Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, August 18, 2017

DUWA LA KUKU....38


Siku hiyo sikuwa na raha kabisa,…na tofauti na siku nyingine ambayo nilipenda kumfuata fuata huyo bint kwa siri, nikimuangalia alifanya usafi, siku hiyo nilijaribu kumkwepa, na hata alipotaka kufanya usafi ndani kwangu, sikutaka anikute hapo, nakumbuka siku moja alipotaka kufanya usafi, nilidhamiria kumshika kwa nguvu, lakini nilipomkaribia tu, nikahis kichomi kikali  tumboni, nikanywea na kwa haraka nikarudi nyuma…

Kwa huyu binti, kila nilipojaribu kumfanya chochote ilikuwa ni kama kuna mtu anamlinda, kama ilivyokuwa kwa yule binti wa awali, nikakumbuka maonyo, kuwa huyu binti naye ana mtu wake, na yule halikadhalika alikuwa na mtu wake, na wote hao ni hao wachawi…

Basi nikatoka hapo nyumbani, baada ya kuhakikisha kuwa kweli huyo mbwa hayupo, na kwenda kwenye shughuli zangu na baadae nikampigia simu huyo mtaalamu nia ni kumuulizia  kuhusu kijana wangu na je kulifanyika nini huo usiku na je kilichofanyika kimeweza, au kitaweza kumsaidia kijana wangu.

Nilipiga simu ikaita kwa muda baadae akawapokea na kuwa hewani,, nikajitambulisha kwake, akasema ameshanitambua mimi ni nani,...na sauti aliyotoa ilionekana ina uhai,  nikamuuliza

‘Vipi mtaalamu ulifanikiwa…?’ nikamuuliza

‘Nusu nusu, kama nilivyokuambia, mkeo aliondoka mapema, na kijana wako pia..kwahiyo..mambo mengi yakashindikana kufanyika,..tukajaribu kumtuma  mbwa wetu usiku huo, akaone alipokwenda huyo mkeo, na tuone kama tunaweza kufika huko angalau kwa muda, lakini kilichotokea huko ikawa ni mkosi wa siku …’akasema

'Mkosi !....mkosi wa nini...?' nikauliza


‘ Jamaa alinaswa....'akasema

'Alinaswa na nani sasa…?’ nikauliza

‘Hao wakwe zako naona safari hii wamejiimarisha, jamaa alifika vyema na alipojaribu kufanya vitu vyake, akajikuta anaonekana...nguvu zake za kinga zikawa hazifanyi kazi, na hakuwa na jinsi, akapatikana,...na alaichukuliwa kwenda polisi na hata hivyo watayaona maajabu yake…’akasema

‘Maajabu gani…?’ nikamuuliza kama sijui

‘Tuyaache hayo,…ila mbwa wanaye bado, nimeacha abakia huko kidogo, atatusadia mambo mengine ya huko, na usiku atawatoroka, huyo hana shida, hawamuwezi…’akasema.

‘Atawasaidia nini huko polisi, huyo mbwa…?’ nikamuuliza

‘Tatizo lako hunijui mimi…lazima nijue wamepanga nini huko baada ya hilo tukio….’akasema

‘Sawa nimekuelewa…’nikasema hivyo, nikasikia akipiga miayo halafu akasema;

‘Haya niambie unataka kujua nini zaidi, hayo mazungumzo mengine tuyaache kwanza…’akasema.

 ‘Sawa mimi usiku huo mlipofanya hayo mambo unajua siwezi kuona yanayotendeka ila wewe ndio unanisimulia, je hmlifanya nini..na je mlifanikisha hayo mambo maana siku alizo nipa kijana wangu ndio hizo zinakwisha…’nikasema.

‘Nashangaa leo unataka kuyafahamu mwenyewe tofauti na siku nyingine,….’akasema

‘Ndio wewe huoni hali ilivyokaa sasa hivi…..’nikasema.

‘Japokuwa mke wako alikimbia na kijana wako, lakini tuliweza kufanya baadhi ya mambo yetu, hasa mambo yetu ya kujilinda, na huyo adui yetu, sasa yaliyotukwamisha ni mambo yako, lakini mambo yetu yamekamilika….’akasema.

‘Mambo yenu yapi sasa, na kama ni mambo yenu kwanini mje kuyafanyia hapa kwangu, hamuoni mnanifanya niwe kwenye wakati mgumu, …na,…na…mke wangu…?’ nikamuuliza na nilipotaka kuongea zaidi akanikatisha na kusema;

‘Nilikuambia kitu, huyo binti hapo ndani ametufaa sana, kuanzia sasa kachukua nafasi ya yule binti wa awali japokuwa sijakata tamaa, maana huyu hatanifaa mimi , kama mimi,…yule binti mwingine alikuwa ni mke wangu, huyu sio wa kwangu…ila tumemtumia sana,…na mambo mengi yamefanikiwa, na kijana wako, kama angelikuwepo hali yake ingelijirudia kama kawaida…’akasema

‘Sasa kwanini kwani ni mpaka awepo ndio hayo mambo yafanikiwe…?’ nikauliza

‘Sasa tutamfanyia vipi ili kuhakikisha karejea kwenye hali yake, ilitakiwa yale matendo ya awali yafanyike, mkabidhiane tena, na …hilo litasubiria, utajua mwenyewe jinsi ya kumweka sawa, ukitaka tumnyamizishe tunaweza lakin hamtapendezewa na hiyo hali hasa mke wako…’akasema

‘Na, na yuleo mbwa wenu atarudi tena hapo nyumbani…?’ nikamuuliza

‘Huyo  mbwa , keshamaliza kazi yake kama mbwa…, kuna kazi alitakiwa kuifanya hapo ndani ya kafara maalumu la kuunda silaha mpya, kombora litakalomumaliza kabisa huyo adui yangu…na limefanikiwa,….’akasema

‘Kwa vipi huyo ni mbwa au sio…mumemfanyia nini na huyo binti wa watu…?’ nikauliza

‘Hahaha..huyo ni mbwa kwa uoni wenu wa macho, huyo ni shetani wetu , yeye anaweza kujigeuza mbwa, paka, nk…na tumemtumia kwenye mambo hayo makusudi ili kuficha ukweli…, na yeye kwa hivi sasa ndiye bwana wa huyo binti ….’akasema

‘Bwana wa huyo binti,  binti yupi…una maana gani kusema hivyo?’ nikauliza nikiwa na mashaka.

‘Binti yupi tena si huyo hapo nyumbani kwenu, yeye katunukiwa na huyo shetani-mbwa wetu..kwahiyo hana budi kumtumia huyo binti, na kupitia kwake tutafanikisha mambo mengi sana nyota yake ina nguvu sana kwenye makafara yetu…usiku huo tulimchukua huyo binti hadi kuzimuni, akachezewa  huko kuwafurahisha hao mashetani ..’akasema.

‘Mungu wangu, kwanini mumefanya hivyo, huyo binti wa watu ni masikini tena yatima, sio vizuri jamani…’nikawaambia

‘Sisi hatuangalii huko, mambo yetu ni kishetani, na yanafuata mkonodo huo…wewe ulitaka utajiri hukuupata,unafikiri uliupataje, ni njia hizo hizo…..sasa umetaka mengine…haya tufanyeje…ni lazima mambo hayo yafanyike ili mambo yetu yafanikiwa, ukiwa na huruma hiyo hawezi kufanikiwa….’akasema

‘Hapana, hilo mimi sipo na nyie kabisa…’nikasema

‘Hupo na sie k, kwahiyo unataka kijana wako aendelee kuwa hivyo, maana bila hayo yaliyofanyika kijana wako hataweza kurejea kwenye hali yake, huyo ndiye atatusaidia kila hatua,… si ndio unataka hivyo…mtoto wako arejee kwenye hali yake, au unataka nini…?’akauliza.

‘Kwa-kwa-hiyo mumefanikisha kuhusu mtoto maana hapo sijakuelewa…?’ nikauliza nikiwa sina hamu maana kila hatua najikuta naingia kwenye mambo mabaya zaidi,..

‘Tutawezaje kuanikisha  wakatu wahsuika wakuu hawakuwepo, mke wako, haya kijana wako, ..tulijaribu kuwafuatilia, mtumishi wangu ndio akanaswa huko,..unajua nikuambie kitu, .sio kila mahali tunaweza kuingia, …’akasema.

‘Kwahiyo lini tena, maana siku zimekwisha unajua sitaki kijana wangu anifikiri vibaya, hivi sasa anaonekana kujua kila kitu sijui ni nani kamuambia…’nikasema.

‘Ndio maana tunatakiwa kumnyamazisha hadi haya mambo yakamilike…’akasema.

‘Una maana gani kumnyamazisha…?’ nikauliza.

‘Anakuwa kama zezeta, hawezi kufikiri wala kuongea , …ni swala la muda mfupi tu…vinginevyo hiyo hali inaweza ikakujia wewe, na ikikujia wewe ndio basi tena, kwahiyo ni bora kuifanya hivi sasa kwa kijana wako ili iwe rahisi kwetu kufanikisha haya mambo, asitusumbue…’akasema

‘Hapana….kwa kijana wangu sitaki tena, sitaki muiguse familia yangu tena, imetosha…’nikasema
 ‘Hahaha hapo ulipofikia huwezi kurudi nyuma . kama nilivyokuambia kuachana na haya mambo ni mmoja wenu afe….hilo sitanii ndugu yangu…na hivi huoni kuwa ile nyota imeshaanza kurudi kwa wenyewe…wenzako pia wanahangaika kivyao, usipojitahidi, sio kwamba tu utafirisika kabisa, lakini pia unaweza kuwa kichaa, na ikitokea hivyo umekwisha..…’akasema.

‘Oh…..mtaalamu, fany aufanyavyo, kijana wangu arudie hali yake, usijali kuhusu mimi…na mke wangu arudi nyumbani, …lakini kwa hivi sasa usifanyie nyumbani kwangu…’akasema.

‘Kwangu hatuwezi kupaacha, labda umuhamishe huyo binti kwenda sehemu nyingine ambayo tunaweza kumpata kiraisi…umenisikia…’akasema na kukata simu.

Mimi …pale nilipokuwa nimekaa nilianza kujisikia vibaya, ina maana mimi nimeolewa na mbwa-shetani, na usiku walinipeleka makaburini,maneno hayo yalinichefua zaidi na zaidi hapo sikutaka hata kumuangalia huyo mzee, maana hata mimi nilishaanza kujihisi kama huyo mama,  moyo wangu ulishaanza kumchukia huyo mzee, lakini sikusema neno.

Nikasogea hadi dirishani kupata hewa, naona wote wakageuka kuniangalia mimi.

‘Upo sawa…?’ akaniuliza mama Ntilie.

‘Nipo sawa..hewa ilikuwa nzito…’nikasema

*********************

 ‘Tuendelee…?’ akauliza huyo mzee, alipoona mimi nahangaika…

‘Endelea lakini naomba uongee mengine sio hayo ya  kunihusu mimi…’nikasema nikijaribu kutafuta hewa, maana nilikuwa kama nakabwa, pumzi ilikuwa ndogo.

‘Muache aendelee ni vyema ukajua walichokufanyia, ili ujue ni kwanini mimi nakataa kumsamehe huyu mtu, tamaa zake ndio zitufanye tuzalilishwe, unajua ni mangapi waliyokuwa wakiyafanya kwako na kwangu, na hujui ni nini hatim,a ya iyo mimba yako , …’akasema.

‘Kwangu mimi inatosha…’nikasema nikitikisa kichwa nilitaka nitoke nje kabisa
‘Ni mengi yalifanyika, baadae wakikutumia wewe, na kipaba zaidi licha ya mimi kugoma kuwa wasifanye hayo mambo yao hapo nyumbani kwangu, lakini waliendelea kuja, na bado walinitumia nikisimamia …’akasema.

‘Ina maana kuna mambo mengine yaliendelea kufanywa kwa huyo binti…?’ akaulizwa.

‘Wanasema walikuwa wakitengeza shetani ambaye atakuwa mlinzi wa kupambana na hayo yanayoendelea kati yake na huyo adui yake, na wamegundua kuwa huyu binti ana damu itayowezesha hayo,..kwahiyo waliendelea naye kila hatua, kwani walihitajia shetani ambalo litazalishwa kupitia kwenye tumbo la huyu binti….’akasema.

‘Oh….’nikajitizama tumboni, na kuhisi tumbo likianza kuniuma, nikahisi kizungu zungu, kutaka kutapika…

‘Ina maana kilichopo tumboni ndio hayo mambo yao..?’ akauliza mama Ntiliye

‘Mimi kiukweli yaliyokuwa yakifanyika baadae sikutaka kujua, nilishaanza kuogopa, mambo yalishaanza kuniwia magumu kwangu, na kijana wangu tukawa hatuonani akija anaongea na hyu binti anaondoka, na mama yake akija anaongea na huyu binti anaondoka zake kwahiyo, ili niwasiliane nao ni kwa kupitia huyu binti,  mimi nikawa kama nimetengwa

 ‘Hawakukuambia kitu gani kinaweza kupatikana kwa huyu binti, kuwa atazaaje ….?’ Akaulizwa

‘Hawakuniambia. Ila walisema iwapo atapata ujauzito kuna mambo alitakiwa kufanyiwa kabla hajajifungua….’akasema.

‘Je aliwahi kufanyiwa hayo mambo…?’ akaulizwa.

‘Mhh..hapana kwa jinsi nijuavyo mimi…’akasema.

‘Ikawaje sasa..maana ulisema kuwa kijana wako alikupa muda wa kumrejeshea hali yake..au nguvu zake, iliwezekana au ilikuwaje, kijana wako alipokuja kwako, uliwezaje kuliweka hilo sawa, na je hajaweza kurejewa na nguvu zake mpaka sasa…?’ akaulizwa.

‘Haikuwezekana , maana baada ya hapo, huyu mtaalamu alisema mwenzake kaharibu kila kitu chake alichokuwa nacho, na sasa iliyobakia ni kuweka mitego yake anayoijua yeye mwenyewe,  ili kumnasa huyo adui yake, na hiyo mitego inahitajika kuwekwa kwenye nyumba ambazo huyo adui wake huwa anapita mara kwa mara wakiwindana…ndio maana akawa anawaomba hao akina mama, kwa kusingizia kuwa kuna mazindiko na kitu kama hicho,…’akasema.

‘Kumbwe hakukuwa na mazindiko kama alivyotuambia sisi, sasa kulikuwa na kitu gani …?’ akauliza mke.

‘Hakukuwa na mazindiko, yeye ndio alitaka kuyaweka hayo mazindiko kwa ajili ya kupambana na adui yake, na kama mlivyoona hakufanikiwa, mwenzake alimuwahi…kipindi hicho yupo huko Ocean road, na huko ndio mlikutana naye…yaliyotokea huko mnayafahamu zaidi kuliko mimi.’akasema.

‘Sasa swali, je ina maana hii mimba ya huyu binti ndio huyo shetani wa kupambana na huyo adui yake na ina maana ni mimba ya huyo mbwa -shetani…?’ akaulizwa.

‘Hapo mimi sijui, lakini kwa mara ya mwisho kuongea na huyo jamaa aliniambia hivyo, kuwa ni moja ya silaha zao za kupambana na huyo adui wake, sasa zaidi ya hapo, mimi sijui, na wala sikuwahi kuongea naye kuhusui kuwa hiyo mimba ni ya nani, zaidi ya kauli hiyo, kwa kipindi hicho nilikuwa na mawazo jinsi gani nitaongea na kijana wangu…’akasema.

‘Kwa kifupi unataka kusema kuwa hii mimba sio ya kawaida, mtoto aliyepo tumboni sio wa kawaida, atajifungua kioja au sio…?’ akaulizwa.

‘Mimi hapo siwezi kujua, naomba mnielewe hivyo, siwezi kudanganya, maana sikupata muda huo wa kuongea na huyo mtaalamu tena…baada ya tukio lililotokea….’akasema.

‘Kwahiyo hapa tunabakia na mambo mawili makubwa, la kwaza ni hilo la mimba ya huyu binti….,je atasaidiwaje maana hapo alipofikia hakuna jinsi ni lazima ajifungue, na hatujui atajifungua kitu gani, je hakuna jinsi gani nyingine ya kumsaidia,…hiyo ni kazi yako wewe uliyesababsiha hili..au sio jamani….’akauliza mke wake.

‘Ni kweli, wao ndio sababu na wao ndio wanatakiwa wajue jinsi gani ya kumsaidia huyu binti…’akasema mama Ntilie, mimi nikawa kimia tu, sikuwa na nguvu ya kuongea kabisa.

‘Lakini  la pili ni kuhusu kijana wako, je alikuambiaje mlipokutana baada ya siku saba kupita, na yeye utamsaidiaje kurejesha hali yake,…?’ akaulizwa.

‘Ni kweli siku saba zilikuwa zimeshapita, maana hapo kulipita siku mbili tatu hivi baada ya jamaa kusema mwenzake kamuwahi kaharibu kila kitu chake, na ilitokea kabla haijafika hiyo siku ya saba.,..’akatulia.

‘Kijana muda wote huo alikuwa haki hapo nyumbani kama nilivyosema, alikuwa akikaa na babu yake, na huko hawakuwa hivi hivi, walikuwa wakimuhangaikia, kwa namna wanayoijua wao,kwani alimuelezea babu yake kuwa kapatwa na mambo ambayo hayafahamu na yamemuathiri..wakakimbilia kumuambia labda ni sababu ya madawa ya kulevya..

‘Babu sio madawa ya kulevya, …’akasema

‘Sasa unahisi ni nini…?’ akaulizwa

‘Babu nimepimwa haospitalini, wanasema eti kwa umri huo nina martatizo ya kisukari…mara shinikizo la damu, ni kweli babu, hayo sio magonjwa ya wazee…?’ akauliza.

‘Hahaha, mjukuu nikuambie kitu, sasa hivi ni wewe unajiumiza, kwanini unatumia vilevi, madawa ya kulevya, hujui athari zake ndio hizo…’akaambiwa

‘Babu mimi sikupenda iwe hivyo..ni hali ya hapo nyumbani …wazazi wangu nawapenda sana, lakini yanayotokea hapo yananipa mawazo sana, naamua kutumia hivyo vilevi…’alimuambia babu yake hivyo.

‘Hayo mazungumzo, niliyapata kutoka kwa huyu mama yake hapa….nashukuru kuwa wao hawakuweza kukimbilia kusema kuwa kijana kafanyiwa mabaya, kwahiyo ilikuwa ni swali gumu kwangu, nikijiuliza je kijana wangu aliambiwa na nani hayo mambo…

Nilikuwa na wakati mgumu sana na siku saba zikapita bila mchezo,…na kijana hajapona, na aliahidi kama asipopona, atamwambia mama yake na atamwambia mbele ya babu na bibi yake,…


Ilikuwa siku ya saba nikiwa nipo kwangu, siku hiyo sikuweza hata kutoka kwenda kwenye shughuli zangu, siku hiyo mke alikuwa hayupo , na kipindi hicho hata huyu binti hayupo, maana kuna kikao kilifanyika nyuma ikashauriwa huyo binti aondoke, ni kipindi hicho hicho, nahangaika….na nashukuri kuwa hata kwenye hicho kikao kijana wangu hakuweza kuliongelea hilo,

 Sasa safari hii sizani kuwa atanisamehe…na nitamuambia nini, ili anielewe, hapo nipo mimi mwenyewe nawaza na kuwazua, mtaalamu anaumwa hawezi kunisaidia tena, je akifa kabla hajamsaidia kijana wangu itakuwaje, nitakwenda kwa nani, ..nikawa najiuliza maswali mengi kichwa …na.mara nikasikia mlango ukigongwa, maana kwa usalama nilikuwa nimefunga milango, nikajua ni mke wangu.

Nikakimbilia kufungua mlango, na mlango ulipofunguka …moyo ukanilipuka utafiri nimeona kitu gani,...nilibaki nimeduwaa, ….

NB: Ngoja niishie hapa kwanza


WAZO LA LEO: Familia hujengwa na mshikamano wa wanafamilia, wote wawe kitu kimoja na lengo moja, kusiwepo na sintofahamu ya kila mtu anakuwa na jambo lake binafsi, kwa kufanya hivyo ni kumpa nafsi shetani, ambaye raha yake ni kuhakikisha ndoa hazisimami, ndugu kwa ndugu hawaelewani…...
Ni mimi: emu-three

No comments :