Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, August 4, 2017

DUWA LA KUKU....29


Nikiwa bado hospitalini, akaja mume wa yule mama  aliyeibiwa, akanihoji, alinihoji kwa taratibu tu, na baadae akasema;

‘Mtafuteni huyo mdada, huyu hawezi kuwasaidia kitu, hamuoni,….huyu atawasaidia nini kumpata huyo mwizi, muwe mnaelewa,..mnapoteza muda kwa mtu huyu huyu, haya niambieni mumefikia wapi..?’ akawauliza watu wake wakamuelezea, halafu akasema.

‘Nataka huyo mdada apatikane, nawapa siku mbili tu..mkishindwa nitaifany amwenyewe…’akasema na kutoa amri kuwa niachwe huru. Hapo nikawa na amani, na baada ya amri hiyo, nilipona haraka kuliko ilivyotarajiwa…na siku napewa ruhusa ya kutoka hospitalini, akaja bint wa kule nilipokuwa nakaa kwa muda huo.

Alikuwa kabeba begi la nguo, akaja hadi pale nilipokuwa nimesubiria dawa na baada ya hapo niondoke kurudi nyumbani, huyo mdada sijui alijuaje nitatoka, na hakuwahi kuja kuniona kabla, wengine walikuwa wakijitahidi kufika, sikumlaumu kwani nilishamfahamu tabia yake.

Alipofika na kuniona nasubiria, akaniangalia kwa dharau, ni kawaida yake kuniangalia hivyo, utafikiri yeye ana kwake, au ana maisha yake ya hali ya juu,…yeye na wenzake wanaishi kwa wazazi,..sawa ni wazazi wake ana haki ya kuringa, lakini yeye kazidi, ananichukia sana,  na yeye ni mkubwa tu kuliko mimi , lakini hana mume, nasikia aliolewa akaachika.

Akanisogelea na kusema;

‘Pole na kuumwa, najua umeshapona, vinginevyo utakuwa unadeka tu, …ili uendelewe kuletewa chakula,…’akasemaa

‘Ndio nimeshapona namshukuru mungu, na nimeruhusiwa nilikuwa nachukua dawa, nitafute usafiri…’nikasema.

‘Sawa endelea kumshukuru, na kumuomba sana, haya kabla hujatafuta usafiri,  …. hapa kuna barua yako kutoka kwa mama, si unajua kusoma wewe…eeh…’akasema akinishikisha mkononi, na mimi kwanza nikasita kuipokea, akanishikiza kwa nguvu, halafu akasema;

‘Isome mwenyewe,..maana mjumbe hana kosa au sio..haya soma mpendwa…’akasema huku anacheza mguu chini kwa nyoda na dharau, huku kashika kiuona,…huyu mdada ni katika mabinti wa pale, wanaonichukia sana, yeye tofauti kama wengine, wengine kidogo wana afadhali, lakini huyu kazidi kunichukia sijui kwanini;

Nikasoma ile barua, iliandikwa hivi;

Sasa umepona, nimempigia simu docta wa hapo, sasa ni hivi, muda niliokubaliana na mume wangu wa kuishi kwangu umeshapita, sasa kwa wema kabisa, ninakushauri urudi kule ulipotokea, wao ndio walikutoa kijijini na kukuleta hapa mjini, sasa ni wao wajua jinsi gani utaishi,..kwangu sitaki kukuona tena, usije ukaniibia kama mwenzako alivyoiba huko, samahani kwa usumbufu, mimi mama …’

‘Sasa mimi nitaende wapi, jamani, si angenipa muda kidogo, ndio nimetoka hospitalini…oh, mbona mtihani huu...?’ nikamuuliza huyu mdada, akabenua mdomo kwa dharau na kuniangalia juu chini, halafu akageuka kuangalia mbele, na kusema;

‘Mimi isjui ndivyo nilivyoambiwa, unasikia, usije kunitolea machozi hapa, maana kulia kwako ni wimbo wa taifa, sasa ukalilie huko mbele , sio mbele yangu, ukanitia uchuro…. na begi lako la nguo hilo hapo…umeliona eeh,  mpendwa umesikia, …’akasema akigusa begani, baada ya kuniona nimeduwaa, na mimi sikusema kitu,

Akatembea hatua moja mbili kama anazihesabu halafu akageuka na kusema , sasa kwa sauto ya kawaida, ili watu wamuone kama tunaagana kwa wema; Anajua kuigiza huyu binti,…kuna muda anaweza kuigiza mtu mwema, utamuona ni katika wema waliofuzu, lakini unayemfahamu tabia yake, hutatamani kukaa naye dakika mbili, …


‘Kama kuna kitu kingine kimebakia kule wewe niambie nitakuja kukuletea huko utakapokwenda kuishi…, sawa, pole sana, eeh, halafu nimesahau…’akarudi na kufungua pochi yake, akatoa pesa
‘Chukua hii pesa, itakusaidia kujikimu, hapa nimekata nauli yangu, usije kusema umepewa pungufu, unasikia, haya tukijaliwa tutaonana, kwaheri eeh mpendwa, usijali, maisha ndivyo yalivyo, …’akasema na kunikabidhi hizo pesa, na mimi nikawa nimeduwaa tu, hata sijui niende wapi, nilikaa pale hospitalini kama mgonjwa tena, na mdada huyo akaita bajaji na kuondoka zake.

Nilikaa pale kwa muda mrefu, unajua ni kama mtu kafukuzwa nyumbani kwao, na hajui wapi kwingine pa kwenda, akili imeduwa, haijui hata ifikirie nini, …nikawa nawaza hili na lile, nikamuomba mungu kwa imani zangu zote anionyeshe njia, …mpaka sasa sijui nifanyeje…

Baadae sana likapita gari, na mara likasimama, alikuwa ni yule mbaba, askari, ambaye ndio walioibiwa, akaniona bado nimekaa hapo hospitalini ndio akaniuliza mbona sijaondoka;

‘Mbona bado upo hapa, si nasikia umesharuhusiwa tatizo ni nini tena…?’ akauliza

‘Wamesema nisirudi kule tena, wanadai nitawaibia, na mimi sijawahi kuiba maisha mwangu,…na sasa hata sijui nitakwenda wapi..’nikasema huku machozi yakinilenga lenga.

‘Oh, sasa hilo ni tatizo jingine, na wewe huna ndugu yoyote hata mmoja hapa Dar…?’ akaniuliza

‘Sina, aliyenichukua toka kijijini ni yule mama wa kule, mwenye matatizo na mume wake,..naye hakutaka nikae kwake tena, hata sijui niende wapi tena ..’nikasema.

‘Sasa kwanini wanakufanyia hivyo, na hiyo mimba ni ya nani…?’ akaniuliza akinikagua tumbo langu.

‘Mimi sijui, ..’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya mashaka, halafu akasema;

‘Wewe hujui,..mbona sikuelewi,…sasa unajua,…hebu ingia ndani ya gari, nikupeleke nyumbani kwangu, nitaongea na mke wangu, najua sasa hivi yupo na hasira sana, lakini tutaona tufanyeje, hawawezi kukufanyia hivyo sio utu…’akasema

‘Kwako tena, si ndio huko walipoiba, naogopa kukutana na mkeo, najua ana hasira za kuibiwa nay eye anahis labda nimeshirikiana na huyo mdada, kumbe mimi sijui lolote..’nikasema
‘Wewe twende tu…tutajua mbele kwa mbele…’akasema na nikaingia kwenye gar hadi nyumbani kwake.

Nilipofika tu, aliyetufungulia mlango ni huyo mke wake, aaliponiona aliniangalia kwa uso uliojaa hasira, akageuka na kuingia ndani, hakusema neno. Mimi na begi langu la nguo, nikaingia na kukaa kwenye kiti, nikisubiria maongezi ya wawili hao,…hawa nao wana familia, lakini kwa muda huo watoto wapo shuleni, kwahiyo ndani kulikuwa kimia.

Wawili hao wakaanza kuongea taratibu, mara sauti zikaanza kuongezeka, mara ikawa sasa ni mshike mshike mwanamke hakubali, na hasikii chochote anachoambiwa na mume wake,..

‘Kama umeamua kumleta huyu, haya ngoja mimi niwapishe, maana hata hiyo mimba mpaka sasa haijajulikana ni ya nani huenda ni yako….’akasema huyo mama

Baadae sana, mume mtu akanijia na kusema;

‘Unajua sitaki matatizo, mke wangu ana shinikizo la damu, naogopa ukiendelea kukaa hapa, italeta shida nyingine, sasa ngoja kidogo,…akapiga simu kwa mtu, na akawa anaongea naye;

‘Kile chumba bado kipo, hakijapata mtu, eeh, safi kabisa, mimi kitanifaa, kuna binti, ..hana mume…eeh, hana matatizo, hilo nakuhakikishia, sawa, anakuja sasa hivi, hana mizigo yoyote ndio anaanza maisha, hivyo hivyo, ..usijali, tutaongea…’akakata simu

‘Oh, afadhali, …kuna chumba, sasa mimi nina rudi kazini,kuna kazi nyingi huko, lakini siwezi kukuacha hapa, mtaishia kubaya na mke wangu, wewe ingia kwenye gari twende…’akasema na mimi nikaingia kwenye gari, hao tukaondoka.

Wakati tupo kwenye gari, akampigia yule mfadhili wangu wa kwanza, kuwa kapata chumba, na kinafaa mimi nikae huko, wanasema kuhusu kusaidia kulipia kodi, na jinsi gani ya kuishi…

Mfadhili wangu wa awali, akasema hawataki hata kuniona kwani hivi sasa wanapambana na maisha magumu, yeye alifika nikiwa hospitalini akanieleza kila kitu, na hivi sasa mume wake amekuwa kama kachanganyikiwa, mtoto naye kagundulikana ana matatizo makubwa, kwa hivi  hawezi kubeba mzigo mwingine, keshachoka.

‘Oh, mbona inawia ngumu, sawa kwa vile nipo naye nitaona jinsi gani ya kufanya, ila msisahau kuwa nyie ndio mlimchukua huko kijijini, tukifuatilia sheria mnaweza kuwa matatani, unielewe,…hamna shida, mimi nitajitahidi kadri niwezavyo,…hamna shida, sawa shemeji, poleni sana…’akasema na kukata simu

Tukafika kwenye hiyo nyumba, ilikuwa nyumba ya kawaida tu, ila kuna vyumba vya uwani, vya kawaida tu, na akaongea na mama mmoja, ..huyu mama ndio mwenye nyumba, akaniangalia halafu akasema;

‘Sawa mimi sina shida, wanawake ni wazuri maana sitakwua na shida ya usafi, ila sitaki mlevi humu au Malaya, tutakosana…’akasema na kutembea kuelekea kwenye hicho chumba, ..

‘Chumba ndio hiki,…unakiona kilivyo, hakina tatizo, …ukitumie na ukiache kama kilivyo, sawa, nimekupa hiki chumba kwasababu ya huyu mtu, kanisaidia sana, …fadhila zake ndizo zimenifanya nikubali, ila kodi sasa itakuwaje…?’ akauliza akimuangalia huyo mbaba.

‘Kwanza nitakulipa kodi ya mwezi huu..shilingi ngapi….’akasema akifungua pochi lake, akatia pesa, na huyo mama akazipokea na kuanza kuzihesabu, na kusema;

‘Oh, sasa hii si kodi ya mwezi mmoja tu, sio makubaliano yetu  hayo…’akalalamika

‘Wewe si unanifahamu, nyingine zitakuja, usijali, ngoja nifike kazini, huyu sasa ni mtu wako, …unanisikia mengine tutaongea…’akasema na kuanza kuondoka, niliogopa hata kumuuliza nitaishije…

Na mar akarudi tena, sasa akiwa na mifuko mwili na hisi ni ya kilo tano tano, mmoja una unga mwingine mchele, na…mafuta kwenye chupa,……halafu akatoa pesa mfukoni akanikabidhi na kusema;.

‘Sasa mimi nimejitahidi hadi hapa,…sikulitegemea hili, cha kushuru ni kuwa sasa.umepata chumba, nimelipia mwezi mmoja, unasikia, utalala vipi, hilo siwezi kuliwazia kwa sasa, tumetoka kuibiwa, si unalewa hasara tuliyoipta, sasa mimi nakucha,…’akasema
‘Ahsante nashukuru sana kwa wema wako…’nikasema
‘Muhimu kwa hivi sasa,  kama una jamaa unaowafahamu basi watakusaidia zaidi…na, kwa miezi mingine..nitaona jinsi gani ya kufanya, tatizo wewe una mimba,..ok, hilo utajua mwenyewe, sizani kama unaweza kupewa mimba usijue ni ya nani, kwani ulibakwa…?’ akaniuliza

‘Hapana, sijabakwa…’nikasema.

‘Ulipenda mwenyewe…?’ akauliza.

‘Nimekuambia mimi hata sijui mimba imetoka wapi,…hakuwahi kukuelezea mama…maana wao wanajua…’nikasema.

‘Hapana, huwa hatoongelei mambo ya watu, mimi na mke wangu, huwa nina sheria zangu, anyway, hilo utajua wewe mwenyewe…’akasema, na kugeuka kuondoka, halafu akageuka tena na kuniuliza.

‘Ina maana wewe kweli huna rafiki yoyote wa kiume…?’ akaniuliza akinikagua tumbo.

‘Mimi sina tabia hiyo, sina kabisa rafiki wa kiume…’nikasema

‘Haya tutaona….basi nitaona jinsi gani ya kukusaidia, ila…usije kusema kwa mke wangu kuwa ni mimi nimekusaidia hadi hapa unasikia,…au kwa yoyote yule, sawa…nitakuja nikipata muda, ila sikuahidi unielewe,…zaidi nitakuwa nawasiliana na huyo mama mwenye nyumba wako, huyo mama ni mtu mwema sana, ananifahamu sana…’akasema na kunitupia jicho….nilihisi namna ya mashaka, wanaume hawaaminiki, lakini nikamuomba mungu apitishie mbali.

Basi nikachukua vile vitu na kuingie kwenye chumba hakina kitu chochote …zaidi naona kulikuwa na jiko la mchina, na sufuria moja, sijui ni vya nani, nikasema moyoni, hivyo ndio vya kuanzia maisha.

Huyu mbaba akaondoka na gari lake, nikabakia humo kwenye chumba, kitupu, nikahesabu pesa nilizopewa na huyo mbaba na zile za yule mdada aliyekuja hospitalini, nikaona nitaweza kuishi siku mbili tatu, lakini sasa humo nitalalaje, hakuna godoro,..ila shuka ninayo,…nikafungua lile begi, nikakuta shuka, na khanga zangu, …sio haba, nitaishi.

 Hapo, nikakaa chini kwanza, nikiwaza….na mara moja nikayakumbukia maisha yangu na mama, yalikuwa ya dhiki hivi hivi, lakini tulikuwa na kitanda, hapo machozi yakaanza kunitoka na haikupita muda nikashikwa na usingizi, na mara mama akanitokea

‘Mwanagu, usikate tamaa, unakumbuka usia wangu,…usiogope kusema ukweli hata kama utakuumiza wewe au huyo unayemuambia huo ukweli..ukweli uwe ndio silaha yako..na pia usimuamini kila mtu, sio kila akuchekeaye ana nia njema na wewe, cheka naye, lakini akili kichwani mwako, jingine nilikuambia, uwe mbali na wanaume, na usipende kupokea misaada yao, kwani kila wakitoacho kina namna ya ghiliba,..

Muhimu mwanangu, ishi ukimtegemea mungu wako, kwani kila alilokujalia nalo lina maana yake, usijione upo mpweke, mungu wako yupo nawe kila mahali,usichoke kumuomba...na kumbuka jambo moja,sasa ndio maisha yako yameanza,..subira yako ndiyo itakufikisha kwenye mafanikio,…kamwe usikate tamaa..

‘Sasa mama na hizi pesa za huyu mbaba, na vile vitu alivyoninunulia nivirudishe kwake..?’ nikauliza na mara nikazindukana.

 Nikasikia mtu anagonga mlango, nikaitikia karibu, 

‘Kuna mgeni wako huko nje…’nikasikia yule mama akiniambia, lakini sauti ya mashaka

‘Haya nakuja…’nikasema hata sijui ni nani kaja kunitembelea ambaye anajua nimehamia hapo..,

*****************

 Alikuwa ni yule mama aliyeibiwa, sikumkaribisha ndani, na yeye hakuonekana kutaka kukaa, akasema

‘Ndio sehemu mume wangu kakuleta huku, eeh...mume wangu ni wajabu sana, ..hahaha....kwahiyo kakuleta huku muwe mnakutania mara kwa mara nilijua tu kuna kitu kati yako wewe na mume wangu, au sio..?’ akaniuliza.

‘Mama , mbona unanishutumu kitu ambacho mimi sikijui, yeye, kanileta huku, wala sijui…’nikasema na yeye akanionyeshea mkono wa kuwa hataki kunisiliza.

‘Ila mimi nakuonya tu, nitakuwa nakufuatilia hatua kwa hatua siku nikimkuta mume wangu hapa, mpo naye…utanitambua mimi ni nani…umenisikia, labda mtafute sehemu nyingine, nisiwagundue, lakini nitawafikia tu, siku hiyo ndio hasira zangu zote zitaishia kwako…’akasema na kugeuka kuondoka.

Na alipoondoka yule mama mwenye nyumba akaja na kuniuliza

‘Huyu kajuaje kuwa upo hapa, maana mume wake hakutaka kabisa mkewe ajua kuwa upo hapa, ooh, sasa naona nyie watu mnataka kuniletea balaa kwenye nyumba yangu, kama ni hivyo tutashindwana..’akasema.

‘Lakini mama mimi sijui chochote,  hata huyo mume wake kanichukua hospitalini na kunileta hapa, sikujua kama ana lengo lolote baya…’akasema.

'Lengo lolote baya, kwani hujui kwanini kakuleta hapa...hahaha wajifanya huelewi eeh,,,,'akasema

'Mimi ninachojua ni usamaria wake mwema tu ...'nikasema

‘Kwahiyo wewe na yeye, hamjaelewana chochote kuwa ukae hapa kwa vipi ...?' akaniuliza.

‘Kuelewana kwa vipi mama, ..?’ nikauliza.

‘Kwani hiyo mimba sio yakwake..?’ akaniuliza

‘Hapana..’nikasema bila kuongeza maneno na huyo mama akanikagua kwa macho halafu akasema;

‘Ya nani sasa, binti,..hala hala… usije ukawa na matatizo, sitaki matatizo kwenye nyumba yangu, namuheshimu tu huyo askari, kwasababu kanisaidia mambo mengi, vinginevyo nisingelikukubalia wewe, kwasababu huna kazi, je utanilipaje, nikajua huyo askari ni mwenza wako, kumbe tena, huna mahusiano naye,..oh, ngoja nitaongea naye…’akasema

‘Mama , kwangu usiwe na wasiwasi sina matatizo na mtu yoyote…, sina tabia mbaya kamwe haya yaliyonikuta ni mitihani tu ya mungu, na wala sijui hata hii mimba imeiingiaje,...’nikasema

‘Imeingiaje, kwani mimba zinaiingiaje, usinichekeshe binti, mimi ni mtu mnzima usinifanye mtoto mdogo, ina maana labda ulibakwa au..?’ akaniuliza

‘Yaani mama mimi sijui...hata sijui nikueleze vipi unielewe…’nikasema.

‘Sawa mimi sina tatizo, ila masharti yangu ni hayo, kukitokea tatizo lolote, wanaume kuja kugombana huku au wake zao kuja kuleta zogo humu, unaondoka,…sawa…’akasema na kuondoka.

****************

Kumbe huyo mama alikuwa na biashara zake , alikuwa anatengeza chapati na kuuza chai, na mara nyingine mama ntilie, na sijui ni kwanini anasema huyo askari alimuokoa hadi biashara zake bado zipo…sikupata muda wa kumdadisi saa maana muda mwingi, alikuwa kwenye shughuli zake na wateja wake.

Siku iliyofuata nilifika kwa huyi mama anapofanyia shughuli zake nikamuomba nimsaidie atanilipa chochote, atakachoweza na nikashangaa, akanikubalia tu.

Halafu siku hiyo ikawa ni kama bahati, kukawa na wateja wengi, kiasi kwamba hata huyo mama alishangaa, ikabidi aagize vitu vingine vya kupika na kupika mara mbili, isivyo kawaida yake.

'Haijawahi kutokea, yaonekana wewe umekuja na bahati, kesho uje tena…wewe naona unanifaa…’akasema na mimi nikamkubalia kwa furaha nikijua sasa nimepata sehemu ya kujishikiza.

 Basi ikawa hivyo, namfanyia kazi zake, ikifika usiku ananilipa ujira wangu, wiki ikapita, na kila nikienda dukani kununua vitu, naomba maboksi, na mifuko fuko, na hiyo nikatengeneza kitanda, siku zikaenda, maisha yakasonga mbele…

 Kila siku ilikuja na neema zake, nikaja kupata kitanda kilikuwa kinatupwa, nikakiomba, nikampelekea fundi, akanitengenezea vizur tu, huku naendelea kusaidiana na yule mama katika shughuli zake za biashara, akanipenda sana, wateja wakawa wanamiminika…

Pamoja na hayo yote, tumbo lilikuwa linanisumbua sana, ilikuwa mtoto tumboni hatulii, na zile dalili za kukanguliwa zikawa ndio zinazidi, lakini mimi sikujali vile vitisho kuwa ni dalili za kuwa mtoto huyo atakayezaliwa atakuwa si mtoto wa kawaida, atakuwa na dalili za shetani.

'Kama nitazaa mtoto mwenye sijui tabia za shetani, basi hata yeye ni kiumbe cha mungu, yeye aliyekiumba atajua jinsi gani ataishi,..ila nakuomba ewe mola wangu, mimi nikiumbe chako dhaifu, nakuomba sana ewe mola wangu nisaidie niyashinde haya majaribu maana mimi sikuomba hili linitokee…’nikawa kila nikiwaza au kutokea na maumivu hayo namuomba mungu wangu hivyo.

 Siku moja nikawa naumwa sana tumbo, yule mama akaniambia nipumzike tu, yeye ataendelea na malipo yatakuwa kama kawaida, basi ikawa hakuna jinsi,lakini sikutaka kwenda kulala kule ndani kwangu, nikatafuta sehemu hapo hapo huyo mama anapofanyia kazi, nikajiliza, sio mbali na hapo, na sehemu  huyo mama anapofanyia shughuli zake. Nilitaka nikijisikia vizuri nimsaidia hata kusoha vyombo.

 Wakati nipo hapo, hali ikazidi kuwa mbaya sana, na wakati napambana na maumivu mara nikasikia huyo mama akiongea na mteja mmoja, cha ajabu niliweza kusikia kwa mbali wanvyoongea, lakini sikuweza hata kujiinua, mwili wote ulikuwa umeishiwa nguvu,  mwili umelegea kabisa siwezi hata kuinua mkono au kutoa sauti, nikawa nasikia maongezi yao, kama ndoto vile, kwa mbali kweli…

'Mimi nimetokea huko kijijin kwetu nilikuja kutafuta wafadhili, wa ujenzi wa nyumba ya ibada…..’nikasikia hivyo, lakini mengine sikuyasikia,…baadae nikasikia, huyo mama akimuuliza huyo mteja..

'Ina maana hakuwahi kuwa na mtoto….’sauti ikakatika, na nikajihisi sasa kama napoteza fahamu kabisa, natamani nipige ukelele lakini sikuweza hata kufunua mdomo.

'Alikuwa naye…., tumemtafuta hapatikani, nasikia, alikuja….  Tujenge…ibada, na kama…..’nikawa nasikia vipande vipande wanavyoongea, mengine sikuyasikia, na sikuweza hata kutafakari, walikuwa wakiongea nini…ila mwishoni nikasikia, hivi;

'Je akitokea na ikawa yeye hataki hilo jengo, anataka kujenga nyumba yake ya kuishi mtafanya nini…?’ ilikuwa sauti ya huyo mama,  hapo nikasikia vyema, na sauti ya kiume ikasema;

'Tutamtafutia…….’hapo sauti ikakata,…sasa hapo ndio hali ikawa mbaya kabisa, na nikahisi kupoteza kumbukumbu masikio yakawa hayasikii tena, nikazama kwenye giza na kupoteza fahamu.

 Kumbe kwa bahati nzuri, walivyoniambia baadae, alipita mmoja wa wateja eneo hilo, sijui alikuwa anatafuta nini, ndio, akaniona, akatoa taarifa kwa huyo mama, na walichofanya hapo siwezi kujua, ila walikuja kuniambia walinibeba na kunitoa nje ili nipate hewa, lakini haikusaidia, wakahisi nimekufa,..ila wakajadiliana kuwa nipelekwe hopsitalini.

 Kwa tukio hilo nililazwa karibu wiki, na baadae nikatoka na nilipotoka, nikarudi kwenye chumba changu, na yule mama akawa sasa ndiye ndugu yangu wa karibu…., na tukaanza kuzoeana kiukweli, hata ikafikia hatua nikaanza kumuhadithia baadhi ya maisha yangu, alisikitika sana, mengi ya huko nilipofikia na yaliyotokea kwa hao akina mama, sikumuhadithi, nilimuhadithia, ya nyumbani nilipotokea na kupata taarifa ya kuwa mama kafariki kwa kuchomewa nyumba moto..

'Wewe, unajua kuna mzee mmoja,..tena siku ile ulipozidiwa ndio alikuja akawa ananihadithia,…umesema kijiji gani, ..ndio huko huko, ..yeye alikuja hapa na karatasi anachangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya ibada, nimemzoea tu, kila akifika safari zake za kutoka kijijini anapitia hapa sio mara ya kwanza kuoana naye, lakini hatuna udugu naye kabisa….

'Sasa nitampataje huyo mzee…?’ nikamuuliza nikiwa na hamasa fulani, japokuwa sikupenda kabisa kurudi huko, lakini kwa vile wametaja eneo, nikawa nimekumbuka eneo la mama, hata hivyo sikuwa na tamaa nalo maana hata kuchomewa nyumba na visasi vinawezekana ni kutokana na eneo hilo.

'Aliacha karatasi ya kuchangisha watu kwa ajili ya ujenzi wa hiyo nyumba ya ibada, mimi sikutilia maanani, sikjui kama ipo ngoja tukimaliza kazi nitaitafuta, kama ipo au nimefungua wateja vitafunio,…’akasema na tukaendelea na shughuli zetu, tukasahau, siku pili, hata hatukukubuka kuliongelea, ila siku ya tatu, akaja na hiyo karatasi.

Kweli kwenye ile karatasi kulikuwa na namba ya simu, anasema alimpigia na akamwambia na yeye alikuwa na mipango ya kuja huku dar, wiki ijayo, basi tukasema tusubirie….

 Nikawa namsaidia huyo mama napata ujira wangu, japo kidogo sio haba, na humo humo, nikaanzisha mradi mwingine wa uji, kidogo kidogo nikaanza kuwekeza, nikanunua godoro la bei ndogo, ili nikifungua nipate pa kulala na huyo mtoto nitakayejifungua mungu akipenda.

 Siku moja akaja mbaba mmoja kafuga madevu, alionekana kama kachanganyikiwa vile, akaagiza chain a vitafunioa, na uji,…vitu alivyoagiza, tuliingiwa na wasiwasi huenda asilipe, lakini cha ajabu akaomba apigiwe mahesabu yake, na alipotajiwa ni kiasi gani akalipa, na kuanza kula, taratibu hana haraka.

Na muda wote alikuwa kainamia vitu vya kula, hakuwa akimuangalia mtu…sasa alipomaliza, akajifuta mdomo na midevu yake, akasimama akitaka kuondoka, ndio akaweza kuniangalia mimi,..muda alikuwa kashika gilasi ya maji, aliomba maji ya kunywa na mimi ndiye nilimpelekea,  aliponiona akashtuka, na kudondosha ile gilasi ya maji ikavunjika…

‘Vipi mzee mbona wanivunjia vyombo vyangu…’mama akamuuliza na jamaa akasema.

'Samahani mama Ntilie, na..na...nataka kuongea na huyu binti....tafadhali...' akasema


'Wa nini...kuongea naye nini...?' akaulizwa na kabla hajajibiwa akaanza kulia, kulia kweli kweli, na alipotulia akanisogelea na kunipigia magoti....watu kimia, kila mmoja anajiuliza hili na lile kichwani, kunani kwa huyu mzee ambaye anaonekana kama kachanganyikiwa!

NB: Je ni nani huyu.


WAZO LA LEO; Sio kila baya lina ubaya, mabaya mengine yanatokea kwa minajili ya kuleta neema fulani ambayo sisi kama wanadamu hatuwezi kuifahamu kwa hapo hapo, na sio kile jema lina wema wote, wema mwingine unaweza ukawa mtego wa kukupeleka kubya, kwahiyo, kila jambo likitokea, shukuru na mkabidhi mola wako, kwani yeye ndiye anajua zaidi.
Ni mimi: emu-three

No comments :