‘Kabla
hujaendelea mbele naona muda unakwisha,
nauliza maana mpaka hapo ulipofikia, sijasikia kuwa ni nani mwenye huu
mzigo, hiyo mimba ni ya nani,...’alikuwa mama Ntilie akinionyeshea mimi kidole tumboni, na hapo
akili ya kufuatilia hiki kisa ikapotea na kurejea kwenye hali yangu,…
Mzee
mzima akageuka na kuniangalia, akatikisa kichwa na kusema;
‘Yaani
sijui nisemeje…kama nilivyoelezea awali mambo ya usiku mimi nilikuwa siwezi
kuyaona, sasa siwezi kudanganya, …’akasema.
‘Yawezekana
ni yako..ndio maana unavuta vuta muda…’akasema mama Ntilia
‘Mhh..hebu
kwanza tuendelee na muendelezo, kama kuna swali mtakuja kuuliza baadae maana
huko mbele ndio tutapata ufumbuzi, wa swali lako…na mimi nitawaambia maamuzi
yangu ambayo yamenifanya nifike hapa hii leo, najua wengi watanishangaa lakini
haina budi…’akasema mke wa jamaa
Yule
mbaba akamuangalia mke wake kwa macho ya huruma, na alipoona kuwa yeye ndio
anasubiriwa kuendelea kuongea, kwanza akakohoa…
Tuendelee
na kisa chetu.
********
‘Baada ya kupokea simu hiyo kutokwa kwa yule
mlinzi nilichanganyikiwa, kumbe sikuchukua ile bahasha yenyewe, nilikuwa
nimechukua bajasha nyingine, lakini pale nilipoichukua bahasha hiyo hakukuwa na
bahasha nyingine, labda hiyo yenye video alikuwa kaiweka kwingine,…Ilichobakia
hapa ni kuchukua hatua…
Kwanza
nikageuka kumwangalia mke wangu, yeye alikuwa kainamisha kichwa chini,
nikageuka kumuangalia kijana, kijana alikuwa akinitazama mimi na ile bahasha bado ipo mikononi mwake,
alipoona namuangalia akheuka kumuangalia mama yake hapo akafanya kosa, mimi kwa
haraka nikatembea kwa kasi na kumkabili kijana, na kubakua ile bahasha mkononi
mwa kijana, yaonekana hakulitegemea hilo, na kabla hajasema kitu,.nikisema kwa
hasira.
‘Sasa
unaona …babu yako keshajua kila kitu, haya nikutokana na mambo yako ya kitoto,
nilikuambia uniamini mimi, haya nenda kwa babu yako akusaidie na huu mkanda
ndio unataka mama yako akauangalia, haya ngoja nimpe akaangalia yaliyomo ,
tuone matokea yake yatakuwaje..’nikasema na kutembea kuelekea kwa mke wangu
nikimkabidhi huo mkanda, lakini mke wangu hakuinua mkono kuipokea hiyo bahasha.
‘Chukua
sasa uangalie kilichopo, ambacho ndicho huyo kijana wako kampalekea baba yako…’nikasema
moyoni nikiomba ujanja wangu ufanye kazi, ni ujanja wa kuwajulia hawa watu
tabia zao..nilijua kabisa mke wangu hawezi kuchukua kwa haraka hivyo.
‘Kwanza
ni nini kipo ndani ya hiyo bahasha…aah, hayo ni mambo yenu sitaki hata kuyaona…’akasema
na moyoni nikasema bao moja tayari, nikageuka kumuangalia kijana na kusema.
‘Haya
unasemaje sasa….?’ Nikamuuliza
‘Baba,
…huko kwa babu …’kabla hajasema kitu, mara simu ya mke wangu ikalia, na mke wangu akaipokea na
kusikiliza;
‘Unasemaje
baba…?’ akauliza.
‘Mjukuu
wako nipo naye hapa, kuna nini..?’ akauliza
‘Mzigo
gani..?’ akauliza
‘Kwahiyo
unataka kusema nini…?’ akauliza
‘Ok,
sawa atakuja muonane naye…’akasema na kugeuka kumuangalia kijana, na kusema;
‘Babu
yako anasema uende mkaonane naye…’akasema
‘Huo
mzigo keshaupata..?’ nikauliza lakini mke wangu hakujibu kitu, akawa
anamuangalia kijana wake kwa makini,
‘Hebu
sasa niambie una tatizo gani mpaka uende, na….na kitu gani hicho ulichompelekea
babu yako..?’ akamuuliza.
‘Mama kila kitu kimejielezea humo, sikutaka
kuongea, sikutaka hii hali ya kuulizwa ulizwa maswali, mimi sipendi kuulizwa
ulizwa maswali,…na…’akasema sasa akimuangalia baba yake ambaye alikuwa
kashikilia hiyo bahasha.
‘Huyu mtoto wako hana akili, hajui
alivyoharibu, anatuvizia na kutupiga picha tukiwa tunagombana,..kila tukio
analiweka kwenye video, hiyo ni tabia gani …sasa ndio kaamua kumpelekea baba
yako ili aone jinsi gani hatupo sawa, nia yake ni nini kuvunja ndoa yetu,…’nikasema
na sasa nikitaka njia ya kutoka humo ndani.
‘Basi
kama ni hivyo, basi, ngoja tuone
kilichomo, halafu nitajua la kufanya…’akasema mke wangu akiangalia ile bahasha
niliyo nayo mkononi.
‘Hakuna
cha maana hapa, hivi sio vitu vya kuweka, maana vikitua kwa watu wabaya
tutapata shida sana…tatizo ni hiyo aliyoipeleka kwa baba yako,..sijui
itakuwaje…’nikasena sasa nikiiweka ile bahasga kwenye koti langu.
‘Kama
ni hayo uliyoyaelezea sizani kama kuna tatizo, labda kuwe na jamabo jingine
ambalio wewe hutaki kulisema, eti kijana wangu niambie ukweli…’akasema mama.
Kijana
akawa katulia tu, …na mara simu ya mke wangu ikaita;
‘Nini
tena baba, mara ya pili unanipigia simu..nipo kwenye kikao…, ndio..tupo wote
hapa kuna nini kwani baba…?’ mke wangu akauliza.
‘Unasema
unataka kuja huku, eeh, kuhusu nini…?’ akauliza na kusikiliza.
‘Bahasha
gani hiyo, kutoka kwa kijana wangu, ya nini..?’ akauliza na kutulia kimia
akisikiliza
‘Hapana,
sina habari yoyote..’akasema mke wangu huku akimuangalia kijana, na kijana
akageuka kutaka kuondoka na mama akamuashiria kwa mkono asiondoke.
Na
alipomaliza kuongea na simu akamuambia kijana…
‘Unakwenda
wapi subiri babu yako anakuulizia, …’ akasema
‘Hapana
mama mimi nataka kuondoka,…sitaki tena kukaa humu ndani…’akasema sasa akitoka
kwa kasi humo ndani, kama anakimbia..
Mimi
nikawa namuangalia mke wangu kutaka kujua atasemaje , lakini hicho cha babu
yake kuja hapa, kama kauona huo mkanda nafahamu kabisa ni nini
kitakachoendelea, na kama keshauona huo mkanda ni bora nisikutane naye kabisa,,
ili kuwa na uhakika nikauliza;
‘Baba
yako anasemaje..?’ nikauliza
‘Anataka
kuja hapa nyumbani, na anataka sote
tuwepo,…’akasema.
‘Sote tuwepo…!
Na wakati kijana ndio huyo kakimbia, kagundua upuuzi alioufanya hauna maana,
kwani baba kasemaje kuhusu hicho kikao ni kuhusu nini hasa…?’ nikauliza
‘Hajasema,
ngoja….’
Baadae
mke wangu akaamua kumpigia baba yake kuwa kikao hicho anachokitaka yeye kwa leo
hakitawezekana..
*************
Nilibakia
na mke wangu, nikisubiria amalize kuongea na simu, na wakati anaongea na baba
yake mara simu yangu ikalia..nikaipokea kwa haraka;
‘Nani
mwenzangu..?’ nikauliza,na huyo mtu akaongea kwa sauti kama ya kuigiza, mimi
moja kwa moja nikajua ni yule mlinzi
‘Unataka
nini, si umefanya ulichotaka, sawa bwana, najua malipo ya wema wangu kwako ndio
hayo, sasa umepata faida gani…?’ nikamuuliza na kusikiliza alichokuwa akiongea,
sikuamini kuwa mtu huyo anaweza kunifanyia hivyo.
‘Unasema
nini…?’ nikasikiliza kwa makini anachokiongea
‘Unasema
unataka nikulipe niini…acha uhuni wewe mtu…wewe kama haja yako ni pesa, sio
lazoma utumie njia hiyo, unasikia,…aah, hapana hatuendi hivyo,…hebu jiulize, je
nikiamua kumwambia bosi wako kuwa, huoni utapoteza kazi yako, au unasemaje
nimwambie…’nikasema na simu ikakata.
Huyu
mlinzi anasema kuwa ile bahasha hajaipeleka, kapeleka bahasha nyingine tu, na
hiyo bahasha anayo yeye mkononi, na amegundua kuwa ndani ya ile bahasha kuna
video, video ambayo ni hatari ikiingia mikononi mwa watu hasa watu wa mitandani
na magazeti, na pia ikifika kwa mzee, baba mkwe wangu, kwahiyo kwa hivi sasa
anayo hiyo video, kama nitaka yeye anahitajia pesa nyingi tu, hakusema kiasii
gani, vinginevyo atamkabidhi bosi wake,
na kumuomba msamaha …’akakata simu.
Niliwaza
sana hilo, na wakati nawaza hayo nikawa namuangali mke wangu, sikutaka kabisa
ajue hicho kinachoendelea kati yangu na mlinzi wa baba yake,….na baadae mke
wangu akamaliza kuongea na simu, akaja na kuniangalia usoni…
‘Mzee anasema tuhakikishe leo tunakutana na
yeye, atakuja yeye mwenyewe …’akasema
‘Kwani
hilo lina tatizo, tatizo ni kijana wako, je tunaweza kumpata..?’ mume akauliza
‘Hilo
sio tatizo, baba keshaongea naye, na kakubali kuwa atakuwepo kwenye hicho
kikao, kwani yeye ana mengi ya kuelezea,...na anao huo ushahidi wa hicho
anachotaka kukisema…’akasema
‘Oh,
kwahiyo kumbe bado hajanielewa..’mume mtu akasema na kutizima nje, akilini
akijua ana majanga mawili tayari, sijui aanze lipi kwanza.
‘Akuelewe
vipi, baba gani wewe, mwenye tabia ya ajabu, hata ingelikuwa mimi, ningelifanya
hivyo hivyo..sasa ujiandae, nafahamu maamuzi ya baba, na nikuambie ukweli safari hii,
tutasigishana,..ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wazazi wangu,
vinginevyo…’akatulia
‘Vinginevyo
nini…?’ nikauliza
‘Vinginevyo,
…nitayaongea hayo kwenye kikao,….na najua hicho kitakuwa kikao cha mwisho baada
ya hapo sitaki tena kikao na wewe…’akasema na kuanza kuondoka
‘Je
kikao kitafanyika saa ngapi mbona unaondoka…?’ nikauliza lakini mke wangu
hakujibu akawa keshaondoka, na mimi nikabakia peke yangu nikijiandaa kwenda
kukabiliana na huyo mlinzi.
*******************
Wakati hayo yakiendelea, mbaba akiendelea
kusimulia yaliyomsibu,
Mimi ghafala akili ikahama, nikawa nawaza
mengine tofauti, ikafika muda hata sisikii hicho wanachokiongelea sijui kwanini
mawazo hayo yaliteka akili yangu…
Nilijiuliza ni kwanini mimi ndiye yanikute
hayo yote….mimi nimezaliwa masikini, wazazi wangu walikuwa omba omba, kula yetu
na maisha yetu yalitegemea kile tutakachopewa na wasamaria wema,..na kwa bahati
ndio nikapata hiyo kazi ya ufanyakazi wa ndani,…lakini badala ya kupata kile
nilichotegemea ndio nikazidi kuingie kwenye mtihani mkubwa.
Mama yangu niliyemuacha huko kijijini,
akisubiria angalau jasho la binti yake, akaishia, kuangamizwa kwa kuchomewa
banda lake na yeye kufariki kutokana na majeraha ya huo moto, je ana kosa gani,
je walifanya hivyo ili iweje,..
Nasikia kumbe lile kundi la uharamia, la
vijana hao waliotelekeza dhuluma hiyo lilikuwa likisimamiwa na huyo huyo marehemu,
nia na lengo lake ilikuwa kupora ardhi ,lakini hata baada ya adhima yake hiyo
kutekelezwa, akajikuta bado anagombea eneo hilo na hasimu wake.
Hayo nilikuja kusimuliwa na wale watu wa dini
waliokuja kunitembelea wakinitafuta mumiliki halali wa eneo hilo, na hilo
lilikuja kukubaliwa baada ya watu kushindwa kulimiliki. Kwani hao waliotaka
kulimiliki kwa dhuluma, hawakuweza hata kujenga nyumba, kila walichofanya
kilishia kibaya.
Lakini hayo hayakunisumbua sana, kilichonisumbua
sana akilini ni mawazo ya hatima yangu, tumboni nina kiumbe, je ni mtoto kweli,...na kama sio mtoto itakuwa ni nini...na huenda akawa ni mtoto, atakuwaje nikijifungua, na mpaka hapo , maelezo yote ya huyo mbaba, hakuna sehemu inayofichua ukweli wa hii mimba, ni nani anahusika, sio hoja kwangu, hoja ni je atazaliwa kiumbe wa namna gani
Nikawa najiuliza sana hilo swali, lakini hata nikijiuliza ni nani atafahamu, hapo nikaona nimuachie mola mwenyewe,, ..kila nilichowaza hapo hakikuwa na ufumbuzi, ..nikiisia kujiuliza tu, kwanini mimi…kwanini mimi nizalilishwe hivyo, kwanini mimi
yanitokee hayo yote, nimekosa nini jamani…’hapo machozi yakawa yanazidi kunitoka
kwa wingi.
Sasa nikaona mawazo hayo hayatanisaidia, ndio nikazama kwenye imani ..nikawa sasa namuomba
mola wangu nikisema kimoyo moyo…
.
'Ewe mola wangu, nisamehe kwa dhambi hii, mimi sijui nimetenda madhambi gani hadi haya yanikute, wewe peke yake ndiye unaye ujua ukweli wa haya yote, mimi ni kiumbe dhaifu tu,..uwezo
wa kuyabeba haya kwa hivi sasa sina tena.., kama kweli wapo watu wenye uwezo wao waliamua kuyafanya
haya, wewe unawajua, na sipendi kusikia tena walitaka nini kwangu, na hata hivyo, mimi sina nia ya kuwaombea mabaya,...wasamehe tu... na sina lengo la
kulipiza kisasi, ninachokuomba uwasamehe tu hilo kwangu ni faraja…’nikapandisha viganga vyangu usoni na
kuyafuta machozi.
‘Nakuomba mola wangu uwasamehe, hususani huyu baba hapa, nawatambua hawa kama walezi wangu, najua walichokifanya ni kibaya, lakini
ni katika kuhangaika kwao, walijua wakifanya hivyo labda watafanikiwa lakini ni shetani tu kawazidi nguvu, mimi nakuomba uwasamehe, na nitajua kuwa umewasamehe kama
nilivyowasamehe mimi, nikisikia wamesameheana na kurejeana kama mke na
mume....' hapo ni machozi tu yanatoka,..hata nilipojitahidi kuyazuia sikuweza.
‘Nakuomba ewe mola wangu, na huyo kijana wao, apone, aondokane
na mitihani inayomakabili arudi na kuungana na wazazi wake..hili kwangu
litakuwa ni faraja kubwa sana, na huyo binti naye aachiwe awe huru, kwani na yeye ni miongoni mwa waathirika wa mitihani hii ambayo, wewe peke yake ndiye unajua ni kwanini ilifanyika kwetu, huyo binti kadhulumiwa na yeye, lakini najua na yeye atasamehe , na kusamehewa,..nakuomba ewe mola wangu wangu unitimizie maombi yangu hayo,
..sijui nifanye nini ili unitekelezee hayo maombi yangu…’nikainua viganja
vyangu na kufuta machozi yangu tena.
Hapo nikahisi hicho kiumbe tumboni kikinikwangua, nilihisi maumivu na baadae yakapoa, nikaendelea na mawazo yangu sasa yakiwa ya kuomba tu.....
‘Pamoja na hilo, …nakuomba mola wangu, kinyume
na imani za hao watu walionifanyia hivyo, nakuomba tena na tena hii mimba, huu,
uja uzito uwe ni faraja, kwangu, nimzae mtoto aje kunifuta haya machozi, zaidi ya wewe sina wa kumtegemea, zaidi ya huyo mtoto hakuna wa kunifuta haya machozi.....’hapo
sikuweza kuvumilia nilijikuta nikilia kilio cha kwikwi , na muda huo ndio watu wote mle
ndani walikuwa wamenigeukia..mimi....hapo sijijui nimezama kwenye duwa, kwenye maombi kwa mola wangu
Kumbe wawili hawa wapo mbele yangu wamepiga magoti mimi sijui...ao wanajua nalia kutokana na hayo yaliyotokea, wao wananibembeleza ili niwasamehe..sijui ...na ndipo akili ikafunguka,, na kutoka kule kwenye imani, na mawazo niliyokuwa nayo yakapotea na kuwaona wawili hao wamenipigia magoti baba na mama mfadhili.
‘Kwanini…mnafanya hivyo…?’ nikauliza, huku nikihangaika kujifuta machozi...
‘Kwanini wewe unalia, ina maana muda wote ulikuwa
kwenye mawazo, na hata hujui tulichokuwa tunaongea..?’ akauliza mama Ntilie
‘Oh, kwakweli,
nilipotea, nisameheni sana, ila…mimi sina kinyongo na nyie wazee wangu
naombeni msimame, msifanye hivyo, mimi sio mtu wa kupigiwa magoti, hamuniamini kuwa mimi nilishawasamehe nyote, mimi nawauliza tu, je nyie wawili mumeshasameheana..?’
nikawauliza
Wote mle ndani wakashikwa na mshangao, na mama Ntilie akasema
'Inaonekana hukuwepo humu ndani kabisa...'akasema mama Ntilie.
Na wawili hao wakaangaliana, na tabasamu
likatawala kwenye midomo yao, na kwa pamoja wakasema
‘Ndio….kwa ajili ya familia, kwa ajili yako,
na kwa ajili ya mola wetu tumesameheana…’wakasema, hapo kiukweli nilijikuta
machozi yakitoka tena lakini sasa kwa furaha, kilichoendelea hapo ni furaha, .....na baadae tukaongea kidogo wao wakaaga kuondoka kwani walikuwa wakisubiriwa na familia zao, na kabla hawajaondoka simu ikapigwa, kijana wao kaachiwa, yupo huru, ila yule binti bado kashikiliwa, hata hivyo, hata yeye atachiwa baadae.
Mambo hayo yalitokea siki hiyo hiyo...
Kwahiyo familia hiyo ikaondoka ikiwa na furaha...na hakuna aliyefikiria kuniuliza vipi hatima yangu itakuwaje,..hilo sikujali, moyoni nilijua, kama hayo yametokea, ina maana duwa langu kwa muumba limeshapokelewa, ...najua hata mimi mambo yangu yatakuwa mazuri,..mungu hamtupi mja wake...imani yangu ilisema hivyo
‘Siamini,...ina maana hao watu wamesameheana, kiukweli.. kwani ilikuwaje…, unajua mimi nilipotea, nikazama kwenye mawazo ilikuwaje, hebu niambie jamani...?’ Hayo nilimuuliza mama Ntilie, wakati wawili hao wameshaondoka..
Muda wa kunisimulia hayo haukupatikana, wageni, wateja..ikawa kazi siku hiyo ikapita, na kesho yake ukaingia ugeni...
NB: Tutakutana kwenye hitimisho
WAZO LA LEO: Tujiepushe sana na tabia ya kiburi,
hasa ukijaliwa mali, nguvu, cheo au na neema yoyote ile, usijione wewe umefika,
usijione kuwa umevipata hivyo kwa ujanja wako, jiulize wangapi wenye uwezo kama
wako, walikuwa na akili sana madarasani, walikuwa na namna nyingi sana, lakini
hawajapata kama ulivyopata wewe, sio kwamba wao ni wajinga hawaju njia za
kupata kama ulivyopata wewe, ..ni neema za mola ambaye humpa mja wake kwa kadri
aonavyo ni sawa, basi ukipata mshukuru mola wako, na saidia wenye kutaka
msaada, na shukuru na kuwaombea wasio nacho wapate kama wewe au zaidi yako.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment