‘Najua mumekusanyika hapa kuhusu yanayotokea humu ndani,
najua nyote mtakuwa mumeninyoshea kidole mimi, kutokana na tuhuma za huyo mtoto
wenu kuwa mimi ni …mchawi au namini ushirikina, najua kuna mengo mnataka
kusikia kutoka kwangu…’akaanza kuongea huyo binti.
‘Tunachokitaka kutoka kwako ni ukweli, je hayo yanayosemwa
ni kweli…?’ akaulizwa
‘Yapi hayo....kuwa mimi ni mshirikina, kuwa labda nimemfanyia
kitu mtu humu ndani, au si ndio hivyo,..?’ akauliza.
‘Hapana sisi hatuna maana hiyo, labda utulie tukuulize
maswali utujibu kwa ukweli unavyoujua wewe…’akaambiwa.
‘Mimi nimekuja kuusema ukweli... ili niwahi kazini
kwangu, najua labda itakuwa ni hatari kwangu, lakini sina jinsi, kutokana na wema niliotendewa na hawa watu,...na.. labda nikiri kuwa kweli haya yanayotokea humu chanzo ni mimi…’akasema na
watu wakamkodolea macho.
‘Tuelezee kwa vipi?
‘Ehee….ngoja nianze tokea awali ili mnielewe vyema japokuwa naogopa nitachelewa huko kwa mabosi zangu….’akasema.
‘Sawa endelea, kwa haraka kidogo, ili usichelewe….’akaambiwa.
‘Mimi nilifika kwenye nyumba hii, nikitokea mitaani,..' akaanza hivyo.
'Huyu baba, ndiye alinikuta siku moja nikiwa na hali mbaya sana, nina njaa, naumwa,
akanionea huruma, bada ya kunihoji hoji, …akaninunulia chakula na kunipeleka
hospitalini. Huko nikalazwa,…nililazwa wiki hivi, na yeye alikuwa akija kunijilia
hali na hata kuniletea chahakula…kiukweli niingiwa na faraja, na badala ya
kufurahi nikawa nalia…’akatulia kidogo.
‘Kwanini sasa ulie..wakati mtu kajitolea kukusaidia…?’
akaulizwa.
‘Unajua huwezi kuelewa haya mpaka yakukute, nililia
kwasababu nilijiuliza hivi sisi tulikosa nini, …ina maana na mimi nilitakiwa
niwe na baba kama huyu, je yupo wapi huyo baba yangu, haya mama alifariki,
lakini …..aah, sitaki nikumbuke, nililia kwakweli, na…namshukuru mungu…japokuwa
sikuelelewa kwenye mazingira ya dini, lakini najua mungu yupo….’akatulia.
‘Ehe ikawaje…?’ akaulizwa.
‘Baada ya wiki hivi nikaambiwa nimepona, hapo nilitamani
niwadanganye pale hospitalini kuwa sijapona ili niendelee kubakia hapo, ili niweze kupata chakula cha
kupikwa sio cha kuokota majalalani…ili nilale kitandani, sio kulala kwenye
maboksi, huku mbu ndio marafiki zako…ili..jamani msiombee maisha haya, nyie
mliojaliwa kuwa na wazazi, mshukuru sana….’hapo akageuka kuangalia huku na kule kama anamtafuta mtu, na
watu walibakia kimia.
‘Je utakwenda wapi ukitoka hapa..?’ akaniuliza huyu mfadhili
wangu, alipofika na kusikia kuwa natakiwa kuruhusiwa nimeshapona.
‘Mimi sijui pa kwenda, sina wazazi, sina ndugu, …nyumbani
kwangu ni mitaani tu…’nikasema na huyu mfadhili akaniangalia kwa jicho la
huruma akasema;
‘Oh,… basi ngoja nitaongea na mke wangu tutaona jinsi gani
ya kukusaidia…’akasema na aliondoka siku hiyo, akijua nitaruhusiwa, lakini
nahisi alishindwa kunichukua moja kwa moja mpaka akaongee na mke wake…mimi
nilibakia pale nikisubiria taratibu za hospitalini, ili niweze kuondoka na
kurejea mitaani, na haikupita muda docta akaja akaniambia nipo huru kuondoka.
‘Nikiwa nimekata tamaa,…nikijua sasa ndio maisha yangu tena
yameanza, mara nikaona gari likija, muda huo nimeshatoka nipo nje, napiga plani
za wapi nianzie maana maisha yetu ilikuwa kuomba omba, …kutukunwa, na usiku ku…zalilishwa,
tulishazoea hivyo.
Gari likasimama, kumbe ni huyu baba wa watu, sasa alikuwa
kaja na mke wake, wakaniuliza nimeambiwaje, nikawaambia, wao wakaenda kuongea
na docta, kuona kuwa kila kitu kipo sawa, kama kuna dawa, au gharama yoyote,
walipomalizana huko, wakaniambia niingie kwenye gari.
Basi ndio wakanichukua kwenye gari lao hadi nyumbani kwao,
ndio nikanza maisha ya kuishi kwenye nyumba, sisi makazi yetu yalikuwa mitaani,
vichochoroni,…..mara ya kwanza naingia kwenye nyumba nzuri, bila kutukunwa, kwa
kukaribishwa na kuulizwa nitakula nini..kwanini machozi yasinitoke, nililia
sana..nililia mpaka wenyeji wangu wakashangaa, wakaniuliza nalilia nini tena..,
na mimi niliwajibu tu;
‘Nyie acheni tu…nalia, nimemkumbuka mama yangu, ….’nilisema
hivyo, wakajua ni hivyo, lakini sikuwa nalia kwasababu hiyo tu, nilikuwa nalia,
nikijiuliza maswali mengi,…na sikuamini kuwa hata siku moja nitakuja kupata
fadhila kama hizo, mungu awazidishie watu kama hawa wenye moyo wa upendo….’akasema
na aliyeitikia amina alikuwa kiongozi wa dini.
‘Kiukweli nilifika kwa watu hawa nikiwa sina mbele wala
nyuma, nilifika hapa mchafu sijui hata kuoga, nikaambiwa nikaoge, nikapewa nguo
za kubadilisha,..nikafundishwa mambo mengi tu ya maisha,…japokuwa kiukweli mimi
sio mvivu, kazi za ndani, kuosha vyombo kufagia, nilifundishwa na mama yangu,
navijua sana, lakini yale maisha ya watu wenye uwezo, umeme…na vitu vya kisasa,
nilikuwa sijui kuvitumia.
Kwa haraka sana nikazoea maisha hayo mazuri, na unajua tena,
ukitoka kwenye shida ukapata raha, mwili hubadilika kwa haraka sana…nikawa
binti mrembo, watu , hasa wanaume wakawa wakiniangalia kwa macho ya tamaa,…sisemi
haya nia mbaya, lakini ndivyo ilivyokuwa, hata wafadhili wangu waliniambia
hivyo, kuwa mimi ni binti mrembo sana…mimi sijui…’akatulia.
Kuna kipindi niliona mabadiliko kwa wafadhili wangu hasa
kijana..hahaha, hivi yupo wapi, samahani kwa hilo, ila inabidi niseme tu,
nilivyoona mimi, labda nimekosea lakini ndivyo ilivyokuwa, sio kama ilivyokuwa
awali, nikaona macho ya aina yake, kwangu mimi niligundua ni macho ya namna
gani,…maana mitaani, na maisha niliyoishi nilijifunza mambo mengi bado nikiwa
na umri mdogo….’akatulia.
‘Ningelipenda huyu kijana wa humu ndani awepo ili nisije
kuonekana mimi ni muongo maana mengi anayafahamu na aje kuyathibitisha haya nitakayoyasema,
na ili baadae litakolotokea, maana ndicho kilichonisukuma hadi kuja hapa,…ili nisije
kulaumiwa…’akasema.
‘Ehee, hebu muiteni
huyo kijana…una maana huyu kijana wa humu ndani…?’ akaulizwa.
‘Ndio namuita kijana japokuwa kwa umri tupo sawa, tulizoea
kumuita hivyo …’akasema huyo binti, na Kijana akaitwa, na huyo kijana
alipoingia tu na kumuona huyo binti, akashikwa na mshtuko kidogo, halafu akasema.
‘Huyu mdada msimuamini kabisa, huyu mshikirina huyu…atawadanganya
na kubadili badili maneno, mimi simuamini kamwe…’akasema huyo kijana.
‘Ndio maana nimekuja unionyeshe huo ushirikina wangu, hiyo
kauli yako mimi siipendi, nakuambia kabisa……na nitaongea ukweli wote leo,
…uukane sasa, hata yale uliyosema nisiseme nitasema yote,….mimi sio mshirikina
kama unavyohisi wewe…,na kama unadai kuwa mimi ni mshirikina nataka unionyeshe
huo ushirikina wangu la sivyo tutafikisha kubaya….’akasema huyo binti.
‘Aaah, wewe tulia, hayo hayana nafasi hapa endelea kuelezea
historia yako ya kuishi humu ndani, ilitokea nini, unasema ulipoanza kupendeza
kijana akaanza kukutamani, kwani humu ndani alikuwepo kijana peke yake wa
kukutamani, hebu tuambie hapo una maana
gani…?’ akaulizwa.
‘Ni kweli, kwasababu kijana ndiye tulikuwa naye wakati
mwingi, wengine walikuwa wakija na kuondoka, na hata baba alikuwa anaonekana
usiku tu na siku za wikiendi, kwahiyo mtu niliyekuwa naye karibu alikuwa huyu
kijana…kwani nadanganya, aseme yeye mwenyewe, huyu kijana maana yeye ndiye
aliyenianza kunitongoza, nikamkatalia, akaanza kunifanyia vitimbwi, aseme
ukweli…’akasema
Kijana akawa kimia tu, hakusemi neno hapo, ila mama yake
aliniangalia kwa macho ya hasira, akitaka kusema neno, lakini mdada huyo
hakumpa nafasi akaendelea kuongea.
.
‘Kijana huyu akaanza kunisemea kwa wazazi wake kuwa mimi
usiku natoka kwenda kufanya uhawara, au huo ushirikina anaousema,..wakati hata
siku moja sijawahi kufanya hivyo, kisa nimemkatalia.., …kwanini niende nje
wakati wanaume wapo humu ndani,…eti, tena wenye pesa, lakini nikavumilia, na
siku moja kijana akaanza visa vyake, muulizeni alinifanyia nini…’akasema.
‘Wewe elezea, alikufanyia nini…?’ akaulizwa
‘Alitaka kunibaka, nikapiga ukelele…’akasema
‘Mwongo huyu, …ananisingizia, hata siku moja sijawahi
kufanya hivyo, yeye usiku alikuwa akifanya madawa yake, nikamfuma, akiwa nje
uchi…si umetaka niseme ….na…siku anayosema nilitaka kumbaka alikuwa akipiga
kelele, nikawa namshika, maana alikwua akigonga gonga,…’akasema kijana.
‘Hahaha…eti nikiwa nje uchi, wakati ni mambo yenu humu
ndani,…. ndio yalinifanya nitoke nje, nikiwa sijitambui,…nimejikuta niko nje
uchi,….na kama ningeliendelea kubakia humu , bila ya kwenda kuhangaikiwa sijui
ingelikuwaje,…labda ningekuwa kichaa...kuna kitu kilikuwa kikiniingia kichwani
nakuwa kama nimechanganyikiwa, navutwa kufanya mambo nisiyoweza kuyafanya
nikiwa na akili zangu, nilikuwa sio mimi…’akasema.
‘Oh, kwahiyo…sio huyu kijana ni kitu kingine kilitokea kwako,
?’ akaulizwa.
‘Huyu kijana ana yake, lakini kiukweli mimi niliambiwa
matatizo hayo yametoka huko kwetu, kuna watu wananitaka nirudi
nyumbani…nikaolewe huko, kuna mjamaa mmoja anaogopewa sana huko, eti aliniona
akanipenda, kipindi fulani nilikwenda huko, …wakati nimeshapendeza, nilipata
ruhusa , na kwenda kuona asili yetu, nikiwa na rafiki yangu mmoja wa kutokea
huko kijijini walipotokea wazazi wangu...’akatulia.
‘Akamuambia huyu rafiki yangu aniambie kuwa yeye anataka
kunioa, mimi nikamkatalia, kwanza nilikuwa mdogo, japokuwa umbo langu, lipo
hivi, naonekana mkubwa lakini sio sawa na umri wangu…’hapoa akatulia kwa muda
kidogo.
‘Sasa ikawaje, ?’ akaulizwa.
‘Nilimkataa, na ndipo akasema atanikomoa…na huyo rafiki
yangu alinisihi nikubali, kwani nispokubali, huyo mtu anaweza kunifanyia vituko…mimi
nikamwambia sitaki, na huko sitarudi tena, bai huyo jamaa akamwambia huyo
rafiki yangu, atanifanyia mambo mpaka nitakubali, na huko ninapoishi wote
watakoma ubishi, mpaka wanifukuze.
‘Mimi …nilikuja nikawaambia humu ndani, ndio wakaanza
kuniita mimi mshirikina, hasa huyu kijana, mama aliniambia kama nina tabia hiyo
ya kishirikina niache kabisa, lakini ujumbe niliufikisha…’akasema.
‘Kwahiyo ulimwambia mama kuhusu huyu mzee….?’ akaulizwa.
‘Kwanza nilimuambia huyu kijana maana ndiye nilikuwa karibu
naye…’akasema
‘Kwanini ulikuwa karibu naye..?’ akaulizwa.
‘Nilianza kusema awali, kuwa nilianza kupendeza, na huyu
kijana akawa aknitongoza, kila siku, kiukweli kama …isingelikuwa ni tofauti za
hali, ningelisema nikubali, si nitaolewa kwenye nyumba ya watu wanaojiweza,
lakini nafsi ilinisuta, nikamkatalai kata kata…sasa nilipopata taarifa hiyo ya
huyo mzee, nikamwambia kijana.
‘Umenikataa mimi, sasa nenda kaolewa na wazee wa kijijini….’akaniambia.
‘Mimi siwezi kuolewa huko, na wala sitaki kuolewa,…’nikamwambia.
‘Ila kuna kitu nataka umwambie mama, huyo jamaa kasema
nisipokubali kuolewa na yeye atanifanyaia kitu kibaya, na hata nyumba hii
mtafanyiwa hivyo hivyo…’nilimuambia hivyo, na yeye akasema, huyo mzee hawezi,
hayo ni mambo ya kishirikina, na neno hilo lilianzia hapo.
‘Na haikupita muda, huyo jamaa akanitembea usiku, nikiwa
usingizini sijijui…’akasema.
‘Una maana gani hapo,
kukutembea usiku, kwa vipi..?’ akaulizwa.
‘Kutokana na nilivyoambiwa, huyu jamaa ni mchawi, huko
kijijini wanamfahamu sana, na akitaka jambo lake ni lazima alipate, kwahiyo
alivyonitaka mimi na kukataa, ndio akawa anakuja usiku, humu ndani…’akatulia.
‘Unamuona..?’ akaulizwa.
‘Siku ya kwanza nilimuona, …lakini ni kama njozi, na
akaniambia ..sasa nimekuja, wewe si hunitaki, sasa nitakufanyia mambo mabaya,
mpaka ujute kuzaliwa….nikawa sijui nifanyeje, na akasema, yeye, nia yake ni
kunioa, ila kwa vile sitaki, basi atawatumia watu wa humu ndani kunizalilisha….’akatulia.
‘Watu gani…?’ akaulizwa.
‘Baba na kijana…’akasema na watu hapo wakahema.
‘Ni kweli alifanya hivyo…?’ akaulizwa.
‘Hahaha, hivi hamuamini hayo…muulizeni mama aliona nini,
aliniambia alimuona baba akija chumbani kwangu, mimi nilimkatalia kwasababu
yaliyokuja kutokea baadae, mimi nilikuwa sioni, nakuwa kama nipo kwenye njozi,…siwezi
kufanya lolote zaidi ya ufanyiwa hayo anayoyataka huyo mzee….’akasema.
‘Lakini uliambiwa, hujawahi kuona kwa macho yako…?’
akaulizwa.
‘Kiukweli hivyo vitendo, nafanyiwa, ila wanaonifanyia
siwaoni, maana ninakuwa usingizini…’akasema.
‘Na sikuyajua hayo, mpaka nilipokuja kuambiwa…ila siku ya
kwanza huyo mzee nilimuona kwenye njozi zangu, akiniambia kuwa atakuwa anakuja
kila siku kunifanyia vitendo vibaya, na atawatumia watu wa humu ndani,
kunizalilisha, huku yeye akiniangalia, na kunikaba….’akasema.
‘Kwahiyo ni kweli kuwa baba mwenye nyumba na kijana huwa
wanakuja usiku na kukufanyia hivyo, bila hata yaw ewe kujua, …kuwaona..kujua
unajua kwa vile uliambiwa, sio ila wanapokuja huwaoni kwa sura si ndio hivyo..?’
akaulizwa.
‘Ndio wanakuja, muulizeni hata mama aliwahi kwuafuatilia
akawaona, anasema ana ushahidi wa kuonyesha hayo, mimi kiukweli sijawahi
kuwaona ila nakabwa, ..na kuhisi nazalilishwa, na watu nikiwa kwenye ndoto..ni
kama ndoto…’akasema
‘Unasema nini wewe…?’
aliyeuliza sasa ni baba mwenye nyumba.
‘Nasema nilivyoambiwa, na yanayonikuta,…huyo jamaa lengo
lake ni kunikomoa, unielewe hapa, ndio maana nimesema sasa nataka kuufichua
ukweli, sasa iwe ni kazi kwenu…kama mtahangaika sawa, kama mtakaa kimia sawa,
ila kama msipohangaika ndoa yenu itakuwa matatani, ndivyo alivyoahidi kwani
alitaka kunioa na nyie mlinishauri nikatae…’akasema.
‘Kwani wewe ulimwambi ahivyo, kuwa umeshauriwa na wafadhili wako usikubali....?' akaulizwa
'Hata, sijaongea naye, unajua yeye mara nyingi alikuwa akiongea na huyo rafiki yangu sio mimi, sasa sijui alifahamuje hivyo...siwezi kujua,...'akasema
'Kwahiyo kwa kifupi, haya yote yanayotokea humu ndani kumbe kisa ni wewe?’
akulizwa.
‘Kisa ni mimi ndio, kama nilivyoambiwa,….ndio maana nimekuja kuwaambia, ili isje
kujulikana baadae mkaniona mimi ni mbaya, au kama anavyoniita huyo kijana kuwa mimi ni mshirikina,…na nilimuambia mama, yeye
hakuniamini, na wakafanya mbinu niondoke humu, wakijua nikiondoka huenda mambo
hayo yataisha,… lakini huyu mtu alishasema atawakomoa na nyie mlionishauri
nisiolewe na yeye…’akasema.
‘Sasa hebu tueleze inakuwaje, yaani huyu jamaa si anaishi
huko kwenu mbali kabisa anawezaje kufika huku usiku, na anawezaje kumchukua
huyu baba mwenye nyumba atoke naye waingie kwako na kuanza kukusumbua, si ndio
hivyo, yeye anasafiri na nini hadi huku..?’ akaulizwa.
‘Ina maana hamuamini hayo mambo, mimi pia nilikuwa siamini,
lakini anakuja kweli, ananifanyia hayo wanayofanya, na je kweli mama hajawahi
kumuona baba akiingia chumbani kwangu susiku….?’ Akauliza akimuangalia mama.
‘Wewe ndio utuambie…’akaambiwa.
‘Huyu jamaa ana njia zake za kusafiri , niliambiwa anasafiri
kwa njia za kichawi, usiku, na kila mara anafika hapa,…sasa anasafirije mimi
sijui,….’akatulia.
‘Na eti wewe mdada, haya mambo hayayajakutokea na wewe…maana
alisema na yoyote atakayeingia humu naye atakumbana na matatizo hayo, na hasa
baada ya mimi kutibiwa nasikia alisema keshapata badili yangu, ..lakini hao
watu waliosababisha yote hayo, ataendelea kuwasumbua mpaka wakome ubishi…’akasema.
‘Haya hebu tuambie ukweli, katika siku zote ina maana hukuwahi
kumuona baba mwenye nyumba akiingia chumbani kwako usiku,..?’ akaulizwa.
‘Tatizo ni kuwa huyo jamaa, anapokuja nyumbani kwako, wewe
mlengwa huwezi kumuona labda uwe umezindikwa,..au una imani safi ya dini, wapo
wenye imani za dini mungu anawalinda, hawezi kufanyiwa mambo hayo, lakini wengi
wetu imani zetu ni haba, kama mimi sikuwahi kufundishwa dini, nikamjua mungu,
nikajua kujilinda kwa kupita kwa mwenyezimungu….’akasema.
‘Sasa akija anaingia ndani, sote tumelala, hakuna anayweza
kumuona, na wanafanya mambo yao, unachohisi ni kama kukabwa, maana wanakuzuia
usije kuzindukana,..na wakimaliza kazi yao wanaondoka huku nyuma ukizindukana
usingizi unahisi athari hizo,…alinifanyia hivyo, lakini kwa kupitia kwa baba
mwenye nyumba na kijana wake…’akasema.
‘Hatujakuelewa hapo…’akaambiwa.
‘Ni hivi nia yake ni kunikomoa mimi…, kwahiyo anachofanya
akija, anawavuta wawili hao wakiwa usingizini, wanakuja kwangu,
wananizalilisha, huku yeye akiniangalia na kunikebehi,…’akasema.
‘Sasa akifanya hivyo, wewe huoni, na wala hujui, huwaoni hao wanaokufanyia hivyo, sasa yeye anapata faida gani..?
‘Si ndio hivyo,…mimi silali kwa raha, nahsi nakabwa, ni yeye
ananikaba,…huku hao wawili wananizalilisha, yeye anafurahia hivyo,…mimi naona
kama hamuniamini, sasa ni hivi mkitaka muamini kama hamtaki shauri lenu, mimi
naondoka…’akasema.
‘Ngoja kwanza..’akasema kiongozi wa dini pale huyo msichana
alipotaka kuondoka.
‘Ningoje nini tena hapa, huo ndio ukweli wenyewe hangaikeni …’akasema.
‘Nasikia wewe uliwahi kupata mimba, ni kweli si kweli..?’
akaulizwa.
‘Ndio nina mimba mpaka sasa, ila yeye alinifanya nisiione
hiyo mimba, nikaenda kuangaikiwa, nikapona na huyo mzee akasalimu amri baada ya
mimi kuhangaikiwa, na akaja kuniachia, sasa yupo kwa wengine sio mimi tena,
labda kwa huyu mdada hapa, kama haamini basi,…ila mimba nilikuwa nayo ikapotea,
….’akasema.
‘Kwa vipi? Akaulizwa.
‘Nilitaka kuitoa, kwasababu nilimbiwa nitazaa kioja sio
mtoto kamili anaweza akawa shetani, huyo mzee kaniwekezea shetani tumboni…,
ndio nikaona niwaambie hapa wanisaidie tuitoe, tukaitoa, kumbe yote ilikuwa
kiini macho tu, ikaonekana nimeharibu hata kizazi, kumbe ni huyo mzee
ananichezea, hata hospitalini waliona kizazi kimeharibika, lakini wiki
iliyopita baada ya kutibiwa, nimeenda kupimwa , tatizo hilo halipo tena,…’akatulia.
‘Kwahiyo bado una mimba?’ akaulizwa.
‘Ndivyo walivyosema hospitalini kuwa bado nina mimba, haikutoka…’akasema.
‘Sasa mimba hiyo mimba ni ya nani..?’ akaulizwa.
‘Hapo mimi sijui…’akasema.
‘Kwa vipi, maana kama ni hiyo ya awali ilitoka sasa hiyo
uliyo nayo, utakuwa umeipatia wapi..?’
‘Nasema mimi sijui tusubirie nizae, kiumbe kikitoka
tutakipima na ukweli utajulikana ni mimba ya nani…na safari hii siitoi, …sitaki
kuja kuharibu kizazi changu….’akasema.
‘Hebu kwanza naona unataka kuharibu ukweli, nataka unijibu
kwa uwazi,..je mume wangu aliwahi kuingia ndani kwako mkafanya uchafu wenu..?’
aliyeuliza hivyo ni mama mwenye nyumba.
‘Mimi sikuwahi kumuona, unielewe hapo, nilikuja kuambiwa
kuwa wawili hao, wanakuja kwangu, kwa kuongozwa na huyo mzee, wakiwa hawajijui,
na kunifanya wanachoamrishwa kukifanya, sasa kama waliingia , hawakuingia, mimi
sijui, niliambiwa hivyo, kama huamini shauri lako….’akasema.
‘Usitake kunitania wewe, sema ukweli wako, kwanza umeanza kusema mume
wangu na kijana walianza kukutamani, hiyo kauli inaashiria kuwa wewe ulikuwa na
njama nao, sasa nataka useme ukweli la sivyo, nitakuitia polisi kuwa wewe
unakuja kwenye majumba ya watu na kuharibu ndoa za watu..’aliyesema hivyo ni
mama mwenye nyumba.
‘Waite hapo polisi,..nenda kawaita na mimi nitawaambi ahuo
ukweli wote,… kama wataweza kukusaidia haya,….hivi mimi kuamua kuwaambia huu ukweli
ndio nimekuwa mbaya, sawa, waite nikafungwe, nyie si mna pesa zenu, ila nazidi
kuwatahadharisha, humu ndani hakuna usalama, huyo mzee keshafanya humu ndani
ndio makao yake …hangaikeni …’akasema sasa akitaka kuondoka.
‘Kijana wewe unasema ulimuona huyu mdada akifanya mambo ya
kishirikina akiwa uchi, sawa si sawa ?’ akaulizwa kijana.
‘Ni kweli nilimuona usiku akiwa uchi,…na sio mara moja,
aliniambia kuhusu huyu mjamaa huko kijijini, mimi sikuamini, na hilo la kuwa
tunakwenda usiku kwake, niliona ni mambo ya kishirikina, ila, yalinipa mawazo
sana, sikupenda kuwasumbua wazazi wangu…’akasema.
‘Ulipomuona ulifanya nini..?’ akaulizwa.
‘Nilishindwa kufanya lolote, nilitaka kupiga kelele au
kumuendea lakini sikuweza kabisa, ilikuwa kama nimenatishwa,…’akasema.
‘Je wewe ulishawahi kuingia chumbani kwake usiku ?’ akaulizwa.
‘Ndio, nilitaka kuhakikisha kuwa kweli huyo mtu ni
mshirikina au la…na siku zote nilipoingia nilimkuta ndani kalala…’akasema.
‘Ila uliwahi kumuona nje, akiwa uchi..?’ akaulizwa.
‘Ndio..?’
‘Alikuwa akifanya nini..?’akaulizwa.
‘Kasimama tu, au kachuchumaa, au anatembea tembea, ni kama anasubiria kitu…lakini
sikuweza kufanya lolote, maana nilikwua kama nimegandishwa….’akasema.
‘Oh…sasa hili ni tatizo…’akasema mzee mmojawapo.
‘Wazee, huyu binti ni muongo, nahisi kuna kitu
anatuficha….’akasema mama mwenye nyumba.
‘Kama ni muongo, au ni mkweli, sisi tutakuja kumjua
tu,….watu kama hawa hawawezi kushindana na mungu, sisi hatutakwenda huko kwa
waganga wa kienyeji, sis tunafanya yetu kwa kumtegemea mungu, na yote haya
yatakwisha…ila tunachotaka ni nyie wawili mkubaliane, muwe kitu kimoja, maana shetani
lengo lake ni kuharibu ndoa za watu, na ndio matokea yake haya, niliwaambi
awali kuna kitu nimegundua, sasa kimejitokeza, na haya yataisha kama mtaungana
na kuelekeza nguvu zenu kwenye imani ya kweli…’akasema kiongozi wa dini.
‘Sasa mimi nakwenda…’akasema huyo binti.
‘Sawa unaweza kuondoka, ila tutakihitajia tena,…’akaambiwa.
‘Hahaha, kama hamjaamini, subirini mtakachokiona huyo mzee
akijua mumemfahamu atakuja kuwafanyia baya zaidi ya hilo…’akasema.
‘Atafanya nini acha kutisha watu hapa…’akasema kiongozi wa
dini.
‘Sawa mimi nawatisha,..lakini jiulizeni mangapi yamefanyika humu
ndani na hamkuweza kuyazuia…jamaa huyo alikuwa anakuja kwangu usiku, wewe mama
uliweza kumzuia…hujaweza kumzuia,…na nani anapata shida, ndio mimi nimepata
shida, lakini hata nyie, …..mimi nimejitolea kuja kuusema ukweli kwa vile
mumenisaidia sana…’akasema.
‘Ila tunakuonya kama wewe upo nyuma ya haya mambo utakuja
kupata shida …’akaambiwa na hao wazee.
‘Wazee wangu, ..ndio maana nimekuja, nimeona nateseka kwa
kuiweka hii siri moyoni mwangu, hawa watu walinipokea wakanilea, wakanihifadhi,
na haya yanatokea kwasababu yangu mimi, ..kwanini nikae kimia, hapana, ..mungu
mwenyewe anajua ila nimetimiza wajibu wangu, sasa iliyobakia ipo mikononi mwenu
kwaherini…..’akaaga, na alipofika mlangoni, akageuka na kusema
‘Na wewe binti mdada mwenzangu, uwe makini, kwani
yaliyonipata mimi , huenda ndio hayo yanayokupata na wewe, siku ile nilikuona
unalia, huenda hayo yameanza kwako, …sasa ni juu yako kuhangaika au kukaa kimia
na kusema,..’mimi sijui….’haya endelea kutokujua, …kwaherini…’binti akasema na
kuondoka.
NB Tuendee…. hapana tusubirie sehemu ijayo.
WAZO ZA LEO:
Mwenyezimungu alitujua sisi wanadamu tulivyo, kuwa kuna wengine nafsini mwao ni
zaidi ya mnyama, roho mbaya, na wengine wanyonge, ndio maana akatuambia
vyovyote iwavyo, yeye yupo karibu nasi kuliko mshipa wa damu uliopo mwilini
wetu, tumuombe yeye, tumtegemee yeye, lakini ukweli wa kumuamini, na sio kwa
kinafiki au kwa kumshirikisha. Tumuombe mola wety atupe imani thabiti ya
kumuamini yeye, na kumtegemea yeye..Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment