Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, July 29, 2017

DUWA LA KUKU...24


‘Huyo mtu hana kitu tana..., nimeshauchukua mkoba wake ndio maana anatapatapa, haniwezi tena…..’

Wale akina mama wakaangaliana na kunyosha mikono juu ya ushindi,

‘Sasa mzee, muda tuliopewa wa kukaa humu kwenye ofisi ya watu umekwisha, na tumeongea mengi, na mpaka hapa tulipofikia, umeshakiri kuwa wewe pamoja ya kuwa ni mganga wa kienyeji, lakini pia wewe ni mchawi, hilo halina mjadala…na huo mkoba wa uchawi mkuu unao wewe, kama ulivyosema hapa sasa hivi....’akaambiwa na yeye akabakia kimia tu.

Tuendelee na kisa chetu.

***************

‘Unajua wanadamu tunajisahau, na tunapofanya majambo tukafanikiwa tunajiona sisi ni washindi, tunasahau kuwa dunia hii ni ya kupita tu, wangapi walikuwa majbali, wachawi, wengine matajiri, watawala wenye nguvu..lakini sasa wapo wapi..nikujisahau tu…’akasema huyo mama.

‘Sasa ndugu yangu kwa ushauri, kama ulivyosema awali, wewe una shida na sisi pia tuna shida,..lakini shida zetu chanzo chako ni wewe…usilikatae hili kupoteza muda, kama utazidi kubisha sisi tutaingia kwenye sehemu nyingine ambayo haitakuwa nzuri kwako, hilo tuna uhakika nalo, sio kwamba sisi tumekuja hapa hivi hivi tu, sio kwamba tunafanya haya tukikisia tu, hapana….’akasema na jamaaa akaendelea kukaa kimia.

‘Kuingia kwenye majumba ya watu kwa namna yoyote ile bila idihini ya wenyewe ni makosa,utasema ni nani aliniona kwasbabu umefanya kwa njia ya uchawi, usiku watu wamelala, huonekani,…na nikuambie kitu,.uchawi japokuwa kwenye sheria hakuna namna ya kuithibitisha, lakini matendo yake yanaweza kuthibitishwa, kama yataonekana jinsi gani yanavyoathiri jamii, unawafanya wengine wasiishi kwa amani, kuna mauaji, kuna madhara ya kuumiza wengine wakawa wanaumwa, ..sasa hayo yakifika mbele ya sheria ni makosa makubwa.

‘Umesikia hata kwenye vyombo vya habari, kuna watu wanajiita ni waganga, lakini kazi yao kubwa ni kuwapotosha watu, wanafanya mambo ya kichwai, ushirikina mtupu...wao wanasema kuwa wanaweza kuleta utajiri, lakini waangalie hali zao, kama wanaweza kufanya hivyo kwanini wao wasiwe matajiri, kwanini ili waifanye hiyo kazi mpaka walipwe, yeye atakuwa na shida gani kama aweza kutengeneza huo utajiri.

Watu hao wamefikia hatua mbaya, ya ku-ua, wanaua, wanadamu wenzao, kwa imani hizi za kishirikina, iweje miili ya watu itumike kuleta utajiri, kama miili yao inegkuwa ni sababu ya utajiri mbona hao watu wanaouliwa sio matajiri, ni mtu kufikiri tu, ngozi kuwa tofauto ni madhara ya kimaumbile tu, angeliweza kuwa mweusi, au mweupe, lakini ni viasilia vimekosekana tu, …hao wachawi wanatumia utofauti huu kuwapotosha watu,..

Haya kuna hao wanaosema wanaweza kuvuta mapenzi, lakini yeye mchunguze kwenye ndoa yake, hana mapenzi na mke wake, hana maisha mazuri na familia yake, au hana familia kabisa, sasa kwanini yeye alishindwa kwanza kujitengeza mwenyewe,…ipo mifano mingi kadha wa kadha…ukichunguza watu wa aina hii, kazi yao umegubikwa na utapeli tu, tamaa za kidunia, ya kuwapumbaza wengine wenye uoni hafifu wakubali na kufanikisha malengo yao…ambayo kifupi ni ushatani tu.

‘Sisi hatutaki kufika huko, kukufikisha wewe mbele ya sheria, maana awali ulitaka kujua sisi tutafanya nini kama hutatii masharti yetu hayo….hatua nyingine ni wewe kufikishwa mahakamani, lakini sisi tupo tayari, kumalizana na wewe kama utakubaliana na sisi, tumeshaongea na waathirika wa uchawi wako, wamesema kama utakubaliana na hayo masharti wapo tayari kukaa na wewe meza moja na kuyamaliza….’akaambiwa.

‘Hahaha, nyie watu, hao watu mumewajuaje,..na hivi, haya ..sawa, mimi nawasikilia tu…’akasema.

‘Muhimu kwako wewe kama wewe kumbuka jambo moja tu, kuwa hii dunia ni ya kupita tu,..hakuna atakayeishi milele, na mwisho wa yote tutarejea kwa mola wetu, aliyetuumba, na yale yote tuliyokuwa tukifanya huku duniani, yatahukumiwa, na hakimu wa mahakimu ..mola wetu, …

Sasa kama uliua, ulifanya madhambi mengi kwa siri, siku hiyo yote yatadhihirishwa, sote tukiona…na nikuambie kitu adhabu nyingine huanzia hapa duniani.. huwezi kumfanyia mtoto wa mwenzako madhambi, halafu mungu akuache hivi hivi..hutahukumiwa,kuanzia hapa hapa duniani.

Magonjwa mengine mabaya ni adhabu, licha ya kuwa mtu yoyote anaweza kuumwa, hata kama hana madhambi hayo, lakini wengine wanaumwa, kutokana na matakwa ya muumba, iwe kama adhabu, ili wamkumbuke mola wao , ili waweze kutubu dhambi zao..na watu hao wakitubu ukweli wa kutubu, na kumuomba mola wao, wanapona, wangapi tumewaona wakipona,…au hilo wewe hulijui…?’ akaulizwa

‘Mhh..’akaguna akijitizama mguuni, lakini hakusema neno.

Nimechukua muda huo kwa maelezo hayo, nia ni kukutanabahisha hili kwa mifano, ili unielewe, kabla sijafikia huko kwenye masharti yenyewe…’akaambiwa na yeye akabakia kimia tu.

‘Sasa je ndugu mpendwa, upo tayari kutubu madhambi yako…?’ akaulizwa, kwanza akacheka, na kutikisa kichwa,

‘Hahaha, unajua mimi nimekusikiliza sana, sio kwamba siwezi kupingana na wewe, lakini kama ulivyosema, muda umetutupa mikono, na lengo letu halijakamlika bado, nia ya nyie kufika hapa bado hutajaweza kufanikisha lolote, sijui nyie muelekeo wenu,..lakini,  sawa, mimi nipo tayari kusikiliza hayo masharti yenu, kama nitaweza nitayatimiza, maana kiukweli hata mimi nina shida,…’akatulia kwanza.

‘Sasa tunakusikiliza wewe…’akaambiwa

‘Nilikuwa nafikiria kwanza, maana umenigusa sehemu ambayo nashidwa hata nisemeje, ingelikuwa nipo mzina sina tatizo, ningekujibu kwa matendo..sikufichi, unajua nilifikia sehemu nikaapa, kuwa kw haya yaliyonikuta, yoyote yule atakayekuwa nyuma ya hayo atajibu, kwa mapigo makali…,..lakini nifanyeje sasa…’akasema sasa akishusha sauti kwa uchungu.

‘Kwahiyo kumbe ipo sababu kuwa yaw ewe kujiingiza huko kwenye uganga na uchawi…?’ akaulizwa, na hakujibu hilo swali, yeye akaendelea kuongea kuendeleza maelezo yake ya awali…

‘Kama ulivyosema yawezekana,….’akauangalia mguu wake, na huku anaongea,

‘Na sio yawezekana hata mimi nimeambiwa kuwa haya yote ni sababu na makosa yangu, sawa nimekubali kuwa na mimi nina makosa…, lakini mbona watu hawaangalii undani wa sababu za makosa hayo,mimi sio mnyama kihivyo, kunasababu,..lakini nani atakusikiliza kwa hivi sasa….’akatuli kidogo.

‘Sawa utakuja kutuambia, ili tukimbizane na muda, tuendelee na ajenda yetu…’akaambiwa

‘Sawa tusipoteze muda, niambieni mnataka nini,.?’ Akauliza akiwaangalia hao akina mama.

‘Sisi tunachotaka ni wewe kukubaliana na hayo masharti tutakayokupa, ili tuende sawa, au vinginevyo, maana sisi, tumeathirika, na uchawi, wako, kama ulivyotuthibitishia,…tuna haki ya kuchukua hatua nyingine ambayo hutaipenda..?’ akaulizwa

‘Niwaulize kwanza ni hatua gani hiyo nyingin, maana tusitishane, huruma yangu ndio iniponze, hapana, tusitishane, kabisa,…kwasababu kwanza, hamfahamu nikwanini haya yote yemetendeka,…hamjui, lakini nyie mumelichukulia hili swala juu kwa juu, na hamjui kabisa kuwa mimi nimejitokea kwa ajili yenu, vinginevyo ningelikaa kimia tu…’akasema akitikisa kichwa

‘Jamani hamjui tu, …hivi ni vita, na kwenye vita hakuna mcho tena, adui akiwa mbele yako pambana na kama kuna kikwazi cha kumficha adui kiharibu, jenga ukuta, jilinde, na uweke sababu za maadui kukuogopa, na kwanini nikae kimia wakati nafahamu kuwa napigwa vita,..walianza wao, acha na mimi nimalize, mimi sasa najibu mashambulizi, na sitakoma mpaka wasalimi amri, wasijiche nyuma ya pazia, mimi nawaona.. sasa ni mimi au wao…hapa sasa naona wameshashindwa sasa wana tapa tapa, na nyie mnatumika tu…’akasema

‘Mhh…unatufumba, kama ni vita, kama kuna sababu, hizo utakuja kutuambia, lakini kwanza tukubaliane kwa haya ili tuweze kumalizana kwa leo, tutakuja rasmi siku nyingine au tutapanga wapi pa kukutana kwa ajili ya utekelezaji, kwa yale ambayo hayataweza kutekelezwa haraka, ..’akasema mama

‘Sawa wewe yataje hayo masharti, mimi nitayasikiliza, na mimi nitayatimiza yanayowezekena kutimizika, mimi ni binadamu siwezi kuahidi kitu ambacho sijakisikia, je nikishindwa,…’akasema

‘Kushindwa huwezi, maana sisi tumeyapitia na kuyaona kuwa yapo ndani ya uwezo wako, ni utashi wako tu …muhimu ni wewe kukubali, na kutiikia, halafu kutekeleza…’akaambiwa.

‘Lakini mkumbuke kuwa mimi nipo hospitalini, mimi natakiwa kupata pesa za matibabu, mimi naumwa, kwahiyo vyovyote iwavyo, mnatakiwa mliangalie na hili pia, na hapa nilipo nimekwamba kipesa, nyie ndio wakunisaidia ili na mimi niweze kuwasaidia,….’akasema

‘Hayo yote yapo ndani ya  uwezo wako, tatizo ni akili yako imefungwa na maagano yenu, sio kwamba huwezi kujitibia, uwezo huo unao, labda ni kwasababu ya imani zenu, na mipaka mliyojiwekewa, huo ndio ukweli …’akaambiwa

‘Kwa vipi…hivi mnaniona mimi ni juha au, niwe na uwezo huo nisubiria nini, kufa…hapana, sina uwezo huo kwa sasa, na sina muda wa kurudi nyumbani na kuanza kufanya michakato mingine nimeshaambiwa na madocta..sasa labda mniambie nyie..kwa vipi?’ akauliza.

‘Kwanza ,ni kwanza…upo tayarii sasa kuyasikiliza hayo masharti, na ukishaanza kuyasikiliza, hatuna tena kurudi nyumba, ukija kukataa, sisi hatutajiuliza mara ya pili, hatua zingine zitachukuliwa, …na hapo utapambana na mkono wa sheria, hilo tunaweza na tumeshajipanga ikibidi, maana ushahid tunao, na mashahidi wapo…’akaambiwa
Hapo akatulia kidogo, halafu, akamuangalia mdada, halafu mimi, halafu akainama chini, halafu akasema

‘Sawa niambieni ni masharti gani hayo, nipo tayari kuyasikiliza…?’ akauliza, na kusema

****************

‘Ni masharti gani hayo?...umetuuliza, ikiwa na maana umeshakubaliana na sisi
Haya, sisi tuna nakala tumezichapisha,..zinaweza kurekebishika hatua kwa hatua, maana tuna nakala yake kwenye komputa zetu,…wewe unachotakiwa, kila kipengele kwenye ukurasa wake kuna sehemu yakuweka sahihi yako, nitatoa maelezo kila sharti, moja baada ya jingine ili uelewe, na uliza pale ambapo hutaelewa,..sawa..?’ akaambiwa

‘Sawa….nyie wasomi bwana, mpaka muandike, …hahaha, haya bwana, tuendelee..’akasema, na huyu mama akatoa bahasha kubwa, na kutoa nakala zenye maelezo , na kumkabidhi jamaa karatasi zenye maelezo,  na kutoa nakala nyingine na kuwakabidhi wengine, na alipohakikisha watu wametulia, akaanza kusema…

‘Kama unavyoona, kwanza kabisa tumeanza kuwa wewe umekubali makosa,…sawa ? yakuwa wewe umekubali kuwa umekosa, hilo ni sharti namba moja, …umekosa kwa vipi, maelezo hayo hapo chini, kuwa umekubali kuwa wewe ni mganga na pia wewe ni mchawi, na umekuwa ukiutumia uganga wako, kama sababu, lakini huku unafanya mambo ya kishirikina, je unakubaliana na hilo…?’ akaulizwa.

‘Hapana..sikubaliani nalo, siwezi kusaini, kitu kama hiki, kipengere hichi tukiruke, tuendelee na sehemu nyingine,..’akasema.

‘Mzee tunapoteza muda hapa, haya ni kwa manufaa yako, kwani baada ya hapa, tutakuwa sasa tunaanza kazi nyingine ya kuangalia jinsi ya matibabu yako, sasa tukiendelea kuvuta muda, hatutafika kokote, kukubali kwa kuweka sahihi, ni kitu kingine lakini kwa kauli yako umeshakubali, na ushahidi tunao,…’akaambiwa.

‘Huo ushahidi upo wapi…?’ akauliza na mdada akamuashiria mwenzake na kuanza kuwasha simu yake na jamaa akasikia jinsi alivyokuwa akiongea awali, alivyokuwa akiulizwa maswali na kuyajibu, halafu kwanza alitulia baadae akasema;

‘Nyie watu, ina maana yote hayo mlikuwa mnanitega, au sio…hahaha, huo kwangu hauwezi kuwa ni ushahidi hata mkiupeleka mahakamani, huo hauwezi kukubalika kama ushahidi mnajipotezea muda wenu bure..’akasema

‘Unajua ni kwanini tulikuuingiza kwenye hii ofisi, angalia pale juu, kile pale ni kifaa maalumu kinachochukua matukio yote humu ndani, tuliomba watuhifadhie, wanatumia kwa kazi zao, lakini kwa tukio hili, tutaweza kupata nakala zake, kwa ajili ya ushahidi…, sasa kama huu wa simu unauona sio ushahisi na huu wa video je, sas aunasemaje,…maana sisi hatujafikia huko …tuliona hili jambo halina haja ya kwenda mbele…ukikubaliana na sisi…..’akaambiwa

‘Nyie ni wajanja sana, lakini mtakuja kujuta…kwa hili, nyie hamnijui tu, huwa sijaribiwi….’akasema
'Una maana gani sasa, kwanini unatoa lugha ya vitisho, huo ni ushahid mwingine wa tabia yako…?’ akaulizwa na kuambiwa.

‘Sawa tuendelee…’akasema.

‘Kwahiyo kama umekubaliana na kipengele hicho weka sahihi yako hapo chini, …’akaambiwa, na kupewa peni,

‘Sikilizeni kwanza…mimi siwezi kukubali kuwa mimi ni mchawi, maana hamjui ni kwanini haya yalifanyika, kwanini tusiendelee na vipengele vingine, halafu tukimaliza kupitia vyote, ndio hapo, kama ni lazima tutafikia huko kwenye kuweka sahihi yangu, lakini mkisema mimi nikubali moja kwa moja kuwa mimi ni mchawi, hahaha, hivi mnaniona mimi ni juha, nisiyeelewa mambo eeh, hamnipati kwa namna hii…’akasema.

‘Lakini ulishakubali, au…?’ akaambiwa.

‘Kukubali, mimi, a wapi…hahaha, nikubali kuwa mimi ni mchawi, nani kasema hivyo….’akasema

‘Ulikubali kutokana na maelezo yako wakati tunakuhoji,….’akaambiwa

‘Mimi nilitoa maelezo hayo kwa ujumla wake…, kuwa waganga pia wanaweza kuwa wachawi, lakini sio kukubali kuwa mimi ni mchawi, sijaweza kufikia huko, msinifanye mimi ni mjinga…’akasema

‘Lakini wewe ni mganga wa kienyeji, au sio, na ulikubali kuwa mlikuwa mnafanya uchawi kwa kupma dawa zenu, mliweza kupambana na maadui zenu, na mliweza pia kufanya mambo ya kichwi ili kumshinikiza mtu akubaliane na matakwa yenu, hayo ulisema na kukubali, sasa …usitake turejee huko nyuma…’akaambiwa

‘Hapana msinifanye mimi ni mjinga, siwezi kusaini, nifanyeni mnalolitaka, hayo unaongeza wewe, mimi hapa sisaini, umenisikia, siwezi kufanya hivyo kamwe…’akasema

‘Kwahiyo wewe unatakaje…?’ akaulizwa

‘Mimi nataka hivi, tuyasome yote haya, na itafikia mahali nitajieleza, lakini kwanza tuyasome moja baada ya jingine ili mimi niyaelewe, lakini sio kwa kunitega, kila kipengele niweke sahihi hapana, hapa kuna mtego, na mimi siwezi kutegeka kirahisi, kihivyo…’akasema

‘Ok, sawa, sisi tutayasoma na maelezo kidogo, ..lakini tukifikia mwisho, kama utaendelea kukataa basi tutawaachia wenyewe serikali, wafanye kazi yao, na hutaamini kitakachofuata baadae, ukumbuke kuna watu wengi wameathirika kwasababu yako uchawi wako, wameshafika kutoka huko kijijini kwako,kwa ajili ya kutoa ushahdi, sasa ni wewe kukubali, na kutuachia sisi tuone jinsi gani ya kukusaidia, ili haya yaishe kwa amani…’akaambiwa.

‘Tuyasome …mimi sio kama mnavyonifikiria,…kuwa labda, mimi ni mchawi, hapana, haya yametokea kwasababu tu, mimi napambana na maadui zangu na nimfanya hivyo kwa madhumuni ya kujilinda, sasa ilitokeaje, mpaka ikawa hivyo… nitakuja kuwaelezea ikibidi… lakini kwanza nninataka kuyasikia hayo masharti yenu,…’akasema na kunitupia jocho mimi, halafu akaangalia kile kifaa alichoambiwa kina mumulika yeye na kuchukua matukio ya humo ndani

‘Sawa tuendelee, sisi hatuna shida, nia ni kukusaidia wewe…ambaye umeyataka haya…’akaambiwa

‘Hata mimi nia ni kuwasaidia nyie, nyie hamjui tu…’akasema

‘Haya tunarudia maelezo yetu,…kama tullivyoandika, ila hapo sasa tutarekebisha na kuandika hivi…

Kwanza ukubali ukweli kuwa kwa maelezo yako wewe, wewe ni mganga lakini pia umekuwa ukitumika kwenye uchawi…labda tuiweke hivyo, tutahitajia sababu zako, kwanini ulitumika hadi kufanya mambo hayo ya kichwai, sawa, hapo tupo sawa….’akaambiwa

‘Hapo kidogo tupo sawa, japokuwa bado mumenibana kiunjanja…’akasema

Utakuja kutuambia ni kwanini ulijiingiza huko hadi kufanya uchawi, ngoja kwanza tuendelee sehemu na sharti la pili, maana muda umekwenda…’akaambiwa.

‘Sawa…tuendelee…’akasema sasa kipiga miayo.

 Pili ukiri makosa yako uliyofanya, maana kama ulijihusisha na mambo ya uchawi, utakuwa ulifanya mambo mabaya mengi kwa watu mbali mbali, sasa ili toba yako ikubalike, tutahitajia toba yako kwanza kwa maneno, pili kwa vitendo,wewe ndiye unayewajua hao uliowafanyia huo uchawi, sizan kama utashindwa kuwakumbuka,..lengo hapa kama umewafanyia hivyo, utahitajika kuwatibia, …unaelewa hapo…’akaambiwa.

‘Ni ngumu….’akasema


‘Kwanini ni ngumu..?’ akaulizwa

‘Siwezi kuwataja wote, halafu, nitakwendaje kwa kila mmoja wao nianze kumwambia nilikufanyia hivi, sasa nimetubu, sasa nataka nikuponye, haiwezekani jamani…mnataka nipigwe, niuwawe…hahaha, mimi sio juha kihivyo…’akasema

‘Unaelewa maana ya toba, maana sasa unatakiwa kutubu madhambi yako…, kuwa hayo yaliyotokea huko nyuma hutarudia tena, si ndio hivyo..?’ akaulizwa

‘Hivyo sawa, …nitatubu sawa, …ni kweli kwa jinsi hali inavyokwenda nahitajika kufanya hivyo, kuachana kabisa na shughuli hizi, lakini sio rahisi kama mnavyofikiria nyie…’akasema

‘Shughuli gani , hebu fafanua hapo, kuachana na shughuli gani….?’ akaulizwa

‘Hizo za uganga ambazo wkati mwingine nahitajika kuwasaidia watu, au wale wanaotaka niwauzie, madawa ya kuwafanyia wengine uchawi, hayo nitaachana nayo kabisa, nikijiweka vyema, maana sio kazi rahisi,…’akasema

‘Na wewe je..maana na wewe mwenyewe ulikuwa ukiyafanya kwasababu zako au sio, sasa na wewe unatakiwa ukubali kuwa hutayafanya tena hayo mambo, muhim utuhakikishe kuwa wewe kama wewe, hutajishughulisha na uchawi tena,na wale uliowafanyia hivyo, utawatibia kuondoa huo uchawi wako kwao, ili usiendelee kuwatesa, na pia utakwenda kuwaomba msamaha kwa hayo uliyowafanyia….likifanikiwa hilo, nina imani watakusamehe, haina haja tena ya kwenda mahakamani

‘Hivi mnafikiri hilo ni rahisi hivyo, hebu fikirieni zaidi, hapana siwezi…’akasema

‘Sisi tutakusaidia, tumeshajipanga kwa hilo…’akaambiwa

‘Kwa vipi nyie mtanisaidia, haya sawa,…kama nyie ndio mtanisaidia kulifanya hilo, aah mimi sina kikwazo,…’akasema

‘Kukusaidia kwetu nikuwasiliana na hao watu, ukitutajia ni huyu na yule, sisi tuna watu wametoka huko, watashirikiana na sisi kuwasiliana na hao watu wengine, lakini ikija kwenye uwatibia, kuwarejeshea hali zao, kama uliwafanyia hiki na kile hiyo ni kazi yako…sawa…’akaaambiwa

‘Ndio hapo nasema hivi hilo ni gumu, halitawezekana kwa kiasi hicho…’akasema

‘Ugumu wake ni nini hapo, kwani wewe hutaki kupona, kwani wewe hutaki kuachana na madhambi yako, kwani wewe huogopi kuumbuliwa , kupelekwa mahakamani,…mbona wenzako wamefanya hivyo na sasa wapo huru…’akaambiwa

‘Akina nani wamefanya hivyo..…?’ akauliza, na huyo mama akaendelea kusoma maelezo;

 ‘Wewe unatakiwa uwaombe msamaha uliowakosea, japokuwa ni ngumu kama unavyodai,…, lakini wapo wengine tupo hapa, sisi pia ni wahanga wa uchawi wako,.. sawa? Kwahiyo wewe ukiri kwetu, kuwa ulitufanyia hivyo, na ututibie, na kutuhakikishia kuwa hutarudia tena, ….’akaambiwa

‘Kwahiyo , kumbe mnataka hivyo, wajanja kweli nyie…si simseme tu, kuwa ni nyie mnataka kutibiwa,.. kuwa hayo mazindiko yaliyofanyika kwenu yaondolewe, hahaha,  si ndio hivyo mnataka….?’ Akauliza

‘Kwani sio wewe uliyetufanyia hayo mazindiko,,…kwani sio wewe uliyewafanyia hawa madada wawili hadi wakafikia hapo walipo, nia ni kutokana na kumtaka huyo mmoja na alipokukatalia ukataka kumuonyesha kuwa wewe ni nani…kweli si kweli..?’ akaulizwa

Hapo akawageukia wale madada wawili, akakunja uso, kuashiria chuki fulani, halafu akasema

‘Najua hawa ndio sababu ya haya yote kwenu nyie…, sawa, mimi kwenu nyie nitajitahidi kufanya hivyo, nitatubu mbele yenu, kuwa nayfahamu hayo, … na nitawatibia, lakini …nawapa angalizo moja.., msifikirie ni rahisi hivyo…kwanini nasema hivyo…, kwasababu hayo mambo yanatokana na sababu nyingi kutoka huko nyuma, sio kwamba yamefanyika tu, kama navyofikria nyie, haya ni matokea ya historia, na mapambani kati yangu na hao maadui zangu …’akasema

‘Hizo sababu utakuja kuzisema, ikibidi tutapoteza muda mwingi, waakti tunahitajia haya mambo yaishe,..lakini kidogo kidogo, tujeshaanza kukuelewa, kuwa hufanyi mambo haya kwa matakwa yako, kuna sababau,…lakini muhimu ukubaliane na hili kuwa upo tayari, kutubu, kuwaomba masamaha uliowafanyia hivyo,..kuwaponya, na tutataka kusikia hizo saabu,  lakini tunaogopa muda, ila tukiwa hapa, ututibie uondoe huo uchafu wako kwenye majumba yetu, na uape kuwa hutarudia tena....’akaambiwa

‘Lakini hapo hapo na nyie mkubali kunisaidia pesa za matibabu yangu…’akasema
‘Hilo litakuja baadae, halina shida ..muhimu ni wewe uanze kazi hiyo…’akaambiwa

‘Sawa,…’akasema na hapo hapo akaweka sahihi kwenye kipengele hicho, na kusema,

‘Unaona kwa hili nimekubali na halina shida,..lakini sio hilo la kipengele cha kwanza, hilo mlitaka kunifunga hapana mimi sio mchaiwi, narudia tena, mimi sio mchawi, na haya yaliyotokea yana sababu kubwa sana, nitakuja kuwaelezea , ….’akasema

‘Sawa tuendelee na kipengele kingine…?’ akaulizwa

‘Sawa..ila hapa, nimeweka sahihi mapema, nilitakiwa tuendelee kusoma hadi mwisho,halafu ndio tuanze kazi ya kuweka sahihi…’akasema

‘Usijali, tupo pamoja…’akaambiwa
‘Nyie wajanja sana, hasa wewe, kiukweli sitakusahau, kwa hili aah, sijui…’akasema na huyo mama akasema

‘Usije kujaribu kuniloga tena, ..mimi nimefanya ubinadamu tu, ila ningeamua kukufanyia malipizo, usingeliweza kuinua mdomo wako, ogopa malipizo ya kunyanyua mikono juu  na kumkabidhi mwenyezi-mungu, usije ukalogwa, ukasema, ni duwa ya kuku tu, haiwezi kumpata mwewe, kama ulivyowahi kusema kumuambia huyo binti,... wewe…..ogopa duwa ya mwenye kudhulumuwa, unaona unavyoonza kupata taabu, kabla hujachelewa tubia,maana huijui kesho yako, utakuja kujuta muda umeshakwisha…’akaambiwa

‘Sawa nimekuelewa, ..si ndio hivyo tunaanza kuelewana,  mimi sio mbaya kihivyo, …’akasema

 ‘Sasa kwa vile kuwachawia watu wengine, kumeleta madhara, kuna watu wameathirika, mfano familia yangu, kumetokea mataizo makubwa, ushakubali kuwa unahusika kwa hilo na utaitibia, hewala,… lakini wapo hawa mabinti wawili,wapo wenzangu hapa, unatakiwa, uwatibie wote kwa gharama zako wewe mwenyewe,,,, kwa kuondoa hayo mazindiko yako, na uwahakikishie usalama wao, na ikibidi uwafidie..’akaambiwa.

'Wacha hiyo,…haiwezekani kabisa, kwa vipi..hapana hapo pa kuwafaidia kwa vipi, mimi sina pesa ..ningekuwa kwanini ifikie mahali pa kuwaomba mnisaidie hapana hapo hapana, hicho kipengele kigumu…’akasema.

‘Tutakirekebisha, hapo kwenye kufidia muda ukifika, si umesema tusome kwanza, hapa tunaweka alama kuwa kunatakiwa kurekebishwa, au turekebishe sasa hivi..?’ akaulizwa

‘Mhh…nyie ni wajanja sana, hebu endelea kipengele kingine…’akasema.

'Kipengele kingine kutokana na hayo madhara, kwa Mfano hawa mabint, huyu mmoja  sasa hivi ni mja mnzito, utuambie hiyo mimba imeingiaje mwilini mwake, maana ulisema hiyo mimba sio mimba ya kawaida, ni mimba ya namna gani wewe unajua hilo, sasa utafanyaje iwe mimba ya kawaida wewe unalijua hilo, lakini pia, wewe unajua ni mimba ya nani,,..maaana wewe ndiye ulifanya , ukasimamia, ukawepo vikifanyika,  na huenda na wewe umeshiriki kumzalilisha huyu binti wa watu…sasa hili nalo, ni sehemu ya masharti yetu…’hapo akakatiza na kusema

‘Hapana, mimi sijashiriki, kumzalilisha hapo napo kuna utata, ….wapo waliotenda, lakini sio mimi, sikutakiwa kufanya hivyo kabisa, ndio maana nilimtaka huyu binti nimuoe, sikutaka kumzalilisha, kama ningelitaka ningelifanya hivyo, naweza hapo sikatai… …’akasema

‘Ungeliweza kwa vipi, si kwa uchawi, au…?’ akaulizwa

‘Kwa namna ya madawa ya kumvuta, ukiita uchawi sawa, lakini sikutaka nikataka njia ya kawaida, akakataa, sijaendelea kumlazimisha…’akasema

‘Lakini ulimfanyia mambo, ma athari zake ndio hizi zimetupata na sisi…au sio…?’ akaulizwa

‘Yaliyotokea ni katika mapambano, muulizeni ni mimi peke yangu niliyemtaka kumuoa,….muulizeni labda hilo hajawaelezea, ndio maana nataka kuja kutoa maelezo zaidi, isije kutokea kuwa hayo katendewa na wengine na mimi natumbukizwa kiaina…’akasema

‘Ni nani mwingine alitaka kumuoa..?’ akaulizwa

‘Anamfahamu yeye, kwanini hamumuulizi yeye mwenyewe…’akasema

‘Wewe ndiye unatakiwa kuweka sahihi hapa tumalizane na wewe, maana kipengele hiki kinakuhusu wewe, tunaweza kuongeza kuwa wewe ulikuwa ukishindana na mtu mwingine katika kumpata huyu binti, au sio, sasa ni nani huyo, tuambie..?’ akaulizwa

‘Mimi siwezi kumtaja amtaje yeye mwenyewe, na kwa sababu hiyo kipengele hicho nacho kinahitajia marekebisho, kabla sijakikubalia…’akasema

‘Kwa upande wako wewe…tuache kwa huyo, wewe unajua huo ujauzito upoje umeshatuambia kuwa sio wa kawaida, kwa vipi, ukubali kulifafanua hilo, na ukubali kutuambia ulivyoingia, na utausawazishaje uwe uja uzito wa kawaida, lakini pia…ni nani walishiriki kwa mauchawi yako hadi wakampachika huo uchawi…utatuelezea, sawa….’akaambiwa

‘Hao,…watu, unataka niwataje, wewe unataka, ili iweje, huogopi kuwa itaathiri ndoa yako…’akasema

‘Kwa vyovyote iwavyo, wao hawakupendelea hilo, wewe ndio sababu, …’akaambiwa

‘Ndio maana nasema mengine yana ugumu kutoka na taaluma yenyewe, sitaweza kufanya kama nmnavyotaka nyie….’akasema

‘Utaweza, hili hapa ni lazima uweze, kama wewe ulifanikisha hili, ukaingia ndani kwangu, ukafany aulivyofanya, familia yangu ikahusika, nataka uwaelezee ni nani na nani,..na ilifanykaje, na ni nani alihusika..kama ni wao waanhsuiak na huo uja uzito, ninataka kujua,…’akaambiwa

‘Hahaha wewe…lakini nikuambie kitu, kwenye maeleo nitakayotoa, kwanini nilifikia huko, utaweza kuona kuwa haina sabbu yaw ewe kutaka kujua hayo, ila ukitaka, sawa…hata kama sio mimi niliyefanikisha hilo, ila kwa vile family yako imehusika, basi, nitakusaidia kuwataja…lakini sikupendelea iwe hivi, mbele ya watu hawa…’akasema

‘Sawa nimekuelewa, tutalirekebisha, kuwa wewe utanitajia nikiwa mimi na wewe, ..sawa, ili kuondoak hicho unachosita, mimi isogoi wakisikia, maana hawa ni wenzangu ni marafiki zangu, na tumeamua kulibeba hilo kwa pamoja..’akasema

‘Sawa, tuendeee…’akasema

‘Kwa hawa mabinti kuna kipengele cha gharama, na majukumu, maana sababu ya mimba hii ni wewe, sasa wewe ndiye utabeba hizo gharama, hadi kujifungua, huduma za mtoto, nk….na hilo tutakuja kuliweka vizuri, kuwa utafanya hiki na kile pale ukija kutuambia ni nani walioshiriki, na ni nani aliyempa mimba huyu binti, sawa…?’ akaulizwa

‘Hapo pagumu….’akasema

‘Kwanini…ni pagumu kwanini.., usipoteze muda hapa.., unaanza kunifanya nisikuelewe, kwanini ni pa gumu hapo, wewe hukuwepo wakati linafanyika, wewe hukulisimamia hilo, …ukahakikisha huyu binti wa watu anazalilishwa, huyu ana kosa gani na wewe, hebu tuambie, huyu ulimtaka na yeye akakukatalia, ni unyama ulioje ulioufanya…, hili litakufikisha kubayai usipokubaliana na sisi, na mimi nitalisimamia, hatua kwa hatu, unanielewa,.?’ Mama sasa akawa aoangea kwa ukali,

Jamaa akanitupia jicho mimi, na mimi nikawa namuangalia kwa uso uliojaa hasira, na kabla hajasema neno, mara docta akaingia na kumnong’oneza yule mama mwingine ambaye ndiye katumika kuongea na huyo docta, ilionekana kuna jambo.

Huyo mama aliyeongea na docta, akaja kwa huyu mama muuliza maswali akamnong’oneza kitu sikioni, na huyu mama muuliza maswali, akaonekana kuwa mashaka, …akatupa jicho kuangalia kile kifaa cha matukio, halafu, akatikisa kichwa kukubaliana na huyo mama, na kusema

‘Sawa….iwe hivyo, hatuna muda tena….’akasema, kitendo hicho sasa kilimfanya huyu jamaa awe na mashaka,…akaonekana kuwaangalia akina mama hao kwa makini, akatupa jicho kuangalia kile kifaa alichoambiwa kinachukua kumbukumbu za humu ndani, akawa anakuna kichwa kwa haraka haraka, na akaanza kuhema kwa kasi,..
Ilionekana jamaa hayupo vizuri…hali ikaanza kumbadilika,…..

NB: Kidole kinauma


WAZO LA LEO: Kuwatendea wengine ubaya, tunaona ni jambo rahisi sana, lakini kitendo kama hicho kikitokea kwako, kitakuumiza sana, swali ni kwanini ukaona ni rahisi kwa wengine lakini kwako ikawa ni maumivu, kama hivyo, kabla ya kuwatendea wengine ubaya, hebu tujaribu kujiuliza, je nikitendewa mimi naitarizika, hili litasaidia kutushtua tusiendelee kuwatendea wengine mabaya.

Ni mimi: emu-three

No comments :