Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, August 9, 2017

DUWA LA KUKU....32



Yule jamaa aliposikia gari limesimama nje, akatoka mbio mbio uso wake ukionyeha furaha sana, sisi tukabakia ndani tukimaliza kupanga vitu vyetu, na ilichukua muda , jamaa akawa anaongea na huyo mgeni ambaye bafo tulikuwa hatujafahamu ni nani, japo tulihisi huenda akawa ni huyo mke wa huyu jamaa kama ni kweli, ..

Tulisikia sauti sauti za kuongea lakini hatukuweza kufahamu wanaongea nini hasa, na baadae mlango ukafunguliwa , aliyeingia alikuwa huyo jamaa akiwa na tabasamu tele mdomoni. Aalipofika ndani akasimama na kugeuka nyuma, hamuoni mwenzake, akasita kidogo, lakini akawa anaongea hivi;

‘Jamani, natumai muda umefika, najua nimewasumbua sana, na pia nimemsumbua mke wangu, kumbe alikuwa kwenye kikao muhimu cha matatizo ya familia ambayo kisa ni mimi, madeni yamekuwa mengi, matatizo ni mengi kweli kweli, na ..aah, kisa ni mimi, lakini nina imani sasa, kwa vile nitakuwa nimepona natumai hivyo, nitayalipa hayo madeni kwa mikono yangu hii..’akasema akionyesha mikono yake miwili.

Sasa akawa anaangalia nje, akimsubiria mwenzake lakini kukawa kimia, huyo mwenzake hakuonekana, sisi tukabakia kuangalia mlangoni kwa hamasa, na huyo jamaa alipoona kimia, akaita

‘Mke wangu mbona unasita kuingia ndani, ingia, umuone huyo bint, ninayekuambia, ndiye sababu ya kupona kwangu, na ndiye sababu hal zetu zitarejea tena, nina imani hiyo, ingia, mbona …..’akanigeukia na mimi nilikuwa nimesimama nikiangalia huko mlangoni, na huyo anayesema ni mke wake hakuingia mara moja,  ikawa twajiuliza kuna nini tena huko nje mbona huyo mtu haingii. Nikaona niendelee na kazi zangu…nikawaacha, nikiendelea kuingiza vitu sehemu tunapovihifadhia.

Wakati narudia kuchukua vitu vingine mara nikamuona huyo jamaa akielekea huko nje, kumfuata huyo mke wake, sijui kwanini huyo mke wake, amegomea huko nje,…

Mara nikasikia huyo jamaa akisema;

 ‘Mke wangu unalia nini, yote hii ni mitihani ya mungu haya yametokea kuwa fundisho kwetu, hasa mimi, kwanini unalia, ingia kwanza tulimalize hili, na nina imani mengine yatakwisha tu kwa mapenzi yake mola, nisamehe sana na nakuomba tuendelee kuwa pamoja, usichukulie hasira, na mimi ni binadamu, kutelekeza kupo, nakuahidi hayo hayatatokea tena…’akasema.

;Hayo hayatatokea, ni rahisi kusema hivyo au sio…lakini madhara yake utayalipaje, umwaumiza watu wengi, hadi familia yako,..najua utasema hivyo kwa vile wewe unaitetea nafasi yako, au sio,…aah, sijui kama nitaweza hili na hali irejee tena kama awali,..sijui….’ilikuwa sauti ya kike.

‘Mke wangu ulisema umenisamehe, sasa hayo yanakujaje tena…ingia kwanza tuyamalize haya ya hapa, najua baada ya hapa hakutakuwa na matatizo tena, nakuahidi hilo…’akasema huyo mume mtu.

‘Sawa, ..nakuja….’akasema

Baada ya muda nikasikia hodi ya kike, nikajua wawili hao watakuwa wameshaingia ndani. Kwa muda huo nilikuwa kwa ndani nikipanga vitu vizuri, moyoni nilikuwa na hamasa sana nimuone huyo mke wa huyo jamaa yupoje, na yawezekana ni watu wanaojiweza maana kaja na gari…

Nikawa naharakisha kupanga viitu vyema, ili sije kuwa usumbufu wakati wa kuvichukua, sikutaka kuharibu kazi yangu japokuwa nilikuwa na hamu ya kumuona huyo mke wa huyo jamaa, nikamaliza, na niliskia huyo jamaa akimtambulisha mkewe kwa huyo mama, hapo nikaamini kuwa ni kweli, maana bado tulikuwa tunamtilia mashaka, huenda hata mke hana….

‘Huyu ndiye mke wangu, niliwaambia nina mke mnzuri, unamuona..kakondoa tu kwasababu ya matatizo, lakini …atarejea hali yake hivi karibuni…’akasema huyo jamaa.

‘Mke wangu huyu ni mama Ntilie amenifaa sana, chai nzuri,…na chakula, lakini mara nyingi niliwa sili chakula hapa, maana nilikuwa natimiza wajibu wa kuzunguka kuwatafuta niliowakosea,..na sikupenda kula mchana,…huwa nilikuwa nakunywa chai ya nguvu, nikishiba mpaka kesho tena,..kwangu mimi, kiukweli ulikuwa mchana wa toba, wa kuomboleza, ndivyo maisha yangu yalikuwa hivyo, baada ya kuwakimbia, hayo nakumbuka sana….’akasema huyo mbaba.

‘Oh, nashukuru sana, mama Ntilie, kama alivyokuita mume wangu maana tumehangaika sana kumtafuta huyu mtu, mpaka ikafikia muda, tukasema basi huenda huyu mtu hayupo tena duniani, jana tu tulikuwa kwenye kikao cha wanandugu kuamua hatima yake, unajua tena mtu akipotea siku nyingi wengine hufikiria vibaya, na leo ilikuwa kutoa maamuzi,…bahati ndio nikapata hiyo simu, sikuamini….’akasema huyo mwanamke.

‘Walijua nimekufa ee, watakufa wao kwanza…watu wengine bwana wanakimbilia kuona wenzao wamekufa….walifurahi nimechanganyikiwa hawachakoma, sasa wanazua nimekufa, wajinga sana hao watu…sasa nipo hai, na nkuja kivingine,…hivi hapa kuna slooni karibu..eeh, ngoja…’jamaa akasema sasa akishika shika maywele yake akihis vibaya

‘Sio hivyo wewe mwanaume, ilikuwa, ni…ni namna ya kutafuta njia ya kuhakikisha upo wapi na je upo salama…wewe fikiria umepotea muda gani, hujulikani wapi ulipo,…hivi hata ingelikuwa wewe unaglifikiriaje,..na yote umayataka wewe mwenyewe…’akasema huyo mwanamke.

‘Sawa, mke wngu… mimi nipo salama kama unavyonioana na ni kwa mara ya kwanza leo nimeweza kujitambua, waulize hawa watu ambao walikuwa wakiniona kwa siku chache nilizoweza kufika hapa,…siku nyingine zote ilikuwa kama nipo gizani, sijijui sijui nipo wapi,…na najua huku kupona sio bure , ni baada ya huyo mdada kukubali kunisamehe, vinginevyo sijui ingekuwaje…’akasema.

‘Mdada yupi huyo maana na wewe ulikuwa mwingi sana, umewakosea mabinti wa watu wengi tu, sijui wangapi, kiukweli inatakiwa uwaendee wote mmoja baada ya mwingine, maana bila hivyo…utakuwa bado, hujafanikiwa,..na ni kweli haya yote yaliyokupata ni sababu ya uzandiki wako,, na tatizo ni kwamba madhara yake yametukumba na sisi tusio husika na madhambi yako, yupo wapi huyo binti jamani natamani nimuone …’akasema huyo mama akiangalia huku na kule.

‘Anakuja…’akasema huyo mama na mimi ndio nikatokea..

**************
Unajua ni maajabu sana, wakati natokea huyo mama mgeni alikuwa kageukia mlango mwingine, akijua huko ndio nitatokea,  sasa mimi nikatokea mlango mwingine uliopa nyuma yake, aliposikia sauti ya nyayo zangu, ndio akageuka, macho yake yakakutana na yangu…hata mimi mwenyewe nilipigwa na butwaa, kuachia yeye ambaye, akabakia mdomo wazi, na macho kayatoa, ananiangalia tu…na kuniangalia, akawa hanimalizi…

‘Ndio wewe ….mungu wangu, ni wewe au ..hapana siamini…’akasema sasa akishika kichwa, na hakuishi ahapo akapiga magoti, akasimama, akasogea , ikawa kama anatafuta hewa, au siju anataka kukimbia…

‘Hata mimi ilikuwa hivyo hivyo mke wanguu nilipomuona huyu binti…sikuamini kuwa ni yeye….kabadilika eeh…lakini sura haipotei, unamuona alivyo, na nasikia….’akasema mume wake, na kabla hajamaliza mke wake akamkatili na kusema;

‘Mungu wangu,..ooh, unajua hii dunia, …samahani sana binti…niliambiwa huyu binti kafariki…’akasema na akawa anatikisa kichwa, sasa akimuangalia huyo mama Ntilia. Na kauli hiyo ikanifanya hata mimi nishutuke.

‘Nani alizuia hivyo…unaona watu walivyo, mimi wanafikiria nimekufa, na huyo binti naye walimzulia kuwa amekufa, kwanini wao hawajifikirii kuwa wamekufa…watu wabaya kweli…ni nani huyo alikuambia hivyo…?’akaulizwa na mume wake.

‘Yaani, akili hapa haipo sawa, na unajua aliyesema hivyo ni nani, alikuwa yule rafiki yake, yule binti mwingine aliyeiba na kutoroka…na yeye anasema kasikia kwa watu…’akasema

‘Kwani keshapatikana..?’ akauliza mume wake sasa akimuangalia muke wake kwa macho ya hamasa.

‘Unacheza na serikali wewe..na hata hivyo za mwizi ni arubaini, walitegwa wakanaswa, utaiba utatumia zitakwisha, lazima utatoka tu…na cha wizi hakidumu, kamwe,…’akasema huyo mama.

‘Oh afadhali …kama wamepatikana eeh, sasa wataenda kunyea debe, si wameshafungwa au….?’akasema mume wake, na kuuliza.

‘Basi huyo binti aliniambia hivyo, nilipokwenda kuwaona, wakiwa jela …yeye sijui alisikia wapi, akaniambia ana masikitiko sana, kwani kapata taaarifa kuwa rafiki yake, yule binti aliyekuwa kwangu, akaondoka, kafariki,, aliumwa sana akalazwa na kutokana na yale mazindiko, na masharti aliyopewa ambayo aliyapuuzia, akaacha kuyafuatilia, yalianza kumpatiliza…’akasema huyo mama.

‘Waongo hao…’akasema huyo baba.

‘Sasa sikiliza …,  basi huyo binti alipokuwa huko hospitalini, alizidwa sana, uamuazi ukawa afanyiwe upasuaji, na kabla hawajafanya hivyo, akafariki, na mtoto alifarikia tumboni…na alipopasuliwa kumtoa mtoto, akatokea kiumbe wa ajabu sana…’akasema huyo mama.

‘Mungu wangu ni nani huyo alitengeneza huo uzushi..?’ akauliza huyu mama Ntilia.

‘Aaah, tuyaache hayo, mungu akupe maisha marefu binti….na kiukjweli, huyu mwanaume kanieleza mengi hapo nje, kuwa kakuomba msamaha, na mimi sitakuwa mbali na yeye na mimi nakuomba unisamehe sana, najua mengi yaliyotokea…eeh,…’akawa ananisogelea kunipigia magoti.

‘Mama usifanye hivyo, hustahiki kunipiga magoti mimi, wewe hujanikosea kabisa hata huyu baba, mimi sijui kanikosea nini, mpaka sasa hajatuambia nilichomkosea, nashangaa tu kaja anasema nimsamehe, nimsahemeh anini sasa, hata hivyo mimi nishamsamehe, kama kuna lolote alinifanyia, mungu amsamehe tu maana yeye ni sawa na mzazi, …’nikasema, na huyo mama akaniangalia kwa macho ya kushangaa na huruma

‘Kakukosea sana tu…na ni kwa vile hakujakusimulia….’akasema huyo mama, na akashika kichwa kama anawaza jambo, na kama vile kakumbuka kitu akasema

‘Unajua, ...usije kumdharau mtu katika hii dunia, hata kama unacho, una uwezo, lakini hujui ni kitu gani kamtunuku mja wake, ambacho wewe huna…huyu binti mungu kamtunuku jambo ambalo wengi hawana,…hata wakijifanya wanalo, lakini ni gumu sana kuwa nalo….’akasema

‘Nakushukuru sana binti yangu,…maana kwa uoni wangu, mimi najua nimekukosea sana, hivi sasa ndio naanza kulitambua hilo, lakini muda ule ambao nilikuwa na uwezo wangu, maisha mazuri, nilikuwa silioni hilo kabisa…kwa muda ule ilikuwa rahisi kuchukua maamuzi ya haraka, hasira, dharau, vilinitawala sana, njia rahisi ni kufukuza, si nitapata mfanyakazi mwingine,..nilijiona nimesoma, pesa ninazo,  watu kama hawa hawawezi kunibabaisha,…sasa mitihani iliponizidi, nikaanza kuchanganyikiwa, vyote nilivyokuwa navyo havikuweza kunisaidia…’akasema.

Nilimuangalia huyu mama akiwa anaongea na akilini nikawa nawaza sana maisha ya mwanadamu yalivyo, jinsi gani mwanadamu anavyoweza kubadilika kwa muda mfupi, maana huyu mama alikuwa kibonge siku zile, mwenye nazo, anajiamini , leo hii anaonekana kakonda,kazidi kuzeeka, ..mvi zinameta meta, kichwani, anaoenakan hana raha kabisa, ni kwa muda mfupi tu,….moyoni nilimuonea huruma sana.

 ‘Najua utanisamehe, lakini moyo unanisuta kwa maana ni mimi ndiye nilikutoa kijijini nikaahidi kuwa nitakutunza, nikachukua dhamana hiyo kwa mama yako, na hadi anafariki alijua mtoto wake yupo mahali salama, lakini sikuikumbuka dhamana hiyo na adhabu zote zimenishukia mimi,…adhabu za familia nimezibeba mimi, kila nikiwazia hilo, naona nimekukosea sana, unajua niliwahi kumuota mama yako alinilaumu, ananiambia saa umefany anini..hivyo, sasa nimefanya nini, ina maana ananisuta, ananilaumu….’akasema.

‘Mama kiukweli mimi sina kinyongo na wewe, najua hata ingelikuwa mimi nipo kwenye hiyo sehemu yako labda ningelifanya hivyo hivyo,..na una maana huyu baba ndiye yule mume wako, mbona kabadilika hivi, .?.’nikasema na kuuliza

‘Ndio yeye, ni hiyo midevu na hali ngumu, ndivyo vimemfanya usimkumbuke,  ndiye yule aliyekusababishia hayo yote, huku sasa akinichunguza tumboni na mimi nikajitahidi kujiminya kwa ndani ili ile mimba isionekane kwa vile nimevaa dera, lakini haikuwezekana, yeye akasema

‘Ina maana hiyo mimba ndio imekuwa hivyo, jamani watu waongo, hata siwezi kumuamini mtu tena, ..hapana…’akasema sasa akificha uso wake na mikono.

‘Ndio hivyo mama,  nasubiria kudra za mungu, nina imani mimi nitajifungua salama na mtoto wangu atakuwa mwema tu, sizani kama yale waliyoongea watu yanaweza kuwa ni ya ukweli, hata asipokuwa na baba, mimi sijali, nitamlea kama mtoto wangu….’nikasema
‘Safi kabisa, utazaa na utazaa mtoto mwema kabisa, hiyo ndiyo imani sahihi, nikuambie ukweli kwenye matatizo unakutana na vishawishi vingi, mimi walikuja watu wakanishawishi niende kwa waganga wa kienyeji kwa matatizo ya huyu mwanaume….’akasema nilishangaa kwa nini hasemi mume wangu kama zamani,

‘Ilibidi nikubali tu maana nipo na mtoto wa watu, ni mume wangu, ningefanya nini, lakini kwa bahato nzuri sijui ilikuwaje mwanaume huyu akatoroka, na akapotoea hadi leo ndio tunampata…sasa kumbe ndio alikuwa akikutafuta wewe…’akasema

‘Mimi sijui kama alikuwa akinitafuta mimi..’nikasema nikimtupia jicho huyo mzee, yeye alikuwa kainamisha kichwa chini, …

‘Hisia ndizo zilikuwa zinamtuma hivyo, nakumbuka alipoanza kuchanganyikiwa ni pale nilipokuwa namuuliza, je atakuja kusema nini mbele ya mungu kwa  hayo aliyokufanyia wewe..baada ya kuanza kuugundua ukweli,.. unajua nimekuja kugundua mengi yaliyokuwa yakitendekea pale ndani, na kumbe kisa ni huyu mzee,…’akatulia akimuangalia mume wake.

‘Waambie tu, ukweli mke wangu mimi nipo tayari, maana  nilitaka wewe uje uyaseme yote, maana nikisema mimi watafikiria bado nimechanganyikiwa, waambie ukweli wote kunihusu mimi..ila sasa aujue na akisamehe ajue ni kwanini nimehangaika hivi na kwanini namuomba huo msamaha…’akasema.

‘Nina imani nikisema kila kitu huyu bint hataweza kukusamehe kamwe…’akasema huyo mama

‘Hapana mwambie tu…nipo tayari ..’akasema huyo mzee

‘Kwani ni lazima kuniambia…kama mnaona kuna utata, na huenda nika…lakini mimi vyovyote iwavyo, siwezi kuwa mbaya kiasi hicho, furaha yangu ni kuona nyie wawili mnarejeana kama mlivyokuwa awali,…familia yenu iwe na furaha…’nikasema.

‘Kiukweli…ni ngumu,…’akasema.

‘Ina maana mlifikia hatua hiyo, mpaka wewe na yeye mkataka kuachana,au mumeshaachana tayari…?’ nikauliza

‘Hatujaachana…’akasema huyo mzee

‘Sasa tatizo ni nini hapo….?’ akauliza mama Ntilie

‘Sijaachana na yeye kisheria, mnielewe hapo, lakini upendo wa kweli ni kutoka moyoni, huwezi ukaishi na mtu mpo mpo tu…ni kama unafuga nyoka,…maana mtu kama alifikia hapo, akayafanya mambo mabaya kiasi hicho, ni sawa na nyoka tu, siku yoyote angeliweza kuniua,…ohooo, hapana nyie hamjayasikia aliyoyafanya….’akasema.

‘Sasa mimi na kushangaa..ina maana wewe hukutaka mume wako apone au..?’ akauliza huyo mama

‘Kupna ni kitu kingine,.sawa nimefurahi kapona, kama binadamu maana hakuna binadamu eliyekamilika anayeweza kumuombea mwingine mabaya, akitokea hivyo, huyo ni shetani,..mimi sio shetani…ila moyoni, nikiyawazia yaliyotokea, nilivyoteseka, na walivyoteseka wengine unaaambiwa chanzo ni mtu mnayeishi naye,….’akasema

‘Na ni kweli ….?’ Akauliza huyo mama Ntilie

‘Ni kweli si huyu hapa, …muulizeni…..’akasema

‘Lakini hata hivyo, kupona kwake, ni kupona kwa familia, na haya yakiisha ni mafamikioa ya familia yenu au sio…sasa kama wewe upo hivyo, mnatarajia nini kwa huyu binti, kama wewe umeshindwa kumsamehe mume wako, huyu binti afanyeje sasa…?’ akauliza huyo mama Ntilie.

‘Hapana, yeye, ni kwa utashi wake,hilo siwezi kumuingilia na nashukuru kwa moyo wake huo, ni mtu wa pekee katika hii dunia,na sijui labda nahisi ni kwa vile hajausikia ukweli wote, kuhusu alichofanyiwa na huyu mwanaume…sijui kwanini watu kama hawa ..wanaoa…’akasema akimuangalia mume wake kwa hasira.

‘Lakini mama, mimi sioni kosa, kukosea kupo, ina maana wewe hujamkosea mtu, akakusamehe…?’ nikamuuliza

‘Si kama hivyo nilikukosea wewe, na umenisamehe lakini sio kama hayo aliyonifanyia huyu mtu…’akasema

‘Lakini mimi nimekusamehe sijaona kosa kubwa ulilonifanyia yeye, ..muhimu, nionavyo mimi,  ni kuliona kosa lolote ni kosa tu la kibinadamu, na wanadamu tunateleza, ten asana, muhimu ni kusameheana,na mimi nimemsamehe kwa lolote lile alilonifanyia nimemsamehe…’nikasema.

‘Hapana kabla hujasikia hayo aliyokufanyia, usiseme hivyo kuwa umemsamehe, nafsi itakuja kukusuta baadae, subiria kwanza, ngoja nikusimulia tu… na ukiyasikia ukimsamehe na mimi , labda…nitaweza kuingiwa na nguvu hiyo labda na mimi mungu atanijalia niwe na moyo kama wa kwako, ili niweze kumsamehe…’akasema.

‘Oh, kama unaona ni lazima kunisimulia, lakini…sawa,  ….lakini mimi vyovyote iwavyo, nimeshamsamehe huyu baba, yeye ni baba yangu, na alichukua jukumu hilo, kama baba yangu, na wewe ni mama yangu ulinichukua kijijini kwa wema wako, yaliyotokea ni mapito tu, …’nikasema.

‘Huyu ndio binti yangu, natamani ningelikuzaa mimi…’akasema mama Ntilie

‘Hata kama hujanizaa nakuona sawa na mama yangu, sitakusahau maisha mwangu …’nikasema kumuambia huyo mama Ntilia, na huyo mam Ntilia akainua mkono juu wa ushindi.

‘Haya tuambie hayo ambayo huyu mbaba alimfanyia huyu binti…..’akasema huyo mama Ntilie,na huyo mama akamgeukia mume wake na kusema.

‘Upo tayari mume wangu niyaseme madhambi yako yote…?’ akaulizwa

‘Ndio maana nilisubira uje uyasema yote wayasikia,usifiche kitu hata kimoja..nipo tayari…’akasema

NB: Haya yale maswali yote yatajibiwa humo…


WAZO LA LEO: Tukikoseana ni wajibu wetu kusameheana, ni mangapi tunawafanyia wengine, mabaya zaidi, lakini tunasamehewa, ni mangapi tunamkosea mola wetu anatusamehe, tunaiba maofisini, njiani ..kwa dhahiri na kwa kificho, tunafanya makosa mbali mbali, pasi na kuonekana, lakini tukitendewa sisi ni wepesi, kutumia mikono yetu hata kuua,..chuki zipo mbele kuliko upendo,  je ingelikuwa hivyo, tunafanyiwa sisi, tungelikuwa hai……tusamehe ili na sisi tuje kusamehewa.
Ni mimi: emu-three

No comments :