Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, August 17, 2017

DUWA LA KUKU---37



‘Baba nimegundua kuwa matatizo haya niliyo nayo sababu kubwa ni wewe,….’kijana alimuambia baba yake

‘Nani kakuambia hayo, ni nani …?’ baba akamuuliza kijana wake akiwa kama kapigwa kofi usoni.

‘Nimeshajua kila kitu baba…, unachonifanyia mimi,..na nakupa siku saba, baba mimi nakupenda sana, nawapenda sana wazazi wangu, ...lakini kwanini unifanyie hivi, kwanini baba, sasa baba, japokuwa, nawapenda, japokuwa nyie ni wazazi wangu, lakini kwa hili umevuka mpaka, ..baba,..nakuomba, ... usiporejesha hali yangu, nitamuambia mama yoote, mbele ya babu na bibi, unasikia mbele yao, …’kijana akasema na kuondoka..

'Mwanangu sikiliza kwanza...we....'alikuwa ameshaondoka.

 Ndio nikaamua kuongea na mtaalamu akasema hiyo ni kazi ndogo kwake, na kwa vile humo ndani kuna binti ambaye anaweza kulifanikisha hilo, basi atakuja...lakini pamoja na hayo anahitajika mbwa. 

Mbwa…ndio mbwa….!!!

‘Mbwa , mbwa wa nini…?’ nikamuuliza

Tuendelee na kisa chetu…..

****************************

‘Nilimuuliza swali hilo, lakini hakunijibu hapo kwa hapo, akasema tutajua huko usiku ukifika,…’akasema

‘Kwahiyo huyo mbwa alitoka wapi..ni wewe ulimtafuta, au…?’ akaulizwa

‘Yeye aliniambia tunahitajika kutafuta mbwa, na hakusema nimtafute mimi, lakini cha ajabu kulipopambazuka nikasikia mke wangu akilalamika kuwa kuna mbwa yupo hapo nje na hataki kuondoka, nikakumbuka maneno ya mtaalamu kuwa hilo kafara la usiku linahitajia mbwa…basi ili kulificha hilo, nikamwambia mke wangu.

‘Huyo ni mbwa nimepewa na rafiki yangu, atatusaidia kwenye kazi ya ulinzi wa hapa nyumbani..

‘Mimi sitaki mbwa, mimi na mbwa tofauiti,…na kwanini mpaka tutafute mbwa, nani kakuambia kuna tatizo la wezi hapa nyumbani kwetu…’akalalamika mke wangu.

‘Ni kuwa huyo rafiki yangu kasafiri, na huyu mbwa wake hana sehemu ya kumweka, basi nikaona nimchukue tu mimi maana ni mbwa aliyefunzwa vyema…, akirudi atamchukua mbwa wake, tatizo lipo wapi mke wangu…’nikasema na mke wangu akaondoka bila mabishano zaidi , na huyo mbwa akawa hapo kwetu, sikujua anatakiwa kufanyiwa nini kwa muda huo,….na sikuwa na uhakika kuwa huyo mbwa ndiye aliyeletwa na huyo mtaalamu au la…’akasema

‘Ina maana hukumuuliza huyo mtaalamu wako….?’ Akaulizwa

‘Sikukumbuka hili hutaamini, mpaka usiku ukafika….ghafla wakati naingia ndani kutoka kwenye shughuli zangu nasikia mnguromo wa mbwa, nikashtuka, na nilipochunguza vyema nikamuona huyo mbwa kalala pembeni mwa nyuma karibu na dirisha la mdada….’akasema.

****************

‘Endelea, ehe mbwa huyo alifanya nini maana hapo unatutisha…na mbwa tena….’akasema mama Ntilie.

 Mimi alipomtaja huyo mbwa, ndio nikamkumbuka vyema, mbwa huyo nilimuona alipokuja, siku hiyo nilikuwa nafanya usafi, mara nikaona mbwa kasimama karibu na geti, mlango wa geti ulikuwa wazi, nikajua katokea nje, nikamfukuza kwa mawe, ili atoke nje,  hakuondoka, badala yake akaja kusimama karibu na mlango, na akawa ananitizama ninvyofanya usafi...

Basi mimi nikamuacha nikaendelea na shughuli zangu, na mama mwenye nyumba alipomuona akaniuliza huyo mbwa katokea wapi, mimi nikamwambia sijui...basi akajaribu kumfukuza lakini hakuweza maana huyo mbwa alikuwa akikimbia kuzunguka nyumba, hatoki nje, na alipochoka kumfukuza akamuacha na kumuuliza mumewe kumuhusu huyo mbwa, na sijui waliongea nini.

Cha ajabu cha huyo mbwa, akawa karibu na mimi sana siku ile,  na mimi kwa huruma nikampa chakula mchana ule, na usiku akalala nje, karibu na dirisha langu, nakumbuka kweli, usiku alikuwa akitoa mngurumo wa ajabu, kama analia wakati mwingine kama mtoto, au..kama sauti ya mtu hivi analia.....sikumjali sana, maana mimi nimetokea kijijini, milio ya mbwa, paka, ni kitu cha kawaida huko kijijini.

Ila cha ajabu kingine ninachokikumbuka ni kuwa usiku ile niliota ndoto, kuwa huyo mbwa, kaja kulala na mimi, hiyo ni ndoto lakini,...nikajaribu kumfukuza lakini hakutoka, na nikamuacha akalala ubavuni mwangu..ndivyo nilivyokumbuka na mengine yalikuwa yale ya kukabwa, na nakumbuka huyo mbwa ndiye alikuwa akinisaidia, hadi nilipokuwa sikumbuki tena kilichotokea hadi asubuhi, 

Kulipopambuzuka huyo mbwa alikuwa hayupo....!


************

 Huyo mzee akawa anaendelea kusimulia,...

‘Usiku sikuwa na raha kwanza kuhusu kijana wangu, nilijiuliza kajuaje,…maana yanayotokea usiku inakuwa sisi tumelala,na hatuyaoni….na labda kuna mtu kamuambia, atakuwa ni nan…nikawa najiuliza bila kupata hjibu.

Na nikakumbuka kuwa kuna kauli ya wakwe zangu kwa pesa zangu ni za kishetani, na wao wameshanipa muda nijikoshe, kwa kusema ukweli hayo ninayoyafanya, la sivyo wao wataingilia kati, hawawezi kuona mtoto wao yupo kwenye maattizo wao wakae kimia,..na pia wao wamesema wameshagundua ninafanya mambo ya kishirikina, na kwa hilo watahakikisha nazalilika, hilo sikulijali sana, maana vitisho vyao sio kwa mara ya kwanza, lakini hili la mtoto wangu lilinifanya nisiwe na raha kabisa.

Mke wangu siku hiyo alisema atachelewa maana mke wangu kwa shughuli humtoi, na hakujua kuwa shughuli zake ndizo hawa watu walitumia kufanikisha mambo yao…’akasema.

‘Kwa vipi, kwani zinawasaidiaje..?’ akaulizwa

‘Mara nyingi mke wangu akirudi kwenye shughuli huwa kachoka, hana muda wa ibada, yeye ni kukimbilia kulala, na hao jamaa ndio wanatumia mwanya huo kufanya mambo yao, sijui wanajuaje kuwa mke wangu leo ana shughuli na ndio wakati wao muafaka wa kufika…’akasema.

‘Kwahiyo usiku huo, wakafika, niliwahisi kama kawaida, na kipindi hicho sikuwa nalala kitanda kimoja na mke wangu, tulikuwa hatuivani kila mtu na kitanda chake, …’akatikisa kichwa kusikitika.

‘Kwahiyo mke wako alikuwa hajui kuwa hali yako imerejea kama kawaida, …?’ akaulizwa

‘Sijui, nahisi hakuwa anajua na aliona nikiwa na wasichana ni kama kujipotezea pesa tu, ndio maana hakujali sana….’akasema.

‘Basi nikawa nasubiri nione mtaalamu atakavyonisaidia,…kumbe alikuwa yupo dar,  alikuwja kufuatilia matibabu yake,, ….alikuwa anahangaika na hospitali, na kwa kipindi hicho alikuwa kaandikiwa kwenda Muhimbili. Kwahiyo haikuwa ile safari ya kutoka huko mikoani, ….’akasema

‘Ulijuaje…?’ akaulizwa

‘Alikuja kuniambia baadae….’akasema

Usiku wakafika na kikosi chake, na nilihisi kuwa wapo kamili, kuna hali niliihisi hivyo, na na ile hali yangu ya kuishiwa nguvu ikanijia, na nakumbuka wakati hali hiyo inatokea, nikaona mke wangu akihangaika, akipambana pale kitandani, na hata kabla sijapotezaa fahamu zangu kabisa, nilimuona mke wangu akiinuka kitandani, ana akawa anatoka nje, ….nikajua itashindikana..na hapo hapo mimi nikazama kwenye giza…

***************

Mimi sikujua kilichotokea ule usiku, …ila asubuhi mke wangu alkuwa hayupo, nikaulizia, wakasema mke wangu aliondoka usiku huo hukalala hapa nyumbani…nikampigia simu, na akasema;

‘Nipo kwetu,….’akasema

‘Kwanini…?’ nikamuuliza

‘Sikuweza kulala usiku, mbwa, alikuwa akitoa mngurumo wa ajabu, kuna milio kama ya bundi…kuna hali nahsi kuna watu wanaifanyia mabaya, nikaona humo ndani hakulaliki, ndio nikaondoka…’akasema

‘Sasa mbona mimi nimebakia humu ndani, kwanini hukuniamuisha…?’ akaulizwa

‘Nilikuaga, lakini hakusema kitu,…ulikuwa kama unaweweseka weweseka, nikajua ni dharau zako tu…, nikaondoka zangu, na wakati napita kwa huyo binti nilisikia makelele fulani , nikajua ni kawaida yake ya kuota , sikutaka kusubiria, nyumba ilikuwa inatisha muda huo, ajabu nilipotoka nje sikumuona huyo mbwa, wakati nikiwa ndani nilisikia sauti ya mngurumo kama wa mbwa…’akaniambia.

‘Huyo mbwa atakuwa alienda wapi, au alikuwa katoka nje…?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui alienda wapi , sikutaka kujua, nikaondoka zangu…’akasema

‘Ni kijana wetu je, hukutaka kumuangalia, ulijijali mwenyewe…?’ nikamuuliza mke wangu.

‘Kwanini nisimjali, nilipotoka nilikwenda chumba chake, na kugonga, hakukuwa na mtu ndani, nikajua hakulala humo ndani…’akasema mke wangu.

‘Atakuwa alienda wapi usiku huo..?’ nikamuuliza mke wangu.

‘Labda alikwenda kulala kwa marafiki zake, alinilalamika kuwa kuna jambo linaendelea humu ndani, linampa shida, usiku analala kwa shida, na hali yake imekuwa mbaya sana anahisi tatizo linatokea humu ndani, sikutaka kumuuliza sana mambo hayo, maana sitaki mambo ya kishirikina,…kwahiyo kuanzia sasa kaamua,kuwa hatalala hapa nyumbani siku zote…’akasema

‘Atakwenda kulala wapi, na kwanini hajaniambia mimi mmwenyewe…?’ nikauliza

‘Kasema anakuja kulala huku kwa babu yake, na hilo la kwanini hajakuambia sio kweli, kasema kuwa keshakuambia, na kakupa wiki moja umpatie jibu….’akasema

‘Kaniambia nini, wiki moja ya nini,…kasema hivyo, anataka jibu gani..?’ nikamuuliza, nikijifanya kushangaa

‘Kasema wewe unajua ni kitu gani, na kaapa kuwa usipompa jibu atakachokifanya humu ndani tutakuja kumsikia kwenye vyombo vya habari, sasa labda nikuulize wewe kuna nini kinachoendelea humo nyumbani kwetu, nisingelipenda kusikia yanayosemwa na wazazi wangu lakini hali iliyopo inanilazimisha kuamini hayo…’akasema

‘Kwani wewe hajakuambia ni kitu gani…?’ akaniuliza

‘Kaniambi wewe unajua kila kitu, sasa ukiniuliza mimi nakushangaa, hamjaongea naye…?’akasema na kuniuliza

‘Oh, haya  ngoja nitaongea naye..’nikasema

‘Mim sitarudi hapo nyumbani kwa leo, nitakuwa narudi mara moja moja kuna kazi naifanya kwanza, …huyo binti atakusaidia saidia kazi za hapo nyumbani,..ila nakuonya huyo binti wa watu, kama kuna lolote unalomfanyia, sitakusamehe kabisa…muogope mungu…’akasema.

‘Nimfanyie nini mimi huyo binti,…., si unanijua nilivyo, hali yangu si unaijua, ukiniona nastarehe, ni kujipooza tu , ili kuondoa mawazo…’nikasema.

‘Ulivyo eeeh, unanifanya mimi mtoto mdogo, sioni kinachoendelea, unakumbuka uliniambia kuwa unajiona umepona, je ulipona nini…kwako wewe kupona imekuwa kama ng’ombe wa ndani kufunguliwa nje, unaparamia kila mtu, haya endelea na tabia yako hiyo mbaya, unachokitaka utakuja kukipata, …’akasema.

‘Mke wangu hayo umeyapatia wapi, hali sasa mbaya, wewe huoni, …?’ akaniuliza

‘Umenisikia bara bara, na kwa vile hata mtoto wako kakufahamu ulivyo..basi itakuwa rahisi kwangu, kuchukua hatua muda ukifika, usije kusema sikukuambia,..nasubiria watoto wengine wakija watoto ndipo kila kitu kitawekwa bayana,, sasa hivi naogopa kumuumiza kijana wangu…’akasema

‘Ndio maana umekwenda kwenu, kumbe umeshaanza kuwafuata wazazi wako wanavyotaka au sio, sas ahuko unafuata nini wakati wazazi wako hali zao ni mbaya…?’ nikamuuliza

‘Nilikuwa sina sehemu nyingine ya kwenda usiku huo, mimi siwezi kuchukua haya mambo kiharaka hivyo, ninajua sheria za ndoa, na mimi ni mtu mnzima…muda utafika utapata nafsi ya kufanya hayo unayoyataka, siku hizi si una nyumba, una pesa, au…’akasema

‘Mke wangu, si nimeshakuambia, sasa hivi hali imekuwa mbaya, kuna mambo yamekwenda tofauti kabisa.. hali imeharibika nyumba , magari yamechukuliwa kulipia madeni…’nikamwambia mke wangu.

‘Kwanini leo unaniambia hayo mambo yako…?’ akaniuliza

‘Wewe ni mke wangu lazima nikuambie mambo yetu ya famalia, nilishakuambia kuwa hali ni mbaya, hukutaka kuniamini, na…na… haya yote nilikuwa nikifanya kwa ajili ya familia yetu…’nikasema.

‘Yatakushinda, ila nakuonya, kama kuna kitu unachokifanya kwa ajili ya wazazi wangu, utakachokipata utakuja kujuta, hawa ni wazazi wangu, na sijui kwanini unashindana nao…’akasema

‘Nani kakuambia hayo mke wangu, hayo ni mawazo yao, kama wameishiwa wameishiwa kwa mambo yao wasinisingizie mimi…’nikasema.

‘Sio swala la kuishiwa, kwani kuishiwa imeanza leo, wazazi wangu wamekuwa wakikutana na mitihani kama hiyo mara kwa mara, na wanakuja kuinuka tena, biashara ndivyo zilivyo, wao hawafanyi mambo ya kishirikina, kama ya kwako..’akasema,

‘Mambo gani hayo ya kishirikina mke wangu mbona huniamini, kama ningelikuwa nafanya hivyo si ungeliniona,..?’ akauliza.

‘Kuna mtu alikutwa nyumbani kwa wazee akiwa uchi, ..anafanya mambo ya ajabu alipobanwa sana akasema katumwa kuchukua vitu humu kwa wazazi wangu na wewe…’akasema

‘What!!…na mimi kwa vipi, …’nikauliza huku miguu ikiniishia nguvu.

‘Ndio hivyo huyo mtu kachukuliwa na polisi kupelekwa kituoni,…’akasema

‘Kituo gani hicho, nitakwenda kumuona maana mimi sijui kitu kama hicho,…’nikasema
‘Kumuona wapi,…maana hapo walipokuwa wamemfungia, hawakukuta mtu, walikuta mbwa, na huyo mbwa sawa na huyo niliyemuona hapo nyumbani, sasa najiuliza iweje, mtu ageuke kuwa mbwa, wewe mwanaume niambie ukweli kuna kitu gani kinachoendelea hapo nyumbani kwangu…’akasema mke wangu.

‘Mungu wangu, mi-mi….sijui kitu mke wngu na huyo mtu ni muongo mnafiki tu, usiwasikilize hao watu, na uwe unaniuliza mimi kwanza…’nikasema kumuambia mke wangu.

‘Siku zenu sinahesabika, najua kuna jambo unalifanya, ... ila jingine tena la muhimu, ni kuhusu huyo binti wa watu, hajui kujitetea, hataki kunieleza ukweli, ila najua kuna kitu mnamfanyia, ...nakuonya tena kuhusu huyo binti wa watu ogopeni hao watu, mayatima,..masikini, hivi hamna huruma nyie watu....sawa ngoja tuone mnachokitaka kitaishia wapi, utakuja kujuta kwa hilo…..’akasema

'Mke wangu achana na mambo hayo ya kishirikina...'akasema

'Na je huyo mbwa bado yupo hapo nyumbani..?' akaniuliza

'Ina maana ndiye unamuogopa, mimi sijamuona hapo nje...'nikasema na yeye akakata simu.

Kiukweli kauli hiyo ilinichoma moyoni, nilijaribu kuvuta hisia,...nikijaribu kuona ni kitu gani hao watu walimfanyia huyo binti...lakini baadae nikapotezea, kujipa matumaini...sio mimi niliofanya hayo japokuwa ni mshiriki, .., shauri lake huyo mtaalamu, na watu wake...hata hivyo sikuwa na raha...niliona mambo yanazidi kuongezeka, ndio nikatoka nje kuhakikisha kama huyo mbwa hayupo kweli,..hakuwepo

'Huyu mbwa kaenda wapi...?' nikauliza lakini hakukuwa na mtu wa kunipatia jibu, binti alikuwa anafanya usafi huko jikoni na sikutaka kuonana naye, nafasi inanisuta...

Baadae ndio nikasema;

'Ngoja nimpigia Mtaalamu simu yeye atanisaidia kwa haya mambo maana naona hali inazidi kuwa mbaya...'nikasema na kuchukua simu yangu kumpigia huyo jamaa

****************

 Nikampigia simu mtaalamu..nikapiga simu ikawa inaita tu, haipokelewi, nikajaribu tena na tena, na nilipotaka kukata tamaa baadae ikawa hewani, na alipopokea sauti niliyosikia ilikuwa ya mgonjwa aliyezidiwa sana.

‘Mtaalamu vipi, mbona simu hupokei..?’ nikamuuliza

‘Oh,… mimi naumwa sana hali imekuwa mbaya ghafla, tokea nirudi jana usiku, mambo hayaendi vyema, nahisi adui yangu huyo…’akawa anaongea sauti ya mgonjwa ambaye hata kuongea ni shida,

‘Unaumwa nini….?’ Nikamuuliza

‘Si nilikuambia naumwa, nimekuja hapa Dar, kwa matibabu, na…hali inazidi kuwa mbaya, hiyo jana usiku nilifika kwa nguvu za mizimu na kilichonipata huko kimenizididshia matatizo….’akasema.

‘Kwahiyo, jana hukufanikiwa , nitamuambiaje kijana wangu sasa , …?’ nikamuuliza

‘Nitakuambia subiria nipate dawa hali ni mbaya sana…yule mbwa, wamemkamata…na yeye ndiye ooh, kijana wako, ngoja nitakuambia, su-su--aaah….’simu ikakatika.

NB: Naishia hapa kwa leo, kuna mambo naweka sawa kuhusu sehemu hiyo inayokuja...ili tuweze kuhitimisha hiki kisa bila maswali megi....


WAZO LA LEO: Ukiishi kwa kutegemea dhuluma, ukawa unafanya mambo ya kishetani, kula yako, kipato chako, maendeleo yako, mienendo yako,..hakika wewe ni shetani kimatendo, na kwahiyo wewe unakuwa adui wa mwenyezimungu, tubia ewe mwana –wa adamu kabla milango ya toba haijafungwa,…
Ni mimi: emu-three

No comments :