Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 27, 2017

DUWA LA KUKU...22


‘Halafu ndio ukataka kumuoa huyu mdada, au sio,..? ‘akauliza na kubakia kimia, halafu akainua kichwa kumuangalia mdada, na kukunja uso, mdada atakatabasamu, na kutikisa kichwa kuashiria kuwa sasa mzee mzima kapatikana.

Sasa tuanzie hapo, usiogope tupo sawa, au…’ akaambiwa

‘Sawa tuendelee, tatizo, hayo maswali yako yanajirudia rudia kama kunitega…’akasema

‘Hapana, ni lazima nikuulize ili nikuamini, mimi hapa nawawakilisha wenzangu sitaki niwaangushe, umenielewa hapo,, swali langu ni hili…’akasema akimuangalia jamaa na jamaa naye akamkazia macho.

‘Je huyu mdada ulimuona wapi kwa mara ya kwanza, ukampenda..na hata kumtaka kumuoa?’ akaulizwa

‘Mhh, lakini,….’akatulia kidogo, halafu akasema;

‘Ok, sawa nitakujibu usije kuniona siwajali wateja wangu..’akasema

‘Sawa kabisa, haya tujibu…’akaambiwa

‘Kuna kipindi walikuja na …na.rafiki yake aliyemleta huko kijijini, unajua huyu alikuwa anaishi mjini na mama yake, waliondoka akiwa mdogo sana, kwahiyo huko kijijini kwa asili yao, hapajui, alipoletwa ndio nikamuona…’akasema

‘Kwahiyo kwa mara ya kwanza kumuona sio siku alipokuja kutaka kutibiwa..au sio?’ akaulizwa
‘Nahisi hivyo…’akasema akiangalia pembeni.

‘Aaah, jibu swali, wewe ni mtaalamu unajua mambo zaidi yetu, huwezi kuhisi unajua au hujui sema ukweli wako,…?’ akaulizwa.

‘Ndio kwani kuna taizo hapo mara ya kwanza nilimuona tu, nikaongea na rafiki yake, ili anitambulishe kwake, na mara ya pili ndio nikakukutana naye ndio nikamuelezea lengo langu kuwa mimi nataka kumuoa,….’akasema.

‘Yeye akakuambiaje?’ akaulizwa.

‘Eeeh, unajua tena wanawake, hakunijibu hapo kwa hapo,..alisema tu, yeye hajataka kuolewa kwa sasa, na kitu kama hicho anahitajia muda wa kutafakari…kiukweli nilishangaa sana, maana sikutegemea…’akasema.

‘Kwanini…?’ akaulizwa

‘Kwa maono yangu, sikutakiwa kukataliwa…japokuwa hakusema hanitaki hapo hapo…, maana wengi wananitaka niwaoe, lakini mimi sikutaka kuoa haraka baada ya kukosana na mke wangu wa kwanza, nilihitaji muda wa kutafakari, na ili niweze kumpata ambaye tutaendana naye…, sikutaka kukurupuka tena..’akasema.

‘Ni kweli hayo..kuwa wengi wanakutaka, …mbona awali ulisema watu wanakuchukia, sio ndio pamoja na hao mabint…?’ akaulizwa na hapo kidogo akasita, na baadae akasema.

‘Mbona maswali yako hayalengi swala husika, kwani wewe unahitajia nini hapo, mimi nilitaka uniulize maswala ya tiba au sio…sasa naona maswali kama ya polisi unanitia wasiwasi kidogo, lakini mimi isjlai wewe uliza tu..?’ akauliza.

‘Mimi nina mashaka na wewe kuwa matibabu yako yana walakini, ndio maana nataka kujirizisha, kwanini huyu mdada alikukukataa, kwanza ulipomtaka umuoe, na pili huko kwenye matibabu, kwanini…?’ akaulizwa.

‘Mimi ninavyohisi eeh,…labda, na ndio hivyo yeye alisikiliza maneno ya mitaani…..’akasema akimtupia jicho mdada, na mdada akawa anatabasamu tu, tofauti na ilivyokuwa kwangu, nilikuwa nimekunja uso kwa hasira.

‘Maneno gani hayo ya mitaani mpaka akukatae wakati umesema wewe kwa uaoni wako asingelikukata,..?’ akaulizwa na hapo akatabasamu na kutikisa kichwa, akasema;

‘Unajua sasa nimeelewa, nyie mlishaongea na huyu mdada akawaelezea yote wanayoyaongea watu huko kunihusu mimi, huo ni uwongo, msiwaamini kabisa hao watu, nilimuambia huyu mdada, asiwasikilize, na akija kwangu atapata kila kitu anachokihitajia, haamini, sasa….’akasema.

‘Aaah, kwasasa tunaongea na wewe, sio wao, na hilo unalosema kuwa tunawasikiliza watu wa huko sio kweli, hatujaongea nao, sisi tumekuja kwako rasmi ili ikiwezekana tupate huduma yako, sasa jiamini kama docta wa kienyeji, maana wewe ni mtaalamu, huogopi, au sio…?’ akaulizwa.

‘Watu kule hasa maadui zangu wamekuwa wakinipakazia uwongo, nahisi huyu mdada alipofika, na kuwaambia kuwa mimi nataka kumuoa, wakamuambia kuhusu huo uvumi usio na ukweli…ndio akanikataa, kwasababu hakunikatalia hapo hapo, alisema nimpe muda, jibu akaja kumpa rafiki yake kuwa hanitaki…’akasema.

‘Hebu kidogo hapo, huo uwongo wa watu wa mitaani, unasemaje, walikuwa wanakusema kuhusu nini..?’ akaulizwa hapo akakaa kimia na mama huyu akaliacha hilo swali na kuuliza swali jingine. Na kabala hajauliza akaingia docta na kuomba kuongea na mmoja wa akina mama yule aliyeongea naye awali, akamuita kwa nje.

Baadae huyo mama akarudi, na kusema;

‘Tuendelee, nashukuru docta katupa muda zaidi, ….’akasema huku akiwaminyia wenzake jicho.

Kuna kitu kinachoendelea kati ya hawa akina mama…, na huyu mgonjwa alikuwa hajakigundua, kwasababu wakati wanapeana ishara za macho mara nyingi yeye huwa kainama, nahisi angeliwaona angeligundua kuwa wenzake wana jambo dhidi yake.

**********

‘ Sasa kutokana na muda, ..twende haraka haraka, jamani wenzangu huyu mimi ninavyomuona anaweza kutondolea hili tatizo, kwasababu katutisha sana,…’akasema

‘Sio nawatisha, ni kweli, ogopeni haya mambo, hayatibiki hospitalini…na hawawezi kuyaona, utapata shida, unatibiwa huku na kule, kumbe tatizo ni jingine kabisa…mimi nimewajali sana, mpaka nikachukua hatua hii…’akasema

‘Ni sawa, .. lakini mimi bado nina Swali,…kuhusu mtalaka wako, umesema yeye mlikosana naye, bado sijaridhika na huko kukosana naye, unaweza kutufafanulia kidogo hapo maana mtu anapokosana na mkewe au familia yake, lazima kutakuwa na walakini kati ya mmojawapo, na hapo ndipo unaweza kumpima mtu..?’ akaulizwa

‘Hahaha…sawa mimi nitawajibu tu,…unajua kijijini usipokuwa makini, utakosana na kila mtu, na hasa ukiwa na maendeleo watu wengine watakuonea wivu, nilmuambia mke wangu awe makini, lakini hakunisiliza mimi ,akawa anawasikiliza watu wa  nje, nikamuambia njia ni nyeupe, aondoke zake…’akasema.

‘Hivyo tu..mbona haiji akilini, hivi kweli mke unampenda, itokee kosa kama hilo, umuambie nje nyeupe aondoke,..kwahiyo akaondoka kwasababu hiyo..?’ akaulizwa.

‘Kama kuna mengine, ni ziada tu…, lakini la kwangu muhimu ni hilo, na kwa vile hakunisikia,..tena na tena, nikaona sasa nimeoa au nimeolewa, nikamkabidhi kilicho chake, akaondoka, ..kwaheri kabisa, sio kwa kupigana, hapana mimi sina tabia hiyo…’akasema.

‘Mliwahi kusuluhishana kwenye mabaraza ya wazee au ilikuwaje, kwenu..?’ akaulizwa

‘Tuliwahi tena sana, sikupendelea kufanya hivyo…lakini niliona nifuate utaratibu wa kinyumbani,, na aliyoyaongea hapo kwa wazee, ni yale yale wanayoyaongea watu huko mitaani..fitina, majungu…iliniuma sana, mke wangu na yeye hataki kuwa upande wangu akanitetea, na yeye anaunga mkono maneno ya mitaani, kiukweli nilikasirika, ..na nikaona hanifai..mtu anatoa siri zangu, na zingine sio za kweli anaongezea na chumvi, hapana nikaona hanifai ….’akasema akitikisa kichwa

‘Kabla hatujazijua hizo fitina,..maneno ya watu, nk..ngoja turudi kwa huyu mdada, tunataka tuliweke hili sawa maana tunataka umtibie na yeye, na tunataka na yeye aondoe chuki , na kama ikibidi , sisi tutamsihi muoane, au sio…sasa ni wewe tu kujikosha kwetu,…’akaambiwa.

‘Hahaha, ndio maana nimekubali kuwajibia maswali yenu yote, najua nyinyi ni waelewa, na mtamuelewesha huyu binti, kwakweli nampenda sana…’akasema

‘Unajua sisi tunajiuliza tu, huyu na yeye, umsema naye kasikiliza maneno ya nje, kwahiyo kitabia hana tofauti na mtalaka wako, kwa haraka tunaweza kusema hivyo,..natabia za mke utaziona mapema,… au sio, sasa kwanini bado umemshinikiza kutaka kumuoa..?’ akaulizwa.

‘Hapana,yeye kwa muda mfupi niliomchunguza hawezi kuwa kama huyo mtalaka wangu mimi nina imani tukioana mimi nay eye,  atanijulia , na atanielewa, nimempima nikaona nimuelewi zaidi, unajua yule wa mwanzo, niliongea wee, nikamkanya, tukasuluhishwa, lakini hakubadilika kabisa, ikafika muda akasema wazi kuwa hanitaki…’akasema

‘Akasema kabisa hakutaki, kwahiyo sio wewe uliyemuacha kwa ridhaa yako, ni yeye alikukataa, au mbona unatuchanganya..?’ akaulizwa

‘Baada ya kushindwana na kuona msimamo wangu ndio akasema hanitaki, lakini mimi nilishafikia hatua hiyo kuwa hatutaelewana tena,….nikamuacha…’akasema.

‘Hapo, bado….unatutia mashaka, tunaogopa kama ukimchukua huyu binti yetu, inaweza ikawa sawa na huyo mtalaka wako….tuthibitishie, na ukweli wako ndio utatusaidia kutoa maamuzi, ya kutibiwa kwako na ikiwezekana tumshawishi huyu bint, huenda akakubali…’akaambiwa.

‘Huyu nina imani, hatakuwa hivyo..na mimi nitajaribu kujishusha, nimegundua kuwa awali nilichukulia mambo kwa hasira, …unajua ujana tena, sasa nimeshakua mtu mzima, hatutakosana kabisa, muhimu asiyasikilize maneno ya mitaani…’akasema.

‘Hivi hayo maneno ya mitaani ya yepi..?’ akaulizwa na mama mwingine na huyu muuliza maswali akatikisa kichwa kumuashiria mwenzake asiende haraka hivyo, lakini swali lilishaulizwa, na jamaa akasema;

‘Achana nayo…hayana maana hayana ukweli…’akasema

‘Unaogopa kuyasema…au?’ akaulizwa.

‘Sio kwamba naogopa kuyasema, unajua vitu vingine uongee ukiwa na ushahidi, mtu anakuambia eti wewe ni muhuni, unatembea nje, una …warubuni wanawake kwa madawa wanajileta wenyewe kwako..ni mambo hayo ya uwongo kabisa, mimi sina tabia hiyo mimi nilikuwa muaminifu kwenye ndoa yangu ,maana kazi yangu inanikataza kufanya hayo mambo…’akasema

‘Una uhakika na hilo..?’ akaulizwa.

‘Uhakika wa lipi hasa..kuwa mimi sina tabia hiyo..ndio ukweli wenyewe kazi yangu inanibana nisiwe hivyo, sina shaka na hilo na kwanini waseme hivyo, wangeniambia nimetembea na huyu na yule kama wanavyodai wao, basi angenionyesha hao watu, lakini alikuwa hana ushahidi, kama hao wapiga domo wa nje, hawana kazi, kazi zao ndio hizo, ndio maana hawana maendeleo..’ akasema.

‘Kwahiyo wewe kamwe hujawahi kutembea nje na mwanamke mwingine,…wewe si rijali,..ndivyo mnavyojiita, aah, sema ukweli bwana,..?’ akaulizwa

‘Hahaha..hayo tuyaache,….’akasema.

‘Sasa  na hilo la kuwa unarubuni wanawake kwa madawa ni maneno tu, kweli hujatokea kuwapenda, hasa wateja wako maana waganga ndio zenu akija unampenda, unataka umjaribu, ?’ akaulizwa

‘Hapo nahisi unanitega…..’akasema

‘Ni hivi nakuuliza hivyo nikiwa na maana, hata sisi wanawake tunataka hayo madawa, kuwaweka sawa wanaume zetu,..unayo hayo madawa?’ akauliza.

‘Ninayo sana…’akasema kwa kujitapa.

‘Na hayo madawa yanafanyaje kazi…?’ akaulizwa.

‘Ni kutegemea na wewe unataka nini, kumfanyaje mke au mume wako…wewe unafunguka unavyotaka.., nataka hivi na vile, na mimi nakutengenezea kabisa, na inafanikiwa, haina shaka…’akasema.

 ‘Na unayo madawa ya kumvuta mwanamke akaja kwako, na ukamfanya utakavyo, au, …ulisema awali hata wabaya wako unapambana nao kihivyo, si ndio hivyo, mfano umempata mwanamke ukampenda, lakini hataki, wewe si una dawa za kumpata, au hata kwenda kwake usiku ukamfanyia utakavyo, …?’ akaulizwa.

‘Mhh, swali lako limekaa kimtego, lakini nikujibu hivi…waganga wanaweza kufanya madawa ya namna hiyo, na kuwapatia wachawi, ili wao wakatimize malengo yako,..kama unataka kwenda kwa mtu usiku amelala, basi unafanyiwa hiyo dawa..na kweli unafika usiku wao hawakuoni, wakiwa wamelala, ukafanya unayotaka kuyafanya, sasa mimi nawatibia kujikinga na hayo mambo, na hayo mazindiko wanayowawekea ,…’akasema.

‘Ninachotaka hapa ni uhakika, kuwa hata nyie waganga mnaweza kufanya hivyo,yaani kutengeneza dawa na kufanya kazi za kichawi…?’ akaulizwa.

‘Tukitaka ndio tunaweza,…si ninajua dawa zake, pia ninajua zinavyofanya kazi, kwanini nishindwe kufanya hivyo….’akasema kama kujitambia.

‘Kwahiyo unakubaliana na mimi kuwa waganga wa kienyeji kama wewe pia ni wachawi …?’ akaulizwa

‘Inawezekana, siwezi kukataa, kwa msimamo huo…inategemea sasa na tabia ya mtu mwenyewe, au malengo yake ni nini…’akasema

‘Kwahiyo hata wewe unafanya hivyo, au uliwahi kufanya hivyo…?’ akaulizwa

‘Mimi kama mimi, kwanini nifanye hivyo, kwanza nimeshakuambia, kazi yangu ina miiko,siwezi mimi kufanya hivyo, kama ninataka kupambana na mtu, maana wenyewe kwa wenyewe tunajaribiana, pia kuna maadui zako unataka kuwakomoa, nitafanya hivyo, lakini kwangu mimi aah, kwanini nisumbuke, ninaweza kufanya hivyo ikinilazimu lakini kwa kupitia kwa mtu mwingine…’akasema.

‘Kwahiyo wewe ukitaka kumkomoa mtu, au ukitaka kupambana na adui zako, au ukitaka kulazimisha jambo liwe kwa hao unaowaita maadui zako au yoyote yule , wewe huwa hufanyi  hivyo peke yako, unawatumiwa watu wengine...sasa unawatumiaje, je utakuwaje na uhakika kuwa kazi yako imefanyika...?' akaulizwa

'Uhakika kwa vipi, maana unayemtuma hawezi kufanya tofauti na wewe..yeye anafuata dhamira yako, anakuwa sio yeye tena hajitambui kabisa.. na wakati mwingine unaweza kuongozana na yeye,, ukitaka kuhakikisha, si ndivyo unataka kujua hivyo au..?’ akasema na kuuliza.

'Kwahiyo wewe mara nyingi unafanya hivyo ukitaka kufanikisha mambo yako, labda kwa maadui zako au kwa mpinzani wako, si ndio hivyo., na mara nyingi kiuhakika na wewe unafika kushuhudia kuwa kazi imefanyika au sio, kwahiyo kila kilichotendeka ambacho kina kuhusu wewe utakuwepo, au sio.....?' akaulizwa

‘Mimi hahaha, wewe bwana wacha kunichanganya, nikuambie kitu,…usitake kunijua zaidi, ukitaka hayo, utanihisi vibaya bure..., mimi sio mbaya kihivyo, ila ukinichokoza, kazi yangu ni kubwa wenyewe waulize watakuambia ...hata hivyo najiuliza ni kwanini unaniuliza mswali kunihusu mimi, au huyu mdada kawaambia nini cha kuwatia mashaka? ’ akauliza.

‘Swali langu lipo wazi, usiogope kujibu, jiamini, je wewe ukitaka, hasa kwa maadui zako unaweza kufanya hivyo, au sio…?’ akaulizwa hapo akakaa kimia kidogo.

‘Naona unaogopa kulijibu hilo swali, kwanini unasita, unaogopa nini…?’ akaulizwa

‘Sio kwamba ninaogopa, niogope nini, mimi najiamini,…tatizo maswali yako mengi ya sasa yana mlengo wa kunishutumu hivi, labda mdada kalalamika kwenu...hapana sivyo hivyo mnavyofikiria nyie, kama ningelikuwa na nia mbaya nisingeliwaita kuja kuwasaidia…’akasema akimtupia jicho mdada, unajua mdada alikuwa kasimama mbele yake, wanakuwa kama wanaangaliana kwahiyo hakuwa na ujanja ni lazima kila akiinua uso wanaangaliana, na hilo naona lilikuwa linampa shida.

'Sasa kwanini hujibu swali...?' akaulizwa

‘Kwanza, unielewe mimi ni mganga wa kusaidia watu, mara nyingi, waganga walivyo, wanaweza kujaribu madawa yao, kama yanafanya kazi, kwahiyo wanaweza kujigeuza wachawi pia wakitaka…wengine kwa malengo ya kuthibitisha madawa yao,, au kuonyesha ubabe wao, yote yawezekana japokuwa sio wachawi, wapo watu wa namna hiyo…’akasema.

‘Na wewe ni mmojawapo.. au sio?’ akaulizwa, akimuangalia huyo mama huku akicheka, …

‘Hahaha, hayo tuyaache, maana utataka nikueleze kila kitu ninachokifanya, kitu ambacho hakiwezekani..kifupi ndivyo ilivyo kwa waganga na wachawi na tofauti zao…, na ndio maana nawashauri msikimbilie tu watu ovyo, uliza kwanza, huyu mdada angenisikiliza mimi nahisi sasa hivi angekuwa hana tatizo kabisa…’akasema

‘Kwahiyo kumbe kosa lake ni kutokukusikiliza wewe, ikiwa ni pamoja na kwa vile kakutakaa au sio...?' akaulizwa

'Hapana sio kwa vile kanikataa, kwa vile alipopatwa na matatizo hakutaka kunisikiliza mimi yale niliyomshauri, akaona aende kwa wengine, huko wakamdanganya, ndio walimtibia lakini mengine sio sahihi, hao ni maadui zangu, wanaweza kusema mambo ili kuniharibia.....'akasema

'Nina imani kuwa angekukubalia wewe umuoe, asingelipata hiyo mitihani, au sio…?’ akaulizwa

‘Hahaha, hapana,.... usije kunifikiria hivyo, kuwa labda kwa vile yeye kanikataa, basi mimi ndiye niliyemfanyia hivyo, kwanini nifanye hivyo wakati nikitaka naweza kumvuta kwa namna nyingine,….’akasema

'Kwa namna nyingine kwa vipi..?' akaulizwa

'Hiyo ni siri yangu, siwezi kuwaambia mbinu zangu za kuwashinda maadui zangu...'akasema

'Kwahiyo mtu akikataa matakwa yako, mara nyingi anakuwa adui yako, au sio...?' akaulizwa

'Sio lazima, lakini kama inabidi..lakini sio lazima...'akasema

'Huyu mdada alipokukataa, wakati hapo kijijini wanakuogopa, ukitaka jambo lako unapata, au sio, wewe ni mganga mwenye kuogopwa, na kusifika pia, ..hebu tuambie, alipokukata huyu mdada ulihisi vipi, kukasirika, kuwa kakuzalilisha kwa vile hujawahi kukataliwa au ulijisikiaje..?' akaulizwa

'Kawaida tu...'ni hivyo tu, sina zaidi ya hayo..nimechoka....'akasema akibenua mdomo kwa dharau

'Sema ukweli...kama ulivyoniambia...'akasema mdada, na jamaa akamtupia jicho baya mdada, halafu akakwepesha kumuangalia, na kutikisa kichwa kama kusikitika, hawa akina mama wakawa wanaangaliana huku wanatikisa kichwa kukubaliana kwa ishara, kama vile muda umefika...

************

‘Ndugu unajua nimekuuliza maswali mengi sana nikitaka kujua jinsi ulivyo…naona na muda nao umetutupa, tutakuja kufukuzwa humu,nia yangu ya kukuuliza hayo ni kutaka kukufahamu, jinsi ulivyo,maana sisi kama ulivyosema tuna shida, kama ulivyotuambia tumewekewa mazindiko au sio, sasa hatuwezi kukurupuka tu kwa mganga, lazima tumuulize maswali tumpime kweli kazi anaiweza, …’akasema

‘Sawa kabisa, kwahiyo mnasemaje?’ akauliza

‘Lakini bado najiuliza, sio wewe uliyempigia simu mwenzetu hapa, ukasema kuwa wewe ulikuwa hivyo ulikuwa mchawi, …kwenye simu, au nimekosea mwenzangu…?’ akageuka kumuulizia mwenzake, na mwenzake akasema

‘Kanipigia mwenyewe, hata sijui alivyoipata namba yangu ya simu, maana siku ile sikumbuki kumpa namba yangu hata mimi nimejiuliza sana…’akasema huyo mama

‘Kuipata namba ya mtu ni rahisi sana,msituone sisi tupo kijijini mkatudharau... sisi ni wajanja kuliko hao wenye mitandao wenyewe, tunachoshindwa tu, ni kuiba pesa benki….’akasema akicheka

‘Ni sawa kama mnaweza kuingia majumbani mwa  watu usiku, sizani kama mtashindwa, au sio...sasa hebu tuambie maana hili linaweza kuleta maulizo mengi, ya kutokuaminiana, je uliipataje hiyo namba ya huyu mama..?’ akaulizwa

‘Hiyo ni siri yangu…siwezi kuwaambia...’akasema akikunja uso kuwa kadhamiria kweli hawezi kujibu hilo swali.

‘Sawa ni siri yako, kama ilivyo siri, ya jinsi gani uligundua kuwa majumbani kwetu kuna hayo..manini vile...lakini sasa ikibidi utatakiwa kutuambia ukweli maana sio vyema kupata namba ya mtu bila kibali chake, au kufika majumbani kwa mtu bila kibali, tena usiku…’akaambiwa.

‘Ikibidi, kwanini unasema ikibidi,…unajua niwaambie kitu, sawa nimekuelewa, kama ikibidi mimi nitajua jinsi gani ya kujietetea, maana hiyo kauli yako ya  ikibidi, ina walakini, mniamini mimi, mimi lengo langu ni kuwasaidia, sio kuwatapeli, unasema nini, usiku, sijakuelewa hapo….’akasema

‘Tutafiikia huko, kwanza ningelipenda utujibu hili,..wewe ulisemaje wakati ulipompigia simu huyu mwenzangu hapa, .?’ akaulizwa, kwanza akamuangalia mdada, halafu madamu wake, halafu akatabasamu , lakini tabasamu la kujiuliza, kabla hajajibu, akatabasamu kidharau, na kusema;

‘Ndio nilimpigia mimi sikatai,...na lengo langu lilikuwa jema kabisa, mikamwambia kama nilivyoongea awali, kuwa majumbani kwenu kuna matatizo, yanahitajika kutolewa….’akasema.

'Ulijuaje kuwa kuna matatizo...?' akaulizwa 

'Aaah, kwani ukifika kwa mganga, inakuwaje, labda nyie hamjawahi kufika kwa waganga, yeye anaweza kukuambia mambo yote ya nyumbani kwako bila hata ya yeye kufika, ..ni utaalamu wetu ...'akasema

'Na hayo  mazindiko yaliwekwaje na nani..?'akaulizwa

'Na wachawi....watu wasio na nia njema na nyie, kwasababu zao ..mimi siwezi kujua ni sababu gani, mpaka niongee na watu wangu...'akasema

'Na wachawi sio....?' akaulizwa

'Ndio ...'akasema

'Sawa sasa hebu tuambie wewe mwenzangu wakati anaongea na simu alikuambiaje, awali kabisa, maana yote hayo tuna ushahidi nayo,..?' akaulizwa

'Si nimeshakuambia...'akasema

'Hakukuambia wewe ni mchawi, ukamjibuje...?' akaulizwa

Ilikuwa kama kazabwa kibao usoni, kwanza akatulia, akageuka kumuangalia huyo mama aliyeongea naye kwenye simu, na huyu mama akawa kashikilia simu kama kuonyesha ushahidi,...Jamaa akainama chini, na kabla hajasema neno, mimi nikasogea mbele na kusimama pale aliposimama mdada kwahiyo wote wawili tukawa tunamungalia yeye moja kwa moja usoni


WAZO LA LEO: Uongo wakati mwingine unasuta, kwani walisema dalili za mnafiki mojawapo ni kuzoea kusema uwongo, hebu tujiulize mara ngapi tunaongopa, mpaka inafikia sehemu hatuogopi tena, hata kuapa tunaapa, ‘haki ya mungu, ..’ halafu tukitwa wanafiki tunakasirika. Jamani tuchungeni sana ndimi zetu, hasa katika jambo hili la kusema maneno yasiyo ya kweli ili tu kupata umaarufu, au kufanikisha malengo yetu,KUMBUKA unatudanganya sisi, lakini yupo yule ambaye hadanganyiki, ipo siku utarejea kwake,..Tumuombe mola wetu atusamehe kwa makosa haya na mengine, na atujalie tuwe wasema ukweli ili tuweze kuzipata radhi zake. 
Ni mimi: emu-three

No comments :