Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 6, 2017

DUWA LA KUKU...7


 ‘Mwanetu, hebu fikiria hivi, wewe haupo duniani, una binti kama huyu, anafika kwenye nyumba za watu wanamfanyiwa mambo kama hayo..kiubinadamu utajisikiaje…, hebu liweke akilini mwako hivyo....'ilikua sauti ya mzee.

'Kuna wengi walikuwa na uwezo wao, wakajua hali ngumu, na mitihani ya dunia haitaweza kuwafika, lakini ya mungu mengi sasa wapo mitaani! Wapo pia walikuwa na hali nzuri, mume akafariki, akawaacha watoto na mama yao huku duniani, wanafamilia hao wakaja kufirikisika hadi kufikia kuwa omba omba, na binti akafikia kwenda kuomba kazi za ndani, haya yapo hayapo....'akasema mzee, akimuangalia mzee mwenzake.

'Yapo sana, na mifano kama hiyo ipo mingi tu....'akasema mzee mwenzake.

'Unajua ukiwa na uwezo, nafsi hukudanganya, unaweza ukajawa na kiburi, na hata ukawadhulumu wengine, wakilalamika kwako na kukuomba, uwasaidie, unawadharau, na wengine wanafikia kumuomba mola wao, mbele ya wenye uwezo, na wenye uwezo kwa kiburi wanajibu, ..toka lini duwa la kuku likampata mwewe....'akasema mzee.

'Ni kiburi kibaya sana hicho....'akasema mzee

'Sasa mwanetu, tusipoteze muda, ubinadamu una madhaifu yake, na kukosa inatokea, na mwenye hekima akikosa huomba msamaha..umekosea, hata kama utajitetea vipi umekosea , sasa ni wajibu wako kuomba msamaha, hatutaki kujitetea, na kuongezea chuki zaidi, haina haja sasa gangeni yayajao,..na humu sasa mna mfanyakazi mwingine, yaliyotokea yametokea, yeye naye kama binadamu atakusamehe kama uliwahi kumfanyia lolote baya...

'Mzee aliposema hivyo, baba mtu akamtupia jich huyo binti, binti alikuwa kainama chini, tu...

'Sasa tuambie, upo tahari kwa hilo...na kulia ni dalili njema kuwa umekiri kosa, unajuta, na ujute basi na kauli yako, kututhibitishia kuwa kweli uliteleza...au sio...?' akasema mzee akimuangalia mzee mwenzake.....

'Sawa tumalize tushikane mkono sisi tuondoke zetu...'akasema mzee mwingine.

Tuendelee na kisa chetu.

*****************


Baba mwenye nyumba. alishika kichwa kwa mikono yote miwili akawa kaegemeza kichwa kwenye viganja vya mikono yake, ikachukua muda, akawa kama anawaza, na baadae akainua kichwa, na sasa akageuka kumuangalia kijana wake...

Alimuangalia kijana wake kwa makini, na inaonyesha labda alikuwa akimuwazia kijana wake huyo huenda atakuwa miongoni mwa hao mashahidi wanaotakiwa kuelezea hicho kinachoendelea hapo nyumbani, yeye anamuamini sana kijana wake na mara nyingi yupo upande wake, lakini kwa namna nyingine hataki kumuumiza mama yake pia...., na huenda keshaongea na mama yake na amekubali kuelezea hayo anayoyafahamu yeye.

‘Mungu wangu, sijui itakuwaje…ni nini hiki, kwanini wananiandama hivi...’akasema kimoyo moyo.

Sasa akageuka kumuangalia binti, tangia waingie hapo, alikuwa akikwepa sana kumuangalia huyo binti usoni,  sasa anawaza kumtafuta huyo shahidi akamtupia jicho kwa mara ya kwanza,…, akamgundua wanaangaliana na kijana wake, na baadae huyo binti akageuka na kuangaliana na baba mwenye nyumba, haraka baba mwenye nyumba akakwepesha macho yake, huku akiwa kakunja uso kwa hasira, alihisi huyu binti anaweza kusema neno ambalo litaiangamiza ndoa yake.

Kilichomuumiza zaidi ni maneno ya baba yake pale aliposema, na kwa maswali aliyokuwa akiuliza alihis kuwa baba yake atakuwa kaamini kabisa hicho alichoambiwa kwa hayo yanayoendelea humo ndani, na kama ni hivyo, basi kwake yeye hana wa kumtetea, na mara akamkumuka yule binti aliyeondoka,…

Binti huyo aliondoka, lakini akiwa kaacha doa kubwa kwenye familia yake, na hadi anaondoka ilisadikiwa kuwa yeye ndiye alimpachika mimba huyo binti, na mpaka ikafikia yeye kutafuta pesa kwa ajili ya kuitoa hiyo mimba mimba, na hapo ndio akakumbuka siku binti huyo alipofika kwake na kuanza kulia mbele yake.

‘Baba haya yote ni kwasababu yako, sasa nina mimba yako, na sijui nitafanya nini masikini wa mungu…’ aliambiwa.

‘Mimba, nani kakupa mimba?’ akauliza akionyesha uso wa mashaka.

‘Unasema nani kanipa mimba, ni wewe baba, umesahau yale yote, nikukanya lakini , ukajifanya huongei, na ukafanya upendavyo, sasa unaniuliza swali kama hilo….’akasema.

‘Wewe binti wewe una uhakika na unachokisema, nimesahau yale yote yapi, una wazimu wewe…?’ akasema kwa ukali, huku akiangalia huku na kule asije akatokea mkewe.

‘Baba,…kwanini unasema hivyo, mara ngapi umekuwa ukifika kitandani kwangu usiku tunalala wote, na matokea yake ndio haya…’akasema huyo binti.

‘Mimi, nahisi wewe umechanganyikiwa,…kwanza hebu toka nje, usiniletee kisirani humu ndani, kama umefanya umalaya wako huko nje, na sasa unatafuta sehemu ya kujitetea, sio mimi, na maneno yako haya inabidi nikufukuze kazi, naona huna nia njema na mimi…’akasema.

‘Unanifukuza kazi, wakati wewe ndiye umeniharibia maisha yangu…na kuapia kabla sijaondoka hapa nitahakikisha nimeongea na mama,..najua yeye ataniamini…kwasabau ipo siku nilimgusia, hakunisikiliza akasema atafanya uchunguzi,….’akasema.

‘Ulimgusia ukamuambia nini wewe, …uliongea naye kuhusu nini...kuwa mimi ndio nimekupa hiyo mimba, wewe binti wewe, unataka nini kwangu, sikiliza hata ukinisingizia, hutapata kitu, na …..’mzee akasikia mlango ukifunguliwa akajua ni mkewe.

‘Nilimuambia tabia yako, kuwa sikuamini na akaniuliza kwanini huniamini nikamwambia una tabia ya kuingia chumbani kwangu usiku, ..na kabla hatujaendelea kuongea, akatokea mgeni , tukakatiza mazungumzo,…kwahiyo usibishe, mimi na wewe tumekuwa tukifanya mausiano ya kujiiba, unabisha nini au kwa vile nina ujauzito wako,…’huyo bint alimuambia baba mwenye nyumba.

‘Mimi,… kwanini nifanye hivyo,…wewe binti wewe una nini lakini, unataka kufanya nini, nitakuharibu, kabla hujatimiza huo ushetani wako humu ndani, nimekuvumilia lakini hili sasa limevuka mpaka,..hebu toka mbele yangu….?’ Akauliza, na kusema kwa hasira.

‘Baba kwanini unanifanyia hivyo, angelikuwa binti yako ungelimfanyia hivyo, au kwa vile sisi ni masikini, mnatufanya mpendavyo,….na hata kama sisi ni masikini, ujue mungu anatuona…hii mimba ni ya kwako, na sitaondoka hapa mpaka kieleweke, umesikia, au niende polisi nikatoe taarifa…’akasema.

Baba aliwaza sana, akajua hayo yakifika kwa mke wake, hataaminika, kwahiyo akatafuta njia nyingine, akili sasa ilishindwa kuwazia, zaidi, sasa akasema;

‘Wewe mimi sitaki huo uongo wako, sijui kwanini umefanya hivyo, nitakupatia pesa ukaitoe hiyo mimba, hata kama sio ya kwangu, na nakuapia baada ya hili sizani kama nitaweza kuishi na wewe humu ndani, utafute kazi sehemu nyingine uondoke, unasikia,…’akasema.

‘Kwanini niitoe hii mimba, unajua hatari yake wewe, au kwa vile….je nikifa, au nikiharibu kizazi changu, nataka unihakikishie jambo la kunilinda, kama lolote litatokea, basi uwajibike…?’ akauliza.

‘Kwani ni ya miezi mingapi hiyo mimba..?’ akaulizwa.

‘Mimi sijui ni ya miezi mingapi…nilianza kujisikia vibaya nikaamua, kwenda kupima, na nilipoona nina mimba, nikachanganyikiwa sikujua la kufanya, na mimi sina mwanaume yoyote niliyewahi kutembea naye zaidi yako wewe…’akasema

‘Nenda kahakikishe ni miezi mingapi, lakini muhimu uitoe hiyo mimba,  unasikia, na usije kuliongelea hili hapa nyumbani, na kwa kuondoa wasiwasi, na sijui kwanini unanifanyia hivyo, wema wangu wote wa kukujali kama binti yangu ndio umefikia hapa, ..sasa ukimaliza kuitoa, utafute sehemu ya kwenda haraka iwezekanavyo, maana na mimi nitatafuta cha kukufanya, hutaweza kunisahau…’akasema, na kumpatia huyo binti pesa za kuitoa hiyo mimba…na kazi ikafanyika.

Na kweli baadae binti akapata kazi sehemu nyingine, na huko akakaa huku akisumbuliwa na tumbo, akaenda kupima, akaambiwa asafishe kizazi, na alipopimwa zaidi akaonekana kizazi kimeathirika, ikabidi kitolewe kabisa.

Binti huyo aikabidi amfuate huyu baba mtu akamuelezea hiyo hali, baba mtu, safari hii alitolewa kwa nguvu, na akaahidiwa kuitiwa polisi, siku akifika tena hapo.

‘Ndio unanifanyia hivyo,…mimi unajua nilipotoka….naahisi hutaishia kwangu, kila atakayekanyaga hapo ndani utamfia hivi, na ole wake ungelikuwa na binti, na yeye angelifanyiwa hivyo….’akasema

‘Nenda zako wewe…nimeshakuambia, nisije kukuona humu tena..unapewa mimba huko unakuja kunibambikia mimi, nimekusaidia bado hujali….kafaney utakavyo, hilo duwa lako ni la kuku tu…’akasema baba mtu kwa hasira.

Baba mtu alipoliwazia hili, akahis machozi yakimtoka, hakujua hayo machozi yanamtoka kwa sababu gani ila alijikuta yakitoka tu….

************

Pale nilipokuwa nimekaa, kichwa kilikuwa kikinawaka moto kwa mawazo, nikifikiria jinsi gani ya kuuongea huo ukweli, lakini huo ukweli usije kuathiri ndoa ya watu. Nilimkumbuka sana mama yangu aliwahi kunionya kuwa vyovyote itakwavyokuwa niwe makini sana kwenye ndoa za watu.

 Nilimuona baba mwenye nyumba akiwa hana amani, wazee walikuwa wakimuhoji kama vile wameshajua kosa lake, na nia yao ni kutaka akiri kosa lake na huenda mkewe akamsamehe.

 Nilijiuliza bila kupata jibu, ni kwanini huyo mbaba akafikia hatua ya kufanya hivyo, mke anaye, tena mke mnzuri tu, hata pamoja na utu uzima alio nao, bado alionekana mrembo, pesa inamfanya mtu asizeeka haraka.. ..na nilipoliwazia hilo nikamtupia jicho huyo mkewe nilimuona mara kwa mara akimuangalia mumewe wake kwa macho ya dharau fulani hivi…, kuonyesha kuwa ana uhakika kuwa mumewe ni mkosaji.

 Nikageuka kumuangalia kijana, macho yetu yakakakutana, kumbe huyo kijana mara kwa mara alikuwa akiniangalia mimi..niliogopa hiyo hali ya kuniangalia itaweza kuleta tafsiri mbaya kwa watu waliomo humu ndani…na tulipoangaliana niliona macho yake yakionyesha mashaka na huzuni…, sijui ni kwanini alikuwa akiniangalia mimi mara kwa mara, nikahisi kuwa huenda ni kwa vile labda mimi nitateuliwa kuwa shahidi wa matendo ya baba yake, na anajua kuwa mimi sitaweza kuficha kitu.

 Ndio ikafika muda baba mwenye nyumba akatakiwa akubali na kukiri kosa laki la sivyo, wataitwa mashahidi, na mama alisema sio masahidi tu, anao mpaka ushahidi wa video, na wazee waliposikia hivyo, walimkazia macho baba mtu ajitoe na kukiri, ili watumie hekima zao za uzee kulisawazidha hilo jambo.

Mke wakati anasubiria mumewe aongee, akasema;

'Wazee wangu, mimi kiukweli nashukuru kuwa mwenzangu ameamua kuwaita nyie wazazi wangu, sikulitarajia hili, nilijua yeye kama muungwana angekuja kwangu na kukiri kosa, aniombe msamaha, na mimi ningelifikiria jinsi gani ya kumsamehe,….sasa yeye kakimbilia kuwaita nyie, labda lengo lake ni zuri kuwa sasa anataka kukiri kosa lake kiukweli na kwamba hatarudia tena,…'akasema mama mwenye nyumba.

'Na nitalifikiria hilo, kama kweli atakiri ukweli wa kukiri,...na itabakia kuamua, kiukweliwazee wangu, nimemvumilia sana, hebu jamani jiulizeni ni nani angelifanyiwa hivyo na bado andelee kuishi na …..hapana hili sasa limevuka mpaka,....siwezi tena, nahisi damu yake bado inachemka sana, akaoe vijana waendane sambamba, si ananiona mimi nimezeeka, yeye bado yumo au sio, sasa nafasi hii ni yake, aamua moja mbele yenu, na kuamua kwake, itategemea na ukweli wake, mimi naufaham ukweli wote, siwezi kumshuku mtu vibaya kwanini ...hapana, nimechoka…’akasema.


 'Unasikia mume mtu, hiyo ndio kauli ya mkeo, kasema yupo tayari kukusamehe, lakini anataka kuona ukweli wako, jinsi gani utakavyojikosha,….maana inavyoonekana kweli umefanya kosa, na waliotendewa wapo, na wamekiri kuwa watasema ukweli, sasa usitake kuumbuka zaidi.

'Wazee wangu, ….hayo anayosema mke wangu, sio kweli, namfahamu sana mke wangu, yeye anachotaka ni mimi nikiri shutuma zake, na kitakachofuata hapo, ni kunifukuza mimi kwenye hii nyumba, alishaniahidi hivyo, sasa mimi siwezi kukubali shutuma hizo…’sasa mbaba akasema na kwuafanya wazee waangaliane tena.

 'Kwahiyo wewe nachoogopa ni hiyo adhima ya mkeo, kuwa takufukuza kwenye hii nyumba, na atakufukuza baada ya kuomba talaka yake, au sio….lakini ukweli ni kuwa umefanya makosa,..na mtu aliye mwema, alitakiwa kukubali makosa,..na kwenye wazee haliharibiki neno..’akasema mzee.

 'Nikiri kosa gani, mimi sijafanya kosa, ni yeye na dhana zake potofu..'akasema mbaba, sasa akimuangalia mkewe kwa uso wa hasira.

 'Ina maana hutaki kukiri kosa, wakati kweli mkeo kathibitisha na kasema yeye ana ushahidi wa kulithibitisha hilo, na ana video ya matendo yako machafu,…unataka nini mwanangu, unataka tuone madhambi yako, ayaonyeshe hapa mbele yetu,hiyo itavuka mpaka, siwezi kuliona hilo, kama kweli unanijali mimi kama baba yako, yamalize haya, kiungwana….’akasema baba yake.

 Mbaba akatikisa kichwa akionekana kusikitika,hakuna aliyejua dhamira yake ni nini..na machozi yalikuwa hayafutika machoni, na hakuna aliyejua kwanini aliyatoa hayo machozi.,machozi ambayo yalimuathiri sana kijana wake, kwa jinsi alivyoonekana akimuangalia baba yake kwa macho ya huruma.

 Kijana akamuangalia mama yake, na alipoona mama yake anamuangalia baba yake kwa kebehi, au dharau fulani, akainamisha kichwa chini na yeye….haikuchukua mdua machozi yakaanza kumlenga lenga, kijana huyu alimpenda sana baba, na sio baba yake tu, aliwapenda sana wazazi wake, hakutaka ndoa hiyo ivunjike, hakutaka kabisa baba yake na mama yake watengane.

 Tendo hilo la kijana kutokwa na machozi, aliliona mdada , na hapo akathibitisha ukweli kuwa kijana huyo kweli anawapenda wazazi wake, lakini swali ni kwanini aukumbutie uovu wa baba yaka kama kweli kayafanya hayo, na je kwanini hamuonei huruma mama yake kwani hali kama hiyo, inamtesa pia mama yake..

Na mara mlango ukagongwa, na wote wakatizama mlangoni...macho ya kila mmoja yalionyesha wasiwasi, walijua labda ni ugeni wa jirani tu,...lakini kwa walengwa, mawao yao yalienda mbali zaidi, maana ugeni humo, ni nadra....

Na aliyesimama kwenda mlangoni alikuwa kijana, ...alisimama kwa haraka na kwenda huko mlangoni, akahakikisha ameufunga mlango nyuma yake, sauti za maongezi huko nje hazikusikika, na baada ya dakika chache, mlango ukafunguliwa, na sasa aliyeingia sio yule kijana, alikuwa ni mtu mwingine..


NB: Ni nani huyo..JAMANI LEO NIMETINGWA SANA NA MAJUKUMU, LAKINI KWA KUWAJALI NIKAONA SIKU ISIPITE HIVI HIVI..

WAZO LA LEO: Wakati mwingine ukweli ukisemwa kwa papara unaweza ukaleta maangamizi, badala ya kusaidia, na kila jambo huwa halitaki papara, tuweni makini sana kuzitumia ndimi zetu, kwani ndimi zinaweza zikawa silaha kubwa zaidi ya bomu la nyukilia. Wenye hekima wanaona ni vyema kukaa kimia kuliko kuongea maneni yenye kuumiza wengine, maneno ambayo hayatakuja kujenga bali ni kubomoa.


Tunaweza kujiona ni washindi wa kuongea, kutukana kudharau, kukebehi, na kuwazalilisha wengine kwa maneno ya kashfa, bila kujali hata umri wa tunayemfanyia hivyo,…jamani tujihadharini sana, kwani ulimi utatupeleka pabaya, ni heri kukaa kimia kuliko kuongea kama unachoongea ni kauli yenye ubaya na dharau  ndani yake. Hala hala sisi tunaotumia mtandao, kama vile tupo kijiweni, tunaandika tu bila kujua madhara yake baadae,..halahala jamani, wenzetu wengine walifikia kuuana kwasababu ya haya haya, na ushahid mmojawapo ni maandishi, ..chungeni sana maandishi yenu..tuache ulimbukeni wa kuandika kama tunavyoongea mitaani…, kwani maandishi ni kauli yako kwa lugha nyingine, yatakuja kukuhukumu wewe mwenyewe.
Ni mimi: emu-three

No comments :