Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, July 26, 2017

DUWA LA KUKU....21


‘Kama wewe ni mtaalamu, na ulinitizamia, na kama unavyodai wewe unafahamu mambo aliyo nayo mtu, sasa niambie, huu uja uzito ni wa nani…?’ nilimuulizaa

‘Unataka nikutajie ni wa nani…hahaha, eti jamani nimtajie…?’ akauliza akionyesha kama mzaha

‘Kasema umtajie, wewe si unajua ni wa nani au…?’ akaambiwa kama anaulizwa

Tuendelee na kisa chetu

************

‘Unajua nyie ni wajanja sana..nyie mnataka niwaambie kila kitu, wakati na mimi hiyo ndio kazi yangu, nikiwaambia kila kitu, malipo yangu nitapata wapi…eti jamani..?’ akawauliza

‘Hili hapa sio swala la malipo, ni swala la wewe kujibu shutuma, mdada anahisi wewe unahusika na hayo yaliyomtokea sasa mjibu swali lake…’akaambiwa.

‘Aaah, kumbe…unajua mimi sikujua, nilijua mnataka niwaambie kazi zangu ili muwe wateja zangu, au sio..?’ akauliza

‘Pamoja na hayo, waganga ni wachawi pia,..tunataka ulikane hilo, je ni kweli au sio kweli kwako wewe.?’ akaulizwa


‘Yategemea, sasa…wewe binti, ukitaka nikuelezee hayo yote, matatizo yako, unatakiwa tuwe wawili, unanielewa, hapa sipo ofisini kwangu…tutaongea, usijali kuhusu malipo wala nini…halefu eti jamani wewe ndiye una mimba, na mimba inakujaje, wewe ndiye utakuwa unamfahamu aliyekupa hiyo mimba ni nani..’akatulia akisubiria mtu kama ataongea

‘Ndio mimi nakubali kuwa mimi nina kipaji, urithi wa uganga, ni-naweza kukuambia hiyo ni mimba ya nani., lakini hilo ni la ndani zaidi, siwezi kukuambia hapa, nitakuambia tukiwa wawili, tukishakubaliana malipo, labda niweke wazi hivyo…’akasema

‘Hapo hapo…umesema hiyo mimba sio ya kawaida,…kwahiyo hata kupatkana kwake sio kwa kawaida, ndio maana hiyo mimba iliingia isivyo kawaida, iweje tena uniambie kuwa mimi namfahamu huyo mtu, kwa vipi sasa...’nikasema

‘Unajua wewe una nidodosa, ili nikuambie kila kitu, lakini siwezi kukuambia hilo kwa sasa …hayo niliyokuambia yanatosha, kama huamini, kaa na hiyo mimba yako, utakuja kunitafuta mwenyewe…’akasema

‘Kama ni tatizo linahitajia matibabu , kwanini mpaka nikutafute wewe…kwani hakuna wengine wanaoweza kunitibia…?’ nikamuuliza

‘Nimeshasema mimi siwezi kuliongelea swala lako zaidi ya hayo niliyokusaidia kukufafanulia, zaidi ya hapo, unanitaka na mimi nisipate ujira wangu….au jamani nakosea…?’ akawauliza wale akina mama.

‘Sasa ni hivi, unasema yeye akipimwa ataonekana ana uja uzito, lakini sio mimba ya kawaida…, kama sio mimba  ya kawaida ni mimba gani, hapo unatuchanganya…?’ akaulizwa na akina mama .

‘Wewe unauliza maswali vizuri sana, wewe ni mwanasheria nini, au…mwalimu…au….aah, nimeshakugundua wewe ni mwalimu…’akacheka.

‘Tujibu swali…’akasema mama mwingine.

‘Huo uja uzito sio mimba ya kawaida, umeelewa hapo…, akichelewa itaendelea kukua kama mimba ya kawaida tu…, lakini kilichopo tumboni sio kiumbe cha kawaida, na anaweza akafikia muda wa kuzaa na kuzaa kama kawaida, ila atazaa nini sasa, hapo ndio tatizo,..wakati huu wa miezi kwenda tisa..kuna dalili atazipata kabla ya kuzaa, kama nilivyosema awali…’akasema.

‘Atazaa nini mtoto au kitu gani…?’ akaulizwa, sasa akanigeukia na kuniangalia akasema;

‘Upo tayari nisema hayo maana ni mambo yako, unaweza ukaogopa, ndio maana nilitaka tuongee mimi na wewe, ngoja nfanye hivi, hili nilitoe kama promosheni, sitakuchaji kitu, navutia biashara, maana huyu mama nimependa anajua kuuliza maswali kihekima, hana jaziba, jaziba za nini..mimi nina kosa gani eeh,…?’ akauliza.

‘Sio jaziba, ni kweli, wewe sema ulichonifanyia, usijifanye kutabiri hapa..mimi nimeshakujua,….wewe ’nikasema na huyo mama akaniashiria ninyamaze, na jamaa akaniangalia halafu akatabasamu kidharau fulani hivi, akazidi kunichefua, …unajua mtu kama alikuzalilisha, akawa anaonyesha hivyo, ni kama anakuona wewe ni nani hasa nimeshakuona ilivyo, kiukweli nilihis vibaya, hasira…

‘Wewe hapo ulipo una mimba na ukiiachia itakua tu…, utakuja kuzaa mtoto…mwanadamu kama kawaida, atakuwa na umbile la mwanadamu, lakini tofauti yake itakuja kwenye matendo, hulka, utachoka kwa jinsi atakavyokuwa, watu wanazaa na hawataki kujisafisha na mauchafu ya mwilini,…sawa kama ana imani ya dini, anaweza kuhudumiwa huko, lakini sisi tunajua mambo yetu ya kimila,…’akatulia kama anawaza jambo.

‘Niwaambie kitu, kuna watu wanazaa, wanataka watoto, wanakwenda kwa wataalamu, wanafanikishiwa, haajui wamewekewa nini…acha hao, kuna watu wanatembea ovyo ovyo, wanakuja kujifungua,, lakini wanakuja kusumbuliwa kweli na walichokizaa, mara unasikia mtoto sio rikizi,…kwanini asiwe riziki,  mtoto jambazi, mtoto hasikii, hashikiki, ..unaona hiyo ni mifano tu, sasa hayo nimekutolea mfano, ila wewe utakuja kuzaa zaidi ya hiyo, sikuambii zaidi ya hapo…’akasema

‘Hapo bado unatuchanganya, ina maana atakuwa kazaa nini, …kama sio mwanadamu, na utamtofautishaje na watu wengine..?’ akaulizwa.

‘Kwa ufupi,..unajua shetani, ibilisi, sio lazima awe huyo tusiyemuona, mnakubaliana na mimi…?’ akauliza

‘Utuambie wewe, maana hata wachawi, …kwa imani zetu ni mashetani…’akasema mama mmojawapo.

‘Umeonaeeh,..sasa huyu atazaa mtoto zaidi ya huyo…kitabia, na matendo yake, atakupa shida sana, lakini unaweza kuwapata watu kama sisi tukakusafishia njia, tukakisafisha hicho kiumbe, tukaondoa hayo mazindiko, maana sio mipango ya mungu, ni watu wamekufanyia hivyo…’akasema
Wale akina mama wakaangaliana, na kutikisa kichwa.

‘Mimi nawaonea huruma sana,..mtasumbuliwa sana na mambo haya, lakini kwanini msihangaike, mkawaona watu kama sisi, tukawaondolea hayo matatizo, nyie tatizo mnajali sana mali, mali ni nini, mali zina fadia gani, kama watoto wanakuwa hivyo, wanaumwa, wanakuwa na tabia mbaya,..ina faida gani sasa…’akawa kama anauliza

‘Sawa wewe mdada, binti, nimekupa hilo kama angalizo, na sio wewe hata nyie sote, hangaikeni,..utazaa mtoto awe jambazi, awe muaji, na mwisho atakuambi anahitajia damu za watu…’akasema na mimi pale nilipo nilihisi mwili ukiniishia nguvu, nikajikaza, ilichukua muda hadi hali ikawa sawa, nashukuru nilikuwa nimeegemea ukuta.

‘Umejuaje hayo, na kwanini ni iwe hivyo na huku hospitalini wanasema ni mimba, ya kawaida na haina tatizo..?’ akaulizwa

‘Nimewaambia mimi nina karama za mambo hayo kujua mambo ya mtu yaliyojificha, kwa kutumia watu wangu, lakini kwa anayeamini siwezi kuwalazimisha watu wote waniamini, unaelewa hapo…, mtu kama haamini hawezi kuwa muumini wa kile kitu…si ndio hivyo…swali jingine, hilo tumalimaliza, kwa huyu tuyaachie hapo…’akasema.

‘Kwa utaalamu wako, unahisi matatizo hayo yametokana na nini, au na nani hasa, maana unasema ana mimba ya lakini sio mimba ya kawaida, sasa imeingiaje mwilini mwake..?’ akaulizwa.

‘Hapo sasa unaingia kwenye sehemu ya ndani ya kazi zangu, hapo kunahitajika makubaliano, promosheni hiyo haiwezi kwenda kiundani ki-hivyo…, hapo sasa ni nipe nikupe, siwezi kutoa utaalamu wangu wote bure , kama anataka nimsaidie basi tukubaliane kwa malipo stahiki, najua yeye ana hali mbaya, hata mshahara wake hataweza kunilipa, na mimi nitaangalia ahueni fulani….’akasema.

‘Bei gani..?’ akaulizwa

‘Mhh..umekwenda mbali, ..kwanini wewe unamuulizia.., wakati mwenyewe yupo,  kama unataka kumlipia sawa, lakini nilitakiwa nikae naye nifanye mambo yangu yaniambie ni kitu gani kinahitajia,…lakini kwa vile nilishalifanyia kazi kabla, naweza kumtajia vifaa kwa ufupi…’akasema .

‘Sisi ndio tumechukua dhamana kama wazazi wake tunataka umtibie, tuambie gharama zake, ili tuwezi kujipiga, tuone kama tutaweza , la sivyo tuta-tafuta mganga mwingine…, au mnaitwaje nyie watu, wataalamu,…tuambie ukweli pamoja na mengine, dhumuni letu mojawapo ni kumsaidia huyu mdada, na wewe umesema unaweza kuifanya hiyo kazi, ulimuambia huyo mdada mwingine si ndio hivyo…’akaambiwa, na akaniangalia mimi kwa muda, halafu akasema;

‘Kwa haraka, ..yaweza ikawa juu au chini, ndio maana sitaki kukadria, lakini kwa uzoefu, ili kuliondoa hilo tatizo, na kumweka huru na hayo mazindiko yaliyotokana na watu,..kuna makafara ya damu ya kimizumu, ili yafanyike kunahitajika ng’ombe mwekundu dume lislo na tatizo lolote,,na pia..mbuzi au kondooo wa rangi mchanganyiko. Kuku wawili, mtetea,…kuna viti vingine vidogo vidogo, madawa ya kufuza…eeh, kwa hivi sasa siwezi kuvitaja mpaka niongee na watu wangu, ila muhimu kunahitajika damu ya kafara, hayo ni mambo yetu ya kitaalamu zaidi….sasa ukipiga gharama hapo utaniambia…’akasema

‘Duuh, ndivyo mnavyofanyia watu hivyo, mbona gharama kubwa sana..?’ akaulizwa

‘Hapo nimemsaidia tu kwa vile ni mtu wa shida, …, la sivyo,..’akatabasamu tabasamu lake la dharau akiniangalia usoni, halafu akatikisa kichwa kama kusikitika.

‘Kiukweli binti huyu ana matatizo makubwa namuonea sana huruma..yeye hajijui tu, sasa kama haamini, yeye abakie hivyo hivyo tu…, kuwa ana mimba, itafikia sehemu ataanza kupata shida sana, atahisi vitu vinatembea tumboni, vinamchoma choma, si unajua shetani lina makucha, lina…sasa siwezi kumtisha, lakini ndio hivyo, haraka afanyiwe hivyo ili asije kuzurika..anaweza akavumilia, akazaa lakini kwa shida pia…’akasema.

‘Jamani sasa mnielewe kwa huyu siwezi kuongea zaidi ya hayo, nimemalizana naye…’akasema akiangalia pembeni

**************
 ‘Sawa…lakini yupo huyu mwingine pia, kabla hutujamalizana, tunataka tujue gharana zako kwa wote wawili maana wote wana matatizo yanayofanana, je huyu mdada mwingine naye ana tatizo gani..?’ akaulizwa

Aligeuka na kumuangalia mdada, lakini akawa hamuangalii kama alivyokuwa akiniangalia mimi, ni kama anamuogopa kumuangalia moja kwa moja usoni, ….akasema

‘Huyu bwana, nakumbuka alikuja kwangu ndio,… ila tulikuwa hatukuelewani kidogo, akaenda kwa wataalamu wengine wakamfanyia walichomfanyia,…siwapuuzi hao wataalmu.. nawaamini, sio haba.., ..na kwa vile alikwenda huko mimi sitakiwi kuwaingilia, yeye mwenyewe kama hajarizika nako basi anione mimi ..’akasema

‘Unasema alikuja kwako mkawa hamukuelewana kidogo…ni kwanini hamuekelewana na huyu mdada, wakati alikuja kwako akiwa na tatizo ina maana mgonjwa akija kwako kama hamtaelewana huwezi kumuhudumia…?’ akaulizwa.

‘Kwanini hatukuelewana, hayo ni kati yangu mimi na yeye ni mambo binafsi kwa kweli..’akasema

‘Lakini sisi tunataka umuangalie na yeye matatizo yake,..bila kujali hayo ya huko nyuma,.. kama matatizo yake yamekwisha au la, sisi tutakulipa, lakini tuwe na uhakika wa kupona kweli, uhakika wa kazi yako,..?’ akaulizwa.

‘Yeye tumeshaongea naye sana, na kwa vile hatujaelewana kwa mabo fulani fulani, siwezi kumlazimisha zaidi, kama atanihitajia sawa, atanitafuta, yeye, ananifahamu , anajua mpaka nyumbani kwangu huko jijini…’akasema.

‘Mhh, unataka kusema nini ina maana matibabu yako yanagusa hata maswala mengine, unavyoongea ni kuwa kuna mambo binafsi kati yako na wewe, hayo yanazuiaje matibabu yake..?’ akaulizwa
Hapo akamuangalia mdada, halafu akasema;

‘Unajua pamoja na hayo, sio kwamba nilikataa kumtibia, ila yeye mwenyewe alipoona nimegusia maswala mengine akajenga chuki,…akawa haniamini tena, na kazi yetu hii ni ya kuaminiana…kwahiyo nikaona aheri aende kwa wengine…’akasema

‘Ni wewe ulisema au yeye mwenyewe ndio aliamua hivyo..?’ akaulizwa

‘Yeye mwenyewe…na mimi sikumfuatilia sana, nilijua ipo siku atanitafuta tu…’akasema

‘Kwanini, akutafute wewe tena, wakati hamukuelewana…?’ akaulizwa

‘Haya mambo yanazidiana, mimi sio kwamba nitamba, lakini waulizeni wote huko kijijini, wanajua kuwa mimi ni mtaalamu zaidi yao,…sio siri, utaalamu wangu unasifika…’akasema

‘Wewe una mke?’ akaulizwa

‘Swali gani hilo jamani, mbona haliendani na haya, kwanini umeniuliza hivyo, mimi naona kuwa, hayo ni mambo yangu binafsi, …?’ akauliza na kabla hajajibiwa akasema

‘Lakini nikujibu tu, nilikuwa naye,..nilikuwa na mke,.. lakini kwa bahati mbaya, tukaaachana naye ..’akasema

‘Kwanini mliachana naye..?’ akaulizwa, na hapo akamuangalia huyo mama, sasa kwa uso wa kushangaa zaidi.

‘Ohh, unataka kujua na maisha yangu,…?’ akauliza
‘Nitakuaminije kuwa unayoyasema ni ya ukweli, …ni lazima nikupime kwanza kabla sijajiingiza kwenye matibabu yako, au una wasiwasi na maisha yako kuwa hayana ukweli..?’ akaulizwa

‘Oh, sawa,..usiwe na shaka nitakujibu tu..ni hivi,…hatukuelewana naye, watu wanaachana kihivyo, au sio..? mimi sio wa kwanza kuacha mke.., au sio….’akasema.

‘Kwanini hamukuelewana naye, kwasabau hapo kutakuwa na maswali ya kuuliza, ni kwanini,  kwa mtu kama mimi ninayekutaka uwe mganga wangu…?’ akaulizwa.

‘Maisha tu ndugu yangu…, sio kila mtu mtaelewana naye, unajua tena ndoa zingine zina mitihani yake..’akasema

‘Ukashindwa kuhimili mitihani ya ndoa, lakini wewe unawaambia watu waje kwako unaweza kuwatengenezea ndoa zao,…hapo huoniunanitia mimi mashaka…?’ akaulizwa

‘Mganga hajigangi, hilo liamini hivyo…ilifikia mahali niliona ni bora kuachana, hata watu wakija kwangu nikiona ndoa zao hazitadumu, kuna tatizo haliwezi kutatuliwa nawashauri hivyo, hata mimi ilifikia hapo…’akasema

‘Kwanini sasa hujaona kwa muda huo wote,….unaishije, au una namna nyingine ya kukuwezesha usiwe na hamu yakuoa..?’ akaulizwa na hapo akacheka na kutikisa kichwa.

‘Wewe mjanja sana…’akasema

'Jibu swali...auunaogopa kujibu kwa kuwa litafichua ukweli wa ulivyo...?' akaulizwa , hapo akacheka, na akageuka kumuangalia mdada, na mdada alipomuangalia na yeye, akageuka kwa haraka kuangalia pembeni, na kabla hajasema neno huyo mama akamuuliza swali jingine.

‘Halafu ndio ukataka kumuoa huyo mdada, au sio, alipokuja kwako ukampenda, nikurahisishie hivyo maana unaogpa kujibu hilo swali kwa vile muhusika yupo huwezi kudanganya,…, au sio..?’ akaulizwa

NB: Msichoke na maswali na majibu kuna kitu kinatafutwa na mwisho wake jamaa ataingia kwenyewe bila kujua, tukumbuke kisa chetu ni swali, je duwa la kuku kweli halimpati mwewe,


WAZO LA LEO: Tunapokuwa kwenye fani zetu, ziwe za kitaalamu, za kiimani, au za kipaji ulichojaliwa nacho, jaribu kuwa mkweli, hata kama ndio fani yako hiyo ndio njia ya kukuwezesha kupata riziki yako, usiingize uwongo, udanganyifu na ujanja ujanja wa kitapeli,…UKWELI, ndio utakuongezea kipato chako kwani utajenga uaminifu kwa wateja wako, lakini ukiwa muongo, ipo siku uongo wako utagundulikana, na wateja wako watakuona wewe sio mkweli na ndio itakuwa mwanzo wa kukimbia.

Ni mimi: emu-three

No comments :