuanza kuondoka. Hakuna aliyemzuia…

Kijana hakuonekana tena hapo nyumbani, na hata huko kwa babu yake hakufika tena, siku zikapita…na mpaka tuliposikia taarifa hiyo ya kukamatwa kwake…

Sasa baada ya kikao kile,…yaliyofuatia hapo kwangu ilikuwa ni mawazo , mawazo….nahisi kabisa sipo sawa…namuwazia kijana wangu nawazia hayo niliyoyaona kwenye hiyo video, nawazia….yaani sielewi..

Nikawa sasa najilaumu,  kwanini nilifanya hayo, kwanini sikukubali kusema ukweli, kwanini sikukubali kuwa hayo yaliyotokea usiku nilikuwa nahusika, nikaungama mbele ya familia yangu, na je nitafanyaje ili kijana wangu apone…mawazo hayo hayakuniacha, mara siku moja nikahisi sauti nyingi zikizizima kichwani mwangu, yaani ikawa kama kichwa na watu wanaopiga kelele…na haikupita muda nikawa sijitambui, nikatoka mbio mbio huku niki-ita…jina la kijana wangu!

‘Kijana wangu njooo..nitasema kila kitu, nimekosa kijana wangu…’ilikuwa sauti yangu ya kila siku nikawa sasa ni mtu wa kushikwa, nataka kukimbia…nikiuliza ni nini shida, kauli ni hiyo,..namtafuta kijana wangu…na hata kijana wangu alipopatikana nikawa simtambui tena, nahisi kama sio yeye, ikawa ni kazi hadi nikafikishwa muhimbili wodi ya wenye matatizo ya akili, baadae nikarejeshwa nyumbani, ikafika muda sijijui kabisa..

Masiku, miezi ,.nipo hivyo..na kuna wakati hali inajirudi, lakini sio kwa kujielewa sana, mke na wanafamilia walijitahidi kila aina ya matibabu,..mwishowe nikawakimbia,..hayo mimi siyajui, nasema sasa kama nilivyokuja kuambiwa…na ndio nikaja kukutana na nyie..

‘Kwahiyo safari zote hizo ni za kumtafuta kijana wako…?’ akaulizwa

‘Ndivyo ilivyoanzia hivyo, na nilipo-potelewa kabisa, akili iliyokuja baadae ni ya kumtafuta huyo binti…anisamehe...’akasema

‘Jamani hicho ndicho kisa changu…

***************

Na alipofikia hapo ndio akageuka kukuangalia wewe, akashanga kukuona anabubujikwa na machozi, hapo, akashtuka, na ile hali ye yeye kushutuka, ikawafanya na wengine wote kugeuka kukuangalia, mimi nilishakuona ulivyo…tokea awali nilikuwa nimetulia tu, ndio mama mtu akasema;

 ‘Oh, binti..usilie, mimi nimeshakubali haya yaishe, na japokuwa kwa shingo upande, nimekubali kumsamehe mume wangu,na wewe sasa tunakuomba utusamehe…..’ilikuwa kauli ya mama huyo

‘Hayo ndiyo yalitokea ukiwa umezama kwenye duwa sijui,..ulikuwa unaomba …si ndio hivyo, mmmh na maombi yako sio mchezo, yakajibu…’akasema mama Ntilie.

******************

Siku zikapita na siku moja, ukafika ugeni, ni ugeni ule wa awali, wa wale watu walikuja kutaka kununua lile eneo la urithi huko kijijini, sasa wakisema wamekamlika, kwahiyo  mimi na wao tuongozane hadi benki ambapo huko ndio malipo yatafanyikia, mama Ntilie akasema kwa siku hiyo yeye hawezi kuacha shughuli zake mimi niende peke yangu tu.

‘Usijali hawa ni watu wema hawawezi kukudhulumu…’akasema na mimi nikaondoka na hao watu hadi benki ambapo nilishafungua akaunti yangu, nikalipwa hizo pesa, tukaandikishana na hao watu, na kila kitu kakamilika kwa mara ya kwanza nikawa na milioni kadhaa benki,

Sasa wakati tunatoka hapo benki, tupo nje ya korido la benki,…mmojawapo akaniuliza;

‘Dasa samahani wewe una matatizo gani yanayokusumbua…?’ akaniuliza na kunifanya nishikwe na mshangao, nikamuuliza hivi

‘Nina matatizo!!...nina matatizo gani!..., kwanini unaniuliza hivyo…?’ nikauliza na mwingine akasema;

‘Huyo hapa mwenzetu ni mtu aliyejaliwa kipaji cha kusaidia watu wenye matatizo, anaweza kukuangalia hivi tu akatambua matatizo yako, na jinsi ganii ya kukusaidia, huwa anajiwa na vitu kama njozi…na tukuambie ukweli, siku ile tulipofika awali alipokuona tu, yeye akagundia kuwa una matatizo makubwa sana…ambayo yanahitajia msaada wa haraka, kabla hujajifungua…’akasema.

‘Mhh…mimi naona hayo hayana umuhimu kwangu, na sihitaji mtu wa kunisaidia,..najua mungu pekee ndiye wa kunisaidia, kama nina matatizo nimeshayafikisha kwa mwenyewe, nasubiria matokeo tu, vyovyote itakavyotokea najua ni kwa matakwa yake…’nikasema.

‘Hapana hakuna malipo yoyote utalipa kwetu, ..sio kwamba tunafanya hivyo kwa vile una pesa, hapana..kamwe hatutaki hata senti moja yako….na sisi hatuwezi kuondoka bila kukuambia hilo na kama utahitajia kusaidiwa, ..na si kusaidiwa, sisi tunachofanya ni kumuomba mola wetu…yeye, huyu mwenzetu kasema hataweza kuishi kwa amani akiondoka bila kukusaidia, na yeye anamtegemea mungu wake,…yeye atakuombea tu, na mengine tutamuachia mungu, utuelewe, sisi ni watu wa imani…’akasema

‘Wapi sasa, hapa hapa, au …?’ nikajikuta nimesema hivyo, niikiwa siamini maneno yao…, sikuwa na mawazo hayo tena kuwa mimi nina tatizo. Nilijua nimeshamkabidhi mola wangu…

‘Vyema turudi kule nyumbani unapofanyia shughuli zako, ili tupate nafasi kuliko hapa, ila ni kama wewe upo radhi, na kama haupo radhi basi, sisi tutakuacha, ila mwenzetu huyu kajaliwa kipaji cha namna hiyo na amewasaidia watu wengi sana tena bure…’akasema huyo kiongozi wao.

Basi mimi sikuwa a kipingamizi tukarudi nyumbani, nilikuwa nimechukua kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kuongezea biashara na mama Ntilie.. Tulipofika, hakukuwa a wateja wengi , nikamuelezea huyo mama kilichofanyika na hayo wanayotaka kuyafanya hao watu,..huyo mama akaniita pembeni.

‘Unawaamini hao watu wasije wakafanya hivyo kesho na kesho kutwa unakuta pesa yote imekwisha huko benki…’akasema

‘Wao ndio wamenilipa, wao ndio wamefanya juhudi yote hiyo, wao ni watu wa dini, mimi nimewaamin, na najua mungu atanilinda, huenda ikawa ndiyo sababu ya kuondolewa hii mitihani, tumuachie mungu anajua zaidi …’nikasema

‘Sawa….kama umewaamini mimi sina shaka…’akasema na basi wale watu wakaniombea na yule mmojawapo ambaye ndiye mwenye hicho kipaji akasema nilale tumbo juu, nikafanya hivyo, yeye akaweka kiganja chake tumboni,i kwangu, nilihisi tumbo likitetemeka kama mtu aliyeshikwa na umeme, iliendelea hivyo kwa muda, badaye likatulia.

‘Pole sana…natumai sasa utajifungua salama…’akasema huyo mtu wa dini.

‘Kwani ni kitu gani umekigundua …?’ akauliza mama Ntilia

‘Inaonekana huo uja uzito una maagano ya shiriki ndani yake, ..lakini yamekwisha, muhimu ukijifungua tu hakikisha unatimiza wajibu wote wa mtoto,…kumuomba mola wako, ..na kamwe usije kumshirikisha mtoto huyu na mambo ya kishirikina…yeye anahitajia imani tahabiti ya dini, ndiyo itakayomsaidia, na ianzie kwako wewe,… hakikisha unamfanyia mambo yote yanayostahiki kwa mtoto, itamsaidia sana yeye huko mbeleni kwenye maisha yake…na kama kutatokea tatizo usisite kutupigia simu..’akasema na wakaaga kuondoka.

‘Lakini lazima niwape kitu kidogo…’nikataka kuwapa pesa, wakakataa, na kusema;

‘Sisi tunarudi huko kijijini, na kuanza kazi za ujenzi, tunashukuru sana, kwani pamoja na hizo pesa tulizokulipa kwa ajili ya hicho kiwanja, lakini fadhila zitakazopatikana kwa ajili ya nyumba hiyo ya ibada zitakusaidia hata wewe na familia yako huko mbele…ukumbuke ukitoa kwa jili ya mwenyezimungu utarajie malipo makubwa sana, hiyo ni akiba yako endelevu, hata ukiwa haupo hai… na hebu fikiria hiyo nyumba ya ibada itadumu muda gani,..na kila siku utakuwa unapata fadhila kiasi gani…umefanya jambo la maana sana…’wakasema

‘Nashukuruni sana, nawashukuruni sijui niwalipe nini, chukue hii sadaka yangu basi…’nikasema, na wao wakasema sio kwa wakati huu kwani itakuwa nimetoa kwa ajili ya hayo waliyoyafanya

‘Usijali…kwani hutakiwi utulipe chochote, ..sisi kazi yetu ndio hii ya kuitangaza dini, na kwa hili umetusaidia sana kwani tutakuwa na sehemu yetu ya kudumu…kwa ajili ya ibada na ofisi ya mambo ya kidini…’wakasema na baadae wakaaga na kuondoka.

Hutaamini baada ya tendo hilo , nilihisi kamaa nimepunguziwa mzigo tumboni, awali nilikuwa kama nimebeba mzigo mzito ambao unahisi unataka kudondoka, lakini baada ya hapo, japokuwa nina kitu tumboni lakini sio kama vile awali, na ile hali ya kusikia vibaya, ikawa imekwisha kabisa,..

Baada ya miezi kutimia nilifikishwa hospitalini, nasema nilifikishwa kwa maana hali hiyo ilinianzia nikiwa nyumbani, na kiukweli, nilipofika hospitalini haikuchukua muda, nikajifungua salama, japokuwa mtoto alitoka akiwa sehemu kubwa ya mwili haina ngozi, ni kama mtu aliyeungua, docta wakasema ni udhaifu tu wa ngozi tu itaisha…

Basi mimi nikafuatilia masharti yote ya jinsi mtoto akizaliwa anatakiwa kufanyiwa kidini, na siku baada ya siku,..hali ya mtoto ikawa inakuwa vyema, ngozi inarejea, kunabakia makovu ya kawaida tu..namshukuru mungu sana, kwani hadi sasa kama unavyomuona  ngozi yake inakuwa kama ya kawaida, ni alama alama zinabakia tu.., na mtoto mwenyewe ndio huyu hapa..’akasema huku akinionyeshea mtoto wake.

‘Mhh..hongera..tena mtoto ana afya nzuri kabisa, sijui kwanini walisema hivyo, kuwa atakuwa sio kiumbe wa kawaida, mbona ni mtoto mnzuri kabisa, imani za shirkiii mbaya sana…’nikasema na hakunijibu hiyo hongera yeye akasema;

‘ Unajua nilijiuliza sana , nilijiuliza tu,…hivi  kweli duwa la kuku halimpati mwewe..’akasema

‘Kwanini ukajiuliza hivyo…na wewe umeliona hilo kivitendo.au sio…wale waliojifanya wao ni zaidi ya wengine, wanaweza kuingia majumba ya watu wakafanya wapendavyo, mbona wameshindwa kupambana na hayo yaliyowakuta…kwahiyo hiyo kauli ilikuwa ya kuwaasa hao watu au sio..?’ nikasema

‘Mhh…kiukweli, mimi sijui, ila najua kuwa msemo huo ulitolewa kwa maana fulani maana wazee wetu walikuwa an hekima sana…ila nimeamini kuwa, masikini silaha yake kubwa ni duwaa, ni maombi kwa mola wake, na muhimu wakati unafanya hivyo uwe na moyo safi, usiwe na hasira za visasi, chuki kwa wengine…mimi hilo nimelithibitisha kwa vitendo..’akasema.

‘Hata hivyo,..kila hali ina mitihani yake, umasikini una mitihani yake mingi tu..kama ulivyo utajiri, na ili uweze kuishinda hiyo mitihani,…yabidi uikubali hiyo hali, lakini usijipweteke, upambane na mazingira, utafute hukio ukiwa huna kinyongo na mtu, na hata ukitendewa mabaya, usikimbilie kulipiza kisasi, kwa njia za uovu, …’akawa anasimama kutaka kuondoka.

‘Ni kweli, lakini kwa walimwengu, sizani kama atakubali atendewe ovu akae kimia tu…wengi tunakimbilia visasi tena wati mwingine hata huna uhakika na hilo jambo…ndio hulka zetu…’nikasema

‘Kwa ushauri wangu, kama wewe ni mnyonge utafanyaje sasa,..kuliko kuingia kwenye shiriki, kwanini tusimuombe mola wetu atusaidie…na wakati unafanya hivyo usiwalipizie maombo mabaya hayo waovu wako, moyoni wasamehe  na ufanye hivyo kwa imani thabiti…imani hiyo thabiti ndio inageuka kuwa silaha ya mnyonge… hutaamini hapa nipo hivi, unaniona bado nipo kama hohe hahe, lakini sio kwamba mimi ni masikini tena,..hapana..’akatabasamu kidogo.

‘Umepata utajiri, kutokana na kile kiwanja au…?’ nikamuuliza

‘Hiyo ilikuwa miongoni mwa neema alizokuja kunipatia mola wangu,…hapa najibana tu,  ili niweze kujiajiri, kuna mipango inakamilika,…maana nilikutana na wataalamu wa ujasiriamali wakanielekeza na kunisaidia jinsi gani ya kuwekeza, kile nilichojaliwa nacho, na ikibid nichukue mkopo kidogo niongezee, nimefanya hivyo,…

‘Na..ni… hatua kwa hatua, lakini najua sio kazi rahisi, inabidi nipambane kweli,  maana mtoto huyu anakua, atahitajia kusoma, sitaki itokee sababu, watu waseme uliambiwa…ni staki nirudie makosa ya nyuma, siwalaumu wazazi wangu, lakini sitaki niwe kama wao..na sitaki mtoto wangu aishie kama mimi nataka yeye awe zaidi ya mimi, na, elimi ndiyo itakayomuokoa huyu mtoto…. nina imani baada ya hapa nitaweza kumiliki duka la vifaa..mbali mbali, na huyu mtoto atakuja kuyafuta machozi yangu….’akasema akitabasamu.

‘Mashallah…hongera sana, nakuombea kila la heri….’nikasema na sasa akawa anataka kuondoka, nikakumbuka kitu na kumuuliza

‘Vipi kuhusu ile familia ya wafadhili wako..iliishia wapi?’ nikamuuliza
‘Ile familia ya wafadhili wangu sasa hivi imeshakuwa kitu kimoja, baada ya wazazi wao kuwapatia idhini, sasa wana mabadiliko makubwa sana,..ndio hapo nimeamini kuwa wazazi ni kitu kingine…na hutaamini,  kijana na baba yake wote walipona, hebu utajua mwenyewe waliponaje, …mola kawafungulia njia…nashukuru sana kwa hilo, na mimi wamenifanya kama mwanafamilia wao, ila sikutaka kuwa karibu sana na wao, nimeamua kuhangaika kivyangu, japo mwanzo mgumu…, ila kila mara nikipata muda nakwenda kuwatembelea…naomba niishie hapa, natumai nimewakilisha..’akasema

NB: Huu ndio mwisho wa kisa hiki. Nawashukuru mliokifuatilia, najua wengi walitaka kiishe haraka wengine kivile, lakini hivi ndivyo ilikuwa ,…tuzidi kuwa pamoja, na mwisho wa kisa hiki ni mwanzo wa kisa kingine,….


                                                 MWISHO

WAZO LA LEO:  Hivi kweli duwa la kuku halimpati mwewe, hii ni kauli ya kuwaasa wale wenye uwezo, wale waliopo kwenye madaraka na hawafuati maadili ya uongozi,  wale ambao wanajiona wanaweza kufanya wapendavyo, kwa wengine, wao ni taifa kubwa, wanaweza kuwadhibiti wengine na wengine hawana nafasi , hata wakionewa, hawawezi kufanyiwa jambo lolote,  ndio wao kwa kiburi wanasema duwa la kuku halimpati mwewe….hivi ni kweli halimpati mwewe?..., duwa la mnyonge huenda moja kwa moja kwa muumba, na malipizo yake yanaweza yasiwe ya haraka, mola mwenyewe anajua ni kwa vipi…

                                    &&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&


*********Mtandao wenu wa ‘Diary yangu’ unawatakia  Iddi el haj, Njema…Iwe ya amani, furaha na upendo, na walioenda kwenye ibada ya Hija, waikamilishe kwa amani na salama na watakachoomba huko kije kutusaidia na sisi, na dunia yetu kwa ujumla…kwani, kumomonyoka kwa maadili kunazidi kuongezeka, watu hawana imani na dini , hawamuabudu yule aliyewaumba, unafiki umejaa kwenye nafsi,....watu wanarejea kule kwenye ujahilia…mambo yanayofanyika ni yale yale yaliyofikia hata kutokea gharika, mambo ya kaumu lut (sodoma na gomora) yanazidi kila siku,  maasi ya kila namna yanaongezeka, watu wanazidi kuchukiana tatizo dogo tu linakuwa ni sababu, kuna zuka makundi ya uhasama...hii ni hatari, tumuombe sana mungu wetu.*******
Ni mimi: emu-three

No comments :