‘Mimi
naona,…tukakutane na huyo mchawi huko huko hospitalini, kwanini anatutishia amano...'alisema huyo mama mwenye nyumba
'Sawa mimi naona iwe hivyo, kwa maana kwanza kama ni kweli yeye aliingia nyumbani kwangu akafanya hayo aliyoyafanya..akaharibu familia yangu na kutia fitina,..mimi mwenyewe , nahitajia kuonana naye...'akasema mama mfadhili wangu wa kwanza.
'Hilo jambo jema,, tuhakikishe tumelimaliza hili ili tuishe kwenye familia zetu kwa amani, maana leo kwako kesho kwangu, kama huyu binti kaja kwangu na mzigo, na huenda huo mzigo ni wake, si lazima atakuja kunisumbua na mimi,...huyu na mwenzake tuwakabidhishe kwake, na huyo mtu, apate kipigo, ajifunze...'akasema yule mama aliyenipeleka hospitalini.
Kiukweli sikuwa na amani, nikajua sasa maisha yangu yanakwenda kuharibiwa kabisa, bado nina mzigo, na simjui baba yake ni nani, na....haya yanayokwenda kutokea huko sijui yatatufikisha wapi, kama akina mama hawa wataamua kufany hayo yaliyopo kwenye nfasi zao
Tuendelee na kisa chetu...
****************
Wale
akina mama watatu wakakubaliana hivyo ikawa ni muda wa kusubiria simu ambayo
ilikuwa inapigwa kwa mume wa mmojawapo hapo, na wengine wakaamua na wao watumie muda huo kuwasiliana na waume zao, ili wajulikane wapi walipo na wanataka kwenda kufanya nini huko.
…
Kiukweli
waume walikubaliana na maamuzi yao, ila waliwatahadharisha kutokuchukua maamuzi ya haraka na kuchukua hatua mikononi mwao, muhimu wafike huko wamuulize wasikie huyo mtu atasema nini,
kwasababu mambo ya kichawi, mara nyingi huwa hayana ushahidi wa moja kwa moja.
Baada
ya kauli hiyo, wale akina mama wakashauriana kidogo, na baadae tukaanza safari
ya kuelekea huko hospitalini, ocean road. Sisi tulipotoka tukawa tunajiuliza
tuingie kwenye gari gani, na bahati nzuri, mimi nikajikuta nipo kwenye gari la
mfadhili wangu wa awali,…pamoja na yote hayo, mfadhili huyu , kwangu mimi
sikumuona na roho mbaya kama hao wengine.
Wakati
tumeshaingia njia kuu, mara mama huyu akanigeukia mara moja na kunitupia jicho,
alinikuta natoa machozi, akaangalia mbele na kuendelea kuendesha gari lake
akiwa kimia, baadae akasema;
'Mimi
sipendi kuongea nikiwa naendesha gari, napendelea kuwa kimia, labda iwe ni kitu
muhimu cha kuongea, sasa ni hivi, nataka kukuuliza maswali, unijibu , na nataka
ukweli, usiwe mtu wa kuzunguka zunguka, huu ni muda wa kusema ukweli la sivyo,
yatakayotokea usije kumlaumu mtu..’akasema.
'Niulize
tu madam..'nikajikuta nimemuita madam, tofauti na nilivyozoea kumuita `mama’ na
hapo akanitupia jicho, hakusema kitu kwa mara moja, akawa kimia kwa muda hivi
huku akiendesha gari lake yeye alikuwa nyuma ya wenzake wote.., halafu akasema;
'Mimi sijakuamini kuwa mume wangu hakuwahi
kukufanyia jambo …au hata kukutongoza, au kukushika kwa nguvu, pia
sijakubaliana na wewe kuwa hukuwahi kumuona akiingia chumbani kwako, sasa
nataka kwa mara ya mwisho uniambie ukweli…’akasema na mimi kwanza nilikaa
kimia, halafu nikasema;
'Kiukweli mama, mengine yote ni hisia, na
hisia huwezi kusema ni ukweli, unaweza ukahisi kitu kumbe sio kweli, ila jibu
langu ni lile lile, kuwa mume wako, hajaweza kunifanyia kitu kama hicho, nikiwa
namuona, kwa macho yangu, mimi siwezi kumsingizia mtu ubaya wakati sijamuona…ndio
hivyo mama…’nikasema.
'Kwahiyo
hata siku ile nillipokukuta umelala sakafuni, yeye yupo juu yako, hukumuona au
wakati unafagia chumbani kwangu hajawahi kukugusa..?’ akaniuliza na hapo
nikajaribu kukumbuka yale matukio, na jibu likanijia hivi…
'Sikuwahi
kumuona…naogopa kusema hivyo,…macho ndio ushahidi unaoutaka, na macho yangu
hayakuwahi kumuona, huo ndio ukweli…mungu anajua zaidi…’nikasema hivyo.
'Na
haijawahi kutokea jambp la kuweza kumuhisi vibaya,…?’ akaniuliza.
'Hapana,
hajawahi…kwa maana mimi huwa siwachunguzi watu, kwahiyo inakuwa vigumu kwangu
kumuhisi vibaya, yeye kama wanaume wengine najitahidi sana kuwa mbali nao…’nikasema
na nilisubiria aniulize kuhusu mtoto wake, hapo majibu huenda yangelikuwa
tofauti.
'Kwahiyo
huwezi kumshuku kwa hiyo mimba, kuwa huenda kutokana na maelezo ya huyo rafiki
yako, inaweza ikawa ni yake…?’ akaniuliza nashangaa hakugusia kuhusu mtoto
wake.
'Nitamshukuje
sasa, mama hebu jaribu kunielewa, mimi naogopa kutenda dhambi, kumshuku mtu
bola ushahidi ni dhambi, au nakosea mama…’akasema hivyo.
'Mfano
kama aliyoyasema huyo mdada ni kweli, na ikatokea kuwa mtoto ni wake, labda
baada ya kujifungu avikachukuliwa vipimo, au huyo mchawi akalithibitisha hilo,
kuwa mume wangu anahusika, je wewe utachukua hatua gani..?’ akauliza na mimi
nikakaa kimia.
'Mimi kwa
hilo sijui, ninachoweza kusema, hayo yote ni mungu mwenyewe kapanga hivyo, nay
eye ndiye atanipa njia, maana mimi kama mimi nitasemaje, je nilikubaliana na
hilo, kama ningekuwa nimshikiriki kwenye makubaliano, au nilithibitisha, ningelisema
ningefanyaje, …ndio maana nachanganyikiwa..’akasema.
'Sawa
mimi nimekuelewa, pamoja na yote,…ila kwa hali ilivyo mimi siwezi kukusaidia
zaidi ya hapo, na pia siwezi kubeba huo mzigo, ni wewe mwenyewe ujipange, na
uhangaike, kutafuta jinsi gani ya kufanya, au unataka mimi nikusaidieje kwa
hilo..?’ akaniuliza
'Ndio
hapo, naona nabebeshwa mizigo ambayo mimi sijui imetokea wapi, na sijui
nitaenda wapi, labda natakiwa nimfuate mama yangu..kila nikiwaza naona iwe
hivyo, namuomba mungu , kama yawezekana iwe hivyo, maana mimi siwezi jamani,
siwezi hata kufikiria nifanyeje, kwa umri huu, na mambo kama haya ni mageni
kwangu..basi tu, nitazidi kuomba, japokuwa duwa la kuku halimpati mwewe…’nikasema
huku machozi yanaendelea kunitoka.
'Kwahiyo wewe unataka kusema nini, kuwa ni
heri ufe,..hahaha, kwa mtihani huo, ujue dunia hii imejaa mitihani mingi, huo
ni mwanzo tu, ..sikusemei mabaya, lakini umri utakavyokwenda, ujue utaingie
kwenye matatizo, wewe usione mimi nipo hivi, nab ado tuna uwezo, nimetokea
kwenye familia yenye uwezo, lakini matatizo, na mitihani ni mingi ajabu….’akasema.
'Sio
kwamba mimi nataka nife, ila nionavyo, ndivyo watu wanataka iwe hivyo,
najiuliza sana , ten asana kwanini wanatufanyia sisi hivi, tuna nini cha
kuwapa, tuna nini ambacho ni zaidi ya wengine, ..nashindwa kuelewa, ..mungu
mwenyewe ndiye anajua..’nikasema.
'Sikiliza
binti..wewe nimekuchukua kama binti yangu, na nilitarajia kwa vile mimi ndiye
nimekutoa nyumbani unekuwa karibu na mimi ikanieleza matatizo yako…katika
maisha haya vyovyote uwavyo, usikubali kuwa mnyonge kiasi hicho..pambana na
maisha na anzia hapa kuidai haki yako, mimi siwezi kukuambia fanya hivi, maana
mengine yanaweza kuja kuniathiri mimi, na ikifikia kwenye kupambana kudai haki
yangu ukiwa mbele yangu, tutapambana na wewe pambana kivyako…’akasema.
'Sasa mama nikuulize kitu…nachukulia kama mfano,
hivi itokee kuwa mimba ni ya mume wako, mimi sijui lakini nakuuliza wewe tu,
labda alivyosema mdada ikawa ni kweli, utachukua hatua gani kwa mume wako, au
kwa ki-…’hapo sikumalizia maana alinitupia jicho kuniangalia.
'Nichukue
hatua gani hahaha…unajua nimeliwazia sana hilo, nilitaka kuchukua hatua kama
tulivyoongea kwenye kikao, kwa hasira, lakini sasa…navuta subira, maana mambo
kama haya, yana mwisho wake, za mwizi ni arubaini, na mimi kama binadamu nina hatua
zangu za uvumilivu,..kwa hivi sasa sina haja ya kuchukua hatua yoyote, zaidi ya
wewe kuondoka, wewe swali hili nikugeuzie wewe..ingawaje umenijibu awali,…’akasema.
'Mimi
kiukweli jibu langu lipo pale pale… sijui, maana nitashindanaje na tajiri, na
akiwa labda kadhamiria, au kama ndio hivyo sio kwa utashi wake, na alishakataa
kata kata, na ni kweli kama ni kweli alivyoongea huyo mdada, sasa mimi
nitfanyaje hapo…’nikasema.
'Kwahiyo
utakaa kimia, je huyo mtoto utamleaje na hali kama hii, na usitarajia kwa hali
kama hiyo mimi nitatia mguu wangu hapo, dunia itaniona wa ajabu ni kama vile
tulipanga mimi na mume wangu,..ndio huruma ninayo, lakini …hapana, hilo kama ni
hivyo utajua wewe mwenyewe utakavyo mshawishi mume wangu, …ndio hivyo…’akahema
kama vile katua mzigo mnzito.
'Mungu
anajua zaidi mama, nashukuru wewe umekuwa mkweli wangu…na kama mungu
kanibebesha mtihani huu kwa maana maalumu, basi nitafanyaje, nitaubeba tu..na
nitajitahidi kumuambia huyo mtoto nitakaye mzaa, kuwa hana baba,…na mimi nina
imani kuwa mungu kama kanipa mtihani huu, bado nitamuomba anipe njia ya kuishi,
njia ya kumlea huyo mtoto…sitamtupa…’nikasema nivuta pumzi ya mtu anayelia.
'Wewe
ni mtu wa ajabu kweli, sijawahi kumuona, sijawahi kumsikia mtu anakubali
kirahisi hivyo, imani yako ni ya ajabu…mmh, wote tungelikuwa hivyo, dunia
ingelikuwa nyingine, lakini hayo si ya dunia hii nikuambie ukweli,…..’akasema.
'Sasa
wewe kama mama yangu ungenishaurije..nifanyaje kwa hatua kama hii…?’
nikamuuliza.
'Mimi
siwezi kukushauri kitu zaidi ya hivyo nilivyokushauri, kuwa upiganie haki yako,
usikubali kuwa mnyonge, maana haki wakati mwingine inabidi uipiganie, ili mungu
akuone kweli una nia hiyo, unanielewa hapo….’akasema.
'Nimekuelewa kama sikukuelewa,…mungu anisaidie tu,
unajua mama yangu aliniasa sana alijua dunia itanielemea, lakini alinishauri
sana ten asana, nisije kusema uwongo, na kitu kama sina uhakika nacho ni bora
nikae kimia tu…ndio maana najitahidi kuwa hivyo…’nikasema
'Sawa, ila kama huyo mchawi atakiri kuwa huenda
mimba ni yake, sisi tutakukabidhi kwake, mtajuana wewe nay eye ni nini cha
kufanya hayo ndiyo maamuzi yetu, na kama atasema ni ya mume wangu
halikadhalika, sisi tutakubadihidha kwa mume wangu mtajua namna gani ya
kufanya,..hilo nakugusia tu…’akasema
'Siwezi kukubali, kwa mamaumizi hayo,… hata kama
mimba ni yake, mimi siwezi kushirikiana na mshikirikia matu anayempinga
mwenyezimungu kiuwazi, mchai hapana, ni bora nibakia na mtoto wangu nihangaike
kivyangu…’nikasema
'Tunasemea kama yeye atakiri hivyo…maana yeye kama
hivyo ni kweli, ndiye anayefahamu ukweli wote….’akasema
'Mungu anajua zaidi, siwezi kujua
yajayo, kadara zake zitatenda, mimi kwa ufupi namuachia yeye aliyeyakadria
haya, sina zaidi mama…’nikasema.
‘Mmmh, kweli tembea uone,
sikubahatika kukutana na mtu kama wewe kabla, nikuambie kitu, dunia hii haipo,
kama wewe unavyofikiria hivyo, na imani ya kweli si hivyo tu, bado inatakiwa
juhudu za kimakusudi, maana kama ingekuwa imani ni hivyo watu tusingelifanya
kazi, mungu si atatupa riziki zetu, unahisi ni kwanini ado tunahangaika…’akasema.
‘Hata mimi nahangaika, sikuwahi kukaa
tu,…mama alinishauri nisiwe mvivu, sasa ndio nimekuja kufanya kazi kwenu
yametokea hayo, ningelifanya nini,…mfano kama ningechukulai hisia zangu tu
nikasema kutokana na hisia zangu tu huoni kuwa ningelivunja ndoa yenu, na sasa
hapo kama je sio kweli….mungu ataniadhibu sana, ndio maana nimeamua kusema
niliyoyasema.’nikasema.
'Haya
sawa, ila nikupe tu kama angalizo, mume wangu hawezi kukuoa, na hata kama mtoto
atakuwa ni wake, sio kwasababu ananipenda mimi, hapana, ni kwa vile lengo lake
ni mali, anajua akiniacha mimi atakosa kila kitu, akija kwako utampa nn, eeh,..utampa
mwili, eeh, mvuto wa ujana, lakini yeye pia anaangalia na maisha huko mbele
yatakuwaje,…au wewe mfano akikuchukua utamsaidia nini ili maisha yasonge
mbele..nikuonavyo wewe utakuwa unamwambia, msubirie mungu atawashuhia riziki….’akasema.
'Mimi sijasema namtaka mume wako, naomba hilo
unielewe mama, mimi sina wazo hilo
kabisa, yeye namuona ni sawa na baba yangu, hata kama mtoto ni wake, kamwe
sitaweza kufanya hivyo..yeye afanye ajuavyo, lakini sio kunichukua mimi, na
asitarajie kuwa mimi atakuja kuniomba….nimkubalie nikiwa na akili zangu hivi,
hilo asahau..kama ni yeye alinifanya hivi basi ashukuru sikuwa na akili zangu
timamu…’nikasema na yeye akanitupia jicho mara moja.
'Sawa,
labda eeh, najua yeye hajui lolote, mfano napo ingelitokea ni kwa kijana wangu,
maana hapo unasema hutamkubalia mume wangu kwa vile ni mzee, ni mkubwa wako,
mfano sasa ikatokea kuwa kijana wangu anahusika, kama alivyosema huyo mdada
rafiki yako…?’ akaniuliza.
‘Nikuulize
na wewe hilo swali , kama ikitokea hivyo, wewe utamkubalia mtoto wako anioe
mimi…?’ nikamuuliza na yeye akakaa kimia kwa muda, mpaka nikajua hataongea
tena, lakini baaadae akasema;
‘Siwezi
kukubali kamwe,..hilo sahau…’akasema.
'Kwasababu
gan, kwa vile mimi ni masikini au kuna sababu gani nyingine na hata kama mtoto
wako kanipenda mimi..?’ nikamuuliza.
'Hebu
wewe jiweke kwenye nafasi yangu, naona wewe una hekima sana, basi jaribu
kujiweka wewe ndio mimi, je ungelikubali hilo litendeke…?’ akaniuliza.
'Kama
ingelikuwa mimi ndio wewe, kwa kutoka moyoni mwangu, na uelewa wangu mdogo,
mimi ningelikubali tu, kwasaabbu gani, ili masikini waweze kusaidiwa, matajiri
wawaoe masikini na waolewe na masikini ili kusaidia kuwawezeshana, ili jamii ya
kimasikini ipungue..na kuwe na usawa, kusiwe na kudharauliana…’nikasema na hapo
akatulia kwa muda tena, halafu akasema;
'Kwahiyo
hilo ndilo lengo lako…?’ akaniuliza na mimi kwanza nikabakia kimia nikiwaza
kwanini nimesema hivyo, sikujua yeye atalichukulia hivyo, na sikusema hivyo
nikimaanisha hivyo, baadae nikasema;
'Hapana
mimi hilo sio lengo langu kabisa, tumeongea kama ingelikuwa hivyo, na sizani
kama ndio hivyo, na hata kama itakuwa hivyo bado mimi sitakubali kwa maana kuwa
nitakuwa nimejirahisisha kwasababu ya mali, na matokea yake nitakuwa mtumwa wa
watu wengine…’nikasema
‘Haa..haya
ngoja tuone maana tunakaribia hospitalini, mimi hapa nilipo hasira zinanizidi
kiasi jinsi gani nikikutana na huyo mtu nitakavyofanya, sijui…huyo mtu
kaniharibia maisha yangu na familia yangu…huyo mtu kaniweka kwenye wakati mgumu…na
kama kweli aliwahi kuingia ndani kwangu na kufanya hivyo…nina ushahidi, lakini
hauna mshiko,…’akasema
‘Una
ushahidi gani, kama unao kwanini usiende polisi…?’ nikauliza
‘Ushahidi
una utata, utaniumiza badala ya kusaidia, ..ngoja tukutane na huyo mtu, nitajua
la kufanya huko tukifiika, ..nikipata mwanya tu, nitakachokifanya watu
hawataamini…’akasema
‘Upo
kama mimi madamu…’nikasema na tukawa tumeshafika
*************
Huku
kwa upande mwingine mdada alipanda gari la madamu wake, na waliendelea kukaa
hivyo hivyo kimia hadi walipokaribia kufika, na madam akasema;
‘Unajua
tangia ulipofika kwangu nilikuwa nahisi mwili ukinisisimuka, unajua wewe
uliletwa kwangu bila hata ya mimi kupata muda wa kukuchunguza, na hasa
ulipofika na kuanza kuongea mambo ya kishirikina, nilianza kukuhisi vibaya…’akasema.
‘Lakini
mimi sio mshirikina…’akasema mdada.
‘Unajua
maana ushirikina,..ni kuamini mambo bila kupitia kwa mola wako, unakwenda kwa
mwanadamu mwenzako ati akupigie ramli, unaamini mambo yatatokea hivi kwa sababu
hii, badala ya kuamini kuwa mambo yanayotokea ni kwa matakwa ya mungu…’akasema.
‘Kwahiyo
hata ukiibiwa,eeh, hata…au ndio hata mume wako akifanya mambo usiyoyataka, au
kama ilivyotokea huko kwa huyo mwenzangu, kwani hajui kabisa kilichotokea, hayo
tuamini tu kuwa ni mungu kapenda, tusihangaike …si ndio hivyo..tatizo sis
hatujasoma, na ..ndio hivyo madamu…’akasema.
‘Ndio
hivyo nini…sikiliza kusoma au kutokusoma hakukuruhusu wewe kujiingiza kwenye
mambo ya nguvu za giza, unajua ramli, au kuamini mambo ya uchawi ukayafuta,
ukayaamini, ni ushirikina, hata bila kusoma utaelewa hivyo tu..’akasema
‘Mimi
niliamua kwenda hivyo baada ya kukutwa na matatizo, nikahangaika hospitalini
bila mafanikio, naota ndoto mbaya..nahisi kuna watu wana…nikaba,
wananidhalilisha, sasa kwa hilo kama hiyo ukiongea hospitalini watakusaidia
nini…ndio maana nikapata ushauri niende kuhangaika, na ndio nikamgundua mbaya
wangu…’akasema
‘Huyo
mchawi ndio mbaya wako, kwahiyo ulimgundua kwa kupitia kwa hao waganga wa
kienyeji au..?’ akauliza
‘Yule
sio …ni mtaalamu, anakuangalai hivi tu, anaanza kukuambia matatizo yako..na
anakuambia mambo mengo ambayo ni kweli yapo , yamekutokea, ..sijaona akipiga
ramli,…’akasema
‘Ulikwenda
huko lini..?’ akauliza na mdada akajua ni swali la mtego akasema;
‘Kabla
sijaja kwako…’akasema
‘Na
hujawahi kwenda huko tena..?’ akauliza
‘Sijawahi,
maana sina pesa za kumlipa hata deni la kwanza sijamaliza…’akasema
‘Mfano
sasa tukifika kwa huyo mtu wako utafanyaje, maana ndio hivyo kasema
usipomsaidia pesa za matibabu hataondoa, nini vile kitu gani..zandi…..’akashindwa
kutaja
‘Mazindiko…’akamalizia
mdada
‘Ehh,
hayo wanayawekaje..?’ akauliza
‘Mimi
sijui ..wanawekaje…’akasema
‘Kwahiyo
anakuona kila unachokifanya..?’ akauliza
‘Ni
kitu kama hicho…’akasema
‘Nitamuua
huyo mtu, ina maana atakuwa anatuona hata tukiwa uchi..?’ akauliza
‘Kama
anaweza kufika usiku bila yaw ewe kukuona akakuchukua, akakufanya atakavyo,
unahisi hawezi kukuona kwa kila ukifanyacho…’akasema mdada
‘Weee,
anaweza kufanya hivyo, sio kweli, na wala siamini, unasikia hayo mambo ni
uwongo, na kama yapo labda uwekwe vifaa vya kitaalamu, huyo kakudanganya,
sikiliza mume wangu ni askari, ana cheo kikubwa tu, atamtesa mpaak atasema kila
kitu..hata hivyo sizani kama nitasubira mume wangu aje, …nitajua cha kumfanya,
watu kama hao hawastahiki kuishi, unasikia,…yaani umenifanya nihisi vibaya
sana. Maana anaweza kuwafanya vibaya watoto wangu, na juzi niliota ndoto mbaya
sana,…nilimuona,..na wewe, …’akasema akimuangalia mdada kwa macho makali
‘Na
mimi..” akauliza
‘Ok
tumefika…ila kiukweli naanza kuhisi kuna ukweli fulani, ngoja nifike nimuone
kama ndio yeye, atanitambua…mtanieleza mlichokuwa mkikifanya…’akasema sasa kwa
sauti yenye hisia za chuki.
‘Uliniona
na mimi, mungu wangu, uliota, anakufanya nini, na mimi nafanya nini…?’akauliza
mdada kwa shauku, lakini akionyesha wasiwasi, lakini huyo mama hakujibu na gari
likawa limefika hospitalini.
NB: Naishia
hapa kwa leo..
WAZO LA LEO: Hakika dhana mbaya ni madhambi katika madhambi
makubwa, dhana mbaya humsukuma mtu kujenga chuki na kuleta uadui kwa wenzake,
sio vizuri kushutumu, kusakama, au kuchukua hatua kwa kutegemea dhana tu, kwani
hebu jiulize hapo, kama hiyo dhana sio
kweli, kiasi gani huyo mtu au kundi la watu waliodhaniwa hivyo walivyumia, je hayo maumivi unaweza kuyalipa.
Dunia sasa hivi
imegubikwa na tabia hiyo, watu kudhaniana ubaya, kwa malengo ya kujenga fitina,
watu wanakosana, mataifa yanapigana, damu zinamwagika, wasio na hatia wanapata
taabu, je hi dhuluma hatuioni ilivyo mbaya. Tumuombe mola wetu atuongeze kwenye
njia sahihi, na ubaya uwe dhahiri ili watu wasiingie kwenye dhana mbaya, na ikiwezekana
ubaya huo upotee, na wenye kutenda hayo watubu, na kukiri,na kujirudi… ili
dunia iwe salama na haki.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment