Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 5, 2017

DUWA LA KUKU....6


‘Haya, sasa jiandae uje kuna maongezi, nataka uje uelezee kila kitu, ukinificha, basi shauri lako, ..yatakayokutokea usije kunilaumu..mimi nawafahamu sana hawa wanaume, ..unanisikia, mimi nataka nikusaidie wewe haya yasije kutokea tena…unanielewa…, kwahiyo sema kila kitu kinachotokea humu ndani, na kama uliwahi kufanyiwa jambo lolote na mume wangu, uliongee, huu ndio wakati wako…’

Hiyo ilikuwa kauli ya mama mwenye nyumba

.Unasikia,….uwe makini na kauli zako, mama ni mjanja sana, anatafuta njia ya kumuona baba ana makosa, nina uhakika kuwa baba hana makosa mimi namfahamu sana baba yangu, na ikithibiti kuwa kuna kitu kinahusiana na baba, na mama akasikia kutoka kwako,…utavuruga ndoa yao,…na hapo hutapata mtetezi tena, baba ndiye mtetezi wako, na alipanga mambo mengi ya kukusaidia....'alinionya huyo kijana

Niliwazia hayo...na kunifanya niwe njia panda...

Tuendelee na kisa chetu...


****************

 Nilifika kwenye hicho kikao nilichoitiwa, nilijua labda ni hao wanandoa wawili na mimi mwenyewe, lakini humo nikawakuta wazee wawili,….niliambiwa mmoja ni mzazi wa baba na mwingine ni baba mkubwa wa mama, wenye nyumba.

 Baadae yule kijana alikuja…kama nilivyosema huyu alikuwa na umri karibu sawa na mimi,kama kanizidi mimi ni kidogo tu…huyo kijana alipoingia, kwanza aliwatupia macho hao wazee, halafu akanigeukia mimi na kuniangalia kwa mashaka, kama ananionya kuhusu jambo fulani, mimi sikumjali, dhamira yangu ilikuwa kusema ukweli tu, sikutaka kudanganya tena, ila kwa mbali akilini nikawa nakumbuka onyo la huyu kijana..

‘….na uwe makini na kauli zako, mama ni mjanja sana, anatafuta njia ya kumuona baba ana makosa, nina uhakika kuwa baba hana makosa mimi namfahamu sana baba yangu, na ikithibiti kuwa kuna kitu kinahusiana na baba, na mama akasikia kutoka kwako,…utavuruga ndoa yao,…na hapo hutapata mtetezi tena, baba ndiye mtetezi wako, na alipanga mambo mengi ya kukusaidia…’

Nilijiuliza kwanini huyo mama anatafuta makosa ya mumewe, ili ndoa ivunjike…au sikumuelewa vyema huyo kijana, ….na kwanini ukweli wangu uje uvunje hiyo ndoa, sasa nifanyeje, niseme ukweli au nikae kimia, na je ikijulikana kuwa mimi nasema uwongo,….hapana, mimi nitafuta ushauri wa mama yangu, mama yangu wakati wote aliniusia kuwa mkweli…hata kama ukweli huo utaniumiza.

Nilisalimia kwa adabu halafu nikaambiwa nikae , nilikaa sehemu ambayo naangaliana uso kwa uso na huyo kijana, nilimuona akinitupia jicho la aina yake, na mara nyingi alikuwa kainamisha kichwa chini.

' Haya tuambieni mlichotuitia…’alianza mzee mmojawapo., na baba mwenye nyumba ndiye akaanza kuongea;

'Wazee wangu, samahani sana, imebidi niwaite,..nilishawaita kabla lakini tukaweza kuyamaliza wenyewe, ila hili la sasa limeshindikana…nikaona ni bora, niwasumbue…lakini hata hivyo, nyie ni wazazi wangu, mara nyingi matatizo ya kifamilia yakifikia hatua mbaya, ni lazima tuyafikishe kwenu kuliko kukimbilia mahakamani kwanza….ili muweze kutusaidia…’akaanza kuongea na wale wazee wakatikisa kichwa kukubaliana, lakini hawakusema neno.

‘Wazee wangu ndoo yangu imeingiliwa na matatizo….’akasema na kumtupia mkewe jicho, mkewe alikuwa kaangalia pembeni.

 'Sawa, kuna tatizo gani…tuambie…’akasema mzee.

 ' Mke wangu haniamini, kafikia kunishuku ugoni, na hata kunitaka tuachane, kwasababu za kunishuku tu, hana ushahidi, maana sio kweli kwa hayo anayonishuku nayo….’akasema.

 'Hilo tu…?’ mzee akauliza na baba mwenye nyumba akamuangalia huyo mzee kwa macho ya kushangaa, na kutahayari, akasema;

 ' Wazee, hilo mwaliona ni dogo, ..jamani, mpka nimeamua kwuaita mjue kuwa mimi nimeshindwa kumshawsihi mke wangu, kang’ang’ania kuwa tuachane….na kuachana huko anataka mimi niondoke kwenye hii nyumba…’akasema.

'Mimi nimeuliza kama kuna nyongeza ya hilo,nikitaka ufafanuzi zaidi, sina maana ya kuliona hilo jambo kama jambo dogo, udogo wake na ukubwa wake, unategemeana na maelezo yenu, maana hata sisi tumepitia huko…’akasema mzee.

'Mengine ya ziada ni kiwa mke wangu kwa hivi sasa haniheshimu kama mume wake, amekuwa akitafuta mwanya wa kunichafulia heshima yangu….na kunidharau, sawa, mimi..labda kwa vile hii nyumba tumepewa na wazazi wake, ..lakini tulikubaliana na wazee wakaridha kuwa hii ni nyumba yetu sote, sikulipinga hilo nikijua haya ni maisha yetu ya mume na mke…’akasema.

'Labda tuanza kulidodosa hili jambo, maana naona utakimbilia kutoa maelezo mengine ambayo hayayaweza kuleta suluhu, nikuulize kisa hasa nini nini..ndio huko kukushuku, kwanini akushuku, kuna tukio lilitokea, au …?’ akauliza.

 'Labda tumuulize yeye ambaye ananishuku mimi….’akasema baba mwenye nyumba, na mzee akasema;.

 'Kabla ya kumuuliza yeye…sisi kwanza tunataka tukukabili wewe baba mwenye nyumba, na kwa vile wewe ndiye umefikia kutuita sisi, yeye, atakuja kuulizwa, lakini kwanza tunataka kusikia kutoka kwako wewe, kichwa cha familia..swali  je ni kweli, kuhusu shutuma hizo…?’ akaulizwa.

'Sio kweli wazee wangu, ndio maana nikaziita shutuma, ni hisia tu, na sijui kwanini anafikia kunishuku hivyo….’akasema.

 'Je mke wako kwa bahati mbaya, aliwahi kukufumania ukiwa na mwanamke mwingine…?’ akaulizwa na akamuangalia huyo mzee kwa uso wa kujiuliza ni kama vile anahisi mzee anamkandamiza, lakini huyo ni baba yake mwenyewe.

 'Hapana,..hiyo haijawahi kutokea,…ndio maana nashindwa kumuelewa…’akasema.

 'Sasa ilitokeaje mpaka akafikia kukushuku…maana yeye sio mtoto mdogo, kuna sababu kakuambia, au hamjawahi kuliongelea hilo…nakuuliza hili nikiwa na maana mpaka, wanandoa wanafikia hatua ya kuwaita wazee, ni lazima wameliongea, wakazozana, wakawa hawaweze kuafikiana, na katika kuzozana huko ni lazima mwenzako atakuwa kakuambia …na hata kukutokea ushahidi wake, au sio mzee mwenzangu…?’ akasema huyo mzee.

Mzee mwenzake, akatikisa kichwa kukubaliana na maneno hayo.

 'Kuna matukio yalitokea, yeye akanihisi vibaya, lakini kiukweli sivyo hivyo kama ilivyoonekana…’akasema.
'Ilikuwaje..tuambie, maana kama mumetuita, basi tunahitajia ukweli wote…’akasema huyo mzee.

'Kwa tukio la hivi karibuni ambalo limevuka mpaka,…mimi nilirudi nyumbani na kumkuta mdada wa kazi akiwa kapoteza fahamu….’akasema na sasa aliyeuliza ni huyu mzee mwingine.

'Kapoteza fahamu…!!, kwa vipi…hebu tuelezee hapo…’akasema huyo mzee mwingine.

'Nilimkuta kalala sakafuni akiwa hajitambui, …akiwa kapoteza fahamu….’akasema.

'Oh, kwanini awe hivyo, labda mnajua sababu yake, na je hiyo ni ara ya kwanza kwa tukio kama hilo..?’ akaulizwa.

 'Mhh, kuna kipindi ilitokea hivyo, na aliyekuwepo, na kumuona ni mke wangu, na wakawahi kumpeleka hospitalini….’akasema.

 'Kwani huyo bint ana tatizo gani hasa…?’ akauliza.

 'Hicho kipindi alipodondoka, na kupelekwa hospitalini walimpima na wakagundua kuwa aalikuwa na malaria,ana malaria hiyo ilikuwa imepanda kichwani….’akasema.

‘Kwahiyo wewe ulipomkuta kapoteza fahamu hukutaka kumpeleka hospitalini au…?’ akaulizwa

 'Kwanza ukimkuta mtu kapoteza fahamu si unatakiwa umkague, na kumpa huduma ya kwanza, si ndio hivyo wazee wangu…’akasema.

‘Kwahiyo wewe uliamua kumkagua kwanza kama ulivyosema awali….na ulipomkagua ukaona haina haja ya kumpeleka hospitalini au ulifanyaje..?’ akaulizwa.

 'Nilimkagua ndio nikahakikisha kuwa kapoteza fahamu…na ndio nikaanza kumpatia huduma ya kwanza…’akasema.

 'Ulifanyaje…?’ akaulizwa, wazee hawa ni wasomi, kwahiyo maswali yao yalikuwa ya ujanja ujanja, jamaa wakati mwingine aliona kama wazee hawa na wao wanamshuku vibaya, hata hivyo aliendelea kuwajibu bila kukasirika.

‘Kwanza nilimlegeza khanga aliyokuwa kajitanda mwilini….’akasema.

‘Kwanga, kwanza alivaaje, maana ukisema khanga, …..ok, alivaaje,…?’ akaulizwa.

 'Mhh,… alikuwa kafunga khanga moja, ile unafungwa shingoni, na kufunika mwili mnzima.

'Kwanini akawa kavaa hivyo, ina maana alivaa khanga moja tu, …bila kitu kingine, ndio kawaida yake au…?’ akauliza huyo mzee kwa mashaka.

 'Hilo la kwanini, mimi siwezi kujua, labda atajieleza yeye mwenyewe….’akasema akimtupia mke wake macho, hakumuangalia huyo binti.

 'Kwahiyo wewe ulifanyaje….ulipomkuta huyo binti kapoteza fahamu baada ya kumkagua…?’ akauliza mzee.

‘Ina maana mnataka niongee kila kitu, mengine naona kama hayana umuhimu ….’akalalamika

‘Kijana, mwaneti, sisi ni wazee wako, tuna maana kubwa ya kukuuliza haya, fununu za hayo yanaytokea humu ndani tumeyasikia sana tukayapuuzia, sasa tunataka uyajibu maswali yetu, …kwani kuna ubaya ukituelezea…?’ akaulizwa.

 'Kwasababu alikuwa kapoteza fahamu, muhimu nijuavyo mimi ukimkuta mtu wa namna hiyo cha kwanza ni kumlegeza nguo alizovaa, kama zinambana, kabla ya kumfanyia huduma ya kwanza….’akasema.

 'Umesema huyo binti alikuwa kavaa khanga moja, na khanga tujuavyo sisi ni nguo nyepesi sana, je ilikuwa inambana, …..?’ akaulizwa.

 'Ndio kwasababu, ile kanga alikuwa kaifunga shingoni, huoni itakuwa imekaza mishipa ya damu shingoni..’akasema.

 'Haya,bwana, halafu..ukaifungua shingoni, na kumuacha uchi au…?’ akauliza na hapo akacheka ile yakuonyesha anakerwa na hayo maswali.

‘Hakubalia uchi, ililegea kwenye ule mkunjoa wa kufungwa shingoni,…..’akasema

‘Kwahiyo ukamaliza au ulifanya nini tena…?’ akaulizwa

 'Nikamminya kifuani, mara moja, …mbili….na tatu…ili kurudisha mapigo yake ya moyo…’akasema

'Ok, huo ni utaalamu, unajua wewe,….hebu tukuulize tu, huo utaalamu wewe ulijifunza wapi..?’ akaulizwa

 'Huduma ya kwanza, nilijifunza chuoni…tunafundishwa, hata vitabuni ipo, kwenye mitandao ipo, ni kitu cha kawaida tu….’akasema.

 'Kifuani kulikuwa wazi…maana mfano khanga ikifningwa hivi, ukaifungua huku singoni, si inaacha kifua wazi, na kwa vile alikuwa hajavaa nguo nyingine ni …..atabakiwa huku wazi, au sio…?’ akauliza mzee.

 'Mzee hakubakia wazi, alikuwa kavaa khanga..kanga ilimfunika….’akasema.

 'Khanga tu, hakuvaa sidiria…hata sidiria….’akasema mzee.

'Wazee, mbona mnauliza maswali hayo…mimi sioni kama yatasaidia….’akalalamika.

 'Mwanetu, sisi sio watoto wadogo, tunakudodosa tujue ukweli ulivyo, huyo ni mdada, mwili wake wote unatia hamasa kwa mwanaume, katika maelezo yako hatukusikia neno, kuogopa kumgusa,  nay eye kuna maelezo alimuelezea mama yake,…je hukumguza zaidi ya kumminya kifuani mara tatu, maana labda tutasema aliota…’akasema huyo mzee, na jamaa akamtupia mkewe jicho, lenye kuonyesha chuki fulani.
 'Mzee, huyu ni sawa na bint yangu, namuona kama mtoto wangu, na kwa hali niliyomkuta nayo, nisingeliweza kuwa na mawazo kama hayo mabaya…sijui kawaambia nini, au mke wangu kawaambia nini,…lakini mimi nilifanya kile kilichokuwa ni sahihi….’akasema sasa kwa ukali kidogo.

 'Je ungemkuta yupo kwenye hali tofauti, ungefanyaje..labda kavaa kahanga moja kama hivyo, kama hujawahi, maana kama alivaa hivyo, yaonyesha ni kawaida,…au sio, …?’ akaulizwa.

'Mimi kama mzazi, ningelimkemea kuwa haifai kuvaa hivyo, na mimi sijawahi kumuona akiwa kavaa hivyo kabla….’akasema.

 'Je ni mara ya ngapi umemkuta,akiwa katika hali kama hiyo…..?’ akaulizwa
 'Una maana gani mzee, unajua wazee, mimi huwa natoka asubuh, narudi usiku, huwa nipo nyumbani siku za wikiendi tu na mara nyingi, siku kama hizo, mke wangu yupo….’akasema.

‘ Ni mara ngapi...hivi umeelewa swali..?’ akaulizwa.

 'Sikuweza kujua hilo, kifupi, sijawahi kumuona akiwa katika hali hiyo kabla…, hiyo ni mara ya kwanza kwangu akasema na mkewe alionekana kutikisa kichwa kama kusikitika kuashiria kuwa mumewe anadanganya..
 'Una uhakika na hilo, je ukitolewa ushahidi kuwa hiyo sio mara ya kwanza kumuona hivyo utasemaje..?’ akaulizwa
 'Mzee…..’akataka kulalamika na mzee hakumpa nafasi, akamuuliza.

'Hilo tuliache, nikuulize, japokuwa hili ni swali la nyie wote wawili, ni kwanini ulimkuta huyo binti huko chumbani kwenu…?’ akaulizwa, na kwanza akamtupia mkewe jicho, kama kutaka kumlaumu lakini akaona mkewe hamuangalii, akasema;

 'Labda alikuwa anafanya usafi…’akasema

‘Labda, huna uhakika…kwahiyo yeye huwa anafanya usafi hadi chumbani kwenu, anatandikia, ana…panga nguo zenu,..si ndio hivyo…?’ akaulizwa.

 'Mzee kwani hapo kuna ubaya gani, huyo ni kama binti yangu tu, yupo makamo sawa na huyu kijana hapa..kwahiyo hata akiingia akafanya usafi, kwangu mimi sioni kuwa ni tatizo…..’akasema.

'Hahaha,…mwanetu…. eti unasema nini,…kuwa hilo sio taizo, labda niseme kwangu mimi na uzee wangu huu, na kwa mila na desturi, na…hata ukiangalia, kiuhalisia, na kiubinadamu , hilo kwangu ni tatizo, huwezi kumruhusa mfanyakazi wa ndani, kufanya usafi hadi chumbani kwenu, huko ni sehemu ya siri kati yenu wawili, hamjafundishwa hilo jamani, mtasema mnaishi kidhungu au sio…mwanetu, hilo ni kosa, …sisubirii kulisema huko mwishoni..hilo ni kosa..na adhabu yake ndio hiyo…’akasema.

 'Mzee..adhabu gani…?’ akauliza.

'Msijitetee, mambo mengine mnajitakia nyie wenyewe..mimi hilo naliwekea alama ya kuuliza, nyie wananda mna matatizo, kama mumeiga,, kama mlifanya hivyo, kwa vile mnamuona huyo ni sawa na binti yenu,…lakini sio binti yenu huyo ndio maana hayo mengine yalitokea,….’akasema mzee

‘Mengine yapi mzee…?’ akauliza sasa akionyesha mashaka.

‘Mzee mwenzangu unasemaje kuhusu, wewe unona ni kawaida kumruhusu binti wa ndani afanye usafi ndani, chumbani, atandike,…na kuvaa kwenyewe ndio huko…hivi kweli mna akili nyie…’mzee akasema kwa hasira.

 'Mhh, hata mimi najiuliza, labda ndio usasa huo…na madhara yake ndio hayo, na watu hawataki kujifunza, wanaiga tu,….kiukweli sio sahihi, …’akasema mzee mwenzake.

 'Haya ulipomshika kifuani, ukakandamiza , mara tatu, halafu ikawaje…?’ akauliza huyo mzee sasa akicheka.

'Mzee naona mnielewe, kama hili mwalichukulia mzaha, mimi ….’akasema

‘Mwanetu, hatukuja kupoteza muda hapa, sisi tunataka kuwaonyesha madhaifu yenu, ili mjifunze, msione sisi wazee tulikuwa tunafanya hivyo, tunayajua hayo sana, binadamu ni mdhaifu, nafsi ni kitu kingine,..msiige tu bila kujua madahara yake…..’akasema huyo

‘Haya atujibu Sali letu, hapa sasa mpo mahakamani, mnatakiwa mjibu maswali kama yanavyoulizwa, sisi ni wazazi, hata kama mumezaa mna watoto wakubwa, lakini mkiwa mbele yetu, nyie ni watoto tu…’akasema huyo mzee.

‘Hakuzindukana…’akasema sasa akiwa katahayari.

 'Ukafanyaje ulipoona hakuzindukana…?’ akaulizwa.

'Mzee, kuna huduma ya kumpuliza mdomoni..kama hiyo ya kifuani haikufanya kazi….’akasema
'Ehee..haya makubwa hayo, ya mdomoni...!!..’akasema huyo mzee, wazee hawa wawili wakaangaliana.

'Ndio mzee, kwahiyo hayo si yanajulikana jamani….’akasema
'Kwahiyo ukaifanya hiyo, au sio…?’ akaulizwa.

'Hapana mzee..sikufanikiwa kuifanya….wakati najiandaa kuifanya hiyo, ndio mke wangu akatokea,…..’akasema kwa sauti ya kunywea kidogo.

‘Ukaacha kuifanya hiyo huduma, kwanini sasa….?’ Akaulizwa

'Ndio nikaacha kwasababu….’hakumalizia.

'Kwanini uliacha na wewe ulikuwa ukimuhudumia mgonjwa, hebu nikuulize docta akamuhudumia mgonjwa, je akitokea docta mwenzake ataicha hiyo kazi, kwa vile mwenzake katokea…?’ akaulizwa.

 'Nilisita,kwa jinsi mke wangu alivyoniangalia, macho yake yalionyesha kuhisi vibaya, yalimtoka kama vile kani..’akasita kumalizia.

'Malizia..hilo neno ni muhimu sana tukalisikia…’akaambiwa.

'Ni kama kaona kitu cha kutisha vile….na mimi nikashikwa na mshangao, kwanini ananiangalia hivyo….’akasema

"Ni kama vile kakufumania au sio...?" akasema huyo mzee

'Nahisi hivyo..lakini sio kweli….’akasema

'Kwanini akuhisi hivyo, kwani alikukutaje, ulikuwaje, wakati unafanya hayo…?’ akaulizwa

 'Mimi Sijui kwanini alionekana kuniangalia hivyo, na hakunipa nafasi ya kujieleza…’akasema

'Hebu nikuulize wakati unamfanyia huyo mdada huyo huduma ulikuwa umekaaje…?’ akaulizwa

 'Mzee kwa vyovyote nitakuwa nimepiga magoti, nimemuinamia….ningafanyaje ..?’ akaulizwa

‘Kwanini ulivua shati, …?’ akaulizwa na hapo akashtuka.

‘Mzee hapo ni chumbani kwangu,….nilipofika nilivua shati, nilihisi joto, na nilitaka nibadili nichukue jingine nilivua hilo hata kabla sijajua kuwa kuna mtu humo ndani…..’akasema.

‘Una uhakika kuwa ulimshika kufuani, tu ukambinya mara tatu tu….maana ukumbuke hilo tendo, hukulifanya ukiwa peke yako, kuna watu walikuona, na mtendewa mwenyewe …unajua..mwanetu, humu ndani kuna tatizo,….mna mataizo makubwa, mpaka sisi tunakubali kufika hapa, mjue kuna tatizo, na sio wajinga sisi kukuuliza maswali kama hayo….sasa kabla hatujaanza kumuhoji mkeo, ..kabla hatujaanza kumuuliza binti, na kabla hatujawaleta mashahidi kuwa..hapa ndani kuna tatizo, nakupa nafasi ya mwisho.

‘Mzee, unataka kusema nini, kuwa mimi …’

‘Mimi ni baba yako, nimekuzaa mwenyewe, na haya yaliyotokea humu ndani yalilifika hadi kwangu, awali nilikutetea sana maana sivyo nilivyokulea hivyo , na sikuamini nilipoambiwa hayo, nikataka kutafuta ushahidi, na..nimekuhoji maswali hayo nikiwa na maana…kijana, mimi ni baba yako nimemuangukia mzee mwenzangu ili haya yaishe,..lakini yataishaje kama hujauangama…ukakiri kosa yakaisha…

‘Baba….’akawa kakasirika sasa.

‘Nataka wewe ukiri ukweli, useme ukweli haya yaishe, mwenzako kasema ukikiri ukweli, yupo tayati kukusamehe, lakini kama utaendelea kuwa mkaidi, na wakati unajua ulitenda kosa, na yaliyashatendeka awali akakusamehe, …sasa ni mara ya pili…mimi nitanawa mikono, nimekudhamini kuwa wewe utasema ukweli na kukiri kosa, sasa nakupatia nafsi hiyo ya mwisho kabla hatujamuuliza bint ambaye ndiye mtendewa, najua ataelezea yote yaliyowahi kumtokea, na hilo, ulipojifanya unamfanyia huduma ya kwanza,..na kuna mashahidi wengine…..’akasema huyo mzee.

‘Mwanetu, hebu fikiria hivi, wewe haupo duniani, una binti kama huyu, anafika kwenye nyumba za watu wanamfanyiwa mambo kama hayo..utajisikiaje…, hebu liweke akilini hivyo. Maana usiseme kwako haiwezi kutokea, mungu ni wajabu sana, wangapi walikuwa wanahali nzuri sana, lakini sasa wapo mitaani, wangapi walikuwa na hali nzuri, walipofariki, wakawaacha nyuma wanafamilia, wakaja kufirikisika hadi kufikia kuwa omba omba..hawa waliomba..hapana,…hii inaweza kumtokea yoyote, …liwazie sana hilo mwanangu…’akasema mzee

‘Kama unaona sio kweli, tutaanza kuitisha mashahidi…na hapo sijui utasemaje,…maana nimesikia mengi,..kuna binti alikuwa hapa awali, ilitokeaje,…utasema ni uzushi….ee , na huo ni uzushi…nakuuliza wewe….?  mwanangu ndivyo nilivyokulea hivyo, kuna tatizo gani….sasa ni muda wa kuniambia ukweli, kama umeniita hapa kuja kuikoa ndoa yako, sasa nahitajia ukweli, na…huyu binti wa watu apate haki yake, sipendi watu kama hawa wateseke, eti kwa vile masikini….je upo tayari kuusema ukweli…na …’akatulia.

Baba mwenye nyumba akageuka kumuangalia kijana wake, halafu binti, kwa mara ya kwanza akamuangalia huyo binti,…sasa akiwa kakunja uso kwa hasira, baadae akainamisha kichwa chini, na alipoinua machozi yakawa yanamtoka…huku uso umejaa hasira.

NB: Imebidi niliweke hili hivi…ili kufunua ukweli wa maisha katika familia.


WAZO LA LEO: Ili uishi kwa amani,…jitahidi kuepuka,..kuweka visasi moyoni, kupenda kulalamika-lalamika, kulaumu wengine…, kufanya mambo kwa vile umefanyiwa, wewe fanya mema vile itakiwavyo bila kujali kuwa na wewe umefanyiwa au la…maana kufanya hivyo, kuna neema yake, kuliko kutokufanya, na ukifanya kwa vile umefanyiwa hiyo ni ria, na ria ni shrike ndogo,…wewe fanya ukijua ni wajibu wako, na Mola atakuzidishia baraka kwa kujitolea kwako kwa mema unayoyafanya.
Ni mimi: emu-three

No comments :