Kwa vile kuna kipindi nilizama kwenye mawazo,
nikapotea kabisa kifikra, sikusikilia alichokuwa akisimulia yule mbaba, kwahiyo
nikamuuliza mama Ntilie anihadithie walichokiongea, hadi wawili hao wakafikia
kusameheana mtu na mke wake,… lakini haikuwezekana kwa muda huo yeye
kunisimulia kwani walifika wateja wakihitajia huduma na siku hiyo ikapita, na
siku ya pili ikawa hakuna kazi nyingi sana, na tulipopata muda na ndio nikaweza
kuelezewa na mama Ntilie, kabla hatujaingiliwa na ugeni mnzito….
Tuendelee na hitimisho la kisa hiki….
**********
Ni
siku ya pili yake baada ya hicho kikao changu na baba na mama , wafadhili wangu
ambao waliondoka baada ya mimi kuhakikishiwa kuwa kweli wamesameheana,
nashukuru mungu kuwa kweli, kwa hali ilivyojionyesha watu hao sasa ni mke na
mume wema.
Kila
muda nilikuwa najiuliza nilipitwa na nini hapo kati, maana sikumbuki jinsi
walivyofikia hapo, ndio ikafikia muda nikamuuliza mama Ntilie..
‘Hebu
niambie ilikuwaje siku ile..?’ nikamuuliza mama Ntilie.
Mama
Ntilie akasema;…
‘Unajua
nilikuona ukiwa umezama kwenye mawazo, sikutaka kukusumbua, nikakuacha tu,
nikawa mimi nasimama badala yako, wakikuuliza swali nakujibia, na ndipo ikafika
ile hatua ya wao kuja kukupigia magoti, nikawaambia…
‘Mngelijua
moyo wa huyo binti ulivyo, hapo yupo kwenye imani na mungu wake, hapo yupo na
mola wake, mimi naona msijisumbue kumpigia magoti, ni nyie tu, kwanza mumuhakikishie kuwa
mumeshasameheana, vinginevyo hataweza kuwa na amani, na kama mlivyosema hatima
yenu itategemeana na huyo binti kwa vile yote yalitokea kutokana na hayo
aliyofanyiwa,…’nikawaambia hivyo.
‘Oh….ina
maana ni hivyo tu…?’ nikaguna na kuuliza.
‘Ndio
nakuanzia, sijui wewe ulianza kupotea wapi, ila nikirudia hapo, baada ya
kuwaambia hivyo, mume mtu akauliza
‘Ina
maana mke wangu asiponisamehe, na yeye msamaha wake hauna maana au sio, sasa
mke wangu muambie kilichopo moyoni mwako, je umenisamehe kiukweli…’akasema.
‘Ndio,
aliniambia kuwa msipofanya hivyo, yeye atamlilia mola wake mpaka musamaheane na
hapo anamlilia mola wake, mimi namfahamu sana…’nikasema wakati huo moyo wangu
una mashaka, ni kwanini upo hivyo, unalia, huongei….’akasema.
‘Mke
wangu unasikia…’akasema mbaba.
‘Mhh, wewe tatizo lako hunielewi, isingelikuwa
ni wazazi wangu sijui kama ningelikusamehe, lakini nimekusamehe, kwa ajili ya
familia yangu…’akasema.
‘Sasa
tumuonyeshe binti yetu,…lakini kwanini anaendelea kulia tu…’akauliza huyo mbaba
akiniangalia mimi, na hao nikasema;
‘Tumpe
muda bado yupo kwenye kumlilia mola wake….’nikasema
‘Unajua
mama Ntilie, tangia tunafika hapa, nilishafikia uamuzi fulani,..maana huko
nilipotoka ilikuwa shughuli kubwa, mimi nilikutana na wazazi wangu, nikiwa nataka ndoa
ivunjwe, lakini cha ajabu sasa wazazi wangu hawataki ndoa nivunje …’akasema mke
mtu.
‘Kwanini…?’
nikamuuliza wakati huo wewe upo kama ulivyokuwa machozi, huongei…
‘Wazazi
wangu wamasema wao sasa wanakiri kuwa
wamefanya makosa, na mitihani wanayokutana nayo kwa hivi sasa inaweza ikawa inatokana
na wao kuwa mbali na watoto wao, hususani mimi na mume wangu…’ akasema.
‘Kiukweli
niliwaonea huruma sana wazazi wangu..na nikawaza sana, nikaona kweli inabidi
tusahau yaliyopita tugange yajayo, ni vigumu lakini utafanyaje…ndio ikabidi
nimtafute huyu mwanaume, sikumuambia nilichoongea na wazazi wangu..nilitaka
nisikie kauli yake ya sasa na ukweli wote,na kama angelificha safari hii,…,
nisingelimsamehe, safari hii alikiri yote tofauti na yaliyotokea kipindi kile
kabla hajachanganyikiwa…’akasema.
‘Kwani
kipindi mlipoitwa na baba yako ilikuwaje…?’ akaulizwa.
‘Siku
ile niliumia sana, kwani alipokuja baba, baba akiwa kajiandaa kumsamehe, yeye
aliendelea kuficha ukweli, mbele ya kijana wetu ambaye alikuwa anafahamu kila
kitu, siku ile…baba alikuja, akatuuliza kuna tatizo gani kwa kijana wetu mbona
kuna kitu kinamsumbua.
‘Kijana
huyu achana naye, nitamalizana naye, ni tatizo dogo tu... Nilishaongea naye,
tatizo hanielewi, unajua watoto wa siku hizi walivyo, …’akasema mume mtu.
‘Eti
kijana kuna tatizo gani…?’ akaulizwa, na kijana sasa alionekana kuwa na
wasiwasi, akawa kidogo anamuangalia baba yake kwa mashaka na mara nyingi
anaangalia chini. Halafu alipoona anasubiriwa yeye kuongea akasema;
‘Mimi
nataka baba aongee yeye mwenyewe, kama hataki kuongea …mimi siwezi kuongea
tena…nimeamua bora yaishe …nitajua la kufanya mwenyewe…’akasema.
‘Kwanini,…
si ulisema utaongea kila kitu…sasa hiki kikao kina maana gani…’akaambiwa.
‘Hapana
nimewaza sana, nikaona ..baba ndiye angelipaswa aongee au seme ukweli..lakini
kama hataki kuusema ukweli,… basi, mimi nitaamua la kufanya mimi
mwenyewe…’akasema
‘Auseme
ukweli gani sasa…ina maana sisi tumekuja hapa kupoteza muda wetu, tukitarajia
kusikia hilo jambo, ambalo lilikupeleka hadi kwa babu yako, ..na hiyo bahasha
yenye ujumbe ipo wapi..?’ akauliza huyo mzee.
‘Mhh..mimi
sijui…’akasema akimuangalia baba yake.
‘Haya
baba mtu hebu tuambie kuna tatizo gani hapa nyumbani kwako…?’ akaulizwa na baba
mkwe.
‘Hakuna
tatizo mzee, matatizo ni ya kawaida, kama ujuavyo maisha yalivyo, kunatokea
mitihani ya hapa na pale, sasa haikuwa na lazima wewe uje, kama ingebidi hivyo,
sisi wakubwa tungekuita rasmi,…, unajua vijana siku hizi wamepata simu, wana
mitandao, wanahisi kila kitu ni kupiga video, hawajui madhara yake,…nimeongea
naye najua keshajirudi..’akasema baba mtu.
`
‘Una
uhakika huna cha kuongea…?’ mama mtu akamuuliza kijana wake, na kijana akainua uso
kumuangalia baba yake halafu akasema;
‘Baba
kama hataki basi…’kijana akasema.
Mimi hapo nilikuwa na ajenda yangu kichwani
sikutaka kusema lolote, nilijua nikisema kitu baba atachukua hatua mara moja,
sikujua baba ana kitu gani moyoni,..na pia nilitaka kusikia mume wangu atasema
kitu gani, hakujua kuwa mimi nilishagundua ukweli wote…’akasema mke mtu.
‘Ukweli
wote uliupataje huo ukweli..?’ akaulizwa na mama Ntilie.
‘Mimi
nilishaupata huo mkanda wa kijana wangu, na ni ule alioupeleka kule kwa babu
yake…’akasema na kila mtu akashikwa na mshangao
‘Kwa
vipi…ina maana muda wote huo ulikuwa nao…?’ akaulizwa.
‘Siku
ile wakati huo mkanda unaletwa kule nyumbani kwa wazazi wangu, nilikuwepo,
nilifika kule kwa mambo yangu, na wakati kijana anaingia na kuonana na mlinzi
nilikuwa dirishani namuangalia, sijui waliongea nini na mlinzi, ila niliona
kijana akimkabidhi huyo mlinzi bahasha,….kwa muda ule nikajua labda mlinzi
alipomuambia kuwa mimi nipo ndani, kijana akaona aondoke, labda alikuwa
akinikwepa, lakini kumbe mlinzi
hakumuambia mimi nipo humo ndani…
Nilitaka
nitoke nje kwa haraka nimuite huyo kijana tuongee naye, lakini hakusubiria,
hata wakati natoka nje alikuwa keshaondoka,..alikuwa anaendesha piki piki lake…na
muda huo mlinzi alikuwa kashika hiyo bahasha wakati natoka, kwahiyo mlinzi
hakupata muda wa kuikagua vyema…mimi kwa haraka nikaona jina la baba juu ya ile
bahasha…sikuwa na shaka nilijua ni mzigo wa baba,..lakini nikajiuliza ni
kwanini aulete huyo kijana…na kabla sijamuuliza mlinzi , yeye akasema;
‘Kijana
wako kaleta bahasha hapa, kaniambia nimpatie babu yake mkono kwa mkono, lakini
mume wako alisema kama kuna mzigo utaletwa hapa na kijana au mtu mwingine
yoyote, nisimpatie baba yako, kwani una makosa, inahitajiak urejeshwe nyumbani,
alinisisitizia sana, je ndio huu, au kuna mwingine…?’ akaniuliza
‘Ni
kweli, wewe nipe nitampatia, kama ndio wenyewe…’nikasema akilini mwangu
nikihisi kuna jambo, kwanini kijana alete huo mzigo, na kwanini baba yake asema
hivyo, akili ikachanganua na kuhisi kuna jambo, na hapo hamasa ya kuchunguza
hiyo bahasha ikanijia…’akasema
‘Unajua
nimekumbuka kuna kazi nilimuachia mume wangu, nahisi ndio hii, ngoja nione kama
kuna cha kubadili nitafanya hivyo, haina haja mpaka yeye aje kuuchukua, ngoja,
nitaongea naye kwenye simu..’nikamwambia huyo mlinzi
‘Lakini
mume wako…’akalalamika
‘Nitampigia
kwani una wasiwasi gani, kwani alikuambia nini kuhusu huu mzigo…?’ nikamuuliza
‘Alinisihi
nisimpe mtu mwingine mpaka yeye aje kuuona mwenyewe….’akasema
‘Alikuambia
huo mzigo ni kwake unakuja hapa kwa baba, atauleta huyu kijana..?’ nikamuuliza
‘Ndio….’akasema
‘Basi
haina shida..nitaongea naye ikibidi nitamsubiria, huenda yupo njiani anakuja,
tutakutana naye hapa…’nikasena na yeye akakubali shingo upande, na hali hiyo
ikazidi kunipa hamasa, nahisi kuna jambo kati ya mume wangu na kijana wangu, na
kuna kitu nyuma ya pazia. Nikaingia na hiyo bahasha ndani, nikaichunguza ndio
nikagundua kuwa video.
Kwa
haraka nikaenda kwenye deki,, bila kujali kuwa huenda ni mzigo wa baba, huenda
ni kazi fulani kijana alipewa kuifanya na baba, …nikaona kwanza niondoe mashaka
moyoni mwangu, nikaiweka kwenye deki na kuanza kuiangalia, kiukweli
nilihamaki..nilikasirika, na kama …sio subira…nashukuru hata baba hakuwepo..’akasema.
Basi
nikawaza sana, nikaona ngoja kwanza nione huu mchezo mwisho wake ni nini, ndio
nikatoka nje nikamsomesha mlinzi anisaidia jambo moja, na hayo aliyoyafanya
mlinzi ni yale niliyomuelekeza mimi..na wakati huo nikapata muda wa kuatafakari
haya mambo vyema, na mpaka hapo nikawa nimejua ni kitu gani kilichokuwa
kikiendelea ndani ya nyumba yangu.
Kiukweli
hadi hapo nikawa nimeazimia uwe mwisho wangu na huyu mwanaume, tuachane tu kwani hayo niliyoyaona sio ya mtu
wa kawaida, hayo ni ya mchawi…na nitaishije ndani na mchawi, ndio, kuna namna
inaonyesha kuwa sio dhamira ya huyu mwanaume kufanya hivyo, lakini
kwanini..kama ni tatizo kwanini asiniambie…na nilipoona ile sehemu ambayo
niliipeleka kule kwa yule mtu anichunguzie, ndio hapo nikazidi kutishika zaidi,
kuwa kumbe naishi na shetani ndani ya nyumba….sasa sina jinsi, kwani ushahidi
ninao, lakini moyoni, nikasema ngoja nimpatie nafasi ya mwisho huyu mtu, unajue
tena mumeshazaa naye, watoto wakubwa, kuna mambo yanakusuta…’akasema mke mtu..
‘Ndio
ikaja hicho kikao chako na baba yako au sio…?’ akauliza mama Ntilie
‘Ndio,
lakini hicho kikao sikuitisha mimi, hicho kikao ni cha kijana kutaka kusema
jambo na alishaongea na babu yake kuwa ana jamabo la kutaka kuongea, na nilion
ajabu ni kwanini tena kijana akaghairi, na sizani kama aliongea na baba yake
akatishiwa, nahisi kuna kitu aliogopa, na sikuwahi kumuuliza..…na cha ajabu
mume wangu hakutaka kusema ukweli, hapo nikajua kweli huyu mwanaume ana tatizo…’
akasema
‘Ni
kwanini hakukubali kusema ukweli, ni ili hali hakuwa na uhakika kuwa hiyo
bahasha iliyotumwa huko kwa baba ipo kwa mlinzi, au baba yake ameshaipata…?’
akaulizwa
‘Hakukubali,
akijua kuwa siri hiyo haijajulikana, yeye alikuwa na uhakika bahasha hiyo bado
anayo mlinzi, na nilimuambia mlinzi amuambie hiyo bahsha bado anayo,… na
walishapanga na mlinzi kuwa alipe kitu kidogo, apewe hiyo bahasha, kwahiyo
akajiona yeye bado yupo salama, …
‘Unajua
mtu kama huyu mpaka mabaya yamkute ndio anaweza kukubali ukweli..sasa utaona
yaliyotokea baadae, ambayo yalimpa fundisho, hebu atuelezee mwenyewe ilivyokuja
kutokea adhabu kutoka kwa mola mwenyewe…’ mkewe akamgeukia mumewe.
*****************
Hapo
ndio mume mtu akaanza kuelezea ilivyokuja kutokea baadae….
‘Ni
kweli, tulikuja kukutana na baba mkwe akiwemo kijana…na nilishangaa mzee alipokuja
alikuwa na sura tofauti na siku nyingine,…alinisalimia kwa unyenyekevu, badala
ya mimi kuanza kumsalimia, ..mzee huyo ni mkali, hana utani kwa watoto,
‘Watoto
wangu nisameheni sana,..nahisi nimekuwa mkaidi kwenu….na naona sasa nahatarisha
ndoa yenu mpaka kijana anakuwa hana raha…na nimegundua bila ya mimi kutoa
idhini yangu kwenu hamtaweza kuishi kwa amani, nimeliwazia hilo sana, kwahiyo kuanzia
sasa nipo radhi na nyie, nimeikubali ndoa yenu, lakini kabla ya hilo nataka
jambo moja kutoka kwa huyu mkwe wangu..je upo tayari kubadilika na tabia yako
hiyo mbaya…?’ akasema
‘Tabia
mbaya, baba nina tabia gani mbaya,..sawa labda mimi nina kiburi, labda…basi
kama ni hivyo mimi nikubali nitabadilika,
nipo tayari kubadilika….!’nikasema
hivyo.
‘Je
upo tayari kubadilika, na kuacha hayo mambo unayoyafanya yasiompendezesha mungu
na ndoa yako..?’ nikaulizwa na mke wangu.
‘Mke
wangu mambo gani yasiyompendezesha mungu…ambayo mimi nayafanya..?’ nikauliza
kwa mshangao.
‘Mume
wangu…unajua hapa yupo baba, hapa yupo kijana, na kijana ana mambo anataka
kuyasema …ambayo yamekuwa yakimkera, ana ushahidi, bado wewe unaendelea kusema
huna tatizo, je huo ushahidi ukitolewa utakuja kusema nini…?’ nikauliza
‘Ushahidi
gani jamani..eti kijana wangu una ushahidi gani kuwa mimi nina tabia mbaya,
nimefanya kitu gani, sema ..au utoe huo ushahidi wako…mmi nipo tayari…na sijui
kwanini haya yote mimi sina tatizo, sijamkosea mtu yoyote na kama nimemkosea
basi..nisamaheeni…’akasema huku nikiwa na mashaka mashaka.
‘Umesikia
binti, huyu mume wako hajabadilika..umesikia mwenyewe, nilikuambia kama kweli
kabadilika basi mimi nitakwua radhi na nyie, lakini kwa hili, bado…bado,
sikiliza binti yangu, mimi nipo tayari kuwapa idhini yangu, lakini nahisi bado,
siwezi kukutelekeza binti yangu kwa mtu ambaye ninajua ana matatizo, kama
utaniamini haya, kama hutaniamini haya,..sisi tutazidi kumuomba mungu, kama upo
ukweli wa haya aje autoe, sina zaidi, labda tumsikia kijana atasema nini…’akasema
baba, na mke angu hakukata tamaa akaniuliza tena..
‘Mume
wangu kwanini unanilazimisha nifanye nisicho kipenda, kwanini hutaki kutubu,
ukajirudi, tukapata baraka za wazazi wetu..mume wangu wewe hadi kijana kasema
una mambo unayoyafanya usiku, sasa unafanya nini, tuambie tukusaidie, kwanini
upo hivyo…?’ mke wangu akaniuliza.
‘Nani
mimi..oh,…hahaha, hivi mke wangu hayo yametoka wapi,..hivi wazazi wangu
wangelikuwepo hapa wakayasikia haya,
wangehisije, kuwa mim kijana wao ni mchawi, au si hivyo unavyotaka kusema...sio
vizuri jamani, mnanifanya nijishi mpweke baba na binti yake mnanisingizia mambo
ambayo sio kweli…’nikasema
‘Na
kama ni kweli, ujue utapata mabaya makubwa sana, maana sisi tunamuomba mola
atusaidie, awasaidie na nyie muondakane na hayo yanayowasumbua, na kama upo
ukweli, aje audhihirishe, utakuja kuumbuka mkwe,…’akasema baba mkwe
‘Nasema
ukweli hakuna kitu kama hicho, mimi sijawahi kufanya hayo unayoyasema baba, au
mke wangu kijan huyu hapa aseme mwenyewe, ..hao waliotaka kufanya hivyo ndio
hao wamelipiliziwa mimi wala sijui walikuwa wakitaka nini…wamekufa ,
wangekuwepo mungeliwauliza wenyewe…’nikasema na baba alipoona sijabadilika akasimama
kutaka kuondoka, kijana wangu akasema;
‘Baba
kwanini hutaki kusema ukweli..?’ aliponiuliza kijana hivyo, hapo nikashtuka…nikajua
sasa kijana anataka kuusema ukweli. Nikamwangalia kwa kumkazia macho, kijana
wangu toka utotoni anajua sura yangu ikiwa vipi nipo na hasira hapo anakuwa
makini na hata kuogopa kuongea, naona hadi sasa kawa mkubwa anajua hulka yangu,
‘Sikiliza
kijana hujui haya…nilikuambiaje mambo ya wakubwa usiyaingilie litakalotokea
utakuja kujuta mwenyewe.., kaa pembeni,…usipende kuingilia mambo ya watu
wakubwa, wewe tabia yako ya unga ndio imekuharibu, acha tabia hiyo,… mimi
sijafanya hayo unayoyafikiria wewe, wewe ni mzushi, ni unga wako unakupeleka
kubaya, na tabia yako hiyo mbaya, uiache mara moja, unasikia, sitaki tena
kusikia kijana wangu anatumia unga, iwe mwisho leo……’nikasema kwa ukali…
Kijana
alitulia kwa muda, machozi yakawa yanamlenga lenga…kijana wangu sio mdogo,
angeliamua la kufanya hapo angelifanya, lakini nahisi kuna kitu kilimpata au
kuna mtu kamshauri akaona awe hivyo.
‘Basi
mimi naondoka kwenye hii nyumba, maana sasa naonekana kuwa mimi nii mzushi,
maana sasa kila mtu ananionyeshea kidole mimi kuwa nilitunga uwongo, na mambo
yangu yote niliyoyaweka kama ushahidi umeyaharibu, sasa…naonekana mimi kama
mzushi, na hata huku kuumwa nazusha tu…, haya, mimi naondoka zangu, nitajua
mwenyewe la kufanya….’akasema na kuanza kuondoka. Hakuna aliyemzuia…
Kijana
hakuonekana tena hapo nyumbani, na hata huko kwa babu yake hakufika tena, siku
zikapita…na mpaka tuliposikia taarifa hiyo ya kukamatwa kwake…
Sasa
baada ya kikao kile,…yaliyofuatia hapo kwangu ilikuwa ni mawazo , mawazo….nahisi
kabisa sipo sawa…namuwazia kijana wangu nawazia hayo niliyoyaona kwenye hiyo
video, nawazia….yaani sielewi..
Nikawa
sasa najilaumu, kwanini nilifanya hayo,
kwanini sikukubali kusema ukweli, kwanini sikukubali kuwa hayo yaliyotokea
usiku nilikuwa nahusika, nikaungama mbele ya familia yangu, na je nitafanyaje ili
kijana wangu apone…mawazo hayo hayakuniacha, mara siku moja nikahisi sauti
nyingi zikizizima kichwani mwangu, yaani ikawa kama kichwa na watu wanaopiga
kelele…na haikupita muda nikawa sijitambui, nikatoka mbio mbio huku niki-ita…jina
la kijana wangu!
‘Kijana
wangu njooo..nitasema kila kitu, nimekosa kijana wangu…’ilikuwa sauti yangu ya
kila siku nikawa sasa ni mtu wa kushikwa, nataka kukimbia…nikiuliza ni nini
shida, kauli ni hiyo,..namtafuta kijana wangu…na hata kijana wangu
alipopatikana nikawa simtambui tena, nahisi kama sio yeye, ikawa ni kazi hadi
nikafikishwa muhimbili wodi ya wenye matatizo ya akili, baadae nikarejeshwa
nyumbani, ikafika muda sijijui kabisa..
Masiku,
miezi ,.nipo hivyo..na kuna wakati hali inajirudi, lakini sio kwa kujielewa
sana, mke na wanafamilia walijitahidi kila aina ya matibabu,..mwishowe
nikawakimbia,..hayo mimi siyajui, nasema sasa kama nilivyokuja kuambiwa…na ndio
nikaja kukutana na nyie..
‘Kwahiyo
safari zote hizo ni za kumtafuta kijana wako…?’ akaulizwa
‘Ndivyo
ilivyoanzia hivyo, na nilipo-potelewa kabisa, akili iliyokuja baadae ni ya
kumtafuta huyo binti…anisamehe...’akasema
‘Jamani
hicho ndicho kisa changu…
***************
Na
alipofikia hapo ndio akageuka kukuangalia wewe, akashanga kukuona anabubujikwa
na machozi, hapo, akashtuka, na ile hali ye yeye kushutuka, ikawafanya na
wengine wote kugeuka kukuangalia, mimi nilishakuona ulivyo…tokea awali nilikuwa
nimetulia tu, ndio mama mtu akasema;
‘Oh, binti..usilie, mimi nimeshakubali haya
yaishe, na japokuwa kwa shingo upande, nimekubali kumsamehe mume wangu,na wewe
sasa tunakuomba utusamehe…..’ilikuwa kauli ya mama huyo
‘Hayo
ndiyo yalitokea ukiwa umezama kwenye duwa sijui,..ulikuwa unaomba …si ndio
hivyo, mmmh na maombi yako sio mchezo, yakajibu…’akasema mama Ntilie.
******************
Siku
zikapita na siku moja, ukafika ugeni, ni ugeni ule wa awali, wa wale watu
walikuja kutaka kununua lile eneo la urithi huko kijijini, sasa wakisema wamekamlika,
kwahiyo mimi na wao tuongozane hadi
benki ambapo huko ndio malipo yatafanyikia, mama Ntilie akasema kwa siku hiyo
yeye hawezi kuacha shughuli zake mimi niende peke yangu tu.
‘Usijali
hawa ni watu wema hawawezi kukudhulumu…’akasema na mimi nikaondoka na hao watu
hadi benki ambapo nilishafungua akaunti yangu, nikalipwa hizo pesa,
tukaandikishana na hao watu, na kila kitu kakamilika kwa mara ya kwanza nikawa
na milioni kadhaa benki,
Sasa
wakati tunatoka hapo benki, tupo nje ya korido la benki,…mmojawapo akaniuliza;
‘Dasa
samahani wewe una matatizo gani yanayokusumbua…?’ akaniuliza na kunifanya
nishikwe na mshangao, nikamuuliza hivi
‘Nina
matatizo!!...nina matatizo gani!..., kwanini unaniuliza hivyo…?’ nikauliza na
mwingine akasema;
‘Huyo
hapa mwenzetu ni mtu aliyejaliwa kipaji cha kusaidia watu wenye matatizo,
anaweza kukuangalia hivi tu akatambua matatizo yako, na jinsi ganii ya
kukusaidia, huwa anajiwa na vitu kama njozi…na tukuambie ukweli, siku ile
tulipofika awali alipokuona tu, yeye akagundia kuwa una matatizo makubwa sana…ambayo
yanahitajia msaada wa haraka, kabla hujajifungua…’akasema.
‘Mhh…mimi
naona hayo hayana umuhimu kwangu, na sihitaji mtu wa kunisaidia,..najua mungu
pekee ndiye wa kunisaidia, kama nina matatizo nimeshayafikisha kwa mwenyewe,
nasubiria matokeo tu, vyovyote itakavyotokea najua ni kwa matakwa yake…’nikasema.
‘Hapana
hakuna malipo yoyote utalipa kwetu, ..sio kwamba tunafanya hivyo kwa vile una
pesa, hapana..kamwe hatutaki hata senti moja yako….na sisi hatuwezi kuondoka
bila kukuambia hilo na kama utahitajia kusaidiwa, ..na si kusaidiwa, sisi
tunachofanya ni kumuomba mola wetu…yeye, huyu mwenzetu kasema hataweza kuishi
kwa amani akiondoka bila kukusaidia, na yeye anamtegemea mungu wake,…yeye
atakuombea tu, na mengine tutamuachia mungu, utuelewe, sisi ni watu wa imani…’akasema
‘Wapi
sasa, hapa hapa, au …?’ nikajikuta nimesema hivyo, niikiwa siamini maneno yao…,
sikuwa na mawazo hayo tena kuwa mimi nina tatizo. Nilijua nimeshamkabidhi mola
wangu…
‘Vyema
turudi kule nyumbani unapofanyia shughuli zako, ili tupate nafasi kuliko hapa,
ila ni kama wewe upo radhi, na kama haupo radhi basi, sisi tutakuacha, ila
mwenzetu huyu kajaliwa kipaji cha namna hiyo na amewasaidia watu wengi sana
tena bure…’akasema huyo kiongozi wao.
Basi
mimi sikuwa a kipingamizi tukarudi nyumbani, nilikuwa nimechukua kiasi fulani
cha pesa kwa ajili ya kuongezea biashara na mama Ntilie.. Tulipofika, hakukuwa
a wateja wengi , nikamuelezea huyo mama kilichofanyika na hayo wanayotaka kuyafanya
hao watu,..huyo mama akaniita pembeni.
‘Unawaamini
hao watu wasije wakafanya hivyo kesho na kesho kutwa unakuta pesa yote imekwisha
huko benki…’akasema
‘Wao
ndio wamenilipa, wao ndio wamefanya juhudi yote hiyo, wao ni watu wa dini, mimi
nimewaamin, na najua mungu atanilinda, huenda ikawa ndiyo sababu ya kuondolewa
hii mitihani, tumuachie mungu anajua zaidi …’nikasema
‘Sawa….kama
umewaamini mimi sina shaka…’akasema na basi wale watu wakaniombea na yule
mmojawapo ambaye ndiye mwenye hicho kipaji akasema nilale tumbo juu, nikafanya
hivyo, yeye akaweka kiganja chake tumboni,i kwangu, nilihisi tumbo likitetemeka
kama mtu aliyeshikwa na umeme, iliendelea hivyo kwa muda, badaye likatulia.
‘Pole
sana…natumai sasa utajifungua salama…’akasema huyo mtu wa dini.
‘Kwani
ni kitu gani umekigundua …?’ akauliza mama Ntilia
‘Inaonekana
huo uja uzito una maagano ya shiriki ndani yake, ..lakini yamekwisha, muhimu ukijifungua
tu hakikisha unatimiza wajibu wote wa mtoto,…kumuomba mola wako, ..na kamwe
usije kumshirikisha mtoto huyu na mambo ya kishirikina…yeye anahitajia imani
tahabiti ya dini, ndiyo itakayomsaidia, na ianzie kwako wewe,… hakikisha
unamfanyia mambo yote yanayostahiki kwa mtoto, itamsaidia sana yeye huko
mbeleni kwenye maisha yake…na kama kutatokea tatizo usisite kutupigia simu..’akasema
na wakaaga kuondoka.
‘Lakini
lazima niwape kitu kidogo…’nikataka kuwapa pesa, wakakataa, na kusema;
‘Sisi
tunarudi huko kijijini, na kuanza kazi za ujenzi, tunashukuru sana, kwani
pamoja na hizo pesa tulizokulipa kwa ajili ya hicho kiwanja, lakini fadhila
zitakazopatikana kwa ajili ya nyumba hiyo ya ibada zitakusaidia hata wewe na familia
yako huko mbele…ukumbuke ukitoa kwa jili ya mwenyezimungu utarajie malipo
makubwa sana, hiyo ni akiba yako endelevu, hata ukiwa haupo hai… na hebu
fikiria hiyo nyumba ya ibada itadumu muda gani,..na kila siku utakuwa unapata
fadhila kiasi gani…umefanya jambo la maana sana…’wakasema
‘Nashukuruni
sana, nawashukuruni sijui niwalipe nini, chukue hii sadaka yangu basi…’nikasema,
na wao wakasema sio kwa wakati huu kwani itakuwa nimetoa kwa ajili ya hayo
waliyoyafanya
‘Usijali…kwani
hutakiwi utulipe chochote, ..sisi kazi yetu ndio hii ya kuitangaza dini, na kwa
hili umetusaidia sana kwani tutakuwa na sehemu yetu ya kudumu…kwa ajili ya
ibada na ofisi ya mambo ya kidini…’wakasema na baadae wakaaga na kuondoka.
Hutaamini
baada ya tendo hilo , nilihisi kamaa nimepunguziwa mzigo tumboni, awali
nilikuwa kama nimebeba mzigo mzito ambao unahisi unataka kudondoka, lakini
baada ya hapo, japokuwa nina kitu tumboni lakini sio kama vile awali, na ile
hali ya kusikia vibaya, ikawa imekwisha kabisa,..
Baada
ya miezi kutimia nilifikishwa hospitalini, nasema nilifikishwa kwa maana hali
hiyo ilinianzia nikiwa nyumbani, na kiukweli, nilipofika hospitalini haikuchukua
muda, nikajifungua salama, japokuwa mtoto alitoka akiwa sehemu kubwa ya mwili haina
ngozi, ni kama mtu aliyeungua, docta wakasema ni udhaifu tu wa ngozi tu
itaisha…
Basi
mimi nikafuatilia masharti yote ya jinsi mtoto akizaliwa anatakiwa kufanyiwa
kidini, na siku baada ya siku,..hali ya mtoto ikawa inakuwa vyema, ngozi
inarejea, kunabakia makovu ya kawaida tu..namshukuru mungu sana, kwani hadi
sasa kama unavyomuona ngozi yake inakuwa
kama ya kawaida, ni alama alama zinabakia tu.., na mtoto mwenyewe ndio huyu
hapa..’akasema huku akinionyeshea mtoto wake.
‘Mhh..hongera..tena
mtoto ana afya nzuri kabisa, sijui kwanini walisema hivyo, kuwa atakuwa sio
kiumbe wa kawaida, mbona ni mtoto mnzuri kabisa, imani za shirkiii mbaya sana…’nikasema
na hakunijibu hiyo hongera yeye akasema;
‘
Unajua nilijiuliza sana , nilijiuliza tu,…hivi kweli duwa la kuku halimpati mwewe..’akasema
‘Kwanini
ukajiuliza hivyo…na wewe umeliona hilo kivitendo.au sio…wale waliojifanya wao
ni zaidi ya wengine, wanaweza kuingia majumba ya watu wakafanya wapendavyo,
mbona wameshindwa kupambana na hayo yaliyowakuta…kwahiyo hiyo kauli ilikuwa ya
kuwaasa hao watu au sio..?’ nikasema
‘Mhh…kiukweli,
mimi sijui, ila najua kuwa msemo huo ulitolewa kwa maana fulani maana wazee
wetu walikuwa an hekima sana…ila nimeamini kuwa, masikini silaha yake kubwa ni
duwaa, ni maombi kwa mola wake, na muhimu wakati unafanya hivyo uwe na moyo
safi, usiwe na hasira za visasi, chuki kwa wengine…mimi hilo nimelithibitisha
kwa vitendo..’akasema.
‘Hata
hivyo,..kila hali ina mitihani yake, umasikini una mitihani yake mingi tu..kama
ulivyo utajiri, na ili uweze kuishinda hiyo mitihani,…yabidi uikubali hiyo
hali, lakini usijipweteke, upambane na mazingira, utafute hukio ukiwa huna kinyongo
na mtu, na hata ukitendewa mabaya, usikimbilie kulipiza kisasi, kwa njia za
uovu, …’akawa anasimama kutaka kuondoka.
‘Ni
kweli, lakini kwa walimwengu, sizani kama atakubali atendewe ovu akae kimia
tu…wengi tunakimbilia visasi tena wati mwingine hata huna uhakika na hilo
jambo…ndio hulka zetu…’nikasema
‘Kwa
ushauri wangu, kama wewe ni mnyonge utafanyaje sasa,..kuliko kuingia kwenye
shiriki, kwanini tusimuombe mola wetu atusaidie…na wakati unafanya hivyo
usiwalipizie maombo mabaya hayo waovu wako, moyoni wasamehe na ufanye hivyo kwa imani thabiti…imani hiyo thabiti
ndio inageuka kuwa silaha ya mnyonge… hutaamini hapa nipo hivi, unaniona bado
nipo kama hohe hahe, lakini sio kwamba mimi ni masikini tena,..hapana..’akatabasamu
kidogo.
‘Umepata
utajiri, kutokana na kile kiwanja au…?’ nikamuuliza
‘Hiyo
ilikuwa miongoni mwa neema alizokuja kunipatia mola wangu,…hapa najibana tu, ili niweze kujiajiri, kuna mipango inakamilika,…maana
nilikutana na wataalamu wa ujasiriamali wakanielekeza na kunisaidia jinsi gani
ya kuwekeza, kile nilichojaliwa nacho, na ikibid nichukue mkopo kidogo
niongezee, nimefanya hivyo,…
‘Na..ni…
hatua kwa hatua, lakini najua sio kazi rahisi, inabidi nipambane kweli, maana mtoto huyu anakua, atahitajia kusoma, sitaki
itokee sababu, watu waseme uliambiwa…ni staki nirudie makosa ya nyuma,
siwalaumu wazazi wangu, lakini sitaki niwe kama wao..na sitaki mtoto wangu
aishie kama mimi nataka yeye awe zaidi ya mimi, na, elimi ndiyo itakayomuokoa
huyu mtoto…. nina imani baada ya hapa nitaweza kumiliki duka la vifaa..mbali
mbali, na huyu mtoto atakuja kuyafuta machozi yangu….’akasema akitabasamu.
‘Mashallah…hongera
sana, nakuombea kila la heri….’nikasema na sasa akawa anataka kuondoka,
nikakumbuka kitu na kumuuliza
‘Vipi
kuhusu ile familia ya wafadhili wako..iliishia wapi?’ nikamuuliza
‘Ile
familia ya wafadhili wangu sasa hivi imeshakuwa kitu kimoja, baada ya wazazi
wao kuwapatia idhini, sasa wana mabadiliko makubwa sana,..ndio hapo nimeamini
kuwa wazazi ni kitu kingine…na hutaamini, kijana na baba yake wote walipona, hebu utajua
mwenyewe waliponaje, …mola kawafungulia njia…nashukuru sana kwa hilo, na mimi
wamenifanya kama mwanafamilia wao, ila sikutaka kuwa karibu sana na wao,
nimeamua kuhangaika kivyangu, japo mwanzo mgumu…, ila kila mara nikipata muda
nakwenda kuwatembelea…naomba niishie hapa, natumai nimewakilisha..’akasema
NB: Huu
ndio mwisho wa kisa hiki. Nawashukuru mliokifuatilia, najua wengi walitaka
kiishe haraka wengine kivile, lakini hivi ndivyo ilikuwa ,…tuzidi kuwa pamoja,
na mwisho wa kisa hiki ni mwanzo wa kisa kingine,….
MWISHO
WAZO LA LEO: Hivi
kweli duwa la kuku halimpati mwewe, hii ni kauli ya kuwaasa wale wenye
uwezo, wale waliopo kwenye madaraka na hawafuati maadili ya uongozi, wale ambao wanajiona wanaweza kufanya
wapendavyo, kwa wengine, wao ni taifa kubwa, wanaweza kuwadhibiti wengine na
wengine hawana nafasi , hata wakionewa, hawawezi kufanyiwa jambo lolote, ndio wao kwa kiburi wanasema duwa la kuku halimpati mwewe….hivi ni kweli
halimpati mwewe?..., duwa la mnyonge huenda moja kwa moja kwa muumba, na
malipizo yake yanaweza yasiwe ya haraka, mola mwenyewe anajua ni kwa vipi…
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
*********Mtandao
wenu wa ‘Diary yangu’ unawatakia Iddi
el haj, Njema…Iwe ya amani, furaha na upendo, na walioenda kwenye ibada ya Hija, waikamilishe kwa
amani na salama na watakachoomba huko kije kutusaidia na sisi, na dunia yetu
kwa ujumla…kwani, kumomonyoka kwa maadili kunazidi kuongezeka, watu hawana imani
na dini , hawamuabudu yule aliyewaumba, unafiki umejaa kwenye nafsi,....watu
wanarejea kule kwenye ujahilia…mambo yanayofanyika ni yale yale yaliyofikia
hata kutokea gharika, mambo ya kaumu lut (sodoma na gomora) yanazidi kila siku, maasi ya kila namna yanaongezeka, watu wanazidi kuchukiana tatizo dogo tu linakuwa ni sababu, kuna zuka makundi ya uhasama...hii ni hatari, tumuombe sana mungu wetu.*******
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment