Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, August 21, 2017

DUWA LA KUKU...39


‘Ni nani hao waliingia …mbona huwataji?’ akaulizwa mama Ntilie akiwa na hamasa ya kujua kilichotokea, lakini mume wa mtu hakujibu swali hilo kwa haraka, ….kama vile anaogopa, kama vile tukio hilo lipo mbele yake.

‘Unajua siku ile nilitarajia kuwa kijana wangu atakuja, kama alivyopanga,..kuwa ikipita siku saba, hajapona basi atamwambia mama yake, na sio mama yake pia na babu yake,…mimi sikutarajia kuwa kijana atakuja mapemda hivyo,…. namfahamu sana kijana wangu, pamoja na hayo yakliyotokea, lakini yeye, ana mapenzi sana kwa wazazi wake.

'Baba naona umegoma kuniondolea hilo tatizo ,ambalo nina uhakika ni wewe uliyelisababisha….’kijana wangu akaanza kuongea, tulipokaa kwenye viti, huyo mwanamke mwengine alikuwa bado nje akiongea na simu. Nilimtupia jicho huyo mgeni, ambaye sikuwa nimemtambua vyema, na sikupenda mambo hayo yaongelewe mbele ya mtu mwingine.

'Subiri kijana wangu tutaongea mambo hayo baadae, huoni kuna mgeni hapa…..'nikisema nikiwa na maana asiongee hayo mambo mbele ya huyo mgeni , lakini ilikuwa kama nampandisha jaziba za kuongea zaidi.

'Mzee hili halina kusubiria, maana nipo kwenye hali mbaya, natamani ninywe sumu tu, kuliko hii aibu ninayokumbana nayo ambayo wewe ndiye chanzo chake….’akasema kijana wangu.

'Kwanini unasema hivyo mwanangu, mimi sikupenda yakukute hayo…na hata mimi linaniumiza sana, lakini bado nalihangaikia hilo swala, tatizo mama yako haamini mambo haya ya kienyeji, kama angetoa ushiriakiano wa kutosha tungeshalimaliza kabisa hili tatizo…, wewe hujui tu…’nikasema

'Najua , usijaribu kukwepesha ukweli, najua haya yote yametokea kwasababu ya kuutaka utajiri…’akasema

‘Mwanangu nielewe hapo..mimi sifanyi mamabo kwa masilahi yangu mwenyewe…kama nilifanya jambo ujue ni kwa ajili ya familia yetu..kama ni utajiri, lakini uwe kwa familia yetu…’nikasema.

‘Ina maana baba kweli unathamini utajiri kuliko mimi mwanao, upo tayari kuizalilisha familia yako, ili tu utajirike, upo tayari kumfanyia mama mambo mabaya ili…..’hapo kijana akashika kichwa kwa kusikitika.

'Wewe unaongea nini mambo hayo, kwanini,…huoni kuna watu hapa hawafai kusikia mambo ya kifamilia, ….’nikasema na kijana bado alikuwa kashikilia kichwa na kuinamisha kichwa kabisa, hataka kuniangalia.

'Huyu anajua kila kitu, bila ya yeye nisingeliweza kuyajua haya yanayoendelea humu ndani, nimemuamini kwa vile kila alichonielezea kimetokea humu ndani, ninavyoteseka usiku na zaidi ni kuwa huyo mtu anayemuelezea kuwa ni adui yake nimeshamuona mara nyingi mkiongea naye, na simuamini huyo mtu kamwe…hata yule mdada wa kwanza alinisimulia kuhusu habari zake…’akasema huyo kijana.
'Ni nani huyu kwani…?’ nikauliza sasa nikianza kuingiwa na mashaka naye, nikamtupia jicho, na yeye akawa kanikazia macho, ..mimi nikagwaya na kuangalia pembeni.

'Baba usitake nifanye kitu kibaya, na kabla ya kukifanya hicho kitu, nitahakikisha mama ameyafahamu hayo yote uliyoyafanya humu ndani, najua ana wakati mgumu na yeye najua na yeye anahangaika kujua humu ndani tumeingiliwa na kitu gani..hajui kuwa adui anayemtafuta wanaishi naye chumba kimoja…’akasema
'Sikiliza kijana wangu, hawa watu ndio wachonganishi,usiwasikilize, hawa ndio wanaovunja ndoa za watu, hawa ndio waoingia kwenye familia na kuzifanya zisiwe kitu kimoja, usiwasikilize kamwe..’nikamwambia kijana na kijana ni kama hakunisikia akasema;

'Baba sio swala la kuambiwa, kwani hali halisi haijionyeshi, kwani mimi sina matatizo, je haya matatizo yametokea wapi, hebu niambie wewe baba, si nilikuja nikakuambia nina matatizo hayo, umenisaidia nini mimi, zaidi ya kuhangaikia utajiri wako unaoutaka …kama ni utajiri sawa, utafute kwa njia zako, kwanini unaniumiza na mimi, kwanini unamutesa na mama, kwanini unawatesa watu wengine baki…binti wa watu kawakosea nini…’kijana akasema.

'Hayo matatizo yako nitayashughulikia, kuna mtu namuamini sana, tutayamaliza, usiwe na wasiwasi ,haina haja ya kutefuta watu wa pembeni, watu ambao hawana huruma na familia yako..haya yataisha, nakuahidi mwanangu..’nikasema
'Huyo mtu unayemuamini ndio huyo mchawi wako wa usiku…’kijana akauliza na kunifanya nishtuke, na kumtupia jicho huyo jamaa, huyo jamaa alikuwa habandui macho kwangu, unafikiri ana kitu hataki akikose kwangu.

 Hapo, hapo nikahisi kuwa huenda huyo jamaa ndiye kamuambia kila kitu huyo kijana yawezekana ni mganga wa kienyeji,..au hata sijui ni nani,niliiona ni sura ngeni kwangu, sikuweza kuvumilia, nikasema;

‘Hebu kwanza tutambulishane huyu ni nani, na huyo huko nje anayeongea na simu muda wote huo ni nani…?’ nikaulizai
'Baba kwanza tumalizane na hili langu, nilikupa siku saba, na siku saba zimekwisha, sioni mabadiliko yoyote,…niambie unataka nini kwangu, unataka nijiue…au………?’ kijana akauliza

'Samahanini kidogo, naombeni niwakatize kidogo, samahan sana mzee mwenzangu, unajua kijana kakimbilia kukulalamikia badla ya kunitambulisha mimi kuwa ni nani..ndio utaratibu ulivyo, lakini naona matatizo aliyo nayo yanamnyima amani…’akasema huyo mgeni.

'Wewe ndiye umemdanganya kijana wangu kuhusu hayo anayoongea…?’ nikamuuliza sasa nikiwa nimekunja sura ya hasira.

'Nimemdanganya au ni kweli, hayo aliyoongea ni kweli tupu, niambie uwongo wa hayo aliyoyaongea ni upi,…yeye, alikuja kwangu akiwa na shida zake, kaelekezwa kwangu, kwanza tuliwasiliana kwa simu, nikamwambi akarubuni nitakuja huko….na nikawa nimefika..’akatulia kidogo.

‘Basi nilipofika hapa nikawasiliana naye, nikamwambia aje tukutane, akaja  akanisimulia matatizo yake, na kwa bahati nzuri, alikuja sehemu sahihi, kwasababu huyo mtu anayekusaidia hadi mkaingia kwenye matatizo hayo, mimi namfahamu sana….’akasema
'Sina mtu anayenifanyia mambo yoyote kama aliyoyaongea huyu kijana, hizo ni hisia zake tu,..na wewe ndiye umemjaza maneno yenu ya kiganga ya uwongo…’nikasema.

'Huyo mtu unaye…sio kwamba na kisia, au ramli au nini…huyo namfahamu ilivyo maana alikuwa mwanafunzi wangu , aliletwa kwangu nimfundishe mambo ya uganga,… akaasi, akaniibia hata mikoba yangu ya uganga…, na kwenda kujihusisha na mambo ya kichawi badala ya kufuata yale niliyomfundisha,…huyo ndiye anayekutumia, lengo lake sio zuri, anawatumia kwa masilahi yake binafsi….’akasema.

'Tafadhali,  hayo unayoyaongea ni uwongo, na sijui yametokea wapi, nakuomba tafadhali tena sana, usimpoteze kijana wangu kwa mambo yenu hayo ya kishirikina, …’nikasema.

'Sio mimi ninayempoteza kijana wako…, tatizo wewe umeshatekwa akili,  na huyo mtu, wewe ndiye unayempoteza kijana wako kwa kumharibia maisha yake… na usipofanya juhudi utakuja kujuta, utakuja kumuharibu kijana wako kabisa kabisa…, na maisha yake ya baadae yatakuwa ni ya giza…atakuwa punguani…, na pia umeiharibu familia yako mwenyewe, , kwa kutumiwa na huyo mtu, huyo mtu hana wema kwenu, akimaliza kuwatumia, atarudi kijini kwake na ukimtafuta ataishia kuwazidishia mavumba ya kuwaharibu kabisa…’akasema.

'Sasa wewe unataka nifanye nini…maana naona umeshamuhadaa kijana wangu na amekuamini kuliko hata mimi baba yake..umefanya vibaya sana, fikiria kama angelikuwa kijana wako kakufnyia hivyo ungelijisikiaje…na ni nini lengo lako,…, unataka mimi nifanye nini …?’ nikauliza.

'Huyo mtu.unayeshirikiana naye haaminiki, anachojali ni masilahi yake, anawaharibu mabint za wenzake, ..uchawi wake unategemea sana kuwatumia mabinti, kweli si kweli…kila siku mabinti wanaokuja hapa wanatumiwa kwenye mambo yao ya kishirikina ya usiku, na mashetani na wachawi wenzake, hebu fikiria hilo kama mzazi…’akasema hyo mzee.

'Mimi sijui unachokiongea…’nikasema nikiangalia pembeni, lakini moyoni nilishaona kuwa sasa nimepatikana.


'Kijana, kama nilivyokuambia, huyu baba yako keshalishwa kiapo hawezi kusema ukweli, na usipofanya kama nilivyokuambia, hutaweza kuokoka na hilo tatizo ulilo nalo, hili tatizo lako asili yake ni kutoka kwa baba yako, wewe mpigie simu mama yako, aje na babu yako apa, kabla muda haujakwisha, hao ndio watakaoweza kukusaidia kutoka kwenye hili tatizo, huyu hataweza kukusaidia…’kijana akaambiwa.

Kijana akamuangalia baba yake kwa amcho yaliyojaa hasira huku akitoa simu yake kwenye mfuko wake, nikajua sasa keshatekwa na huyo jamaa, anamsikiliza yeye kuliko mimi na nisipojitahidi kulizuia hili mapemaa, basi mimi nitafukuzwa kwenye nyumba hii kama mbwa…

'Wewe mwanangu ina maana umefikia hatua hiyo ya kumuamini mtu wa nje kuliko hata mimi  baba yako, unataka kumuua mama yako kwa shinikizo la damu, maana akisikia haya mambo ya kizushi ataishia kudondoka, kwa shinikizo la damu, unajua jinsi alivyo…’nikamwambia huyo kijana wangu.

‘Baba wewe ndiye unataka kumuua mama kwa shinikizo la damu, nimegundua kuwa wewe hutujali tena…kwahiyo ngoja nimuite mama, maana yeye ana uchungui na familia yake, yeye hawezi kuniumiza mimi kwa masilahi ya utajiri, au ubinafsi…’akasema sasa akiwa anaanza kubonyesha simu yake kutafuta namba ya mama yake. Na huyu mzee akawa ananiangalia mimi usoni.

‘Subiri kwanza mwaanagu, niongee naa huyu mchonganishi…’nikasema, nikimuangalia huyo jamaa machine, na huyu jamaa akawa ananiangalia bila kupepesa macho..

‘Wewe mtu wewe….hebu niambie unataka mimi nifanye nini, maana hujaniambia unachokitaka, zaidi y kuziei kutaka kuiangamiza familia yangu….’nikamwambia huyo jamaa. Na kuwa muda huo kijana akswa kaishikilia simu yake tayari kumpigia mama yake. Niliangalia kuhakikisha kuwa simu hiyo haipo hewani.

'Lengo la kuja hapa ni kutaka kumsaidia kijana wako, aondokane na hilo tatizo alilo nalo, ukiangalaia utagunduaa tatizo hilo ndilo ulikuwa nalo wewe, sasa limehamia kwa mtoto, iweje matatizo yako ya kizee, yahamie kwa kijana mdogo kama huyu, kama sio hayo mliyoyafanya wewe na huyo mwenzako…’akasema huyo jamaa.

‘Sasa mimi nimekuja kumuokoa huyu kijana na kuikoa hii familia kutoka kwenye mikono ya huyo mchawi ambaye anajifanya kuwa anakusaidia kumbe anakutumia tu….’akasema.

'Kumsaidia kijana wangu, safi kabisa, kama ni hivyo basi kwani kuna tatizo gani hapo, mimi sijakukutaza, sikuelewa dhjumuni lenu, haya niambia mimi nifanye nini,…ila kwa maoni yangu, tatizo hili la kijana ni letu tu hapa, tusimuhusishe mama yake kwanzaa, huyo mama yake kwa hivi sasa yupo kwenye matatizo makubwa…, ukimuongezea na hili utamuua kabla muda sio wake…wewe humjui mke wangu …………….’nikasema.

'Ni hivi ili niweze kumsaidia huyu kijana, natakiwa nipambane na huyo mchawi, nim-malize kabisa, ili niweze kuchukua mikoba yangu ya uganga wangu ambao aliniibia na humo ndio nitapata mwongozo wa kuweza kumtibia huyu kijana, hayo ni mambo ya kimizimu, yanahitajia kibali cha huo mkobwa, na hilo tatizo limefungwa kwenye huo mkoba, huwezi kwenda kokote, ukatibiwa, …’akasema.

'Kwahiyo kumbe, nimekuelewa wewe lengo lako ni kutaka kumtumia mtoto wangu kufanikisha mambo yako…wewe unautaka huo mkoba wako, lakini hwezi kuupata mpaka umtumie mtoto wangu, kwanini unafany ahivyo…’nikasema kumuambia huyo mzee.

‘Mambo gani, ya kunifanikisha mimi, hapana, wewe sasa unataka kupotza muda,..mimi nayafahamu sana hayo mambo, najua kabisa, wewe ulishalishwa amini kuwa usiseme kitu…., ni sawa kwa mfumo huo, lakini amini uliyokula ni ya ulaghai,haita fanya kazi, muhimu kwa sasa ni familia yako, usipoijali familia yako ukajali mali, ukajali nafsi yako, wewe sio mzazi mwema…’akasema.

‘Wewe ni mchonganishi, wewe ni mchawi kuliko hao wachawi unaowasema wewe…’nikasema kwa hasira

'Kijana piga simu kwa mama yako, kwa haraka, muda unakwisha….usipoteze muda zaidi,…huyu mtu haelewi ninachotaka kukufanya, na haelewi ugumu na hatari ya hilo jambo, unavyozi kuchelewa huyo jamaa huko alipo anazidi kuficha makucha yake..tatizo linazidi kuwa kubwa, sasa hivi keshagundua kuwa anakaribia kushindwa, nimeshamzunguka, ukichelewa ataficha kila kitu, mimi sitaweza kukusaidia baada ya hapo….’akasema huyo mzee, na kijana akawa anataka kubonyesha kitufe cha kuita kwenye simu.

 Nilipoona kijana anataka kupiga simu nikamzuia…na kumshika ule mkono alioshika simu, na mzee akataka kusogea kunizuia, hapo nikasema kwa haraka;

'Sikilizeni kwanza niwaambie, mwanagu usipige simu, kama kweli unampenda mama yako, kama huyu mtu kaja kwa nia ya kukusaidia kweli , hata mimi nitafurahi, nitatoa ushirikiani wote kuhakikisha wewe unapona,..lakini haya mambo akiyasikia mama yako utamchanganya kabisa, mimi namjali sana mama yako huyu hamjali, hata akipatwa na matatizo…’nikasema

'Kijana piga simu, muda unakwenda sijaja hapa kupoteza muda wangu, nina mambo mengi ya kufanya, kama hupigi mimi naondoka, na usije kujilaumu kwa hilo,….’akasema huyo jamaa na kijanaa sasa akabonyesha kitufe cha kuita simu.

Mimi kwa haraka nikaibetua hiyo simu mkononi mwa kijana, na ile simu ikadondoka chini,..na nikasikia sauti ya mama yake akisema;

‘Halloh, unasemaje, mbona huongei….’ Na simu ikatulia.

Kijana akawa anainama kutaka kuichukua, nikasema;

‘Izime hiyo simu tuongee,… maana mama yako alisema atakwenda hospitalini, huenda sasa hivi yupo na docta, na wewe unataka kumsumbua, tusitake kumchanganya kichwa, niambia wewe mchonganishi  ulitaka mimi nifanye nini, nipo tayari kutoa ushirikiano…’nikasema.

‘Kwanza mkaribisheni huyo mama huko nje, yeye atatusaidia sana kwa hili jambo…’akasema

*************

Aliingia mama mmoja na kusalimia, nikamkaribisha kiti, na alionekana kuwa na wasiwasi kweli, akawa anaangalia huku na kule, na yule mzee akasema;

‘Huyu ni mke aliyatalikiwa na huyo mchawi anayekutumia, huyu anamfahamu huyo mtu kuliko mwingine yoyote, aliishi na huyo mchawi kwa muda, na kipindi kirefu amekuwa akiona alichokuwa akikifanya huyo mtu, yeye akajaribu kumvumilia, kwa tabia zake mbaya, lakini baadae alipoanza kutaka kumuingiza na yeye kwenye uchawi wake, ndio akaamua kuondoka….’akasema na mimi nikamkagua huyo mwanamke kwa makini,

‘Sasa mbona unapoteza muda tena, unaona ulivyo muongo….’nikasema

‘Sio muongo, huyu ndiye anaweza kukitafiti hicho kitu tunachokitafuta kwa maana yeye anakijua wapi kilipo kutokana na mizimu ilivyo…tutaweza kukipata…?’ akamuuliza huyo mwanamke, na huyo mwanamke akawa ananusua nusa kwa pua…baadae akasema;

‘Hapa kuna kitu…’huyo mwanamke akasema sasa akiangalia muelekeo wa chumba anacholala yule mfanyakazi wa ndani.

‘Huko ndani au…?’ huyo mzee akauliza na huyo mwanamke akakubali kwa kichwa…na mzee huyo akasema;

‘Yaonekana huko ndipo mambo yalikwua yakifanyika, …sasa ndugu yangu tusipoteze muda, kuna kitu tunakitafuta, kakiacha humu ndani, tukikipata hicho, tutaweza kupambana na huyu mtu kirahisi tu, na hatimaye nitapata mkoba wa kuweza kumtibia mwanao…’akasema.

‘Kitu gani mbona mimi sikijui…’nikasema nilimuangalia huyo mzee na hatimaye huyo mwanamke.

‘Unaweza usikijue, lakini kumbuka siku ya kwanza alikuambia anataka kufanya nini ndani ya hii nyumba….mimi nimeshaanza kujua wapi kilipo, lakini wewe mwenye nyumba, unaweza kuturahisishia kazi…’akaambiwa, na mimi nikakumbuka huyo jamaa alichimba shimbo nyuma ya nyumba, na huko chumbani anapolala mdada kuna kitu alikipandikiza..juu ya kona ya chumba,…

‘Huku ndani ni chumba cha msichana wa kazi,sasa hivio hayupo…’nikasema na mama akatikisa kichwa kukubali, na huyo mzee akatoa kitu chake kwenye mkoba, kama pembe ya mnyama, akawa anakiielekeza huko,

‘Unaturuhusu kuingia huko ndani..?’ akauliza

‘Sawa ingineni,  mimi sijui kitu…’nikasema

Wawili hao wakaingia ndani, na baadae wakatoka, na kusema;

‘Kuna vingine havipo humu ndani, vitakuwa  nje….’akasema na wakatoka nje baadae wakarudi, na kusema;

‘Kuna sehemu mbili hazipo kabisa humu ndani, kwenye eneo lako, kuna sehemu kaziweka,…sasa ni hivi, hapa tupo kwenye mapambano, huyo jamaa siku zake zinahesabika, sijui, kama ataweza…ngoja kwanza tuvitafute hivyo vitu vingine kabla hajavificha, tunakwenda na muda,..’akasema na wao wawili wakatoka.

‘Sawa fanyeni muwezavyo, ila mimi sijui kitu…’nikasema

 Wakatoka na baadae huyo jamaa akarudi na kusema;

‘Wewe kijana ngoja tutafute hivyo vitu vingine, sisi tunaondoka ubakie hapa na baba yako, usiondoke,..hakikisha baba yako hatumii simu, maana anaweza kumpa taarifa ya kinachoendelea, akaharibu kila kitu,… kama tukifanikiwa tutarudi, ukituona kimia ujue bado tupo kwenye mapambano…’akasema na wawili hao wakatoka mimi nikabakia na kijana wangu.

Tulikaa kimia, bila kusema neno baadae nikasema;
‘Kijana wangu usiwaamini sana hao watu, kama wana nia ya kukusaidia kweli…., sawa, mimi sina tatizo na hilo, ila hilo la kusema mimi nahusika, sikubaliani nalo kabisa, ni waongo na lengo lao ni kuisambaratisha familia yetu….’nikamwambia kijana na yeye akabakia kimia tu, nikataka kutoka nje , hapo akasema.

‘Umesikia walivyosema, tusitoke humu ndani…, kuna mambo wanayafanya, usitake wakaharibu hayo matibabu, mimi hapa nilipo sina raha, nateseka,..hivi wewe baba hunionei huruma, nimefikia kutumia madawa ya kulevya, bila kupenda, ili kuondoa mawazo, kumbe ndio yamezidi kuniharibu, baba unataka nini, unataka mimi nife kwanza nio urizike,..kama hili halitafanikiwa, sina budu nitafanya hivyo unavyotaka wewe…’kijana akaongea huku akitaka kulia.

‘Mwanangu unataka nikuambie nini ili unielewe, hivi nikuulize kipindi kile unatumia utajiri, unafurahi, ulijua huo utajiri umetokea wapi..mbona muda ule hukuja kuniuliza, hujui ni vipi nateseka kwa ajili yah ii familia, tatizo wewe unamsikiliza huyo mtu bika kuataka kunisikiliza mimi…niamini mimi, mimi ni baba yako siwezi kufanya jambo baya kwa mtoto wangu mwenyewe…umenielewa…?’ nikasema na kumuuliza.

‘Najua ni wewe ulifanya hayo mambo ya kishetani, ukaniwekea mimi, na mimi sikujau, sikuwa na akili yakuyatambua hayo, lakini baadae ndio ukaamua kuyachukua hayo mambo , ili utajiri uhamie kwako, hayo nayafahamu yote, …ila ulichokosea ni kuchukua na hali yangu,….unanifanya mimi niadhirike, nionekane sina maana , mabinti wengi sasa wananidharau, mchumba wangu kani….’akashika kichwa.

‘Sikiliza kijana, hayo mimi nitahakikisha yanakwisha, hilo nakuahidi ilimradi uhai uwepo, mimi nitakusaidia utapona, hata kama ni kuchukua sehemu ya viungo vyangu, hata kama ni mimi kuharibikiwa, hata kama tutakuwa masikini, mimi ni baba yako mimi ni mzazi wako,…lakini tuwe na subira..maana haya mambo sina uwezo nayo mimi, ila yupo mtu ambaye ananisaidia…’nikasema.

‘Huyo mtu si ndio huyo mchawi , huyo anayekutumia, huyo mchawi kawaharibu wasichana wa watu, wewe hujiulizi, kama anawatumiwa watoto wa wenzake, anawaharibu bila kuwajali, huoni jinsi gani alivyo mnyama,.. ..hata huyo mdada alikuwa akikaa humu ndani kamfanyia mambo mabaya sana…’akasema

‘Mambo gani..ambayo unayajua wewe aliyomfanyia huyo mdada, usiamini mambo hayo, ..au ni nani kakuambia hayo mambo..unaona ilivyo, …keshakuingiza kwenye mambo ya kishirikina, …ni mangapi kakuambia, hebu niambie..?’ nikamuuliza.

‘Huyo mjaamaa ni adui wa huyo mchawi, wamekuwa wakiwindana tokea huko kijijini, na wamefukuzana hadi hapa, na kaniambia huyo mdada aliyekuwa hapa kapandikiziwa shetani,…’akasema

‘Kapandikiziwa kwa vipi…uwongo huo…’nikasema

‘Sio uwongo baba,..hayo ya kupandikiza shetani, hayakuanza leo,…wamekuwa wakimfanya huyo mdada mambo mengi mabaya…hiyo mimba ya huyo mdada akikua, na hayo mambo yao yanakuwa, yanamuingia huyo mdada, na huyo mtoto akizaliwa hatakuwa na hali ya kawaida…’akasema

‘Unataka kusema nini , kuwa huyo mdada, ohoo, nimegundua, kumbe wewe ulimpachika huyo mdada mimba na lengo lenu ni kuiharibu au sio, niambie ukweli, mimi baba yako nitakusaidia…’nikatulia.

‘Ukweli upi baba, mwenyewe unajua, sina uwezo huo…labda ni wewe, labda ni wao, …ila nijuavyo, kwa jinsi alivyoniambia, huyo mdada ni mke wa shetani –mbwa, na wamekuwa wakimfanyia mambo mengi, wewe ukihusishwa PIA….’akasema.

‘Na wewe pia…’nikasema halafu nikashtuka kuwa nimeropoka, nikasema

‘Na wewe ukiamuamini…Ina maana kakuambia  hayo, kwanini akuambie wewe, sije kuniambia mimi,……?’ nikauliza

‘Akuambie wewe wakati wewe unashirikiana na adui yake…..’akasema

‘Muongo huyo anataka kukutumia wewe ili kupambana na adui yake, tunatakiwa hapa tuwe makini…’nikasema

‘Baba huelewi, naona wewe hutaki mimi nipone, kwa hivi sasa nipo tayari kufanya lolote lile, ili nipone, najua wewe unachofanya ni kujiangalia hali yako, lakini ukumbuke mimi sikuwa na matatizo, matatizo yako umehamishia kwangu, uone baba ulivyo, kwanini unichague mimi, kwanini unanichukia hivyo,…’akasema

‘Nikuchukie kwanini nikuchukie, hapana usifikirie hivyo mwanangu,na wala usije kuliongea hilo, hakuna mzazi anayewachukia wanae…’ akasema.

‘Unaweza kusema hivyo usoni kwa watu, lakini moyoni ikawa tofauti na ikipatikana nafasi kama hii huwezi kusita kufany akama ulivyonifanyia mimi, lakini baba, hata kama wewe hunipendi, lakini mimi nawapenda sana wazazi wangu, nimejitahidi sana kuombea nyie na mama muishi kwa amani, na upendo, lakini sijui kwanini, na hili sasa limetokea, yaonyesha kuwa wewe ndiye una matatizo baba….’akasema.

‘Kijana wangu haya ni mambo ya kikubwa hutakiwi kuyaingilia,…utaumia muda sio wako, nisikilize, mimi na mama yako tumekuwa hivi, ..kuna kukosana , badae tunapatana, ni hali ya kawaida ya ndoa, hilo lisikuumize kichwa kabisa, unajua nimekuelewa, mawazo hayo ndiyo yamekufanya upatwe na matatizo hayo uliyo nayo, sio hayo anakudanganya huyo mtu,…umenielewa hapo…?’ nikauliza
‘Baba mimi sijui…usitake kunificha …mimi ninachotaka nipone, kama huwezi kunisaidia wewe, najua mama atanisaidia, …..’akasema

‘Hilo mwanangu lipo mikononi mwangu haya ni mambo ya wanaume,mama yako hawezi kuyafahamu, ngoja tuaone huyo mtu wako atafanya nini, akishindwa mimi nitalifuatilia mpaka utapona, yatakwisha tu….’akasema

 ‘Kwahiyo baba, kama nisipopona hili tatizo ina maana mimi sitaweza kuoa tena…?’ kijana wangu akaniuliza

‘Kwanini usipone, ..tatizo huyo mtu kakuvuruga akili tu…mimi najua hayo mambo yapo na yanapona,…niamini mimi utapona,…mimi nitahangaika kumtafuta bingwa wa hayo mambo, tutayamaliza, kitu muhimu, iwe siri kati yangu mimi na wewe..hakikisha mama yako halijui hili…’nikasema

‘Babu nilimuambia ..kuwa nahisi kuwa nina tatizo la namna hiyo sikumfafanulia jinisi ilivyo,  akasema ni sababu ya madawa na ulevi, niache nitapona, lakini sio kweli, najua kuna tatizo zaidi ya hilo, na huyo mtu ndiye kanifichulia ukweli,……’akasema.

‘Hata mimi naamini ni kwasababu ya madawa na ulevi,…muhimu wewe na subiria tu,…niamini mimi haya mambo, nitayamaliza mimi mwenyewe…’nikasema huku moyoni nawaza nifanye nini kumthibitishia kijana wangu kuwa mimi namjali kama mzazi wake, je ni yupi nimuamini kati ya hao watu wawili, huyo mtaalamu wangu au huyo adui yake.

‘Baba mimi nakuahidi hapa, kama hili tatizo halitatafutiwa ufumbuzi mimi nitafanya jambo…mtakuja kujuta wenyewe, lakini kabla ya kulifanya hilo jambo, nitahakikisha familia nzima inafahamu kila kitu kilichowahi kutokea hapa kwenye hii nyumba nitakiweka wazi,,…kuanzia yule binti wa awali, hadi huyu wa sasa…kuwa wewe ndiye unayehusika, hilo baba sikufichi, …’akasema.

‘Kwanini mwanangu unasema hivyo…kwanini huaniamini mimi….’akasema

Kabla hatujaendelea na maongezi, mara simu ikalia, ilikuwa simu yangu nikaichukua, alikuwa anapiga mke wangu,…

‘Halloh,…?’ nikaita na kusikiliza kwa makini…

‘Unasema nini…kwani wewe upo wapi, hospiatalini …mmh, nakusikiliza…?’ nikauliza kwa mshangao huku jicho limenitoka…..nikawa namsikiliza huku namuangalia kijana wangu ambaye naye alivutika kusikia hicho ninachoambiwa na mama yake, lakini asingeliweza kusikia kile mama yake anachokiongea.

NB: Ni kitu gani kitakachoendelea.


WAZO LA LEO: Usimuombee mwenzako ubaya hata kama ni adui yako, maana huwezi kujua , huenda huo ubaya anaokufanyia wewe unaweza ukawa ni neema ambayo mola wako kakukadria kukupa huko mbeleni, muhimu ni kuvuta subira na kuendelea kutenda mema. 
Ni mimi: emu-three

No comments :